JK akoshwa na ziara ya Ivory Coast
*Awaandalia chakula maalumu Golden Tulip
*Ammwagia sifa Drogba, amkabidhi uzi wa Stars
*Awaombea watwae taji, aahidi Watz kuwashangilia
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ameelezea kufurahishwa na ujio wa timu ya taifa ya Ivory Coast The Elephant kwani umeutangaza nchi kutokana na wachezaji wake nyota wa kimataifa kujulikana akiwemo mshambuliaji wa klabu ya Chelsea Didier Drogba.
Akizungumza katika hafla maalumu ya chakula cha mchana aliyoiandaa kuwakaribisha Ivory Coast, kwenye Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar leo JK kasema Tanzania imepata sifa kubwa duniani baada ya kutangazwa kwa mara ya kwanza katika kituo cha televisheni cha Sky News, kuhusiana na ziara ya The Elephant katika habari za michezo, sambamba na kuonyesha picha.
Kikwete alisema, kutangazwa kwa mechi kati ya Tanzania na Ivory Coast ni sifa kubwa kwa nchi, hasa ukizingatia Taifa Stars iliweza kuwamudu The Elephant ambao walikuwa wamesheheni nyota wa kulipwa na kutoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0, lililofungwa na Drogba.
Rais alimpa pongezi kubwa mshambuliaji huyo ambaye pia ni tegemeo wa klabu ya Chelsea ya England, kwa kuitangaza Tanzania alipokuwa akihojiwa na Sky News Sports, ambako hakusita kusifu kiwango cha wachezaji wa Stars, kuwa ni kikubwa.
"Jana nilifurahi sana nilipokuwa nikiangalia kituo cha Sky News Sport, kwa mara ya kwanza kuona wakitangaza timu ya Ivory Coast ikiwa nchini, ambapo mchezaji nyota wa kimataifa Drogba alikiri kwamba, Tanzania soka lipo huku akisifu kiwango cha Stars," alisema Kikwete.
Kikwete alisema, kutokana na Drogba kuwa mchezaji maarufu duniani, kwa kupitia umaarufu wake, Tanzania imeweza kujitangaza duniani kote na hiyo itasaidia kuwavutia nyota wengine kufanya ziara hapa nchini.
"Hivi sasa Dunia nzima inatambua kiwango cha soka la Tanzania, natoa shukrani nyingi kwa Ivory Coast kuichagua nchi yetu kupiga kambi ya kujiandaa na fainali hizo za Angola," alisema Kikwete.
Aidha alisema, alipanga kuandaa hafla hiyo na kuwaalika wachezaji wa Ivory Coast, lakini baadaye akaona ni bora ajumuike na timu zote tatu, ambazo ni wenyeji Tanzania, Rwanda na Ivory Coast.
Katika hatua nyingine, Kikwete aliwataka wachezaji wa Rwanda Amavubi, kucheza kwa kujituma na ushirikiano mkubwa ili kuwafunga Ivory Coast, baada ya Stars kufungwa 1-0 licha ya kuwa, angalau wangeweza kutoka sare, lakini bahati haikuwa yao.
Aliongeza kuwa, Tanzania itajivunia hivi sasa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kutokana na Ivory Coast kuichagua pekee kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na fainali za Angola, pamoja na Kombe la Dunia litakalofanyika Afrika Kusini.
"Ninaamini kuwa, Bara hili la Afrika lina timu nyingi huku Ivory Coast ikiwa inaongoza kwa ubora, hivyo kwa kuchagua kuja nchini kwetu kufanya mazoezi ya mwisho ya kujiandaa kwenda Angola katika Fainali za Afrika, ni jambo la kujivunia kwa kila Mtanzania," alisema Kikwete.
Wakati huohuo, Kikwete alisema, anawaombea kwa Mungu na Miungu mingine kutwaa ubingwa wa Afrika, ili kurejea na Kombe hilo kama walivyopanga kulileta na kulipeleka Mlima Kilimanjaro na kuongeza kuwa, ana imani watashinda.
Aidha alisema, Tembo hao wa Ivory Coast watakapotinga hatua ya fainali, Watanzania watakwenda kuipa sapoti ili kutwaa taji hilo.
Mwisho wa hafla hiyo, Rais Kikwete aliwakabidhi jezi ya Taifa Stars, wachezaji nyota wa kimataifa wa Ivory Coast, Didier Drogba, Kolo Toure, Emmanuel Eboue, Solomon Kalou na Yaya Toure.
Fainali za Mataifa ya Afrika zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 10 hadi 30, mwaka huu nchini Angola.