Naona mijadala kuhusu Lowassa haulengi kutatua changamoto zilizopo, na badala yake umetawaliwa na malalamiko, nahali ya kukata tamaa. Tulijadili hilo japo kidogo. Kwa hali ya sasa, Edward Ngoyai Lowassa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni suala lililo katika ‘count-down' kama vile kuelekea mwaka mpya. Njia za kuzuia hilo lisitokee ni kumi. Mosi, Lowassa arukwe na akili, au apate ulemavu wa kudumu ili apoteze sifa za kugombea. Pili, Lowassa apoteze maisha yake, hivyo kupotea katika medani hii. Tatu, Lowassa apatikane na kesi ya kujibu kuhusu uhujumu uchumi, itakayomtia hatiani, hivyo kumpotezea sifa za kugombea. Nne, Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete aongoze mkakati kama ule wa Mkapa mwaka 2005 kuhakikisha jina la Lowassa linakatwa katika hatua za awali, na kuwa na mikakati kabambae pia ya kumvunja nguvu aki defect. Tano, Edward Lowassa mwenyewe kufanya maamuzi magumu na kuamua kutogombea mwaka 2015. Sita, vituo vya televisheni na radio vya kitaifa, viwe na ujasiri wa kuanza sasahivi, kuelezea umma kwanini Lowassa hafai, kwa kutumia sababu mbalimbali, zikisindikizwa na hotuba za Mwalimu Nyerere, ingawa akina Jussa wameshajazwa nondo, na kuanza kum-denounce Nyerere ikiwa ni moja ya mikakati ya kuhakikisha Lowassa anakuwa chaguo la Wazanzibari.
Saba, wazanzibari wajazwe ‘madini' kuhusu Lowassa kwamba ni hatari sana kwa taifa, na vile vile kwa Zanzibar, hivyo asiungwe mkono. Nane, CCM ibadilishe utaratibu wa kumpata mgombea Urais, iweke msumeno mkali kuzuia rushwa kwa wajumbe, sambamba na kuhakikisha kwamba wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa watakaoteuliwa mwaka huu (2012), wengi wao watakuwa sio wa Lowassa na watabakia hivyo mpaka mwaka 2015. Tisa, wale wote wanaomuunga mkono Lowassa, vijana kwa wazee, wake kwa waume, washawishike kwamba Lowassa hafai, na hivyo kuacha kumuunga mkono. Na kumi, wanachama wa CCM kwa wingi wao nchi nzima (sio wananchi, bali wanachama wa CCM), na UWT, UVCCM, waanze maandamano sasa (sio mwaka 2015), na ya mara kwa mara, kutoa matamko kwamba Lowassa avuliwe gamba, kwani anaharibu hali ya hewa ya nchi, hafai kuwa rais ajaye, hivyo adhibitiwe sasa. Na lazima waaandamanaji hawa wajiandae kupoteza maisha yao, kwa wingi sana.
Vinginevyo,sio magazeti, wala Jamii Forums, au mijadala majumbani, itakayoweza kumzuia Lowassa kutimiza ndoto yake. Kwa mfano, magazeti Tanzania hayana mzunguko wa kutosha nchi nzima, kwani hakuna gazeti linalotoa zaidi ya nakala elfu kumi kwa siku. Ni aslimia moja tu ya watanzania wanafikiwa na magazeti kila siku. Pia ni kawaida kwa magazeti yote kusambaza asilimia 60 ya nakala zao jijini Dar-es-salaam, na asilimia 40 katika mikoa iliyobakia nchi nzima. Tukumbuke, hili ni taifa lenye watu karibia milioni 45. Pia tusisahau kwamba wapiga kura wengi hawasomi magazeti kwa sababu mbalimbsli kama vile, kutokujua kusoma na kuandika, lakini pia kutokuwa na uwezo wa kununua magazeti.
Kuhusu Jamiiforums, pamoja na umuhimu wake, bado haijaweza kuufikia UMMA wa Tanzania kwa mapana zaidi. Kwa wastani, idadi ya watu wanaozuru JF ambao wanaishi Tanzania haizidi elfu sita kwa siku, na hawa ni kwa ujumla wake – yani wale wanaofuatilia siasa na wale wanaofuatilia mengine nje ya siasa. Watu hawa pia ni wale wa mijini pekee. Mbaya zaidi ni kwamba, ni asilimia nne tu ya watanzania wana uwezo wa Internet (sawa na watanzania milioni moja na ushehe). JF ina wanachama karibia elfu 60, lakini active kwa siku ambao wanaishi Tanzania hawazidi watu elfu sita. Vinginevyo, asilimia 85 ya watanzania wanatumia radio (84% vijijini, 85% mijini), na asilimia 27 wanatazama televisheni (59% mijini, 14% vijijini).
Tuseme hayo hapo juu yote hayatekelezeki kumzuia Lowassa mwaka 2015, hivyo kutuacha na uwezekano mmoja tu – wa Mwenyekiti wa CCM Taifa Jakaya Kikwete, kuongoza mkakati wa kukata jina la Lowassa, kama mkapa alivyofanya mwaka 2005. Je Kikwete ana uthubutu? Tatizo ni kwamba, kama Kikwete anataka kubakia salama katika maisha yake ya ustaafu, ni Rais Lowassa ndiye atakayemlinda. Vinginevyo mgombea yoyote mwingine atakae bebwa na Kikwete na kufanikiwa, (iwe Nahodha, Migiro, Amina Salum Ali, Dr. Mwinyi, Mbawala, n.k), wote hawa wataingia katika migogoro mikubwa sana ya kiuongozi, kutokana na jitihada za Lowassa na Rostam. Serikali hiyo itaanguka baada ya muda sio mrefu. Tusisahau kwamba ushindi wa asilimia 60 wa Kikwete mwaka 2010 ulitokana na njama za kina Lowassa na Rostam kutaka Dr. Slaa ashinde. Ndio maana tangia awali, Kikwete aliamua kuhamishia kampeni kwenye familia yake. Vinginevyo, angewaachia kina Makamba kampeni, angepoteza Urais.
Kwahiyo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, hana jinsi bali kumpisha mwenye nguvu – Edward Lowassa kumpokea Urais mwaka 2015. Ni muhimu sana tukawa na ufahamu kwamba majadiliano yetu humu JF hayatamzuia Lowassa kuwa Rais, na tusidanganyike kwa kufananisha na nguvu ya JF kuhusu ile list of shame, kwani ile ilipata nguvu pale tu viongozi wa CCM wenyewe walipoamua kuibeba kama hoja, ili wamlinde mfalme, na sio vinginevyo.
Kwa kumalizia, ni muhimu kuwaonya wale wanaompinga Lowassa kwamba wajiangalie sana wanapoenda huko kwenye maeneo ya kunywa vilevi na kuongea maneno ya kashfa juu ya Edward Ngoyai Lowassa, kwani mnaweza msifike nyumbani ili kujiunga na familia zenu, na iwapo mtafika, basi angalau mtakuwa ngeu usoni, kwani huko kwenye mabaa, wamejaa wapambe na wapiga debe wa Lowassa, wakilinda jina hili kama vile yeye ndiye baba wa taifa. Edward Ngoyai Lowassa ana jeshi kubwa sana, na sio kwamba wote wanalipwa kufanya shughuli hiyo, kwani jeshi kubwa zaidi ni la vijana na wazee waliojitolea kumpigania hadi mwisho. Mwaka 2012, Dodoma itachafuka na mashabiki mbalimbali ambao watakuwa wamechukua likizo zao ili kwenda kule kuhakikisha jina la Edward Ngoyai Lowassa linapita katika nafasi atakazogombea. Mwaka 2015, Dodoma ndio itachafuka zaidi, na iwapo jina lake halitapita, maisha mengi sana yatapotea mjini Dodoma mwaka huo, huku CCM nayo ikivunjika vipande vipande, kitu ambacho kitamhitaji huyo huyo Lowassa na wenzake kurekebisha hali hiyo, kwa kumpa ‘halali' yake' yani Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nadhani kwa wale wasiopendelea Lowassa awe Rais wa Tano wa Tanzania, angalau sasa mnajua wapi kwa kuanzia kuzima ndoto yake hiyo. Vinginevyo, kwa wale mashabiki wa Lowassa, hakika mnagundua jinsi gani ni vigumu kwa kipenzi chenu kukatishwa safari yake ya kuelekea mahali pale patakatifu – Ikulu.