Muungano ulipigiwa kura na Bunge la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar. Pande zote mbili zilijadili (najua wengi hawajui historia hiyo). Nyerere alileta hoja Bungeni na kuwaelewa wabunge wetu kwanini mataifa mawili haya yataungana. Wabunge wakaridhia na ni baada ya hapo ndio Muungano ukafanyika.
Kama ni hivyo ni jambo lililo bora na zuri wananchi wakayazungumza mambo haya aidha kupitia mabunge yote mawili au kwa kura ya maoni kwa sababu inavyo onekana hakuna taifa hata moja katika mataifa haya mawili yaliyoko kwenye huu Muungano aliyemlazimisha mwenziwe kuungana.
Na hakuna ubaya wowote wala dhambi kwa pande zote mbili kusikilizana nini mwenziwe anataka. Kama upande mmoja unafikiria kuwa jambo hili wakati wake umekwisha tulibadilishe, basi wasikilizane tu na sio kufanyiana vitisho.
Hivyo ni Muungano halali na ni jukumu la kila Mtanzania kuulinda. Katika kuulinda huko ni jukumu letu kuwapinga pasipo kuwapepesea macho wale wote wanaotaka Muungano uvunjike kwa sababu hawataki kufanya maamuzi magumu au kuzungumzia mambo yanayoleta utata katika Muungano. Wapo watu wa bara ambao kwa kawaida hatupendi sana migongano, tunapenda vitu lelemama kiasi kwamba tumekuwa kama tumedekezwa hivi!
Huu Muungano ni mali ya Tanganyika na Zanzibar kama kuna kero kutoka upande wowote ni busara kuelezana kupitia vyombo husika na si kufikiria kuwa upande mmoja mawazo yao ni ukoma au yule mwenye kuuliza mambo yaliyoko kwenye Muungano ni msaliti...! Nyerere na Karume walikuwa ni binadamu kama mimi na wewe, nao walikuwa na mapungufu yao.
Muungano unajadilika tena sana na bila wasi wasi wowote.
Serikali ikisema "hawa wanaleta mgawanyiko katika jamii" basi kama watoto tunakubali na kuwakimbia wenzetu kwa sababu "serikali imesema"; Serikali ikija na kusema wapinzani wanataka kuligawa taifa basi tunakimbia kama watoto huku tumenyanyua mikono tubebwe huku tunaonesha vidole "yule anataka kuligawa taifa mama!".
Watanzania wengi hawajazoewa kufikiria wenyewe, wakati wa zidumu fikra za mwenyekiti zishapitwa na wakati kwani sasa mfumo wetu si wa kijamaa tena... huu ni wakati wa fikra mbali mbali m-badara... Wakati wa kutishana tulisha uzika pale alipozikwa Nyerere kule Butiama... Tumekubali vyama vingi basi tukubari fikra mpya as long tunatumia vyombo husika tena bila kutishiana maisha.
Hatutaki kugonganisha mawazo na matokeo yake hata kwenye vikao vya kazi tumekuwa hivi hivi tu. Mtu anayebisha sana anaonekana "mbishi tu"; mtu anayetaka maelezo zaidi anaonekana kama anataka kujipendekeza. Tunataka mambo ya upole upole na taratibu.
Ndio maana utaona watu wengi wa bara wanaotaka Muungano uvunjike wanafanya hivyo kwa sababu utaondoa "migongano" na kubishana bishana. Tunataka "utulivu, amani, na mshikamano" wa uongo. Ndio maana watu wa bara wanaona kama Zanzibar ni wakorofi kweli kumbe kule Zanzibar wao wameshazoea zile siasa za kujibizana, kubishana na serikali, na kutunishiana misuli.
Tatizo lipo uko uko kwa waliokamata madaraka, mbinu wanao tumia ni ile ya kumwita Mbwa jina baya ili haonekane mbaya apate kipigo toka kwa watoto mitaani.
Serikali inatakiwa kuondoa hizi choko choko za maneno kama nilivyoa andika hapo juu... dawa ni kukaa vikao husika tena ka kushirikisha vyama vyote vya siasa na kuwepo na kula moja mtu mmoja, kwa maana kila mwakilishi hawe na haki sawa na si kutumia hili bunge lililo jaa wabunge wa chama kimoja na kila jambo kuwa na maamuzi ya jazba bila kuangalia maslahi ya taifa.
Ninaamini athari kubwa sana ya ukoloni katika psyche ya watu wa bara ni unchecked docility ya ajabu sana. Na watawala wetu wanatumia sana hii kuwatuliza watu wa bara.
Muungano tutaulinda na tutaudumisha na kuuboresha. Tutawapinga watu wa bara wanaotaka kuuvunja kwa sababu hawataki kubishana na kulumbana na kugongana kifikra na tutawapinga watu wa visiwani wanaotaka kuuvunja kwa sababu wanaogopa kukubali ukweli wa umuhimu wa muungano.
Tutawaunga mkono wale wote majasiri ambao watasimama na kutoa hoja za jinsi ya kuudumisha, watakaokuwa tayari kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuuboresha na wale watakaonesha uongozi wa kuboresha muungano wetu kwa uwazi na ukweli na ujasiri usio kikomo.
Natumaini hatutawafumbia macho wala kuwaonea haya kuwashughulikia pasipo kuwabembeleza watu wanaofanya njama za kuuvunja muungano wetu.
Muungano daima!
Tusiwazuie Watanganyika na Wazanzibar kuzungumza masuala ya Muungano na Katiba, kama kuna baadhi ya mambo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho, yafanyiwe bila kuonekana wengine wachawi, serikali isiwatishe watu watu wanao hoji mustakabali mzima wa mambo ya Muungano kama katiba inafaa au haifai dawa ni kuangaliwa upya.
Hii katiba ina viraka kama nguo ya mwenda wazimu... Na hivyo viraka vimewekwa na hao walioko madarakani, wakati umefika sasa ya kushona nguo mpya...! Kama kweli serikali inataka umoja wa kitaifa ni bora kutengeneza katiba mpya.
Hali hii ya baadhi ya watu kutaka kuvunja Muungano ni matokeo ya serikali tawala kukaa kimya na kuwatisha wale wote wenye kuulizia mambo ya Muungano na katiba.
Hivi hao waliokuwa viongozi (marehemu Nyerere na Mzee Karume) hawakuwahi kuhitilafiana kwenye masuwala ya Muungano mbona tunawaona kama vile walikuwa malaika? Kama walihitilafiana nina uhakika kabisa walikaa na kuyazungumza yakaisha... basi nasema kuwa wakati huu si wa marais wawili kukaa peke yao na kuzungumza kero ya Muungano na katiba ni haki ya Watanganyika na Wazanzibar kukaa kitako na kuyazungumza hadi kukubaliana. Tatizo lililopo sasa ni kuwa viongozi hao wa juu hawataki kuzungumza na kila mwenye kusema anaonekana kuwa ni mwenye kutaka kuvunja Muungano.
Wakati ni huu sasa tuwe wakomavu wa fikra, hakuna lisiloweza au kuzungumzika.