Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) ni Taasisi pekee bobezi katika matibabu ya mifupa, ajali, upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Taasisi hii imekua tegemeo kubwa hapa Tanzania na nchi nyingine barani Afrika. Katika kuhakikisha inaendelea kutoa huduma za kisasa zinazoendana na ubora wa kimataifa, Januari 30, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo
Prof. Abel Makubi alisema wanatarajia kuanza matibabu kwa njia ya teknolojia ya kisasa ya kutumia roboti na akili bandia (artificial intelligence) katika upasuaji ili kuongeza ufanisi wa tiba kwa wagonjwa.
Je, MOI hukata miguu ya kila Bodaboda anayefikishwa hapo?
Pamoja na umahiri mkubwa wa Taasisi hii katika kutibu wagonjwa wa mifupa na Ubongo, baadhi ya vijiwe na mitandao ya Kijamii Tanzania huzungumzia madai yanayohusisha Taasisi hii na ukataji wa miguu ya bodaboda (waendesha pikipiki) wanaofikishwa hapo wakipata ajali.
Kwa mujibu wa
taarifa ya Januari 9, 2024 iliyochapishwa na gazeti la Mwananchi, Taasisi ya MOI hupokea kati ya majeruhi 20-25 kwa siku ambapo 60% kati yao huwa ni bodaboda, 30% ni majeruhi wa ajali za barabarani na 10% ni ajali zingine.
Mathalani, Juni 25, 2013, mtumiaji mmoja wa Mtandao wa X (
Omarilyas) aliandika
“Nasikia pale MOI kuna tabia ya madaktari kukimbilia kukata mikono na miguu ya wanaopata ajali za pikipiki bila ya jitihada za kuwatibu”
Hii inathibitisha uwepo wa madai hayo ambayo JamiiCheck iliona kuna haja ya kuyafuatilia.
Makala ya
Gazeti la Habari Leo toleo la Agosti 4, 2023 lilichapisha kanusho la Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Abel Makubi.
Kwa mujibu wa Prof. Makubi, madaktari wa MOI wanakata mguu mgonjwa aliyefika kwa ajili ya kumuokoa na athari zinazoweza kujitokeza sehemu nyingine za mwili kama asipokatwa.
“Kuna dhana imejengeka kuwa bodaboda akipata ajali akifikishwa MOI atakatwa miguu, hii sio kweli. Kuna bodaboda wamekuja MOI na wametibiwa.Wanaolazimika kukatwa miguu ni wale ambao wamepata matatizo ambayo akiendelea kukaa na mguu utasababisha madhara makubwa kwenye sehemu nyingine ya mwili. Hakuna mtu anapenda kukata kiungo cha mtu mwingine, iwe mkono au mguu,” alisema Prof. Makubi.
Pia, Januari 30, 2024,
Azam TV kupitia channeli yake ya UTV ilizungumza na Prof. Makubi kuhusu suala hilo ambaye alikanusha tena.
"Hakuna ukweli wowote kuwa bodaboda wanaokuja MOl kwa matibabu wanakatwa miguu bali ni baadhi ya watu tu waliamua kuharibu jina la Taasisi miaka ya nyuma kwani MOl imekua mkombozi mkubwa wa Bodaboda"- Prof. Abel Makubi
Kwa mujibu wa Ripoti maalumu iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Utengenezaji wa Vifaa Tiba la nchini Marekani linalojulikana kama
SIGN Fracture Care International imeonesha kuwa MOI inashika nafasi ya pili duniani kwa umahiri wa kutibu wagonjwa waliovunjika mifupa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani ambapo katika mwaka 2023 ilifanikiwa kuwafanyia upasuaji wagonjwa 713 waliovunjika mifupa ya paja (femur) na ugoko (tibia), ikiwa nyuma ya Hospitali ya
Kossamak ya nchini Cambodia ambayo imefanya upasuaji kwa wagonjwa 1,029.