Ndugu Zangu,
Nimeona mada niliyoianzisha kwenye mjengwablog imeingizwa humu na wengi wameshiriki kuichangia, na mimi pia. Mada inasema " Nilichokiona Jana pale Mwembetogwa". Lakini ziada ya pale Mwembetogwa ni ukweli kuwa mwanzoni kabisa mwa hotuba yake, Dr Slaa alitoa kauli mbele ya umati ule. Kauli ambayo binafsi niliisikia na ilinishtua sana. Dr Slaa alisikika akitamka kuwa kuna kiongozi wa mkoa ( CHADEMA) ( Alimtaja jina) ambaye amehongwa na mgombea ubunge wa CCM jimbo lingine la Iringa ( naye alimtaja jina) ili asirudishe fomu zake. Dr Slaa akataka kiongozi huyo wa zamani wa CHADEMA apuuzwe na akitaka aende mahakamani.
Nadhani katika wakati huu kuna umuhimu wa kuwafahamu zaidi wagombea wetu. Na kumtakia mema Dr Slaa ni pamoja na kumwambia yale tunayoyaona ni mapungufu. Si kummwagia sifa tu. Maana, kwa kitendo kile, Dr Slaa kwa mtazamo wangu alimdhalilisha kiongozi yule wa CHADEMA mbele ya umati ule. Na bahati mbaya au nzuri kiongozi huyo wa CHADEMA alikuwapo. Kwa macho yangu nilimwona kiongozi huyo wa CHADEMA akishiriki kupiga makofi kuungana na umati uliokuwa ukishangilia kauli ya Dr Slaa. Masikini, kiongozi yule wa CHADEMA, bila shaka alipigwa na butwaa na hakuwa na la kufanya bali naye kupiga makofi!
Kwangu nilishtushwa na kusikitishwa sana. Bado naamini Dr Slaa hakumtendea haki kiongozi yule wa CHADEMA. Kama Dr Slaa alikuwa na ushahidi wa alichokisema, basi, hakuwa na haja ya kumtuhumu na kumtolea hukumu kiongozi yule pale hadharani. Kiongozi yule wa CHADEMA aliyehukumiwa hadharani ni mwanajamii hapa Iringa. Ameshapigwa mhuri mbaya bila hata kupewa fursa ya kujitetea. Kwa mzazi kama mimi naelewa jinsi kiongozi yule atakavyojisikia vibaya mbele ya familia yake, mke na watoto wake. Kwamba ametoka kwenye mkutano wa mgombea urais huku yeye akitajwa hadharani kuwa amehongwa asirudishe fomu.
CHADEMA wana vikao vyao, kwa kutanguliza busara wangeyamaliza ya kwao kwenye vikao vyao vya ndani, si hadharani. Na kama mgombea Urais, Dr Slaa anapaswa awe mfano wa kuheshimu utawala wa sheria. Hili ningelisema kama nilivyolisema hata kama lingefanywa na Kikwete wa CCM, Lipumba wa CUF au mgombea ye yote yule. Nisingelisikia nikalinyamazia. Kuandika ni kushauri pia. Tusingependa Dr Slaa apitishwe njia ya Mrema, ina miba na matope. Anayesoma na kuhusika na kilichoandikwa ana uhuru wa kupokea ushauri na kuufanyia kazi au kuachana nao. Nimechokoza mjadala....
Maggid,
Iringa.