Na Mwandishi Wetu,
Arusha.
Makamu mwenyekiti Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara komredi Abdulrahman Omar Kinana ameishauri na ameiomba serikali kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wale wote waliotajwa kwenye ripoti ya mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali (CAG).
Akizungumza kwenye mkutano wa ndani wa chama hicho mjini Arusha, Kinana amesema ni muhimu wote waliotajwa kwenye ripoti ya CAG wakachukuliwa hatua.
“Wakati umefika kwa serikali kuchukua hatua kwa wahusika wote waliylotajwa kwa kuisababishia serikali hasara, upotevu au ubadhirifu wa fedha za umma kupitia ripoti ya CAG” amesema Kinana na kuongeza
“ Ripoti ile inaonesha mambo ya hovyo yamefanyika, Si uzushi kazi ile ya ukaguzi imefanywa kisayansi na kitaalamu, wabunge wameijadili kwa ukali sana, hata wasomi na wananchi wengine wameijadili kwa ukali vile vile, Mimi nadhani ingekuwa vyema hatua ziwe zinachukuliwa papo kwa papo ili watu wajenge nidhamu na heshima kwa fedha za wananchi.” alisititiza Kinana
Kinana ambaye alikuwa anahitimisha ziara yake ya mikoa minne kukagua uhai wa chama, alisema pamoja na kwamba hana mamlaka ya kutoa amri kwa serikali lakini atamwambia Rais juu ya ushauri huo.
“Kwa nafasi yangu nazungumza kwa niaba ya mwenyekiti wetu ambaye ni Rais kwamba wahusika wachukuliwe hatua. Si kila jambo lazima Rais aagize, tujenge utamaduni wa kuwajibika sisi wenyewe.'
Amesema lazima kuwe na utaratibu wa kuwajibika mtu anapofanya kosa na akishindwa kufanya hivyo vyombo na taasisi zenye wajibu wa kusimamia uadilifu kwa viongozi na watendaji nchini hususani kwenye kujenga nidhamu na fedha za umma zichukue dhidi yake.
“Tujenge utamaduni wa kuwahi kuchukua hatua kwa wakati, mtu akae pembeni apishe uchunguzi na akithitika apishe wengine kwani kuna watu wengi wana uwezo hawana kazi!" alisema na kuongeza
“ Kila ripoti ya CAG inapotolewa tukianzia na hii wale wanaotajwa wawajibishwe kujibu na kuchukuliwa hatua. Ikiendelea kubaki hivi, ripoti inatolewa na kuwekwa kabatini fedha za wananchi zitaendelea kuchezewa.”
Kinana akiambata na katibu wa NEC itikikadi na uenezi Shaka Hamdu Shaka alihitimisha ziara yake ya mikoa minne ya Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Arusha kukagua uhai wa chama leo mkoani Arusha.