Mwaka 1992, Maaskofu wa Kanisa Katoliki Malawi walitoa waraka kama huu wa kwetu - uliolenga kero za watu (kuboresha huduma za jamii, mgawanyo mzuri wa raslimali za nchi, umaskini, uhuru wa kutoa mawazo, haki za binadamu nk) - na kwa vile ilikuwa mara ya kwanza kupinga hadharani upungufu uliokuwepo katika utawala wa Dr Kamuzu Banda, maaskofu hao waliwekwa chini ya ulinzi na kuitwa wajieleze mbele ya Rais.
Hali ilikuwa tete sana na hata printing press iliyochapa waraka huo ilichomwa moto mara moja!
Wakati huohuo chama tawala (Malawi Congress Party - MCP) kilifanya mkutano wa siri namna ya ama kuwafukuza maaskofu hao nchini au kuwafanya wapotee wasionekane tena bila watu kujua wako wapi. Baadhi ya walikuwa viongozi wa Kanisa na wanachama wa MCP walikana dini hadharani kwa kusema maaskofu wamemdhalilisha Rais wao na hivyo wao wenyewe hawana sababu ya kuendelea kusali kwenye Kanisa ovu namna hiyo.
Maaksofu walitungiwa kila aina ya ubaya lakini kwa vile haki na ukweli husimama mpaka mwisho, wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 1994, chama tawala MCP kilianguka vibaya sana na United Democtatic Front (UDF) kikawa madarakani. Baada ya Dr Banda kuangushwa maaskofu waliombwa wafungue kesi ya kutishiwa kuuawa na Dr Banda lakini walisema wameshamsamehe na hivyo kesi yake kufutwa.
Baada ya Dr Banda kufariki, viongozi waliokana dini hadharani walirudi tena kuomba radhi kanisani kwa kusema walichokisema hakikuwa kimetoka moyoni mwao bali ilikuwa kulinda maslahi yao ya kisiasa tu!
Tanzania tunaelekea kwenye njia ya namna hiyo na hakika haki na ukweli kuhusu waraka huo vitasimama hadi mwisho! Kama kweli nia ya waraka ni kumchagua Rais Mkatoliki au Mkristo au kuleta udini na kinachosemwa dhidi ya Kanisa Katoliki ndiyo kero halisi za Watanzania, basi mwisho wa yote Mungu mwenyewe ataamua ukweli uko wapi!