Kipi kipo nyuma ya shamrashamra za mastaa wa Kimataifa wanaokuja Bongo: Kuna jambo, au tunatolewa kwenye reli?

Kipi kipo nyuma ya shamrashamra za mastaa wa Kimataifa wanaokuja Bongo: Kuna jambo, au tunatolewa kwenye reli?

DodomaTZ

Senior Member
Joined
May 20, 2022
Posts
197
Reaction score
233
Katika kipindi cha hivi karibuni, Tanzania imeshuhudia ujio wa watu maarufu duniani kama Didier Drogba na Rio Ferdinand ikielezwa kuwa ni kwa mwaliko wa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo inayoongizwa na Paul Makonda. Kwa juu juu, hatua hii inaweza kuonekana kama jitihada za kuitangaza nchi kimataifa au kukuza sekta ya michezo na utalii. Lakini nyuma ya pazia, kuna maswali muhimu ambayo wananchi wanajiuliza?

Je, ziara hizi zina malengo gani ya moja kwa moja kwa maendeleo ya wananchi? Je, kuna mikataba ya uwekezaji, programu za vijana, academies za michezo au miradi endelevu iliyoambatana na ujio wa watu hawa? Au ni matukio ya muda mfupi yenye msisimko wa kisiasa na matumizi makubwa ya fedha za umma bila matokeo yanayoonekana?

Katika mazingira ambayo wananchi wanakabiliwa na changamoto za gharama za maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana, pamoja na mijadala mikubwa kuhusu huduma za kijamii kama bei za mafuta na uwajibikaji wa Serikali, ni muhimu kujiuliza kama shamrashamra ya ujio wa mastaa wa kimataifa inalenga kuleta tija kwenye mambo muhimu au ni mkakati kuhamisha mijadala ya kitaifa kutoka kwenye masuala ya msingi kwenda kwenye burudani ?

Historia ya siasa duniani inaonesha kuwa wakati mwingine Serikali hutumia ushawishi wa watu maarufu kujenga hisia chanya kwa umma, kupunguza ukosoaji, au kuimarisha taswira ya viongozi mbele ya wananchi. Hata matukio haya yanapaswa kutazamwa kwa jicho la kizalendo ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa manufaa ya wengi, si kwa propaganda za muda mfupi.

Ni vigumu kusema Serikali haitoi fungu kama anavyodai Msemaji wa Serikali, Msigwa. Kwamba watu hao wamekuja kutokana na connection ya Waziri mwenye dhamana, jambo hilo sio la kweli. Nani anaratibu shamrashamra kuanzia uwanja wa ndege, safari na matukio mbalimbali ambayo yanaonesha kuhusisha pesa kwenye uratibu?

Wananchi wana haki ya kupewa uwazi: gharama za ziara hizi ni kiasi gani? Faida zake za muda mrefu ni zipi? Na kwa nini vipaumbele hivi vinaonekana kupewa nguvu kubwa kuliko hoja zinazogusa maisha ya kila siku ya Watanzania?

Hakuna ubaya kwa Tanzania kujitangaza kimataifa. Tatizo linaanzia pale ambapo burudani na propaganda vinapopewa nafasi kubwa kuliko majibu ya changamoto halisi za wananchi. Serikali inapowekeza nguvu kubwa kwenye matukio ya kuvutia hisia za umma, wananchi wanapaswa kuwa makini kutofautisha kati ya maendeleo ya kweli na maigizo ya maendeleo au propaganda.
 
Back
Top Bottom