Kisiwa chenye hazina

Kisiwa chenye hazina

SURA YA KUMI NA NNE: MTU WA KISIWANI.

Kwenye mteremko wa kilima nilisikia kokoto zikiteremka; nikaona kiumbe kinakuja kwa kasi, sikujua kama alikuwa ni mnyama au binadamu, . Nikazidi kutazama, nikaona ni kama nyani kwa kuwa uso wake ulikuwa na nywele nyingi, na moyo ukanipiga kwa hofu nisiweze hata kumeza mate. Sasa nikajiona kweli nimo hatarini, nyuma yangu kuna mabaharia wauaji, na mbele yangu kuna kiumbe anayetisha; nikaanza kurudi nyuma kwenye hatari nilizozijua kuliko kwenda mbele kwenye hatari nisizozijua. Nikaanza kurudi lakini kile kiumbe kilinizungulca kipate kunikata njia mbele yangu. Basi nikachoka sana, lakini hata ingekuwa sikuchoka, nisingeweza kushindana nacho kwa jinsi kilivyoweza kuruka na kwenda mbio.Nilipotazama
sana nikaona kuwa ni binadamu; nikaanza kukumbuka habari nilizozisikia za watu wanaokula watu, nikakaribia kupiga yowe kwa hofu.

Hata nilipofikiri nikaona kuwa huyu ni mtu tu, basi nikajipa moyo nikaanza kumkaribia. Yeye alijificha nyuma ya mti mnene. Mimi nikienda mbele yeye hurudi nyuma na kujificha nyuma ya miti. Mradi tukaendelea vivi hivi. Mwishowe alinyosha mikono na kupiga magoti, kama mtu anayesihi, nami nikasimama na kumwuliza, “Nani wewe?”Akajibu lakini sauti iikuwa imefifia kama sauti ya mtu asiyezoea kusema kwa siku nyingi, “Mimi ni Ben Gun. Sasa yapata miaka mitatu sikusema na binadamu.”

Basi katika kumtazama zaidi nikaona kuwa sura yake ilikuwa nzuri, tena ni mweupe kama mimi, lakini kwa sababu ya jua kali amegeuka rangi. Nguo zilitatukatatuka na ndevu zake zilikuwa ndefu sana. Nikasema, “Miaka mitatu! Loo! Kwani ulisukumiwa hapa na mawimbi?”
Akajibu, “Rafiki yangu, nilitupwa hapa na wanadamu miaka mitatu iliyopita, na tangu wakati huo ninaponea wadudu ya porini na chaza wa baharini. Sasa natamani sana kula chakula cha kwetu cha kizungu. Mara nyingi nikilala huota ndoto za chakula.”
Basi nikamwambia, “Vema, kama nikijaaliwa kurudi tena melini,
nakuahidi kuwa utashiba kwa chakula kizuri.”

Akajibu, “Wasema ukijaaliwa kurudi tena melini. Je, kwani kitu gani kitakachokuzuia usirudi?” Basi tukaongea kidogo, kisha akainamisha kichwa chake karibu na sikio langu kuninong’oneza; akasema, “Mimi ni tajiri sana, nina mali nyingi nami nitakutajirisha kwa sababu wewe ni mtu wa kwanza uliyeniona.” Kisha akakunja uso na kusema, “Sasa niambie kweli, meli ile si meli ya Flinti?”

Nikamwambia, “Meli ile si meli ya Flinti, na yeye Flinti mwenyewe amekwisha kufa lakini mabaharia wake wamo ndani ya ile meli.” Akauliza “Je, yumo mmoja mwenye mguu mmoja?”
Nikajibu, “Ndiyo, huyo
ni John Fedha.”Kisha akasema, “Ikiwa wewe umetumwa na mtu huyo basi nimekwisha kufa.” Sasa nikaona afadhali nimwambie habari zote. Nikaanza kumweleza tokea mwanzo mpaka mwisho. Basi akasema, “Ama wewe
ni kijana mzuri nami sina haja ya kuogopa, wala wewe nawe usiniogope, niamini tu. Mimi napajua mahali palipofichwa hazina zote. Zilifichwa na Flinti na watu wake sita, na alipokwisha kuzificha aliwaua wote sita. Basi baada ya miaka mitatu nilikuwa katika meli nyingine tukipita njia hii hii; kuona kisiwa tu nikasema, ‘Rafiki, hazina za Flinti zilifichwa katika kisiwa hiki.Twendeni tukazifukue.’ Nahodha akakasirika sana na kutugombeza lakini mimi pamoja na mabaharia wengine tukashuka pwani kutafuta hazina. Muda
wa siku kumi na mbii tulitafuta tusiivumbue, tukarudi melini. Tulipofika melini, Nahodha akasema, ‘Wewe Ben Gun sikutaki tena, chukua bunduki na baruti urudi kisiwani ukazitafute hazina peke yako.’ Basi wakaniacha hapa kisiwani, na hapa nimekaa sasa muda wa miaka mitatu. Basi sasa tukiisha fika melini nataka ueleze yote niliyokwambia, maana naona haya kwa hali yangu ilivyo. Tena ninayo mashua nimeificha karibu na hori.”

Mara tukasikia mlio wa mzinga, akaniuliza, “Nini hicho?”
Nikasema, “Nadhani wameanza vita! Nifuate.”

Basi nikaanza kukimbilia kule kulikokuwa na meli, na yeye akanifuata. Baada ya kitambo kidogo tukasikia bunduki zinapigwa na baada ya kukimbia kidogo, nikaona mbele yangu bendera ya Uingereza inapepea juu.

(Wasomaji lazima wafahamu ya kuwa mpaka hapo aliyesimulia hadithi ni yule kijana anayeitwa Jim Hawkins. Sasa yeye anaacha kusimulia na Bwana Daktari ameshika zamu ya kuhadithia mambo yaliyotokea.)

SURA YA KUMI NA TANO:
(Bwana Daktari anaendelea
kusimulia hadithi)

TWAFANYA SHAURI KUTOKA MELINI.

Twafanya shauri kutoka melini Ilikuwa saa saba na nusu mabaharia walipokwenda kutembea pwani. Nahodha na Bwana Treloni na mimi tulikuwa tukiongea katika shetri. Kama upepo ungalikuwako nadhani tungaliwapiga mabaharia wale waliobaki melini tukang’oa nanga kwenda zetu. Lakini upepo haukuwako na zaidi ya hayo tulisikia kuwa mwenzetu mmoja, Jim Hawkins alishuka pwani pamoja na mabaharia.

Hatukufikiri kuwa Jim Hawkins ameasi ila tulikuwa na wasiwasi kuwa labda huko atadhurika, hasa kwa sababu mabaharia wamekasirika. Basi tukaenda sitahani kutazama pwani, tukaona mabaharia wamekwisha teremka pwani na wawili wamebaki mashuani kulinda zamu. Wale sita waliobakia melini walikaa gubetini wakizungumza huku wamejaa chuki. Kungojea huku kulikuwa kubaya sana, nikawa sina budi kushuka pwani na baharia mmoja jina lake Hunta. Tukaingia mashuani, tukavuta makasia mpaka tukafika pwani. Wale watu wawili waliokuwa wakilinda zamu walipotuona wakaingiwa na shaka, tukawaona kama wanaofanya mashauri ya kufanya jambo, lakini mwishowe wakakaa tu. Na sisi tulishuka pwani kwa mbali kidogo na mahali pale waliposhukia wale mabaharia. Sasa nikaanza kutembeatembea na hapo ndipo nilipoona boma lenyewe. Hilo boma lilikuwa limejengwa kwa magogo na lilitosha kuingia hata watu arobaini, na sehemu ya nje kuzunguka boma palikuwa peupe sana. Boma liijengwa madhubuti sana, na ndani kulikuwa na kisima.

Basi nikapeleleza, nikaona kuwa watu wakiingia katika boma hili hawana hofu kabisa kwa kuwa wataweza kuwazuia watu wanaowashambulia kabla hawajafika karibu na boma, maana walio ndani wataweza kuwapiga. Basi nikaona mahali hapa patatufaa sana, iliyobaki ni kuweka chakula cha kutosha tu.

Basi nilipokuwa nikifikiri, mara nikasikia sauti ya mtu kama amepigwa risasi; nikafikiri kuwa sasa Jim Hawkins amekufa. Basi nikafanya haraka kurudi kwenye mashua ili turudi melini. Hata nilipo fika pwani nikawakuta wenzangu wakitetemeka kwa hofu, na wale mabaharia nikawaona kuwa hata na wao wakiogopa sana. Basi tulipofika melini nikaeleza yote niliyoyaona na niliyokuwa nayo moyoni. Tukaanza kukusanya chakula na nyama kisha tukatia mashuani pamoja na bunduki na baruti.

Basi ikabaki kutengeneza shauri la mabaharia wale sita waliobakia melini. Nikamtuma mtu mmoja wa upande wetu, nikampa bunduki na nikamweka upande mmoja wa meli, huku nyuma Nahodha na Bwana Treloni wakazunguka upande wa pii, wakamwita mkubwa wa mabaharia wale wakamwambia: “Sisi watu wawili tupo hapa na mtu yeyote akifanya au akionyesha hata dalili ya uasi atakufa.”

Wakashangaa sana na baada ya kusemezana wenyewe kwa wenyewe wakazunguka kutaka kutokea kwa nyuma, lakini wapi! Walipokuwa wakizunguka wakamwona yule mtu tuliyemweka, wakashindwa. Basi Nahodha akawaamuru washuke chini, nao wakashuka.

Basi mimi na Hunta na mwingine jina lake Josi tukaingia katika mtubwi na tukavuta makasia na tukafika pwani tena. Wale mabaharia wawili walipotuona tumerudi safari ya pili pwani wakataharuki sana na mmoja akatoka mbio, nami nikajua kwamba alikwenda kupeleka habari kwa mkubwa wao, John Fedha.

Basi hivi tukafanya safari tatu,
na kila safari tukachukua chakula na nyama na dawa na bunduki na baruti mpaka tukaisha kuweka vitu vya kutosha katika lile boma. Nikawaacha watu wawili humo kulinda boma Hata yote yalipokuwa tayari, tukarudi tena melini, na kwa kuwa katika wale mabaharia sita waliobaki melini kulikuwa na mmoja niliyetaka afuatane nasi, maana nilimjua kuwa hayumo katika kushauriana na waasi, nikamwita na kumwambia, “Gray, kama ukitaka kuja njoo upesi. Sasa tunatoka melini, nami najua kuwa huafiki mipango ya waasi, basi njoo upesi.”
Kimya! Kimya!
Nikazidi kumwambia, “Haya ati!Kama wataka kuja njoo upesi; sasa twatoka.”Basi mara nikasikia ghasia, tena nikamwona akitoka mbio; nikatambua kuwa wengine walijaribu kumzuia.

SURA YA KUMI NA SITA:
(Hadithi ya Bwana Daktari)
SAFARI YA MWISHO YA MTUMBWI WETU.

Safari hii ilikuwa na hatari nyingi, maana mtumbwi ulikuwa mdogo nasi sote watu watano tulikuwa watu wazima na tena tumepakia chakula na vitu vingine. Basi kila mara mawimbi yalipokuja maji yalikuwa yakiingia ndani. Mradi tulikuwa katika hatari ya kuzama.

Lakini zaidi ya hayo tuliingia katika mkondo wa maji tukachukuliwa mbali kidogo, lakini tulipokaribia pwani nguvu za mkondo wa maji zikapungua, ikawa kazi nyepesi. Lakini hatari haikutuacha bado, maana tulisahau kuwa kuna mzinga melini. Tukawa mara kwa mara tukitazama nyuma; tukawaona wale mabaharia watano waliobaki melini wanaondoa turubali la mzinga. Basi sasa ikawa vimoto kabisa, na bwana Nahodha akauliza, “Je, nani aliye na shabaha barabara?”
Tukajibu, “Huyu Bwana Livesi, ndiye hodari kwa shabaha.”
“Vema, haya Bwana Livesi, twaa bunduki yako, mpige yule mtu mmoja na labda wale wengine wataogopa.” Basi akatwaa bunduki, akaelekeza
na kuipiga. Hakumpiga yule aliyekuwa tayari kupiga mzinga, maana ile risasi llimkosa, ikampiga mtu mmoja aliyekuwa amesimama karibu yake, akaanguka na kulia kwa sauti kubwa. Basi mara tukasikia wengine wakipiga kelele tukatazama pwani tukawaona mabaharia wale walioshuka zamani wote wanakuja mbio pwani. Basi sasa tukawa na haraka kufika pwani kabla hawajawahi kufika mahali tulipokusudia kushukia. Tukavuta makasia kwa nguvu zetu zote. Hata tulipokuwa karibu kufika pwani mara wale watu wa melini wakapiga mzinga na risasi yake ikapita juu, lakini kwa kishindo chake, mashua yetu ikazama. Kwa bahati tukawa tumekwisha fika karibu na pwani, maji ya magoti tu.

Basi tukatoka upesi tukaenda pwani, lakini hatukuwahi kuteremsha chakula
na vitu vinginevyo, ikawa tukapata hasara. Na katika zile bunduki zetu tano, mbili tu ndizo zilizokuwa hazikupata maji.
Tulipofika pwani hatari ikazidi, maana tulisikia sauti za watu wanaotoka upande wa boma letu; basi tukafanya haraka kwenda huko kunako boma tuone mambo gani yatakayotokea.
 
SURA YA KUMI NA SABA:
Hadithi ya Bwana Daktari)

MWISHO WA VITA YA SIKU YA KWANZA.

Tulikwenda upesi kadri tuwezavyo ili tuvuke sehemu ile ya pwani iliyokuwa kati yetu sisi na boma letu, na kila hatua tuliyokuwa tukienda tulikuwa tukisikia sauti za watu zikikaribia, na mwishowe tukasikia hata nyayo zikikanyaga majani na vijiti. Sasa nikabaini kuwa kabla hatujafika katika boma letu itatulazimu kupigana.

Nikashindilia bunduki yangu tayari na nikamwambia Nahodha kutoa bunduki yake ampe Bwana Treloni, kwani yeye ndiye mwenye shabaha, tena kwa kuwa yake iliingia maji tulipozama. Kisha niipoona Gray hana silaha, nikampa upanga wangu. Nilipompa nikafurahi kuona namna alivyoushika, nikajua kwamba huyu ni hodari sana.

Basi tulipokwenda kiasi cha hatua arobaini tukafika kando ya msitu, tukaona boma mbele yetu, lakini mara tukawaona mabaharia wale waasi saba wanakuja mbio. Walipotuona wakashtuka, wakawa wamepigwa kwanza na bumbuazi; na kabla hawajazinduka vizuri, Bwana Treloni na mimi tukapiga bunduki zetu, na mara ile ile wale watu wawili tuliowacha kulinda boma nao pia wakapiga bunduki zao. Basi bunduki nne zikalia; na adui mmoja akaanguka na wengine wakakimbia kuingia msituni.

Tulipokwisha kushindilia tena bunduki zetu, tukamkaribia yule adui aliyeanguka, tukamkuta amekwisha kufa. Basi tukafurahi, lakini mara tukasikia kishindo cha bastola na mtu mmoja wa upande wetu akaanguka. Tukamtazama, lakini mimi nilijua kuwa lazima atakufa. Basi tukamwinua na kumchukua kumpeleka ndani ya boma, na kwa bahati nzuri wale maadui hawakupiga tena bastola.

Tukamlaza yule mwenzetu aliyejeruhiwa juu ya majani.
Akauliza, “Je wenzangu, nitakufa?” Mimi nikamwambia, “Ewe rafiki yangu, kufa ni lazima ufe kwani siku zako zinakaribia kwisha.” Akasema, “Laiti ningalipata nafasi kupiga bunduki kwanza, wangalinitambua. Baadaye kidogo akasema, “Ningependa mtu aniombee dua kama desturi.” Basi akajinyosha kidogo, akafariki dunia.

Nahodha akatoa vitu vingi mifukoni mwake. Akatoa bendera ya uingereza, na Biblia na kamba, na kalamu na wino, na kitabu cha meli, na tumbaku. Kisha akatafuta mti mrefu, akaukata na kuufanya mlingoti, akautweka bendera. Halafu akauliza, “Je, ile meli ya pili itafika lini?”
Bwana Treloni akamjibu, “Niliagiza kuwa kama hatukurudi kabla ya mwisho wa Agosti meli ingine itoke bandarini kutufuata.”
Nahodha akasema, “Vema lakini naona itakuwa shida, maana chakula chetu si kingi.” Mara tukasikia kishindo cha mzinga, lakini ulipita kwa juu. Wakapiga tena mzinga, na wakati huu yake uliangukia uani lakini haikupiga kitu.

Basi Bwana Treloni akasema, “Wanajaribu kufanya nini hawa?Nadhani hawaoni nyumba wakiwa melini. Labda wanalenga kwa kubahatisha tu kwa kuona hii bendera. Ni afadhali ishushwe.”
Nahodha akasema “Sikubali hata kidogo kushusha bendera.”
Basi ikawa mara kwa mara mizinga iliangukia karibu karibu, lakini kwa bahati hapana mtu aliyepigwa. Tukaridhika, maana tulijua kuwa hawana mizinga mingi na wakiendelea hivi itakwisha upesi.

Sasa maji yakawa yamekupwa,
na nahodha wetu akataka watu waende pwani wakajaribu kuleta chakula tulichokiacha huko mashuani wakati ilipozama. Hata watu walipokwisha kwenda zao pwani, yeye akatoa kitabu cha meli akaanza kuandika hivi:

“Nahodha Smollet; Daktari Livesi; Seremala Gray; Mwenyewe Treloni; wengineo, akina Hunta na Josi, hawa ndio waliobakia katika sisi tuliotoka Uingereza. Tumefika hapa kisiwani
leo, pamoja na chakula kinachotosha muda wa siku kumi, kama tukikitumia taratibu. Mwenzetu mmoja ameuawa na adui; na Jim Hawkins, kijana ...“ Basi wakati huo mimi nilikuwa nikifikiri habari za kijana huyu Jim Hawkins, mara nikasikia mtu akipiga kelele, akiita, ‘Bwana Daktari! Nahodha! Hunta!”Basi nikamkimbiia.Kutoka mlangoni nikamwona Jim Hawkins akipanda juu ya boma salama.


SURA YA KUMI NA NANE: YALIYOTUPATA NDANI YA BOMA
(Sasa Jim Hawkins anasimulia tena hadithi. Anaanza alipoishia kwenye sura ya kumi na nne)

Ben Gun alipoiona bendera alisimama kimya, kisha alinishika mkono akisema, "ama hawa ndiyo rafiki kweli."

Mimi nikajibu, "La, nachelea, pengine hawa nao ni waasi."

Yeye akasema, "sifikiri, maana kama hawa wangalikuwa waasi, John Fedha angalipandisha bendera inayopandishwa na waasi kwa desturi yao, na bendera hiyo ni nyeusi yenye chapa ya fuvu la kichwa na mifupa. Hawa si maadui, ni marafiki."

Nikasema, "vema, basi ni afadhali nifanye haraka kwenda kwa rafiki zangu."

Akajibu, "heri uende na kama ukitaka kuonana na mimi njoo
mahali pale pale tulipoonana leo. Na atakayekuja kuniita lazima achukue kitu cheupe kiwe ndiyo dalili, tena lazima aje peke yake.”
Nikajibu, “Vema, nadhani nafahamu kwa nini hutaki kunifuata sasa. Labda una maneno unataka kuyasema kwanza kabla ya kupatana nasi. Utaonekana saa ngapi?”

Akajibu, “Tokea saa sita mchana mpaka saa kumi na mbili”
Basi tulipokwisha kupatana hivi, nalitaka kumwacha niende zangu lakini mara tukasikia kishindo cha mzinga,
na mzinga ukapita juu. Basi nikazunguka pwani, kila mara nikijificha katika miti.

Hata jua liipoanza kutua nikatokea mahali wazi; nikaona meli imetia nanga bandarini
na bendera ile aliyoitaja Ben Gun, yaani bendera ya waasi, imepandishwa. Mzinga ukalia tena na hii ilikuwa ndiyo mara ya mwisho. Basi nikalala chini kifudifudi na kutazama. Mara nikaona mabaharia wakivunja kitu kule pwani karibu na boma, nikabaini kuwa ni mtumbwi. Kwa mbali kidogo nikaona moto mkubwa, tena nikasikia sauti za watu. Nikafahamu kuwa wengine wamekunywa mvinyo.

Basi sasa nikaona kuwa labda nitaweza kurudi kwenye boma.
Nikapita pwani pwani kwenye miti, ndipo nikafika kwenye boma, nikaingia ndani salama na kwa furaha sana. Boma lenyewe liikwenda juu kimo cha mtu mrefu sana. Ndani yake mlikuwa mmejengwa nyumba kwa magogo manene. Katika ua wa boma mlikuwamo kisima. Nilipoingia ndani nikaona moto ukiwaka, lakini kwa kuwa lile tundu la kutokea moshi lilikuwa juu sana, nyumba ilijaa moshi tukawa tunakohoa kwa moshi na machozi kututoka machoni.

Humo bomani nilimwona Gray ambaye alikuwa kaumizwa usoni
kwa dharuba ya upanga, na pia nilimwona yule mtu aliyeumizwa kwa bastola amelazwa maiti na amefunikwa bendera.

Tungaliachwa kukaa kimya kufikiri, tungalikata tamaa upesi, lakini nahodha hakutuacha.
Alituita sote akatugawia zamu. Wengine washike zamu toka saa fulani mpaka saa fulani, na wengine toka saa fulani mpaka saa fulani. Na wale ambao hawakupata zamu akawambia wakatafute kuni, na wengine kuchimba kaburi. Na Bwana Livesi akaambiwa awe mpishi Mimi naliwekwa mlangoni kulinda zamu.

Basi kabla hatujapata chakula cha usiku, tukawa tumekwisha mzika
yule maiti, na wengine wamekwisha leta akiba ya kuni, lakini hazikutosha. Nahodha akasema, “Kesho asubuhi kila mtu lazima afanye bidii kuleta kuni nyingi.” Hata tulipokwisha kula tukakaa kuongea habari zilizotokea, ikaonekana kuwa tutakuwa na shida ya chakula, na waasi wakiendelea kufanya vita itatulazimu kusalimu amri kwao kwa sababu ya njaa. Azma yetu ilikuwa ni kuwaua mmoja mmoja mpaka tuwashinde. Maana kwanza walikuwa kumi na tisa, lakini sasa walibaki kumi na tano tu, wawili wengine walipata majeraha, na mwingine ameumizwa vibaya sana. Tena tulijua kwamba watajiharibia wenyewe kwaajili ya kunywa mvinyo mwingi.

Ingawa kambi yao ilikuwa mbali, mwendo wa robo saa kutoka bomani, tuliweza kujua kwamba wengi wamelewa, maana tulikuwa tukisikia kelele zao.

Basi kwakuwa nilichoka sana kwa mambo yote yaliyotokea siku ile, nililala upesi, wala sikuamka upesi. Nilipoamka niliwakuta wenzangu wote wamekwisha amka zamani tena wameleta kuni nyingi. Mara mwenzetu mmoja akasema, “Wanakuja, tena wana kitambaa cheupe mkononi kuwa dalili ya amani.Wanataka kusema nasi. Yule ni John Fedha mwenyewe." Basi nikaenda kutazama.

SURA YA KUMI NA TISA: WAASI WAMEMTUMA JOHN FEDHA KULETA UJUMBE.

Basi nilipoangalia nikaona watu
wawili, mmoja ni Jan Fedha mwenyewe, na mwingine ni baharia ameshika kitambaa cheupe mkononi; hii ndiyo alama ya kuonyesha wamekuja kwa amani kutaka kushauriana na sisi.

Ilikuwa asubuhi mapema tena kulikuwa kuna baridi sana na nchi yote ilifunikwa na ukungu.
Basi Nahodha akatuamuru tusitoke nje, akanena,
“Kila mtu akae ndani, maana nadhani hii ni hila tu.”Ndipo alipowauliza, “Nani
nyinyi? Mnataka nini? Simameni au tutakupigeni risasi!”John Fedha akajibu,
“Hii ni alama ya kuonyesha kuwa tumekuja kwa amani.”

Basi Nahodha akageuka akatwambia sisi tuliokuwa ndani, “Bwana Livesi shika zamu kwa upande wa kaskazini, Jim wewe shika zamu kwa mashariki, Gray wewe shika zamu upande wa magharibi. Basi alipofika karibu akapiga saluti kwa heshima nyingi; naye alikuwa amevaa nguo zake nzuri.

Basi alipokaribia Nahodha akasema, “Sasa umekuja, je, wataka nini?”
Akajibu, “Kwanza afadhali nikaribishe ndani nikae maana naona baridi mno”
Nahodha akajibu, “Kama ungalikuwa mtu mwaminifu hata hivi sasa ungalikuwa umekaa jikoni mwako melini.
Ni shauri yako mwenyewe.”

Basi akaingia ndani na kutuamkia sote na kutupa mikono kwa heshima, akasema, “Kazi ni kazi, basi afadhali niseme maneno yangu. Siku ile usiku mlikuwa na bahati sana na kweli nyinyi ni mahodari sana, na yaliyotokea usiku ule yalitushtua mno. Lakini nakwambia Nahodha kuwa hayatafanyika mara ya pill. Tokea sasa tutashika zamu kulinda kambi, na tena tutakuwa tukinywa mvinyo kidogo tu. Labda ulidhani kuwa sote tulilewa, lakini sivyo, mimi nilikuwa sikulewa hata kidogo ila nalichoka tu nikalala usingizi mzito. Kama ningaliamka upesi zaidi ningalimkamata, maana yule mtu alikuwa bado hajafa wakati nilipomfikia.” Basi niliposikia maneno haya nikatambua kuwa Ben Gun ndiye aliyekwenda usiku kumwua mtu mmoja katika wale waasi, tena nikafahamu kuwa sasa wamebaki watu kumi na nne tu.


Basi John Fedha akaendelea kusema, “Basi maneno yetu ni haya, twataka zile hazina.
Hayo ndiyo maneno yetu. A fadhali uzitoe na maisha yenu yatakuwa salama. Ramani mmepata, sivyo?”
Nahodha akajibu, ‘Labda.”
John Fedha akasema, “Najua kuwa mnayo, basi sasa nataka ile ramani.
Mkitupa ramani na kuacha vita, basi mwaweza kuja pamoja nasi, nami naapa yakuwa tutakuchuicheni nyote salama mpaka nchi nyingine, au kama mkitaka tutakuacheni papa hapa pamoja na chakula cha kutosha, na mkikubali hivi basi naapa kuwa meli ya kwanza itakayoonekana nitamwambia nahodha wake apitie hapa kukuchukueni.”

Basi Nahodha wetu akasema, “Basi ni hayo tu, basi?”
Akajibu, “Ni haya tu basi,
na kama hamkubali, basi hamnioni tena ila mtaona risasi zangu.”

Sasa Nahodha wetu naye akasema, “Basi nisikilize
na mimi; kama nyinyi mkikubali kuja hapa mmoja mmoja bila silaha zenu, mimi naapa nitakufungeni nyote kwa minyororo, na kukuchukueni mpaka Uingereza, mkahukumiwe kama waasi wote wanavyohukumiwa. Na kama hamkubali hayo, basi sina neno jingine. Hamwezi kuvumbua hazina wala hamwezi kuendesha meli, kwa sababu hamna mtu anayefahamu habari za kuendesha meli, wala hamwezi kutushinda katika vita; na sasa nimesimama hapa kukwambia kuwa haya ndiyo maneno yangu ya mwisho. Haya toka! Kawaambie watu wako maneno niliyoyasema.”Basi akaondoka
kwa shida akasema, “Vema lakini kabla haijapita saa nitabomoa nyumba yenu kama pipa la mvinyo. Sasa ndiyo chekeni, lakini kabla ya kupita saa moja mtakuwa mkilia na wale watakaokufa watakuwa bahati yao nzuri.” Basi akatutukana
sana kisha akaondoka pamoja na mtu wake, wakatokomea porini.
 
SURA YA ISHIRINI: SHAMBULIO

Mara walipokwisha kutoka Nahodha akarudi ndani ya nyumba, akatukuta sote tumetoka kwenye zamu zetu, tumesimama kutazama.
Lo! Alikasirika sana, akatuamuru tuondoke upesi. Ama tuliona haya sana! Baadaye akasema, “Ndugu zangu, nimemtolea maneno
makali sana John Fedha, naye asema kabla haijapita saa watakuja kutushambuiia. Kumbukeni kuwa wao ni wengi na sisi ni wachache, na kama nyinyi msipofuata amri zangu barabara tutaangamia.”

Akazunguka kutazama kila upande wa nyumba, kisha akasema, “Haya zimeni moto ili tupate kuona, kwani moshi wake unatuingia machoni. Haya wewe Bwana Livesi shika zamu mlangoni.” Halafu akatuweka kila mtu mahali pake, tukajitayarisha kwa vita.

Tukangoja muda wa saa nzima hatukuona kitu, tukawa tumechoka. Mara mwenzetu mmoja akauliza, “Je, kama nikimwona mtu ninayo ruhusa ya kumpiga risasi?” Nahodha akajibu, “Ndiyo.” Basi tukakaa vivi hivi, lakini tangu kuambiwa maneno yale macho yakatutoka kabisa, na wote tukawa macho.

Mara yule Josi akaelekeza bunduiki akapiga. Muda si muda tukasikia vishindo vya bunduki kutoka kila upande na risasi nyingine zikapiga nyumba yetu lakini hapana hata moja iliyopenya ndani. Hata moshi wa bunduki ulipoondoka tukatazama tusione kitu, kukawa kimya. Basi tukawa tunangoja. Mara ghafla, tukasikia kelele za watu, kutazama tukaona kundi la waasi linatokea upande wa kaskazini linakuja mbio penye boma. Mara na wengine wakatokea porini, wakapiga bunduki zao, ikawa moto. Wale wa kwanza wakafika, wakawa wanapanda bomani kama nyani, na Bwana Treloni na Gray wakapiga bunduki zao mfululizo mmoja, watatu wakapata risasi, wawili wakaangukiana nyuma na mmoja akaanguka mbele ndani ya ua. Lakini mmoja wao hakuumia sana, akaondoka upesi akakimbilia porini. Basi tukaona kuwa wawili wamekwisha kufa, mmoja amekimbia, lakini wanne wamekwisha ingia uani, na huku wale wanne waliojificha porini walikuwa wakipiga bunduki zao. Wale waliokwisha ingia uani wakaja mbio kwenye nyumba, tukajaribu kuwapiga, lakini kwa sababu ya kuhangaika kwingi hatukumpata hata mmoja. Basi hao wanne walitushambulia, na wakati huu walipiga makelele ili kujipa moyo, na sisi tupate kutishika.

Basi sasa mambo yakawa yamebadilika, na sisi tukawa katika hatari, maana watu wanne waliweza kutupiga, na sisi tulikuwa hatuwaoni kwa sababu ya moshi wa bunduki. Lakini naona ule moshi ulituokoa pia kwa sababu nao hawakuweza kutuona vizuri.

Basi Nohodha akapiga kelele, akanena, “Haya shime watu wangu, kila mtu ashike upanga wake tuwatokee nje tuwashambulia.” Mimi nikashika upanga wangu na mara hiyo hiyo nikapigwa mkononi lakini sikuona maumivu kwa sababu ya ghasia na mchafuko.

Lo! Ilikuwa vimoto sana. Mradi tukafanya kazi yetu barabara, na baadaye kidogo tukaona wale watu wanne waliowahi kuingia uani, watatu wamekwisha pigwa na yule aliyebaki anajaribu kupanda juu ya boma apate kutoka.

Mara ikawa kimya, wala hapakuwa na dalili ya shambulio ila wale watu watano, yaani wale wanne waliouawa ndani ya ua, na mmoja aliyepigwa akaangukia nje.

Basi tukarudi tena ndani ya nyumba.
Hata moshi ulipoanza kuondoka, tukamwona Hunta amelala chini kazimia, na Josi amepigwa risasi ya kichwa amekufa, na Nahodha amekaa katikati ya chumba amejeruhiwa. Basi tukamwuliza Nahodha hali, akasema, “Njema
sana; sasa wamebaki tisa tu, na sisi ni wanne. Kwanza tulikuwa watu saba, wao walikuwa kumi na tisa.”

SURA YA ISHIRINI NA MOJA: YALIYONIPATA BAHARINI

Wale waasi hawakurudi tena siku ile, wala hatukusikia kishindo hata mara moja kutoka upande wao. Labda mambo yaliyotokea siku ile yaliwatosha. Sasa kama alivyosema Nahodha tuliona afadhali tutengeneze mambo yetu yote tupate kupumzika. Ingawa hatari ilikuwapo, mimi na Bwana Treloni tukapika chakula chetu nje ya nyumba na hata pale nje hatukuwa na raha kwa sababu wale majeruhi jinsi walivyokuwa wakiugua.

Katika wale watu wanane waliopigwa risasi katika vita, watatu tu ndio waliokuwa hai: mwasi mmoja,
na Hunta na Nahodha; wale wawili wa kwanza walikuwa wakikata roho, na mwasi mmoja akafa wakati alipokuwa akiuguzwa na Bwana Livesi, na Hunta naye hakuamka tena.

Maumivu ya Nahodha wetu yalikuwa machungu
sana lakini hayakuwa ya kumpotezea maisha. Risasi moja ilimpiga begani ikamvunja mfupa na kuingia kidogo katika pafu, na risasi nyingine ilimpiga mguuni penye chafu, ikakata baadhi ya mishipa. Bwana Livesi alisema kuwa atapona lakini lazima akae kimya bila kutumia mguu au mkono kwa siku nyingi, wala asisemeseme ovyo ila aseme neno la haja sana tu. Maumivu yangu hayakuwa maumivu kitu na mkono ulifungwa dawa.

Baada ya kwisha kula Bwana Treloni na Bwana Livesi na Nahodha walikaa pamoja kufanya mashauri; na baadaye kidogo nikamwona Bwana Livesi akiondoka; akavaa kofia yake akatoka nje ya boma. Mimi
na Gray tulikuwa tumekaa pamoja; basi akauliza kwa nini Bwana Livesi ametoka nje? Ana wazimu nini?Mimi nikamjibu, “La, hana wazimu; nadhani anakwenda kumtafuta yule mtu wa kisiwani, Ben Gun.”

Basi nikakaa ndani, lakini jua lilikuwa kali mno, hata nikatamani kutoka nje nikatembee porini. Nilimuonea wivu bwana Livesi akipata upepo kwenye miti hali mimi nimezungukwa na maiti na damu. Basi nikaondoka nikaenda nikajaza mifuko yangu mikate kwenye mifuko ya koti langu, na nilipoona kuwa hapana mtu anayeniona nikatoka upesi. Nilikuwa na bastola mbili na baruti na risasi, basi nikajiona ni tayari kwa hatari zozote.

Baadaye nikaona kuwa nimefanya vibaya kuondoka ilhali kuna watu wawili tu walio wazima kulinda boma,
lakini kwa mambo yalivyotokea baadaye nalifanya vema sana.

Basi nikaelekea pwani, na mara naliburudika kwa upepo mzuri, nikawa nimefurahi kuondoka katika lile boma. Nikatembea pwani kidogo, mara nikatokea mahali palipo wazi, na mbele yangu naliona meli yetu, imetia nanga bandarini, na bendera ya waasi imepandishwa juu mlingotini. Mbavuni mwa meli kulikuwa na mtumbwi umefungwa, na ndani yake nikamwona John Fedha pamoja na watu wawili wengine. Baadaye kidogo wakaanza kuvuta makasia wakaja pwani kwa mbali kidogo.

Basi niipoona kuwa jua karibu kutua nikasema mwenyewe
kwa mwenyewe kuwa nikitaka kuiona ile mashua lazima nifanye haraka kuitafuta. Nakumbuka yule Ben Gun aliniambia kuwa ameificha chini ya mwamba mweupe, na nilipotazama nikaona mwamba mweupe kwa mbaali kidogo, basi nikaelekea huko, hata nilipofika giza lilikuwa limekwisha ingia, nikawa sioni kitu ila hiyo mashua yake aliyoifanya yeye mwenyewe. Ilikuwa kamamtumbwi, lakini nyepesi sana, hata niliweza kuichukua peke yangu.

Basi nikakaa kula mikate, hata jua lilipotua kabisa nikaiinua ile mashua na kuichukua mpaka ufukoni.

Kwa mbali nikaona moto katika kambi ya wale waasi,
na bandarini nikaona taa melini, basi nikaishusha ile mashua majini.

SURA YA ISHIRINI NA MBILI: MAJI YANAKUPWA.


Mashua ni kitu cha msaada sana, lakini hii ilikuwa ya matata sana. Kila nifanyavyo vyote ilitaka kurudi nyuma badala ya kwenda mbele, na hasa tabia yake ilikuwa ya kuzungukazunguka. Baadaye Ben Gun mwenyewe alikiri kuwa mashua ile ilitaka mtu mwenye kuizoea sana. Ama mimi sikujua tabia yake maana ilikuwa ikienda nisipoitaka iende. Na kwa kadiri nliivyovuta makasia, mashua ilichukuliwa na maji. Meli yetu, Hispaniola, ikonekana kwa mbali kama wingu kubwa jeusi lakini nilipoikaribia niliona milingoti na meli yenyewe; mara nikafika penye kamba iliyofungiwa nanga, nikaishika.

Kamba ilikuwa imekaza
sana kwa kuwa maji yakisukuma meli, na nyuma ya meli mawimbi madogo madogo yalikuwa yakipiga. Basi nikafikiri nikaona kama nikikata kamba meli itakuwa huru na itachukuliwa na maji. Lakini nilipozidi kufikiri nikaona kuwa nikikata kamba ingali imekazika hivi, itafyatuka kwa nguvu na pengine itanisukumia baharini.

Basi nikakaa kimya, mara nikaona kamba inalegea maana upepo ulianza kuvuma kidogo, na meli ikarudishwa mbele kufuata nanga, na kwa hivyo kamba ikalegea. Basi nilipoona hivi sikukawia tena, nikachomoa kisu changu alani nikaikata kamba. Wakati nilipokuwa nikikata kamba, nikasikia sauti za watu melini, na nikatambua sauti ya mtu mmoja jina lake Hands, na ingine ya Obraien. Tena nikaona kuwa wote wawili wamelewa sana, na bado wangali wakinywa; na wakati nilipokuwa nazidi kusikiliza mtu mmoja akatupa chupa baharini. Kulewa wakilewa lakini pia wakigombana, ndipo nikatambua kuwa kila mmoja wao alikuwa ameghadhibika kabisa.

Kutazama pwani nikaona mwangaza wa moto mkubwa na wale waasi wailkuwa wakiimba na wakati mwingine nilikuwa nikisikia hata maneno ya wimbo wao, kwani nakumbuka sana kusikia maneno haya:
“Ila mmoja tu alibaki mzima, katika hao sabini na tano waliokuja.”

Nikafikiri nikaona kuwa
ni wimbo mbaya sana kuimbwa na watu kama wao waliopata hasara kama ile waliyopata asubuhi ile. Baada ya kukata kamba nikajiona bado niko karibu na meli. Mashua ilikuwa ubavuni mwa meli na zote mbili zikichukuliwa na maji. Nilijitahidi sana niwe mbali na meli kwa kuwa nilijua kama nisipoweza kutoka lazima nitakufa baharini, na kwa bahati mikono yangu ikashika kamba ndogo iliyokuwa imefungwa juu ya meli, ndipo niliposhikwa na udadisi wa kutazama ndani ya dirisha la meli. Nikapanda pole pole nikatazama dirishani nikawaona wale watu wawili wameshikana sawasawa wamo katika kupigana.

Mara nilishuka nikaingia mashuani. Nikajaribu kulala lakini ijapokuwa nilifumba macho, nilikuwa nikiwaona wale watu wawii wenye nyuso za ukatili wameshikana kupigana kwa nguvu zao zote. Tena na huko pwani nilisikia sauti za waasi zikivuma baharini:

‘Watu kumi
na tano, Yo-ho-ho-ho!

Juu ya sanduku la mfu, Yo-ho-ho-ho!

Na chupa ya mvinyo, Yo-ho-ho-ho!


Ulevi na shetani amewaua wengine ,Yo-ho-ho-ho!

Na chupa ya mvinyo, Yo-ho-ho-ho!


Basi nikachukuliwa katika mashua ile ikanipeleka huku
na huku mpaka nikachoka nikalala, nikawa nimejisalimisha katika mikono ya Mungu, nikafikiri pengine nitachukuliwa na mawimbi nikatupwe juu ya mwamba nipotee kabisa.

Basi mwishowe nikashikwa
na usingizi, nikamwota mamangu na nyumba yetu.
 
SURA YA ISHIRINI NA TATU: SAFARI YA MASHUA

Hata nilipoamka jua lilikuwa limekwisha panda juu kabisa nikajiona niko upande
wa kusini wa Kisiwa chenye Hazina, na mawazo yangu ya kwanza yalikuwa ni kuvuta makasia na kufika pwani tena; lakini nikaliacha wazo hilo upesi, nilipotazama nikaona miamba mingi, tena nikasikia mawimbi yakivuma karibu na pwani. Nikajua kwamba nikijaribu kufika pwani kwa mahali pale lazima nitaangamia kabisa. Basi nikakumbuka maneno ya John Fedha aliposema kuwa kuna mkondo wa maji, nikafahamu kuwa nimo katika mkondo ule, nikaona afadhali nikae nitulie tu mpaka nichukuliwe mahali pengine pa kufaa zaidi.

Basi nikachukuliwa na mawimbi. Mara kwa mara niliweza kidogo kuongoza mashua kwa kutumia kasia kuwa ni usukani. Lakini pia mara kwa mara niliogopa sana jinsi mawimbi yalivyokuwa makubwa kama mlima. Basi nikachukuliwa kwa kitambo mpaka nikaona kwa mbele yetu ile meli yetu nayo imechukuliwa na mawimbi vile vile, basi nikaitazama nikaona inachukuliwa mara huku mara huko, nikajua kuwa wale waasi waliomo ndani wamelewa kabisa maana hawaangalii usukani hata kidogo.

Basi nikawa nachukuliwa kidogo kidogo, mpaka nikajiona nakaribia ile meli tena; nikazidi kutazama nikaona kweli wale watu waliokuwamo wamelewa, au wamekufa, basi hapo
nikafikiri jinsi ya kupanda melini na kuiongoza mpaka kuliko wenzangu na Nahodha mwenyewe. Basi nikajaribu kuvuta makasia pole pole nipate kufika melini, na kwa jitihada nyingi nikafaulu; nikafika karibu, na wimbi moja lilipokuja nikaruka na kwa mkono mmoja nikadaka moja ya nguzo zinazotokea hadi pembeni ya meli ili kuongeza upana wa tanga, huku nikitweta. Mara nikasikia kishindo, nikajua kuwa meli imepiga kumbo mashua yangu, nami nimeachwa katika meli Hispaniola bila njia ya kukimbiia.

SURA YA ISHIRINI NA NNE: NIMO MELINI

Basi sikukawia tena, nikatambaa juu ya bomba la nguzo ile mpaka nikafika sitahani, nikajificha kwanza.
Zile mbao za sitahani ambazo siku zote zilikuwa safi kabisa, sasa ni chafu kupita kiasi, na chupa zilikuwa zimetupwa kila upande na kugongana kila mara meli ilipokwenda mrama kwa mawimbi. Nilipokwisha kupumzika kidogo nikaanza kutambaa pole pole kutazama kila mahali ndipo niipowaona wale watu wawili, mmoja amelala chali na mikono yake amenyosha na meno yake ya wazi na Hands alikuwa amekaa ameegemea pipa, na uso wake ulikuwa kama uso wa maiti.

Basi meli ikaenda huku
na huku, ikarukaruka kama mnyama mkali, tena mara kwa mara wimbi liikuwa likija juu stahani. Na kila meli iipokwenda mrama yule mtu wa kwanza alijongejongea na Hands naye kila mara alizidi kuteremka chini mpaka akalala chali kabisa. Ndipo nilipoona wote wana alama za damu, nikaanza kufikiri kuwa watu hawa wawili wameumizana sana.

Basi nilipozidi kutazama nikamwona Hands akijaribu kujiweka vizuri, na akiugua kwa maumivu, nikamhurumia lakini pia nikakumbuka maneno niliyomsikia akisema wakati nifipojificha katika pipa la machungwa. Basi nikamwendea nikasema, “Hands, nimekuja.”
Yeye hakufanya kitu ila alinikodolea macho tu, kwani hakuwa na akili timamu.

Mwisho nikamsikia akisema, “Lete mvinyo.” Basi nikaona kuwa huyu ni taabani, nikaenda upesi kumletea mvinyo. Lo! ghasia na fujo gani zilizokuweko chini shetrini! Vitu yimetupwa ovyo na kila mahali kumevunjwavunjwa chupa. Dawa za Bwana Daktari zimetupwatupwa, na vitabu vingine vimetatuliwa.

Basi nilimletea mvinyo akanywa, akaburudika kidogo, nami nilikaa kitako kula chakula, maana nalikuwa na njaa sana. Halafu nikamwuliza, “Je, umeumia sana?”

Akajibu, “Laiti kama Bwana Daktari angekuwako, angeweza kunitibu mara moja.
Lakini mimi sina bahati. Mtazame yule amekwisha kufa, lakini haidhuru, hakuwa mwanamume.”Kisha akaniuliza, “Je, wewe unatoka wapi?”

Nikamjibu, “Mimi nimekuja hapa kutunza meli, na tokea sasa jua kuwa mimi ndiye nahodha mpaka nifike kwa Nahodha mwenyewe, na wewe lazima ufuate armri zangu zote.”

Basi akanitazama sana akaanza kukasirika. Tena nikasema, “Na zaidi ya haya niliyosema mimi sipendi kabisa kuona bendera ile kupandishwa juu ya mlingoti wa meli yangu, na tangu sasa naishusha.” Basi nikaishusha bendera ile ya waasi.

Sasa Hands akaona afadhali aje matao ya chini, akasema, “Naona heri tuwe shauri moja
mimi na wewe.”

Nikajibu, ‘vema, haya sema utakalo.”Basi akasema, “Mtu huyu amekwisha kufa, nani atakayeweza kuongoza meli?
Wewe pekee bila ya kuambiwa namna ya kufanya huwezi kabisa. Basi sasa nakwambia hivi, kama ukinipa chakula na mvinyo, na kitambaa cha kufungia majeraha yangu mimi nitakuwa nikikwambia namna ya kuiongoza.”

”Basi nikaona kuwa hili ni shauri jema, na mara nikaanza kuongoza meli yetu ifike karibu na pwani upande wa kaskazini, kwa kuwa hapo ndipo nilipokusudia kuiweka. Basi nikafunga usukani kwa kamba, nikawa namsaidia kufunga majeraha yake, kisha nikampa chakula akala akajiona hajambo sana. Sasa upepo ulipokuja ukatusaidia sana, nikaanza kuwa na tamaa tena, nikaona kwamba hata ikiwa nimekosa kwa kuondoka bomani kwetu bila ruhusa, haidhuru kwani nimeweza kuokoa meli yetu na chakula kingi kilichomo ndani yake.
 
KISIWA CHENYE HAZINA

Mtunzi: Robert Louis Stevenson,1883.
Mtafsiri: F johnson na Edwin W Brenn, 1928.
Marekebisho: Pictuss, 2021.

Pictuspublishers@gmail.com

Kinapatikana ndani ya maktaba app by pictuss.

View attachment 1783797

SURA YA KWANZA: MZEE KAPTENI



Kuna mabwana wameniomba niandike habari zote za kisiwa chenye hazina tokea mwanzo mpaka mwisho, nisifiche hata neno moja ila pale mahali palipo kisiwa chenyewe tu, kwa sababu hazina nyingine zipo mpaka leo na bado hazijafukuliwa. Basi katika mwaka huu wa kumi na saba, naanza kushika kalamu yangu na kujaribu kukumbuka zamani, wakati baba yangu alipokuwa na nyumba ya wageni. Siku moja mzee mmoja baharia alikuja kupanga kwetu. Mzee huyu alikua na kovu la pigo la upanga usoni, na hata sasa naweza kuukumbuka uso wake ulivyokuwa.

Nakumbuka sana, kwani naona kama ni jana tu, alipofika alikuwa na sanduku lake kubwa likimfuata nyuma katika gari. Alikuwa mrefu, mwenye nguvu, tena mnene, na rangi yake nyeusi kidogo; nguo zake zilikua kuukuu zilizochafukachafuka. Kucha zake zilikua zimepasukapasuka, na hilo kovu alilokuwa nalo usoni lilikua liking’aa kuliko uso wake. Tena nakumbuka sana jinsi alivyokua akitazama huku na huku alipokua akiimba wimbo mmoja ambao alipenda kuuimba mara kwa mara katika siku za baadaye:

‘Watu kumi na tano Yoh-ho-ho-ho.

Juu ya sanduku la mfu Yoh-ho-ho-ho.

Na chupa ya mvinyo Yoh-ho-ho-ho.'

Basi akaja akabisha mlangoni kwa fimbo yake, na baba yangu alipofungua mlango, akaagiza kikombe cha mvinyo, akainywa kwa kusukutua kinywa kwanza apate kuona utamu wake vizuri, kisha akasema, “Mahali hapa ni pazuri na nyumba nayo ni nzuri. Je, Rafiki, watu wengi huja hapa kupanga?”
Baba yangu akajibu, “Watu wanaokuja si wengi.”
Basi yule mzee baharia akasema “Vema basi,mahali hapa patanifaa sana.” Akamwita yule mwenye gari akamwambia alete sanduku lake, tena amsaidie kulichukua na kuliweka nyumbani. Halafu akasema, “Mimi sina makuu, kama nikipata chakula changu na mvinyo na mahali pa kutazama meli zinazopita, basi sina haja ya kitu tena.
Na mimi ninaitwa ‘Kapteni’.”Basi akampa yule mwenye gari ujira wake.

Yule mwenye gari alituambia kuwa yule mzee baharia alifika kwenye gari lililofika mjini asubuhi, akauliza habari ya nyumba za wageni, ndipo akaambiwa kuwa nyumba yetu ndiyo bora, basi akamwambia amletee sanduku lake katika gari. Basi hatukuweza kupata habari Zaidi ila hii tu.

Yule mzee Baharia yaani Kapteni alikua mtu mkimya kabisa, na mchana kutwa alishinda pwani akitazama baharini huku na huku kwa darubini yake, na kila jioni alikaa katika chumba cha kunywea mvinyo. Mara nyingi alikua akiulizwa neno alikuwa hajibu na baada ya siku chache tulimzoea na kufahamu alikua hataki kujishughulisha na watu, ndipo tukamuacha kukaa kimya. Kila jioni aliporudi kutoka kutembea aliuliza mabaharia wengine wamepita na kwanza tulifikiri ya kuwa anamtaraji rafiki mwenziwe baharia, lakini badaye tulifahamu ya kuwa alitaka kuepukana nao. Mabaharia wengine walipokuja kupanga pale nyumbani kama walivyokua wakifanya mara kwa mara, yeye huja kuchungulia dirishani kwanza ili apate kuwaona kabla hajaingia humo ndani. Tena katika siku wanazokuwapo mabaharia wengine yeye huwa kimya kupita desturi ya siku zote. Mimi nilijua habari zote, kwa sababu siku moja aliniita faraghani na kuniahidi kunipa fedha kila mwezi kuwa ujira wangu ili siku zote niwe nikiangalia sana na kumwambia mara tu nikimwona baharia mwenye mguu mmoja.

Pengine mwisho wa mwezi nilipokuwa nikienda kudai ujira wangu, alikua akinitazama tu lakini kabla ya kupita juma nzima alikua akiniita na kunipa, akaniambia nizidi kupeleleza

Kwa kufikiri kwangu mara nyingi nilikuwa nikiota ndoto; hata siku moja nikaota kumwona baharia mwenye mguu mmoja tu, niliota mguu wake mmoja umekatikia penye goti, au penye paja. Kwa kweli ndoto hizo zilinitisha mno nikaona kuwa nastahili kupewa fedha zile. Na ingawa niliogopa kuja kumwona baharia mwenye mguu mmoja, yule mzee Baharia, Kapteni nilimwogopa zaidi ya watu wote wengine. Pengine ni sababu alikunywa mvinyo kupita kiasi, na hivyo ndipo tulipopata kumsikia akiimba wimbo wake kwa sauti kubwa: ‘na chupa ya mvinyo, yo-ho-ho-ho.’ Na alipokuwa amelewa alikuwa anakuwa mtu wa kutisha kweli kweli tena hushurutisha kila mtu kuimba pamoja naye, wala hakumruhusu hata mtu mmoja atoke nje ya nyumba mpaka aishe kulewa na kushikwa na usingizi.

Hasa yaliyowatisha watu yalikuwa ni hadithi alizozisimulia, hadithi za kutisha zilizohusu kunyonga watu, kuwatosa baharini, na matendo maovu mengine katika nchi za mbali. Kwa kujigamba kwake mwenyewe alisema kwamba alikua akiishi miongoni mwa watu walio waovu kabisa kuliko wote waliojaliwa na Mungu kusafiri baharini; na maneno aliyoyatumia yalishtusha watu kwa namna yalivyokuwa ya matusi. Mara nyingi baba yangu alikua akisema kwamba sifa ya nyumba yake itaharibika kabisa, na watu wengi watakataa kuja kupanga kwake tena kwa sababu ya tabia ya mtu huyo.

Mara moja tu ndipo nilipomwona kukasirika kabisa. Ilikua siku moja bwana daktari kaja kumtazama baba yangu ambae alikuwa mgonjwa, naye huyu kapteni alilewa sana siku hiyo akaanza kuimba kwa sauti kuu:

‘Watu kumi na tano Yoh-ho-ho-ho.
Juu ya sanduku la mfu Yoh-ho-ho-ho.
Na chupa ya mvinyo Yoh-ho-ho-ho.’

Mara ya kwanza niliposikia maneno yake, ‘Sanduku la mfu’ nilifikiri kama ni sanduku lile kubwa alilokuja nalo, na mara nyingi niliota katika ndoto zile za baharia mwenye mguu mmoja. Bwana daktari ndiyo kwanza asikie wimbo ule, nae akawa hataki kelele. Alafu yule kapteni akapiga meza kwa kishindo kikubwa, na sisi tuliokuwa tumemzoea, tukajua kuwa hii ndiyo ishara ya mzee kapteni kushurutisha watu wanyamaze, ila Bwana Daktari hakuwa na habari akaendelea katika maongezi yake. Mara kapteni akageuka kumtazama na kupiga meza mara ya pili na kumtukana, akimwamuru anyamaze.

Bwana Daktari akageuka kumuuliza, "Je,wasema na mimi?” Na alipomwambia ndiyo, akasema, "Basi mimi ninayo maneno machache nitakayokwambia. Ndiyo haya: Kama wewe utaendelea kunywa namna unavokunywa sasa, dunia itafarakana na mtu mwovu na mchafu.”

Lo! Hasira zilioje! Mzee kapteni aliruka gafla na kuvuta kisu chake kutaka kumpiga Bwana Daktari. Lakini yeye hakustuka hata kidogo ila alimwambia kwa upole, "kama usipoweka mara moja hicho kisu chako katika ala yake, nakwambia kuwa utahukumiwa na kunyongwa bila shaka.”

Basi baada ya kutazamana kidogo Mzee Kapteni akaweka kisu chake katika ala na akakaa na kununa kama mbwa aliyepigwa. Bwana Daktari akaendelea kusema, “Na sasa, maadam najua kuwa wewe wakaa mtaa huu, lazima nikuangalie sana. Mimi ni kadhi wa serikali, na nikipata habari ya matata yako kidogo tu, basi nitafanya niwezavyo upate kufukuzwa katika nchi hii." Basi Akaondoka akaenda zake. Na Mzee Kapteni akakaa kimya kabisa kwa mda wa siku nyingi.


SURA YA PILI: KUTOKEA NA KUTOWEKA KWA MBWA MWEUSI

Baada ya siku chache, nakumbuka kuwa siku moja baba yangu alikuwa hajiwezi sana hata ikamlazimu mama yangu kukaa pamoja naye kumuangalia, mimi nilikuwa nikitandika meza tayari kumwandalia Mzee Kapteni, maana yeye kama ilivyokuwa desturi yake alikwenda pwani kutembea basi mara mlango ukafunguliwa na mtu akaingia ndani; mtu huyo alikua mrefu na mkono wake mmoja ulikatika vidole viwili, tena ijapokuwa alikua na upanga kiunoni, nafikiri hakuwa shujaa.

Nikamuuliza haja yake, nae akaniambia nimletee kikombe cha mvinyo; basi nilipokuwa nikienda, akaniita, "Njoo, njoo hapa karibu.” Hata nilipomkaribia akaniuliza, “Je, unamtandikia meza rafiki yangu?” Nikajibu, “Simjui rafiki yako.” Akasema, “Vema, lakini jina la rafiki yangu ni Kapteni. Ana kovu la pigo la upanga usoni. Basi sasa niambie kama rafiki yangu yumo humu.”

Nikamwambia, “Rafiki yako amekwenda kutembea pwani.”
Basi akakaa mlangoni kumngojea, na kuitazama njia niliyomwonesha. Mara kitambo kidogo tukamwona Mzee Kapteni anakuja. Yule mgeni akasema, “Haya sasa na tuingie ndani tujifiche nyuma ya mlango, ili Mzee akifika tupate kumshtusha.”

Tukaingia ndani tukajificha nyuma ya mlango, lakini nilijua kuwa huyu mgeni ni mwoga sana. Kwani upanga wake katika ala ulilegea, na mara kwa mara alikua akimeza mate kwa hofu aliyokuwa nayo.
Basi Mzee Kapiteni akaja akafungua mlango kwa kishindo akaingia ndani, wala hakugeuka kutazama mkono wa kulia au kushoto, ila akaendelea tu mpaka mezani nilipoweka chakula chake. Mara yule mgeni akamwita akasema “Mzee” na Mzee Kapteni akageuka kwa upesi kabisa, hata uso ukampauka kwa kugutuka, akawa kama mtu alieona zimwi. Yule mgeni akasema, “Je! Mzee umenisahau? Humkumbuki rafiki wa zamani?”

Mzee Kapteni akashikwa na bumbuwazi kama mwenye kigugumizi. Kisha naye akamwita, “Mbwa mweusi!” Yule mgeni akajibu, “Mimi ndiye mbwa mweusi nimekuja kukutazama rafiki yangu wa zamani. Ah Mzee! Ama mimi na wewe tumeona mambo mengi tangu vidole vyangu vilipokatika.”

Mzee Kapteni akajibu, “Kweli! Na sasa umeniona ndiyo wataka nini? Sema, wataka nini?”
Basi wakaniamuru niwaletee mvinyo, kisha wakaniambia nitoke chumbani niwaache peke yao wasemezane wala mimi nisiwepo karibu kusikiliza. Basi nikawaacha. Na kwa muda sikusikia sauti ila ngurumo tu, lakini mara nikasikia sauti ikisema, “Hapana! Hapana! Hapana kabisa! Kama ni kunyongwa vema tunyongwe sote pamoja.”

Mara tena nikasikia kelele za ghasia nyingi na matusi na vishindo vya meza na viti kutupwatupwa, na milio ya panga zikipambana. Punde nikasikia kama mtu alieumizwa sana akiugua na nikamuona yule mgeni aliyeitwa mbwa mweusi akitoka mbio na huku akifukuzwa na yule Mzee Kapteni, na damu ikimtoka yule mgeni kama maji. Mara nikamwona mzee akimtupia tena upanga kwa nguvu zake na kama ungalimpata ungalimpasua pande mbili, lakini kwa bahati haukumpata, akazidi kukimbia, ijapokuwa alikwisha umizwa sana. Mzee Kapteni akasimama kiasi kidogo kama mtu mwenye wazimu kwa hamaki, alafu akaingia ndani ya nyumba, na mara akapepesuka kutaka kuanguka. Nikamuuliza kama umeumizwa, nikatoka kwenda kumletea mvinyo ili apate kujiburudisha, lakini mara nilipotoka chumbani nikasikia mkoromo mkubwa mno, nikarudi mbio, nikamkuta amelala chini. Basi na mama yangu akawa amesikia zile kelele akatoka na kunituma kumwita Bwana Daktari.

Alipokuja Bwana Daktari tukamuuliza ameumia wapi. Bwana Daktari akajibu, “Kuumia! Hakuumia hata kidogo! Mtu huyu ameshikwa na kiharusi kama nilivyomwonya juzi.” Basi akatwaa bakuli na kisu chake kumtoa damu, na baadaye kidogo Mzee akainuka tena, na mara alipomwona Bwana Daktari akakunja uso, lakini aliponiona mimi akawa hana neno. Badaye akauliza, “Je, Mbwa mweusi yupo wapi?”

Bwana Daktari alikuwa hana habari ya mambo yaliyopita, akajibu, “Hayupo mbwa mweusi hapa ila yule wa Maungoni mwako tu. Wewe umezidi kunywa mvinyo hata umepatwa na kiharusi kama nilivyokuonya juzi, nami nimekuponya, nusura ufe.”
Basi tukamsaidia kumwinua, tukamweka kitandani na Bwana Daktari akamwambia,
“Sasa tulia usilewe, kama ukinywa hata tone moja la mvinyo fahamu ndiyo mauti yako.” Basi tukatoka chumbani na Bwana Daktari akaniambia kuwa sasa yu salama, lakini kama akishikwa na kiharusi tena atakufa.
Moja ya vitabu bora nilivyowahi kusoma na kurudia kuvisoma tena na tena zaidi ya mara tano.
 
SURA YA ISHIRINI NA TANO: HANDS

Basi upepo ulipokuwa ukivuma kutoka upande ule tuliotaka, tukauelekeza usukani kupeleka meli yetu kwa magharibi kidogo, na yule Hands akawa ananieleza namna ya kufanya, nikafuata maelezo yake. Baadaye akanita, “Nahodha, sipendi kuona maiti ya mtu huyu Obraien; afadhali umtupe baharini.”

Nikasema, “Mimi sina nguvu za kumwinua na kumtupa baharini, na tena sipendi kumgusa. Basi mwache alale hapo hapo.”
Akasema, “Meli hii haina bahati kabisa maana watu wengi wamekwisha kuuawa katika meli hii Hispaniola. Watu wengi wamefariki dunia tangu siku tuliyotoka bandari ya Bristol. Sijaona safari mbaya kama safari hii Mimi si mtu mwenye elimu nyingi, lakini wewe kijana umesoma na kuhitimu. Je, waonaje? Mtu akiisha kufa ndiyo basi au aweza kufufuka tena?”
Nikajibu, “Hands, kweli waweza kuua mwili lakini huwezi kuua roho, na labda hata sasa hivi Obraien yuko ulimwengu mwingine anatuona.”

Basi akasema, “Kama ni hivyo naona tumepoteza bure wakati wetu kwa kuwaua watu wale. Basi sasa nataka uende chini ukanipatie chupa ya mvinyo, maana ule uliyoniletea kwanza naona ni mkali mno, na labda utanilevya.”

Basi moyoni mwangu nikajua kwamba alitaka kufanya hila, maana ule mvinyo ulikuwa mzuri
sana wala si mkali mno. Nikatambua kuwa maneno yake ni uwongo tu, wala sikujua kwa sababu gani alinitaka niondoke pale, ila nilimwona kuwa hanitazami kwa macho mazuri, na pengine nilimwona akitazama huku na huku, lakini kunitazama machoni hasa hakuweza; lakini mimi sikusitasita, nikamwambia, “Vema, nitakwenda kuuchukua, lakini itakuwa kazi kuutafuta katika shetri.”

Basi nikaondoka kwa haraka, nikavua viatu vyangu nikaenda kujificha ili nipate kuona atafanya nini. Nami kweli nikaona ana hila, kwani nilipotoka ikawa yeye anajiinua, na ingawa yale majereha yalimwumiza sana lakini alijikokota hata mahali palipowekwa mgele (yaani kisu kikubwa) akakitwaa na kukificha kifuani katika koti lake, akarudi pale pale nilipomwacha.

Basi hivi ndivyo nilivyotaka kujua; yaani Hands sasa aliweza kujimudu, na juu ya hayo amepata silaha. Na maadam alifanya jitihada kujipatia silaha, basi nia yake ilionyesha waziwazi kuwa alitaka kuniua. Tena nikafikiri kidogo kuwa yeye hataki kuniua upesi, kwa maana yale ninayotaka mimi ndiyo anayoyataka yeye, yaani kuingoza meli mahali salama. Nikajua kuwa maisha yangu ni salama mpaka tuishe kazi ya kuifikisha meli kwa Nahodha.

Basi nikachukua mvinyo nikarudi sitahani, nikamkuta amejifanya
kama aliyezimia. Lakini nilipomkaribia akazinduka na akafumbua macho yake, akanywa mvinyo akaburudika.Kisha akatoa tumbako yake akanitaka nimkatie kipande atafune, akaniambia, “Tafadhali nikatie kipande cha tumbako nitafune, maana sina kisu cha kukatia. Naona kuwa hicho kitakuwa kipande changu cha mwisho kwa sababu najua nitakufa, ajali yangu imefika.”

Nikamwambia, “Vema, nitakukatia; lakini wewe mwenyewe waona kuwa
utakufa? Ikiwa ni hivyo si afadhali ujitie mikononi mwa Mungu mwenye rehema na kuomba akusamehe dhambi zako nyingi za duniani!” Basi akanywa mvinyo akasema, “Nimesafiri baharini kwa muda wa miaka thelathini sasa, nami nimeona mema na mabaya, nimeona shari na shwari, nimeona shibe na njaa, na pia nimeona mauaji. Mimi katika maisha yangu yote sijaona faida ya wema. Yeye aanzaye kupiga ndiye nimpendaye; wafu hawaumi; basi hayo ndiyo maneno yangu. Basi sasa tuuache upuuzi huu, sasa fuata maelezo yangu, uongoze meli”

Basi nikafuata kwa bidii kama alivyosema, nikaongoza meli, pengine katikati ya miamba, na pengine katikati ya mafungu na kazi ikanipendeza sana. Basi punde kidogo tukafika mahali palipofaa kutia nanga, na Hands naye akaona kuwa ndipo mahali palipofaa sana kuweka meli, pwani kabisa, inapoweza kutoka tena wakati wa maji kujaa.

Basi kazi hii ya kutazama mwendo wa meli ilinipendeza sana hata nikasahau kabisa hatari iliyo karibu, na kama isingalikuwa moyo wangu kunionya kwa namna ya ajabu, ningalianguka bila ya kupata nafasi ya kujitetea. Labda nilisikia kidogo au labda niliona kivuli, au labda nilisikia harufu kama wanyama; lakini kwa hakika nilipogeuka nikamwona Hands yupo karibu yangu amesimama tayari, kisu mkononi. Nilipotazama hivi mara sote wawili tukalia pamoja, sauti yangu ilikuwa nyembamba, lakini yake yeye ilikuwa ya kunguruma kama fahali. Basi mara akanirukia nami nikamwepa, na wakati huo nilipokuwa nikiepa niliacha kushika usukani. Nadhani kufanya hivyo ndiko kulikoniponya, maana ule usukani ulifyatuka ukampiga kifuani, ukamkomesha. Basi kabla hajaweza kunijia tena, nikaondoka mbele penye hatari nikaenda kusimama penye mlingoti nikatoa bastola yangu kutaka nimpige, wala risasi isitoke! Nikatambua kuwa baruti imeingia maji, wala haifai kitu tena. Nikajilaumu sana kwa kutokuangalia zaidi. Kwa nini sikukumbuka kutoa baruti iliyopata maji na kutia nyingine tayari? Ningalifanya hivi nisingalikuwa kama kondoo akimbiaye kuchinjwa.

Ingawa alikuwa amejeruhiwa aliweza kwenda upesi upesi, tena
uso wake ulikuwa mkali wa kutisha sana kwa kukasirika. Sikupata hata nafasi ya kushindilia bastola yangu, basi ikawa tunafukuzana, na kwa kuwa mimi nilikuwa kijana na yeye alikuwa amejeruhiwa, nikaweza kumshinda. Lakini nilisahau kuwa niko baharini, mara mawimbi makubwa yakaja na sote wawili tukasukumwa tukaanguka kwa kugongana. Kwa bahati nikaondoka na kusimama kwanza maaana yeye alijizonga na yule maiti, sasa nikawahi kutazama mahali pengine pa kujiweka salama. Basi nikafanya haraka, nikaruka nikapanda mlingoti wa kalmi, nikapanda mpaka juu katika matanga, wala sikupumzika mpaka nilipofika juu kabisa. Nilijiokoa kwa kupanda upesi upesi maana mara aliponiona akanitupia kile kisu, kikachoma katika mlingoti katikati. Basi nikakaa katika mti wa juu kabisa na kutazama chini, nikamwona anatazamajuu kwa mshangao.

Basi sikusahau tena; nikatoa bastola yangu, nikaitoa risasi
na baruti iliyoingia maji nikashindiia vingine nikawa tayari. Basi aliponiona nikifanya hivi, Hands akafadhaika sana, akaona kuwa sasa nitamshinda, na baada ya kusimama kidogo, na yeye akaanza kupanda mlingoti wa kalmi, lakini kwa taabu sana, maana kila alipojaribu kupanda alikuwa akiumia sana kwa majeraha yake. Basi nilipoona hivi nikamwelekeza bastola yangu. Nikamwambia, “Ukizidisha kupanda hatua moja ingine nitakupiga nikuue; ulisema kuwa wafu hawaumi!”

Basi akakoma pale pale, kisha akafikiri akasema, “Jim, nadhani nimefanya vibaya, heri ningalikuua, lakini
mimi sina bahati kabisa na hivi nakubali kuwa umenishinda.”

Basi niliposikia hivyo nikacheka
na huku nikimtazama tu, na mara nikaona amenitupia kisu, kikanichoma begani; nikaona kama niliyepigiliwa mlingotini kwa kisu. Lo! kwa kustuka hivi sana, bastola ikanifyatuka ikalia. Risasi haikuanguka peke yake, maana nilimwona Hands akianguka, kichwa chini miguu juu, na kutumbukia baharini.

SURA YA ISHIRINI NA SITA: VIPANDE VYA DHAHABU


Kwa namna ile meli ilivyolala ubavu naliweza kumwona yule Hands alipotumbukia baharini.
Mara akaja juu, ndipo nilipoona dalili ya damu, halafu akazama chini wala sikumwona tena. Hata yalipotulia tena, kwa kuwa maji yale yalikuwa safi, nikamwona amelala chini amekwisha kufa. Basi nilipokuwa na yakini kuwa amekufa nikaingiwa na hofu moyoni, nikaona moyo kunichafuka, nikawa kama mtu nitakaye kutapika. Damu moto ikanichuruzika mgongoni na kifuani. Kisu kile kilichonifunga juu kilikuwa kama kinachonichoma moto; lakini hasa kilichonitia hofu, nilikuwa nikiona kuwa nitatumbukia baharini karibu na maiti ya Hands. Basi nikajishika kwa mikono yangu yote miwili mpaka kucha zangu zikauma, nikafumba macho yangu ill nisione ile hatari ya chini, na kidogo kidogo moyo wangu ukawa unatulia, nikawa najiweza tena.

Kwanza nilitaka nikichomoe kile kisu kilichonifunga, lakini kilikuwa kimekaza, sikuweza kuvumilia maumivu, nikakiacha, nikawa natetemeka sana. Kusema kweli kile kisu kilikuwa kimenichoma kidogo tu, tena kilinichoma kwenye ngozi tu, na nilipokuwa natetemeka ile ngozi ikatatuka nacho kikatoka, basi na damu ikazidi kuchuruzika. Mradi sasa nilikuwa huru, lakini kilichoniweka juu ni koti langu lililokuwa limenaswa. Kwa hiyo nililitatua koti na kufanya upesi kushuka sitahani, wala sikuthubutu tena kupanda huko juu.

Basi nikaenda shetrini kutafuta kitambaa cha kufunga jeraha langu, lakini lilikuwa dogo tu, wala halikunizuia nisitumie mkono wangu. Kisha nikazunguka kukagua mwote mle melini, nikafikiri sasa kweli mimi ni nahodha kamili. Nikajipa moyo, nikatwaa maiti ya yule Obraien nikaitupa baharini

Basi sasa nikawa peke yangu melini na upepo ulipovuma nikafanya kama niwezavyo kuweka kila kitu mahali pake, nikaenda mbele nikatazama bahari nikaona kuwa sasa ni maji mafupi, basi nikashika kamba pole pole nikajishusha pwani.

Lo! Nilishukuru kutoka baharini tena! Kisha nikawa sikurudi mikono mitupu. Meli sasa tayari, waasi wametolewa na sisi tumekuwa wenyewe tena. Nia yangu sasa ilikuwa kufika bomani kwetu na kujisifu kama niwezavyo kwa mambo niliyoyatenda, kisha nikafikiri kuwa labda watanilaumu kwa jinsi nilivyotoroka, lakini pia watanishukuru kwa uhodari wangu. Basi nikaanza kuelekea bomani na moyo wangu ulijaa furaha, nikapita mahali nilipokutana na yule mtu wa kisiwani, Ben Gun, nikaenda kwa uangalifu sana na kila mara nilikuwa nikitazama huku na huku. Mwishowe giza likaingia na nikapata taabu kwa kuwa sikujua mahali pa kwenda; milima iikuwa ikionekana kama vivuli tu, na nyota hazikuwa nyingi, tena mara kwa mara nikajikwaa kwenye mawe na mizizi ya miti na majani yakanizonga miguuni.

Basi nilipokuwa nikienda, mwezi ukachomoza nikaweza kuona, lakini nilikuwa nikienda pole pole, kusudi nisije nikapigwa bunduki na wenzangu, maana wakiniona watanidhania kuwa adui. Basi kwa hivi nikapata kutokea penye kile kiwanja mbele ya boma letu, nikaona moto mkubwa ukiwaka. Nikashangaa kwa kuwa sikusikia hata sauti ya mtu mmoja, tena nilijua kuwa si desturi yetu kuwasha moto mkubwa, na pia Bwana Nahodha alihimiza kila mara tutumie kuni chache tu.

Basi nikazungukazunguka huku nikiwaza kuwa wenzangu wanafanya makosa
kwa sababa hawalindi zamu vizuri, na laiti kama wangalikuwa wakilinda zamu zao barabara lazima wangaliniona. Basi nikafika mlangoni nikachungulia ndani nisione kitu kwa giza. Nikaingia nikafikiri kwenda kulala mahali pangu, lakini tena nikafikiri jinsi watakavyostaajabu kama wakiamka asubuhi na kuniona nimo ndani! Basi wakati nilipokuwa nikienda nikajikwaa, kumbe ulikuwa mguu wa mtu aliyelala; akastuka lakini hakuamka. Mara nikasikia sauti nyembamba ikitoka gizani ikinena, “Vipande vya dhahabu! Vipande vya dhahabu! Vipande vya dhahabu! Vipande vya dhahabu! Vipande vya dhahabu.”Iliendelea vivi hivi bila kunyamaza. Lo! Nikatambua kuwa ni yule kasuku wa John Fedha aliyeitwa ‘Kapteni Flinti’ ndiye aliyekuwa mlinzi wao!

Punde si punde nikasikia sauti ya John Fedha ikiuliza, “Nani?”
Nikageuka kukimbia, nikaenda nikampiga kumbo mtu aliyekuwa akiniziba njia, nikafika mikononi mwa mtu mwingine, akanishika kwa nguvu hata sikuweza kutoka. Basi John Fedha akasema, “Lete mwenge,” na mtu mmoja akaondoka kwenda nje kuleta mwenge wa moto.


SURA YA ISHIRINI NA SABA: KATIKA KAMBI YA ADUI

Basi mwenge ulipoletwa nikaweza kuona ndani ya nyumba nikafadhaika
sana. Kumbe wale waasi wameshika boma na chakula chote, na hasa kilichonitia hofu zaidi ni vile ambavyo sikuona hata dalili ya mfungwa. Basi kwa hivyo nikaona kuwa wenzangu wote wamekwisha uawa. Mle bomani mlikuwa na waasi sita, watano walikuwa wamesimama na mmoja alikuwa amelala mgonjwa sana, na kichwa chake kilikuwa kimefungwa kitambaa kilicholoa damu.

Basi John Fedha akasema, “Ah!
Jim Hawkins kumbe ni wewe? Je, umekuja kutuamkia?” Kisha akakaa kitako juu ya pipa, akatwaa tumbako akatia kikoni mwake, akasema, “Maadam umekuja nitakupa shauri; fahamu kwamba nilikuwa nikikupenda, maana ulivyo wewe ni kama hivyo nilivyokuwa mimi wakati nilipokuwa kijana. Tangu mwanzo nilikuwa nataka uingie katika mipango yetu, na sasa hivi ni lazima ukubali kuwa hutaweza kurudi kwa wenzio maana hawakutaki sasa, na kwa hivyo lazima uwe mtu wa kundi letu.”

Basi maneno haya yakanipa moyo maana nilitambua kuwa wenzangu kuwa wahai hata sasa,
ila niliona hofu kidogo kwa kuwa wenzangu watafikiri kuwa niliwatoroka kusudi niende upande wa waasi. Naye akazidi kusema, “Je, utakubali kuwa mmoja wetu?” Mimi nikauliza, “Je, sasa ndiyo nijibu?
Basi najibu hivi, ikiwa ni lazimu nichague, kwanza nataka habari za wenzangu, tena kwa nini mnakaa hapa bomani?”

Akajibu, “Jana asubuhi alikuja Bwana Livesi amechukua alama ya amani, akaniita akasema, ‘John Fedha, meli imekwisha kwenda, sasa tufanye mapatano!’
Basi tukafanya mapatano na sisi sasa tuko hapa pamoja na chakula na kila kitu.”

Nikauliza, “Na wao?”
Tena akajibu, “Wao sijui walipokwenda.” John Fedha akaendelea kusema, “Basi, nikamwuliza Bwana Livesi, Je nyinyi sasa wangapi?’Akajibu, ‘Wanne tu na mmoja amejeruhiwa.

Yule kijana sijui aliko wala sijali.
Ametuchosha.’ Basi hayo ndiyo yaliyokuwa maneno yake.”

Nikamwuliza, “Hayo tu?”
Akajibu, “Ndiyo hayo
tu.”Nikamwuliza, “Na sasa je, ndiyo lazima nichague?
Siyo?”Akajibu, “Ndiyo hayo
tu.”

Nikajibu, “Vema, mimi si mpumbavu kwani najua mwenyewe yanayonikabili. Na yatokee yatakayatokea nami siogopi. Juu ya hayo nimeona watu wengi wakifa tangu nalipokutana nawe! Lakini lazima nikwambie maneno mawili matatu; la kwanza ni hili: Nyinyi mmo katika hali mbaya kabisa: Meli imepotea na hazina nazo zimepotea, watu wenu wengi wamepotea, na mashauri yenu yote yamekuwa ya bure kabisa. Na kama mnataka kujua nani aliyefanya hayo yote, ni mimi. Mimi nilikuwako ndani ya pipa lile la machungwa usiku ule tulipoona nchi kavu, nikasikia yote mliyokuwa mkisema, nami mara nikatoa habari kwa wenzangu. Na habari za meli, mimi ndiye niliyekata kamba yake, tena ndiye niliyemwua yule mtu aliyekuwamo ndani, tena nimeiongoza meli mpaka mahali msipoweza tena kuiona, basi mimi nina bahati, wala sina hofu hata kidogo. Sasa niue au niache ukipenda. Na neno jingine ndiyo hili: Ukiniachilia, nitasahau yote yaliyopita, na nyinyi hapo mtakapokamatwa na kuletwa mbele ya baraza kuhukumiwa nitafanya kadiri niwezavyo kukusaidieni.”Nilipokwisha haya nikanyamaza wala hapakuwa
na mtu aliyenijongelea hata kidogo wakati nilipokuwa nikisema, wote walikaa kimya wakikodoleana macho. Basi halafu wakaanza kusemezana, na mara mmoja wao akaruka na kisu chake mkononi akataka kunirukia, lakini John Fedha akamzuia, akamwambia, “Unajifikiri wewe nani? Wadhani kuwa wewe ndiye mkubwa?Ukinikasirisha kidogo tu utauawa mara moja. Basi tulia.”

Sasa wakaanza kunung’unika,
na John Fedha akauliza, “Je, yuko mtu anayetaka kushindana nami? Kama yuko asinyamaze kimya, na aseme sasa hivi. Mimi tayari, na yeye anayethubutu kusema na achukue upanga tupigane.”

Hakuna mtu aliyethubutu kusema; akaendelea kusema, “Kumbe ndiyo namna yenu, waoga kabisa. Basi sasa fahamuni ya kuwa mimi ndiye mkubwa hapa, nanyi wenyewe mlinichagua niwe mkubwa wenu mpaka hapo mtakapomchagua mtu mwingine, na sasa lazima kutii amri zangu upesi upesi. Mimi nampenda huyu kijana maana ni mwanamume barabara kushinda yeyote katika nyinyi. Mtu atakayemdhuru huyu na mimi nitamdhuru vile vile.” Basi wote wakanyamaza na yeye akawatazama tu. Kisha wao wakaondoka mmoja mmoja kwenda katika chumba cha mwisho, kusemezana huko, na mara kwa mara walikuwa wakigeuka kumtazama John Fedha. Basi John Fedha akatema mate na kuwaambia, “Ama nyie mna maneno mengi sana msemayo huko, haya niambieni maneno yenu.”Mmoja akajibu, “Niwie radhi nahodha, labda umesahau tulivyopatana.
Sisi tumekasirika, nasi hatukubali shauri lako kwa kuwa wewe mwenyewe ulisema mashauri tufanye sisi wenyewe.”

Basi wote wakatoka nje, lakini kwanza walimpa saluti John Fedha. Hata walipokwisha kutoka John Fedha akaniambia, “Angalia Jim Hawkins, wewe ukaribu sana na mauti na labda watakutesa kwanza. Tena nadhani wanataka kuniondosha katika ukubwa wamweke mwingine. Lakini nitakusaidia wewe katika balaa yoyote itakayozuka, na baadaye kama ukipata nafasi lazima unisaidie na mimi nisinyongwe, nikija kuhukumiwa.”

Nikajibu, “Nitakusaidia kadiri niwezavyo.” Basi John Fedha akasema, “Lazima ufahamu
Jim, mimi si mjinga. Najua kwamba umeiweka meli mahali salama. Uliweza namna gani sijui! Lakini siwezi kufahamu kwa sababu gani Bwana Livesi alinipa ile ramani. Sijui ni kisirani au nini.”
 
SURA YA ISHIRINI NA NANE: DOA JEUSI TENA.


Basi wale waasi waliokwenda nje kufanya shauri wakakaa muda kidogo, kisha mmoja akaingia ndani, akaomba ruhusa kuchukua mwenge
wa moto, akauchukua akatoka akaenda zake. Mimi nikaenda dirishani kuchungulia nje, nikawaona wanashughulika motoni. Baadaye kidogo wakaja mlangoni wakamsukuma mmoja ndani, naye akaja kwa John Fedha amechukua kitu mkononi mwake. Kule kumkaribia kwake alikuwa kama mtu anayeogopa, lakini John Fedha akamwambia, “Njoo, usiogope, mimi sitakudhuru. Haya nipe, mimi najua desturi.”

Basi akaja akamtia kitu mkononi, kisha akatoka nje tena.
John Fedha kutazama mkononi akasema, “Doa Jeusi! Nilijua kuwa itakuwa hivi, je, wamepata wapi karatasi? Ama hiki ni kisirani. Lo! Wamekata ukurasa mmoja wa Biblia.” Basi tukasikia mtu mmoja akisema, “Sivyo nalivyokwambia; sasa itatushukia baa kabisa.”

John Fedha akasema, “Ndiyo, maana sasa mmemaliza kabisa kazi yenu, na bila shaka nyinyi nyote mtanyongwa. Nani aliyeharibu kitabu kitukufu?” Mmoja akajibu, “Diki ndiye aliyeharibu.”
John Fedha akajibu, “Diki!
Ikiwa ni yeye nadhani atapatikana.”

Mara mtu mmoja mrefu jina lake George akasimama mbele akasema, “John Fedha, acha upuuzi wako sasa. Sisi tumekwisha kupa doa jeusi, nawe sharti utazame lilivyoandikwa na kisha waweza kusema.”

John Fedha akasema, “Ahsante George. Ama wewe siku zote ni hodari wa kushughulikia mambo. Basi nitalitazama. Ah kumbe! Nimeondoshwa katika ukubwa! Lakini nani aliyeandika hivi? Ooh! Kumbe ni maandishi yako wewe? Basi labda sasa wewe utakuwa mkubwa!”George akasema, “Huwezi kutulaghai tena, nguvu zako sasa zimekwisha. Na iliyobaki sasa ni kuchagua mkubwa mwingine, maana hiyo ndiyo desturi.” John Fedha akajibu, “Hivyo wewe wasema kuwa wajua desturi zote, lakini labda umesahau kuwa siwezi kuondolewa mpaka
nyinyi mnieleze vema kwa nini.”

George akasema, “Usidhani kuwa hatujui sababu. Kwanza toka mwanzo wa mashauri yetu wewe umeharibu kila kitu. Tena uliwaachilia adul zetu kutoka hapa. Tena ulitukataza tusiwashambulie. Na baada ya hivyo sasa wataka kumweka kijana huyu aliye mmoja wa adui zetu. Basi kwa hivi twakuona kwamba wewe si mmoja wetu tena.”

John Fedha akajibu akasema, “Vema, basi sasa nisikilizeni; kama hapo kwanza mngalifuata shauri langu tungalikuwa melini hata sasa, pamoja na hazina zote tayari. Basi nani aliyeharibu shauri langu? Si nyinyi wenyewe? Nakwambieni hivi: Kila nikifumba macho naona sote tumefungwa juu kwa kamba tunanyongwa, na huyu kijana hamwoni kuwa ni shauri zuri kumweka ili awe mdhamini wetu kesho? Na tena kwa nini sikupendelea kutoa ruhusa kushambulia adui? Je, hamwezi kukumbuka faida ya kuwa na Bwana Daktari? Hasa katika nchi hii ya maradhi? Na tena mmesahau kuwa meli nyingine itafuata meli ile iliyopotea? Na tena hamkujua kuwa nalipata ramani? Basi hii hapa!” Akaitoa akaitupa mbele yao chini. Lo! Mara walipoiona wakairukia kama paka anavyorukia panya, wakaitazamatazama na kuchekacheka kama iliyokuwa ndiyo hazina yenyewe. Basi John Fedha akasimama akasema, “Tazama George, nakuonya kuwa kama ukisema neno hata moja tena tutapigana tu. Na sasa fanyeni shauri lenu mchague mkubwa mnayemtaka, mimi nimechoka.”

Basi wakati ule alipokuwa akisema vile nyoyo za waasi wote zikageuka kabisa na wakasema kwa sauti moja, “Twakutaka wewe tu uwe mkubwa wetu.”Basi John Fedha akanitupia mimi lile Doa Jeusi lililokuwa kama kipande cha karatasi mfano wa shilingi moja, nikaliweka mfukoni na hata sasa lipo. Basi mashauri yote yakaisha, tukala tukalala.

SURA YA ISHIRINI NA TISA: NIMEFUNGWA KWA AHADI


Hata ilipofika asubuhi sisi sote tuliamka tuliposikia sauti kali ikinena, “Hodi! Boma! Boma! Mimi Bwana Daktari nimeflka.” Na kweli nilipotazama nikamwona Bwana Daktari Livesi, nikafurahi sana, lakini nalipokumbuka jinsi nilivyowatoroka wenzangu na namna nilivyowaacha katika hatari nikahuzunika sana na kutahayari.

Mara John Fedha akaenda kumwamkia akasema, “U hali gani Bwana?” Kisha akamgeukia George akamwambia aende akamsaidie Bwana Livesi kupanda juu bomani. Halafu akasema, “Bwana, nadhani wagonjwa wote hawajambo kidogo leo.”

Basi akaongea namna hii mpaka bwana Livesi alipoingia bomani.
John Fesha akasema, “Ah, Bwana leo utaona ajabu sana kwa sababu Jim Hawkins alifika hapa jana usiku.” Basi Bwana Livesi akasema, “Vema, lakini kazi ya kwanza lazima nitazame wagonjwa wangu.” Basi akaingia ndani ya nyumba akanitazama kidogo, kisha akaanza kutazama wale waasi waliokuwa wagonjwa, akawaangalia kwa wema sana kama kwamba walikuwa watu wema badala ya kuwa waasi waovu.

Basi akamtazama yule mwenye kuumia kichwa, kisha akamtazama na yule George, ndipo mmoja aliposema, “Diki anasema kuwa hajisikii vizuri.” Mara John Fedha akasema, “Ho!
Hii ni kwa sababu yeye kaharibu ile Biblia?”

Bwana Daktari akajibu, “ Hii sababu yake ni kuwa nyinyi hampambanui hewa safi, na hewa mbaya yenye sumu. Nadhani nyinyi nyote mtashikwa na homa kwa sababu ya kukaa katika kambi hii chafu.” Basi akaendelea kazi yake mpaka ikaisha, halafu akasema, “Sasa nataka mnipe nafasi ya kusema na kijana huyu.”

Mmoja akasema, “Hapana ruhusa.” Lakini John Fedha akasema, “Nyamaza wee!”
Kisha akamgeukia Bwana Livesi akasema, “Bwana najua wampenda kijana huyu nami nitakupa ruhusa useme naye ikiwa ataahidi kuwa hatoroki.” Basi nikatoa ahadi na Jan Fedha akasema, “Vema, basi Bwana Livesi hapo utakapotoka nje nitamleta Jim.” Mara Bwana Daktari akapanda tena boma akatoka nje, nami nikafuatana na John Fedha hata hapo juu alipokuwapo Bwana Livesi. Ndipo John Fedha aliponong’ona ili wale waasi wasimsikie, akasema, “Bwana kumbuka kuwa mimi nememwokoa kijana huyu na ukimwuliza yeye atakueleza yote. Basi ikiwa nitakamatwa na kuletwa kuhukumiwa kuuawa, pengine utakumbuka kunisaidia.”

Bwana Daktari akamwuliza, “Je, waogopa?” Akajibu, “La, siogopi! Lakini lazima nikiri kuwa kila nikifikiri habari ya kuhukumiwa
na kunyongwa naona hofu.” Basi alipokwisha kusema hayo akarudi bomani.

John Fedha alipokwenda zake Bwana Livesi akaniambia, “Je, Jim waona faida ya kutoroka sasa? Siwezi kukulaumu sana lakini lazima niseme haya: Kama Nahodha wetu angalikuwa mzima usingalithubutu kutoka nje, lakini ulimwona mgonjwa ukatoka. Ama tendo uliolifanya ni baya kabisa!” Basi kusikia hivi nikasikitika sana nikaanza kulia, nikasema, “Bwana usinilaumu, nimekwisha jilaumu, na sasa maisha yangu yamo mikononi mwa waasi hawa waovu. Kama si uhodari wa John Fedha wangaliniua zamani.” Basi Bwana Livesi akajibu, “Jim, siwezi kukuacha hapa. Haya!tukimbie.”

Nikajibu, “Bwana, siwezi kuvunja ahadi niliyotoa.” Akajibu, “Kweli, niwie radhi kwa
kujaribu kukuchukua. Lakini haidhuru, kimbia tu na lawama zote zitakuwa juu yangu.”

Na mimi nikajibu, “Bwana, wewe mwenyewe wajua kuwa siwezi kuvunja heshima yangu kwa kuvunja ahadi niliyotoa. John Fedha ameniamini, basi sina budi kurudi bomani. Lakini sasa nataka kukwambia neno kubwa sana. Wakati nilipokimbia nilikwenda kwa waasi melini nikafanya hila hata nikapata meli yetu iliyokuwa imetekwa, na sasa hawa waasi labda watanitesa na katika maumivu yangu pengine watanishurutisha kutoa habari za meli. Basi sasa nakwambia kuwa meli nimeipata na nimeificha katika ile hori ya kaskazini.”

Bwana Livesi akanitazama
sana kwa kustaajabu, akasema, “Meli! Wewe uliweza kuiokoa meli! Ama jambo hili ni la ajabu sana kwani naona kwa kila ufanyalo unajaaliwa kutuokoa maisha yetu, nawe wadhani kuwa sisi tutaweza kukuacha maisha yako yapotee? Wewe ndiye uliyebashiri habari za kuasi kwao; wewe tena ndiye uliyemwona Ben Gun, na kumwona Ben Gun imetokea ni kuwa jambo kubwa mno.” Basi baada ya hayo akampigia kelele John Fedha na kumwita aje kunichukua, na alipokuja akamwambia, “John Fedha, ninakunashihi usifanye haraka kuvumbua hazina.”

John Fedha akajibu, “Sina budi nifanye kama niwezavyo maana nataka nijiokoe maisha yangu na maisha ya kijana huyu kwa kuivumbua hazina.”
Bwana Livesi akasema, “Vema John Fedha, lakini nakwambia utakapovumbua hazina hiyo utavumbua na matata.”
Jan Fedha akamwuliza, “Kwa sababu gani mlitoka katika boma hili? Na kwa nini ulinipa ramani hii?”

Bwana Livesi akajibu, “Mimi siwezi kukwambia siri zetu, lakini nakuahidi kuwa nikitoka katika matata haya, nitafanya kadiri niwezavyo kukusaidia usinyongwe.”

Basi John Fedha akafurahi akasema, “Basi ninaamini kwamba utafanya hivyo usemavyo.” Kisha Bwana Livesi akasema, “Nataka ukae karibu
na kijana huyu na kama utataka msaada basi upige yowe tu. Nami sasa nakwenda zangu kutafuta msaada, na kama ukiitafuta hazina utaiona.” Basi Bwana Livesi akanipa mkono akaniaga, akatoka akaenda

zake, nami nikaingia ndani.

SURA YA THELATHINI: KUITAFUTA HAZINA—RAMANI YA FLINTI.

Baadaye mimi na John Fedha tukawa peke yetu, akasema, “Tazama Jim, kama nilivyokuokoa maisha yako, na wewe vile vile umeniokoa maisha yangu; wala sitasahau. Maana ulipokuwa ukiongea na Bwana Livesi nalimwona akikukonyeza, nikafahamu kwamba akijaribu kukushawishi utoroke. Na kama ungalitoroka basi watu hawa wangaliniua mimi, maana mimi ndiye niiyekutakia ruhusa iliupate kuongea naye. Basi sasa kazi yetu ni kuitafuta hazina nawe lazima ushikamane nami sana ndipo tutakapoweza kusaidiana.”

Basi tulipoitwa kwenda kula nikaona kuwa wanatumia chakula ovyo, na kwa hivyo siku za shida zitakuja upesi. Walipika chakula kingi sana, hata kilichobakia na kutupwa kilizidi kile kilicholiwa. Na kingine kilitupwa hata motoni, na John Fedha akakaa kimya asiwakaripie hata kidogo, ila akasema, “Ndivyo hivyo wenzangu, tena bahati njema sana mimi kuwapo hapa na kufanya mashauri kwa niaba yenu. Nimepata nilivyotaka, maana lazima wameipata ile meli sijui tu wameiweka wapi, lakini mara tukiisha ivumbua hazina, itakuwa kazi yetu kuitafuta meli mpaka tuione, ndipo itakapokuwa wale wenye kushika meli ndio wao wenye kutawala.” Basi akazungumza nao vivi hivi wakati tulipokuwa tukila chakula, na kwa njia hii aliwatuliza na kuwatia moyo tena. Akaendelea kusema, “Na huyu kijana ambaye mimi ni mdhamini wake, naona hatapata nafasi ya kuongea na rafiki zake. Niliyotaka kuyajua nimeyajua na kwa hiyo namshukuru. Na hapo tunapokwenda kutafuta hazina, mimi mwenyewe nitamchukua nipate kumwangalia vema, na nitamtunza sana sana. Basi tutakapopata hazina, na zote tumezipakia melini, ndipo hapo tutakapojilipiza kisasi.”

Basi wale watu wakachangamka
na kufurahi. Lakini mimi nalikata tamaa kabisa, nikafikiri itakavyokuwa huyu John Fedha akizighilibu pande zote mbili. Sasa amekwisha tia mkono pande zote mbili, yaani amekwisha patana na Bwana Livesi na kumtaka msaada wake, tena amejitia katika mashauri ya
waasi na kuwatia nyoyo za tamaa. Nikaona kuwa sasa ajali yangu yategemea kwa wale watakaoshinda.

Tena nikafikiri kwamba hata
kama yeye ilimlazimu kumwamini Bwana Livesi, itakuwaje kama wale waasi watagundua vitendo vyake? Bila ya shaka watatushambulia na kutuua sote mara moja. Basi kwa mawazo mengi niliyokuwa nayo, moyo wangu ukawa mzito sana. Basi tulipokwisha kula tukatoka nje tupate kuanza kazi yetu ya kutafuta hazina. Nadhani kama watu wangalituona wangalicheka sana, maana sote tulikuwa tumevaa matambara machafu, na waasi wote walikuwa wamejifunga silaha zao, na zaidi ya mambo, yule kasuku, Kapteni Flinti, alikuwa amekaa juu ya bega la John Fedha. Mimi nalifungwa kiunoni iii nisipate nafasi kutoroka. Wengine walichukua majembe, na sururu, na vyakula. Basi tukaanza kutafuta hazina. Kwanza tuliingia katika mashua ndogo tukavuta makasia mpaka tukafika penye alama iliyowekwa juu ya ramani. Labda mtakumbuka namna ilivyo andikwa nyuma ya ramani:

“Mti mrefu, mlima wa darubini upande wa kaskazini ya mashariki. Kisiwa cha mifupa.
Mashariki upande wa kusini. Hatua kumi.”

Basi tukaenda tukafika penye miti, lakini miti yote ilikuwa mirefu wala hatukuweza kutambua ni mti gani mmojawapo. Tena tukaenda mpaka penye kilima kile cha darubini na hapo tukatawanyika, kila mtu akashika njia yake ya kutafuta mahali iipofichwa ile hazina. Baada ya kwenda kidogo tukashtuka kwa kusikia sauti ya mtu aliyekuwa akipiga kelele kwa hofu. Basi sote tukaelekea upande huo kwenda kumtafuta. Tulipomwona tukamkuta anatazama chini ya mti mmoja mrefu, na pale chini tukaona mifupa ya mtu. Lo! Kuona hivi nikaona kila mmoja ameingia hofu, na tulihisi kama mifupa hiyo iliwekwa na mtu kusudi. Miguu imenyoshwa na mikono imenyoshwa kukabili miguu.

Jan Fedha akasema, “Nadhani mtu huyu amewekwa hapa kusudi awe kama dira, yaani kuonyesha njia. Ndiyo hasa, tazama namna anavyoelekeza. Huu ndio mchezo mmoja wa Kapteni Flinti. Yeye na watu sita tu walikuja, na aliwaua wote hakubaki hata mtu.” Basi wale waasi wakawa wanazungumza habari zilizokwisha pita, mpaka John Fedha akasema, “Haya ati, wacheni yaliyopita, na tushughulikie ya sasa.” Basi tukawa kazini lakini nyoyo za waasi zilijaa woga, wala hawakuwa na furaha tena, wakawa kimya-a-a!
 
SURA YA THELATHINI NA MOJA: KUTAFUTA HAZINA — SAUTI KATIKA MITI

Basi tulipofika juu ya mlima, wote tukakaa chini kupumzika kidogo. Kilima kilikuwa kimeinama kidogo kuelekea pwani, tukaona miti mingi chini yetu, na nyuma ya miti tukaona mawimbi ya bahari yakipigapiga pwani. Upande wa baharini hatukuona kitu wala mtu, kulikuwa kimya kabisa. Basi John Fedha akatoa dira yake akatazama ndipo akawaonyesha watu njia ya kwenda, akasema, “Sasa si kazi ila ni mchezo tu. Naona nitakula chakula kwanza.”

Mmmoja akajibu, “Mimi sioni njaa hata kidogo. Nadhani ni kwa sababu ya kufikiri habari za Kapteni Flinti na jinsi alivyokufa, na kwa kuona ile mifupa.”

Tangu tulipoona ile mifupa ya mtu, walisemezana
kwa kunong’ona kama waliokuwa wakiogopa kitu. Mara tukasikia sauti mwituni. Ilikuwa sauti nyembamba kali ikitetemeka na kuimba maneno yale yale:

‘Watu kumi
na tano, Yo-ho-ho-ho!

Juu ya sanduku la mfu,
Yo-ho-ho-ho!

Na chupa ya mvinyo, Yo-ho-ho-ho!’

Lo! jinsi walivyoshtuka waasi wale siwezi kueleza, wengine waliruka juu na wengine walikumbatiana kwa hofu. Mmoja akanena, “Lo, ni Flinti, ni Flinti!” Mara sauti ikanyamaza na watu wakasimama tu na kupigwa na mshangao. John Fedha akasema (hata yeye alisema kwa shida kwa namna ya midomo yake ilivyokuwa ikitetemeka), “Haya watu wangu. Haifai hivi. Msiogope hivi maana ni mtu mzima bila shaka, na sisi hatumwogopi mtu mzima.”

Basi aliposema hivi wengine wakaanza kujipa moyo, wakatulia. Mara ile sauti ikanena tena, “Dabi Makgraa! Dabi Makgraa! Lete mvinyo, Dabi Makgraa!”

Maharamia wale walikaa
kama waligeuka kuwa mawe, na baadaye mmoja wao akasema, “Basi sasa yatosha, twendeni zetu, maneno yale ndiyo maneno ya mwisho aliyosema Flinti alipokuwa akikata roho.”

Yule mtu aliyeitwa Diki akatoa Biblia yake akawa anajaribu kusoma na wengine wakawa hawana la kutenda. Lakini John Fedha hakukubali kushindwa, akasema, “Hakuna mtu katika kisiwa hiki anayemjua Dabi. Mimi nimenuia kuipata hazina ile, nami sikubali kushindwa na mtu wala pepo. Flinti sikumwogopa hapo alipokuwa hai, na Wallahi! nitamshinda tu hata hivi alivyokufa! Kuna mali nyingi katika ile hazina, na mimi sishindwi kamwe na baharia mlevi, tena amekwisha kufa.”

Lakini wale maharamia hawakuwa na la kusema, wote wakawa wametishika kabisa; basi Jan Fedha akazidi kuwatia moyo, akafikiri kidogo akasema, “Sauti ile ni ya mtu ninayemjua. Je, ni ya nani? Lo, nakumbuka! Ni sauti ya yule Ben Gun!”

Mara mwingine akaruka akasema, “Haidhuru hata
kama ikiwa ni sauti ya Ben Gun, yote mamoja pia, maana hata yeye hayuko hapa kisiwani.”

Lakini wengine wakacheka
sana wakasema, “Hatumwogopi Ben Gun, akiwa yu hai, au akiwa amekufa, hapana anayemwogopa.’

Sasa wote wakawa wamepata nguvu wakawa wanazungumza tena. Basi tukaendelea hata tukafika penye mti mrefu wa kwanza, tulipopima tukaona kuwa sio, na wa pili vile vile.

Hata tulipofika penye mti
wa tatu tukajua kuwa huu ndio. Sasa nia za watu hawa zikabadilika sana maana wote walikuwa wakifikiri hazina ile iliyofichwa chini ya kivuli cha mti huu. John Fedha akatambatamba na kunivuta mimi huku na huku kwa kamba niliyofungiwa. Na kwa namna ya uso ulivyombadiika nikatambua kuwa maadam amefika karibu na hazina, amesahau kabisa alivyotuahidi mimi na Bwana Livesi. Nikabaini kuwa nia yake sasa ni kushika hazina, kisha atafute meli apakie, halafu awaue wote ila maharamia wake.

Basi nikafadhaika sana lakini sikuwa na la kufanya. Sasa tukawa tunafuata njia iliyoonyeshwa katika ramani, tukafika kwenye alama, na mara watu waliokuwa wametangulia mbele wakasimama kimya kisha wakapiga kelele. Kwa mbele yetu tukaona shimo kubwa lililokwenda chini sana. Kutazama ndani tukaona mpini wa sururu uliovunjika, na mbao za sanduku. Ikawa dhahiri kabisa kuwa hazina zimekwisha gunduliwa na watu wengine, nazo zote zimekwisha chukuliwa!
 
SURA YA THELATHINI NA MBILI: UASI MIONGONI MWA WAASI.


Watu wote sita walisimama kama waliopagawa, lakini katika muda huo mchache, John Fedha akawa amepata akili yake, akanivuta karibu na kuninong'oneza, "Twaa bastola hii uwe tayari kwa matata." Akanipa bastola na akaanza kujongea polepole na kunivuta karibu naye mpaka tukawa tumejitenga na maharamia wale.

Mara wale maharamia wakaanza kutukana na kutoa maneno machafu na makali, na mmoja wao ambaye aliokota vipande viwili vya dhahabu, akavitupa akasema, "hivi ndivyo hazina zote? Wewe ndiye uliyetuongoza, wewe ndiye uliyeharibu mambo yote tangu mwanzo mpaka mwisho."

John Fedha akajibu, "chimbeni rafiki, chimbeni, huenda labda mkaona karanga."

"Jamani mwasikia asemavyo? Nakwambieni kuwa huyu alijua habari hizi tangu mwanzo."

Basi sasa wote wakageuka nia na mmoja wao akasema, "Jamani hawa ni watu wawili peke yao, mmoja ni kilema ambaye ndiye aliyetuleta kwenye shida hii, na mwingine ni kijana ambaye huyo nitamuua mimi. Haya sasa jamani." Akainua mkono kuanzisha vita. Mara ghafla tukasikia milio mitatu ya bunduki iliyopigwa msituni. Watu wawili wakaanguka palepale wakafa na wengine wakageuka na kuanza kukimbia kwa nguvu zao zote.

Basi nasi, John Fedha na mimi tukapiga bastola zetu. Na hapo bwana Livesi, Gray na Ben Gun wakatokea msituni na bwan Livesi akasema, "Haya wafuateni upesi, wasije wakafika kwenye meli." Loo! Tukaanza kuwafuata mbio sana, mpaka tulipojua kuwa sisi tupo katikati yao na meli ndipo tukapumzika.

John Fedha akasema, "ahsante sana bwana Livesi, umetuokoa, na kama ungalichelewa kidogo, mimi na Jim tungaliuwawa. Na wewe Ben Gun, je, habari gani?"

Sasa basi tukawa tunakwenda polepole tunashuka mlima, tukafika pwani tulipoweka mtumbwi wetu na bwana Livesi akawa anahadithia habari zote zilizotokea. Zile hazina zilikwisha vumbuliwa na mtu wa kisiwani, Ben Gun. Alipoachwa pale kisiwani kazi yake ilikuwa kutembea huku na huku kutafuta hazina mpaka akazivumbua, akazichukua na kuziweka katika pango lake. Basi alipomwambia bwana Livesi hayo, likifanywa shauri kutoka mule bomani na kuwaachia wale waasi, na sababu ya kupewa ile ramani ni kwasababu ilikuwa haina kazi tena! Na sababu ya kuwaachia kile chakula ni sababu Ben Gun alikuwa ameweka akiba ya nyama ya nbuzi mwitu.

Basi bwana Livesi alipojua kuwa mimi nimekamatwa na waasi, alifanya mpango wa kuniokoa watakapofika kwenye hazina, maana alitambua kuwa waasi wakijua kuwa hazina imekwisha vumbuliwa lazima kutakuwa utata, uasi katika waasi. Tena ndiye aliyetia fikra ya kumuambia Ben Gun aimbe kule msituni ili kusudi awatishe wale waasi.

Basi tukaingia mtumbwini na kuvuta makasia kwenda kutafuta meli yetu. Tukaiona imetoka uguoni inaelekea bandarini. Sasa tukapanda melini na kukuta kila kitu tayari. Basi tukatengeneza nanga ingine na kuifunga mahali pa kufaa, halafu tukashuka kwenda pwani kwenye lile pango, huko tukamkuta bwana Treloni ambaye alifurahi sana kuniona. Lakini akamwambia John Fedha, "wewe ni mtu mwovu kabisa, tena mwovu sana. Nimeambiwa kuwa sisi tumeahidi kutokushtaki, basi hata mimi nimekubali, lakini sina budi kukuambia kuwa damu za watu hawa zitakuwa kama mzigo juu yako mpaka mwisho wa maisha yako."

John Fedha akacheka na kusema, "asante sana bwana." Hatimaye tukaingia pangoni na kumkuta nahodha Somllet amelala mbele ya moto, na humo nikaona hazina zote zimepangwa. Kulikuwa na vyungu vikubwa vya fedha na dhahabu. Tena dhahabu zingine zilikuwa mfano wa mitalimbo mifupi, ndizo hizi zilikuwa hazina za Flinti tulizozijia. Nikafikiri sana nikaona kuwa, katika wote tuliosafiri na meli ya Hispaniola, wamekufa watu kumi na saba. Je, katika hao waliotangulia, wangapi wamekufa katika kazi hii ya kutafuta hazina?

Basi bwana nahodha akafurahi sana kuniona, akasema, "wewe ni kijana mwema Jim, lakini nadhani mimi na wewe hatutasafiri tena pamoja. Wewe una bahati sana. Oh! Na wewe John Fedha wataka nini?

John Fedha akajibu, "nimerudi kazini. " Nahodha akajibu, "vema" bila kuongeza neno jingine. Basi usiku ule tukafanya karamu, tukakaa usiku kucha tukihadithiana. Na John Fedha naye akakaa pale pale akicheka na kufurahi kama ambaye hakuwemo katika wale maharamia na wale walioasi!
 
Back
Top Bottom