Lugha nyingi zina lahaja, ikiwemo Kiswahili.
Utofauti wa lahaja huwa upo kwenye tahajiia, matamshi, uanuai wa misamiati, na kadhalika.
Ndio na ndiyo, yote ni maneno sahihi ambayo hutumika kwa kubadilishana.
Pia, ndio huwa lina maana nyingine kutegemea na muktadha unaotumika.
Neno ndio, katika muktadha mwingine na lahaja tofauti, hutamkwa kama ‘ndo’.
Maelezo yote haya ni kwa mujibu wa kamusi zangu za Kiswahili sanifu.
Wewe una kamusi yoyote ya Kiswahili hapo ulipo?
Ngeli ya
A/WA (mtu, mnyama, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndiye (katika umoja) na
ndio (katika wingi).
1. Mnyama huyu
ndiye mwenye kasi zaidi.
2. Wanachama hai
ndio sehemu ya ufanisi wa kila shirika.
Ngeli ya
KI/VI (mfano kiatu, kiti, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndicho (katika umoja) na
ndivyo (katika wingi).
1. Kiatu chake cha uongozi
ndicho kinampatia umaarufu mkubwa.
2. Viti kadhaa vya ubunge
ndivyo vitapotezwa na chama tawala.
Ngeli ya
I/ZI (mfano harakati, karatasi, kalamu, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndiyo (katika umoja) na
ndizo (katika wingi).
1. Kalamu mkononi mwa mtu mweledi
ndiyo silaha madhubuti kuliko mtutu wa bunduki.
2. Harakati za uchaguzi mkuu
ndizo zimeshika kasi nchini kuliko chochote kingine.
Ngeli ya
U/ZI (mfano uzi, ubao, ubongo, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndio (katika umoja) na
ndizo (katika wingi).
1. Ubongo
ndio ogani pekee mwilini ambayo seli zake hazina uwezo wa urajilishaji; zikifa zimekufa.
2. Mbao za mninga
ndizo mashuhuri sana, japo si imara kama za mtiki.
Ngeli ya
LI/YA (mfano shamba, gari, yai, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndilo (katika umoja) na
ndiyo (katika wingi).
1. Yai
ndilo lilianza kuwepo ndipo kuku akafuata.
2. Magari yatumiayo mfumo wa gesi
ndiyo mkombozi wa uchumi na mazingira.
Ngeli ya
U/I (mfano muziki, mfumuko, mwanga, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndio (katika umoja) na
ndiyo (katika wingi).
1. Mfumuko wa bei
ndio unawarudisha nyuma kiuchumi wafanyabiashara wengi.
2. Kwa sasa, miziki duni
ndiyo chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili duniani.
Ngeli ya
I (mfano sukari, simanzi, ari, oksijeni, surua, Dodoma, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndiyo. Haina wingi.
1. Oksijeni
ndiyo gesi ya pili kwa ujazo hewani baada ya Naitrojeni.
2. Dodoma
ndiyo imetashifika kufuatia uwekezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo.
Ngeli ya
U (mfano mchana, unadhifu, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndio. Haina wingi.
Unadhifu
ndio unambeba katika suala zima la ajira.
Ngeli ya
KI (mfano Kipemba, Kiswahili, Kichina, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndiyo (aidha, hutumika
ndicho). Haina wingi.
Kiswahili
ndiyo lugha rasmi ya taifa letu.
Kichina
ndicho kitakapiku Kiingereza hivi karibuni.
Ngeli ya
PAMUKU (mfano pangu, mwetu, kusini, nk)
Hutumia urejeshi wa
ndipo,
ndimo, na
ndiko mtawalia. Haina wingi.
Pangu
ndipo panavuja tangu masika iliyopita.
Mwetu
ndimo alianzia kufanya utafiti wake.
Kusini
ndiko kutulivu zaidi.