SURA YA TATU
‘MWANAKWETU.’
Nilionekana kama kibonzo cha Li’l Abner. Nilionekana kama mtu wa kutoka Mason, Michigan hasa. Nywele zangu ngumu na nyekundu zilikuwa zimekatwa kwa mtindo wa kishamba, na wala hata sikuwa nazipaka mafuta. Mikono ya koti langu la kijani liliishia juu kidogo ya kifundo cha mkono. Na suruali ilionyesha soksi. Juu nilivaa koti jingine kubwa na refu ambalo lilikuwa na kijani iliyokuwa tofauti kidogo na suti yangu. Muonekano wangu ulimshangaza hata Ella. Lakini baadaye alikuja kuniambia kuwa amekutana na wanafamilia wengine wa Little kutoka Georgia ambao walikuwa vituko zaidi yangu.
Ella aliniandalia chumba kizuri ghorofani. Na alikuwa mwanamke wa Georgia hasa pale alipoingia jikoni kushughulika. Alikuwa ni aina ya mpishi ambaye alijaza sahani yako kwa nyama, maharage, njegere, samaki wa kukaangwa, kabeji, viazi vitamu na mkate wa mahindi. Na kadri ulivyokula sana ndivyo alivyofurahi zaidi. …
Bado Ella aliendelea kuonekana kama mwanamke yuleyule-mkubwa na mweusi kama, na aliyezungumza bila kuuma maneno niliyeonana naye kule Mason na Lansing. Majuma mawili kabla ya mimi kufika alikuwa ametengana na mume wake wa pili, Frank. Japo sikusema lakini niliweza kujionea waziwazi jinsi ambavyo ilikuwa ni vigumu kwa mwanaume wa kawaida kuishi na mwanamke ambaye ana hulka ya kutaka kusimamia kila kitu kinachomhusu, kutia ndani mimi mwenyewe. Baada ya kukaa pale kwa siku mbili, Ella akaniambia kuwa hataki nianze kutafuta kazi mara moja, kama ambavyo watu weusi wengine ambao ni wageni wa mji hufanya. Aliniambia kuwa aliwaambia wote aliowaleta Boston kuwa wawe na subira, watembee na kusafiri kuona mji kwa mapana na marefu, na kuijua Boston ikoje hasa kabla ya kubanwa na kazi, maana hawatapata nafasi nyingine tena ya kuuona na kuujua vizuri mji wanaoishi. Aliniambia kuwa wakati wa mimi kutafuta kazi ukifika atanisaidia kutafuta.
Basi nikaanza kuzunguka maeneo ya Roxbury-Waumbeck na Homboldt, mahali ambako ni kama Sugar Hill ya Harlem, mahali ambako niliishi hapo baadaye. Niliona watu weusi ambayo tabia na maisha yao sijawahiona kwa watu weusi wowote maishani mwangu. Hii ilikuwa ni mitaa ya watu weusi waliojivuna, walijiita “Mia nne” nao waliwadharau weusi wengine walioishi maeneo waliyoyaita ya “Ghetto”, au mahali walikokuita “Town” sehemu ambayo Mary, yule dada yangu mwingine aliishi.
Wakati huo nilidhani ninachokiona huko Roxbury ni watu weusi wenye daraja la juu, watu wenye kazi nzuri na za maana. Nyumba zao tulivu zilikuwa zimepandwa nyasi sehemu ya mbele. Watu hawa walitembea barabarani wakionekana kama watu wa maana na wenye heshima zao. Sasa ndiyo naelewa kuwa nilichokuwa naona ni aina ileile ya watu weusi wa Lansing waliojiona kuwa “wamefanikiwa” kwa kufanya kazi kama wafanya usafi na wahudumu, tofauti ni kuwa hawa walikuwa kwenye jiji kubwa na walipumbazwa akili hata zaidi. Walijivuna kuwa wamestaarabika na wanajiheshimu zaidi kuliko ndugu zao walioishi maeneo ya maghetto, ambako kwa kweli kulikuwa umbali wa kurusha jiwe tu. Cha kusikitisha; kwa kudhania kuwa kuiga wazungu kutawafanya kuonekana bora, watu weusi hawa walijihangaisha na kujitesa sana.
Familia yeyote ya watu weusi iliyoishi Boston kwa miaka mingi hadi kuweza kumiliki nyumba, ilionwa kuwa ni moja wa familia za daraja la juu, haikujalisha kuwa baadhi yao walihitajika kukodisha baadhi ya vyumba vyao ili kukidhi mahitaji. Pia wazaliwa wa New England nao waliwadharau jirani zao wahamiaji kutoka kusini, kama Ella. Wakazi wengi wa Kilimani walikuwa ni watu weusi kutoka kusini kama Ella na wale wa kutoka visiwa vya Karibeani. Watu weusi wa kutoka New England na kutoka kusini waliwaita watu weusi kutoka visiwa vya Karibeani “Wayahudi Weusi.”
Mara nyingi ilikuwa ni watu weusi wa kutoka kusini na wale wa kutoka visiwa vya Karibeani ndiyo waliomiliki nyumba, na walau nyingine ya kupangisha. Wengi wa wale wa New England hawakuwa na mali kama hao.
Wakati huo kule Kilimani, yeyote aliyeweza kujiita ana “Taaluma”, waalimu, wahubiri, au wauguzi, alijiona ni bora sana. Wanadiplomasia wanaweza kuwa waliiga namna ya kujiendesha kutoka kwa watu weusi wa Roxbuy waliofanya kazi kama watu wa posta, wahudumu kwenye migahawa ya kwenye treni na makuli wa kwenye treni.
Nafikiri nane ya kumi ya watu weusi wa Roxbury, pamoja na kuwa na kazi zenye majina mazuri, kiukweli walifanya kazi za chini na kama wahudumu. “Anafanya kazi benki,” au “Mwanausalama.” Ilionekana kama wanamuongelea Rockefeller au Mellon na si mzee mfanya usafi wa benki, au mtumishi wa ofisini. Wapishi na watumishi kwenye nyumba za matajiri wa kizungu nao walijipa vyeo na kujiita majina mazuri ili waonekane watu wa maana. Sifahamu ni wanaume wangapi wa miaka ya arobaini na hamsini ambao walitoka kilimani wakiwa wamevaa kama mabalozi, suti nyeusi na shati jeupe, wakienda kufanya kazi za “Serikali,” au “Za kisheria,” au “Za Kifedha.” Wakati huo na hata sasa sijawahi acha kustaajabia jinsi ambavyo watu wengi weusi wanavyoweza kuvumilia kudharauliwa kunakotokana na kujidanganya namna ile.
Baada ya muda mfupi nikatoka Roxbury na kuanza kutembelea maeneo mengine ya Boston. Kila nilikoangalia niliona majengo ya kihistoria, sanamu na alama za matukio na watu maarufu kwenye historia. Moja ya sanamu hizo ilinistaajabisha sana: ilikuwa ni sanamu ya mtu mweusi aliyeitwa Crispus Attucks, huyu alikuwa ni mtu wa kwanza kufa katika mauaji ya Boston, sikuwahi kufahamu kitu kama hicho.
Nilizurura kila mahali. Nilitembea hadi kufika chuo kikuu cha Boston. Siku nyingine nilipanda treni ya chini ya ardhi na kushuka mahali waliposhuka watu wengi, nilikuwa nipo Cambrige. Nikazunguka kila sehemu ya chuo kikuu cha Harvard, nilikuwa nimeisha sikia juu ya chuo kikuu cha Harvard lakini sikujua mengi kukihusu. Hakuna mtu ambaye angeweza kuniambia siku ile kuwa miaka ishirini ijayo nitatoa hotuba kwenye kongamano la shule ya sheria ya Harvard.
Pia nilitembea sana kuzunguka katikati ya mji. Sikuweza kuelewa kabisa kwa nini mji una vituo viwili vikubwa vya treni. Kituo cha kaskazini na cha kusini. Nilisimama kwenye vituo vyote na kutazama watu wakija na kuondoka. Pia nilienda kushangaa-shangaa kwenye stendi ya basi ambako Ella alikuja kunipokea. Uzururaji wangu ulinifikisha hadi bandarini ambako nilisoma mawe yaliyoandikwa habari za meli zilizokuwa zikifika hapo zamani.
Nilieleza yote haya kwenye barua niliyowaandikia Wilfred, Hilda, Philbert na Reginald, niliwaeleza hayo na kuhusu mitaa myembamba iliyosakafiwa kwa mawe, na juu ya nyumba zilizobanana. Niliwasimulia juu ya maduka makubwa ambayo sijawahi kuyaona, na migahawa na hoteli za wazungu huko katikati ya mji. Nilikuwa nimeazimia kuwa nitatazama kila filamu itakayoonyeshwa kwenye zile kumbi nzuri zenye viyoyozi.
Kwenye barabara ya Massachussetts, pembeni ya moja ya kumbi hizo za sinema, kulikuwa na jumba kubwa la dansi, la Roseland. Mabango makubwa yaliwekwa mbele ya ukumbi huo, yakitangaza bendi maarufu nchini, za kizungu na za weusi zilizopata kupiga hapo. Siku ile niliona bango kubwa likitangaza ujio wa Glenn Miller juma linalofuata. Nilifikiria jinsi ambavyo karibu nyimbo zote zilizopigwa kwenye dansi kule shuleni, Mason zilikuwa za Glenn Miller. Sipatii picha umati ule ungesimama mahali ambapo bendi ya Glenn Miller ilienda kupiga jukwaani? Sikujua kama ningekuja kuijua Roseland vilivyo.
Ella akaanza kuwa na wasiwasi maana japo nilikuwa nimezurura vya kutosha, bado sikupendelea kukaa Kilimani. Mara kwa mara alikuwa akidokezea kuwa ninapaswa kuchangamana na vijana wazuri wa umri wangu ambao walikuwa wakishinda kwenye duka la dawa la Townsend, mtaa wa tatu kutoka nyumbani kwake na maeneo mengine kadhaa. Lakini kabla hata ya kuja Boston nilikuwa nawaona watu wote wa umri wangu kama “Watoto” kama nilivyomuona mdogo wangu Reginald. Mara zote nao walinitegemea kama vile nilikuwa mkubwa kwao. Mwishoni mwa juma nilipokuwa nikienda Lansing ili kuwa mbali na wazungu wa Mason, nilikuwa nashinda kwenye maeneo ya watu weusi pamoja na rafiki za Wilfred na Philbert. Japo wote walinipita umri kwa miaka kadhaa lakini nilikuwa na mwili mkubwa na nilionekana mkubwa kuliko wengi wao.
Sikupenda kumuudhi au kumuangusha Ella, lakini nilianza kwenda kwenye maeneo ya magetto pamoja na ushauri wake dhidi ya hilo. Dunia hiyo yenye migahawa ya bei rahisi, baa, vibanda vya kuchezea pool na makanisa yaliyokuwa kwenye vyumba vya maduka, ilikuwa kama sumaku kwangu.
Si tu kuwa eneo hili la Roxbury lilikuwa na amsha-amsha, lakini nilijisikia utulivu zaidi nikiwa kati ya watu weusi ambao hawakuishi kwa kujifanya. Japokuwa niliishi Kilimani, lakini hulka yangu haikuwa na haijawahi kuwa ya kujihisi bora kuliko watu weusi wengine.
Kwa mwezi wangu wote wa kwanza nilikuwa nikistaajabia kila kitu. Vijana waliovalia nadhifu, na kushinda kwenye mabanda ya pool, kona za mitaa, baa na migahawa. Walionekana wazi kuwa hawana kzi yoyote. Sikuweza kuacha kushangaa nywele zao zilizokuwa zimenyoka na kung’aa kama za wazungu; Ella aliniambia kuwa staili hiyo iliitwa, ”Conk.” Mpaka wakati huo nilikuwa sijawahi kuonja pombe wala kuvuta sigara, lakini huko nilishangaa watoto weusi wa miaka kumi na kumi na mbili, wakicheza kamari, wakigombana. Watoto hawa walikuwa na matusi sijawahiona, na waliongea maneno mengi ya mtaani yaliyokuwa mageni kabisa kwangu. Kila usiku nilipolala, maneno haya mapya yalizunguka kichwani mwangu. Nilishangazwa sana baada ya kuona mara kadhaa msichana wa kizungu na mwanaume mweusi wakitembea usiku mjini huku wameshikana mikono, na wapenzi wenye rangi tofauti wakinywa waziwazi kwenye baa na si kwa kujificha gizani kama ilivyokuwa kule Lansing. Niliwaandikia Wilfred na Philbert kuhusu hilo pia.
Ili kumshangaza Ella niliamua kujitafutia kazi mwenyewe. Siku moja kuna kitu kiliniambia niingie kwenye banda la kuchezesha pool nililokuwa nachungulia kupitia dirishani. Nilikuwa nimechungulia ukumbini mle mara nyingi. Si kwamba nilikuwa na hamu ya kucheza pool, ukweli ni kuwa sikuwahi hata kushika fimbo iliyotumika kuchezea. Nilikuwa nimevutiwa na vijana “Wajanja” waliokuwa wamesimama mle ndani, wameinamia meza kubwa ya kijani, wakicheza kamari na kupiga mipira yenye kung’aa iingie kwenye matundu. Nilipokuwa naendelea kushangaa kupitia dirishani, kitu fulani kilinifanya niamue kuingia ndani na kwenda kuongea na kijana fulani mfupi na mnene ambaye alikuwa akiwapangia wacheza pool mipira, nilisikia wakimwita “Shorty.” Siku moja alitoka nje na kuniona nimesimama, akaniambia, “Vipi, Red,” hilo lilinifanya nimuone kuwa ni mtu mwenye urafiki.
Kwa polepole kadri nilivyoweza, niliingia ndani, kisha nikakwepa watu na kuelekea nyuma ya ukumbi ambako Shorty alikuwa akiujaza mkebe poda ambayo wacheza pool hupaka kwenye mikono yao. Aligeuka kuniangalia(Baadaye Shorty alikuwa akinitania kuwa kwa kuniangalia tu kule alijua alijua mimi ni mtu wa aina gani “Dah, Kijana yule alikuwa bado akinuka ukijijini! Alisema huku akicheka. “Miguu yake ilikuwa mirefu na suruali yake fupi. Kichwa chake hakikueleweka kabisa.”
Lakini mchana wa siku ile Shorty hakuonyesha kuwa aliniona mshamba. Nilimuuliza mtu anawezaje kupata kazi kama yake.
“Kama unamaanisha kupanga mipira,” alisema Shorty. “Sifahamu kijiwe chochote cha pool maeneo haya kinachohitaji mfanyakazi. Au unamaanisha unataka utumwa wowote utakaopatikana?” “Utumwa” ulimaanisha kazi.
Aliniuliza ni kazi gani nimewahi kufanya. Nilimwambia kuwa nimewahi kuosha vyombo kwenye mgahawa huko Mason, Michigan. Karibu adondoshe mkebe wa poda. “Wa nyumbani! Mtu wangu! Acha utani, mimi pia natokea Lansing!”
Sikuwahi kumwambia Shorty na wala hakuwahi kuhisi kuwa amenizidi karibu miaka kumi. Alinichukulia kama mtu wa rika moja naye. Mwanzoni niliona aibu kumwambia ukweli, lakini baadaye sikuona haja ya kumwambia. Shorty alikuwa ameacha shule akiwa mwaka wa kwanza wa sekondari huko Lansing, aliishi na shangazi na mjomba wake kwa muda huko Detroit, na kwa miaka sita iliyopita amekuwa akiishi Roxbury na binamu yake. Lakini nilipomtajia majina ya watu na maeneo ya Lansing alikumbuka vyema, haikuchukua muda tukawa tunaongea kama watu wa kutoka mtaa mmoja. Mara moja niliweza kuona jinsi shorty alivyokuwa hana unafiki ndani yake na siwezi kuelezea bahati niliyokuwanayo kwa kumpata rafiki kama yeye.
“Huu ni mji wenye mishe nyingi,” alisema Shorty. “Wewe ni wa nyumbani, nitakuonyesha mambo yanavyoenda.” Nilisimama pale nikiwa nimekenua kama mpumbavu. “Kuna sehemu unaenda? Kama hamna nisubirie hadi nitakapotoka.”
Kitu pekee nilichokipenda mara moja kutoka kwa Shorty ni kutokuwa na unafiki. Nilipomwambia ninakoishi, aliniambia kitu ambacho tayari nilikifahamu, hakuna mtu anayewapenda watu weusi wa Kilimani. Lakini alisema kuwa anadhani dada ambaye alinipatia sehemu ya kukaa bila ya kunitoza kodi wala kunifukuza nikatafute “utumwa” hawezi kuwa mtu mbaya.
Shorty aliniambia kuwa utumwa anaofanya kwenye pool ni kwa ajili tu ya kuweka mambo sawa huku akijifunza kupiga
saxophone. Alisema kuwa miaka kadhaa nyuma baada ya kushinda bahari nasibu alinunua saxophone. “Ipo kabatini kwa ajili ya kujifunza usiku.” Shorty alikuwa akijifunza pamoja na vijana wengine na alitarajia siku moja kuanzisha bendi yake mwenyewe. “Kuna pesa nyingi unaweza kupata kwa kufanya kazi za hapa na pale huku Roxbury,” aliniambia Shorty. “Sina mpango wa kujiunga na bendi kubwa ili tu kusema nilipiga mziki na Count au Duke au mtu fulani.” Nilifikiri kuwa huo ulikuwa mpango mzuri sana. Nilitamani nami ningekuwa nimejifunza saxophone; lakini sikuwahi kupata nafasi ya kuwa karibu nayo. Alipokuwa anaenda kwenye meza ya pool na kurudi, alikuwa akiniambia; kwa sauti ya chini-ni nani kati ya waliokuwepo pale aliuza bangi, nani katoka gerezani karibuni nk. Shorty aliniambia kuwa huwa anacheza walau dola moja kila siku kwenye mchezo wa bahati nasibu, na kuwa mara tu atakaposhinda, atatumia pesa hizo kuanzisha bendi yake.
Niliabika kusema kuwa sijawahi kucheza bahati nasibu. “Hukuwa na chochote cha kucheza,” aliniambia kunifariji, “Lakini utaanza ukipata utumwa, na ukishinda unaitumia pesa hiyo kufanyia kitu cha maana.”
Alinionyesha baadhi ya wacheza kamari na baadhi ya makuwadi. “Baadhi yao wana Malaya wa kizungu,” alininong’oneza. “Sikudanganyi, nimeishatembea na Malaya wa kizungu wa dola mbili.” Alisema Shorty. “Usiku kuna mambo mengi sana yanaendelea hapa: utajionea mwenyewe.” Nilimwambia kuwa nimewaona baadhi yao. “Umewahi tembea hata na mmoja?” aliniuliza.
Aibu yangu kwa kutokuwa na uzoefu wa mambo hayo ilionekana. “Wala usione aibu, mimi nilitembea nao kadhaa kabla ya kutoka Lansing. Wale wasichana wa kipoland waliokuwa wakija kule darajani. Hapa wengi wao ni waitaliano na
wairish. Lakini haijalishi ni wa wapi lakini ni wa pekee sana! Na hakuna kitu wanapenda kama kijana mweusi.”
Mchana ule Shorty alinitambulisha kwa wacheza pool na wale wanaoshinda hapo. “Kijana wa nyumbani,” alisema. “Anatafuta utumwa, kama umesikia chochote.” Wote walisema kuwa wataangalia na kumjulisha.”
Ilipofika saa moja jioni mpanga mipira wa usiku alifika. Shorty akaniambia kuwa anatakiwa kuwahi kwenye mafunzo ya saxophone. Lakini kabla ya kuondoka alinipiatia sarafu zilizokuwa dola sita au saba hivi alizopewa na kama bakshishi. “Unachochote mfukoni mtu-wangu ?” Alisema huku akinipatia pesa hizo. Niko “Niko vizuri?” nilimwambia, nina kama dola mbili. Shorty aliniongezea dola tatu. “Za kutunisha mfuko,” alisema. Kabla hatujatoka alifungua sanduku lake la saxophone na kunionyesha. Ilikuwa saxophone ya daraja la alto iliyong’aa ”Usijali mtu-wangu. Njoo kesho. Baadhi ya watu watakuwa wameshapata utumwa kwa ajili yako.”
***