Kitabu: Maisha ya Malcom X

Kitabu: Maisha ya Malcom X

SURA YA TATU

‘MWANAKWETU.’

Nilionekana kama kibonzo cha Li’l Abner. Nilionekana kama mtu wa kutoka Mason, Michigan hasa. Nywele zangu ngumu na nyekundu zilikuwa zimekatwa kwa mtindo wa kishamba, na wala hata sikuwa nazipaka mafuta. Mikono ya koti langu la kijani liliishia juu kidogo ya kifundo cha mkono. Na suruali ilionyesha soksi. Juu nilivaa koti jingine kubwa na refu ambalo lilikuwa na kijani iliyokuwa tofauti kidogo na suti yangu. Muonekano wangu ulimshangaza hata Ella. Lakini baadaye alikuja kuniambia kuwa amekutana na wanafamilia wengine wa Little kutoka Georgia ambao walikuwa vituko zaidi yangu.

Ella aliniandalia chumba kizuri ghorofani. Na alikuwa mwanamke wa Georgia hasa pale alipoingia jikoni kushughulika. Alikuwa ni aina ya mpishi ambaye alijaza sahani yako kwa nyama, maharage, njegere, samaki wa kukaangwa, kabeji, viazi vitamu na mkate wa mahindi. Na kadri ulivyokula sana ndivyo alivyofurahi zaidi. …

Bado Ella aliendelea kuonekana kama mwanamke yuleyule-mkubwa na mweusi kama, na aliyezungumza bila kuuma maneno niliyeonana naye kule Mason na Lansing. Majuma mawili kabla ya mimi kufika alikuwa ametengana na mume wake wa pili, Frank. Japo sikusema lakini niliweza kujionea waziwazi jinsi ambavyo ilikuwa ni vigumu kwa mwanaume wa kawaida kuishi na mwanamke ambaye ana hulka ya kutaka kusimamia kila kitu kinachomhusu, kutia ndani mimi mwenyewe. Baada ya kukaa pale kwa siku mbili, Ella akaniambia kuwa hataki nianze kutafuta kazi mara moja, kama ambavyo watu weusi wengine ambao ni wageni wa mji hufanya. Aliniambia kuwa aliwaambia wote aliowaleta Boston kuwa wawe na subira, watembee na kusafiri kuona mji kwa mapana na marefu, na kuijua Boston ikoje hasa kabla ya kubanwa na kazi, maana hawatapata nafasi nyingine tena ya kuuona na kuujua vizuri mji wanaoishi. Aliniambia kuwa wakati wa mimi kutafuta kazi ukifika atanisaidia kutafuta.

Basi nikaanza kuzunguka maeneo ya Roxbury-Waumbeck na Homboldt, mahali ambako ni kama Sugar Hill ya Harlem, mahali ambako niliishi hapo baadaye. Niliona watu weusi ambayo tabia na maisha yao sijawahiona kwa watu weusi wowote maishani mwangu. Hii ilikuwa ni mitaa ya watu weusi waliojivuna, walijiita “Mia nne” nao waliwadharau weusi wengine walioishi maeneo waliyoyaita ya “Ghetto”, au mahali walikokuita “Town” sehemu ambayo Mary, yule dada yangu mwingine aliishi.

Wakati huo nilidhani ninachokiona huko Roxbury ni watu weusi wenye daraja la juu, watu wenye kazi nzuri na za maana. Nyumba zao tulivu zilikuwa zimepandwa nyasi sehemu ya mbele. Watu hawa walitembea barabarani wakionekana kama watu wa maana na wenye heshima zao. Sasa ndiyo naelewa kuwa nilichokuwa naona ni aina ileile ya watu weusi wa Lansing waliojiona kuwa “wamefanikiwa” kwa kufanya kazi kama wafanya usafi na wahudumu, tofauti ni kuwa hawa walikuwa kwenye jiji kubwa na walipumbazwa akili hata zaidi. Walijivuna kuwa wamestaarabika na wanajiheshimu zaidi kuliko ndugu zao walioishi maeneo ya maghetto, ambako kwa kweli kulikuwa umbali wa kurusha jiwe tu. Cha kusikitisha; kwa kudhania kuwa kuiga wazungu kutawafanya kuonekana bora, watu weusi hawa walijihangaisha na kujitesa sana.

Familia yeyote ya watu weusi iliyoishi Boston kwa miaka mingi hadi kuweza kumiliki nyumba, ilionwa kuwa ni moja wa familia za daraja la juu, haikujalisha kuwa baadhi yao walihitajika kukodisha baadhi ya vyumba vyao ili kukidhi mahitaji. Pia wazaliwa wa New England nao waliwadharau jirani zao wahamiaji kutoka kusini, kama Ella. Wakazi wengi wa Kilimani walikuwa ni watu weusi kutoka kusini kama Ella na wale wa kutoka visiwa vya Karibeani. Watu weusi wa kutoka New England na kutoka kusini waliwaita watu weusi kutoka visiwa vya Karibeani “Wayahudi Weusi.”

Mara nyingi ilikuwa ni watu weusi wa kutoka kusini na wale wa kutoka visiwa vya Karibeani ndiyo waliomiliki nyumba, na walau nyingine ya kupangisha. Wengi wa wale wa New England hawakuwa na mali kama hao.

Wakati huo kule Kilimani, yeyote aliyeweza kujiita ana “Taaluma”, waalimu, wahubiri, au wauguzi, alijiona ni bora sana. Wanadiplomasia wanaweza kuwa waliiga namna ya kujiendesha kutoka kwa watu weusi wa Roxbuy waliofanya kazi kama watu wa posta, wahudumu kwenye migahawa ya kwenye treni na makuli wa kwenye treni.

Nafikiri nane ya kumi ya watu weusi wa Roxbury, pamoja na kuwa na kazi zenye majina mazuri, kiukweli walifanya kazi za chini na kama wahudumu. “Anafanya kazi benki,” au “Mwanausalama.” Ilionekana kama wanamuongelea Rockefeller au Mellon na si mzee mfanya usafi wa benki, au mtumishi wa ofisini. Wapishi na watumishi kwenye nyumba za matajiri wa kizungu nao walijipa vyeo na kujiita majina mazuri ili waonekane watu wa maana. Sifahamu ni wanaume wangapi wa miaka ya arobaini na hamsini ambao walitoka kilimani wakiwa wamevaa kama mabalozi, suti nyeusi na shati jeupe, wakienda kufanya kazi za “Serikali,” au “Za kisheria,” au “Za Kifedha.” Wakati huo na hata sasa sijawahi acha kustaajabia jinsi ambavyo watu wengi weusi wanavyoweza kuvumilia kudharauliwa kunakotokana na kujidanganya namna ile.

Baada ya muda mfupi nikatoka Roxbury na kuanza kutembelea maeneo mengine ya Boston. Kila nilikoangalia niliona majengo ya kihistoria, sanamu na alama za matukio na watu maarufu kwenye historia. Moja ya sanamu hizo ilinistaajabisha sana: ilikuwa ni sanamu ya mtu mweusi aliyeitwa Crispus Attucks, huyu alikuwa ni mtu wa kwanza kufa katika mauaji ya Boston, sikuwahi kufahamu kitu kama hicho.

Nilizurura kila mahali. Nilitembea hadi kufika chuo kikuu cha Boston. Siku nyingine nilipanda treni ya chini ya ardhi na kushuka mahali waliposhuka watu wengi, nilikuwa nipo Cambrige. Nikazunguka kila sehemu ya chuo kikuu cha Harvard, nilikuwa nimeisha sikia juu ya chuo kikuu cha Harvard lakini sikujua mengi kukihusu. Hakuna mtu ambaye angeweza kuniambia siku ile kuwa miaka ishirini ijayo nitatoa hotuba kwenye kongamano la shule ya sheria ya Harvard.

Pia nilitembea sana kuzunguka katikati ya mji. Sikuweza kuelewa kabisa kwa nini mji una vituo viwili vikubwa vya treni. Kituo cha kaskazini na cha kusini. Nilisimama kwenye vituo vyote na kutazama watu wakija na kuondoka. Pia nilienda kushangaa-shangaa kwenye stendi ya basi ambako Ella alikuja kunipokea. Uzururaji wangu ulinifikisha hadi bandarini ambako nilisoma mawe yaliyoandikwa habari za meli zilizokuwa zikifika hapo zamani.

Nilieleza yote haya kwenye barua niliyowaandikia Wilfred, Hilda, Philbert na Reginald, niliwaeleza hayo na kuhusu mitaa myembamba iliyosakafiwa kwa mawe, na juu ya nyumba zilizobanana. Niliwasimulia juu ya maduka makubwa ambayo sijawahi kuyaona, na migahawa na hoteli za wazungu huko katikati ya mji. Nilikuwa nimeazimia kuwa nitatazama kila filamu itakayoonyeshwa kwenye zile kumbi nzuri zenye viyoyozi.

Kwenye barabara ya Massachussetts, pembeni ya moja ya kumbi hizo za sinema, kulikuwa na jumba kubwa la dansi, la Roseland. Mabango makubwa yaliwekwa mbele ya ukumbi huo, yakitangaza bendi maarufu nchini, za kizungu na za weusi zilizopata kupiga hapo. Siku ile niliona bango kubwa likitangaza ujio wa Glenn Miller juma linalofuata. Nilifikiria jinsi ambavyo karibu nyimbo zote zilizopigwa kwenye dansi kule shuleni, Mason zilikuwa za Glenn Miller. Sipatii picha umati ule ungesimama mahali ambapo bendi ya Glenn Miller ilienda kupiga jukwaani? Sikujua kama ningekuja kuijua Roseland vilivyo.

Ella akaanza kuwa na wasiwasi maana japo nilikuwa nimezurura vya kutosha, bado sikupendelea kukaa Kilimani. Mara kwa mara alikuwa akidokezea kuwa ninapaswa kuchangamana na vijana wazuri wa umri wangu ambao walikuwa wakishinda kwenye duka la dawa la Townsend, mtaa wa tatu kutoka nyumbani kwake na maeneo mengine kadhaa. Lakini kabla hata ya kuja Boston nilikuwa nawaona watu wote wa umri wangu kama “Watoto” kama nilivyomuona mdogo wangu Reginald. Mara zote nao walinitegemea kama vile nilikuwa mkubwa kwao. Mwishoni mwa juma nilipokuwa nikienda Lansing ili kuwa mbali na wazungu wa Mason, nilikuwa nashinda kwenye maeneo ya watu weusi pamoja na rafiki za Wilfred na Philbert. Japo wote walinipita umri kwa miaka kadhaa lakini nilikuwa na mwili mkubwa na nilionekana mkubwa kuliko wengi wao.

Sikupenda kumuudhi au kumuangusha Ella, lakini nilianza kwenda kwenye maeneo ya magetto pamoja na ushauri wake dhidi ya hilo. Dunia hiyo yenye migahawa ya bei rahisi, baa, vibanda vya kuchezea pool na makanisa yaliyokuwa kwenye vyumba vya maduka, ilikuwa kama sumaku kwangu.

Si tu kuwa eneo hili la Roxbury lilikuwa na amsha-amsha, lakini nilijisikia utulivu zaidi nikiwa kati ya watu weusi ambao hawakuishi kwa kujifanya. Japokuwa niliishi Kilimani, lakini hulka yangu haikuwa na haijawahi kuwa ya kujihisi bora kuliko watu weusi wengine.

Kwa mwezi wangu wote wa kwanza nilikuwa nikistaajabia kila kitu. Vijana waliovalia nadhifu, na kushinda kwenye mabanda ya pool, kona za mitaa, baa na migahawa. Walionekana wazi kuwa hawana kzi yoyote. Sikuweza kuacha kushangaa nywele zao zilizokuwa zimenyoka na kung’aa kama za wazungu; Ella aliniambia kuwa staili hiyo iliitwa, ”Conk.” Mpaka wakati huo nilikuwa sijawahi kuonja pombe wala kuvuta sigara, lakini huko nilishangaa watoto weusi wa miaka kumi na kumi na mbili, wakicheza kamari, wakigombana. Watoto hawa walikuwa na matusi sijawahiona, na waliongea maneno mengi ya mtaani yaliyokuwa mageni kabisa kwangu. Kila usiku nilipolala, maneno haya mapya yalizunguka kichwani mwangu. Nilishangazwa sana baada ya kuona mara kadhaa msichana wa kizungu na mwanaume mweusi wakitembea usiku mjini huku wameshikana mikono, na wapenzi wenye rangi tofauti wakinywa waziwazi kwenye baa na si kwa kujificha gizani kama ilivyokuwa kule Lansing. Niliwaandikia Wilfred na Philbert kuhusu hilo pia.

Ili kumshangaza Ella niliamua kujitafutia kazi mwenyewe. Siku moja kuna kitu kiliniambia niingie kwenye banda la kuchezesha pool nililokuwa nachungulia kupitia dirishani. Nilikuwa nimechungulia ukumbini mle mara nyingi. Si kwamba nilikuwa na hamu ya kucheza pool, ukweli ni kuwa sikuwahi hata kushika fimbo iliyotumika kuchezea. Nilikuwa nimevutiwa na vijana “Wajanja” waliokuwa wamesimama mle ndani, wameinamia meza kubwa ya kijani, wakicheza kamari na kupiga mipira yenye kung’aa iingie kwenye matundu. Nilipokuwa naendelea kushangaa kupitia dirishani, kitu fulani kilinifanya niamue kuingia ndani na kwenda kuongea na kijana fulani mfupi na mnene ambaye alikuwa akiwapangia wacheza pool mipira, nilisikia wakimwita “Shorty.” Siku moja alitoka nje na kuniona nimesimama, akaniambia, “Vipi, Red,” hilo lilinifanya nimuone kuwa ni mtu mwenye urafiki.

Kwa polepole kadri nilivyoweza, niliingia ndani, kisha nikakwepa watu na kuelekea nyuma ya ukumbi ambako Shorty alikuwa akiujaza mkebe poda ambayo wacheza pool hupaka kwenye mikono yao. Aligeuka kuniangalia(Baadaye Shorty alikuwa akinitania kuwa kwa kuniangalia tu kule alijua alijua mimi ni mtu wa aina gani “Dah, Kijana yule alikuwa bado akinuka ukijijini! Alisema huku akicheka. “Miguu yake ilikuwa mirefu na suruali yake fupi. Kichwa chake hakikueleweka kabisa.”

Lakini mchana wa siku ile Shorty hakuonyesha kuwa aliniona mshamba. Nilimuuliza mtu anawezaje kupata kazi kama yake.

“Kama unamaanisha kupanga mipira,” alisema Shorty. “Sifahamu kijiwe chochote cha pool maeneo haya kinachohitaji mfanyakazi. Au unamaanisha unataka utumwa wowote utakaopatikana?” “Utumwa” ulimaanisha kazi.

Aliniuliza ni kazi gani nimewahi kufanya. Nilimwambia kuwa nimewahi kuosha vyombo kwenye mgahawa huko Mason, Michigan. Karibu adondoshe mkebe wa poda. “Wa nyumbani! Mtu wangu! Acha utani, mimi pia natokea Lansing!”

Sikuwahi kumwambia Shorty na wala hakuwahi kuhisi kuwa amenizidi karibu miaka kumi. Alinichukulia kama mtu wa rika moja naye. Mwanzoni niliona aibu kumwambia ukweli, lakini baadaye sikuona haja ya kumwambia. Shorty alikuwa ameacha shule akiwa mwaka wa kwanza wa sekondari huko Lansing, aliishi na shangazi na mjomba wake kwa muda huko Detroit, na kwa miaka sita iliyopita amekuwa akiishi Roxbury na binamu yake. Lakini nilipomtajia majina ya watu na maeneo ya Lansing alikumbuka vyema, haikuchukua muda tukawa tunaongea kama watu wa kutoka mtaa mmoja. Mara moja niliweza kuona jinsi shorty alivyokuwa hana unafiki ndani yake na siwezi kuelezea bahati niliyokuwanayo kwa kumpata rafiki kama yeye.

“Huu ni mji wenye mishe nyingi,” alisema Shorty. “Wewe ni wa nyumbani, nitakuonyesha mambo yanavyoenda.” Nilisimama pale nikiwa nimekenua kama mpumbavu. “Kuna sehemu unaenda? Kama hamna nisubirie hadi nitakapotoka.”

Kitu pekee nilichokipenda mara moja kutoka kwa Shorty ni kutokuwa na unafiki. Nilipomwambia ninakoishi, aliniambia kitu ambacho tayari nilikifahamu, hakuna mtu anayewapenda watu weusi wa Kilimani. Lakini alisema kuwa anadhani dada ambaye alinipatia sehemu ya kukaa bila ya kunitoza kodi wala kunifukuza nikatafute “utumwa” hawezi kuwa mtu mbaya.

Shorty aliniambia kuwa utumwa anaofanya kwenye pool ni kwa ajili tu ya kuweka mambo sawa huku akijifunza kupiga saxophone. Alisema kuwa miaka kadhaa nyuma baada ya kushinda bahari nasibu alinunua saxophone. “Ipo kabatini kwa ajili ya kujifunza usiku.” Shorty alikuwa akijifunza pamoja na vijana wengine na alitarajia siku moja kuanzisha bendi yake mwenyewe. “Kuna pesa nyingi unaweza kupata kwa kufanya kazi za hapa na pale huku Roxbury,” aliniambia Shorty. “Sina mpango wa kujiunga na bendi kubwa ili tu kusema nilipiga mziki na Count au Duke au mtu fulani.” Nilifikiri kuwa huo ulikuwa mpango mzuri sana. Nilitamani nami ningekuwa nimejifunza saxophone; lakini sikuwahi kupata nafasi ya kuwa karibu nayo. Alipokuwa anaenda kwenye meza ya pool na kurudi, alikuwa akiniambia; kwa sauti ya chini-ni nani kati ya waliokuwepo pale aliuza bangi, nani katoka gerezani karibuni nk. Shorty aliniambia kuwa huwa anacheza walau dola moja kila siku kwenye mchezo wa bahati nasibu, na kuwa mara tu atakaposhinda, atatumia pesa hizo kuanzisha bendi yake.

Niliabika kusema kuwa sijawahi kucheza bahati nasibu. “Hukuwa na chochote cha kucheza,” aliniambia kunifariji, “Lakini utaanza ukipata utumwa, na ukishinda unaitumia pesa hiyo kufanyia kitu cha maana.”

Alinionyesha baadhi ya wacheza kamari na baadhi ya makuwadi. “Baadhi yao wana Malaya wa kizungu,” alininong’oneza. “Sikudanganyi, nimeishatembea na Malaya wa kizungu wa dola mbili.” Alisema Shorty. “Usiku kuna mambo mengi sana yanaendelea hapa: utajionea mwenyewe.” Nilimwambia kuwa nimewaona baadhi yao. “Umewahi tembea hata na mmoja?” aliniuliza.

Aibu yangu kwa kutokuwa na uzoefu wa mambo hayo ilionekana. “Wala usione aibu, mimi nilitembea nao kadhaa kabla ya kutoka Lansing. Wale wasichana wa kipoland waliokuwa wakija kule darajani. Hapa wengi wao ni waitaliano na wairish. Lakini haijalishi ni wa wapi lakini ni wa pekee sana! Na hakuna kitu wanapenda kama kijana mweusi.”

Mchana ule Shorty alinitambulisha kwa wacheza pool na wale wanaoshinda hapo. “Kijana wa nyumbani,” alisema. “Anatafuta utumwa, kama umesikia chochote.” Wote walisema kuwa wataangalia na kumjulisha.”

Ilipofika saa moja jioni mpanga mipira wa usiku alifika. Shorty akaniambia kuwa anatakiwa kuwahi kwenye mafunzo ya saxophone. Lakini kabla ya kuondoka alinipiatia sarafu zilizokuwa dola sita au saba hivi alizopewa na kama bakshishi. “Unachochote mfukoni mtu-wangu ?” Alisema huku akinipatia pesa hizo. Niko “Niko vizuri?” nilimwambia, nina kama dola mbili. Shorty aliniongezea dola tatu. “Za kutunisha mfuko,” alisema. Kabla hatujatoka alifungua sanduku lake la saxophone na kunionyesha. Ilikuwa saxophone ya daraja la alto iliyong’aa ”Usijali mtu-wangu. Njoo kesho. Baadhi ya watu watakuwa wameshapata utumwa kwa ajili yako.”
***​
 
Sura ya tatu inaendelea.

Nilipofika nyumbani Ella aliniambia kuwa kuna simu iliingia ya mtu aliyejiita Shorty. Alikuwa ameacha ujumbe kuwa huko kwenye ukumbi wa Roseland, kijana mng’arisha viatu alikuwa akiacha kazi usiku huo, na Shorty alikuwa amemwambia aniwekee kazi.

“Malcom, hauna uzoefu wowote wa kung’arisha viatu,” alisema Ella. Sauti yake na jinsi alivyoongea ilionyesha kuwa hakufurahia mimi kufanya kazi ile. Lakini sikujali, tayari nilikuwa nimejawa na furaha ya kuwa karibu na baadhi ya bendi maarufu zaidi duniani. Niliondoka mara moja, hata sikusubiri kula chakula cha usiku.

Ukumbi ulikuwa tayari umechangamka nilipofika pale. Mlinzi wa mlangoni alikuwa akiwaingiza wanamuziki wa bendi ya Benny Goodman. Nilimwambia kuwa nilitaka kuonana na kijana mng’arisha viatu, Freddie.

“Wewe ndiye kijana mpya?” aliuliza. Nilimwambia kuwa nafikiri hivyo, akacheka. “Pengine nawe pia utashinda bahati nasibu na kupata Cadillac.” Aliniambia kuwa nitampata Freddie kwenye maliwato ya wanaume yaliyokuwa ghorofa ya pili.

Lakini kabla ya kupanda nilichungulia kidogo ukumbini. Sikuweza kuamini ukubwa wa sehemu ya kuchezea dansi! Mbele jukwaani wanamuziki wa bendi ya Benny Goodman walionekana wakizunguka huku na huku, wakiongea na kucheka huku wakipanga vifaa vyao.

Kule ghorofani nilipokelewa na kijana mmoja mwembamba na wa rangi ya maji ya kunde, nywele zake alikuwa ameweka dawa. “Wewe ndiye jamaa yake na Shorty?” nilimwambia ndiyo naye akasema yeye anaitwa Freddie. “Alinipigia, Yaani kusikia tu nimeshinda fedha nyingi akafikiri mara moja kuwa nitaacha kazi.” Nikamwambia Freddie kuwa mlinzi wa mlangoni alikuwa amezungumza kuhusu Cadillac. Alicheka na kusema, “Inawakera sana wazungu wakisikia umepata kitu fulani, niliwaambia kuwa nitanunua moja ili niwakoge.”

Kisha Freddie akaniambia niwe makini, na kwamba atakuwa na shughuli nyingi, hivyo niangalie kwa makini lakini nisimtinge. Atajaribu kunifundisha ili kwenye dansi ijayo, siku kadhaa mbele niwe tayari kupokea kazi.

Freddie alipokuwa akishughulika na kuweka sawa vifaa vyake vya kazi aliniambia, “Fika hapa mapema . . . kila kitu weka mahali pake ili usipoteze muda unapoharakishwa. Nilijifunza pia, wakati unang’arisha viatu, pia unakuwa unaangalia wateja wanaotoka maliwatoni. Unawafuata na kuwapatia taulo dogo la mikono. “Watu wengi huwa hawaoshi mikono. Wakati mwingine unawakimbilia ukiwa na taulo na kuwaaibisha. Mataulo ndiyo shughuli itakayokulipa zaidi hapa. Inakugharimu kama senti tano kununua taulo moja nao watakupatia walau senti kumi kama ahsante.”

Huko chini muziki ulishaanza kusikika. Nafikiri nilibaki nimeduwaa. “Hujawahi ona dansi kubwa?” aliuliza Freddie. “Nenda kaangalie kidogo.”

Kulikuwa na wapenzi kadhaa wakicheza. Lakini kilichonivutia zaidi ni umati uliokuwa ukiingia. Wanawake wakizungu waliojipamba kwa namna ambayo sijawahi ona, vijana kwa wazee. Vijana wa kizungu wakiwa dirishani kununua tiketi na kutoa noti kubwa kubwa.

Niliporudi nilimkuta Freddie akiwa na wateja tayari. Aking’arisha viatu na kuwapatia mataulo mara tu walipokaribia sinki la kunawia. Alionekana akifanya vitu vinne kwa wakati mmoja. “Chukua hii brashi ya kufutia nguo,” alisema. ‘utawafuta mara mbili au mara tatu hivi.”

Pilika zilipopungua kidogo aliniambia, “Leo cha-mtoto, subiri siku ya dansi hasa.” Kila alipopata nafasi aliendelea kunifundisha. “Kamba za viatu kwenye droo hii. Kwa vile ndiyo unaanza nitakupa hizi kama zawaidi. Nunua hizi kwa mbili kwa senti tano, waambie wateja kuwa viatu vyao vinahitaji kamba, wakikubali wachaji senti ishirini na tano.”

Kila nyimbo ya Benny Goodman niliyowahi kusikia maishani mwangu ilionekana kupenya na kusikika kule juu tulikokuwa. Wateja walipopungua tena, Freddie aliniruhusu kwenda kusikiliza kwa mara nyingine. Peggy Lee alikuwa akiimba kwa sauti tamu. Alikuwa ametoka tu kujiunga na bendi hivi karibuni. Alikuwa anatokea North Dakota na kwa muda mrefu alikuwa akiimba na kundi moja huko Chicago, huko ndiko bibi Benny Goodman alikomuona, tulisikia baadhi ya wateja wakisema hivyo. Alimaliza kuimba na ukumbi ulilipuka kwa shangwe. Alikubalika sana.

“Hata mimi mara ya kwanza kufika hapa nilichanganyikiwa,” alisema Freddie niliporudi, huku akikenua. “Umewahi ng’arisha viatu?” Alicheka nilipomwambia kuwa sijawahi isipokuwa vyangu mwenyewe tu. “Basi tuanze kazi, hata mimi nilipoanza nilikuwa sijawahi.” Alinionyesha jinsi ya kufanya kwa kutumia viatu vyake. Brashi, dawa ya kung’arishia, nta, kitambaa cha kung’arishia, kupaka soli vanishi . . . alinionyesha cha kufanya hatua kwa hatua.

“Lakini unatakiwa kufanya kwa haraka zaidi. Hutakiwi kupoteza muda!” Freddie alinionyesha jinsi ya kung’arisha kwa kasi kwa kutumia viatu vyangu. Na kwa sababu pilika zilikuwa zimepungua, alinionyesha jinsi ya kufanya kitambaa cha kung’arishia kilie kama baruti “Umenipata?” aliuliza. Nilijaribu kufanya kwenye viatu vyake. Nilikuwa nimeelewa vyema. “Unatakiwa tu kufanya kwa haraka zaidi. Watu wanatoa bakshishi nzuri wakiona kuwa unafanya kazi kwa bidii!”

Mwisho wa dansi Freddie aliniruhusu kung’arisha viatu vya wateja walevi watatu au wanne aliowashawishi kuwa viatu vyao vinahitaji kung’arishwa. Nilifanya mazoezi ya kung’arisha kwenye viatu vya Freddie hadi vikawa kama vioo. Baada ya kuwasaidia wafanya usafi kusafisha ukumbi baada ya dansi, tukiondoa taka zote, vipisi vya sigara na chupa tupu za pombe. Freddie kwa ukarimu aliniendesha hadi nyumbani Kilimani kwa Buick ya mtumba iliyokuwa na rangi ya damu ya mzee. Alisema kuwa ataiuza na kununua Cadillac. Aliongea njia nzima. “Nafikiri si vibaya nikikuambia kuwa ununue kondomu kadhaa. Uliwaona wale vijana walionifuata mwishoni mwa dansi? Basi baadhi yao wakipata wanawake wapya, watakuja kukuuliza kuhusu kondomu. Wauzie kwa dola moja, na kawaida utapata na zaidi kama ahsante.”

Alinigeukia na kusema, “Shughuli zingine ni mapema sana kwako kuzifanya. Kuna watu watahitaji pombe, wengine bangi, wewe lakini usiwe na chochote zaidi ya kondomu mpaka hapo utakapokuwa na uwezo wa kutambua yupi ni polisi.”

“Ukifanya kazi yako vizuri unaweza kutengeneza dola kumi hadi kumi na mbili kwa dansi,” alisema Freddie kabla sijashuka. “Kitu pekee unachotakiwa kukumbuka ni kuwa kila kitu duniani ni mapambno. Kila la kheri Red.”

Nilipoonana tena na Freddie ilikuwa ni majuma kadhaa mbele, nilikuwa nipo mjini usiku mmoja. Alikuwa amepaki Cadillac yake ya kijivu cha lulu, inang’aa balaa, “ametulia zake.”

“Hakika ulinielimisha,” nilimwambia naye alicheka. Alijua ninachomaanisha. Haikuchukua muda mrefu kugundua kuwa kazi hasa ya Freddie haikuwa kung’arisha viatu na kutoa mataulo bali kuuza pombe, bangi na kuwakuwadia malaya weusi kwa wazungu. Pia nilijifunza kuwa wasichana wa kizungu mara zote walihudhuria dansi ya weusi-baadhi yao wakiwa ni malaya ambao makuwadi wao wamewaleta kufanya biashara na starehe, wengine walikuja na wapenzi wao weusi na wengine wakija peke yao, wakitafuta wanaume weusi waliowatolea mate.

Lakini kwenye dansi ya wazungu hakuna mweusi aliyeruhusiwa, na hapo ndipo makuwadi wa malaya weusi walipomuonyesha kijana mpya mng’arisha viatu namna ya kujipatia pesa kwa kuwapatia namba za simu wanaume wa kizungu waliokuwa wakitafuta malaya weusi mwishoni mwa dansi. Walihitaji namba za simu au kuwaelekeza mahali pa kuwapata malaya hao.

***​
 
Sura ya tatu inaendelea.

Dansi nyingi zilizofanyika ukumbi wa Roseland zilikuwa za wazungu, na kulikuwa na bendi za wazungu tu. kwa kumbukumbu zangu, bendi pekee ya wazungu kucheza kwenye dansi ya weusi ilikuwa ni ya Charlie Barnett. Sababu ni kuwa ni bendi chache sana za wazungu zilizoweza kuwaridhisha wacheza dansi weusi. Lakini nafahamu jinsi Charlie Barnett “Cherokee” alivyowapagawisha watu weusi kwa mtindo wake wa “Redskin Rhumba.” Alijaza sana watu. Wasichana weusi wakiwa wamevalia mavazi ya Hariri na satini. Nywele zao zikitengenezwa kwa mitindo ya kila aina. Wanaume nao wakiwa na suti zao za zoot na nywele zao zikiwa zimetiwa dawa.

Baadhi ya wanabendi walifika kwenye maliwato ya wanaume kama saa mbili hivi kabla ya kazi kuanza na kung’arisha viatu vyao. Duke Ellington, Count Basie, Lionel Hampton, Cootie Williams na Jimmie Lunceford, ni baadhi tu ya walioketi kwenye kiti changu. Kwa kweli niliweza kufanya kitambaa cha kung’arishia kilie kama baruti za kichina. Bado namdai pesa zangu za kunga’arishia viatu Jonny Hodges, mpiga saxophone wa Duke. Siku moja aliketi kitini pangu na kuanza kubishana kirafiki na Sonny Greer, mpiga ngoma, ambaye alikuwa amesimama pembeni. Nilipogonga chini ya kiatu chake kumuashiria kuwa nimemaliza. Alishuka, aliingiza mkono mfukoni ili kunilipa, lakini ghafla na kufanya ishara kama amekumbuka kitu na kutokomea. Sikuweza kuthubutu kumghasi mtu aliyeweza kufanya aliyoyafanya kwenye “Daydream” kwa kumdai senti kumi na tano.

Nakumbuka nimewahi kuongea kidogo na Jimmie Rushing, muimbaji wa blues wa Count Basie. Jimmie Rushing ni maarufu kutokana na vibao kama “Sent for you yesterday, here you come toda na vingine vingi. Nakumbuka miguu ya Rushing ilikuwa ni mikubwa na yenye umbo la kuchekesha—haikuwa mirefu kama ilivyo miguu mingine mikubwa, bali ilikuwa kama ya mviringo na iliyotuna-kama Rushing mwenyewe. Mbali na hayo, alinitambulisha kwa wanamuziki wengine wa Basie, wanamuziki kama Lester Young, Harry Edison, Buddy Tate, Don Byas, Dickie Wells na Buck Clayton. Walikuwa wakiingia na kusema, “Vipi Red,” walikaa kwenye kiti changu huku mimi nikisugua viatu vyao kwa kitambaa cha kung’arishia kwa kufuatisha nyimbo zao zilizokuwa zikipiga kichwani mwangu. Popote pale, wanamuziki hawajawahipata kijana mng’arisha viatu aliye shabiki wao kama mimi. Nilikuwa nawaandikia ndugu zangu kule Lansing nikiwaeleza hayo.

***

Sikuwahi kupata “ahsante” yoyote ya maana wakati wa dansi ya watu weusi mpaka ilipofika katikati ya dansi, huo ndiyo wakati watu walianza kujisikia furaha na kujiachia. Kawaida baada ya dansi ya wazungu, nilipokuwa nikisaidia kufanya usafi, tulitupa dazani kadhaa za chupa tupu za pombe. Lakini baada ya dansi ya weusi, tulitupa chupa ambazo bado zilikuwa na pombe, na si pombe za bei ya chini-pombe za gharama na majina makubwa, hasa hasa Scotch.

Wakati ambao hakukuwa na pilika nyingi kule maliwatoni niliweza kupata dakika tano za kwenda kuangalia dansi. Wazungu walicheza kama vile wamefundishwa—kushoto, moja mbili; kulia, tatu, nne. Wakicheza namna ile ile tena na tena, kama vile kuna mtu anawaongoza. Lakini hakuna mtu angeweza kuwafundisha watu weusi wale kucheza namna ile, walifanya wanavyotaka, walikamata wapenzi wa kucheza nao—hata wasichana wa kizungu waliokuja kwenye dansi ya weusi. Na ndugu zangu weusi wanaweza kunichukia kwa kusema hivi—wasichana wengi weusi walikuwa karibu kukanyagwa-kanyagwa na wanaume weusi waliokuwa wanagombania kupata wanawake wa kizungu; ungeweza dhani labda Mungu ameshusha baadhi ya malaika wake.

Baadhi ya wapenzi walicheza miondoko ambayo huwezi amini ipo. Niliweza kuhisi midundo ya muziki hadi kwenye mifupa yangu, japokuwa sikuwahi kucheza dansi.

“Showtime!” Watu walikuwa wakipaza sauti wakati wa saa ya mwisho ya dansi. Hapo wapenzi kadhaa, “wehu” kabisa ndiyo walibaki kwenye ulingo. Wasichana walibadili viatu na kuvaa raba za chini-chini. Hapo bendi ilipiga muziki mzito sana, na watu wengine walitengeneza duara kuwazunguka, wakipiga makofi na kupiga kelele kwa shangwe. Ukumbi mzima ulijikusnya sehemu moja, wakichukua robo tu ya ukumbi. Bendi, wachezaji na watazamaji walifanya ukumbi wa Roseland uonekane kama meli inayosongwasongwa na mawimbi makubwa. Taa zilimulika rangi mbalimbali, zikiwamulika wanaocheza ambao walikuwa kama wamepandwa na wazimu. “Ndiyo! Ndiyo!” Watu waliipigia bendi kelele, nayo ilipiga mzuki mpaka wachezaji walipoanza kuishiwa nguvu na kupepesukia kwa watazamaji, wamelowa jasho mwili mzima. Nyakati nyingine nilikuwa nasimama ndani ya ukumbi karibu na mlango, nikitingisha mwili kutokana na mdundo wa muziki hadi meneja alipokuja huku akifoka kuwa nina wateja kule juu.

Sikumbuki nilivyoanza kunywa pombe, kuvuta sigara na kuvuta bangi. Lakini nakumbuka nilianza vyote kwa pamoja, pamoja na kucheza kamari na kutumia dola moja kila siku kucheza bahati nasibu. Nilianza yote hayo nilipoanza kushinda na Shorty na rafiki zake usiku. Utani wa Shorty juu ya jinsi gani nilivyokuwa mshamba ulituchekesha sote. Naelewa kuwa bado nilikuwa mshamba lakini nilifurahia sana kuwa pamoja nao kwa sababu walinikubali. Tulikuwa tukikusanyika nyumbani kwa mmoja wetu, mara nyingi kwa mmoja wa wasichana na kuwasha bangi na kufanya kila mmoja sehemu ile alewe. Kila mmoja alielewa kuwa nywele zangu zinatakiwa kukua kiasi ili Shorty aweze kuniweka dawa. Moja ya usiku kama huo niliwadokezea kuwa nilikuwa nimetunza pesa za kutosha kuweza kununua suti

“Umetunza?” alisema Shorty akiwa haamini. “ Wa nyumbani hujawahi kusikia kuhusu mkopo?” aliniambia kuwa atawapigia duka la nguo la mtaani kesho aubuhi na mapema, na kuwa natakiwa kuwahi huko asubuhi.

Asubuhi nilipofika dukani hapo, nilikutana na muuza duka, kijana mdogo wa kiyahudi. “Wewe ni rafiki yake Shorty?” Niijibu ndiyo; nilishangazwa na jinsi Shorty alivyojuana na watu. Muuzaji yule aliandika jina langu na sehemu ninayofanya kazi kwenye daftari, na anuani ya nilikoishi-nyumbani kwa Ella. Jina la Shorty liliandikwa kama mdhamini. Muuzaji yule aliniambia, “Shorty ni mmoja wa wateja wetu wazuri sana.”

Nilipimwa na kisha kijana yule alivuta suti moja aina ya zoot iliyokuwa ya ajabu sana: ilikuwa na suruali ya bluu, magotini ikiwa na upana wa inchi thelathini, kisha inapungua upana kuelekea chini hadi kufikia upana wa inchi kumi na mbili kwenye pindo la chini. Koti lake lilikuwa refu, lilinibana kiunoni na kujiachia kuanzia magotini.

Muuzaji aliniambia kuwa watanipatia na mkanda mwembamba wa ngozi wenye herufi “L”—kifupisho cha jina langu kama zawadi. Aliniambia kuwa natakiwa kununua na kofia pia, nilifanya hivyo, nilinunua kofia ya bluu iliyokuwa na unyonya mrefu pembeni. Kisha nikapewa zawadi nyingine, mnyororo mrefu wenye rangi ya dhahabu ambao niliuning’iniza kwenye luksi. Kuanzia hapo nilikopa siku zote.

Nilipojaribu suti ile mbele ya Ella alisema, “Nilitarajia hili kutokea,” nilienda studio kupiga picha tatu, kwa senti ishirini na tano kwa picha, nikikaa mikao kama ambavyo masela wavaao suti hizi hukaa, kofia nimeiinamisha kidoo, nimebana miguu kwenye magoti na chini kuiachia. Picha moja niliisaini na kuwatumia ndugu zangu huko Lansing, kuwaonyesha jinsi mambo yanavyoninyokea. Nyingine nilimpatia Ella na nyingine nilimpa Shorty ambaye alifurahi sana, nilijua hilo kwa jinsi alivyosema-alisema: “Shukrani wa nyumbani.” Haikuwa kawaida yetu kuambiana maneno ya hisia.

Baada ya muda kidogo, Shorty akaonelea kuwa nywele zangu zilikuwa na urefu wa kutosha kuwekwa dawa. Alikuwa ameniahidi kunifundisha jinsi ya kuepuka gharama ya dola tatu au nne wanazochaji vinyozi kwa kunifundisha jinsi ya kutengeneza mchanganyiko wa dawa na kujiweka mwenyewe.

Nilichukua orodha ya vitu alivyoniandikia na kwenda nayo dukani, nilinunua mkebe wa alkali iliyoitwa Red Devil, mayai mawili na viazi vyeupe vya ukubwa wa kati. Kisha nikaenda duka la dawa lililokuwa karibu na kibanda cha pool na nikanunua kopo kubwa la mafuta ya Vaseline, kipande kikubwa cha sabuni na chanuo lenye meno makubwa na chanuo jingine lenye meno madogo. Nikanunua pia aproni ya ngozi na gloves mbili.

“Ndiyo unaenda kuanza kuweka dawa nywele?” aliniuliza muuzaji wa duka la dawa. “Ndiyo” nilijibu kwa kujivuna huku nikikenua.

Shorty alikuwa akilipa dola sita kila juma kama kodi katika makazi duni aliyokaa na binamu yake. Binamu yake hakuwako nyumbani. “Ni kama tu makazi yangu, binamu yangu hutumia muda mwingi kwa mwanamke wake,” alisema Shorty. “Sasa niangalie.”

Alimenya viazi na kuvikata vipande vidogovidogo, aliviweka kwenye chupa na kuanza kuvikoroga huku akimiminia ile alkali polepole kwa kutumia kijiko cha mbao. “Kamwe usitumie kijiko cha chuma; alkali itakibadilisha kuwa cheusi,” aliniambia.

Mchanganyiko wa alkali na viazi ukawa uji mzito. Kisha akavunjia mayai mawili kwenye mchanganyiko na kukoroga kwa kasi sana. Mchanganyiko ukabadilika na kuwa wa manjano hivi. “Shika chupa uone,” alisema Shorty. Niligusa pembeni ya chupa na kuondoa mkono haraka sana. “Ni ya moto eeh! Alkali hiyo,” alisema. “Fahamu kuwa itaunguza nitakapokupaka—inaunguza balaa. Lakini kadri unavyoivumilia kwa muda mrefu ndivyo nywele zinavyonyoka vizuri zaidi?”

Alinikalisha chini kisha akanifunga vizuri aproni ya mpira shingoni na kunichana nywele. Baada ya hapo akachukua mafuta ya kutosha kutoka kwenye kopo la Vaseline na kunipaka kwa kusugua kwa nguvu kwenye kichwa kizima, hadi kwenye ngozi. Pia alinipaka Vaseline ya kutosha shingoni, kwenye paji la uso na kwenye masikio.

“Nitakapokuwa nakuosha kichwa hakikisha unaniambia sehemu ambayo unahisi kuchomwa,” alinionya Shorty. Aliosha mikono yake na kuvaa gloves na aproni yake ya mpira. “Unatakiwa kukumbuka kuwa mchanganyiko wowote utakaobaki kichwani mwako utakusababishia kidonda.”

Nilianza kuhisi joto la congolene mara tu Shorty alipoanza kuiweka kwenye nywele zangu kwa kutumia chanuo. Ghafla kichwa changu kikaanza kuwaka moto. Niliuma meno huku nimeshikilia meza ya jikoni kwa nguvu. Nilihisi kama chanuo kinabandua ngozi yangu. Machozi na kamasi vilinitoka. Sikuweza kuvumilia zaidi, niliinuka na kukimbilia kwenye sinki la kunawia. Nilimlaani Shorty kwa majina yote niliyoyajua. Alianza kunimwagia maji na kupaka sabuni kichwani mwangu.

Alinipaka sabuni na kunisuuza karibu mara kumi na mbili kwa maji ya baridi, na hilo lilisaidia kwa kiasi.

“Bado unahisi sehemu yoyote inachomachoma?” “Hapana,” nilijibu. Magoti yalikuwa yakitetemeka. “Basi kaa, nafikiri kila kitu kimeenda sawa.”

Kichwa kilianza tena kuwaka moto baada ya Shorty kuja na taulo na kuanza kunifuta, akifuta kwa nguvu, “Polepole!” nilipiga kelele.

“Mwanzo mgumu. Muda si mrefu utakuwa umezoea. Umejitahidi sana kuvumilia. Nywele zako zimetoka vizuri sana.”

Shorty aliponiruhusu kusimama na kujiangalia kwenye kioo, nywele zangu zilikuwa zimelala kichwani. Kichwa bado kilikuwa kinawaka moto lakini si sana; niliweza kuvumilia. Aliniweka taulo mabegani na akaanza tena kunipaka mafuta kichwani. Kisha kwa uangalifu mkubwa, akatumia wembe kunirekebisha nywele za nyuma ya shingo na kunichonga masharubu.

Maumivu yalisimama kwa muda baada ya kujiangalia kwenye kioo. Nimeona nywele zilizotengenezwa vizuri, lakini unapoona za kwako kwa mara ya kwanza kichwani mwako, baada ya kuwa na nywele ngumu maisha yako yote-inastaajabisha sana.

Shorty aliyekuwa nyuma yangu naye alionekana kwenye kioo. Wote tulikuwa tukikenua huku tukivuja jasho, kichwani kwangu kulikuwa na nywele nyekundu—nyekundu kabisa na zimenyooka kama nywele za mzungu.
 
Mtu akiwa amepigilia zoot

1694415957694.jpeg
 
Jinsi gani nilikuwa kituko! Mjinga kiasi cha kuweza kusimama pale nikistaajabia kwa kuwa nywele zangu sasa zilionekana kama za mzungu. Niliapa kuwa sitaacha kuweka nywele zangu dawa tena, na kwa miaka mingi nilitimiza ahadi hiyo.

Hii ilikuwa ndiyo hatua yangu kubwa katika kujidharaulisha. Nilipovumilia maumivu yote yale, karibu kuunguza ngozi ili tu nywele zangu zionekane kama za mzungu nilikuwa nimeungana rasmi na umati wa watu weusi katika Marekani, wanawake kwa wanaume, umati ambao umeaminishwa kuwa mtu mweusi ni duni na mtu mweupe ni bora—watu ambao wako tayari kudhuru miili yao waliyoumbwa na Mungu ili kuonekana “wazuri” kulingana na viwango vya kizungu.

Angalia leo kwenye kila mji mdogo na jiji kubwa kutoka kwenye vibanda vidogo vya wamachinga, hadi kwenye kumbi kubwa za hoteli zinazoruhusu uchangamano kama Waldorf-Astoria utaona wanaume weusi walioweka nywele zao dawa. Na utaona wanawake weusi wakiwa wamevaa mawigi ya rangi ya dhahabu, zambarau, kijani na nyekundu. Wote ni vituko kuliko wachekeshaji wa kujichetua. Mambo hayo yanakufanya ubaki ukishangaa iwapo mtu mweusi amepoteza kabisa kujitambua, iwapo hajielewi!

Utaona watu weusi wengi wa “Daraja la juu” wakiwa wameweka nywele zao dawa, na nasikitika kusema kuwa wengi wao ni wasanii weusi. Sababu moja inayonifanya niwakubali sana baadhi yao, kama Lionel Hampton na Sidney Poiter na wengineo, ni kuwa wamebaki na nywele zao za asili na wamepambana hadi kufika juu. Namkubali sana mwanaume yeyote mweusi ambaye hajawahi kuweka nywele zake dawa—au ambaye alikuwa na akili ya kuacha kama nilivyofanya.

Sijui ni aina gani ya uwekaji dawa wa nywele unaodharaulisha zaidi, ule unaofanywa na wanaoitwa watu wa daraja la “kati” na “juu”—ambao tunategemea wawe wanajielewa zaidi au ule unaouona kwa walio masikini kabisa- wanaume weusi waliojaa ujinga. Namaanisha watu weusi wa kipato cha chini, kama nilivyokuwa mimi nilipoweka nywele zangu dawa kwa mara ya kwanza. Mara nyingi ni kati ya hawa weusi masikini na wajinga ndiyo utaona mtu aliyefunga kitambaa cheusi kichwani kama Aunt Jemima; anajaribu kufanya nywele zake alizotia dawa zidumu kwa muda mrefu kabla hajarudi tena kwa kinyozi. Ni kwa matukio maalumu tu ndiyo anaondoa kitambaa ili kuonyesha jinsi nywele zake zilivyo nzuri. Jambo la ajabu ni kuwa sijawahi ona mwanamke yeyote, mweusi au mzungu anayependezwa na mwanaume aliyeweka nywele dawa. Bila shaka mwanamke yoyote mzungu mwenye mwanaume mweusi hafikirii juu ya nywele zake. Lakini hainiingii akilini kwa mwanamke yeyote mweusi anayejiheshimu na kuheshimu alivyo kutembea mtaani na mwanaume mweusi aliyeweka nywele zake dawa—kama ishara yake kuwa anaona aibu kuwa mweusi.

Kwa aibu, ninapozungumza haya kwanza kabisa najizungumzia mimi mwenyewe sababu huwezi kunionyesha mtu mwingine mweusi aliyekuwa anaweza nywele zake dawa zaidi yangu. Ninazungumza kutokana na uzoefu ninapowazungumzia wanaume weusi wanaoweka nywele zao dawa au mwanamke yeyote mweusi anayevaa wigi-kwamba, kama watajali akili zao kwa nusu tu ya wanavyojali nywele zao, watakuwa bora mara elfu.
Mwisho sura ya tatu​
 
SURA YA NNE

LAURA


Shorty alikuwa akinipeleka kila mahali kulikochangamka. Huko nilikutana na wasichana wazuri ajabu na vijana waliokuwa watanashati na wajanja hasa. Nami ndani ya muda mfupi nikawa naongea lugha yao.

Kama tu mamia elfu ya watu weusi waliotoka mashambani na kuja kwenye maeneo ya maghetto ya watu weusi huku kaskazini kabla yangu, na wanaoendelea kuja, nami pia nilinunua vitu vya anasa vya watu walioishi maghetoni; suti aina ya zoot, niliweka nywele dawa kama nilivyokwisha elezea, pombe, sigara na baadaye bangi-yote ni ili kuficha kuwa nimetoka mashambani. Lakini bado jambo moja la aibu halikunitoka, nilikuwa sijui kucheza dansi.

Sikumbuki hasa ni lini hasa nilijifunza, sikumbuki ni usiku upi hasa. Lakini kucheza dansi ilikuwa ndilo tukio kuu la karamu zile. Nikiwa na pombe na bangi kichwani, na mziki ule wa ukidunda, haikuchukua muda kwa asili yangu ya kiafrika ya kuweza kucheza kujionyesha. Nakumbuka tu kudakwa na msichana fulani-maana hakuna msichana aliyedhani kuna mtu alihudhuria karamu zile na asijue kucheza. Basi nikajikuta naanza kucheza kwa namna hiyo. Ndani ya muda mfupi nakawa nimeelewa nini cha kufanya.

Baada ya kuishi na wazungu kwa muda mrefu kule Mason, siku zote nilifikiri kuwa ili kucheza dansi inatakiwa kufuata mtindo na hatua fulani, kama wafanyavyo wazungu. Lakini hapa katikati ya weusi wenzangu, watu wa kujiachia, nilijifunza kuwa unatakiwa tu kuchezesha viungo vyako kulingana na mdundo.

Kutoka hapo hakuna tafrija iliyofanyika bila mimi kutokea-nikijialika pale ilipobidi-na kucheza dansi kama mwendawazimu.

Nilikuwa mwepesi sana wa kujifunza mitindo mipya. Nafikiri nilikuwa nafidia suala la kuchelewa kujifunza kucheza dansi. Haikuchukua muda wasichana wote wakawa wanataka kucheza name. Niliwapeleka puta sana wakati wa kucheza, na hicho ndicho walichonipendea.

Hata nilipokuwa kazini kwenye maliwato ya wanaume kule kwenye ukumbi wa Roseland sikuwa nikitulia. Kitambaa changu cha kung’arishia kilitoa sauti kwa kufuata mdundo wa mziki uliopigwa na bendi kule ukumbini. Wateja wangu, hasa wakizungu walikuwa wakicheka baada ya kuona miguu yangu ikipiga mitindo kadhaa ya ghafla. Wazungu wako sahihi kufikiri kuwa watu weusi wana vipaji vya asili vya kucheza. Hata watoto wanajua—isipokuwa kwa wale watu weusi ambao “Wamechangamana” sana kama ambavyo mimi mwenyewe nilikuwa kiasi kwamba uwezo wao wa kucheza umefifia. Unavifahamu vile vikaragosi vya watu weusi ambavyo hucheza dansi baada ya kuvizungusha? Basi mimi nilikuwa kikaragosi kilicho hai-na sauti ya muziki ilikuwa ndiyo kuzungushwa kwangu.

Nakumbuka Lionel Hampton alikuwa anakuja kupiga kwenye dansi ya watu weusi iliyofuata kwenye ukumbi wa Roseland-ndipo nilimtaarifu meneja wa ukumbi wa Roseland kuwa ninaacha kazi.

Nilipomwambia Ella sababu ya kuacha kazi alicheka sana: nilimwambia kuwa sikuweza kupata muda wa kung’arisha viatu na kucheza dansi. Lakini alifurahi, hakuridhia mimi kufanya kazi ya hali ya chini. Nilipomtaarifu Shorty, aliniambia kuwa alijua kuwa nitaachana nayo siku moja.

Shorty naye alikuwa ni mcheza dansi mzuri, lakini kwa sababu zake binafsi hakujali sana kuhudhuria dansi kubwa. Alipendelea zaidi kupiga muziki. Alifanya mazoezi ya kupiga saxophone yake na kusikiliza vibao mbalimbali. Nilishangazwa na kitendo cha Shorty kutopendelea kwenda kusikiliza bendi kubwa zikipiga muziki. Lakini kulikuwa na mpiga saxophone mmoja aliyemhusudu sana, Johnny Hodges wa bendi ya Duke Ellington, alidai kuwa wanamuziki wengi vijana walikuwa wakiiga tu kutoka kwa wanamuziki wa bendi kubwa. Pamoja na hayo Shorty hakuwa na kitu alichozingatia zaidi ya muziki wake.

Asubuhi iliyofuata baada ya kuacha kazi niliwahi mapema kwenye duka la nguo. Muuzaji alikagua daftari nakuona kuwa nilikosa kulipa malipo yangu kwa juma mara moja tu: Nilikuwa mteja wa daraja “A-1.” Nilipomwambia kuwa nimeacha kazi yangu akaniambia hilo halina tatizo; naweza kukaa majuma kadhaa bila kulipa kama nikitaka; alijua kuwa nitajipanga na kulipa.

Safari hii nilipita kwenye shelves kwa uangalifu sana na kuchagua suti yangu nyingine ya aina ya zoot. Ilikuwa na kijivu ya papa, koti refu na suruali pana magotini na nyembamba chini. Kwa ushawishi wa muuzaji, nilichukua pia shati, kofia na viatu vipya ambavyo ndiyo vilikuwa mtindo mpya wa wajanja; vilikuwa vya rangi ya machungwa iliyokolea, soli nyembamba na vimetuna kwa mbele. Jumla vyote ilikuwa kama dola sabini au themanini hivi.

Siku hiyo ilikuwa yangu hasa maana baadaye nilienda kupaka nywele zangu dawa kwa kinyozi kwa mara ya kwanza. Kama tu alivyosema Shorty, safari hii maumivu hayakuwa makali sana. Usiku huo nilijiandaa kuingia ukumbi wa Roseland kwa kutegea wakati ambao watu wengi watakapokuwa wanaingia. Kwenye sehemu ya kuingilia niliona baadhi ya vijana wa mjini kutoka Roxbury wakiitupia macho zoot yangu na baadhi ya wanawake warembo wakinitupia macho fulani ya wizi. Nilienda maliwatoni na kunywa pombe kutoka kwenye chupa niliyoweka kwenye mfuko wa ndani wa koti. Kijana aliyenibadili kazi alikuwa yupo kazini. Kijana mmoja, mweusi, mwembamba na muogamuoga aliyeingia mjini karibuni kutoka jiji la Kansas City. Mara tu aliponitambua hakuweza kujizuia kunistaajabia. Nilimwambia awe mpole, na muda si mrefu atakuwa mjanja wa mjini. Nilirudi ukumbini na kila kitu kilionekana kipo sawa.

Bendi ya Hampton ilikuwa ikipiga kazi na watu walijazana ukumbini wakicheza kama wana wazimu. Nilimkamata msichana mmoja ambaye hata sikuwahi kumuona, kuja kushtuka tupo ulingoni tunakenuliana meno. Nilikuwa na wakati mzuri kabisa. Dansi nilizowahi kufurahia zilikuwa kwenye sebule ndogo zilizobanana. Lakini hapa kulikuwa na nafasi ya kujiachia. Baada ya kuzoea nikaanza kudaka wasichana huku na kule, weusi, wa maji ya kunde na baadhi wa kizungu. Nilikuwa kama mwehu. Niliwarusha wasichana hewani, kupitia mabegani na mapajani. Japo nilikuwa bado sijafikisha miaka kumi na sita lakini nilikuwa mrefu na nimekomaa kiasi cha kuonekana nina miaka ishirini na moja hivi; pia nilikuwa na nguvu sana ukilinganisha na umri wangu. Siku hiyo nilicheza kila aina ya mitindo. Baada ya hapo sikuwahi kukosa dansi iliyofanyika Roseland kwa muda wote niliokaa Boston.
***​
 
Sura ya nne inaendelea.

Msichana ambaye nilimkubali zaidi kwenye kucheza naye dansi alikuwa ni msichana mmoja aliyeitwa Laura. Nilikutana naye kwenye kazi yangu nyingine baada ya kuachana na kazi ya kung’arisha viatu. Ella alifurahi sana nilipoacha kazi hiyo na akaenda kunitafutia kazi aliyoona kuwa inafaa. Mtaa wa tatu kutoka nyumbani kwake kulikuwa na duka la dawa la Townsend lililohitaji kijana wa kuuza soda, kijana waliyekuwa naye alikuwa anaenda chuo.

Ella aliponijulisha kuhusu kazi hiyo sikupendezwa nayo hata kidogo. Naye alifahamu kuwa nilikuwa siivi na watu wa Kilimani. Lakini kuongea hilo kumgemkasirisha Ella na sikutaka hilo litokee. Basi nilivaa koti jeupe na kuanza soda, aisikrimu na vinywaji vingine kwa wale watu weusi wenye kujidai.

Kila saa mbili jioni niliporudi nyumbani, Ella alisema, “Natumaini utakutana na vijana wema wa umri wako hapa Roxbury.” Lakini vijana na wazee wa huko waliofika dukani petu pale waliishia tu kunichukiza. Watu kama mhudumu aliyefanya kazi kwa wazungu huko Beacon Hill, akija na kuniletea za, “Oh, my deah” na kuagiza plasta za kutoa sundo sundo kwenye duka l Myahudi kwenye maeneo ya watu weusi. Au mwanamke aliyefanya kazi kwenye mgahawa wa hospitali akija dukani pale siku ambazo haendi kazini, akiwa amevaa koti lenye manyoya shingoni na kumwambia mmiliki wa duka kuwa alikuwa ni “Mtaalamu wa lishe” na hali wote wanajua kuwa anadanganya. Hata vijana wa rika langu ambao Ella alikuwa anawazungumzia. Mahali pa kuuzia soda ndipo palikuwa kijiwe chao. Wakijiongelesha kwa lafudhi za kujifanya kiasi kwamba ukiwasikia kabla ya kuwaona huwezi jua kuwa ni weusi. Walinichefua na kunifanya nitake kuacha kazi mara moja. Hamu yangu kubwa ilikuwa ni saa mbili usiku ifike, niende nyumbani kula, kisha nivae zoot yangu na kwenda kwa rafiki zangu mjini, kucheza muziki na kuvuta bangi, au chochote cha kunipumzisha kutoka kwa vikaragosi wale wa Kilimani.

Haikuchukua muda mrefu kuona kuwa sitaweza kuvumilia kukaa pale kwa saa nane kwa siku. Siku moja karibu niache kazi, nilikuwa nimeshinda dola sitini kwenye kamari(Ndiyo, kulikuwa na wachezesha kamari hata kule Kilimani. Hata watu weusi wenye kujiheshimu nao walicheza kamari.) Tulijirusha sana na Shorty. Nilicheza senti kumi pale dukani, nilitamani ningecheza dola moja kama nilivyocheza kwa wakala wa mjini, huko nilicheza dola moja kila siku na nilimlipa kwa juma. Ingekuwa hivyo ningeacha kazi mara moja. Ningeweza hata nunua gari.

Turudi kwa Laura. Laura aliishi ng’ambo ya barabara kutoka duka la dawa. Baada ya kumuona akija dukani mara kadhaa, nikaanza kuwa naandaa mchanganyiko wa ndizi na matunda mbalimbali, alipenda sana mchanganyiko huo. Alifika dukani pale kila siku baada ya kutoka shuleni. Alikuwa ni msichana pekee wa Kilimani ambaye alikuwa hajifanyi na mwenye urafiki. Mara zote alikuwa na kitabu anasoma. Nilianza kuangalia vitabu anavyosoma, vilikuwa vitabu vigumu vya shuleni—vya kilatini, aljebra nk. Kumuona vile kulinifanya nitambue kuwa toka nitoke Mason sijasoma hata Gazeti.

Niliskia baadhi ya watu waliofika pale wakimwita Laura. Lakini niliona wazi kuwa hawakuzoeana naye sana. Waliishia kusalimiana naye tu naye hakujibu zaidi ya salamu. Hakuwa muongeaji, na hakuwahi kunisemesha zaidi ya kusema ahsante pale nilipomuhudumia. Sauti yake ilikuwa tamu nay a upole. Alikuwa tofauti sana na watu weusi wengine wa Boston.

Nilivutiwa naye sana. Baada ya muda mfupi nikaweza kuongea naye, sikumbuki mada ya kwanza kuongea naye ilikuwa nini lakini alinichamngamkia na aliongea kwa kirefu. Nilifahamu kuwa alikuwa mwanafunzi wa sekondari na wazazi wake walitengana alipokuwa bado mdogo hivyo amelelewa na bibi yake, mwanamke mzee aliyekuwa akiishi kwa kutegemea mafao. Aliniambia kuwa bibi yake alikuwa “mkoloni” na mtu wa dini sana. Laura alikuwa na rafiki mmoja tu, msichana fulani waliyesoma wote lakini yeye aliishi huko Cambridge. Walizungumza naye kwa simu kila siku. Bibi yake hakumruhusu kabisa kuwa na wavulana, na alimruhusu mara chache sana kwenda kwenye kumbi za sinema.

Laura alipenda sana shule. Alisema kuwa alitaka kufika chuo kikuu kusomea sayansi. Kamwe Laura asingeweza kuhisi kuwa amenizidi umri kwa mwaka mmoja. Alikuwa akinichukulia kama vile nina uzoefu wa maisha kuliko yeye, na hilo lilikuwa ni kweli. Nyakati nyingine alipoondoka nilijisikia vibaya kwa jinsi nilivyoachana na vitabu nilivyovipenda sana nilipokuwa Michigan.

Ilifika kipindi nilikuwa namsubiria kwa hamu atoke shule. Niliacha kumlipisha pesa na nilimuongeza aisikrimu nyingi zaidi. Naye hakuficha kuwa alipendezwa nami.

Haikuchukua muda akawa ameacha kusoma vitabu alipofika, alikuwa tu akila aiskirimu na kuongea nami. Kisha akataka kunijua zaidi kwa kuniuliza maswali kadha wa kadha. Niliona aibu nilipomwambia kuwa kuna kipindi nilifikiria kuja kuwa mwanasheria. “Malcom, hakuna sababu ya kukuzuia kuanza ulipoishia na kuwa mwanasheria.” Alikuwa na maoni kuwa Ella atanisaidia kadri awezavyo.

Sikuwahi mwambia Shorty kuhusu Laura. Nilijua kuwa Laura hatamuelewa wala kuelewa wale rafiki zangu wengine. Nao pia wasingemuelewa. Niliamini kuwa hakuwahi guswa, nilikuwa na hakika na hilo, wala kuonja pombe, na wala hangeweza kufahamu bangi ni kitu gani.

Nilishangaa sana baada ya siku moja Laura kuniambia kuwa anapenda kucheza dansi kwa mtindo wa Lindy Hoppy. Nilimuuliza aliwezaje kutoka kwenda kucheza dansi, akaniambia kuwa alijifunza mtindo huo kwenye tafrija ambayo wazazi fulani weusi walimfanyia kijana wao baada ya kukubaliwa kujiunga na chuo cha Harvard.

Ilikuwa ni karibu na muda wa kufunga sehemu ya kuuzia soda. Nilimwambia kuwa Count Basie alikuwa akipiga kwenye ukumbi wa Roseland mwishoni mwa juma, nilimuuliza kama atapenda kwenda.

Laura alifurahi sana. Aliniambia kuwa hajawahi kwenda ukumbi Roseland na kuwa amesikia sana kuuhusu, alikuwa akiwazia tu jinsi kulivyo. Angependa sana kwenda lakini bibi yake hangekubali hata kidogo.

Nikamwambia labda wakati mwingine.

Lakini mchana wa siku ya dansi, Laura alifika na kuninong’oneza kuwa hajawahi kumdanganya bibi yake lakini siku hiyo alikuwa amemwambia kuwa alitakiwa kuhudhuria jambo fulani la kishule jioni ile. Akasema iwapo nitamuwaisha kurudi nyumbani, ataenda nami.

Nilimwambia kuwa tulipaswa kupitia kwanza nyumbani ili nibadili nguo. Alisita kidogo lakini akakubali. Nilimpigia simu Ella kuwa nitapita nyumbani na msichana tukielekea dansini. Ella alijitahidi kutoonyesha kushangazwa na hilo kwenye simu.

Nilikuwa nikicheka sana nilipokuwa nikikumbuka jinsi Ella alivyoshangaa nilipofika nyumbani na msichana safi kutoka Kilimani. Nilipowatambulisha Laura alikuwa mchangamfu sana. Wakati huo Ella alikuwa anaelekea kupata mume wake wa tatu.

Nilipanda chumbani kwangu kwenda kubadili nguo na kuwaacha wakiongea huku chini. Nilipanga kuvaa suti yangu ya rangi ya ngozi ya papa lakini nikabadili wazo na kuamua kuvaa ile ya kwanza kununua, ya rangi ya bluu. Nilifahamu kuwa natakiwa kutoonekana kituko.

Niliposhuka niliwakuta wakiongea kama marafiki waliojuana siku nyingi. Na Ella alikuwa ameandaa chai. Ella aliitupia jicho la wizi suti yangu ya zoot, lakini nafikiri alitulia moyoni alipoona walau nimechagua ya bluu. Kwa nilivyomfahamu Ella, nikajua kuwa tayari atakuwa ameshajua maisha yote ya Laura-nilibaki tu kuvishwa vazi la harusi. Muda wote kwenye taxi wakati wa kuelekea Roseland nilikuwa nikikenua-nilikuwa nimemuonyesha Ella kuwa kama nikitaka naweza kuwa na msichana wa Kilimani.

Laura alikuwa akistaajabu muda wote. Alisema kuwa hakuna yeyote kati ya tuliyekutana naye aliyemfahamu bibi yake. Akaongeza kuwa bibi yake hakwenda mahali popote zaidi ya kanisani, kwa hiyo haikuwa rahisi kwa taarifa kumfikia. Alisem kuwa mtu pekee aliyemwambia habari ile alikuwa ni rafiki yake ambaye naye alifurahi sana.

Haikuchukua muda tukawa tumefika ukumbi wa Roseland. Watu walikuwa wakinisalimia kwa tabasamu na kunipungia mkono. Wakisema “My man” na kuniita “Hey Red!” nami nilijibu “daddy-yo.”

Hatukuwahi cheza dansi pamoja lakini halikuwa tatizo. Watu wanaoweza kucheza mtindo wa lindy wanaweza kucheza pamoja. Basi tukaanza kucheza ulingoni kati ya wapenzi wengine.

Ilikuwa katikati ya dansi nilipogundua namna yake ya kucheza.

***​
 
Sura ya nne inaendelea.

Kama umewahi kucheza mtindo wa lindy utaelewa ninachomaanisha. Kwa wasichana wengi unamgusa tu naye anajua cha kufanya, lakini kwa wachezaji wabovu utahisi uzito wao, ni wazito na wako polepole. Lakini kwa wachezaji wazuri kabisa unahitaji tu kuonyesha kumvuta na kumsukuma, ni wepesi sana. Nilicheza na wachezaji wengi wazuri. Lakini nilichogundua kwa Laura ni kuwa sijawahi hisi mtu mwepesi namna ile. Ni kama nilihitaji tu kufikiria mtindo naye aliufuata. Kama mtu angeniuliza ni msichana gani nilifurahia zaidi kucheza naye dansi basi ningemwambia ni aliyekuwa mwepesi kama Laura, na mwenye nguvu za kuweza kuhimili vishindo vya showtime. Lakini nilifahamu kuwa Laura hakuwa na nguvu hizo.

Miaka kadhaa baadaye nilipokuwa Harlem, rafiki yangu mmoja aliyeitwa “Kuwadi Sammy.” Alinifundisha kitu fulani ambacho nilitamani ningekijua wakati ule na kukiangalia kwenye uso wa Laura. Ni kile Sammy alichosema kuwa ni kiashiria cha hakika cha tabia ya mwanamke, na ukifikiria wanawake wote alioweza kuwageuza kuwa makahaba, basi hakukuwa na shaka kuwa Sammy ni mtaalamu wa eneo hilo. Sammy aliniambia kuwa kama mwanamke amezama kabisa kwenye dansi basi uso wake utaonyesha jinsi alivyo hasa.

Sisemi kuwa sura ya umapepe ilionekana kwa Laura tulipokuwa tunacheza, ni kuwa tu maisha yalimfanyia ukatili sana mara baada ya kukutana name. Ninachosema ni kuwa iwapo ningekuwa na uwezo kama wa Sammy ningeweza kuona kitu fulani usoni mwa Laura, kitu kilichokuja kumshangaza bibi yake.

Baada ya muda fulani kupita onyesha hasa ndiyo lilianza, wakati huu ni wachezaji hodari tu ndiyo walibaki ulingoni. Wakishandana kucheza kwa mtoano. Wacheza dansi wote walizunguka na kutengeneza umbo la “U”, bendi ikiwa mbele.

Wasichana waliokuwa wakishiriki mashindano hayo walivua viatu vyao virefu na kuvaa raba zenye soli ya chini, wasingeweza kumudu vishindo vile wakiwa na viatu virefu. Kawaida kati ya wasichana hao kulikuwa na wanne au watano ambao hawakuwa na mtu wa kucheza naye. Walizunguka huku na huko kumtafuta mtu waliyefahamu kuwa alijua hasa namna ya ku-lindy.

Basi Count Basie akafungulia mziki wenyewe na wacheza dansi wengine wakasogea mbali na ulingo, wakikaa sehemu nzuri ili waweze kuona na kushangilia wacheza dansi waliowapenda. “Red nenda kawaonyeshe kazi!” kisha msichana mmoja mcheza lindy ambaye nimewahi kucheza nae hapo kabla, Mamie Bevels, ambaye alikuwa ni mhudumu na mchezaji wa kupagawa alinikimbilia, Laura akiwa amesimama pembeni yangu. Sikujua cha kufanya. Lakini Laura alirudi nyuma kwa mashabiki huku huku akiendelea kuniangalia.

Bendi ya Count ikaanza kupiga. Nilimkamata Mamie na tukaanza kazi. Alikuwa ni msichana mkubwa na mwenye nguvu, na alicheza lindy kama farasi. Nakumbuka siku aliyojizoela umaarufu pale Roseland. Bendi ilikuwa imechanganya naye alirusha viatu vyake na kuanza kucheza peku huku akipiga kelele, kisha akajitingisha kama aliyepatwa na mashetani ya Kiafrika. Ilimlazimu mtu aliyekuwa anacheza naye kutumia nguvu kumdhibiti. Watazamaji walipenda uchezaji lindy wa namna hiyo.

Basi nikaanza kumpeleka puta kama farasi, namna aliyopenda. Tulipotoka ukumbini baada ya wimbo wa kwanza, tulikuwa tumeloa jasho mwili wote na watu walikuwa wakitushangilia.

Nakumbuka niliwahi kuondoka ili kumuwahisha Laura nyumbani kwao. Alikuwa mkimya sana, na alipokuja dukani, hakuongea mengi kwa kama juma moja hivi. Lakini wakati huo nilikuwa nimewajua wanawake vya kutosha kufahamu kuwa hutakiwi kuwalazimisha wakueleze mawazo yao, watakwambia wenyewe wakiwa tayari.

Kila mara nilipoonana na Ella, hata nilipokuwa nikipiga mswaki, aliniuliza ni lini nitaonana tena na Laura? Nitakuja naye tena nyumbani lini? “Msichana ana adabu sana!” Ella alikuwa ameishanichagulia.

Lakini fikira zangu hazikuwepo sana kwa msichana huyu. Nilikuwa nawazia zaidi “Kupendeza” kwa suti yangu baada ya kutoka kazini na kuelekea mjini kuungana na Shorty na jamaa wengine na wasichana waliowajua—maili milioni moja kutoka Kilimani.

Akili yangu haikuwa kwake kabisa hata pale aliponiomba nimpeleke tena Roseland kwenye dansi ya weusi iliyofuata. Duke Ellington alikuwa anakuja kupiga muziki na Laura alikuwa na shauku sana ya kumuona. Sikuwa na namna ya kujua kitakachokwenda kutokea.

Aliniomba safari hii nikamchukue nyumbani kwao. Kwa jinsi alivyomuelezea, sikutaka kabisa kuonana na bibi yake, lakini ilinibidi tu kwenda. Bibi yake alikuja kufungua mlango, mwanamke mweusi, mwenye makunyanzi na nywele zenye mvi. Alifungua mlango kiasi cha mimi kutosha kuingia tu, bila hata ya kusema “Karibu.” Nimewahi kutana na wapelelezi na watukutu wenye silaha ambao si makauzu kama bibi huyu.

Nakumbuka sebule yao ya kizamani iliyokuwa imejaa picha za Yesu, sanamu za msalaba. Na alama zingine za dini kila mahali.

Kwa sababu bibi yule hakuongea nami, nami sikuongea naye. Leo hii namuonea sana huruma.

Atakuwa alinionaje na zoot yangu, nywele nimetia dawa na viatu vya rangi ya machungwa? Angekuwa ametusaidia sana iwapo angeenda akipiga kelele na kuita polisi. Kama kitu kinachoonekana kama nilivyoonekana kikija leo kubisha hodi mlangoni kwangu, kikitaka kumuona mmoja wa mabinti wangu wanne, najua kuwa nitapasuka kwa hasira.

Laura alipoingia sebuleni, niliweza kuona wazi kuwa alikuwa amekasirika na kuabika. Tulipokuwa kwenye taxi alianza kulia; alikuwa amejisikia vibaya kwa kudanganya ile mara ya kwanza, hivyo safari hii alikuwa ameamua kusema ukweli juu ya anakokwenda na hapo wakazozana sana na bibi yake. Laura alimwambia bibi yake kuwa ataanza kutoka wakati apendao na kwenda kokote apendako, la sivyo ataacha shule, atatafuta kazi na kwenda kuishi peke yake.

Tulipofika ukumbi wa Roseland tulicheza pamoja na kucheza na watu wengine nyimbo kadhaa. Na mwishowe Duke akawasha moto showtime.

Nilifahamu na Laura alifahamu kuwa hawezi kushindana na wasichana wenye uzoefu wa kucheza dansi, lakini bado aliniambia kuwa alitaka kushindana. Kuja kushtuka yuko kati ya wale wasichana akibadili viatu na kuvaa raba. Wasichana wasiyo na wenzi wa kucheza nao waliponikimbilia nilitingisha kichwa kukataa.

Watu walikuwa wakipiga kelele na kupiga vishindo chini. Walishangilia umahiri wangu na mtindo wa uchezaji wa Laura. Taa na macho ya watu wote yalituelekea sisi. Hawajawahi ona mtu mwepesi kwenye kucheza kama Laura. Nilichochea moto, Laura akawa kama anapaa; mara nimemuinua hewani, nimemtua, nimemzungusha, nyuma, juu tena . . . nywele zake zimemziba uso wote, jasho mwili mzima. Sikuweza kuamini kuwa ana nguvu kiasi kile.

Ukuta wa kelele ulituzunguka; walikuwa wamempata malkia mpya. Nilianza kuona kuwa anaishiwa nguvu. Ilinibidi kumshikilia na kutoka ulingoni. Baadhi ya wanabendi walipiga makofi ya pongezi. Na hata Duke Ellington mwenyewe alisimama kutoka kwenye kiti cha piano na kuinama.

Iwapo uliwakosha watazamaji wa showtime ukitoka wanakuzonga sana, unakua kama timu iliyotoka kuchukua kombe. Kikundi fulani kilimzonga Laura, kikawa kimemnyanyua juu juu. Nami nilikuwa napongezwa kwa kupigwapigwa mgongoni . . . ghafla nikagongana macho na binti mmoja wa kizungu mzuri sana. Naye alikuwa akiniangalia. Sikuwahi muona akija kwenye dansi za watu weusi pale Roseland.

Wakati huo huko Roxbury, kama tu ilivyokuwa kwenye maghetto yote ya watu weusi ya Marekani, kuwa na mwanamke wa kizungu ambaye si Malaya anayejulikana ilikuwa ni heshima ya hali ya juu sana kwa mwanamme mweusi. Na huyu aliyesimama hapa akiniangalia alikuwa mzuri kiasi kwamba nilihisi nipo ndotoni. Nywele ndefu mpaka mabegani, ameumbika vyema na amevaa nguo za gharama.

Nasikia aibu kukiri kuwa nilimsahau Laura mpaka pale alipojinasua kutoka kwenye umati na kunifuata. Nadhani aliona kilichokuwa usoni mwa msichana yule na usoni mwangu tulipokuwa tukienda kudansi.

Nitamwita Sophia.

Kulingana na viwango vya watu weusi, hakuwa mchezaji mzuri. Lakini hilo lilijalisha nini? Niliweza kuona watu waliotuzunguka wakitushangaa. Tuliongea na nilimwambia kuwa alikuwa mcheza dansi mzuri na kumuuliza alikojifunza. Nilikuwa najaribu kufahamu kwa nini yupo pale. Wanawake wengi wa kizungu huja kwenye dansi za weusi kwa sababu ambazo nilizifahamu, lakini ilikuwa ni nadra sana kwa watu aina kama yake kuhudhuria dansi hizo.

Alijibu kila kitu kwa mkato. Lakini katika maongezi yale tulikubaliana kuwa nimuwahishe Laura nyumbani na kurudi haraka kwa taxi. Akaniuliza iwapo nitapenda kwenda matembezi kwa gari hapo baadaye. Nilijihisi mwenye bahati sana.

Ndani ya saa moja nilikuwa nimekwisha mrudisha Laura kwao, na kurudi Roseland. Sophia alikuwa nje akinisubiri.

Alikuwa amepaki gari yake ya kufunguka paa mbali kidogo kutoka ukumbini. Alifahamu alikokuwa akienda. Nje ya Boston, aliingia kwenye barabara nyembamba, kisha akaingia kwenye barabara ambayo haitumiki. Hapo alizima kila kitu isipokuwa redio.
***​
 
Sura ya nne inaendelea.

Kwa miezi kadhaa iliyofuata Sophia alikuwa akinichukua kule mjini-kati nami nilimpeleka kwenye dansi, na kwenye baa za Roxbury. Tulienda kila sehemu, wakati mwingine ilikuwa karibu na asubuhi aliponiacha nyumbani kwa Ella.

Nilimuonyesha kwa watu. Wanaume weusi walimpenda naye alionekana kuwapenda watu weusi wote. Tulitoka pamoja usiku mara mbili au tatu kwa wiki. Sophia alikiri kuwa alikuwa anatoka na vijana wa kizungu “Ili tu kuridhisha macho ya watu.” Alisisitiza kuwa havutiwi na wanaume wa kizungu.

Nilitafakari kwa muda mrefu lakini sikuwahi kufahamu kwa nini alinifuata kijasiri namna ile ule usiku wa kwanza. Nilifikiri labda amewahi kuwa na mtu mweusi hapo kabla-lakini sikumuuliza naye hakuwahi sema. Kamwe usimuulize mwanamke juu ya wanaume wengine. Kuna mawili, atakudanganya na ukawa bado huujui ukweli au atakuambia ukweli ambao haukutaka kuusikia.

Pamoja na hayo alionekana kuzama kwangu. Nilianza kuonana mara chache zaidi na Shorty. Na nilipoonana naye na jamaa wengine alitania, “Nilichana nywele zilizogandamana za mwanakwetu na sasa ana mwanamke kutoka Beacon Hill.” Lakini kwa vile ilijulikana kuwa yeye ndiye alikuwa “Mwalimu” wangu. Mimi kuwa na Sophia kulimpa sifa Shorty. Nilipomtambulisha Sophia kwa Shorty, Sophia alimkumbatia na hilo lilimmaliza kabisa Shorty. Wazungu pekee aliowahi kuwa nao walikuwa ni makahaba na wale wengine duni waliofanya kazi viwandani na wakawa wanataka kuona watu weusi wakoje.

Ni wakati huu nilipoanza kuonekana nikiwa na Sophia ndipo nilipoanza kupata hadhi mjini Roxbury. Mpaka kufikia wakati huo nilikuwa tu mmoja wa vijana waliopaka nywele dawa na kuvaa zoot. Lakini sasa, nikiwa na mwanamke mzungu bora kabisa kuwahi kutembelea baa na klabu zile, na kwa jinsi alivyonipatia pesa za kutumia, hata watu wakubwa na maarufu-watoto wa mjini, wachezesha kamari, mameneja wa vilabu na wengineo walianza kunipongeza kwa kunipiga mgongoni, wakitukaribisha kunywa kwenye meza maalumu na kuniita “Red.” Ndiyo, nilifahamu sababu zao kama nilivyofahamu jina langu: walitaka kuniibia mrembo wangu wa kizungu.

Kwenye maeneo ya maghetto, kama tu ilivyo kwenye mitaa bora-mapambano ni yaleyale ya kupambania kupata hadhi zaidi ya wengine. Nikiwa na miaka kumi na sita sikuwa na pesa ya kununua Cadillac, lakini Sophia alikuwa na gari yake nzuri, nami nilikuwa naye-kitu ambacho kilikuwa ni bora zaidi.

Laura hakuja tena dukani katika siku zote nilizoendelea kufanya kazi. Nilipokuja kukutana naye tena alikuwa ni mwanamke aliyekongoroka, mapepe wa Roxbury alieyeenda jela na kutoka. Alimaliza sekondari lakini wakati huo tayari alikuwa ameshaanza kupotea. Kwa kumpuuza bibi yake alikuwa ameanza kutoka usiku na kunywa pombe. Hili lilipelekea kutumia madawa ya kulevya na baadaye kujiuza. Alipoanza kuchukia wanaume waliomnunua, akageuka kuwa msagaji. Moja ya aibu niliyobeba kwa miaka mingi ni kuwa najilaumu kwa yote hayo. Na kumtenda jinsi nilivyomtenda kwa ajili ya mwanamke wa kizungu inanifanya niumie mara mbili. Kujitetea kwangu pekee ni kuwa, kama ndugu zangu weusi wengine wengi leo, nilikuwa kiziwi, mjinga na kipofu.

Haikuchukua muda mrefu kwa Ella kujua kuwa ninatoka na Sophia. Siku moja asubuhi alichungulia dirishani na kuniona nikishuka kutoka kwenye gari ya Sophia. Haikushangaza kwa Ella kuanza kunichukulia kama nyoka.

Wakati huo huo binamu yake Shorty alikuwa amehamia kwa mwanamke wake aliyemchanganya sana. Sophia alinipa pesa ya kuchangia kodi na Shorty. Niliacha kazi kwenye duka la dawa na kupata kazi nyingine.

Nilipata kazi ya uhudumu huko Parker House, Boston. Nilivaa koti jeupe. Nilifika kwenye ukumbi wa kulia chakula, nilibeba vyombo vichafu ambavyo wahudumu waliviweka kwenye sinia kubwa na kuwapelekea waoshaji.

Asubuhi moja nilienda kazini nikitegemea kufukuzwa, nilikuwa nimechelewa sana. Lakini wafanyakazi wote wa jikoni walikuwa wamehamaki na kufadhaika kuweza kutambua kuchelewa kwangu: ndege za Wajapan zilikuwa zimepiga mabomu sehemu moja inayoitwa Pearl Harbor.
Mwisho wa sura ya nne.​
 
SURA YA TANO

MHARLEM

Kahawa! Keki! Pipi! Aisikrimu! Nilipiga kelele huku nikirushwa-rushwa kwenye treni kwa saa nne kati ya Boston Na New York. Safari hizo zilifanyika kila baada ya siku moja. Mze mmoja aliyekuwa kuli wa kwenye treni na rafiki wa Ella alikuwa amenitafutia kazi kwenye shirika la reli. Alimwambia Ella kuwa vita ilikuwa ikichukua wafanyakazi wengi wa reli hivyo nikiweza kutambulika kama nina miaka ishirini na moja atanitafutia kazi.

Ella alikuwa anataka nitoke Boston na niwe mbali na Sophia. Alitamani sana kuniona nimevaa kama vijana weusi waliotembelea Roxbury wakiwa wamevaa sare za jeshi-wakiwa likizo kutoka kambini. Lakini kwa umri wangu wa miaka kumi na sita hilo halikuwezekana.

Nilikubaliana na kazi ya kwenye shirika la reli kwa sababu zangu binafsi. Kwa miaka mingi nilikuwa nimetamani kutembelea jiji na New York. Toka nilipofika Roxbury nilikuwa nimesikia habari nyingi kuhusu New York. Hata nilipokuwa Lansing nilikuwa nimesikia jinsi jiji la New York lilivyo zuri, hasahasa eneo la Harlem. Hata baba yetu aliizungumzia vizuri sana Harlem na kutuonyesha picha za maandamano ya wafuasi wa Marcus Garvey. Na kila mara Joe Louis alipomshinda mpinzani wa kizungu, picha kubwa kwenye magazeti ya weusi kama Chicago Defender, Pittsburgh Courier na Afro American yalionyesha umati wa watu weusi wa Harlem wakishangilia na kumpungia mikono na bondia huyo, naye akiwapungia kutoka kwenye kibaraza cha hoteli ya Theresa. Yote niliyosikia kuhusu jiji la New York yalikuwa ni ya kustaajabisha, vitu kama taa kali za Broadway, ukumbi wa dansi wa Savoy na ukumbi wa Apollo huko Harlem, sehemu ambako bendi kubwa zilipiga muziki na wasanii weusi maarufu na mitindo mipya ya kucheza dansi ilianzia.

Lakini huwezi tu kutoka Lansing au Boston, au kwingine kokote na kwenda New York bila ya pesa. Hivyo sikuwazia sana suala la kwenda New York hadi pale nilipopata usafiri wa bure kupitia maongezi ya Ella na mzee yule ambaye alikuwa ni mshiriki mwenzake kanisani.

Kitu ambacho Ella hakufahamu ni kuwa nitaendelea kuonana na Sophia. Nilipomueleza kuhusu kazi yangu mpya, Sophia aliniambia kuwa anaweza kutoka siku kadhaa za juma, hivyo atatoka kila usiku nitakapokuwa Boston, maana yake nikipata kazi tutaonana kila baada ya siku moja. Sophia hakutaka kabisa niondoke, lakini alikuwa akiamini kuwa nimefikia umri wa kutumikia jeshini na hivyo kazi ya kwenye treni itaniepusha na kuandikishwa jeshini.

Shorty naye alifikiri kuwa itakuwa nafasi nzuri sana kwangu. Alikuwa na wasiwasi sana juu ya kuitwa jeshini ambako alijua hakuko mbali. Kama walivyokuwa mamia ya vijana wanaume weusi walioishi maeneo ya maghetto, kuna vitu alianza kutumia ambavyo vilisemekana vinafanya moyo wako uonekane una tatizo wakati wa kuchunguzwa na madaktari wa jeshi-na hivyo kukufanya uepuke kuandikishwa.

Maoni ya Shorty kuhusu vita yalikuwa kama yangu na watu weusi wengine, kwamba, “Mzungu anamiliki kila kitu lakini anataka twende kupigana na kufa kwa ajili yake? Apambane mwenyewe.”

Basi kwenye ofisi ya ajira ya shirika la reli iliyokuwa kwenye mtaa wa Dover, karani wa kizungu aliyechoka alianza kunisaili nilipofika. Nilipomwambia kuwa nina miaka ishirini na moja hata hakuinua macho kunitazama. Nilitambua mara moja kuwa nimeishapata kazi.

Niliahidiwa kazi ya mpishi namba nne kwenye treni ya kutoka Boston kwenda New York, lakini kwa wakati huo nilifanya kazi kwenye yadi ya Dover nikisaidia kupakia vyakula kwenye treni. Nilifahamu kuwa mpishi namba nne ni jina tu zuri la muosha vyombo, uzuri ni kuwa haitakuwa mara yangu ya kwanza, na kwa kuwa nitakuwa nasafiri nitakako, sikuona shida yoyote. Kwa muda kidogo waliniweka kwenye treni ya “The Colonial” iliyokuwa ikienda Washington D.C.

Wafanyakazi wa jikoni waliokuwa chini ya mpishi mkuu ambaye alikuwa ni mtu kutoka visiwa vya Karibeani aliyeitwa Duke Vaugh. Wafanyakazi hao walifanya kazi yao kwa ufanisi wa hali ya juu sana ndani ya eneo dogo lililobanana. Kwenye kelele za treni iliyokuwa ikienda, wahudumu walitaja mahitaji ya wateja na wapishi walifanya kazi kama mashine, kisha vyombo vyote vichafu vilivyotumika kwenye safari ya maili mia tano vilinifikia. Tulipokuwa tukilala Washington D.C,. Nilienda matembezi kutazama maeneo ya mjini-kati. Nilishangaa kukuta ndani ya mji mkuu kuna maelfu ya watu weusi wakiishi maisha duni kuliko yoyote niliyowahi kuyaona kwenye eneo masikini kabisa la Roxbury. Umbali kidogo tu kutoka Capitol Hill watu hao waliishi kwenye vibanda visivyo na sakafu, barabara za mitaa zikiwa chafu kupita kiasi, zikiwa na majina kama Barabara ya Nguruwe au Barabara ya Mbuzi. Nimeona vitu vingi lakini sikuwahi kuona wauza madawa, makahaba, wazurulaji na wacheza kamari mtaani wamejazana sehemu moja namna ile. Na hata kulikuwa na watoto waliokuwa nusu uchi na peku wakikimbia huku na kule usiku wakiomba pesa. Baadhi ya wapishi na wahudumu wa kwenye treni waliniambia niwe makini kwa kuwa uporaji na kuchomana visu hutokea kila siku kwa watu hawa-umbali kidogo tu kutoka ikulu ya Marekani.

Lakini niliona pia watu weusi wengine wenye afadhali; hawa waliishi kwenye majengo ya matofali mekundu yaliyochoka. Mfanyakazi mmoja wa reli mzee aliniambia kuhusu Washington kuwa na watu weusi wa “Daraja la kati” wengi. Wengi wakiwa na shahada kutoka Chuo Kikuu cha Howard, wengi wao wakifanya kazi za usafi, ulinzi, kupokea mizigo, kuendesha taxi na nyingine kama hizo. Kazi ya kupeleka barua ilikuwa ya heshima sana kwa mtu mweusi wa Washington.

Baada ya safari kadhaa za Washington, nilipata bahati ya kuambiwa kuwa nitambadili mtengeneza sandwich kwenye treni ya kwenda New York. Kufika New York, kabla hata abiria wa kwanza hajashuka tayari nilikuwa nimevaa zoot yangu.

Mpishi alinichukua kwenye taxi hadi Harlem. Maeneo ya wazungu ya New York tuliyoyapita yalionekana kama sehemu ndani ya filamu, kisha punde tu baada ya kupita Central Park, kwenye mtaa wa 110, rangi za watu zikaanza kubadilika.

Barabara yenye pilika nyingi-barabara ya saba ilipita mbele ya eneo moja lililoitwa Small’s Paradise. Wafanyakazi wenzangu waliniambia kabla ya kutoka Boston kuwa hicho ndicho kilikuwa kijiwe chao pendwa cha usiku katika Harlem na kuwa ninapaswa kukitembelea. Hakuna eneo la biashara la watu weusi lililonivutia kama lile. Ndani ya baa nzuri na kubwa ya mviringo kulikuwa na watu weusi thelathini au arobaini wakinywa na kuzungumza.

Nilivutiwa mara moja, nafikiri hasa na nguo zao za kawaida na tabia zao. Sehemu yoyote nilipowaona watu weusi kumi wa Boston, achilia Mbali wale wa Lansing—wakinywa pamoja lazima kungekuwa na kelele nyingi.

Lakini kati ya Waharlem hawa wengi kulisikika tu minong’ono na sauti za chini. Wateja waliingia na kutoka. Nao wahudumu walijua karibu kila mteja anachokunywa na walihudumia bila kuulizauliza. Wengine walikuwa na chupa moja ya pombe mezani. Kila mtu mweusi niliyemfahamu alikuwa akijitahidi kuonyesha ni kiasi gani cha pesa alichonacho. Lakini hawa wa Harlem walilipa bili zao kimyakimya. Walikunywa kwa utulivu na walimpa ishara tu ya kichwa mhudumu kuwa ampatie rafiki yao fulani kinywaji. Wahudumu nao walikuwa wataratibu kama wateja wao.

Tabia yao ilionekana si ya kujifanya au kuigiza. Nilishangazwa sana. Ndani ya dakika tano nilizokaa pale Small’s, nikawa nimeachana na Roxbury na Boston milele.

Nilikuwa bado sijajua kuwa hawa si wale unaoweza kusema ni watu weusi wa kawaida wa Harlem. Baadaye, yaani baadaye usiku huo huo nilifahamu kuwa Harlem kuna mamia elfu ya watu weusi wa aina yangu, watu wenye kelele na wenye kujionyesha kama tu watu weusi wa maeneo mengine. Lakini watu hawa walikuwa walikuwa ni wakongwe wa Harlem, watu wenye kujielewa. Kamari za mchana zilikuwa zimeishaisha na kamari na pilikapilika zingine za usiku zilikuwa bado kuanza. Watu wa kawaida ambao hutoka usiku walikuwa majumbani mwao wakipata chakula cha usiku baada ya kazi za mchana kutwa.

Kutoka Small’s nilichukua taxi hadi ukumbi wa Apollo. (Nakumbuka vyema kuwa bendi ya Jay McShann ilikuwa inapiga, maana baadaye muimbaji wake, Walter Brown, alikuja kuwa rafiki yangu. Walter aliyekuwa akiimba “Hooty Hooty Blues.” Kutoka hapo nilienda upande wa pili wa mtaa wa 125, kwenye barabara ya saba. Niliona hoteli kubwa ya Theresa, ilikuwa ndiyo hoteli bora kabisa ambayo mtu mweusi aliweza kukaa wakati ule, miaka mingi kabla ya hoteli za mjini-kati hazijaruhusu watu weusi kulala. “Kwa sasa Theresa hoteli inajulikana sana kama hoteli aliyolala Fidel Castro alipohudhuria mkutano wa umoja wa mataifa. Kitendo kilichoichanganya kisaikolojia idara ya usalama ya Marekani ambayo ilitaka kumbana kwenye eneo la Manhattan tu, hawakuwazia kabisa kuwa atakaa Harlem na kuwavutia watu weusi namna ile.)

Hoteli ya Braddock haikuwa mbali, ilikuwa kwenye mtaa wa 126, kwenye mlango wa nyuma wa ukumbi wa Apollo. Nilifahamu kuwa baa yake ilikuwa kijiwe maarufu sana cha watu weusi maarufu. Niliingia ndani na kuona watu wengi maarufu kama Dizzy Gillespie, Billy Eckstine, Billie Holiday, Ella Fitzgerald na Dinah Washington.

Dinah Washington alipokuwa akiondoka na rafiki zake, nilimsikia mtu fulani akisema kuwa alikuwa akielekea ukumbi wa Savoy ambako Lionel Hampton alikuwa akipiga usiku huo—wakati huo alikuwa ni muimbaji wa Hampton. Ukumbi wa Savoy ulifanya ukumbi wa Roseland kule Boston uonekane mdogo na wa hovyo. Na uchezaje lindy hoppy wa pale uliendana na hadhi ya ukumbi. Bendi ya Hampton ilikuwa na wanamuziki mahiri kama Amett Cobb, Illinois Jacquet, Dexter Gordon, Alvin Hayse, Joe Newman na George Jenkins. Nilicheza mara kadhaa na wasichana.

Pengine theluthi ya waliokaa pembeni walikuwa ni wazungu, wengi wao wakitizama watu weusi wanavyocheza, lakini baadhi walicheza wenyewe kwa wenyewe—na kama ilivyokuwa Boston, wanawake wachache wa kizungu walicheza na watu weusi. Watu walikuwa wakimpigia kelele Hampton apige kibao cha “Fylin’ Home”, mwishowe alikipiga. (Niliweza kuamini habari nilizozisikia huko Boston kuwa—Siku moja Hampton alipopiga kibao “Flyin’ home” mnegro mmoja mvuta bangi aamini kuwa anaweza kupaa, hivyo alijaribu kupaa kwa kujirusha kutoka kwenye kibaraza cha ghorofa ya pili. Aliishia kuvunjika mguu, tukio hilo limetungiwa hadi wimbo na Earl Hines, unaitwa “Second Balcony Jump.”) Sijawahi kuona uchezaji wa moto namna ile. Baada ya nyimbo chache za kupooza ukumbi, wakamleta Dinah Washington. Aliimba kibao chake “Salty Papa Blues,” watu wale walikuwa karibu kung’oa paa la ukumbi wa Savoy. (Masikini Dinah! Mazishi yake yamefanyika si muda mrefu huko Chicago. Nilisoma kuwa zaidi ya watu elfu ishirini waliona mwili wake, nami nilipaswa kuhudhuri, masikini Dinah! Tulikuja kuwa marafiki wazuri sana wakati ule.)

Usiku wangu huu wa kwanza katika ukumbi wa Savoy, ulikuwa Usiku wa Jikoni, ilikuwa ni utamaduni kwa usiku wa Alhamisi kuwa usiku wa wafanyakazi wa majumbani. Naweza sema idadi ya wanawake ilikuwa mara mbili ya ile ya wanaume, waliohudhuria hawakuwa tu wafanyakazi wa jikoni na wahudumu wa majumbani, bali pia wake wa wanajeshi na wanajeshi wanawake, wakitafuta watu. Nje ya ukumbi nilipotoka, nilimsikia kahaba mmoja akilalama sana kuwa wataalamu wanashindwa kufanya biashara sababu ya wasiojua kazi.

Sehemu yote ya Lenox na barabara ya saba na ya nane ya Harlem ilikuwa kama soko kubwa lililochangamka. Mamia ya wanajeshi na wanamaji weusi, wanajeshi vijana na waliokuwa wakishangaashangaa kama mimi walipita. Kipindi hiki ilikuwa ni marufuku kwa wanajeshi wa kizungu kufika Harlem. Kuna visa kadhaa vya wanajeshi kuporwa na wanajeshi kadhaa wa kizungu walikutwa wameuawa. Polisi nao walikuwa wanajaribu kuwashawishi raia wa kizungu kutokuja, lakini wale waliotaka waliweza kuja. Kila mwanaume ambaye hakuwa na mwanamke aliandamwa na makahaba. Makuwadi nao walisogelea na kunong’ona, “Kila aina ya wanawake, unataka mwanamke wa kizungu?” na wachakarikaji nao walikuwa wakiuza vitu vyao, “Pete ya almasi dola mia moja; saa dola tisini na tisa—ziangalie—chukua zote kwa dola ishirini na tano.”

Miaka miwili mbele ningeweza kuwa mwalimu wao, lakini usiku ule nilistaajabishwa sana. Hii ndiyo dunia yangu hasa. Usiku ule nilianza safari yangu ya kuwa Mharlem. Nilikuja kuwa mmoja kati ya wachakarikaji wanyonyaji kabisa kati ya wakazi milioni nane wa New York. Milioni nne wakifanya kazi na milioni nne nyingine wakiwanyonya.
 
Sura ya nne inaendelea

Usiku nilibeba boksi la sandwich na na kidumu cha kahawa na kupita mabehewani nikiuza-safarini kurudi Boston. Akilini mwangu sikuamini kabisa mambo niliyoyaona na kuyasikia. Nilitamani tungekuwa tunaiva na Ella ili nimuelezee nilivyohisi. Lakini nilimuelezea Shorty na kumshawishi walau aende kujionea ulimwengu wa muziki wa New York. Sophia alinisikiliza pia, aliniambia kuwa sitaridhika na popote isipokuwa New York. Alikuwa sahihi. Kwa usiku mmoja tu New York-Harlem ilikuwa imenilevya. Yule mtu wa sandwich niliyechukua kazi yake alikuwa na nafasi ndogo sana ya kuipata tena. Nilitembea nikipiga kelele mabehewani, nikiuza kahawa, pipi, keki, aisikrimu kwa kasi kadri ambavyo waliweza kunipatia. Haikunichukua hata juma moja kufahamu kuwa unachotakiwa tu kufanya ni kufanya vituko mbele ya wazungu nao watanunua chochote uuzacho. Ilikuwa kama kuliza kitambaa cha kung’arishia viatu. Wahudumu wa mgahawa wa treni na wabeba mizigo walifahamu hilo pia. Walijitia hamnazo ili wapate bakshishi kubwakubwa. Tulikuwa kwenye ile dunia ya watu weusi ambao ni wahudumu na wanasaikolojia kwa wakati mmoja, tukifahamu kuwa wazungu walikuwa wakijichukulia wa muhimu sana kiasi kwamba walikuwa tayari kulipa bila hiyana, na pesa nyingi kwa ajili tu ya kuhisi wanahudumiwa na kuburudishwa.

Kila tulipolala Harlem nilienda kutembelea maeneo mapya. Mara ya kwanza nilikodi chumba kwenye makazi ya YMCA ya Harlem, sababu palikuwa karibu na Small’s Paradise. Kisha baadaye nikapata chumba cha bei rahisi zaidi kwenye nyumba za kupangisha za bi Fishers. Mahali hapo palikuwa karibu na YMCA. Wafanyakazi wengi wa reli walikaa kwa bibi Fishers. Nilitembelea si maeneo ya biashara tu, bali nilienda hadi kwenye makazi ya watu, nilitembelea maeneo ya makazi bora na yale duni kabisa. Kutoka Sugar Hill karibu na viwanja vya Polo, mahali ambako watu wengi maarufu waliishi. Hadi kwenye makazi duni kabisa ambayo yalitambaliwa na kila kitu unachokijua kuwa ni haramu na si cha kimaadili. Mapipa ya taka yaliyojaa au kuanguka, waraibu wa dawa za kulevya, ombaomba. Baa chafu, makanisa ya chumba kimoja ambayo injili ilisikika ikipigwa. Migahawa michafu, saluni za urembo zilizojaa moshi kutokana na kuchomwa kwa nywele za wanawake weusi, saluni za kiume zikitangaza kuwa na wataalamu wa kuweka nywele dawa. Cadillacs mpya na za mtumba zikiwa zimejaa mitaani.

Kila kitu kilikuwa kama Lansing magharibi au Roxbury kusini lakini mara elfu yake. Kulikuwa na kumbi ndogo za muziki za chini ya nyumba, zikiwa na kadi za matangazo zilizosema “Unakodishwa kwa ajili ya tafrija.” Niliingia kwenye moja ya kumbi hizo. Nilikuta watu weusi thelathini au arobaini, wakila, wakinywa, wakicheza dansi na kamari huku jasho likiwatoka. Muziki umefunguliwa hadi mwisho. Huko mtu aliweza kupata kuku wa kukaanga na viazi kwa dola moja. Bia ziliuzwa kwa senti hamsini

Watu, weupe kwa weusi walikuzonga, wakiongea kwa kasi kadri wawezavyo ili kukushawishi kununua nakala ya Daily Worker “Gazeti hili linajaribu kudhibiti kodi za nyumba . . . Litamfanya mwenye nyumba mlafi alazimike kumaliza tatizo la panya nyumbani mwako . . . Gazeti hili linawakilisha chama pekee ambacho kimewahi kuweka mtu mweusi kama mgombea mwenza wa Urais wa Marekani . . . Nataka tu usome. Haitakuchukua muda wako mwingi . . . Unafikiri ni nani alipambana vikali zaidi ili kusaidia wale vijana wa Scottoboro waachiwe huru?” Mambo niliyosikia kutoka kwa watu weusi ni kuwa gazeti lile lilikuwa na uhusiano na Warusi, lakini kwa akili yangu changa ya wakati ule sikuelewa wanachomaanisha. Magazeti na matangazo ya radio yalijaa habari za washirika wetu-Warusi. Watu wenye nguvu, wakulima wanaoisaidia Marekani kupambana na Hitler na Mussolini.

Kipindi hicho New York ilikuwa ni mbingu kwangu. Na Harlem ilikuwa mbingu ya saba. Nilishinda sana Small’s na Braddock kiasi kwamba wahudumu waliponiona tu naingia walinimiminia glasi ya Bourbon, kinywaji changu pendwa. Haikuchukua muda wachakarikaji wa Small’s na wasanii wa Braddock wakaanza kuniita “Red” sababu ya nywele zangu nyekundu. Wakati huo nilikuwa nikitia nywele zangu dawa kwenye saluni ya Abbott na Fogey huko Boston; ilikuwa ndiyo saluni bora kabisa ya kuweka nywele dawa kwenye pwani ya mashariki ya Marekani—kulingana na wanamuziki maarufu walionielekeza huko.

Rafiki zangu sasa wakatia ndani wanamuziki kama Sonny Greer, mpiga ngoma wa Duke Ellington. Mpiga Violini hodari, Ray Nance, na watu wengine kama Cootie Williams na Eddie “Kichwa safi” Vinson ambaye alikuwa akitania kuwa hakuwa na kitu kichwani bali ngozi tu. Pia nilifahamiana na Sy Oliver; alikuwa amemuoa msichana fulani aliyekuwa na rangi nyekundu hivi, waliishi huko Sugar Hill. Nakumbuka kibao chake maarufu kilikuwa ni “Yes, Indeed!”

Mtu wa sandwich aliporudi aliwekwa kwenye treni nyingine. Alilalamika kwamba alikuwa ni mkongwe lakini mauzo yangu yalifanya waweze kumtuliza. Wahudumu na wapishi walianza kuniita “Sandwich Red.”

Kufikia wakati huo walikuwa wakipingiana kwa kutania kuwa sitadumu, haijalishi mauzo yangu yakoje, maana nilikuwa nimekuwa kijana mjeuri kupita kiasi. Matusi ndiyo ilikuwa lugha yangu, nilitukana hata wateja, hasa wanajeshi; hao sikupatana nao kabisa. Nakumbuka wakati fulani malalamiko ya wateja yaliposababisha nipewe onyo na nikaamua kuwa makini, lakini siku hiyo mwanajeshi mmoja wa kizungu aliyekuwa mnene alisimama mbele yangu, alikuwa amelewa sana hadi anapepesuka, kwa sauti kubwa kiasi kwamba kila mtu alisikia, alisema, “Nataka kupigana na wewe Nigger.” Nilicheka na kumwambia, “Sawa nitapigana nawe, lakini umevaa nguo nyingi sana.” alikuwa amevaa koti kubwa la kijeshi. Alilivua, niliendelea kucheka na kumwambia kuwa bado alikuwa amevaa nguo nyingi. Niliendelea kumvua nguo mlevi yule hadi akabaki kifua wazi. Behewa zima lilikuwa likimcheka, baadhi ya wanajeshi wenzake waliamua kumuondoa nami niliendelea na kazi. Sijawahi sahau kuwa nisingeweza kumpiga mzugu yule vilivyo hata kwa kutumia rungu kama nilivyofanya kwa kutumia akili.

Wapishi na wahudumu wengi wa treni za New Haven waliopo kazini leo watakuwa wanamkumbuka mzee Pappy Cousins. Alikuwa ndiye msimamizi wa treni ya “Yankee clipper”. Ndiyo, alikuwa ni mzungu, wa kutoka Maine. (Kuna watu weusi waliofanya kazi kwenye behewa la mgahawa kwa miaka thelathini au arobaini, lakini wakati huo hakukuwa na msimamizi mweusi kwenye treni za New Haven.) Basi huyu Pappy Cousins alipenda sana wiski, na pia alipenda watu wote, hata mimi. Alipuuzia malalamiko mengi ya wateja kunihusu. Alikuwa akiwaomba manegro wazee niliofanya nao kazi kujaribu kuniweka sawa.

“Haambiliki kabisa,” walilalamika. Na kweli nilikuwa siambiliki. Nyumbani huko Roxbury walikuwa wakiniona nikitoka na Sophia, niko ndani ya suti zangu za zoot. Kisha wakashangaa nimefika kazini nikiwa na makelele na mtukutu, kichwani nina bangi na pombe. Na nitakuwa hivyo nikiuza sandwich kwenye mabehewa hadi tunafika New York. Nilishuka na kupasua katikati ya umati wa mchana kwenye stesheni ya Grand Central. Wazungu wengi walinipisha njia na kuniruhusu nipite. Zoot ilikaa vyema kama ukiwa mrefu, nami nilikuwa mrefu wa zaidi ya futi sita. Na nywele zangu zilizotiwa dawa zilikuwa nyekundu kama moto, hakika nilikuwa kituko, lakini ujinga wangu ulinifanya nijione “Maridadi sana.” Kiatu changu kilichobinuka na kutuna mbele hakikuwa kitu kingine zaidi ya kiatucha Florsheims, kiatu hicho kwa watu weusi wa maeneo ya maghetto kilikuwa kama Cadillac. (Baadhi ya makampuni ya viatu yalitengeneza viatu hivi vituko kwa ajili ya kuuza kwenye maeneo ya maghetto ambako watu weusi wajinga kama mimi tulilipia pesa nyingi ili tu kuonekana matajiri). Kutoka hapo, nilipita Small’s Paradise, Braddock Hotel na maeneo mengine kadri ambavyo malipo yangu ya dola ishirini na tano yangeruhusu. Nilikunywa pombe, nikavuta bangi na kuipaka New York “Red” kwa marafiki lukuki, mwishowe nilirudi kwa bibi Fishers kulala kwa saa chache kabla “Yankee Clipper” haijaanza tena safari.

***​
 
Back
Top Bottom