Kitabu: Maisha ya Malcom X

SURA YA NANE

MBANO

Kulikuwa na mtu anagonga mlangoni….

Sammy alipofahamu kuwa ni West Indian Archie, aliweka kioo kilichokuwa na unga wa cocaine chini ya uvungu na kwenda kufungua mlango.

“Red nataka pesa zangu!”

Bastola .32-20. Nilikuwa nimekutana na watu weusi hatari sana, lakini sijawahi kutana na mtu ambaye hakuwa tayari kufa na akamchokoza West Indian Archie. Alinitisha hasa. Sikuelewa kinachoendelea kiasi kwamba maneno yalinikwama.

“Nini kinaendelea?”

Archie akaniambia kuwa alihisi kuna uhuni nilipomwambia kuwa nimeshinda, lakini akanilipa dola mia tatu na kujiambia kuwa ataenda kuhakiki kwenye risiti za kamari; na kama alivyokuwa amehisi, sikucheza namba niliyodai nilicheza.

“Haiwezekani!” Nilianza kuongea haraka haraka. Kwa jicho la pembeni nilimuona Sammy akipeleka mkono wake chini ya mto alikokuwa akiweka bastola yake aina ya .45 “Archie pamoja na akili zako zote bado ukamlipa mtu ambaye hajashinda?”

Archie akamuelekezea bastola Sammy na kumfanya agande kama sanamu. “Nitakupiga risasi.” Kisha akanigeukia, “Hauna pesa zangu?” nitakuwa nilikataa kwa kutingisha kichwa“Ninakupa mpaka kesho saa sita mchana.” Alibamiza mlango na kuondoka.

***

Ni kanuni ya kawaida kwa wachakarikaji kutokubali kupigwa mkwara au kufanywa mjinga-mmoja afe au akimbie. Pesa haikuwa tatizo. Nilikuwa bado na kama dola mia mbili. Kama pesa ingekuwa ndiyo tatizo Sammy angeniongezea; na kama hangekuwa nayo mfukoni, wanawake wake wangeweza kuipata mara moja. Na hata west Indian Archie mwenyewe angeweza kuniazima dola mia tatu iwapo ningemuomba, alishapata dola elfu kadhaa kutoka kwangu kama asilimia kumi ya pesa nilizocheza. Kuna kipindi aliposikia kuwa sina kitu alinitafuta na kunipatia pesa huku akisema, “Weka hizi mfukoni.”

Shida ilikuwa ni hali aliyokuwa ametuingiza kutokana na matendo yake. Kwenye dunia yetu ya kipambanaji heshima ilikuwa ni kitu muhimu sana. Hakuna mchakarikaji ambaye angeruhusu ijulikane kuwa amezidiwa ujanja na kufanywa mjinga. Na zaidi ni kuwa hakuna mpambanaji aliyetakiwa kuruhusu kupigwa mkwara, kuonyesha kuwa anaweza tishwa-kwamba si jasiri.

West Indian Archie alifahamu vyema kuwa wapambanaji huibuka pale wanapofanikiwa kuwazidi ujanja wapambanaji wazee na kisha kuwatangaza. Aliamini nilikuwa najaribu kufanya hivyo.

Mimi pia nilifahamu vyema kuwa atalinda heshima yake kwa kutangaza jinsi alivyonipiga mkwara.

Kwa sababu ya kanuni hii, niliwafahamu wapambanaji ambao baada ya kutishwa waliondoka Harlem kwa aibu. Mara tu taarifa zitakaposambaa hakutakuwa na suluhu tena kati yetu. Watu watakuwa tu wanasubiria taarifa za pambano letu.

Pia nilifahamu mapambano kadhaa ambayo mmoja aliishia chumba cha maiti na mwingine gerezani au kwenye kiti cha umeme kwa mauaji.

Sammy alinipatia bastola yake. Bunduki zangu nilikuwa nimeziacha nyumbani. Niliiweka mfukoni, mkono mmoja mfukoni nimeishikilia, kisha nikatoka.

Sikutakiwa kujificha. Nilitakiwa kuonekana maeneo yangu yote niliyozoea kutembelea. Nilishukuru Reginald hakuwepo mjini wakati huo, angejaribu kunilinda na si kutaka apigwe risasi ya kichwa na West Indian Archie.

Nilisimama kwenye kona nikiwa sijielewi—kama walivyo mateja. West Indian Archie ananipiga mkwara? Ananidhihaki? Baadhi ya wapambanaji wakongwe walipenda sana kuwazingua wapambanaji vijana. Lakini nilifahamu kuwa West Indian Archie hawezi fanya vile kwa ajili ya dola mia tatu. Lakini kwenye msitu wa Harlem kila mtu alikuwa mhuni. Watu waliwazingua hata ndugu zao. Wachezesha kamari mara nyingi waliwazingua mateja walioshinda, mateja hao walikuwa mateja hasa kiasi kwamba hawakuwa na uhakika wa namba walizocheza.

Nilianza kuwaza iwapo West Indian Archie atakuwa amekosea. Ni kweli nitakuwa nimechanganya namba? Nakumbuka vyema kuwa nilicheza namba mbili na kuwa ni moja tu ndiyo ainyumbulishe, je nilichanganya namba?

Ulikuwa ni muda wa kwenda kumchukua Jean Parks kwenda mjini-kati kumuona Billie kwenye club ya Onyx. Mambo mengi yalikuwa yanapita kichwani wakati huo. Niliwaza nimpigie simu na kumwambia kuwa nimeahirisha na kutoa visingizio vya uongo na ukweli. Lakini nilifahamu vyema kukimbia litakuwa ndiyo jambo baya zaidi kwangu. Basi nikaenda nyumbani kwa Jean kumchukua. Tulichukua Taxi hadi mtaa wa 52. Ndani kulikuwa kumejaa watu, club ya Onyx ilikuwa na eneo dogo sana.

Billie alikuwa ametoka tu kumaliza kuimba alipotuona mimi na Jean. Gauni lake jeupe liling’aa kwenye mwanga. Wimbo wake uliofuata alichagua ambao alijua ninaupenda sana “You don’t know what love is.”

Alipomaliza alikuja mezani petu, walikumbatiana na Jean maana walikuwa hawajaonana kwa muda mrefu. Mara moja Billie alitambua kuwa kuna kitu hakiko sawa kwangu. Alifahamu kuwa muda wote nakuwa nimelewa madawa, lakini alinijua vyema kuweza kutambua kuwa kuna jambo jingine linanitatiza, kwa lugha yake ya kawaida ya matusi aliniuliza kinachonitatiza. Nami kwa lugha yangu ileile ya matusi niliyokuwa nayo wakati huo-nilijidai hakuna kitu chochote hivyo akaacha kunihoji.

Usiku huo mpiga picha wa club alitupiga picha ya pamoja. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kumuona Lady Day. Amekufa; madawa na kuvunjwa moyo vimesimamisha moyo ule mkubwa kama banda, na ile sauti na mtindo wa uimbaji ambao hakuna aliyewahi kuuiga ipasavyo. Lady Day aliimba kwa hisia za mtu mweusi zilizotokana na machungu ya kukandamizwa kwa karne kadhaa. Inasikitisha mwanamke yule mzuri hakuishi sehemu ambayo ukuu halisi wa mtu mweusi ulithaminiwa.

Nilienda kwenye maliwato ya Onyx na kuvuta kidogo cocaine niliyotoka nayo kwa Sammy. Tulipokuwa tunarudi Harlem, tukaamua kupitia sehemu kupata vinywaji. Jean alikuwa hajui chochote kinachoendelea hivyo alipendekeza baa niliyopendela sana kwenda, baa ya La Marri-Cherri iliyokuwa kwenye makutano ya mtaa wa 147 na barabara ya St. Nicholas. Nilikuwa na bastola na cocaine ilikuwa imeniongezea kujiamini hivyo nilikubaliana na pendekezo lake. Nililewa sana hivyo nikamwambia Jean achukue taxi arudi nyumbani. Naye sijawahi kumuona tena.

Kama mpumbavu sikuondoka baa ile. Niliendelea kukaa pale kama mpumbavu mmoja mkubwa sana, mgongo nimeuelekeza mlangoni huku nikiwaza kuhusu West Indian Archie. Toka siku ile sijawahi tena kaa sehemu na kuupa mlango mgongo, na sitakuja fanya hivyo kamwe. Lakini ni jambo zuri nilifanya hivyo siku ile. Nina hakika iwapo ningemuona West Indian Archie anaingia, ningempiga risasi kwa lengo la kummmaliza kabisa.

Ghafla nikashtukia Archie amesimama mbele yangu akitukana huko amenitolea bastola. Hakika alikuwa anafanya watu wote wamuone yeye ni nani. Aliniita majina mabaya ya kila aina na kunitisha.

Kila mtu, wateja na wahudumu waliganda kama walivyokuwa. Mziki uliendelea kupiga kwenye Jukebox. Sijawahi muona Archie kalewa zaidi ya wiski. Siku hiyo kilikuwa kitu tofauti. Nilifahamu vyema utamaduni wa wapambanaji kutumia madawa ya kulevya kabla ya kazi.

Kichwani mwangu niliwaza, “nitamuua Archie-nasubiri tu ageuke.”

Ilionekana Archie alisoma mawazo yangu. Aliacha kunitukana na kusema “Unafikiri utaniua Red. Basi ngoja nikuambie jambo unalotakiwa kulitafakari kwa kina. Nina miaka sitini. Ni mzee. Nimeisha kaa Sing Sing, maisha yangu yamefika mwisho. Wewe ni kijana. Hata ukiniua unakuwa umepotea. Utaishia tu jela.”

Nimekuwa nikiwaza kuwa pengine Archie alikuwa anajaribu kunitisha nikimbie ili alinde heshima na maisha yake. Pengine ndiyo maana alikuwa kalewa. Hakuna mtu aliyefahamu kama sijawahi ua mtu, lakini kila mtu, na hata mimi mwenyewe hakuwa na shaka kuwa niliweza kuua mtu.

Sikumbuki vizuri kilichotokea. Lakini kulingana na sheria-iwapo Archie angetoka nje baada ya kunitukana kama alivyofanya, basi ningelazimika kumfuata. Tungetupiana risasi mtaani.

Lakini rafiki zake kadhaa walimfuata wakimsihi, “Archie . . . Archie.” Na wakamvuta pembeni.

Baada ya kukaa kidogo, niliinuka. Nililipia vinywaji na kutoka. Nilitoka nje bila kuangalia nyuma. Nilisimama pale nje baa nzima ikiniona, nilisimama pale kwa kama dakika tano huku nimeweka mkono mfukoni. Nilipoona West Indian Archie hatokei, niliondoka zangu.

***
 
Bado tunafuatilia chief

Sent from my SM-A013G using JamiiForums mobile app
 
Ilikuwa kama saa kumi na moja ya alfajiri nilipomuamsha muigizaji fulani wa kizungu tuliyefahamiana huko mjini-kati, ilikuwa ndani ya hoteli ya Howard katika mtaa wa 45.

Nilihitaji kutumia madawa

Huwezi amini kiasi cha madawa ya kulevya nilichotumia ndani ya saa kadhaa zilizofuata. Nilinunua kasumba kutoka kwa jamaa yule kisha nikachukua taxi kwenda nyumbani kwangu kuvuta. Niliweka bastola yangu tayari kwa lolote, hata ningesikia mbu anakohoa.

Simu yangu iliita, kupokea alikuwa ni yule msagaji wa kizungu aliyeishi mjini-kati. Alinitaka niwapelekee na mchumba wake bangi za dola hamsini.

Nikaona hamna shida maana nimezoea kufanya hivyo. Kasumba ilikuwa imenifanya nibanwe na usingizi mkali sana. Bafuni nilikuwa na chupa ya vidonge vya benzedrine. Nilimeza kadhaa ili kujiweka sawa. Dawa zile mbili kichwani mwangu zilifanya kichwa changu kivutane pande mbili.

Nilimgongea muuza madawa aliyeishi nyumba ya nyuma yangu. Alinipa bangi kadhaa kwa mkopo. Na baada ya kuona kuwa nimelewa alinisaidia kunyonga misokoto kama mia moja hivi. Tulivuta kadhaa tulipokuwa tukisokota.

Sasa kichwani nilikuwa na kasumba, benzedrine na bangi.

Nilipita kwa Sammy nilipokuwa naenda mjini. Mwanamke wake mlatino mweusi alinifungulia mlango. Sammy alikuwa ameanza kukolea kwa mwanamke yule, hakuwahi kukaa na mwanamke mwingine kwa muda mrefu vile lakini sasa alikuwa hata anamruhusu kujibu hodi! Wakati huo Sammy alikuwa teja hasa. Ilionekana hata hakunitambua vizuri. Akiwa bado kalala kitandani, alipeleka mkono uvunguni na kunitolea kile kioo chenye cocaine, alinipa ishara nivute kidogo. Sikukataa. Nilipokuwa naenda mjini-kati kupeleka bangi nilikuwa napata hisia ambazo siwezi kuzielezea, madawa yote yale kwa pamoja! Njia pekee ya kuelezea hisia zile n kuwa sikutambua uwepo wa muda. Siku kwangu ilionekana kama dakika tano tu na nusu saa ningeona kama juma zima.

Sipati picha nilionekanaje nilipofika hotelini. Msagaji yule na mwanamke wake waliponiona namna ile ikabidi wanisaidie kupanda kitandani. Nililala kiupandeupande na kupitiwa na usingizi mkali.

Usiku ule waliponiamsha tayari nusu siku ilikuwa imepita tokea muda wa mwisho wa kumpelekea West Indian Archie pesa zake. Nikarudi Harlem. Tayari taarifa ziliishaenea. Niliona watu niliofahamiana nao wakiniepuka. Nilijua hakuna aliyetaka kupigwa risasi kwa bahati mbaya.

Lakini hakuna kilichotokea. Hata siku iliyofuata ilikuwa hivyohivyo. Niliendelea tu kulewa madawa.

Katika siku zile kuna kijana mmoja mjeuri aliniletea za kuleta ndani ya baa. Nilimtandika ngumi ya mdomo. Alirudi akiwa ameshika kisu; kidogo nimchape risasi lakini kuna mtu aliwahi kumshika. Walimtoa nje akiwa anatukana kuwa ataniua.

Mara moja machale yakaniambia niweke mbali bastola yangu. Nilimuona mpambanaji mmoja ndani ya baa, ile natoka tu kumpa bastola yangu polisi akawa anaingia. Mkono wake alikuwa ameuweka kwenye bastola iliyokuwa kiunoni mwake. Alikuwa anajua kila kitu kuhusu taarifa zilizokuwa zikisambaa; na alikuwa ana hakika kuwa lazima nitakuwa na silaha. Alinisogelea polepole, nami nilitulia tuli—nilijua nikijitingisha tu atanilipua.

Alisema, “Red toa mkono mfukoni polepole.”

Nilitii. Sote tukashusha pumzi baada ya kuona kuwa sina kitu mkononi. Alinipa ishara niongoze kutoka nje, nilitii pia. Polisi mwenzake alikuwa anasubiri nje pembeni ya gari ya doria, walinipekua mwili mzima pale.

“Mnatafuta nini?” niliwauliza baada ya kuwa hawajapata kitu. “Kuna taarifa kuwa unatembea na bastola,” walinijibu. “Nimewahi kuwa nayo lakini niliitupa mtoni,” nilisema. Yule ambaye nilitoka naye ndani ya baa alisema, “Ningekuwa wewe ningeondoka mjini hapa.”

Nilirudi ndani ya baa. Kule kuwaambia kuwa niliitupa mtoni kulifanya wasiende nami mpaka nyumbani kwangu kunipekua. Vitu nilivyokuwa navyo nyumbani vingeweza kunifanya nifungwe mara kumi ya kifungo cha kukutwa na bastola kumi, na hata wao wangepanda vyeo.

Nilizongwa pande zote. Nilikuwa nimebanwa kila upande. West Indian Archie akiniwinda. Waitaliano waliodhani kuwa niliwapora nao wakinitafuta. Yule kijana mjeuri. Polisi.

Kwa miaka minne iliyopita nilikuwa mjanja au mwenye bahati kuweza kuepuka jela, au hata tu kukamatwa. Wala sikuingia kwenye matatizo yoyote makubwa. Lakini sasa nilifahamu kuwa dakika yoyote kuna jambo kubwa litanipata.

***

Sammy alikuwa amefanya jambo fulani ambalo siku zote nimekuwa natamani ningemshukuru sana.

Nilikuwa natembea mtaa wa St. Nicholas niliposikia mlio wa honi. Lakini masikio yangu yalichosikia ni mlio wa risasi. Sikuwazia kabisa kwamba honi hiyo ilikuwa kwa ajili yangu. “Mwanakwetu!”

Niliruka pembeni na ilikuwa karibu nitoe bastola kujibu mapigo. Alikuwa Shorty kutoka Boston. Nilikuwa nimemuogopesha sana, “Daddy-o!”

Niliingiwa na furaha sana. Tulipokuwa kwenye gari aliniambia kuwa Sammy alimpigia simu na kumueleza jinsi mambo yangu yalivyokuwa magumu na kumwambia itakuwa vyema akija kunichukua. Baada ya kupiga na bendi yake, akaazima gari ya mpiga piano wake na kuendesha hadi New York.

Sikubisha kuondoka. Shorty alibaki nje akilinda huku mimi nikikusanya vitu vichache nilivyoona vinafaa kuondoka navyo na kuvipakia garini. Ndani ya muda mfupi tukawa tupo barabarani. Shorty alikuwa hajalala kwa karibu saa thelathini na sita. Baadaye alikuja kunisimulia kuwa kwenye safari nzima nilikuwa naongea vitu visivyoeleweka.

Mwisho wa Sura ya nane
 
Good! Tunasubiri sura inayofuata

Sent from my SM-A013G using JamiiForums mobile app
 
SURA YA TISA

KUKAMATWA

Ella hakuamini kwa jinsi nilivyokuwa mhuni. Niliamini kuwa mwanaume anatakiwa kufanya kitu chochote alicho na uwezo nacho, au alicho na ujasiri wa kutosha kuweza kukifanya, na kuwa mwanamke si kitu bali bidhaa kama bidhaa zingine. Maneno yote niliyoongea yalikuwa ni ya mtaani na matusi. Nina hakika sikuwa na maneno zaidi ya mia mbili niliyoyatumia.

Hata Shorty ambaye nilienda kuishi naye tena hakuwa amejiandaa kwa jinsi nilivyoishi na kufikiri—nilikuwa kama mnyama muwindaji. Kuna nyakati nilimuona akiniangalia huku akinikadiria.

Siku za mwanzoni nililala sana—hata usiku. Kwa miaka miwili iliyopita wakati wangu hasa wa kulala ulikuwa ni mchana. Nilipokuwa macho nilikuwa nikivuta bangi mfululizo. Shorty ndiye aliyenifundisha kuvuta bangi, lakini uvutaji wangu wa sasa ulimstaajabisha sana.

Siku hizo za mwanzo sikutaka kuongea sana. Nilipiga mziki mfululizo, na bangi ilinituliza. Nilipitisha siku nikiota ndoto za mchana.

Ndani ya majuma mawili nilikuwa nimelala vya kutosha kuliko ndani ya miezi miwili yoyote nilipokuwa napambana usiku na mchana huko Harlem. Pale nilipoweza kutoka nje haikunichukua muda kumpata muuzaji wa cocaine katika mitaa ya Roxbury. Hisia za cocaine ndizo zilinifanya nipende kuongea tena.

Cocaine huwafanya wavutaji wake wajihisi vizuri mno na kuwapa kujiamini kupita kiasi-kimwili na kiakili. Inakufanya uhisi unaweza kumtandika bingwa wa masumbwi wa uzito wa juu, na kuwa una akili kuliko watu wote. Pia zile hisia za kutokwepo kwa muda nazo huja. Pia kuna wakati inakufanya unatulia na kutafakari mambo yaliyokutokea miaka ya nyuma kwa umakini wa hali ya juu.

Bendi ya Shorty ilipiga kwenye maeneo kadhaa ya Boston mara tatu hadi nne kwa juma. Shorty alipoenda kazini Sophia alifika na tulizungumza kuhusu mipango yangu. Mara nyingi aliondoka kwenda kwa mumewe kabla hata ya Shorty kurudi. Mara nyingi tulizungumza na Shorty hadi karibu na asubuhi.

Mme wa Sophia alikuwa ametoka jeshini na sasa alikuwa anafanya kazi kama afisa mauzo. Kazi hiyo ilimfanya awe anasafiri kuelekea pwani ya magharibi mara kwa mara. Nilikuwa sihoji juu ya mambo yao lakini Sophia aligusia mara kwa mara kuwa hawapo vizuri. Nilifahamu kuwa sihusiki na hilo. Mume wake hajawahi hata ota uwepo wangu. Mwanamke wa kizungu aliweza kumuwakia mume wake, akimwita kila majina mabaya aliyoyajua na kumwambia maneno ya kila aina ili kumuumiza, angeweza hata kumtukania mama na bibi yake, lakini kitu ambacho kamwe hakuweza kumwambia ni kuwa anatembea na mtu mweusi. Hilo linamtuma mwanaume wa kizungu kuua mara moja, wanawake wa kizungu walitambua hilo.

Mara zote Sophia alikuwa akinipatia pesa, hata nyakati nilipokuwa na dola mia kadhaa mfukoni. Mara nyingi alipokuja Harlem aliniachia kila kitu alichokuja nacho isipokuwa tiketi ya treni kurudi Boston tu. inaonekana kuna wanawake wanapenda kuchunwa. Wasipochunwa basi wanachuna.

Hata hivyo zilikuwa ni pesa za mumewe alizonipatia, nadhani ni kwa sababu Sophia hajawahi kuzifanyia kazi ndiyo maana hakuzibania. Lakini sasa kumtegemea kwangu kulizidi naye alinipatia zaidi. Sikufahamu alikozipata. Siku zote nilikuwa nikimchachafya hapa na pale ili kumuweka kwenye mstari. Inaonekana baada ya muda fulani wanawake huwa wanahitaji hili, au tuseme wanataka hili. Lakini kipindi hicho roho mbaya ilikuwa imenijaa na nikawa namzaba vibao kuliko kawaida, na baadhi ya usiku alikuwa akilia, huku akinitukana na kusema kuwa hatarudi tena. Lakini nilijua kuwa hakuwa hata na wazo la kutorudi.

Uwepo wa Sophia kutokana na ujio wangu ilikuwa ni moja ya mambo yaliyomfurahisha sana Shorty. Kama nilivyosema, sijawahi kuona mwanamume mweusi aliyehusudu wanawake wa kizungu kama Shorty. Toka nimemfahamu alikuwa ametembea nao kadhaa lakini hajawahi kukaa nao kwa muda mrefu maana alikuwa mwema sana kwao. Kama nilivyosema—mwanamke yeyote, mweusi au mzungu, huchoshwa haraka na jambo hilo.

Siku moja Sophia alifika na mdogo wake wa miaka kumi na saba, wakati huo Shorty alikuwa ameachana na mwanamke wake wa kizungu. Shorty na yule binti kidogo warukiane, sijawahi kuona shangwe kama ile.

Kwa Shorty hakuwa tu msichana wa kizungu, bali msichana mdogo wa kizungu. Na kwa msichana yule, Shorty hakuwa tu mwanaume mweusi bali mwanaume mweusi na mwanamuziki. Kwa muonekano alikuwa kama Sophia, Sophia ambaye bado alikuwa anafanya watu wageuze shingo. Wakati mwingine niliwachukua wasichana hao na kwenda nao kwenye sehemu ambazo Shorty na bendi yake walipiga. Watu weusi walikuwa wanaonyesha meno yote thelathini na mbili mara tu walipowaona wasichana wale wa kizungu. Waliweza kuja mezani petu na kusimama pale huku mate yakiwatoka. Shorty hakuwa tofauti nao. Alipiga muziki jukwaani huku akimuangalia msichana yule aliyekuwa akimsubiri huku akimpungia mkono na kumkonyeza. Alikuwa karibu kukanyaga watu kwa jinsi alivyokimbia kuja mezani petu mara tu baada ya kumaliza kupiga mziki.

Wakati huo nilikuwa sichezi tena lindy hop, hata wazo la kufanya hivyo sikuwa nalo, kama tu ambavyo mtu hangenikuta nimevaa suti ya zoot tena. Suti zangu zote zilikuwa ni za kawaida, na hata mfanyakazi wa benki angeweza kuvaa viatu vyangu.

Nilikutana na Laura, tulifurahi sana kukutana. Alikuwa amekuwa kama mimi tu, msichana mapepe. Tuliongea na kucheka. Alionekana mwenye umri mkubwa kuliko uhalisia. Hakuwa na mwanaume mmoja, alitembea na huyu na yule. Ni muda mrefu sana ulikuwa umepita tokea atoke kwa bibi yake. Aliniambia kuwa alimaliza shule lakini aliachana na wazo la kwenda chuo. Kila nilipokutana naye alikuwa yuko bangi—kwa mara nyingine tena; tulivuta pamoja.

***

Baada ya kukaa bure kwa kama mwezi mmoja, nikaamua kutafuta shughuli. Siku nyingine Shorty alipoenda kazini, nilichukua chochote alichonipa Sophia na kujaribu kukizalisha, nilienda kucheza kamari kwenye sehemu ya kamari iliyomilikiwa na John Hughes.

Hapo mwanzo nilipokuwa naishi Roxbury, John Hughes alikuwa mcheza kamari mkubwa ambaye hangeweza hata kuongea nami. Lakini wakati wa vita taarifa za mambo niliyokuwa nafanya huko Harlem zilifika Roxbury, sasa jina la New York nililokuwa nalo lilinipa heshima. Hivyo ndivyo wanavyohisi wapambanaji wa sehemu zote: kama uliweza kuishi New York walikuheshimu sana, na kuwa karibu nawe iliwapa heshima fulani. Basi katika miaka ile ya vita, John Hughes alikuwa ametengeneza faida ya kutosha kufungua sehemu ya kuchezea kamari.

Usiku mmoja John alikuwa akicheza kamari ambayo nami nilikuwa nikicheza. Baada ya kugawiwa karata mbilimbili nikawa nimepata dume, mara dume linguine. Lakini sikuwa na haraka. Nilitulia kuusoma mchezo. Niligonga meza kuashiria anayefuata ndiye apinge. Kitendo changu hicho kiliashiria kuwa sikuwa na karata yangu nyingine haikuwa nzuri hivyo niliogopa kupoteza pesa zangu kwa kupinga.

Mcheza kamari aliyekuwa pembeni yangu aliingia mtegoni. Alipinga pesa nyingi sana. Na waliofuata waliongezea. Pengine walitaka tu kunitisha kabla. Mwishowe zamu ilimfikia John ambaye alipinga kiasi cha juu zaidi, alikuwa na Malkia. John alikuwa mcheza kamari mahiri, kama tu wale niliocheza nao kule New York.

Mizunguko mingine ikapita na nikawa nimelamba dume la tatu! John yeye alikuwa na malkia wawili. Baada ya kuona dau linazidi kuwa kubwa baadhi ya wachezaji wakajitoa. Tukabaki mimi na John. Kama ningekuwa na pesa zaidi ningeendelea kuongeza dau hadi angejitoa. Basi mwishowe nikaonyesha ilionyesha karata zangu na kukusanya ushindi wangu, zaidi ya dola mia tano. John alimuelekeza mhudumu wake kuwa, “Wakati wowote Red akifika na kutaka kitu chochote, mpatie.” Alimwambia kuwa hajawahi kuona kijana anayecheza kama nilivyocheza.

John alikuwa na kama miaka hamsini hivi, japo si rahisi kukisia umri halisi wa mtu mweusi. Kwa yeye kuniita “Kijana” alidhani nitakuwa na miaka kama thelathini hivi, wengi walidhani hivyo. Hakuna mtu wa Roxbury aliyeweza kukisia umri wangu halisi zaidi ya dada zangu, Ella na Mary.

Kisa hicho cha kwenye kamari kilisaidia sana kunipa sifa kati ya wacheza kamari na wapambanaji wengine wa Roxbury. Kitu kingine pia kilichotokea kwenye eneo hilo la kuchezea kamari kilichangia kuniongezea sifa. Ni tukio lililowafahamisha watu kuwa sikuwa tu na tembea na bastola moja, bali bastola kadhaa.

John alikuwa na sheria kuwa yeyote anayeenda kucheza kamari kwenye eneo lake na amebeba bastola, lazima aiache bastola hiyo mapokezi. Mara nyingi niliacha mapokezi bastola mbili. Lakini siku moja mcheza kamari mmoja alipotaka kujifanya mjanja nilitoa bastola ya tatu kutoka kwenye mfuko wa bastola wa kwapani. Hili lilinifanya nijulikane kama “kichaa.”

Nikiangalia nyuma na kutafakari nafikiri kuwa ni kweli akili yangu haikuwa sawa. Niliyachukulia madawa ya kulevya jinsi ambavyo watu wengi wanakichukulia chakula. Nilitembea na bastola kama leo ninavyovaa tai kila sehemu. Moyoni mwangu niliamini kuwa baada ya mtu kuishi kama binadamu kadri awezavyo, anatakiwa kufa kifo cha kikatili. Hivyo wakati huo na hata sasa natarajia kufa muda wowote ule. Lakini tofauti ni kuwa nafikiri kipindi kile nilikuwa nakiita kifo makusudi. Nilikikaribisha kwa njia mbalimbali, wakati mwingine njia za kiwendawazimu kabisa.

Kwa mfano, baharia mmoja aliyenifahamu na kufahamu sifa zangu alikuja siku moja ndani ya baa akiwa na kifurushi. Alinipa ishara nimfuate kwenye maliwato ya wanaume. Kufungua kifurushi chake ilikuwa ni bunduki ya rasharasha—ya wizi, alikuwa anaiuza. Nilimuuliza, “Nitajuaje kuwa inafanya kazi?” Aliweka kasha la risasi na kuniambia ninachotakiwa kufanya ili kuijaribu ni kuminya sehemu ya kupigia tu. Nilichukua bunduki ile na kuikagua-kagua. Ghafla alishtukia mdomo wa bunduki upo tumboni mwake. Nilimwambia kuwa nitamfumua tumbo. Alirudi nyuma-nyuma na kutoka maliwatoni kama ambavyo Bill “Bojangles” Robinson alivyokuwa anafanya alipokuwa anacheza dansi. Alijua kuwa nilikuwa kichaa wa kuweza kumuua kweli. Nilikuwa kichaa kiasi kwamba sikuwaza kuwa atakuja kunivizia na kuniua. Nilikaa na ile bunduki nyumbani kwa Shorty kwa kama mwezi hivi. Baadaye nilipoishiwa pesa niliiuza.

Reginald alikuja kunitembelea Roxbury kunitembelea huku akiwa ameshtushwa sana na yale aliyoyakuta kule Harlem. Tulitumia siku kadhaa pamoja, alikuwa bado ni ndugu yangu wa damu niliyehisi nina ukaribu naye kuliko hata Ella. Ella bado alinipenda, nilienda kumtembelea hapa na pale, lakini hata siku moja hakuwahi kunielewa kwa jinsi nilivyobadilika. Alikuwa ameishaniambia kuwa anaona kabisa nikielekea kwenye matatizo makubwa. Lakini kwa namna fulani nilihisi Ella alikuwa anakubali sana uasi wangu, maana yeye mwenyewe alikuwa na ujasiri kuzidi wanaume wengi, na siku zote alionelea kuzaliwa mwanamke kulimkwamisha kwa namna fulani.

Kama ingekuwa najifikiria mimi tu, pengine ningefanya kucheza kamari kama kazi. Kulikuwa na vijana wacheza kamari wengi sana wasio na uzoefu walioshinda eneo la John Hughes, mcheza kamari mzuri angeweza kuendesha maisha yake kupitia hao. Alichotakiwa kufanya ni kutokosa kwenda siku wanayopokea mishahara. Na pia John Hughes mwenyewe alinipatia kazi ya kuchezesha kamari sema sikuitaka kazi hiyo.

Nilitakiwa kufikiria zaidi ya mimi mwenyewe, kufanya kitu ambacho kitamsaidia Shorty pia. Kutokana na mazungumzo yetu nilikuja kumuonea sana huruma Shorty. Ni hadithi ile ile ya wanamuziki toka zamani. Sifa kubwa ya kuwa mwanamuziki lakini kipato kiduchu sana, baada ya kulipa kodi, madeni, chakula, bangi na vitu vingine vya kawaida hakubakiwa na chochote. Angewezaje kubakiwa na chochote? Nilitumia muda mwingi pamoja na wanamuziki nilipokuwa Harlem na wakati wa kusafiri nao. Hata wale tunaoweza kusema waliotengeneza pesa nzuri kwa kiwango cha wanamuziki hawakuwa na chochote.

Hata mimi mwenyewe pamoja na kushika maelfu ya dola sikuwa na kitu. Uraibu wangu wa cocaine tu ulinigharimu dola ishirini kila siku. Nafikiri kuna dola tano nyingine ya bangi na sigara za kawaida, mbali na kutumi madawa, pia nilivuta kama boksi tano za sigara kwa siku. Na kama ukiniuliza leo, nitakuambia kuwa tumbaku ni dawa ya kulevya kama tu zingine.

Nilipogusia suala langu la kutafuta kitu cha kufanya kwa Shorty, nilianza kwa kumueleza kuwa yeye mwenyewe ni mfano halisi kuwa ni watu wenye mawazo mgando tu ndiyo wanaamini kuwa watafika popote kwa kufanya kazi ya kulipwa

Niliposema kuwa kazi ninayofikiria ni kuvamia majumbani—Shorty alikubali haraka sana. Hilo hata mimi lilinishangaza maana siku zote Shorty hakuwa mtu wa kukubali mambo kirahisi, na wala hakujua chochote kuhusu wizi wa majumbani.

Nilipomueleza jinsi kazi zinavyofanyika, akataka kumleta na rafiki yake mmoja aliyeitwa Rudy. Nilikuwa nimeishawahi kukutana na Rudy, na nilimpenda.

Rudy alizaliwa kwa baba mweusi na mama muitaliano. Alikuwa ni mzaliwa wa palepale Boston. Alikuwa mtoto wa mama hivi. Rudy alifanya kazi kwa wakala mmoja. Huko alikuwa akipata kazi kama mhudumu kwenye tafrija zenye hadhi. alikuwa na shughuli nyingine ya pembeni, shughuli iliyonikumbusha enzi zangu za kupokea wageni wa danguro kule Harlem. Mara moja kwa juma Rudy alikuwa akienda kwenye nyumba ya tajiri mmoja mkubwa na aliyeheshimika katika jamii. Tajiri huyo alikuwa akimlipa Rudy kwa kazi hii; wote walivua nguo kisha Rudy akambeba mzee yule kama mtoto na kumlaza kitandani. Hapo alimpaka poda mwili mzima, Rudy alisema kuwa mzee yule alifika mshindo kwa kufanyiwa hivyo tu.

Niliwasimulia baadhi ya mambo niliyopitia. Rudy alisema kuwa kwa uelewa wake Boston hakuna danguro linalohudumia watu maalumu, mambo hayo yalifanywa na wazungu mmoja mmoja wakihudumiwa na watu weusi waliofika majumbani mwao kama wahudumu, mamessenger, madereva au kazi zingine za watu weusi zilizozoeleka. Kama tu ilivyokuwa huko New York, watu hawa walikuwa ni matajiri na watu wa maana katika jamii. Wengi wao walikuwa ni wanaume wazee waliopita umri wa kuweza kufanya ngono kwa njia za kawaida hivyo walikuwa wakitafuta njia mpya za kujiridhisha.

Rudy alisema kuwa anamkumbuka mzungu mmoja ambaye aliwalipa wapenzi weusi ili atazame wakati wakifanya ngono kitandani pake. Mwingine aliwalipa ili asimame nje kwenye kiti, na aliridhika kwa kuwazia tu yanayoendelea huko ndani.

Nilifahamu vyema kuwa kikosi kizuri cha wizi kilihitaji “mtafutaji” huyu kazi yake ilikuwa ni kutafuta sehemu nzuri ya kuiba. Mwingine aliyehitajika ni mchora ramani. Huyu alitambua njia nzuri ya kuingilia na kutokea nk. Rudy alifaa kwa kazi zote mbili. Kwa vile alikuwa akipangiwa kazi kwenye nyumba za matajiri, haikuwa rahisi kumshuku wakati akikadiria mali zao na kuangalia ramani ya eneo, alipaswa tu kujidai akienda huku na huko akifanya shughuli zake.

Nakumbuka tulivyomueleza Rudy wazo letu alijibu kwa shauku, “Tunaanza lini?”

Lakini sikutaka kuanza haraka bila matayarisho ya kutosha. Nilijifunza kutoka kwa wakongwe wa kazi, na kutokana na uzoefu wangu mwenyewe kuwa ni muhimu kuchukua tahadhari na kupanga mipango vizuri. Wizi wa majumbani, iwapo utafanywa vizuri ulikuwa na hatari ndogo na uwezekano mkubwa wa kufanikiwa. Kama ukifanya kazi yako bila kukutana na wenye mali, unakuwa umepunguza uwezekano wa kudhuru au kuua mtu. Na hata baadaye ukikamatwa na polisi kunakuwa hakuna shahidi aliyekuona. Pia ilikuwa ni muhimu kuchagua meneo maalumu ya kuvamia na usifanye nje ya hapo. Kuna wezi waliovamia majumbani tu, wengine maduka, maghala na wengine walivamia sehemu za kuhifadhia mali za thamani.

Wizi wa majumbani nao ulikuwepo wa aina nyingi. Kuna wezi wa mchana, wa jioni, na wa usiku. Nadhani polisi yeyote anaweza kukuambia kuwa ni mara chache sana hukutana na mwizi wa saa fulani akifanya kazi saa si zake. Kwa mfano; Jumsteady wa kule Harlem alikuwa ni mwizi wa usiku kwenye majengo ya makazi. Ingekuwa ni ngumu sana kumshawishi Jumpsteady afanye kazi mchana hata kama kuna milionea ameenda kula chakula cha mchana na kuacha mlango wake wazi.

Nilikuwa na sababu ya msingi iliyonifanya nisifanye kazi mchana mbali na kutopenda tu. kwa jinsi nilivyokuwa ilikuwa ni rahisi kutambulika. Nilikuwa nawasikia watu wakisema: “Mwekundu—mweupe hivi, mrefu wa zaidi ya futi sita.” Mtu kuniona mara moja tu ilitosha kunielezea.

***
 
Safi sana

Sent from my SM-A013G using JamiiForums mobile app
 
Safi sana mkuu ,lete vitu [emoji106]
 
Sura ya tisa inaendelea

Ili kuunda genge lenye kujua kazi yake nikafikiria kuwaingiza wasichana wa kizungu. Nilikuwa na sababu mbili za kufanya hivyo. Kwanza niliona tutapaka kazi chache sana tukitegemea tu sehemu ambazo Rudy alienda kuhudumia; hakwenda sehemu nyingi hivyo haingechukua muda mrefu kabla hatujakosa sehemu ya kufanya kazi. Pia watu weusi kuonekana wakichunguza-chunguza kwenye mitaa ya wazungu kungezua mashaka mengi. Lakini wasichana hawa wa kizungu wasingepata ugumu huo. Sikupenda kikundi chetu kiwe na watu wengi, lakini tayari mdogo wa Sophia alikuwa karibu sana na Shorty, pia mimi na Sophia tulikuwa kama tumeishi pamoja kwa miaka hamsini, na kwa jinsi Rudy alivyokuwa na shauku na kazi, hakukuwa na hatari ya mtu kutoa taarifa zetu. Tulikuwa kama familia moja.

Sikuwa na shaka kuwa Sophia atakubali. Sophia alifanya kila kitu nilichomwambia. Na mdogo wake naye alifanya chochote alichoambiwa na Sophia. Wote walikubali. Kipindi nawaambia suala hilo mume wa Sophia alikuwa amesafiri kikazi huko pwani ya magharibi.

Nilifahamu kuwa wezi wengi hawakukamatwa wakati wa wizi bali wakati wa kuuza mali waliyoiba. Ilikuwa ni bahati sana kumpata mtu wa kumuuzia mali ya wizi kama yule tuliyempata. Tulikubaliana namna ya kufanya kazi. Hatukufanya kazi na mnunuzi moja kwa moja. Alikuwa na wakala ambaye alikuwa ametoka jela, wakala huyu alifanya kazi na mimi tu ndani ya genge langu. Mnunuzi wetu alikuwa na biashara zake zingine za kawaida, na pia alimiliki gereji na maghala kadhaa mjini Boston. Kazi yetu ilifanyika namna hii. Kabla ya kazi nilikutana na wakala yule na kumueleza tunachotarajia kupata naye alinieleza tutakipeleka kwenye gereji au karakana gani. Nilipopeleka mali wakala yule aliichunguza na kuondoa alama zote zinazoweza kuitambulisha. Baada ya hayo alimpigia simu mnunuzi ambaye alifika kuiangalia. Siku iliyofuata nilikutana na wakala yule sehemu tuliyokubaliana kwa ajili ya kunilipa.

Kitu kimoja ninachokumbuka ni kuwa mnunuzi huyu alilipa kwa pesa mpya tu, alikuwa mjanja sana. Jambo suala la kutembea na pesa mpya mfukoni baada ya kazi lilikuwa na athari fulani za kisaikolojia kwetu. Lakini pengine alikuwa na sababu zake nyingine.

Tulihitaji kupata sehemu ya kufanyia kazi iliyo mbali na Roxbury. Wasichana wale walikodi nyumba huko kwenye eneo la Harvard Square. Tofauti na watu weusi, wasichana wale waliweza kwenda huku na kule kuangalia sehemu nzuri ya kuiba. Nyumba yetu ilikuwa kwenye ghorofa ya chini hivyo wote tuliweza kuingia na kutoka hata usiku wa manane bila kuonekana kirahisi.

***

Kwenye kundi lolote lile lazima kuwe na bosi. Hata kama unafanya kazi peke yako lazima uwe bosi wako mwenyewe.

Kwenye kikao chetu cha kwanza tulijadiliana jinsi tutakavyofanya kazi yetu. Wasichana wale watakuwa wakipita majumbani kuchunguza kwa kujifanya wanauza vitu, wanaandikisha maoni, wanafunzi wa chuo wako kwenye utafiti nk. Wakishaingia ndani walizunguka kadri walivyoweza bila kuzua mashaka kwa wenyeji. Baada ya hapo watarudi kutoa ripoti ya vitu vya thamani walivyoona na mahali vilipo na kutuchorea ramani. Tulikubaliana kuwa wasichana wataenda kufanya wizi iwapo tu tutaona kuna faida ya wao kuhusika. Mara nyingi ni sisi watatu ndiyo tulienda kuiba, wawili wakiingia ndani na mmoja akibaki kuangalia kwenye gari, gari haikutakiwa kuzimwa.

Nikiwa naendelea kuongea nao, nilijitenga nao kidogo na kutoa bastola yangu. Nilitoa risasi zote tano na kisha nikawaonyesha ninavyoirudisha risasi moja ndani yake. Nilizungusha sehemu ya kuwekea risasi na kujielekezea bastola kichwani. “Nataka kuona mna ujasiri kiasi gani.” Niliwaambia.

Wote midomo iliwashuka. Mimi nilikenua tu meno na kubonyesha sehemu ya kupigia risasi—wote tulisikia mlio Click. “Nitaenda kujaribu tena.”

Walinibembeleza niache. Niliweza kuona machoni mwa Shorty na Rudy wakifikiria kunirukia ili kunizuia.

Mlio click ukasikika tena. Wasichana walianza kupagawa. Rudy na Shorty walinibembeleza. “Red acha! Red Acha!” Nilivuta kwa mara nyingine zaidi.

“Nafanya hivi kuwaonyesha kuwa siogopi kufa,” niliwaambia. “Kamwe usimzingue mtu ambaye haogopi kufa . . . basi na tuingie kazini.”

Tokea hapo hakuna aliyesumbua. Sophia alinistaajabia na mdogo wake aliniita “Mr. Red.” Shorty na Rudy hawakunichukulia tena kama zamani. Hakuna aliyelizungumzia tukio lile tena. Waliniogopa, waliamini siko sawa kichwani.

Usiku huo tulifanya kazi kwenye nyumba ya yule mzee aliyekuwa akimuajiri Rudy ampake poda. Ilikuwa kazi safi kabisa. Kila kitu kilienda kama kilivyopangwa. Mnunuzi alifurahi na kutupongeza sana na kutupatia noti mpya kabisa. Mzee yule alimsimulia Rudy kuwa wapelelezi walifika na kumuambia kuwa wizi ule una ishara zote za genge ambalo limekuwa likifanya kazi kwa kama mwaka mmoja ndani ya Boston.

Mara moja mambo yakawa yanaenda kama tulivyotaka. Wasichana walipita kuchunguza maeneo ya matajiri kisha tukaenda kufanya kazi, mara nyingine kazi haikuchukua hata dakika kumi. Ni mimi na Shorty hasa ndiyo tulifanya kazi. Mara nyingi Rudy alibaki kwenye gari.

Iwapo wenyeji hawakuwapo, tulitumia funguo-malaya kufungua mlango. Kwa ile yenye vitasa vya pekee tulitumia kifaa maalumu cha kufungulia. Wakati mwingine tuliingia kupitia madirishani au kwenye paa. Wanawake wazembe waliwaonyesha wasichana wetu sehemu zote za nyumba zao ili kuwastaajabisha kwa vitu vyao vya thamani. Kwa msaada wa michoro yao na tochi ndogo kama kidole tuliweza kwenda moja kwa moja mahali mali ilipo.

Wakati mwingine wenyeji walikuwamo ndani wamelala. Hilo linaweza kuonekana hatari lakini ilikuwa rahisi sana. Kitu cha kwanza kufanya iwapo mtu alikuwepo ndani ilikuwa ni kutulia tuli na kusikiliza namna wanavyopumua. Tulipenda sana wanaokoroma, ilifanya kazi iwe rahisi sana. Kwa kunyata, tulienda chumbani na kukomba saa, pochi na mikebe ya vito.

Nyakati za krisimasi zilikuwa nzuri sana kwetu; watu walikuwa na zawadi za thamani zimetapakaa kote majumbani mwao na pia wanakuwa wametoa benki kiasi kikubwa cha pesa kuliko kawaida. Nyakati nyingine tulifanya kazi mapema kuliko kawaida na hata kwenye nyumba ambazo hatujazichunguza. Iwapo mapazia yote yalikuwa yamefungwa, taa zimezimwa na hakuna aliyejibu wasichana walipopiga kengele—tulijaribu bahati yetu na kuingia.

Naweza kukupa ushauri mzuri sana iwapo unataka kuepuka wezi nyumbani mwako. Taa inayowaka ni ulinzi bora sana. Moja ya jambo zuri unaloweza kufanya ni kuacha taa ya bafuni ikiwaka usiku kucha. Bafuni ndiyo sehemu pekee mtu anaweza kuwapo wakati wowote wa usiku, na anakuwa na uwezekano mkubwa wa kusikia sauti zozote zisizo za kawaida. Mwizi kwa vile anafahamu hilo hawezi kujaribu kuingia. Na pia ni ulinzi wa gharama nafuu sana. Gharama ya umeme ni ndogo sana ukilinganisha na vitu vyako vya thamani.

Kadri siku zilivyoenda ndivyo tulivyozidi kuwa wataalamu wa kazi. Hata wakati mwingine mnunuzi wetu alituelekeza mahali tunakoweza kupata mali nzuri. Nakumbuka ni kwa njia hii, wakati fulani tulikuwa tumebobea kwenye mazulia ya mashariki, zilikuwa moja ya nyakati zetu bora kabisa. Siku zote nimehisi kuwa mnunuzi wetu mwenyewe ndiye aliyewauzia watu mazulia na kisha kutulengesha kwenda kuwaibia. Huwezi amini jinsi mazulia yale yalivyokuwa na thamani. Nakumbuka zulia moja dogo tu lakini lilituingizia dola elfu moja. Na kila mtu alifahamu kuwa mnunuzi wa vitu vya wizi alimuibia mwizi kuliko hata mwizi alivyomuibia mwenye mali.

Kosakosa yetu na vyombo vya dola ilitokea mara moja tu wakati tulipokuwa tukitoka kazini. Wote watatu tulikuwa tumepanda mbele huku nyuma tumejaza mali, ghafla tukaona gari ya polisi ikituijia, lakini ilitupita. Walikuwa tu kwenye doria. Kupitia kioo cha kungalia nyuma tukashangaa inageuza na kurudi, tukajua mara moja kuwa watakuja kutusimamisha. Bila shaka walipokuwa wanatupita watakuwa waligundua kuwa tulikuwa watu weusi, na walifahamu kuwa watu weusi hawana shughuli yeyote ya kuwafanya wawepo maeneo yale saa zile. Ilikuwa hali tete sana. Wakati huo wizi mwingi ulikuwa ukiendelea, tulifahamu vyema kuwa hatukuwa genge pekee la wizi mjini pale. Nilifahamu kuwa ni wazungu wachache sana wanaoelewa kuwa mtu mweusi anaweza kuwazidi ujanja. Kabla hawajawasha king’ora nilimwambia Rudy asimame. Nilifanya nilichowahi kufanya huko nyuma—nilishuka na kuwapungia mkono wasimame huku nikiwaendea. Huku nikongea kama mtu mweusi asiyejielewa, niliwauliza jinsi ya kufika sehemu fulani ya Roxbury. Walinielekeza na kisha tukaachana kila mtu njia yake.

Tulikuwa tunaendelea vizuri sana. Tulikuwa tunatengeneza pesa ya kutosha na kiha tunatulia kwa muda, tukitumia. Shorty bado aliendelea kupiga na bendi yake na Rudy hakuacha kwenda kumhudumia yule mzee au kwenye kazi yake ya uhudumu kwenye tafrija za. Wasichana nao waliendelea na maisha yao kama kawaida.

Mara moja moja niliendelea kutoka na wasichana wale kwenda sehemu ilipopiga bendi ya Shorty au sehemu nyinginezo, tukitumbua pesa kama vile zitaisha muda wake wa matumizi. Wasichana wale walijipamba kwa vito na makoti ya manyoya waliyochagua kutoka kwenye mali tulizoiba. Hakuna aliyejua kazi tuliyofanya lakini waliona tu mambo yetu yakiwa mazuri. Nyakati nyingine tulikutana na wakina Sophia nyumbani kwa Shorty huko Roxbury, au kwenye nyumba tuliyopanga maeneo ya Harvard Square, tukavuta bangi na kusikiliza muziki. Ni aibu kumsema mwanaume mwenzako, lakini Shorty alikuwa anashoboka sana na yule binti wa kizungu kiasi kwamba ikitokea umeme umezima basi alifungua mapazia ili aendelee kumuona kupitia mwanga wa taa za barabarani.

***

Jioni ambazo hatukuwa na kazi nilikuwa nikienda kwenye club moja iliyoitwa Savoy iliyokuwa kwenye barabara ya Massachusetts, na Sophia alinipigia simu huko bila kukosa. Hata tulipofanya kazi nilikuwa natokea kwenye club hii na kisha kurudi tena haraka baada ya kazi. Lengo lilikuwa ni hata likitokea tatizo watu watanishuhudia kuwa nilikuwepo pale saa ambazo wizi ulitokea. Haikuwa rahisi kwa watu weusi kutaja muda hususa wakati wa kuhojiwa na polisi.

Wakati huo Boston kulikuwa na wapelelezi weusi wawili tu. Tokea nimerudi Roxbury, mmoja wa wapelelezi hao aliyeitwa Turner alikuwa amenichukia sana, nami sikumpenda vilevile. Aliongea jinsi ambavyo angenifanya nami nilihakikisha majibu yanamfikia mara moja. Na kwa jinsi alivyokuwa nilijua mara moja yamemfikia. Kila mtu alifahamu kuwa natembea na bastola. Naye alikuwa na akili za kutosha kuelewa kuwa sitasita kuzitumia kwake, hata kama ni mpelelezi.

Basi jioni hii nilikuwa nipo Savoy na simu iliita kama kawaida. Iliita wakati ambao naye Turner ndiyo alikuwa akiingia. Aliniona nikijiandaa kuinuka hivyo akajua itakuwa simu yangu, aliingia ndani ya kibanda cha simu na kupokea.

Huku akiniangalia, nilimsikia akisema, “Hello, hello, hello-” Mara moja nikatambua kuwa Sophia atakuwa amekata baada ya kusikia sauti ngeni.

“Siyo simu yangu hiyo?” nilimuuliza Turner. Alijibu ndiyo nami nikamuuliza. “Sasa kwa nini hukusema?”

Alinijibu kijeuri. Nilifahamu kuwa alikuwa anataka nimuanze. Sote tulifahamu kuwa kila mtu alitaka kumuua mwenzake. Turner hakutaka kuongea chochote kitakachomfanya aonekane mbaya. Nami sikutaka kuongea chochote kitakachofanya nionekane namtisha polisi.

Pamoja na hilo nakumbuka vyema nilichomwambia, tena kwa sauti ili kila aliyekuwepo ndani ya baa asikie. “Najua Turner unajaribu kutengeneza historia. Unafahamu kuwa ukicheza na mimi utaandikwa kweli kwenye historia, maana utalazimika kuniua?”

Turner alinitazama kwa mshangao na kunywea. Kisha akanipita. Nahisi hakuwa tayari kutengeneza historia.

Nilifika hatua ambayo nilikuwa kama natembea ndani ya jeneza.

Ni sheria ya uhalifu kuwa kila mhalifu anatarajia kuja kukamatwa. Anachojaribu kufanya ni kuhairisha tu hilo kwa muda mrefu awezavyo. Madawa yalinisaidia kupotezea wazo hilo. Sasa madawa yalikuwa ni sehemu kuu ya maisha yangu. Nilifika hatua ambayo kila siku nilitumia cocaine, na bangi, au vyote kwa kiasi cha kutosha kuweza kuondoa mashaka yote niliyokuwa nayo. Iwapo mashaka kidogo tu yalifanikiwa kuniingia, niliyasukumia mbali kwa madawa hadi kesho yake, na kesho yake tena.

Lakini wakati zamani niliweza kuvuta bangi na kunusa cocaine bila kujulikana kuwa nimetumia, nyakati hizi nilionekana waziwazi.

Juma moja ya mapumziko nilipokuwa nikilewa tu madawa baada ya kufanya kazi ya pesa nyingi—nilitoka kwenda club za usiku. Niliingia kwenye club moja na kusikia sauti ya mhudumu mmoja ikiita, “Hello Red.” Kutokana na sura ya mhudumu yule nilitambua mara moja kutakuwa na tatizo. Lakini sikumuuliza kitu—nilikuwa na kanuni moja ya kutomuuliza mtu kitu chochote kukiwa na hali kama ile; wenyewe watakwambia wanachotaka usikie. Lakini hata kama alikuwa na nia ya kunieleza, mhudumu yule hakupata nafasi. Nilipoketi tu na kuagiza kinywaji niliwaona.

Sophia na mdogo wake walikuwa wamekaa mezani na mwanaume wa kizungu.

Sijui ilikuwaje nilifanya kosa nililofanya. Ningeweza kusubiri na kuongea naye baadaye. Sikumjua wala sikujali mzungu yule ni nani, cocaine zilinituma kusimama.

Hakuwa mume wa Sophia. Alikuwa ni rafiki wa karibu wa mumewe, walitumikia pamoja jeshini. Mume wake alikuwa amesafiri hivyo alikuwa ameomba awatoe Sophia na mdogo wake kwa chakula cha usiku. Lakini baada ya chakula akawa amependekeza waende maeneo ya watu weusi. Kila mtu mweusi ameona wazungu wa namna hiyo mara elfu kadhaa, wazungu wa kutaka kwenda kuona makazi ya watu weusi na kustaajabia wanavyoishi.

Wasichana wale kwa kuwa walifahamika vyema maeneo ya watu weusi walijaribu kupinga lakini alisisitiza. Basi walijikaza na kuja kwenye hii club ambayo wameingia mara mia na kidogo. Waliingia na kuwakazia macho wahudumu na watu wa kaunta nao walielewa ujumbe wao na kujidai hawawafahamu.

Basi walikaa mezani pale wakiomba asitokee mtu mweusi anayewafahamu na kwenda kwenye meza yao. Ghafla nimetokea. Niliwaita “Baby” nyuso ziliwapauka, na bwana yule uso wake ukawa mwekundu.

Usiku ule niliporudi Harvard Square nilikuwa hoi kwa kuumwa. Haukuwa ugonjwa bali hasa yalikuwa malipo ya maisha yangu niliyoishi miaka mitano iliyopita. Nilikuwa nimevaa nguo za kulalia, usingizi ukinichukua kwa mbali niliposikia mtu akigonga mlangoni.

Mara moja nilijua kutakuwa na tatizo. kila mtu alikuwa na funguo ya pale, hakuna aliyekuwa anagonga mlango. Nilitoka kitandani na kuingia uvunguni. Nilikuwa nimelewa kiasi kwamba sikuwa kabisa na wazo la kuchukua bastola iliyokuwa mezani.

Nikiwa uvunguni nikasikia funguo ikiingizwa mlangoni. Kisha nikaona viatu vikiingia. Niliviangalia vikitembea tembea mle ndani kisha vikasimama. Kila viliposimama nilijua mtu huyo alichokuwa akiangalia. Na nilijua kuwa lazima atachungulia uvunguni kabla hata hajafanya hivyo. Alifanya hivyo. Alikuwa rafiki wa mume wa Sophia. Uso wake ulikuwa kama futi mbili tu kutoka uso wangu. Ulionekana kumkakamaa.

“Ha ha ha nimekupata siyo?” Nilisema. Hata haikuchekesha. Nilitoka uvunguni huku bado najichekesha. Hakukimbia, nimsifu kwa hilo. Alirudi nyuma na kuniangalia kama vile nilikuwa nyoka.

Sikujaribu kuficha kitu ambacho tayari alikifahamu. Baadhi ya vitu vya Sophia na mdogo wake vilikuwa vimetapakaa mle ndani; aliviona vyote. Na hata tuliongea kidogo. Nilimwambia kuwa wasichana hawakuwepo naye akaondoka. Kilichonishangaza hata mimi ni jinsi nilivyojibana uvunguni bila ya bastola. Hakika nilianza kutojielewa.

***
 
Sura ya tisa inaendelea.

Kuna saa moja ya wizi nilikuwa nimeipeleka kwa fundi kutengeneza. Ilikuwa ni siku mbili baadaye nilipoenda kuichukua ndipo mambo yalipoharibika. Kama nilivyosema, nilitembea na bastola kama ambavyo leo huwezi nikuta bila tai. Nilikuwa na bastola yangu kwenye mfuko wa kwapani bega.

Baadaye nilikuja kufahamu kuwa mtu tuliyemuibia saa ile alikuwa amewaeleza polisi matengenezo iliyohitaji. Ilikuwa saa ya gharama sana ndiyo maana nikaamua kuitumia mwenyewe. Basi watu wote waliohusika na saa na mapambo jijini Boston walijulishwa kuibiwa kwake.

Myahudi yule alisubiri hadi nilipolipa ndipo akaweka saa mezani. Kisha akatoa ishara na mtu fulani akatokea nyuma na kunifuata. Mkono mmoja alikuwa ameuweka mfukoni. Nilitambua kuwa alikuwa ni polisi, “Sogea huku nyuma.”

Nilipoanza tu kwenda, akaingi mtu mweusi ndani mle. Nakumbuka baadaye kusikia kuwa alikuwa ametoka jeshini siku ileile. Mara moja polisi yule alimkabili akidhania yuko pamoja nami.

Nilikuwa nimesima, bastola kwapani na mpelelezi yule akiongea na yule mtu huku kanipa mgongo. Hata leo naamini kuwa Allah alikuwa pamoja nami siku ile. Sikujaribu kumpiga risasi, na hilo ndilo liliokoa maisha yangu.

Nakumbuka jina lake aliitwa Slack. Niliinua mikono juu na kumwambia, “Bastola yangu hii.”

Niliona uso wake ukimbadilika alivyokuwa akiichukua. Kwa sababu ya mtu mweusi mwingine kuingia ghafla akawa hajawaza kabisa kuwa naweza kuwa na bastola. Iliguswa sana na kitendo changu cha kutojaribu kumuua.

Basi baada ya kuchukua bastola yangu alitoa ishara na polisi wengine wawili walitoka mafichoni. Walikuwa wananichunguza. Ningejaribu tu kufanya chochote ningekufa. Nilikuwa naenda kupata muda mrefu sana wa kutafakari kuhusu jambo lile huko gerezani.

Kama nisingekamatwa wakati ule basi ningekuja kufa. Rafiki wa mume wa Sophia alikuwa amemsimulia mume wake kuhusu mimi. Mara tu mume wake alipofika alielekea kule tulikopanga akinitafuta na bastola mkononi. Kule yeye anafika kunitafuta, mimi huku napelekwa kituoni.

Polisi walinihoji vikali sana. Lakini hawakunipiga wala kunigusa. Nilifahamu ni kwa sababu sikujaribu kumuua mwenzao.

Walifahamu nilikoishi kwa kuangalia baadhi ya karatasi nilizokuwa nazo. Haikuchukua muda wakawa wameenda kuwakamata wasichana wetu. Shorty alikamatwa akiwa anaimba jukwaani usiku ule ule. Wasichana walikuwa pia wamemtaja Rudy. Hadi leo sielewi Rudy alipataje taarifa, nilifahamu kuwa atakuwa alidandia chochote kilichokuwa kinatoka Boston. Mpaka leo hawajawahi kumkamata.

Siku zote nimekuwa nikitafakari siku ile niliwezaje kuepuka kifo mara mbili ndani ya siku moja. Hiyo ndiyo sababu naamini kila jambo limeandikwa.

Polisi walikuta makazi yetu yamejaa ushahidi-makoti ya manyoya, vito, vitu vingine vidogovidogo na zana zetu za kazi kama zana za kukatia vioo, za kufungulia vitasa, tochi ndogo na ghala ndogo ya silaha. Wasichana walipata dhamana ya pesa ndogo. Walikuwa bado ni wazungu hata kama ni wezi. Uhalifu wao mkubwa ulikuwa ni kujihusisha na watu weusi. Mimi na Shorty tulipaswa kuweka dola elfu kumi kila mmoja kama dhamana, kiasi ambacho walifahamu hatuwezi kuwa nacho.

Watu wa ustawi wa jamii nao walituhoji. Walikazia zaidi suala la wanawake wa kizungu kujihusisha na watu weusi. Wasichana wale hawakuwa unaoweza kuwaita “Mapepe” walikuwa ni wasichana kutoka familia nzuri za daraja la kati la juu. Hilo ndilo lililowahangaisha zaidi watu wa ustawi wa jamii na polisi kuliko hata kesi yenyewe.

Tulikutanaje? Wapi? Lini? Tumelala pamoja? Kiufupi hakuna aliyetaka hasa kujua habari ya wizi tuliofanya. Kitu pekee walichoona ni kuwa nilikuwa nimechukua mwanamke wa mzungu.

Niliwaangalia tu watu wa ustawi wa jamii na kuwaambia, “Nyinyi mnafikiriaje?”

Hata karani na polisi wa mahakama nao walisema “Wasichana safi wa kizungu . . . niggers wenye laana-“ Ilikuwa hivyo hata kwa wanasheria tuliopewa na mahakama. Kabla ya hakimu kuingia nilimwambia mwanasheria wetu, “Inaonekana tunahukumiwa kwa sababu ya wasichana wale.” Aligeuka rangi na kuwa mwekundu, kisha akasema: “Wasichana wa kizungu hawakuhusu kabisa!”

Baadaye nilipokuja kujua ukweli wote juu wa mzungu, nilitafakarai sana juu ya hukumu yetu. Kwa kawaida hukumu ya mwizi wa mara ya kwanza kama tulivyokuwa sisi huwa ni miaka miwili—lakini hatukuwa tunaenda kupata hukumu ya kawaida, si kwa ule uhalifu tulioufanya.

***

Kabla ya kuendelea naomba kusema kuwa sijawahi msimulia mtu yeyote juu ya maisha yangu kwa kina. Na hata sasa sisimulii ili kuonyesha kuwa najivuna jinsi nilivyokuwa muovu na mtu mbaya.

Watu wengi wamekuwa wanajiuliza imekuwaje nipo jinsi nilivyo. Kutambua hilo kwa mtu yeyote, unatakiwa kuangalia maisha yake tokea anazaliwa. Mambo yote tuliyopitia ndiyo yanafanya tuwe jinsi tulivyo. Kila jambo lililotokea maishani mwetu linachangia.

Leo hii, wakati ambao kila jambo ninalofanya linahitaji uharaka nisingeweza kupoteza hata saa moja kuandaa kitabu ambacho lengo lake kuu ni kushawishi watu kwenye upotovu. Lakini napoteza saa nyingi kwa sababu naamini kusimulia mambo yote ndiyo njia pekee ya kueleweka, kueleweka jinsi ambavyo nilikuwa nimezama chini kabisa ya jamii ya Marekani iliyotengenezwa na mzungu—na jinsi nilivyokuja kumjua Allah na dini ya Kiislamu nikiwa gerezani, na maisha yangu kubadilika kabisa.

Mwisho wa sura ya tisa
 
SURA YA KUMI

SHETANI

Mama yake Shorty alifanikiwa kujichanga na kupata nauli ya basi kutoka Lansing hadi Boston. “Mwanangu naomba unisomee kitabu cha ufunuo na usali!” ndivyo alivyokuwa akimwambia Shorty kila alipomtembelea mahabusu. Kuna siku alinitembelea nami pia. Shorty alisoma kitabu hicho na hata alipiga magoti na kusali kama vile shemasi mweusi wa kibapstisti.

Siku ya hukumu tulikuwa mbele ya hakimu kwenye mahakama ya wilaya ya Middlesex(Nadhani kumi na nne ya makosa yetu yalifanyika kwenye wilaya hiyo) Mama yake Shorty alikuwa amekaa kichwa ameinamisha huku akilia na kusali kwa Yesu, pembeni yake alikuwepo Ella na Reginald. Shorty ndiye alikuwa wa kwanza kuitwa. Shorty hakufahamu maneno, “Kutumikiwa kwa pamoja,” yanamaanisha nini.

“Kosa la kwanza, miaka nane hadi kumi, kosa la pili, miaka nane hadi kumi, kosa la tatu, miaka nane hadi kumi . . . ” Na mwishowe, “Adhabu zote zitatumikiwa kwa pamoja.”

Jasho lilimvuja Shorty kiasi kwamba uso wake mweusi ulikuwa kama umepakwa mafuta mengi, na kwa vile hakujua “Kutumikiwa kwa pamoja,” kunamaanisha nini, atakuwa alipiga hesabu kichwani mwake na kuona kuwa atafungwa kwa zaidi ya miaka mia moja. Alianza kulia na kuishiwa nguvu, ilimbidi askari wa mahakamani amshikilie.

Ndani ya sekunde kumi Shorty akawa amegeuka kuwa asiyeamini Mungu kama tu nilivyokuwa.

Nilipata kifungo cha miaka kumi. Wasichana wetu walipata kifungo cha mwaka mmoja hadi mitano kwenye gereza la wanawake huko Framingham, Massachusetts.

Hii ilikuwa ni mwaka 1946, hata miaka ishirini na moja nilikuwa bado sijatimiza. Hata kunyoa ndevu nilikuwa bado sijaanza.

Tulichukuliwa na Shorty, tukapigwa pingu na kupelekwa gereza la Charlestown.

Sikumbuki namba yangu yoyote ya mfungwa. Hilo linanishangaza sababu namba yako ya gerezani inakuwa sehemu yako kubwa sana. Hutasikia ukiitwa kwa jina lako bali namba tu. Namba yako ilikuwa kila sehemu. Kwenye nguo zako, vyombo na kila kitu. Inakuwa ni kama imeandikwa kichwani mwako.

Mtu yeyote anayedai kupenda sana binadamu wenzake, anatakiwa kufikiri kwa kina sana kabla hajachagua kuunga mkono kitendo cha kufunga binadamu wengine nyuma ya nondo. Sisemi magereza yasiwepo, ninasema nondo ndizo zisiwepo. Mtu hawezi kubadilika tabia nyuma ya nondo. Kamwe hawezi kusahau nondo zile.Bbaada ya kutoka hujitahidi kufuta yaliyomtokea lakini hawezi kabisa. Nimeongea na wafungwa wa zamani wengi sana. Cha kushangaza ni kuwa karibu wote akili zetu zimesahau mambo mengi yaliyotokea katika miaka mingi tuliyokuwa gerezani. Lakini kila mmoja atakwambia kuwa kamwe huwezi kusahau zile nondo.

Nikiwa kama “samaki”(Jina la mfungwa mpya kwenye gereza la Charlestown.), nilikuwa na hali mbaya kimwili na mwenye hasira kama nyoka sababu ya kukosa madawa ghafla. Selo hazikuwa na maji. Jela ilikuwa imejengwa mwaka 1805-nyakati za Napoleon na hata mtindo wake ulikuwa kama wa gereza la Bastille. Ndani ya selo chafu na ndogo. Niliweza kulala kitandani na miguu na kichwa vikagusa kuta. Choo kilikuwa ni ndoo yenye mfuniko. Haijalishi una moyo wa namna gani lakini huwezi kuvumilia harufu ya kinyesi kutoka safu ya selo kadhaa.

Mwanasaikolojia w gereza alinisaili na aliishia kutukanwa matusi yote mabaya niliyoyajua, na kasisi wa gereza alitukanwa matusi mabaya zaidi. Nakumbuka barua ya kwanza kupokea ilikuwa ni kutoka Detroit kwa kaka yangu mshika dini, Philbert. Akiniambia kuwa kanisa lao “Tukufu” litaniombea. Nilimtumia barua ya majibu ambayo hata leo naona aibu ninapoifikiria.

Ella alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuja kunitembelea. Nakumbuka jinsi alivyojikaza kutabasamu, sasa nikiwa nimevaa dungaree iliyopauka, namba yangu ikiwa imebandikwa juu yake. Hakuna aliyeweza kupata maneno mengi ya kuzungumza, kulikuwa na ukimya hadi nikatamani asingekuja kabisa. Askari wenye bunduki walikuwepo pale kusimamia karibu wafungwa na wageni hamsini. Nilisikia wafungwa kadhaa wapya wakiapa kuwa siku watakayofunguliwa kitu cha kwanza kufanya itakuwa ni kushughulika na wale askari wa kwenye chumba cha kukutana na wageni. Mara nyingi chuki iliwaangukia hao.

Mara ya kwanza kulewa pale gerezani ilikuwa kwa kutumia kungumanga. Mtu niliyekaa naye selo moja alikuwa mmoja wa watu wengi waliokuwa wakinunua kungumanga za wizi kutoka kwa wafungwa waliofanya kazi jikoni. Walinunua kwa kutumia pesa au sigara. Madawa hayo waliyaficha kwenye viboksi vya viberiti. Nilifakamia kiboksi kile kama vile ndani yake kulikuwa na madawa halisi. Ukichukua kiasi hicho cha kungumanga na kukikoroga na maji ya baridi kwenye kikombe na kunywa, unakuwa kama mtu aliyevuta misokoto mitatu au minne ya bangi.

Hatimaye kwa kutumia pesa alizonitumia Ella niliweza kununua madawa halisi kutoka kwa askari. Niliweza kununua bangi, Nembutal na Benzedrine. Kuwauzia wafungwa magendo ilikuwa ndiyo kazi nyingine ya askari. Kila mfungwa alifahamu kuwa askari jela waliendesha maisha yao hasa kwa njia hiyo.

Nilikaa gerezani kwa muda wa miaka saba. Lakini ule mwaka mmoja na kidogo niliokaa gereza la Charlestown ulijaa matumizi ya kungumanga, madawa mengine, kuwatukana askari, kutupa vitu nje ya selo yangu, kuangusha sinia langu la chakula kwenye ukumbi wa chakula, kugoma kujibu namba yangu ilipoitwa na kusema kuwa nimeisahau na vurugu zingine kama hizo.

Nilipenda kifungo cha kutengwa nilichopewa baada ya kufanya mambo hayo. Lakini kulikuwa na ukomo wa muda ambao mtu anaweza kuwekwa kwenye kifungo cha peke yake. Nilikuwa nikitembea chumbani huku na huko kama chui aliyefungwa bandani, nikijilaani vikali kwa sauti. Pia nilipenda kumlaani Mungu na Biblia. Baadaye watu wakanipachika jina la “Shetani” kutokana na kupinga kwangu dini huko.

Mtu wa kwanza aliyenivutia gerezani alikuwa ni mfungwa aliyeitwa “Bimbi” Nilikutana naye mnamo mwaka 1947 katika gereza la Charlestown. Alikuwa ana weupe kama mimi na hata urefu tulilingana, alikuwa na madoamadoa usoni. Bimbi alikuwa ni mwizi mzoefu na alikuwa ameishafungwa mara nyingi. Kundi letu lilikuwa linafanya kazi kwenye karakana ya kutengeneza vibao vya namba za magari. Kazi ya Bimbi ilikuwa ni kuendesha mashine ya kubandika namba. Mimi nilikuwa sehemu ambayo namba zilipakwa rangi.

Bimbi alikuwa ndiye mtu mweusi wa kwanza ambaye hakujibu alipoongeleshwa kwa lugha ya kihuni. Mara nyingi baada ya kumaliza kutengeneza idadi ya vibao tuliyopangiwa kwa siku, tulikusanyika pamoja kama kumi na au kumi na tano tukimsikiliza Bimbi. Kawaida wafungwa wa kizungu hawakuwaza hata kusikiliza mawazo ya wafungwa weusi, lakini kwa Bimbi ilikuwa tofauti, hata askari walisogea kusikiliza aliyoongea Bimbi.

Alifanya watu wavutiwe hata na mada za ajabu ambazo hukuwahi kuziwazia. Alituthibitishia kwa kutumia sayansi ya tabia ya binadamu kuwa tofauti pekee kati yetu na watu waliokuwa nje ni kuwa sisi tulikuwa tumekamatwa. Alipenda sana kuongelea watu na matukio ya kihistoria. Sikuwa mfungwa pekee ambaye alikuwa hajawahi kumsikia Thoreau mpaka pale Bimbi alipomuelezea. Bimbi alijulikana kama mhudhuriaji mzuri wa maktaba. Kilichonistaajabisha zaidi ni kuwa alikuwa mtu wa kwanza kumfahamu aliyefanya aheshimike kwa kuongea tu.

Ni mara chache sana Bimbi alizungumza name, hakuwa anazungumza sana na mtu mmoja mmoja, lakini nilihisi kuwa alinipenda. Kilichofanya nitake urafiki naye ni jinsi alivyoizungumzia dini. Nilijichukulia zaidi ya mtu asiyeamini Mungu, nilijiona Shetani kabisa. Lakini Bimbi aliielezea falsafa ya kutoamini Mungu kwa namna iliyonifanya niache kutukana dini. Alikuwa na hoja zenye nguvu kuliko mimi, na wala hakutumia matusi.

Siku moja bila kutarajia, Bimbi aliniambia bila kuuma maneno kuwa kama nilikuwa na kichwa kizuri sana kama ningekitumia. Nilitaka hasa kuwa rafiki yake na si ushauri wa aina ile. Nilikuwa nikitukana wafungwa wengine lakini hakuna mtu aliyethubutu kumtukana Bimbi. Aliniambia kuwa itanifaa nikijiunga na kozi zilizotolewa gerezani na kuhudhuria maktaba.

Mara yangu ya mwisho kufikiria kusoma kitu chochote kisichohusiana na upambanaji ilikuwa nilipomaliza darasa la nane kule Mason, Michigan. Na zaidi ni kuwa mitaa ilikuwa imefuta kila kitu nilichojifunza shuleni; sikuweza kutofauti kutofautisha kati ya kitenzi na nyumba! Dada yangu Hilda alikuwa amependekeza kuwa iwapo ninaweza basi nijifunze kiingereza na namna ya kuandika. Nilikuwa nimemtumia barua kipindi kile nauza bangi kwa kusafiri. Ilimpa tabu sana kusoma.

Basi kwa kuona kuwa nina muda mwingi, nikaanza kozi ya kiingereza. Orodha ya vitabu vilivyopatikana maktaba ilipopita niliagiza kitabu kwa kuweka namba yangu kwa nilichokipenda kati ya vile ambavyo havikuchaguliwa. Kupitia kozi ya kiingereza na mazoezi, uelewa wangu wa lugha ukaanza kurudi polepole. Ndani ya mwaka mmoja nikawa na uwezo wa kuandika barua nzuri inayoeleweka. Wakati huo huo, baada ya kumsikia Bimbi akielezea mnyumbulisho wa maneno, nikajiunga na kozi ya kilatini kimyakimya.

Pia kwa uongozi wa Bimbi, nilifanikiwa nikawa nimejifunza mbinu mbalimbali za kuishi gerezani. Mara zote nilikuwa na katoni kadhaa za sigara ndani ya selo yangu; sigara gerezani zilikuwa na thamani kama zilivyo pesa mtaani. Nilichezesha kamari za pesa na sigara wakati wa ndondi na mpira. Sijikusahau hali ilivyokuwa siku ile ya mwezi wanne wa mwaka 1947, siku ambayo Jackie Robinson alipoletwa kuchezea Brookyln Dodgers. Nilikuwa shabiki mkubwa wa Jackie Robinson, sikio langu halikubanduka redioni alipocheza. Hakuna mchezo uliomalizika bila ya mimi kung’amua takwimu zake katika mchezo huo.

***

Siku moja mnamo mwaka 1948, nilipokuwa nimehamishiwa kwenye gereza la Concord, nilipokea barua kutoka kwa kaka yangu Philbert ambaye kila siku alikuwa anajiunga kwenye kitu fulani. Aliniambia kuwa alikuwa amegundua dini ya “asili” ya mtu mweusi. Alisema sasa alikuwa mshirika wa kitu kinaitwa Taifa la Kiislamu(National of Islam), aliniambia kwamba ninapaswa kusali kwa Allah ili kupata wokovu. Nilimjibu Philbert, japo kiingereza changu kilikuwa kizuri lakini ilikuwa barua mbaya kuliko ile ya kwanza niliyomjibu baada ya kuniambia kuwa alikuwa ananiombea kwenye kanisa lake “Takatifu.”

Nilipopokea barua ya Reginald, sikutegemea kabisa ifanane na ya Philbert, japo nilifahamu kuwa alitumia muda mwingi pamoja na Hilda, Wilfred na Philbert huko Detroit. Ilikuwa barua ya kunipasha habari mbalimbali, pia ilikuwa na haya maelekezo: “Malcom usile tena nyama ya nguruwe wala usivute tena sigara. Nitakuonyesha namna ya kutoka gerezani.”

Mawazo yaliyonijia ni kuwa amegundua namna ambayo ninaweza kuilaghai idara ya magereza. Nililala na kuamka huku nikiwa na mawazo itakuwa ni jambo gani hilo. Labda tendo fulani la kisaikolojia kama nilivyowafanyia kule New York ili kuepuka kuandikishwa jeshini! Je nikiepuka kula nyama ya nguruwe na kuvuta sigara ninaweza kuwaaminish kuwa nina matatizo na hivyo kuniachia huru?

“Kutoka gerezani.” Maneno hayo yaliniganda kichwani. Nilitamani sana kuwa huru.

Nilitamani kuongea na Bimbi kuhusu suala hili lakini machale yakaniambia nisimwambie mtu.

Kuacha sigara halikuwa jambo gumu. Nilizoea kuishi bila kuvuta nilipokuwa kwenye kifungo cha peke yangu. Vyovyote ilivyo lakini sitaiacha nafasi hii ipite. Nilisoma ile barua na kisha nikamalizia paketi ya sigara niliyokuwa nimeisha ifungua. Tokea siku hiyo ya mwaka 1948, sijavuta tena sigara.

Siku kama tatu au nne mbele, nyama ya nguruwe iliandaliwa wakati wa chakula cha mchana.

Wakati nakaa kwenye meza ya chakula mawazo yangu hayakuwepo kabisa kwenye nyama ya nguruwe. Ghafla maneno usile tena nguruwe yakapita mbele yangu.

Sinia lilipopita nilisita kidogo kisha nikampasia mfungwa aliyefuata. Mara moja alianza kujipakulia. Kisha ghafla akasimama na kugeuka kuniangalia kwa mshangao.

Nilimwambia, “sili nguruwe.”

Basi sinia liliendelea mbele. Inafurahisha sana jinsi taarifa zinavyosambaa gerezani. Gerezani ambapo hakuna mambo mengi ya kufanya, jambo dogo huzua taharuki kubwa sana. Kufikia usiku jengo letu lote lilikuwa limefahamu kuwa Shetani hali nguruwe.

Kwa namna fulani jambo hilo lilinifanya nijivune sana. Picha waliyonayo watu wengi nje na ndani ya magereza ni kuwa mtu mweusi hawezi kuishi bila kula nguruwe. Ilinifanya nijihisi vizuri kuona kuwa kutoila kwangu kuliwashtua watu, hasa wafungwa wa kizungu.

Baadaye nilipokuja kuusoma na kuuelewa Uislamu, nilifahamu kuwa nilikuwa nimetimiza takwa langu la kwanza la Kiislamu bila kujua wala kuwa muislamu kamili. Kwa mara ya kwanza nilikuwa nimejionea mafundisho ya Kiislamu, “Kama ukichukua hatua moja kumuelekea Allah-Allah atachukua hatua mbili kukuelekea.”

Kaka na dada zangu huko Detroit na Chicago walikuwa wamebadili dini na kujiunga na ile waliyofundishwa kuwa ndiyo “dini ya asili ya mtu mweusi” ambayo Philbert alikuwa ameniandikia kunieleza. Wote walikuwa wakisali ili na mimi nibadili nikiwa bado gerezani. Mwishowe wakaamua kuwa Reginald, mtu wa mwisho kujiunga na ambaye yupo karibu sana nami ndiye atafaa zaidi kuongea nami maana alifahamu vyema maisha yangu.

Mbali na haya, dada yangu Ella naye alikuwa akipambana ili nihamishiwe kwenye gereza la mafunzo lililokuwa kama makazi ya kawaida huko Norfolk, Massachusetts. Hili lilikuwa gereza la majaribio. Wafungwa kwenye magereza mengi walizungumza kuwa iwapo una pesa na una watu wa kukusaidia unaweza hamishiwa kwenye gereza hilo ambalo maisha yake yalisemwa kuwa ni mazuri kiasi ambacho haikuwa rahisi mtu kuamini kuwa yupo gerezani. Ella akawa amefanikiwa na mwishoni mwa mwaka 1948 nikahamishiwa Norfolk.

Ukilinganisha na nilikotoka, mahali pale palikuwa kama mbinguni. Kulikuwa na vyoo vya kisasa, hakukuwa na nondo bali kuta tu. Na ndani yake mtu alikuwa na uhuru mwingi zaidi. Na kwa vile hapakuwa mjini, kulikuwa na hewa safi sana.

Kulikuwa na nyumba ishirini na nne na ndani ya kila nyumba waliishi watu hamsini. Hivyo kulikuwa na jumla ya wafungwa 1,200. Kila nyumba ilikuwa ni ya ghorofa tatu na jambo zuri kuliko yote ni kuwa kila mfungwa alikuwa na chumba chake.

Karibu asilimia kumi na tano ya wafungwa walikuwa ni weusi ambao waligawanywa, kila nyumba ilikuwa na kama wafungwa weusi tisa.

Gereza-makazi la Norfolk lilikuwa ni mtindo wa kisasa kabisa wa gereza. Mahali pa chuki, kuchongeana na askari waliojaa chuki kulikuwa na ustaarabu-ustaarabu wa gerezani. Asilimia kubwa ya wafungwa wa Norfolk walishiriki kwenye mambo ya “kisomi” masuala kama majadiliano na kubishana kwa hoja. Wakufunzi wa mambo ya kielimu walitoka vyuo vikuu vya Harvard, Boston na taasisi zingine za kielimu zilizokuwa karibu. Sheria za kutembelea wafungwa zililegezwa sana ukilinganisha na magereza mengine. Watu waliweza kutembelea karibu kila siku, na waliruhusiwa kukaa hadi kwa saa mbili. Uliweza kuchagua kukaa kwenye kiti kimoja na mgeni wako au kukaa kwa kuangaliana.

Jambo moja la kipekee sana lilikuwa ni maktaba ya gereza. Milionea mmoja aliyeitwa Parkhurst aliacha wosia kuwa maktaba yake wapewe gereza la Norfolk. Pengine alikuwa anapendezwa nasuala la kubadili watu tabia kuwafanya wawe bora zaidi. Inaonekana alipendelea sana kusoma vitabu vya historia na dini. Maelfu ya vitabu vyake yalikuwa kwenye makabati ya maktaba na vingine vingi viliwekwa kwenye makasha baada ya kukosekana nafasi kwenye makabati. Pale Norfolk tuliweza kuingia maktaba na kuchagua vitabu baada ya kupata ruhusa. Kulikuwa na mamia ya vitabu vya kale, vingine vikiwa adimu kabisa. Mwanzoni nilikuwa najisomea tu, lakini baadaye nilikuja kujifunza jinsi ya kuchagua cha kusoma na kusoma kwa malengo.

Sikumsikia Reginald kwa muda mrefu toka nihamie Norfolk, lakini nilihamia pale nikiwa nimeacha kuvuta sigara na kula nyama ya nguruwe. Suala la kutokula nguruwe liliwashtua baadhi ya watu pale. Baada ya muda kupita nikawa nimepokea barua akinitaarifu kuwa atakuja kunitembelea. Alipofika nilikuwa na shauku kubwa ya kusikia mbinu aliyotaka kunipa.

Reginald alifahamu vyema jinsi akili yangu ya mtaani ilivyofanya kazi na hiyo ndiyo sababu njia aliyotumia kuniingia ilifanya kazi vyema.

Mara zote alivalia nadhifu sana na siku alipokuja kuniona alikuwa nadhifu zaidi. Nilikuwa na hamu kubwa ya kusikia kitendawili cha “Usile nguruwe wala kuvuta sigara” kikiteguliwa. Lakini yeye alizungumza kuhusu familia, mambo yanayotokea huko Detroit na Harlem alipopita mara ya mwisho. Kamwe sikuwahi kumhimiza mtu aniambie kitu chochote kabla ya yeye mwenyewe hajawa tayari. Kwa namna alivyoongea kwa kuzunguka nilifahamu kuwa kuna kitu kikubwa kinafuata.

Mwishowe, kama vile kuna kitu kimemgutusha, alisema, “Malcom, fikiria mtu awe anajua kila kitu duniani, atakuwa mtu wa namna gani?”

Tulipokuwa Harlem alikuwa anapenda kuongea kwa njia hii isiyo ya moja kwa moja. Mara nyingi hilo lilinikera sana maana mimi sikuwa mtu wa kupindishapindisha maneno. Nilimuangalia na kujibu, “Atakuwa kama aina fulani ya mungu hivi-”

Reginald akasema, “Kuna mtu anafahamu kila kitu.” “Nani huyo?” niliuliza. “Mtu huyo ni Mungu,” alisema Reginald. “Jina lake halisi ni Allah.”

Allah. Nilikumbuka kuona jina hilo kwenye barua ya Philbert; hiyo ilikuwa ishara ya kwanza iliyonifanya nianze kuunganisha mambo. Reginald aliendelea. Aliniambia kuwa Mungu ana maarifa ya nyuzi 360. Akaongeza kuwa nyuzi 360 zinawakilisha “Jumla ya maarifa yote.”

Kusema kuwa nilichanganyikiwa itakuwa haitoshi. Maana kumbuka kuwa nilikuwa namsikiliza nikitarajia atazungumzia jambo fulani. Niliendelea tu kusikiliza nikijua kuwa mdogo wangu ana jambo anataka kunieleza. Na kama mtu ana jambo anataka kukueleza unatulia na kumsikiliza.

“Shetani ana nyuzi thelathini na tatu tu za maarifa zinazojulikana kama Umasoni.” Alisema Reginald. Nakumbuka maneno yake vyema sababu baadaye niliyatumia kuwafundisha wengine. “Shetani anatumia Umasoni wake kuwatawala watu.”

Akanieleza kuwa Mungu huyo amekuja Marekani na amejifunua kwa mtu aliyeitwa Elijah-“mtu mweusi kama sisi tu.” Mungu huyu amemjulisha Elijah kuwa “muda wa shetani umeisha.

Sikujua hata cha kufikiri. Niliendelea tu kusikiliza.

“Shetani naye ni mtu,” aliendelea Reginald.

“Unamaanisha nini?”

Kwa ishara ya kichwa Reginald alinielekezea upande waliokaa wafungwa wa kizungu na wageni wao, wakizungumza kama sisi. “Hao,” alisema. “Mzungu ndiye Shetani.”

Aliniambia kuwa wazungu wote wanafahamu kuwa wao ni mashetani-“Hasa Ma-masoni.” Sitakuja kusahau: kwa kasi, akili yangu ilichambua aina zote za “wazungu” niliowafahamu; mwishowe iligota kwa Hymie, Myahudi ambaye alikuwa mwema sana kwangu. Mara kadhaa nilikuwa nimeenda na Reginald kwenye kile kiwanda cha pombe za magendo kule Long Island kununua na kupakia pombe za Hymie.

Niliuliza, “Wazungu wote?” “Wote,” alijibu.

“Hata Hymie?” “Kwani kuna tatizo gani iwapo nikakuacha utengeneze dola mia tano wakati mimi natengeneza dola elfu kumi?” Baada ya Reginald kuondoka nilizama kwenye fikra. Nilifikiri na kufikiri. Sikuelewa hata kidogo.

Taswira za wazungu niliowafahamu zilipita akilini mwangu, toka mwanzo wa maisha yangu. Wazungu kutoka serikalini waliokuja nyumbani kwetu baada ya wazungu wengine nisiowafahamu kumuua baba yangu. . . wazungu waliokuwa wakimwita mama yangu kichaa mbele yake, na mbele yangu na ndugu zangu hadi mwishowe alipopelekwa hospitali ya wagonjwa wa akili huko Kalamazoo. . . jaji wa kizungu na wengine waliotutawanya watoto. . . familia ya Swerlin, wazungu wengine wa Mason. . . vijana wa kizungu niliosoma nao, waalimu, mwalimu aliyeniambia niwe “Seremala” nilipokuwa darasa la nane sababu ni upumbavu kwa mtu mweusi kuwaza kuwa mwanasheria. . . .

Kichwa changu kilijaa sura za wazungu. Wazungu wa Boston wakati wa dansi ya wazungu kwenye ukumbi wa Roseland kipindi nilipokuwa mng’arisha viatu. . . Nilipokuwa nikipeleka sahani jikoni kule kwenye mgahawa wa Parker. . . wafanyakazi na wasafiri kwenye treni. . . Sophia. . . .

Wazungu wa New York-polisi na wahalifu wa kizungu nilioshughulika nao. . . wazungu waliojazana kwenye baa za vichochoroni za watu weusi kuja kuonja roho za weusi . . . wanawake wa kizungu waliotaka wanaume weusi. . . wanaume wa kizungu niliowapeleka kwenye “madanguro maalumu” kutimiziwa haja walizotaka. . . .

Mnunua vitu vya wizi kule Boston na wakala wake. . . polisi wa Boston. . . rafiki wa mume wa Sophia, mume wa Sophia ambaye sikuwahi kumuona lakini nilimfahamu vilivyo . . . mdogo wa Sophia . . . Myahudi muuza vito ambaye alisaidia kunaswa kwangu . . . watu wa ustawi wa jamii . . . watu wa mahakama ya wilaya ya Middlesex . . . hakimu aliyenihukumu miaka kumi . . . wafungwa niliokuja kuwafahamu, askari na maofisa wengine. . .

Mtu aliyekuwa maarufu kwenye gereza la Norfolk alikuwa ni mzee mmoja aliyepooza na tajiri, aliitwa John. Alikuwa amefungwa kwa kumuua mtoto wake. Moja ya yale mauaji ya “rehema.” Alikuwa ni mjivuni sana, siku zote akijitapa kuwa ni Masoni wa daraja la 33, na jinsi Masoni walivyo na nguvu kiasi kwamba ni Masoni tu ndiyo wamewahi kuwa marais wa Marekani, na kuwa Masoni anayehitaji msaada anaweza kuwapa ishara ya siri majaji na watu wengine wakubwa.

Nilikuwa bado nawaza mambo aliyoniambia Reginald. Nilitaka kuyajaribu kwa John. Alikuwa amepangiwa kazi nyepesi-nyepesi kwenye shule ya gereza. Nilienda kumuona huko.

“John,” nilisema, “Duara lina nyuzi ngapi?”

“Mia tatu na sitini,” alijibu.

Nilichora umbo mraba na kumuuliza, “Hilo umbo lina nyuzi ngapi?” akajibu mia tatu na sitini. Nikamuuliza iwapo nyuzi mia tatu na sitini ndiyo kikomo cha “nyuzi” kwenye kitu chochote kile.

Akaseme “Ndiyo.” Nikasema, “Kwa nini basi Masoni wanaishia nyuzi thelathini na tatu tu?”

Hakuwa na jibu la kuridhidha. Lakini kwangu jibu lilikuwa ni kuwa Umasoni ni nyuzi thelathini na tatu tu za Uislamu ambao una nyuzi kamili. Nyuzi ambazo kamwe Ma-masoni hawataweza kuzifikia japo walifahamu uwepo wake.

Reginald alipokuja kunitembelea tena baada ya siku chake, aliweza kujionea jinsi waneno yake yaliyoniathiri kwa jinsi nilivyokuwa. Alionekana kufurahi sana. Kisha kwa msisitizo aliongea kwa saa mbili kuhusu “Shetani mzungu” na “Mtu mweusi aliyechotwa akili.”

Reginald alipoondoka aliniacha nikihangaika na mawazo mengi mazito ambayo sijawahi kuwa nayo maishani mwangu: kwamba mzungu alikuwa akipoteza nguvu zake za kukandamiza na kunyonya dunia ya wasio wazungu kwa kasi; na kuwa dunia ya wasio wazungu ilianza kuamka ili kutawala dunia tena, kama ilivyokuwa huko nyuma; kwamba dunia ya mzungu ilikuwa ikianguka, ilikuwa ndiyo inaishia.

“Hata hujijui wewe ni nani,” alikuwa ameniambia Reginald. “Shetani mweupe amekuficha hata hufahamu kuwa jamii yako ni ya watu waliostaarabika zamani za kale, watu matajiri wa dhahabu na wafalme. Hata jina halisi la ukoo wako hulifahamu, hata leo ungeisikia lugha yako ya asili usingeitambua. Shetani mweupe amekuficha maarifa yote kuhusu jamii yako. Umekuwa mhanga wa shetani mweupe toka alipobaka na kuua na kukuiba kutoka nchi yako ya asili . . . ”

Nilianza kupokea barua zisizopungua mbili kila siku kutoka Detroit kwa ndugu zangu. Kaka yangu mkubwa, Wilfred na mke wake wa kwanza, Bertha –wote waliniandikia(Wilfred alizaa wtoto wawili na Bertha, baada ya kifo chake akamuoa mke wake wa sasa, Ruth). Philbert na Hilda pia waliniandikia. Reginald alinitembelea, akikaa kidogo Boston na kurejea Detroit. Wote walikuwa Waislamu, wafuasi wa mtu waliyemtambulisha kwa jina la “Mtukufu Elijah Muhammad,” mtu mmoja mwenye umbo dogo na mpole. Wakati mwingine walimtambulisha kama, “Mtume wa Allah.” Walisema alikuwa ni mweusi kama sisi, mzaliwa wa Marekani, huko Georgia mashambani. Baadaye akawa amehamia Detroit na familia yake na huko akakutana na Bwana Wallace D. Fard aliyedai kuwa alikuwa ni Mungu katika mwili. Bwana Wallace D. Fard alikuwa amempatia Elijah Muhammad ujumbe wa Allah kwenda kwa watu weusi ambao walikuwa ni “Taifa la Kiislamu lililopotelea kwenye nyika za Amerika ya Kaskazini.”

Wote walinihimiza nipokee mafundisho ya mtukufu Elijah Muhammad. Reginald aliniambia kuwa Waislamu hawali nyama ya nguruwe na hawavuti sigara, ilikuwa ni sheria kwa wafuasi wote wa Elijah Muhammad maana hawakupaswa kutumia vitu vya kudhuru kama madawa ya kulevya, tumbaku au pombe. Nilisoma na kusikiliza tena na tena, “Msingi wa Uislamu ni kusujudia, mtu kujinyenyekeza kwa Allah.”

Walinipatia kwa kirefu “Maarifa ya kweli juu ya mtu mweusi” waliyokuwa nayo wafuasi wa Elijah Muhammad kupitia barua ambazo nyakati nyingine zilikuwa na makala zilizochapwa.

***​
 
“Maarifa ya kweli” niliyoyaelewa vyema ni yaliyosema kuwa historia ilikuwa imechakachuliwa na wazungu kwa maslahi yao, na kuwa mtu mweusi amechotwa akili kwa mamia ya miaka. Na kuwa mtu wa kwanza alikuwa mweusi na aliishi barani Afrika, na huko ndiko mwanzo wa binadamu.

Kwamba mtu mweusi, mtu wa asili, alijenga milki na kuanzisha ustaarabu wakati mzungu akiwa bado anatembea kwa miguu minne na akiishi mapangoni huko Ulaya. Na katika historia yote, “Shetani Mweupe” kutokana na ushetani wake, ameponda, amebaka, ameua na kunyonya jamii zingine zote za watu ambao si wazungu. Na kuwa uhalifu mkubwa kabisa kuwahi kutokea duniani ulikuwa ni kitendo cha mzungu kwenda Afrika na kukamata mamilioni ya watoto, wanaume na wanawake weusi na kuwafanya watumwa. Akiwatumikisha kwa mateso na kipigo.

Kisha shetani huyu akamnyima mtu mweusi maarifa juu yake mwenyewe. Maarifa juu ya dini yake, lugha na utamaduni wake halisi mpaka pale mtu mweusi wa Marekani alipokuwa mtu pekee duniani asiyejijua kabisa yeye ni nani.

Na katika wakati fulani, wanawake weusi waliokuwa watumwa walibakwa na mabwana wao wa kizungu hadi kukaanza kutokea jamii mpya, jamii iliyochotwa akili na ambayo haikuwa na rangi ya asili. Jamii ambayo haikujua majina halisi ya koo zao. Mmiliki watumwa huyu wa kizungu alilazimisha jamii hii mpya iliyotokana na ubakaji kutumia jina lake. Akaiita jamii hiyo mpya “Negro”

Mnegro huyu alifundishwa kuwa Afrika, nchi yake ya asili, ilikaliwa na washenzi walioruka mitini kama nyani. Mnegro huyu alikubaliana na hilo na mafundisho mengine ya bwana wake, mafundisho yalidhamiria kumfanya amtii na kumsujudia mzungu.

Wakati dini za watu wote duniani hufundisha juu ya Mungu wanayeweza kumtambua, Mungu ambaye walau anafanana nao kwa muonekano, bwana huyu aliingiza dini yake ya Kikristo kwa mnegro wake. Mnegro akafundishwa kumuabudu Mungu wa kigeni aliyekuwa na nywele, rangi na macho ya bluu kama bwana wake.

Dini hiyo imemfundisha Mnegro kuwa weusi ni laana. Imemfundisha kuchukia kila kitu cheusi, hata kujichukia mwenyewe. Imemfundisha kuwa kitu chochote cheupe ni kizuri na kinatakiwa kuheshimiwa na kupendwa. Dini hiyo imemchota akili mnegro huyu na kumfanya aamini kuwa anakuwa bora zaidi iwapo ngozi yake inaonyesha rangi ya bwana wake. Na hata zaidi, Ukristo wa mzungu umemchota akili mtu mweusi na kumwambia “Ageuze shavu jingine” na akenue, ainame, anyenyekee, aimbe na kuomba kwa chochoten atakachofanyiwa na shetani wa kizungu—na atarajie keki yake kutoka angani na mbingu yake baada ya kufa, huku bwana wake wa kizungu akifurahia mbingu yake hapa hapa duniani.

Mara nyingi nimeangalia nyuma na kujaribu kuchunguza muitikio wangu wa kwanza baada ya kusikia haya. Akili zangu, ujanja na hila zangu za mtaani zilinituma kukataa kila kitu, lakini kwa hili zilikufa ganzi. Nakumbuka wakati mmoja hapo baadaye kwenye gereza la Norfolk nilipokuwa nasoma biblia kwenye maktaba, nilikutana na kisa cha Paulo, kisa ambacho nilikisoma tena na tena. Kilihusu safari ya Paulo alipokuwa njiani kwenda Damascus. Kinasimulia kuwa Paulo aliposikia sauti ya Yesu alishtushwa sana hadi akadondoka kutoka juu ya farasi wake. Si zamani wala si sasa-sijawahi kujifananisha na Paulo, lakini naelewa vema kilichomtokea.

Toka hapo nimejifunza kuelewa kile kilichoanza kunitokea wakati ule. Kwamba ukweli unaweza kupokelewa haraka au hata tu kupokelewa na mtenda dhambi anayekiri kuwa ni mtenda dhambi na anajuta. Kwa maneno mwengine; watu ambao Yesu hakuweza kuwasaidia, Mafarisayo; hawakuhisi kama wanahitaji msaada.

Majuto juu ya maisha yangu mapotovu niliyoishi hapo nyuma ndiyo yaliyoniandaa kuikubali kweli.

Kwa majuma kadhaa sikuweza kukabiliana na ukweli. Hakika ulikuwa kama mwanga wenye kupofusha.

Reginald aliondoka Boston na kurudi Detroit. Nilikuwa nikikaa chumbani mwangu na kutulia nikitafakari. Hata chakula kilikuwa hakipandi, nilikunywa tu maji. Wafungwa wenzangu na askari walionijali waliniuliza nini kinanisumbua. Walinishauri nikamuone daktari lakini sikwenda. Baada ya daktari kujulishwa hali yangu alinitembelea, sijui alinigundua nina tatizo gani, pengine aliona kuwa najifanya tu.

Nilikuwa napitia kitu kigumu lakini cha maana zaidi kinachoweza. Kitendo cha binadamu yeyote kukubaliana na jinsi ulivyo ndani na nje yako ni kitendo cha manaa sana.

Baadaye nilikuja kufahamu kuwa ndugu zangu wa Chicago na Detroit walikuwa wamechanga pesa ili Hilda aje kunitembelea. Hilda aliniambia kuwa Mtukufu Elijah Muhammad alipotembelea huko Detroit aliishi nyumbani kwa kaka yangu Wilfred, mtaa wa McKay. Hilda alinihimiza sana kumuandikia Bwana Muhammad. Aliniambia kuwa Elijah alielewa vyema jinsi ilivyo kufungwa kwenye magereza ya wazungu, maana yeye mwenyewe hana muda mrefu toka atoke gereza la Milan huko Michigan ambako alitumikia kifungo cha miaka mitano kwa kukwepa kutumikia jeshini.

Hilda aliniambia kuwa Mtukufu Elijah Muhammad alifika Detroit ili kuliweka sawa Hekalu lake Namba Moja baada ya kuwa limevurugika alipokuwa gerezani, lakini makazi yake ya kudumu yalikuwa Chicago alikokuwa akisimamia na kujenga Hekalu Namba Mbili. Hilda ndiye aliyeniambia, “ungependa kufahamu mtu mweupe alikujaje duniani?”

Basi akanifundisha jambo hilo, moja ya mafundisho ya msingi ya Bwana Elijah Muhammad, fundisho juu ya uwepo wa shetani ambalo kila dini linalo. Fundisho hilo liliitwa “Historia ya Yakubu.” Elijah Muhammad anafundisha wafuasi wake kuwa hapo mwanzo mwezi ulijitenga na dunia. Kisha mtu wa kwanza akatokea na alikuwa mweusi. Watu hao weusi ndiyo walioanzisha mji mtakatifu wa Mecca.

Kati ya watu hawa weusi kulikuwa na watu ishirini na nne wenye hekima. Mmoja kati yao alitofautiana na wenzake na akatengeneza kabila la watu weusi wenye nguvu sana lililoitwa Shabazz. Na watu weusi wa Marekani ni wa kutoka katika kabila hilo.

Kisha kama miaka elfu sita iliyopita. Wakati asilimia sabini ya watu walikuwa wameridhika na asilimia thelathini wakiwa wasioridhika, alizaliwa bwana Yakubu kutoka jamii ya wasioridhika. Alizaliwa ili kuleta matatizo na kuvuruga amani na kuua. Kichwa chake kilikuwa kikubwa kuliko kawaida. Alipofika umri wa miaka minne alianza shule. Akiwa na miaka kumi na nane akawa amemaliza kusoma vyuo vyote vya nchini mwake. Alijulikana kwa jina maarufu kama “Mwanasayansi mwenye kichwa kikubwa.” Moja ya jambo alilokuwa amejifunza lilikuwa ni kuzalisha jamii za watu kisayansi.

Basi bwana Yakubu akaanza kuhubiri kwenye mitaa ya Mecca. Alijipatia wafuasi wengi hadi mamlaka zikaanza kuingiwa na wasiwasi. Mwishowe walimtimua na wafuasi wake 59,999 kwenda kisiwa cha Patmo—Kisiwa ambacho Yohana alipokea maono aliyoyaandika katika kitabu cha Ufunuo kinachopatikana katika Biblia.

Japo bwana Yakubu alikuwa ni mtu mweusi, lakini kwa hasira zake kumuelekea Allah aliamua kulipa kisasi, aliamua kutengeneza jamii ya mashetani duniani—jamii ya watu waliochujuka rangi, yaani watu weupe.

Kutokana na masomo yake, mwanasayansi mwenye kichwa kikubwa aligundua kuwa watu weusi wana vinasaba viwili, kimoja cha rangi nyeusi na kimoja cha rangi ya kahawia. Alijua kuwa mbegu ya kahawia haikuonekana sana kwa sababu ilikuwa ilikuwa dhaifu. Bwana Yakubu ili kuharibu mpangilio wa asili, akatumia teknolojia ambayo leo tunaiita teknolojia ya vinasaba kutenganisha vinasaba vyeusi na vya kahawia. Alijua kuwa binadamu watakaozaliwa watakuwa dhaifu na muelekeo wa kuwa wabaya na waovu. Kwa njia hii atakuwa amefikia lengo lake la kuwa na jamii ya mashetani weupe.

Alifahamu kuwa itamchukua hatua nyingi za kubadili rangi hadi kupata mtu mweupe kutoka kwa mweusi. Basi akaanza kazi yake kwa kuanzisha sheria za kieugenic(kudhibiti aina ya watu watakaozaliwa) katika kisiwa cha Patmo.

Kati ya wafuasi 59,999 wa bwana Yakubu, katika kila watoto watatu waliozaliwa basi mmoja alikuwa na rangi ya kahawia. Watu hawa walivyokuwa wakubwa, ni mtu wa kahawia na wa kahawia tu au wa kahawia na mweusi tu ndiyo waliruhusiwa kuoana. Bwana Yakubu alitunga sheria iliyowataka wakunga kumchoma mtoto sindano ya kwenye ubongo iwapo alizaliwa mweusi na kisha mwili wake ukachomwe moto. Mama zao waliambiwa kuwa watoto wao walikuwa malaika hivyo wameenda mbinguni kuwaandalia makao.

Lakini mama aliyezaa mtoto wa kahawia aliambiwa amtunze sana mwanaye.

Bwana Yakubu alifundisha pia wasaidizi wa kuendeleza kazi yake. Hata alipokufa akiwa na umri wa miaka mia moja na hamsini na mbili, alikuwa amewaachia sheria na kanuni za kufuata. Kulingana na mafundisho ya Bwana Elijah Muhammad, Bwana Yakubu hakushuhudia malengo yake yakitimizwa, yaani kuzaliwa kwa jamii ya shetani weupe.

Ilihitajika miaka mia mbili kufuta kizazi cha watu weusi katika kisiwa cha Patmo na kubakiza watu wa kahawia tu.

Baada ya miaka mia mbili mingine watu wa kahawia wakawa wa wekundu-kukiwa hakuna kabisa watu wa kahawia. Na baada ya miaka mia mbili zaidi mtu mweupe akatokea. Kufikia hapo hakukuwa na watu wengine wowote katika kisiwa cha Patmo isipokuwa shetani wenye nywele za rangi ya dhahabu, rangi nyeupe na macho ya bluu. Wakiwa na vinyweleo na uchi kama wanyama. Walitembea kwa miguu minne na kuishi kwenye miti.

Ilichukua miaka mia sita mingine kwa watu hawa kurudi bara, yaani kwenda maeneo ya watu weusi.

Elijah Muhammad anafundish wafuasi wake kuwa ndani ya miezi sita, kwa kutumia uongo-watu weupe hawa wakawa wamefanikiwa kuwafarakanisha watu weusi na kusababisha wapigane wao kwa wao. Wakafanya iliyokuwa mbingu duniani kugeuka kuzimu iliyojaa mizozo na mapigano.

Lakini mwishowe watu weusi walitambua kuwa matatizo yao yamesababishwa na jamii hii ya shetani weupe waliotengenezwa na bwana Yakubu. Waliwakamata na kuwafunga kwa minyororo. Waliwaswaga kuvuka jangwa la Uarabuni hadi kwenye mapango ya Ulaya.

Alama ya ngozi ya kondoo na kamba wanayotumia M-masoni leo ni ishara ya jinsi mzungu alivyoficha uchi wake alipokuwa amefungwa minyororo na kuswagwa kwenye jangwa lenye joto.

Bwana Elijah anaendelea kufundisha kuwa shetani mweupe aliishi maisha ya kishenzi sana huko kwenye mapango ya Ulaya. Wanyama walipojaribu kumuua alikimbilia mitini. Na pia alitengeneza marungu ili kulinda familia yake dhidi ya wanyama wa porini waliojaribu kuwashambulia.

Baada ya jamii hii ya mashetani kuishi kwa miaka elfu mbili mapangoni, Allah akamuinua Musa ili kuwastaarabisha na kuwatoa mapangoni. Ilikuwa imeandikwa kuwa jamii hii ya mashetani itatawala dunia kwa muda wa miaka elfu sita.

Vitabu vya Musa vilipotea ndiyo maana haifahamiki kwa watu kuwa alikaa mapangoni

Musa alipofika, watu wa kwanza wa jamii ya kishetani kutoka mapangoni walikuwa ni ambao leo tunawaita Wayahudi.

Kulingana na mafundisho ya hii “Historia ya Yakubu” Biblia inaposema Musa alimuinua nyoka jangwani, ni ishara ya jinsi Musa alivyowatoa jamii ya mashetani weupe kwenye mapango ya Ulaya na kuwafundisha ustaarabu.

Iliandikwa kuwa baada ya jamii ya mashetani weupe waliotengenezwa na Yakubu kutawala dunia kwa miaka elfu sita-hadi nyakati zetu hizi—kutoka katika jamii ya asili, yaani watu weusi, atazaliwa mwana ambaye hekima zake, nguvu na maarifa vitakuwa havina kifani.

Iliandikwa kuwa baadhi ya watu weusi wataletwa Amerika ya Kaskazini kuwa watumwa, lengo hasa ni kushuhudia sura halisi ya shetani mweupe.

Elijah Muhammad anafundisha kuwa Mungu mkuu na mwenye nguvu kuliko wote aliyefika duniani ni W. D. Fard. Alitoka mashariki na kuelekea magharibi. Akitokea katika Amerika ya Kaskazini wakati wa kutimizwa kwa unabii, watu wasioweupe walipoanza kuasi utawala wa weupe, watu weupe walipoanza kusimama na kupigana wenyewe kwa wenyewe—wakati utawala wa shetani weupe uliolaaniwa na Allah ulipoanza kujiharibu wenyewe sababu ya asili yake ya kishetani.

Bwana W. D. Fard alikuwa ni chotara wa kizungu na mtu mweusi. Alikuwa amefanywa namna hii ili kumfanya akubalike na watu weusi wa Marekani ya Kaskazini na kuwaongoza, na wakati huohuo aweze kujichanganya katikati ya wazungu ili aweze kuwaelewa na kuwahukumu maadui wa watu weusi.

Mwaka 1931 Bwana W. D. Fard akijidai ni muuzaji wa vitambaa vya Hariri, alikutana na Elijah Muhammad huko Detroit Michigan. W. D. Fard alimpatia Elijah Muhammad ujumbe wa Allah na Muongozo wake wa kuokoa Taifa la Kiislamu lililopotea, yaani watu weusi waliokuwa Amerika ya Kaskazini.

Hilda alipomaliza kunisimulia “Historia ya Yakubu” aliondoka. Sikumbuki kama niliweza kufungua mdomo na kusema kwa heri. Baadaye nilikuja kufahamu kuwa hekaya za Elijah Muhammad kama hii “Historia ya Yakubu” ziliwakasirisha sana Waislamu wa huko Mashariki. Nilipokuwa Mecca niliwakumbusha kuwa kosa ni lao wenyewe kwa sababu hawajafanya jitihada za kutosha kufanya Uislamu wa kweli ujulikane huko kwenye mataifa ya Magharibi. Ukimya wao uliacha ombwe ambalo tapeli yeyote wa kidini angeweza kulitumia kupotosha watu.

Mwisho wa sura ya kumi​
 
SURA YA KUMI NA MOJA

KUOKOLEWA

Nilimuandikia Elijah Muhammad barua. Wakati huo alikuwa akiishi huko Chicago, nyumba namba 6116 katika barabara ya South Michigan. Nadhani niliandika barua ile ya kurasa moja si chini ya mara ishirini na tano, nilikuwa najaribu kuifanya isomeke na kueleweka vizuri. Wakati huo hata mimi mwenyewe sikuweza kusoma muandiko wangu mwenyewe; ni aibu hata kukumbuka. Muandiko na uundaji wangu wa sentensi ulikuwa mbovu sana. Basi kwa kadri nilivyoweza nilimwambia kuwa nimesikia kumuhusu kutoka kwa ndugu zangu na kuomba aniwie radhi kwa barua yangu mbovu.

Bwana Elijah alinijibu kwa barua iliyochapwa. Niliguswa sana kuona saini ya “Mtume wa Allah.” Alinikaribisha kwenye kweli na kunipa jambo la kutafakari. Alisema kuwa mfungwa mweusi ni ushahidi wa uhalifu wa jamii ya kizungu, uhalifu wa kumkandamiza mtu mweusi na kumfanya aendelee kuwa mjinga ambaye hawezi kupata kazi yoyote ya maana na hivyo kugeukia uhalifu.

Aliniambia niwe jasiri na hata aliniwekea kiasi fulani cha pesa, dola tano. Bwana Muhammad aliwatumia pesa wafungwa waliomuandikia barua kotekote nchini, pengine hata leo bado anafanya hivyo.

Familia yangu iliniandikia mara kwa mara, “Mgeukie Allah . . . Sali kuelekea mashariki.”

Mtihani mkubwa kabisa kukabili katika maisha yangu ulikuwa ni kusali. Nadhani unaelewa. Kuelewa na kuamini mafundisho ya Elijah Muhammad kulihitaji tu akili yangu kuniambia, “Hilo ni sawa,” au “Sikuwahi kufikiri hilo.”

Lakini kitendo cha kupiga magoti na kusali-kitendo hicho kilinichukua juma zima kuweza kukifanya.

Unafahamu jinsi maisha yangu yalivyokuwa. Wakati wa kufungua kitasa cha nyumba nilipokuwa navamia nyumba kuiba ilikuwa ndiyo nyakati pekee nilizopiga magoti.

Ilinilazimu kujilazimisha kupiga magoti. Lakini ghafla wimbi la aibu na fedheha lilinilazimisha kusimama. Jambo gumu kabisa duniani kwa mtu muovu ni kupiga magoti, kukubali makosa na kuomba msamaha kwa Mungu. Kwa sasa ni rahisi kwangu kuliongelea suala hilo. Lakini wakati ule, nilipokuwa “Uovu katika mwili” ulikuwa mtihani mkubwa. Nilijilazimisha tena na tena kupiga magoti kumsujudia Allah. Na hata mwishowe nilipofanikiwa kupiga magoti sikujua cha kumwambia Allah.

Kwa mwaka wote uliofuata nilikuwa kama mtawa pale gerezani. Sijawahi kuwa na shughuli nyingi namna ile maishani mwangu. Bado nastaajabia jinsi mtazamo wangu niliokuwa nao hapo kabla ulivyotoweka haraka, kama theluji inavyoyeyuka haraka juu ya paa. Ilikuwa kama yule aliyeishi kwa upambanaji na uhalifu alikuwa mtu mwingine niliyemfahamu tu.

Sikuweza kueleza namna nilivyohisi ndani ya barua za kurasa moja nilizomuandikia Elijah Muhammad kila siku. Karibu kila siku niliandika barua mbili, nyingine nikiwajibu ndugu zangu walioniandikia. Kila barua waliyoniandikia iliongeza maarifa yangu juu ya mafundisho ya Elijah Muhammad. Nilikuwa ninakaa kwa muda mrefu sana nikitazama picha zake.

Sijawahi kuwa mtu goigoi. Kila kitu kilichonigusa nilikifanyia kazi. Nafikiri ndiyo sababu baada ya kukosa kitu kingine cha kufanya nikaanza kuwaandikia wengine niliofahamiana nao kwenye dunia ya upambanaji. Niliwaandikia Sammy the Pimp, John Hughes, Jumpsteady; yule mwizi maarufu na wauza dawa za kulevya kadhaa. Niliwaandikia yote kuhusu Allah, Uislamu na Elijah Muhammad. Sikujua mahali hasa walipoishi wakati huo. Niliandika barua zipitie kwenye baa na club za Harlem na Roxbury, mahali tulikofahamiana.

Sikupata jibu hata moja. Mpambanaji wa kawaida hakuwa na elimu ya kutosha kuweza kuandika barua. Niliwafahamu wapambanaji wengi wajanja na nadhifu, watu wanaoweza kukufanya ufikiri wanahusika na soko la hisa lakini kumbe wakipokea barua wanatafuta mtu wa kuwasomea. Lakini hata mimi mwenyewe nisingejibu iwapo mtu angeniandikia barua kuwa “Mzungu ni shetani.”

Habari zilizosambaa huko Harlem na Roxbury ni kuwa Detroit Red amepatwa na ukichaa gerezani, au labda anajaribu kuwachezea mchezo mabwana jela.

Kwa miaka yote niliyoishi gereza la Norfolk hakuna ofisa yeyote aliyeniuliza kuhusu barua zile japokuwa barua zote zilikaguliwa. Nina hakika walichunguza niliyoandika na kuweka kwenye makabrasha ambayo kila gereza lilikuwa nayo kwa ajili ya kuweka wafungwa weusi waliofuata mafundisho ya bwana Elijah Muhammad.

Lakini wakati huo nilidhani sababu ya kutoulizwa ni kutokana na mzungu kufahamu vyema kuwa yeye ni shetani.

Baadaye hata niliandika kwenda kwa Meya wa Boston, Gavana wa Massachusetts na Rais Harry S Truman. Hawakunijibu, pengine hata barua zangu hawakuwahi kuziona. Niliwaeleza jinsi ambayo mzungu anahusika na hali mbaya anayopitia mtu mweusi katika Amerika ya Kaskazini.

Ni kwa sababu ya barua zangu ndipo nilianza kuona uhitaji wa kujielimisha.

Nilianza kutatizika sana kwa sababu ya kushindwa kueleza niliyotaka kueleza ndani ya barua, hasa zile nilizomuandikia Elijah Muhammad. Mtaani nilikuwa mpambanaji mwenye uelewa mkubwa sana, watu walinisikiliza nilipoongea. Lakini sasa sikuweza kuandika hata kiingereza rahisi tu, nilikuwa bure kabisa. Sipati picha barua ingeonekanaje iwapo ningeiandika kwa lugha ya mtaani ambayo nilizoea kuzungumza, labda ingekuwa namna hii, “Look Daddy, let me pull your coat about a cat, Elijah Muhammad-”

Wengi ambao huniona leo nikiongea sehemu, au kupitia luninga na redio, au kusoma sehemu mambo niliyosema, hudhani kuwa nimesoma zaidi ya darasa la nane. Hilo linachangiwa hasa na elimu niliyopata gerezani.

Tamaa ya kujifunza ilianza hasa nilipokuwa gereza la Charlestown pale Bimbi aliponifanya nione wivu kwa jinsi alivyokuwa na maarifa. Mara zote Bimbi aliongoza mazungumzo aliyokuwemo. Lakini kila kitabu nilichoshika kilikuwa na sentensi ambazo neno moja au karibu yote yalikuwa kama ya Kichina kwangu. Na nilipofanya kuyaruka maneno hayo, nikawa najikuta sijaelewa kikamili dhana inayozungumzwa na kitabu hicho. Basi nikafika gereza la Norfolk nikiwa najisomea vitabu bila kuelewa kikamili, na nilikuwa karibu kuacha hata kufanya hivyo iwapo nisingepata msukumo nilioupata.

Niligundua kuwa jambo la kufanya ni kutumia kamusi ninapokuwa ninasoma. Kusoma na kuelewa maana ya maneno. Nilikuwa na bahati ya kutambua kuwa natakiwa pia kuboresha muandiko wangu. Muandiko wangu ulisikitisha. Sikuweza hata kuandika kwa kunyooka. Mawazo hayo ndiyo yalinifanya niombe kamusi, kibao cha kuandikia na kalamu ya risasi kutoka shule ya gereza.

Nilitumia siku mbili nikipitia kurasa za kamusi bila kujua hasa nafanya nini. Sikuwahi fahamu kuwa kuna maneno mengi namna ile! Sikufahamu ni maneno gani natakiwa kujifunza. Mwishowe ili kuanza tu, nikaanza kunakili. Polepole na kwa muandiko wangu mbaya nikaanza kunakili kwenye kibao changu kila kitu kilichokuwa kwenye ukarasa wa kwanza, nilinakili hadi alama.

Nadhani ilinichukua siku nzima. Nilipomaliza nikajisomea kwa sauti kila kitu nilichoandika kwenye kibao. Nilisoma tena na tena. Niliamka asubuhi nikiwa nayafikiria maneno yale. Nilijisikia fahari sana baada ya kutambua kuwa si tu nilikuwa nimeandika mambo mengi kwa wakati mmoja, lakini pia kwa sababu nilikuwa nimeandika maneno ambayo sikuwahi dhani yapo duniani. Na zaidi, kwa kujitahidi niliweza kumbuka maana ya baadhi ya maneno yale. Nilipitia tena maneno ambayo sikukumbuka maana yake. Jambo la kuchekesha ni kwamba hadi leo neno la kwanza la kamusi “aardvark” hunijia kichwani mwangu. Kulikuwa na picha yake kwenye kamusi, mnyama mwenye mkia na masikio marefu anayeishi mashimoni huko Afrika. Anaishi kwa kula sisimizi na mchwa. Huingiza ulimi wake mrefu kwenye kichuguu kama wafanyavyo wale wanyama walao mchwa.

Nilihamasika sana kiasi kwamba nilinakili ukurasa uliyofuata. Nao nilivyousoma nilipatwa na shangwe ileile. Kila nilivyoendelea ndivyo nilivyojifunza kuhusu watu, maeneo mbalimbali na matukio ya kihistoria. Kamusi ile ilikuwa kama Encyclopedia ndogo. Mwishowe nikawa nimemaliza herufi A na kuingia herufi B. Hivyo ndivyo nilivyoanza na mwishowe nikanakili kamusi yote. Haikuchukua muda kwa kasi yangu ya kuandika kuongezeka, hasa sababu ya mazoezi. Nadhani kupitia kuandika barua na kunakili kamusi, nitakuwa niliandika maneno milioni hivi.

Nafikiri haikuwa inakwepeka kuanza kusoma vitabu mara baada ya uelewa wangu wa maneno kuongezeka. Kwa mara ya kwanza niliweza kusoma kitabu na kuelewa yaliyoandikwa. Mtu yeyote ambaye hujisomea sana anaweza kuwazia jinsi dunia ilivyonifungukia. Ngoja nikuambie kitu: kutoka wakati huo hadi nilipoondoka gereza lile, kila muda wa ziada niliokuwa nao niliutumia kusoma—maktaba au chumbani kwangu. Usingeweza kuning’oa vitabuni hata kwa tindo. Kutokana na kujifunza mafundisho ya Elijah Muhammad, kutembelewa—mara nyingi na Ella na Reginald na kusoma vitabu, miezi ilikuwa inapita bila hata ya mimi kufikiri kuwa nilikuwa gerezani. Ukweli ni kuwa sijawahi kuwa huru kiukweli maishani mwangu hadi wakati ule.

Maktaba ya gereza la Norfolk ililikuwa kwenye jengo la shule. Mambo mbalimbali yalifundishwa shuleni pale na wakufunzi kutoka sehemu kama Harvard na chuo kikuu cha Boston. Pia kila juma timu za wafungwa zilifanya mijadala ndani ya jengo la shule. Ungeshangazwa sana na jinsi wafungwa walivyoweza kuamshwa na mada kama “Je watoto wanapaswa kunyweshwa maziwa?”

Maktaba ya gereza ilikuwa na vitabu vilivyohusu karibu mambo yote ya maisha. Sehemu kubwa ya vitabu vilivyotolewa na Parkhurst vilikuwa bado kwenye maboksi nyuma ya maktaba—maelfu ya vitabu vya zamani, na kama nilivyosema, ilionekana Parkhurst alipendelea sana dini na historia. Alikuwa na pesa na udadisi wa kuweza kupata vitabu vingi ambazo havikupatikana kwa urahisi. Maktaba ya chuo chochote ingekuwa ni yenye bahati sana kupata vitabu vile.

Kama unavyojua, kwenye gereza ambalo linakazia sana kurekebisha tabia, mfungwa anayeonyesha kupendelea vitabu kuliko kawaida hufurahiwa sana. Kulikuwa na wafungwa kadhaa waliopenda sana kujisomea—hasa wale waliopendelea kushiriki mijadala. Wengine walisemwa na wengi kuwa walikuwa ni Enyclopedia zinazotembea. Walikuwa maarufu sana.

Hakuna chuo duniani kinaweza mtaka mwanafunzi asome kama nilivyosoma baada ya dunia kunifungukia, dunia ya kuweza kusoma na kuelewa. Mara nyingi nilijisomea nikiwa chumbani kwangu kuliko maktaba. Nilipendelea zaidi kusoma nikiwa peke yangu chumbani. Maktaba walimruhusu mfungwa aliyejulikana kusoma sana kuchukua vitabu vingi zaidi ya kiasi kilichowekwa.

Baadaye nikaendelea na kuanza kusoma vitabu vigumu zaidi. Nilikuwa nakasirika sana umeme ulipozimwa saa nne ya usiku. Ilionekana kama kila siku umeme ulizimwa wakati nikisoma sehemu nzuri zaidi. Bahati nzuri nje ya mlango wa selo yangu kulikuwa na taa ya koridoni iliyoingiza mwanga ndani. Mwanga wake ulitosha kusomea, nilisubiri tu dakika chache ili macho yangu yazoee. Hivyo umeme ulipozimwa nilikaa sakafuni na kuendelea kusoma.

Kila baada ya saa moja askari walikuwa wakipita koridoni kukagua vyumba. Niliposikia hatua za askari koridoni nilirukia kitandani na kujidai nimelala usingizi. Mara tu alipopita nilirudi sakafuni na kuendelea kusoma kwa dakika zingine hamsini na nane hadi askari alipopita tena. Zoezi hilo liliendelea hadi ilipofika tisa au kumi usiku. Saa tatu au nne zilinitosha kulala. Mara nyingi nilipokuwa mtaani nililala kwa saa chini ya hapo.

***

Mafundisho ya Elijah Muhammad yalikazia sana jinsi ambavyo historia ilikuwa imechakachuliwa kwa maslahi ya wazungu. Mzungu alipoandika vitabu vya historia hakumuingiza ndani yake mtu mweusi. Hakuna kitu alichoweza kusema Bwana Muhammad kingeweza kunigusa kama hicho. Nilikuwa sijasahau jinsi ambavyo darasani nikiwa darasa la saba na wale wanafunzi wa kizungu kule Mason tulivyojifunza historia ya Marekani. Historia ya mtu mweusi iliandikwa kwenye aya moja tu, na mwalimu aliipitia kwa mzaha tu, “Miguu ya watu weusi ni mikubwa kiasi kwamba wakitembea wanaacha shimo ardhini.”

Hii ni sababu moja iliyofanya mafundisho ya Bwana Muhammad yasambae kwa kasi sana kati ya watu weusi, hata kwa wale ambao hawakuja kuwa wafuasi wake. Kila mtu mweusi aliona ukweli fulani kwenye mafundisho yake. Si rahisi kunionyesha mtu mzima mweusi au mzungu wa Marekani ambaye amejifunza ukweli juu ya mchango wa mtu mweusi kutoka katika vitabu vya historia. Binafsi niliposikia kuhusu historia iliyotukuka ya mtu mweusi, nilianza mara moja kuwinda vitabu vinavyoelezea kwa kina historia ya mtu mweusi.

Nakumbuka vyema vitabu vilivyonivutia mwanzoni, na sasa nimevinunua vitabu vile, ninavyo nyumbani kwa ajili ya kusoma watoto wangu wanapokua. Vilikuwa mfululizo wa vitabu unaoitwa wonders of the world. Vilijaa picha za uchimbuzi wa vitu vya kale na sanamu ambazo kwa sehemu kubwa zinaonyesha watu ambao si wazungu.

Nilipata vitabu vingine kama Story of Civilization cha Will Durant, Outline of History cha H. G. Wells. Kitabu Souls of Black Folk chake W. E. B. Du. Bois kilinipa picha ya historia ya watu weusi kabla hawajaja kwenye nchi hii. Kitabu Negro History cha Carter G. Woodson kilinifungua macho juu ya milki za watu weusi kabla hawajaletwa Marekani, na mapambano ya mwanzo ya mtu mweusi katika kupambania uhuru wake.

Vitabu vitatu Sex and Race vya J. A. Rogers vilielezea juu ya muingiliano wa jamii mbalimbali za watu zamani kabla ya Yesu; kwamba Esopo alikuwa ni mtu mweusi aliyesimulia hekaya; kuhusu mafarao wa Misri; juu ya milki kubwa ya wakristo wa madhehebu ya Kikoptiki; kuhusu Ethiopia, ustaarabu wa kale kabisa wa watu mweusi ambao bado upo-maana China ndiyo ustaarabu kale kabisa duniani ambao bado upo.

Mafundisho ya bwana Muhammad juu ya jinsi mzungu alivyoumbwa yalinipeleka kwenye kitabu Findings in Genetics cha Gregor Mendel. (Nilikuwa nimejifunza maana ya Genetics kwenye eneo G la kamusi). Nilisoma kwa kina sana kitabu hiki kilichoandikwa na kasisi wa Austria. Kusoma kitabu hiki tena na tena kulinifanya nielewe kuwa unaweza zalisha mtu mweupe kutoka kwa mtu mweusi lakini huwezi kuzalisha mtu mweusi kwa kuanza na mtu mweupe sababu vinasaba vya weupe ni dhaifu. Na kwa sababu hakuna anayebisha kuwa kulikuwa na mtu wa asili mmoja tu, basi ilikuwa wazi ni nani mtu wa asili.

Mwaka kama mmoja uliopita, kwenye gazeti la New York Times Arnold Toynbee alitumia maneno “Waliochujuka” alipokuwa anawaelezea wazungu wenye asili ya Ulaya Kaskazini. Pia aliizungumzia Ulaya kama peninsula tu ya bara la Asia. Alisema hakuna kitu kinachoitwa Ulaya. Na ukiangalia kwenye ramani ya dunia utajionea wazi kuwa Ulaya ni sehemu tu ya Asia.(Lakini kwa namna nyingine Tonybee ni moja ya wale waliosaidia kuchakachua historia. Amewahi andika kuwa Afrika ni bara pekee ambalo halina historia. Lakini hataandika hivyo tena. Siku hizi kila siku ukweli unawekwa wazi.)

Sitasahau jinsi nilivyohisi pale nilipoanza kusoma madhira ya utumwa. Ilinigusa sana kiasi kwamba baadaye ilikuja kuwa mada yangu kuu nilipokuwa mhubiri wa bwana Muhammad. Mikono ya wazungu imetenda uhalifu mbaya sana na kumwaga damu nyingi duniani kiasi kwamba si rahisi kuamini. Vitabu kama kile kilichoandikwa na Frederick Olmstead vilifungua macho yangu kuona madhira waliyopitia watumwa walipofika Marekani. Fannie Kimball, mwanamke kutoka Ulaya aliyeolewa na mtu aliyemiliki watumwa huko Kusini ya Marekani, alielezea jinsi binadamu walivyotendewa kama wanyama. Ndiyo, nilisoma Uncle Toms’s Cabin. Naamini hiyo ilikuwa riwaya pekee niliyosoma baadaya kuanza kusoma vitabu makini. Kwenye mkusanyiko wa vitabu vya Parkhurst kulikuwa pia na nyaraka za chama cha wapinga utumwa wa New England. Nilisoma maelezo juu ya ukatili, niliona picha za wanawake weusi wakiwa wamefungwa na kuchapwa mijeledi; mama weusi wakiona watoto wao wakichukuliwa na wasiwaone tena; mbwa zikiwawinda watumwa; wawinda watumwa wakatili; wazungu wakatili wakiwa na minyororo, bunduki na mijeledi. Nilisoma kuhusu Nat Turner, mhubiri aliyekuwa mtumwa, mhubiri aliyeweka hofu ya Mungu ndani ya wamiliki watumwa. Nat Turner hakuhubiri juu ya keki kutoka hewani na kupatikana kwa uhuru wa mtu mweusi bila kumwaga damu. Siku moja usiku mnamo mwaka 1831 huko Virginia, Nat na watumwa wenzake saba walianza na nyumba ya bwana wake, kisha usiku huo huo wakapita kwenye nyumba ya bwana mmoja hadi mwingine wakiua, hadi kufika asubuhi wazungu 57 walikuwa wameuawa na Nat alikuwa na watumwa 70 wakimfuata. Wazungu kwa kuhofia maisha yao walikimbia majumbani mwao, walijifungia kwenye majumba ya umma, walijificha maporini na wengine hata walikimbia jimbo. Jeshi dogo lilichukua miezi miwili kumkamata na kumnyonga Nat. Kuna sehemu nimesoma kuwa mfano wa Nat Turner ndiyo uliomchochea John Brown akiwa na wazungu kumi na tatu na watu weusi watano, kuvamia Virginia na kushambulia kivuko cha Harper miaka thelathini baadaye.

Nilimsoma au niseme nilisoma kumhusu Herodotus, baba wa historia. Na nikasoma historia za mataifa mbalimbali na hilo lilifungua macho yangu hata zaidi. Niliona jinsi ambavyo mzungu ameitenda dunia nzima kishetani, akipora, akibaka nakuifanyia dunia isiyo ya wazungu kila aina ya unyama. Nakumbuka vitabu kama History of Oriental Civilization cha Will Durant na mapambano ya Mahtma Gandhi jinsi alivyopambana kuwatoa Waingereza India.

Vitabu vilizidi kunionyesha jinsi ambavyo mzungu amewaletea watu weusi, wekundu, wa kahawia na wa manjano mateso yatokanayo na kunyonywa. Niliona jinsi ambavyo kuanzia karne ya kumi na sita, watu waliojiita “Wafanyabiashara wa Kikristo” wa kizungu walivyoanza kusafiri baharini kwa tamaa ya kupora milki za Afrika na Asia. Nilisoma na kuona jinsi ambavyo mzungu hajawahi enda kwenye jamii ya watu wengine akiwa amebeba ujumbe halisi wa msalaba na roho ya Kristo—akifundisha unyenyekevu, upole na kufuata mfano wa Kristo.

Kadri nilivyosoma ndivyo nilivyoona jinsi ambavyo mzungu alikuwa tu ni haramia ambaye alitumia Ukristo wake kama tindo ya kuanzishia uhalifu wake. kwanza kabisa aliwapachika jina la upagani na ushenzi wale ambao hawakuwa wazungu. Baada ya kufanya hilo aliwashukia kwa silaha zake za vita.

Nilisoma jinsi alivyoingia India na kukuta watu wa kahawia nusu bilioni. Watu waliokuwa washika dini sana. Lakini kufikia mwaka1759, Muingereza kwa kutumia ulaghai, ahadi za uongo na hila akawa anaitawala sehemu kubwa ya India kupitia kampuni ya Great Britain East India. Kupitia unyonyaji, uongozi wa Waingereza ukaendelea kujipenyeza kwenye sehemu zilizobaki za Bara Hindi. Mwaka 1857 baadhi ya watu wa India walichoshwa na unyonyaji huo hivyo wakaasi. Ukiacha biashara ya watumwa wa Kiafrika, hakuna ukatili mwingine mkubwa uliowahi kufanyika kama uliofanywa na Waingereza wakati wa kuzima uasi wa watu wa India wasio weupe.

Wakati wa biashara ya utumwa, zaidi ya Waafrika weusi milioni 115 waliuawa na kufanywa watumwa—idadi sawa na wakazi wa Marekani mnamo mwaka 1930. Nikasoma jinsi ambavyo mataifa ya Ulaya yalivyojitwalia maeneo mazuri ya Waafrika mara baada ya kukomeshwa kwa biashara ya utumwa. Wazungu wa Ulaya wakifanya unyonyaji wa waziwazi kuanzia Cape Town hadi Cairo.

Mkuu wa jela na askari kumi wasingetosha kuning’oa kwenye vitabu vile. Hata Elijah Muhammad asingeweza kueleza mambo kama vile vitabu, vilikuwa ushahidi kuwa mtu mweupe ametenda kama shetani karibu kila mara alipokutana na watu ambao si weupe. Leo hii nasikiliza kwenye redio, naona kwenye luninga na nasoma kwenye magazeti jinsi ambavyo mzungu ana wasiwasi juu ya China. Mzungu anapojidai hajui kwa nini China inamchukia akili yangu hukumbuka niliyosoma wakati nipo grezani. Nilisoma jinsi ambavyo mababu wakatili wa mzungu huyu walivyoibaka China isiyokuwa na hatia. Wazungu hao wa mwanzo waliojiita “Wafanyabiashara wakristo” walipeleka China mamilioni ya kilo za kasumba(Opium). Kufikia mwaka 1839 Wachina wengi walikuwa mateja kiasi kwamba serikali ya China ili kuukomesha hilo ikaharibu makasha elfu ishirini na nne ya kasumba. Kitendo hicho kikasababisha wazungu kutangaza vita ya kwanza ya opium. Hebu fikiria! Kumtangazia vita mtu aliyekataa madawa ya kulevya! Wachina walipigwa vibaya sana—kwa kutumia unga wa risasi waliogundua wao wenyewe.

Baada ya vita, mkataba wa Nanking ukaitaka serikali ya China kuilipa ile ya Uingereza kwa uharibifu wa kasumba uliotokea; ukawalazimisha wachina kufungua bandari zao kwa meli za kibiashara za Uingereza; kuilazimisha serikali ya China kuondoka Hong Kong; kushusha ushuru wa forodha kiasi kwamba biashara za bei chee kutoka Uingereza zikafurika sokoni na kulemaza ukuaji wa China kiviwanda.

Baada ya vita ya pili ya Opium, ukasainiwa mkataba wa Tientsin, mkataba huo ulihalalisha biashara ovu ya kasumba, ukahalalisha utawala wa Uingereza-Marekani na Ufaransa kwenye mambo ya forodha ya China. China ilijaribu kuchelewesha utiaji sahihi wa mkataba huo, jambo hilo lililosababisha mji wa Peking kuporwa na kuchomwa moto.

“Auawe shetani mweupe!” zilikuwa ndizo kelele walizopiga Wachina wakati wa uasi wa Boxer wa mwaka 1901. Wachina walishindwa vita tena na kufukuzwa kutoka maeneo bora ya Peking kisha kwa majivuno na kiburi, mzungu akatundika lile bango maarufu, “Wachina na mbwa hawatakiwi kuingia.”

Baada ya vita ya pili ya dunia, Uchina ya kikomunisti iliyafungia milango mataifa ya magharibi. Juhudi kubwa za kilimo, kisayansi na kiviwanda za watu wa China zimeelezwa vyema kwenye kitabu kilichochapishwa hivi karibuni na jarida la Life. Baadhi ya watu ndani ya China wamesema kuwa hawajawahi kuona kampeni kubwa ya kuhamasisha chuki dhidi ya watu weupe kama inayoendelea ndani ya Uchina. Kasi ya ongezeko la watu ndani ya China ni kubwa sana. Ndani ya miaka hamsini ijayo Uchina itakuwa na nusu ya watu wote duniani. Na inaonekana kuwa baadhi ya “kuku” wa China watarudi nyumbani kulala(China italipa ubaya waliotendewa), hasa ukitilia maanani mafanikio yao ya karibuni kwenye kuunda bomu la nyuklia.

Tuwe wakweli. Sote tunaona jinsi vikundi vikijiunda ndani ya Umoja wa Mataifa kwa kufuata rangiu za watu vikundi ya mataifa yasiyo ya kizungu. Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Adlai Stevenson amelalamika hivi karibuni kwamba ndani ya Umoja wa Mataifa kuna “mchezo wa rangi ya ngozi unaendelea.” Lakini balozi Stevenson anakuwa kama Jesse James, jambazi maarufu wa enzi hizo-alalamike kuwa askari amebeba bunduki. Ni nani duniani amewahi kucheza mchezo wa rangi vibaya zaidi ya mtu mweupe?

***​
 
Bwana Muhammad ambaye niliendelea kumuandikia kila siku, hakujua chochote juu ya dunia mpya iliyonifungukia kutokana na bidii yangu ya kuchunguza zaidi mafundisho yake vitabuni.

Nilipokuja kukutana na somo la falsafa nilijaribu kugusa kila kulihusu. Polepole nikajikuta nimesoma wanafalsafa wote, wamagharibi na mashariki. Nilikuja kuwapenda zaidi wanafalsafa wa mashariki na baadaye nikaja kuona kama wanafalsafa wengi wa magharibi wameiga kutoka kwa wale wa mashariki. Mfano Socrates alisafiri huko Misri. Na wengine hata imesemwa kuwa Socrates alipata baadhi ya mafunzo ya Wamisri. Hakuna shaka kuwa Socrates alipata sehemu ya hekima yake kutoka kwa watu wenye hekima wa mashariki.

Mara nyingi nimefikiria jinsi usomaji ulivyonifungulia njia mpya. Hata nikiwa bado gerezani nilitambua kuwa usomaji umebadili kabisa maisha yangu. Leo naona kuwa usomaji ule uliamsha njaa ya kuwa na maarifa iliyokuwa imelala ndani yangu. Sikuwa natafuta shahada kama ambavyo vyuo huwatunuku wanafunzi wake kama heshima. Elimu niliyokuwa najipatia ilinifanya niguswe zaidi na ukiziwi, ujinga na ukipofu uliowajaa watu weusi wa Marekani. Muda si mrefu uliopita kuna muandishi wa Uingereza alinipigia simu kutoka London. Moja ya swali aliloniuliza ni “Umesoma chuo gani?” nilimjibu, “Vitabu.” Huwezi kunikuta nikiwa nimekaa tu kwa robo saa bila kitabu, nikisoma kitu fulani ambacho najua kitamsaidia mtu mweusi.

Jana nilihutubia huko Lodnon, Uingereza. Na katika safari yangu ya kwenda na kurudi nilikuwa nasoma kuhusu lengo la Umoja wa Mataifa kuhakikisha upatikanaji wa haki za binadamu kwa jamii za wachache duniani. Ukandamizaji wa watu weusi wa Marekani ndiyo ukandamizaji wa wachache wa aibu zaidi duniani. Kinachomfanya mtu mweusi wa Marekani afikiri kuwa tatizo lake ni la ndani tu ya Marekani ni haya maneno, “haki za kiraia.” Mtu mweusi atapataje “haki za kiraia” kabla hajapata haki za binadamu? Kama mtu mweusi akianza kufikiri juu ya haki zake kama binadamu, na kisha akaanza kufikiri kuwa naye ni sehemu ya watu wa dunia hii; ataona kuwa anaweza kupeleka kesi yake Umoja wa Mataifa.

Sioni kesi inayofaa zaidi ya hii. Kwa miaka mia nne, jasho na damu ya watu weusi vimewekezwa kwenye nchi hii, lakini bado mzungu anamfanya mtu mweusi abembeleze ampatie haki ambazo mhamiaji anayeshuka melini leo hii anazipata ndani ya dakika chache tu.

Natoka kwenye mada—nilimwambia muandishi yule wa Uingereza kuwa chuo nilichosomea ni vitabu, maktaba. Kila mara ninaposafiri kwa ndege huwa nakuwa na kitabu ninachotaka kusoma, na siku hizi nataka kusoma vitabu vingi sana. Kama isingekuwa kila siku kutoka kupambana na mzungu, ningetumia maisha yangu yote yaliyobaki kwa kujisomea-ili tu kukidhi udadisi wangu maana nina udadisi juu ya karibu kila kitu. Sidhani kama kuna mtu alifaidika kwa kwenda gerezani zaidi yangu. Kufungwa kulinifanya nielimike zaidi sana kuliko ambavyo maisha yangu yangekuwa tofauti na labda kupita chuo. Nawaza kuwa shida kubwa ya vyuo ni uwepo wa vikengeushaji vingi sana. Ni mahali gani pengine zaidi ya gerezani ambako ningeweza kupambana na ujinga wangu kwa kusoma kwa kina, wakati mwingine hata kwa saa kumi na tano kwa siku?

Schopenhauer, Kant, Nietzsche—niliwasoma wote. Siwaheshimu, nataka tu kukumbuka wale ambao nilisoma nadharia zao miaka ile. Inasemwa kuwa watatu hawa ndiyo waliojenga misingi ambayo juu yake falsafa za Unazi na Ufashisti vilijengwa. Siwaheshimu kwa sababu kwa mtazamo wangu inaonekana walitumia muda mwingu kubishania vitu ambavyo si muhimu. Wananikumbusha wasomi wengi weusi niliowahi kukutana nao—mara zote huongelea kitu fulani kisicho na maana. Nilivutiwa kwa muda fulani na Spinoza baada ya kugundua kuwa ni mtu mweusi, Myahudi mweusi. Wayahudi walimtenga kwa sababu ya mawazo yake “Mungu mmoja kwa watu wote” Wayahudi walimfanyia Spinoza ibada ya mazishi, wakimaanisha kuwa kwao Spinoza alikuwa amekufa; nafikiri familia yake ilifukuzwa Uhispania na kukimbilia Uholanzi.

Nikuambie kitu kimoja. Falsafa zote hizo za magharibi zimefika ukingoni. Mzungu amejidanganya na kumdanganya mtu mweusi hadi amejifunga mwenyewe. Amefanya hivyo ili kuficha mchango halisi wa mtu mweusi katika historia.

Na leo hii mzungu anakabiliwa uso kwa uso na yale yanayoendelea kwenye bara la watu weusi, Afrika. Angalia vitu vya kale vinavyogunduliwa kule, vinatoa ushahidi tena na tena jinsi mtu mweusi alivyokuwa ameendelea kabla hata ya mzungu kutoka kwenye mapango ya Ulaya. Kusini ya jangwa la Sahara, mahali ambako mababu wengi wa watu weusi wa Marekani walikamatwa kumechimbuliwa vitu vingi vizuri ambavyo havijawahi kuonekana na binadamu wa kisasa. Baadhi ya vitu hivyo vinaonyeshwa kwenye maeneo kama jumba la makumbusho ya sanaa la jiji la New York. Vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu kwa namna isiyo na mfano. Vitu vya kale vilivyotengenezwa na watu weusi . . . na kupambwa kwa namna ambayo hakuna binadamu leo hii anaweza kufanya.

Historia imechakachuliwa na mzungu kiasi kwamba hata maprofesa weusi hawajui chochote kumshinda mtu mweusi mjinga juu ya vipaji, ustaarabu na utamaduni aliokuwa nao mtu mweusi miaka elfu moja iliyopita. Nimefanya mihadhara kwenye baadhi ya vyuo vya watu weusi, na baadhi ya hawa watu weusi waliochotwa akili na Phd zao walikimbilia kwenye magazeti ya kizungu na kuniita “Mnazi mweusi.” Kama ningekuwa rais wa moja ya hivi vyuo vya watu weusi, ningeviuza ikibidi ili niweze kupeleka baadhi ya wanafunzi weusi huko Afrika kwenda kuchimbua ushahidi zaidi juu ya ukuu wa watu weusi katika historia. Wazungu leo hii wako Afrika wanachimbua. Tembo wa Afrika hawezi tembea bila kujikwaa kwa mzungu mwenye sepetu. Karibu kila juma tunasoma juu ya uvumbuzi mkubwa kutoka ustaarabu wa kale wa Afrika. Kilichobadilika ni mtazamo tu wa sayansi ya mzungu. ustaarabu wa kale wa mtu mweusi umekuwepo chini ya ardhi ya Afrika siku zote.

Huu ni mfano mmojawapo: mwanaanthropolojia wa kiingereza aitwaye Dr. Louis S. B. Leakey anaonyesha mabaki ya mtu wakale, mgu, taya, mifupa ya mikono na ya fuvu. Dr Leakey anasema kutokana na uvumbuzi huo inatubidi kuandika upya historia juu ya mwanzo wa binadamu.

Mabaki hayo ni ya binadamu aliyeishi miaka 1,818, 036 kabla ya kuzaliwa Kristo. Yamepatikana huko Tanganyika barani Afrika.

Uongo ulioambiwa vizazi vya watu weusi na wazungu ni uhalifu mkubwa. Watoto wadogo weusi wanazaliwa na wazazi wanaoamini kwamba jamii yao haina historia. Kabla hata hawajaanza kuongea wanaona kwamba wazazi wao wanajiona wenyewe kuwa ni duni. Wanakua, wanaishi na kufa uzeeni wakionea aibu weusi wao. Lakini sasa ukweli unatoka sandukuni.

Kuna vitu vingine viwili maishani mwangu vilivyonibadilisha sana kwenye gereza la Norfolk. Kwanza nilianza kufungua macho ya ndugu zangu weusi waliochotwa akili waelewe ukweli kuhusu mtu mweusi. Na kingine ni kuwa baada ya kuwa nimesoma vya kutosha nikaanza kuhudhuria mijadala iliyofanyika kila juma pale Gerezani—huo ulikuwa kama ubatizo wangu wa kuongea na umma.

Naomba nikiri jambo moja la aibu. Nilikuwa napendelea sana kuwa karibu na wazungu kiasi kwamba sikupendezwa kuona wafungwa weusi wakiwa pamoja-pamoja namna ile. Lakini toka mafundisho ya bwana Muhammad yalipobadili mtazamo wangu kuelekea ndugu zangu, aibu na majuto yaliyonikuta yakanifanya kuwafundisha ndugu zangu mafundisho ya bwana Muhammad kila nilipopata nafasi.

Unatakiwa kuwa makini sana unapomwambia mtu mweusi ukweli ambao hajawahi kuusikia maisha yake yote, ukweli kujihusu, kuhusu watu wa jamii yake na kuhusu mtu mweupe. Ndugu yangu Reginald aliniambia kuwa hilo huwapata Waislamu wote wanapokuwa wanahubiri mafundisho ya Elijah Muhammad. Mtu mweusi amechotwa sana akili kiasi kwamba anaweza kukasirika anaposikia ukweli kwa mara ya kwanza. Reginald alishauri kwamba ukweli unatakiwa kutolewa kidogokidogo. Na inatakiwa kungoja kwa muda kidogo uingie kabla ya kwenda hatua inayofuata.

Kwanza nilianza kwa kuwasimulia ndugu zangu weusi juu ya historia iliyotukuka ya watu weusi-hawakuwahi wazia kabisa mambo niliyowasimulia. Niliwaambia ukweli ambao hawakuufahamu juu ya madhira ya biashara ya utumwa. Niliona sura zao zikibadilika nilipowaambia hilo, mzungu alikuwa amefuta kabisa historia ya watumwa. Mtu mweusi wa Marekani kamwe hawezi kufahamu jina halisi la ukoo wake wala kabila alilotokea; hajui kama ni Mmandingo, Mwolof, Mserer, Mfula, Mfanti, Mashanti nk. Niliwaambia kuwa baadhi ya watumwa walioletwa Marekani waliongea kiarabu na walikuwa Waislamu. Wafungwa wengi hawakuamini, walitaka mpaka wasikie mzungu akisema hayo. Basi mara kwa mara niliwasomea kutoka kwenye vitabu vya wazungu. Niliwaambia kuwa baadhi ya wazungu wasomi walifahamu ukweli lakini kumekuwa na njama ya kuficha ukweli huo usiwafikie watu weusi.

Nilichunguza vyema kila mmoja alivyoitikia. Nilitakiwa kuwa makini sana. sikujua ni wakati gani mmoja wa watu weusi aliyechotwa akili atakubaliana nami na kisha kwenda kuwaambia wazungu niliyosema. Iwapo niliona mmoja wao yupo tayari kupokea ukweli, nilimwambia juu ya mafundisho ya bwana Muhammad, yakuwa; “Mzungu ni shetani.” Mwanzoni hilo liliwashtua wengi wao mpaka pale walipoanza kulitafakari kwa kina.

Pengine hili ndilo jambo linalouhangaisha sana mfumo wa magereza ya Marekani leo-jinsi mafundisho ya kiislamu yanavyowasilimisha wanaume wengi weusi waliofungwa magerezani. Na wanaume weusi ni wengi sana magerezani ukilinganisha na uwiano wa idadi yao uraiani. Na sababu hasa ni kuwa kati ya watu weusi wote, mfungwa mweusi ndiyo yupo tayari zaidi kusikiliza maneno, “Mzungu ni shetani.”

Mwambie hivyo mtu mweusi yeyote na utakuwa umemgusa penyewe. Kasoro labda wachache wanaohusudu uchangamano, wa kujiita wasomi na wale walionawiri, wenye furaha-wakiwa wamefanywa viziwi, vipofu na mbumbumbu kutokana na makombo wanayopata kutoka kwenye meza ya mzungu. Anaweza kuchukua siku kadhaa, mwezi au hata mwaka; anaweza asionyeshe waziwazi lakini uwe na hakika kuwa atakapokuwa anatafakari maisha yake atajionea jinsi ambavyo mzungu amemtendea kishetani.

Kama nilivyosema, kati ya wote, mfungwa mweusi ndiye atakayeitikia zaidi. Hapa kuna mfungwa mweusi amefungwa nyuma ya nondo na mzungu, pengine yupo hapo kwa miaka kadhaa. Na mara nyingi wafungwa hutoka miongoni mwa watu weusi wa daraja la chini kabisa, watu ambao maisha yao yote wamekandamizwa na kutendewa kama watoto—watu ambao hawajawahi kutana na mzungu ambaye kama hatachukua kitu kutoka kwao basi atawafanyia kitu fulani kiovu.

Ukimuacha mtu mweusi huyu aliyefungwa aanze kufikiri kama nilivyofikiri baada ya kusikia mafundisho ya Elijah Muhammad kwa mara ya kwanza; ukimuacha afikiri jinsi ambavyo angeweza kuwa mwanasheria, daktari, mwanasayansi nk. Kumuacha atambue, kama nilivyotambua kwamba toka meli ya kwanza ya watumwa itie nanga Marekani, mamilioni ya watu weusi wamekuwa kama kondoo kwenye makazi ya mbwa mwitu-mambo hayo ndiyo yanafanya wafungwa weusi Kusilimu haraka mara tu wanapopata mafundisho ya Elijah Muhammad kutoka kwa wafungwa waislamu wengine. “Mzungu ni shetani.” Ni maneno muafaka kabisa kuelezea mambo yote aliyopitia maishani mwake.

Nimesema jinsi ambavyo kulikuwa na majadiliano kila juma gerezani pale. Basi kujisomea kukawa kumefanya kichwa changu kuwa moto sana. Niliona nina wajibu wa kuwaambia wazungu “Ukweli” kuwahusu waziwazi. Nikaonelea njia nzuri ya kufanya hivyo ni kujiandikisha kwenye mijadala.

Maisha yangu yote sikuwahi kuwaza kuwa nitakuja kusimama mbele za watu na kutoa hotuba. Nilipokuwa mtaani nikipambana, kuuza madawa na kupora, nilikuwa naota ndoto nyingi baada kutumia bangi, lakini sikuwahi kuota ndoto ya ajabu kuwa nitatoa hotuba kwenye kumbi, kwenye vyuo vikubwa vya Marekani. Kwenye luninga na redioni, bila kusahau huko Misri, Afrika na Uingereza.

Lakini nikuambie kitu, kuongea kwenye mijadala gerezani pale kilikuwa kitu cha kusisimua kwangu kama tu ilivyokuwa kugundua maarifa kupitia kujisomea kulivyonifanya nijihisi. Nikiwa nimesimama pale, umati ukiniangalia, mawazo yangu yakishuka kutoka kichwani mwangu na kupita mdomoni. Kama niliweza kuwashawishi kuwa wakubaliane nami basi nilishinda mjadala. Nilipopewa mada ya mjadala, nilienda na kusoma kila kitu kuihusu. Nilijiweka kwenye nafasi ya mpinzani na kuangalia mbinu ambazo anaweza kutumia ili kushinda; kisha nikatafuta mbinu za kuzishinda hoja hizo.

“Je, kuna ulazima wa mafunzo ya kijeshi kwa raia au hakuna?” Mada hiyo ilinipa nafasi ambayo sikuitarajia. Nakumbuka mpinzani wangu alichafua hewa kwa kusema kuwa Waethiopia walikuwa wakizirushia mawe na mikuki ndege vita za Waitaliano. Akisema huo ni ushahidi kuwa mafunzo ya kijeshi kwa raia ni lazima.

Nilisema kuwa watu weusi wa Ethiopia walikuwa wakisambaratishwa na mabomu yaliyobarikiwa na Papa kule Roma na kuwa Waethiopia wangeweza wangerusha hata miili yao maana waliona wazi kuwa wanapambana na shetani aliyejivika mwili.

Walipiga kelele, “Faulo” kwamba nimeibadili mada kuwa juu ya rangi za watu. Niliwaambia sivyo hata kidogo. Ni ukweli ulio wazi, na kama wanataka kujionea waende kusoma kitabu Days of Our Years chake Pierre Van Paassen. Na mara tu baada ya mjadala ule kitabu kile kikatoweka maktaba. Lakini hilo halikunishangaza. Ni gerezani pale ndipo niliamua kuwa nitatumia maisha yangu kuwaambia wazungu ukweli wao au kufa. Kwenye mjadala uliohusu iwapo Homer aliishi kweli au la, niliwaambia waziwazi wazungu wale kuwa nadharia ya kwamba Homer ni ushahidi jinsi ambavyo wazungu waliteka watu weusi na kuwapofua macho ili washindwe kurudi kwa watu wao. (Homer, Omar na Moor ni majina yanayofanana; ni kama kusema Peter, Pedro na Petra—yote matatu yanamaanisha jiwe). Wazungu waliwafundisha Moors hawa waliopofushwa macho kuimba juu ya ukuu na mafanikio ya wazungu. Niliwaambia waziwazi kuwa ni namna ya kishetani ya mzungu kujiburudisha. Hadithi za Esopo ni mfano mwingine. Esopo lilikuwa tu ni jina ambalo Wagiriki walimwita Muethiopia.

Mjadala mwingine mkali nilioshiriki ulikuwa ni juu ya utambulisho wa Shakespeare. Haukuwa ubishi juu ya rangi; nilikuwa tu nimevutiwa na utata uliomzunguka Shakespeare. Tafsiri ya biblia ya King James ndiyo inachukuliwa kuwa kazi bora kabisa katika maandiko ya Kiingereza. Lakini mtindo wa lugha aliotumia Shakespeare na uliotumika kuandika tafsiri ya King James ni uleule. Wanasema kuwa kutoka mwaka 1604 hadi mwaka 1611, Mfalme James aliwatumia washairi kufasiri biblia na kuiandika. Basi kama Shakespeare alikuwepo wakati huo basi alikuwa ni mshairi wa daraja la juu kabisa. Lakini hakuna popote ambapo Shakespeare anahusishwa na biblia. Kama alikuwepo, kwa nini Mfalme James hakumtumia? Na kama alimtumia kwa nini imefanywa siri?

Nafahamu wengi husema kuwa Francis Bacon ndiye Shakespeare. Kama ni kweli, kwa nini Bacon alifanya siri? Bacon hakuwa mzaliwa wa kifalme, wakati huo watu wenye nasaba za kifalme walitumia majina bandia kwa sababu haukufaa kwa wao kufanya kazi za sanaa. Bacon angepoteza nini? Ukweli ni kuwa angefaidika sana kwa kujiweka wazi.

Kwenye mjadala huu nilisema kuwa Mfalme James mwenyewe ndiye aliyekuwa Shakespeare. Mfalme James alikuwa na akili sana. Ni mfalme bora kabisa kuwahi kukalia kiti cha kifalme cha Uingereza. Nani mwingine kwenye familia ya kifalme wakati ule alikuwa na kipaji cha kuweza kuandika kazi za Shakespeare? Ni yeye ndiye aliyetafsiri Biblia kishairi, Biblia ambayo yenyewe kama yenyewe na tafsiri yake ya King James vimefanya watu wa dunia kuwa watumwa.

***​
 
Sura ya 11 inaendelea.

Reginald aliponitembelea, nilimueleza juu ya ushahidi mpya niliopata, ushahidi unaounga mkono mafundisho ya Kiislamu. Nilisoma Paradise Lost chake Milton. Kinasimulia jinsi Shetani alivyokuwa anajaribu kurudi baada ya kufukuzwa mbinguni. Alikuwa akitumia majeshi na nguvu za Ulaya zilizojivika miili kama Mapapa, Charlemagne, Richard the Lionheart na mashujaa wengine. Nilifafanua kuwa wazungu wanaongozwa na Shetani mwenyewe au akiwa amejivika mwili. Hivyo Milton na Elijah Muhammad walikuwa wanazungumza kitu kimoja.

Sikuamini nilipomsikia Reginald akimuongelea vibaya Elijah Muhammad. Sikumbuki ni mambo gani hasa alisema, zilikuwa shutuma dhidi ya Elijah Muhammad na zilionyeshwa hasa na jinsi alivyosema na uso wake ulivyokuwa kuliko aliyosema.

Sikujiandaa kabisa na kitu kama hicho. Nilichanganyikiwa kabisa. Ndugu yangu niliyemuamini na kumheshimu, aliyenitambulisha kwa Taifa la Kiislamu! Sikuamini! Wakati huo Uislamu ndiyo ulikuwa kitu cha maana kuliko vyote vilivyowahi kutokea maishani mwangu. Uislamu na Elijah Muhammad walikuwa wamebadili kabisa maisha yangu.

Baadaye nilikuja kufahamu kuwa Reginald alikuwa amesimamishwa kushirikiana na Taifa la Kiislamu na bwana Muhammad. Alikuwa hafuati maadili. Aliendelea kuwa na uhusiano haramu na katibu wa Hekalu la New York hata baada ya kuukubali Uislamu na sheria zake. Baadhi ya Waislamu baada ya kugundua hilo walimshtaki kwa bwana Elijah Muhammad huko Chicago naye akamsimamisha.

Kuondoka kwa Reginald kulinitaabisha sana. Nilimuandikia bwana Muhammad kujaribu kumtetea ndugu yangu. Nilimueleza jinsi ndugu yangu huyo alivyo muhimu kwangu. Niliituma barua hiyo na kisha usiku wote huo nilisali kwa Allah. Sidhani kama kuna mtu amewahi Sali kwa Allah kutoka moyoni kama nilivyosali. Nilisali ili mkanganyiko ulionikabili uondoke.

Usiku uliofuata, nikiwa nimelala kitandani, nilishtuka kuona mtu amekaa kitini pembeni yangu. Nakumbuka alikuwa amevaa suti nyeusi. Alikuwa mtu halisi. Hakuwa mzungu wala mweusi. Alikuwa na rangi ya maji ya kunde iliyoelekea weupe, na alikuwa na nywele nyeusi zilizong’aa.

Nilimuangalia kwa kumkazia macho usoni.

Sikuogopa. Nilifahamu vyema sikuwa naota. Sikuweza kuinuka wala sikuongea, naye pia hakuongea. Sijui alikuwa wa jamii gani hasa ila tu hakuwa mzungu. Hadi leo sifahamu alikuwa nani. Alikaa tuli pale kisha akatoweka ghafla kama alivyokuja.

Baada ya muda mfupi bwana Muhammad alinitumia majibu ya barua yangu kuhusu Reginald. “Kama uliamini kweli na sasa unaitilia shaka basi hukuamini tokea mwanzo. Jambo gani linaweza kukufanya utilie shaka kweli zaidi ya udhaifu wako mwenyewe?”

Hilo lilinigusa sana. Reginald hakuwa akiendesha maisha yake kama Muislamu. Na nilifahamu vyema kuwa Elijah Muhammad alikuwa sahihi na ndugu yangu wa damu alikuwa na makosa. Ukweli ni ukweli. Masikini wakati huo sikujua kuwa siku moja Elijah Muhammad atakuja kushutumiwa na wana wake mwenyewe shutuma zilezile zilizomfanya amhukumu Reginald.

Lakini wakati huo kuchanganyikiwa na mashaka yangu yote yalitoweka. Ushawishi wote ambao ndugu yangu alikuwa nao kwangu ulitoweka. Kuanzia siku hiyo nilichukulia kila jambo alilofanya ndugu yangu Reginald kuwa ni makosa.

Lakini Reginald aliendelea kunitembelea. Alipokuwa Muislamu alivalia nadhifu sana, lakini sasa alivaa hovyo, vitu kama tisheti, suruali za ajabu na raba. Niliona wazi akipotea. Nilimsikiliza alivyokuwa akiongea, bado alikuwa ni ndugu yangu wa damu—lakini sikuwa na uchangamfu ule wa mwanzo. Niliona Adhabu ya Allah-akishukiwa na kile Wakristo wanaita laana. Elijah Muhammad alisema kuwa Allah alikuwa akimuadhibu Reginald, na kuwa yeyote atakayempinga Elijah Muhammad ataadhibiwa na Allah. Kwenye Uislamu tulifundishwa kuwa yeyote asiyeijua kweli anaishi gizani. Na anapoitambua kweli na kuikubali, huishi kwenye mwanga, na yeyote atakayeenda kinyume na kweli baada ya kuijua ataadhibiwa na Allah.

Bwana Muhammad alifundisha kuwa nyota yenye pembe tano inawakilisha haki na pia milango mitano ya fahamu ya binadamu. Tulifundishwa kuwa Allah anatekeleza adhabu zake kwa kuadhibu hisi tano za yule aliyemuasi Mtume wake au anayeenda kinyume na kweli yake. Tulifundishwa kuwa hii ndiyo njia ya Allah kuwafanya Waislamu wafahamu uwezo wake wa kumlinda Mtume wake dhidi ya wote wanaompinga inachotakiwa ni Mtume huyo hatakengeuka kutoka katika njia ya kweli. Tulifundishwa kuwa Allah hugeuza na kuvuruga akili za waasi. Niliamini kuwa Allah ndiye aliyekuwa akimfanya ndugu yangu awe vile.

Barua moja, nafikiri kutoka kwa kaka yangu Philbert, ilinijulisha kuwa Riginald alikuwa nao huko Detroit. Sikusikia tena kumhusu Reginald mpaka siku moja, juma moja baadaye Ella aliponitembelea. Aliniambia kuwa amemuacha Reginald nyumbani kwake Roxbury amelala. Aliniambia kuwa alisikia mlango ukigongwa, alipoenda kufungua alikuwa ni Reginald akiwa katika hali mbaya. Alimuuliza, “umetoka wapi?” na Reginald alimjibu kuwa ametoka Detroit. Akamuuliza tena, “Umefikaje hapa?” Naye akajibu, “Nimetembea.”

Niliamini kuwa alikuwa ametembea. Nilimuamini Elijah Muhammad aliposema kuwa adhabu ya Allah kwenye akili ya Reginald kumeondoa uwezo wake wa kukadiria umbali na muda. Elijah Muhammad alisema chini ya Allah, milango mitano ya fahamu ya mtu inaweza changanywa kiasi kwamba ndani ya dakika tano nywele zake zinaweza geuzwa kuwa nyeupe kama theluji, au anaweza kutembea umbali wa maili mia tisa kama vile anavyotembea kupita mitaa mitano.

Tokea niwe Muislamu, nilianza kufuga ndevu pale gerezani. Reginald aliponitembelea hakuwa na amani kabisa kitini alipoketi. Aliniambia kuwa kila ndevu kidevuni kwangu ni nyoka. Aliona nyoka kila mahali.

Baadaye akaanza kuamini kuwa yeye ni “Mtume wa Allah.” Ella alinisimulia kuwa Reginald alikuwa akipita mitaa ya Roxbury na kuwaambia watu kuwa ana nguvu za kimungu. Baadaye akafuzu kutoka hapo na kuanza kusema yeye ni Allah.

Mwishowe akaanza kusema yeye ni mkuu kuliko Allah.

Watu wa serikali walimkamata na kumpeleka kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili. Hawakuweza kufahamu kinachomsumbua. Hawakuwa na namna ya kuelewa adhabu ya Allah. Aliachiliwa lakini alikamatwa tena na kupelekwa hospitali nyingine.

Kwa sasa Reginald yupo katika hospitali ya wagonjwa wa akili. Nafahamu aliko lakina sitasema ni wapi. Sitaki kumsababishia matatizo zaidi ya yaliyompata.

Leo hii naamini kwamba iliandikwa, iliandikwa kwa Reginald kutumika kwa lengo moja tu: kutumika kama chambo ya kunifikia kwenye kina chenye giza cha bahari nilikokuwa ili kuniokoa. Sina namna nyingine ya kumuelezea.

Baada ya Elijah Muhammad mwenyewe kushutumiwa kwa ukosefu wa maadili, nikaanza kuamini kuwa haikuwa adhabu ya Mungu iliyompata Reginald, bali ni uchungu uliompata baada ya familia yake yote kumkataa sababu ya Elijah Muhammad. Na uchungu huo ukamfanya Reginald kurukwa na akili.

Huwezi kumuota wala kuwa na maono ya mtu ambaye hujawahi kumuona. Kumuona kama alivyo ni suala la utabiri. Baadaye nilikuja kuamini kuwa maono yangu yalikuwa ya kinabii kumhusu bwana W. D. Fard, Mesia, mtu ambaye Elijah Muhammad alisema kuwa alimchagua yeye Elijah Muhammad kama mtume wake wa mwisho kwa watu weusi wa Amerika ya Kaskazini.

***

Mwaka wangu wa mwisho gerezani nilitumikia kwenye gereza la Charlestown. Pale kwenye gereza la Norfolk habari zangu zilikuwa zimewafikia hadi wafungwa wa kizungu. Baadhi ya wale wafungwa weusi waliochotwa akili walikuwa wakiongea sana. Nami pia nilifahamu vema kuwa wale waliokuwa wakichunguza barua za wafungwa walitoa taarifa zangu na hilo liliwafanya maofisa wa gereza la Norfolk kukereka. Walitumia kisingizio cha kwamba nimekataa kuchomwa chanjo kama sababu ya kunihamisha.

Kitu pekee kilichonitia wasiwasi ilikuwa ni kwamba nilikuwa na muda mchache sana kabla sijakidhi vigezo vya kuachiwa kabla ya muda kufika. Lakini niliwaza kuwa wataangalia kuhubiri kwangu Uislamu na kuamua kuwa ni bora kuniachia huru.

Niliingia gerezani nikiwa naona vizuri kabisa. Lakini waliponirudisha gereza la Charlestown, nilikuwa nimesoma sana kwenye mwanga hafifu kiasi kwamba nikawa na tatizo la mcho na hivyo nikaanza kuvaa miwani.

Kwenye gereza la Charlestown uhuru wangu ulipungua, lakini niligundua kuwa wafungwa wengi weusi huudhuria somo la biblia hivyo nami nikajiunga.

Aliyekuwa akifundisha alikuwa ni mwanafunzi wa seminari kutoka Harvard. Alikuwa kijana wa kizungu, mrefu, macho ya bluu na nywele za rangi ya dhahabu(“shetani” hasa). Alifundisha na baadaye aliruhusu kipindi cha maswali na majibu. Sijui kati yangu na yeye nani alikuwa ameisoma sana Biblia lakini nimpe sifa kuwa aliijua dini yake vizuri. Nilitafakari sana njia ya kumkwaza na kuwapa watu weusi wale kitu cha kuzungumzia.

Mwishowe nilinyoosha mkono naye aliniruhusu; alikuwa amemzungumzia Paulo.

Nilisimama na kuuliza, “Paulo alikuwa na rangi gani?” Nikaendelea kuongea kwa vituo, “Bila shaka alikuwa mweusi . . . Maana alikuwa ni Mwebrania . . . Na Waebrania wa asili walikuwa weusi . . . sivyo?”

Alianza kuwa mwekundu. Unajua vile wazungu huwa. Alisema, “Ndiyo.” Sikuishia hapo, “Yesu alikuwa na rangi gani . . . Naye alikuwa Muebrania pia . . . sivyo?”

Wafungwa wote, wazungu na weusi waliketi wima kama milingoti. Haijalishi mfungwa ni mbabe kiasi gani, we ni Mkristo mweusi aliyeshikwa akili au “shetani” mzungu Mkristo, wote hawako tayari kusikia kuwa Yesu hakuwa mzungu. Mkufunzi yule alitembea huku na kule. Hakuwa na haja ya kuhangaika. Kwa miaka mingi tokea pale sijawahi kutana na mzungu yeyote mwenye akili aliyejaribu kusisitiza kuwa Yesu alikuwa ni mzungu—Wangewezaje? Alisema, “Yesu alikuwa wa kahawia.”

Niliacha tukubaliane kwa hilo.

Kama nilivyotarajia, mara moja wafungwa wa Charlestown, wazungu na weusi wakaanza kuzumgumzia kisa hicho. Kila nilikoenda niliweza kuona macho yakinitazama. Na kila wakati nilipopata nafasi ya kuongea na mfungwa mweusi nilisema, “Mtu wangu, umewahi kusikia kuhusu mtu anayeitwa Elijah Muhammad?”

Mwisho wa sura ya 11​
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…