SURA YA KUMI
SHETANI
Mama yake Shorty alifanikiwa kujichanga na kupata nauli ya basi kutoka Lansing hadi Boston. “Mwanangu naomba unisomee kitabu cha ufunuo na usali!” ndivyo alivyokuwa akimwambia Shorty kila alipomtembelea mahabusu. Kuna siku alinitembelea nami pia. Shorty alisoma kitabu hicho na hata alipiga magoti na kusali kama vile shemasi mweusi wa kibapstisti.
Siku ya hukumu tulikuwa mbele ya hakimu kwenye mahakama ya wilaya ya Middlesex(Nadhani kumi na nne ya makosa yetu yalifanyika kwenye wilaya hiyo) Mama yake Shorty alikuwa amekaa kichwa ameinamisha huku akilia na kusali kwa Yesu, pembeni yake alikuwepo Ella na Reginald. Shorty ndiye alikuwa wa kwanza kuitwa. Shorty hakufahamu maneno, “Kutumikiwa kwa pamoja,” yanamaanisha nini.
“Kosa la kwanza, miaka nane hadi kumi, kosa la pili, miaka nane hadi kumi, kosa la tatu, miaka nane hadi kumi . . . ” Na mwishowe, “Adhabu zote zitatumikiwa kwa pamoja.”
Jasho lilimvuja Shorty kiasi kwamba uso wake mweusi ulikuwa kama umepakwa mafuta mengi, na kwa vile hakujua “Kutumikiwa kwa pamoja,” kunamaanisha nini, atakuwa alipiga hesabu kichwani mwake na kuona kuwa atafungwa kwa zaidi ya miaka mia moja. Alianza kulia na kuishiwa nguvu, ilimbidi askari wa mahakamani amshikilie.
Ndani ya sekunde kumi Shorty akawa amegeuka kuwa asiyeamini Mungu kama tu nilivyokuwa.
Nilipata kifungo cha miaka kumi. Wasichana wetu walipata kifungo cha mwaka mmoja hadi mitano kwenye gereza la wanawake huko Framingham, Massachusetts.
Hii ilikuwa ni mwaka 1946, hata miaka ishirini na moja nilikuwa bado sijatimiza. Hata kunyoa ndevu nilikuwa bado sijaanza.
Tulichukuliwa na Shorty, tukapigwa pingu na kupelekwa gereza la Charlestown.
Sikumbuki namba yangu yoyote ya mfungwa. Hilo linanishangaza sababu namba yako ya gerezani inakuwa sehemu yako kubwa sana. Hutasikia ukiitwa kwa jina lako bali namba tu. Namba yako ilikuwa kila sehemu. Kwenye nguo zako, vyombo na kila kitu. Inakuwa ni kama imeandikwa kichwani mwako.
Mtu yeyote anayedai kupenda sana binadamu wenzake, anatakiwa kufikiri kwa kina sana kabla hajachagua kuunga mkono kitendo cha kufunga binadamu wengine nyuma ya nondo. Sisemi magereza yasiwepo, ninasema nondo ndizo zisiwepo. Mtu hawezi kubadilika tabia nyuma ya nondo. Kamwe hawezi kusahau nondo zile.Bbaada ya kutoka hujitahidi kufuta yaliyomtokea lakini hawezi kabisa. Nimeongea na wafungwa wa zamani wengi sana. Cha kushangaza ni kuwa karibu wote akili zetu zimesahau mambo mengi yaliyotokea katika miaka mingi tuliyokuwa gerezani. Lakini kila mmoja atakwambia kuwa kamwe huwezi kusahau zile nondo.
Nikiwa kama “samaki”(Jina la mfungwa mpya kwenye gereza la Charlestown.), nilikuwa na hali mbaya kimwili na mwenye hasira kama nyoka sababu ya kukosa madawa ghafla. Selo hazikuwa na maji. Jela ilikuwa imejengwa mwaka 1805-nyakati za Napoleon na hata mtindo wake ulikuwa kama wa gereza la Bastille. Ndani ya selo chafu na ndogo. Niliweza kulala kitandani na miguu na kichwa vikagusa kuta. Choo kilikuwa ni ndoo yenye mfuniko. Haijalishi una moyo wa namna gani lakini huwezi kuvumilia harufu ya kinyesi kutoka safu ya selo kadhaa.
Mwanasaikolojia w gereza alinisaili na aliishia kutukanwa matusi yote mabaya niliyoyajua, na kasisi wa gereza alitukanwa matusi mabaya zaidi. Nakumbuka barua ya kwanza kupokea ilikuwa ni kutoka Detroit kwa kaka yangu mshika dini, Philbert. Akiniambia kuwa kanisa lao “Tukufu” litaniombea. Nilimtumia barua ya majibu ambayo hata leo naona aibu ninapoifikiria.
Ella alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuja kunitembelea. Nakumbuka jinsi alivyojikaza kutabasamu, sasa nikiwa nimevaa
dungaree iliyopauka, namba yangu ikiwa imebandikwa juu yake. Hakuna aliyeweza kupata maneno mengi ya kuzungumza, kulikuwa na ukimya hadi nikatamani asingekuja kabisa. Askari wenye bunduki walikuwepo pale kusimamia karibu wafungwa na wageni hamsini. Nilisikia wafungwa kadhaa wapya wakiapa kuwa siku watakayofunguliwa kitu cha kwanza kufanya itakuwa ni kushughulika na wale askari wa kwenye chumba cha kukutana na wageni. Mara nyingi chuki iliwaangukia hao.
Mara ya kwanza kulewa pale gerezani ilikuwa kwa kutumia kungumanga. Mtu niliyekaa naye selo moja alikuwa mmoja wa watu wengi waliokuwa wakinunua kungumanga za wizi kutoka kwa wafungwa waliofanya kazi jikoni. Walinunua kwa kutumia pesa au sigara. Madawa hayo waliyaficha kwenye viboksi vya viberiti. Nilifakamia kiboksi kile kama vile ndani yake kulikuwa na madawa halisi. Ukichukua kiasi hicho cha kungumanga na kukikoroga na maji ya baridi kwenye kikombe na kunywa, unakuwa kama mtu aliyevuta misokoto mitatu au minne ya bangi.
Hatimaye kwa kutumia pesa alizonitumia Ella niliweza kununua madawa halisi kutoka kwa askari. Niliweza kununua bangi, Nembutal na Benzedrine. Kuwauzia wafungwa magendo ilikuwa ndiyo kazi nyingine ya askari. Kila mfungwa alifahamu kuwa askari jela waliendesha maisha yao hasa kwa njia hiyo.
Nilikaa gerezani kwa muda wa miaka saba. Lakini ule mwaka mmoja na kidogo niliokaa gereza la Charlestown ulijaa matumizi ya kungumanga, madawa mengine, kuwatukana askari, kutupa vitu nje ya selo yangu, kuangusha sinia langu la chakula kwenye ukumbi wa chakula, kugoma kujibu namba yangu ilipoitwa na kusema kuwa nimeisahau na vurugu zingine kama hizo.
Nilipenda kifungo cha kutengwa nilichopewa baada ya kufanya mambo hayo. Lakini kulikuwa na ukomo wa muda ambao mtu anaweza kuwekwa kwenye kifungo cha peke yake. Nilikuwa nikitembea chumbani huku na huko kama chui aliyefungwa bandani, nikijilaani vikali kwa sauti. Pia nilipenda kumlaani Mungu na Biblia. Baadaye watu wakanipachika jina la “Shetani” kutokana na kupinga kwangu dini huko.
Mtu wa kwanza aliyenivutia gerezani alikuwa ni mfungwa aliyeitwa “Bimbi” Nilikutana naye mnamo mwaka 1947 katika gereza la Charlestown. Alikuwa ana weupe kama mimi na hata urefu tulilingana, alikuwa na madoamadoa usoni. Bimbi alikuwa ni mwizi mzoefu na alikuwa ameishafungwa mara nyingi. Kundi letu lilikuwa linafanya kazi kwenye karakana ya kutengeneza vibao vya namba za magari. Kazi ya Bimbi ilikuwa ni kuendesha mashine ya kubandika namba. Mimi nilikuwa sehemu ambayo namba zilipakwa rangi.
Bimbi alikuwa ndiye mtu mweusi wa kwanza ambaye hakujibu alipoongeleshwa kwa lugha ya kihuni. Mara nyingi baada ya kumaliza kutengeneza idadi ya vibao tuliyopangiwa kwa siku, tulikusanyika pamoja kama kumi na au kumi na tano tukimsikiliza Bimbi. Kawaida wafungwa wa kizungu hawakuwaza hata kusikiliza mawazo ya wafungwa weusi, lakini kwa Bimbi ilikuwa tofauti, hata askari walisogea kusikiliza aliyoongea Bimbi.
Alifanya watu wavutiwe hata na mada za ajabu ambazo hukuwahi kuziwazia. Alituthibitishia kwa kutumia sayansi ya tabia ya binadamu kuwa tofauti pekee kati yetu na watu waliokuwa nje ni kuwa sisi tulikuwa tumekamatwa. Alipenda sana kuongelea watu na matukio ya kihistoria. Sikuwa mfungwa pekee ambaye alikuwa hajawahi kumsikia Thoreau mpaka pale Bimbi alipomuelezea. Bimbi alijulikana kama mhudhuriaji mzuri wa maktaba. Kilichonistaajabisha zaidi ni kuwa alikuwa mtu wa kwanza kumfahamu aliyefanya aheshimike kwa kuongea tu.
Ni mara chache sana Bimbi alizungumza name, hakuwa anazungumza sana na mtu mmoja mmoja, lakini nilihisi kuwa alinipenda. Kilichofanya nitake urafiki naye ni jinsi alivyoizungumzia dini. Nilijichukulia zaidi ya mtu asiyeamini Mungu, nilijiona Shetani kabisa. Lakini Bimbi aliielezea falsafa ya kutoamini Mungu kwa namna iliyonifanya niache kutukana dini. Alikuwa na hoja zenye nguvu kuliko mimi, na wala hakutumia matusi.
Siku moja bila kutarajia, Bimbi aliniambia bila kuuma maneno kuwa kama nilikuwa na kichwa kizuri sana kama ningekitumia. Nilitaka hasa kuwa rafiki yake na si ushauri wa aina ile. Nilikuwa nikitukana wafungwa wengine lakini hakuna mtu aliyethubutu kumtukana Bimbi. Aliniambia kuwa itanifaa nikijiunga na kozi zilizotolewa gerezani na kuhudhuria maktaba.
Mara yangu ya mwisho kufikiria kusoma kitu chochote kisichohusiana na upambanaji ilikuwa nilipomaliza darasa la nane kule Mason, Michigan. Na zaidi ni kuwa mitaa ilikuwa imefuta kila kitu nilichojifunza shuleni; sikuweza kutofauti kutofautisha kati ya kitenzi na nyumba! Dada yangu Hilda alikuwa amependekeza kuwa iwapo ninaweza basi nijifunze kiingereza na namna ya kuandika. Nilikuwa nimemtumia barua kipindi kile nauza bangi kwa kusafiri. Ilimpa tabu sana kusoma.
Basi kwa kuona kuwa nina muda mwingi, nikaanza kozi ya kiingereza. Orodha ya vitabu vilivyopatikana maktaba ilipopita niliagiza kitabu kwa kuweka namba yangu kwa nilichokipenda kati ya vile ambavyo havikuchaguliwa. Kupitia kozi ya kiingereza na mazoezi, uelewa wangu wa lugha ukaanza kurudi polepole. Ndani ya mwaka mmoja nikawa na uwezo wa kuandika barua nzuri inayoeleweka. Wakati huo huo, baada ya kumsikia Bimbi akielezea mnyumbulisho wa maneno, nikajiunga na kozi ya kilatini kimyakimya.
Pia kwa uongozi wa Bimbi, nilifanikiwa nikawa nimejifunza mbinu mbalimbali za kuishi gerezani. Mara zote nilikuwa na katoni kadhaa za sigara ndani ya selo yangu; sigara gerezani zilikuwa na thamani kama zilivyo pesa mtaani. Nilichezesha kamari za pesa na sigara wakati wa ndondi na mpira. Sijikusahau hali ilivyokuwa siku ile ya mwezi wanne wa mwaka 1947, siku ambayo Jackie Robinson alipoletwa kuchezea Brookyln Dodgers. Nilikuwa shabiki mkubwa wa Jackie Robinson, sikio langu halikubanduka redioni alipocheza. Hakuna mchezo uliomalizika bila ya mimi kung’amua takwimu zake katika mchezo huo.
***
Siku moja mnamo mwaka 1948, nilipokuwa nimehamishiwa kwenye gereza la Concord, nilipokea barua kutoka kwa kaka yangu Philbert ambaye kila siku alikuwa anajiunga kwenye kitu fulani. Aliniambia kuwa alikuwa amegundua dini ya “asili” ya mtu mweusi. Alisema sasa alikuwa mshirika wa kitu kinaitwa Taifa la Kiislamu(National of Islam), aliniambia kwamba ninapaswa kusali kwa Allah ili kupata wokovu. Nilimjibu Philbert, japo kiingereza changu kilikuwa kizuri lakini ilikuwa barua mbaya kuliko ile ya kwanza niliyomjibu baada ya kuniambia kuwa alikuwa ananiombea kwenye kanisa lake “Takatifu.”
Nilipopokea barua ya Reginald, sikutegemea kabisa ifanane na ya Philbert, japo nilifahamu kuwa alitumia muda mwingi pamoja na Hilda, Wilfred na Philbert huko Detroit. Ilikuwa barua ya kunipasha habari mbalimbali, pia ilikuwa na haya maelekezo: “Malcom usile tena nyama ya nguruwe wala usivute tena sigara. Nitakuonyesha namna ya kutoka gerezani.”
Mawazo yaliyonijia ni kuwa amegundua namna ambayo ninaweza kuilaghai idara ya magereza. Nililala na kuamka huku nikiwa na mawazo itakuwa ni jambo gani hilo. Labda tendo fulani la kisaikolojia kama nilivyowafanyia kule New York ili kuepuka kuandikishwa jeshini! Je nikiepuka kula nyama ya nguruwe na kuvuta sigara ninaweza kuwaaminish kuwa nina matatizo na hivyo kuniachia huru?
“Kutoka gerezani.” Maneno hayo yaliniganda kichwani. Nilitamani sana kuwa huru.
Nilitamani kuongea na Bimbi kuhusu suala hili lakini machale yakaniambia nisimwambie mtu.
Kuacha sigara halikuwa jambo gumu. Nilizoea kuishi bila kuvuta nilipokuwa kwenye kifungo cha peke yangu. Vyovyote ilivyo lakini sitaiacha nafasi hii ipite. Nilisoma ile barua na kisha nikamalizia paketi ya sigara niliyokuwa nimeisha ifungua. Tokea siku hiyo ya mwaka 1948, sijavuta tena sigara.
Siku kama tatu au nne mbele, nyama ya nguruwe iliandaliwa wakati wa chakula cha mchana.
Wakati nakaa kwenye meza ya chakula mawazo yangu hayakuwepo kabisa kwenye nyama ya nguruwe. Ghafla maneno
usile tena nguruwe yakapita mbele yangu.
Sinia lilipopita nilisita kidogo kisha nikampasia mfungwa aliyefuata. Mara moja alianza kujipakulia. Kisha ghafla akasimama na kugeuka kuniangalia kwa mshangao.
Nilimwambia, “sili nguruwe.”
Basi sinia liliendelea mbele. Inafurahisha sana jinsi taarifa zinavyosambaa gerezani. Gerezani ambapo hakuna mambo mengi ya kufanya, jambo dogo huzua taharuki kubwa sana. Kufikia usiku jengo letu lote lilikuwa limefahamu kuwa Shetani hali nguruwe.
Kwa namna fulani jambo hilo lilinifanya nijivune sana. Picha waliyonayo watu wengi nje na ndani ya magereza ni kuwa mtu mweusi hawezi kuishi bila kula nguruwe. Ilinifanya nijihisi vizuri kuona kuwa kutoila kwangu kuliwashtua watu, hasa wafungwa wa kizungu.
Baadaye nilipokuja kuusoma na kuuelewa Uislamu, nilifahamu kuwa nilikuwa nimetimiza takwa langu la kwanza la Kiislamu bila kujua wala kuwa muislamu kamili. Kwa mara ya kwanza nilikuwa nimejionea mafundisho ya Kiislamu, “Kama ukichukua hatua moja kumuelekea Allah-Allah atachukua hatua mbili kukuelekea.”
Kaka na dada zangu huko Detroit na Chicago walikuwa wamebadili dini na kujiunga na ile waliyofundishwa kuwa ndiyo “dini ya asili ya mtu mweusi” ambayo Philbert alikuwa ameniandikia kunieleza. Wote walikuwa wakisali ili na mimi nibadili nikiwa bado gerezani. Mwishowe wakaamua kuwa Reginald, mtu wa mwisho kujiunga na ambaye yupo karibu sana nami ndiye atafaa zaidi kuongea nami maana alifahamu vyema maisha yangu.
Mbali na haya, dada yangu Ella naye alikuwa akipambana ili nihamishiwe kwenye gereza la mafunzo lililokuwa kama makazi ya kawaida huko Norfolk, Massachusetts. Hili lilikuwa gereza la majaribio. Wafungwa kwenye magereza mengi walizungumza kuwa iwapo una pesa na una watu wa kukusaidia unaweza hamishiwa kwenye gereza hilo ambalo maisha yake yalisemwa kuwa ni mazuri kiasi ambacho haikuwa rahisi mtu kuamini kuwa yupo gerezani. Ella akawa amefanikiwa na mwishoni mwa mwaka 1948 nikahamishiwa Norfolk.
Ukilinganisha na nilikotoka, mahali pale palikuwa kama mbinguni. Kulikuwa na vyoo vya kisasa, hakukuwa na nondo bali kuta tu. Na ndani yake mtu alikuwa na uhuru mwingi zaidi. Na kwa vile hapakuwa mjini, kulikuwa na hewa safi sana.
Kulikuwa na nyumba ishirini na nne na ndani ya kila nyumba waliishi watu hamsini. Hivyo kulikuwa na jumla ya wafungwa 1,200. Kila nyumba ilikuwa ni ya ghorofa tatu na jambo zuri kuliko yote ni kuwa kila mfungwa alikuwa na chumba chake.
Karibu asilimia kumi na tano ya wafungwa walikuwa ni weusi ambao waligawanywa, kila nyumba ilikuwa na kama wafungwa weusi tisa.
Gereza-makazi la Norfolk lilikuwa ni mtindo wa kisasa kabisa wa gereza. Mahali pa chuki, kuchongeana na askari waliojaa chuki kulikuwa na ustaarabu-ustaarabu wa gerezani. Asilimia kubwa ya wafungwa wa Norfolk walishiriki kwenye mambo ya “kisomi” masuala kama majadiliano na kubishana kwa hoja. Wakufunzi wa mambo ya kielimu walitoka vyuo vikuu vya Harvard, Boston na taasisi zingine za kielimu zilizokuwa karibu. Sheria za kutembelea wafungwa zililegezwa sana ukilinganisha na magereza mengine. Watu waliweza kutembelea karibu kila siku, na waliruhusiwa kukaa hadi kwa saa mbili. Uliweza kuchagua kukaa kwenye kiti kimoja na mgeni wako au kukaa kwa kuangaliana.
Jambo moja la kipekee sana lilikuwa ni maktaba ya gereza. Milionea mmoja aliyeitwa Parkhurst aliacha wosia kuwa maktaba yake wapewe gereza la Norfolk. Pengine alikuwa anapendezwa nasuala la kubadili watu tabia kuwafanya wawe bora zaidi. Inaonekana alipendelea sana kusoma vitabu vya historia na dini. Maelfu ya vitabu vyake yalikuwa kwenye makabati ya maktaba na vingine vingi viliwekwa kwenye makasha baada ya kukosekana nafasi kwenye makabati. Pale Norfolk tuliweza kuingia maktaba na kuchagua vitabu baada ya kupata ruhusa. Kulikuwa na mamia ya vitabu vya kale, vingine vikiwa adimu kabisa. Mwanzoni nilikuwa najisomea tu, lakini baadaye nilikuja kujifunza jinsi ya kuchagua cha kusoma na kusoma kwa malengo.
Sikumsikia Reginald kwa muda mrefu toka nihamie Norfolk, lakini nilihamia pale nikiwa nimeacha kuvuta sigara na kula nyama ya nguruwe. Suala la kutokula nguruwe liliwashtua baadhi ya watu pale. Baada ya muda kupita nikawa nimepokea barua akinitaarifu kuwa atakuja kunitembelea. Alipofika nilikuwa na shauku kubwa ya kusikia mbinu aliyotaka kunipa.
Reginald alifahamu vyema jinsi akili yangu ya mtaani ilivyofanya kazi na hiyo ndiyo sababu njia aliyotumia kuniingia ilifanya kazi vyema.
Mara zote alivalia nadhifu sana na siku alipokuja kuniona alikuwa nadhifu zaidi. Nilikuwa na hamu kubwa ya kusikia kitendawili cha “Usile nguruwe wala kuvuta sigara” kikiteguliwa. Lakini yeye alizungumza kuhusu familia, mambo yanayotokea huko Detroit na Harlem alipopita mara ya mwisho. Kamwe sikuwahi kumhimiza mtu aniambie kitu chochote kabla ya yeye mwenyewe hajawa tayari. Kwa namna alivyoongea kwa kuzunguka nilifahamu kuwa kuna kitu kikubwa kinafuata.
Mwishowe, kama vile kuna kitu kimemgutusha, alisema, “Malcom, fikiria mtu awe anajua kila kitu duniani, atakuwa mtu wa namna gani?”
Tulipokuwa Harlem alikuwa anapenda kuongea kwa njia hii isiyo ya moja kwa moja. Mara nyingi hilo lilinikera sana maana mimi sikuwa mtu wa kupindishapindisha maneno. Nilimuangalia na kujibu, “Atakuwa kama aina fulani ya mungu hivi-”
Reginald akasema, “Kuna
mtu anafahamu kila kitu.” “Nani huyo?” niliuliza. “Mtu huyo ni Mungu,” alisema Reginald. “Jina lake halisi ni Allah.”
Allah. Nilikumbuka kuona jina hilo kwenye barua ya Philbert; hiyo ilikuwa ishara ya kwanza iliyonifanya nianze kuunganisha mambo. Reginald aliendelea. Aliniambia kuwa Mungu ana maarifa ya nyuzi 360. Akaongeza kuwa nyuzi 360 zinawakilisha “Jumla ya maarifa yote.”
Kusema kuwa nilichanganyikiwa itakuwa haitoshi. Maana kumbuka kuwa nilikuwa namsikiliza nikitarajia atazungumzia jambo fulani. Niliendelea tu kusikiliza nikijua kuwa mdogo wangu ana jambo anataka kunieleza. Na kama mtu ana jambo anataka kukueleza unatulia na kumsikiliza.
“Shetani ana nyuzi thelathini na tatu tu za maarifa zinazojulikana kama Umasoni.” Alisema Reginald. Nakumbuka maneno yake vyema sababu baadaye niliyatumia kuwafundisha wengine. “Shetani anatumia Umasoni wake kuwatawala watu.”
Akanieleza kuwa Mungu huyo amekuja Marekani na amejifunua kwa mtu aliyeitwa Elijah-“mtu mweusi kama sisi tu.” Mungu huyu amemjulisha Elijah kuwa “muda wa shetani umeisha.
Sikujua hata cha kufikiri. Niliendelea tu kusikiliza.
“Shetani naye ni mtu,” aliendelea Reginald.
“Unamaanisha nini?”
Kwa ishara ya kichwa Reginald alinielekezea upande waliokaa wafungwa wa kizungu na wageni wao, wakizungumza kama sisi. “Hao,” alisema. “Mzungu ndiye Shetani.”
Aliniambia kuwa wazungu wote wanafahamu kuwa wao ni mashetani-“Hasa Ma-masoni.” Sitakuja kusahau: kwa kasi, akili yangu ilichambua aina zote za “wazungu” niliowafahamu; mwishowe iligota kwa Hymie, Myahudi ambaye alikuwa mwema sana kwangu. Mara kadhaa nilikuwa nimeenda na Reginald kwenye kile kiwanda cha pombe za magendo kule Long Island kununua na kupakia pombe za Hymie.
Niliuliza, “Wazungu wote?” “Wote,” alijibu.
“Hata Hymie?” “Kwani kuna tatizo gani iwapo nikakuacha utengeneze dola mia tano wakati mimi natengeneza dola elfu kumi?” Baada ya Reginald kuondoka nilizama kwenye fikra. Nilifikiri na kufikiri. Sikuelewa hata kidogo.
Taswira za wazungu niliowafahamu zilipita akilini mwangu, toka mwanzo wa maisha yangu. Wazungu kutoka serikalini waliokuja nyumbani kwetu baada ya wazungu wengine nisiowafahamu kumuua baba yangu. . . wazungu waliokuwa wakimwita mama yangu kichaa mbele yake, na mbele yangu na ndugu zangu hadi mwishowe alipopelekwa hospitali ya wagonjwa wa akili huko Kalamazoo. . . jaji wa kizungu na wengine waliotutawanya watoto. . . familia ya Swerlin, wazungu wengine wa Mason. . . vijana wa kizungu niliosoma nao, waalimu, mwalimu aliyeniambia niwe “Seremala” nilipokuwa darasa la nane sababu ni upumbavu kwa mtu mweusi kuwaza kuwa mwanasheria. . . .
Kichwa changu kilijaa sura za wazungu. Wazungu wa Boston wakati wa dansi ya wazungu kwenye ukumbi wa Roseland kipindi nilipokuwa mng’arisha viatu. . . Nilipokuwa nikipeleka sahani jikoni kule kwenye mgahawa wa Parker. . . wafanyakazi na wasafiri kwenye treni. . . Sophia. . . .
Wazungu wa New York-polisi na wahalifu wa kizungu nilioshughulika nao. . . wazungu waliojazana kwenye baa za vichochoroni za watu weusi kuja kuonja
roho za weusi . . . wanawake wa kizungu waliotaka wanaume weusi. . . wanaume wa kizungu niliowapeleka kwenye “madanguro maalumu” kutimiziwa haja walizotaka. . . .
Mnunua vitu vya wizi kule Boston na wakala wake. . . polisi wa Boston. . . rafiki wa mume wa Sophia, mume wa Sophia ambaye sikuwahi kumuona lakini nilimfahamu vilivyo . . . mdogo wa Sophia . . . Myahudi muuza vito ambaye alisaidia kunaswa kwangu . . . watu wa ustawi wa jamii . . . watu wa mahakama ya wilaya ya Middlesex . . . hakimu aliyenihukumu miaka kumi . . . wafungwa niliokuja kuwafahamu, askari na maofisa wengine. . .
Mtu aliyekuwa maarufu kwenye gereza la Norfolk alikuwa ni mzee mmoja aliyepooza na tajiri, aliitwa John. Alikuwa amefungwa kwa kumuua mtoto wake. Moja ya yale mauaji ya “rehema.” Alikuwa ni mjivuni sana, siku zote akijitapa kuwa ni Masoni wa daraja la 33, na jinsi Masoni walivyo na nguvu kiasi kwamba ni Masoni tu ndiyo wamewahi kuwa marais wa Marekani, na kuwa Masoni anayehitaji msaada anaweza kuwapa ishara ya siri majaji na watu wengine wakubwa.
Nilikuwa bado nawaza mambo aliyoniambia Reginald. Nilitaka kuyajaribu kwa John. Alikuwa amepangiwa kazi nyepesi-nyepesi kwenye shule ya gereza. Nilienda kumuona huko.
“John,” nilisema, “Duara lina nyuzi ngapi?”
“Mia tatu na sitini,” alijibu.
Nilichora umbo mraba na kumuuliza, “Hilo umbo lina nyuzi ngapi?” akajibu mia tatu na sitini. Nikamuuliza iwapo nyuzi mia tatu na sitini ndiyo kikomo cha “nyuzi” kwenye kitu chochote kile.
Akaseme “Ndiyo.” Nikasema, “Kwa nini basi Masoni wanaishia nyuzi thelathini na tatu tu?”
Hakuwa na jibu la kuridhidha. Lakini kwangu jibu lilikuwa ni kuwa Umasoni ni nyuzi thelathini na tatu tu za Uislamu ambao una nyuzi kamili. Nyuzi ambazo kamwe Ma-masoni hawataweza kuzifikia japo walifahamu uwepo wake.
Reginald alipokuja kunitembelea tena baada ya siku chake, aliweza kujionea jinsi waneno yake yaliyoniathiri kwa jinsi nilivyokuwa. Alionekana kufurahi sana. Kisha kwa msisitizo aliongea kwa saa mbili kuhusu “Shetani mzungu” na “Mtu mweusi aliyechotwa akili.”
Reginald alipoondoka aliniacha nikihangaika na mawazo mengi mazito ambayo sijawahi kuwa nayo maishani mwangu: kwamba mzungu alikuwa akipoteza nguvu zake za kukandamiza na kunyonya dunia ya wasio wazungu kwa kasi; na kuwa dunia ya wasio wazungu ilianza kuamka ili kutawala dunia tena, kama ilivyokuwa huko nyuma; kwamba dunia ya mzungu ilikuwa ikianguka, ilikuwa ndiyo inaishia.
“Hata hujijui wewe ni nani,” alikuwa ameniambia Reginald. “Shetani mweupe amekuficha hata hufahamu kuwa jamii yako ni ya watu waliostaarabika zamani za kale, watu matajiri wa dhahabu na wafalme. Hata jina halisi la ukoo wako hulifahamu, hata leo ungeisikia lugha yako ya asili usingeitambua. Shetani mweupe amekuficha maarifa yote kuhusu jamii yako. Umekuwa mhanga wa shetani mweupe toka alipobaka na kuua na kukuiba kutoka nchi yako ya asili . . . ”
Nilianza kupokea barua zisizopungua mbili kila siku kutoka Detroit kwa ndugu zangu. Kaka yangu mkubwa, Wilfred na mke wake wa kwanza, Bertha –wote waliniandikia(Wilfred alizaa wtoto wawili na Bertha, baada ya kifo chake akamuoa mke wake wa sasa, Ruth). Philbert na Hilda pia waliniandikia. Reginald alinitembelea, akikaa kidogo Boston na kurejea Detroit. Wote walikuwa Waislamu, wafuasi wa mtu waliyemtambulisha kwa jina la “Mtukufu Elijah Muhammad,” mtu mmoja mwenye umbo dogo na mpole. Wakati mwingine walimtambulisha kama, “Mtume wa Allah.” Walisema alikuwa ni mweusi kama sisi, mzaliwa wa Marekani, huko Georgia mashambani. Baadaye akawa amehamia Detroit na familia yake na huko akakutana na Bwana Wallace D. Fard aliyedai kuwa alikuwa ni Mungu katika mwili. Bwana Wallace D. Fard alikuwa amempatia Elijah Muhammad ujumbe wa Allah kwenda kwa watu weusi ambao walikuwa ni “Taifa la Kiislamu lililopotelea kwenye nyika za Amerika ya Kaskazini.”
Wote walinihimiza nipokee mafundisho ya mtukufu Elijah Muhammad. Reginald aliniambia kuwa Waislamu hawali nyama ya nguruwe na hawavuti sigara, ilikuwa ni sheria kwa wafuasi wote wa Elijah Muhammad maana hawakupaswa kutumia vitu vya kudhuru kama madawa ya kulevya, tumbaku au pombe. Nilisoma na kusikiliza tena na tena, “Msingi wa Uislamu ni kusujudia, mtu kujinyenyekeza kwa Allah.”
Walinipatia kwa kirefu “Maarifa ya kweli juu ya mtu mweusi” waliyokuwa nayo wafuasi wa Elijah Muhammad kupitia barua ambazo nyakati nyingine zilikuwa na makala zilizochapwa.
***