Sura ya tano inaendelea.
Kufukuzwa kazi lilikuwa ni jambo ambalo halikwepeki. Kilichonimaliza ilikuwa ni barua ya hasira kutoka kwa mteja mmoja. Wasimamizi wa treni nao waliongezea kwa kusema jinsi walivyoletewa malalamiko mengi kunihusu, na maonyo niliyopata.
Lakini sikujali kitu, kwenye wakati ule wa vita, kazi nyingi nilitamani kufanya zilikuwa zinatafuta watu. Nlipolipwa stahiki zangu, nikaonelea ni vyema kwenda Lansing kuwasalimu ndugu zangu. Nilikuwa na ofa ya kusafiri bure kwa treni.
Hakuna hata mmoja kule Michigan aliyeamini kuwa ni mimi. Ni kaka yangu mkubwa tu, Wilfred ndiye hakuwepo. Alikuwa huko Chuo Kikuu cha Wilberforce, Ohio akijifunza ujuzi fulani. Philbert na Hilda walikuwa wakifanya kazi Lansing. Reginald, yule aliyekuwa akinitegemea, alikuwa mkubwa kiasi cha kuweza kudanganya umri, alikuwa amepanga kujiunga na meli za biashara karibuni. Yvonne, Wesley na Robert walikuwa shuleni.
Nywele zangu zilizotiwa dawa na mavazi yangu vilistaajabisha kiasi kwamba ningeweza chukuliwa kuwa ni mtu wa kutoka sayari nyingine. Hata nilisababisha ajali ndogo, dereva mmoja alisimama kunishangaa na wa nyuma yake akamgonga. Muonekano wangu uliwastaajabisha vijana wakubwa ambao hapo zamani niliwaonea wivu na kuwahususdu; wakati wa salamu nilitoa mkono na kusema “
Skin me, Daddy-o!” Simulizi zangu juu ya New York, huku nikiwa bangi muda wote.
“My man! . . . Gimme some skin!”
Kitu pekee kilichoninyenyekeza ni nilipotembelea Hospitali ya Kalamazoo. Mama yangu ni kama hakunitambua sawasawa.
Pia nilienda kumtembelea mama yake Shorty. Nilijua kuwa Shorty atathamini sana mimi kufanya hivyo. Alikuwa ni mwanamke mzee na alifurahi kusikia habari za Shorty. Nilimwambia kuwa Shorty anaendelea vizuri na siku moja atakuwa kiongozi mkubwa wa bendi yake. Aliniambia nimwambie Shorty amuandikie barua na kumtumia chochote kitu.
Nilipita pia Mason kumtembelea bibi Swerlin.
Zoot yangu ya rangi ya papa, viatu vyangu virefu na vilivyotuna mbele na kofia yangu ya pama juu ya nywele zangu nyekundu zilizokolea dawa vilimuelemea vilimmaliza kabisa bibi Swerlin. Alijitahidi tu kuweza kunikaribisha. Namna nilivyoonekana na jinsi nilivyoongea vilimfanya awe na wasiwasi sana, kiukweli sote tulijihisi afadhali nilipoaga na kuondoka.
Usiku wa kuamkia kuondoka kulikuwa na dansi kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Lincoln(Nilijifunza kuwa ukitaka kuwapata watu weusi kwenye mji wowote bila ya kuuliza, nenda kwenye kitabu cha orodha ya namba za simu na tafuta “Lincoln School” Mara zote ilikuwa kwenye maeneo ya watu weusi-hasa katika siku zile.)ningeondoka Lansing bila ya kuhudhuria dansi, lakini sasa nilikuwa ukumbini nikiwarusha wasichana wadogo kupita mabegani mwangu. Mara kadhaa bendi ilisimama na wachezaji wengine walikaa pembeni huku macho yamewatoka kama visosa. Usiku huo kuna watu hata waliniomba kusaini vitu vyao, “Harlem Red” Niliiacha Lansing ikiwa imepigwa na butwaa.
Niliporudi New York, nikiwa sina kitu wala kazi yoyote ya kunitegemeza, nikatambua kuwa kazi ya reli ndiyo ilikuwa kila kitu kwangu, basi nikaenda kwenye shirika la reli la Seaboard kuomba kazi. Mashirika ya reli yalikuwa na uhitaji mkubwa wa wafanyakazi kiasi kwamba nilichofanya ni kuwaambia tu kuwa nilifanya kazi kwenye shirika la New Haven na siku mbili mbele nilikuwa kwenye treni ya “Silver Meteor” iliyoelekea St. Petersburg na Miami. Nilikuwa nikikodisha mito na kusafisha mabehewa, na kuwafurahisha abiria wa kizungu. Nilitengeneza kiasi kama kile nilichotengeneza wakati wa kuuza
sandwich
Haikuchukua muda nikawa nimegombana na mzungu mmoja kutoka Florida ambaye alikuwa ni msimamizi msaidizi. Niliporudi New York wakaniambia nitafute kazi nyingine. Lakini jioni hiyohiyo nilipoenda Small’s Paradise, mmoja wa wahudumu, kwa kufahamu jinsi nilivyoipenda New York, aliniita pembeni na kuniambia kuwa iwapo niko tayari kuacha kazi kwenye shirika la reli, nitaweza kumbadili mhudumu wa mchana ambaye alikuwa ameitwa kutumikia jeshini.
Mmiliki wa bar ile aliitwa Ed Small, yeye na kaka yake aliyeitwa Charlie waliivana sana, na nadhani Harlem hakukuwa na watu walioheshimika na maarufu kama hao. Walifahamu kuwa nilifanya kazi kwenye shirika la reli, jambo ambalo kwa mhudumu lilikuwa ni uzoefu muhimu sana. Niliongea na Charlie Small ofisini kwao. Nilikuwa na wasiwasi kuwa atawauliza baadhi ya rafiki zake wa siku nyingi waliofanya kazi kwenye shirika la reli wampe maoni yao kunihusu. Charlie asingekubali kufanya kazi na mtu yeyote mwenye sifa ya ujeuri. Lakini aliamua kutokana na maoni yake mwenyewe, baada ya kuwa ameniona kwenye baa yao mara nyingi, nikiwa mtulivu, nikiangalia tu pilikapilika zinavyoenda. Aliniuliza iwapo nimewahi ingia matatizoni na polisi nami nikajibu hapana, na mpaka wakati huo hilo lilikuwa ni kweli. Charlie akaniambia kuhusu sheria za wafanyakazi wa pale. Kuchelewa na uvivu ni marufuku. Wizi hautakiwi na hakuna kuwatoa pesa wateja kwa namna yoyote ile, hasa askari. Basi nikawa nimeajiriwa.
Hii ilikuwa ni mwaka 1942, ndiyo nilikuwa nimeingia umri wa miaka kumi na saba.
***
Kwa kuwa Small’s ilikuwa ndiyo kama katikati ya kila kitu, kuwa mhudumu pale ilikuwa mbingu ya saba mara saba. Charlie Small hakuwa na haja ya kunitahadharisha juu ya kuchelewa; nilikuwa na shauku kubwa ya kufika pale. Nilifika saa moja kabla ya zamu yangu kuanza. Mhudumu wa asubuhi alionelea kuwa zamu yangu mchana ilikuwa imelala sana, haina pilikapilika wala bakshishi. Mara kadhaa alibaki nami katika saa hilo na kunifundisha hiki na kile, maana hakutaka kuona nafukuzwa kazi.
Kwa msaada wake nilijifunza vitu vingi kwa haraka-vitu ambavyo vingemgombanisha mhudumu mpya na wapishi na mtu wa kaunta. Watu hawa wote-kulingana na jinsi walivyompenda mhudumu husika, waliweza kufanya maisha yake yawe machungu au matamu-nami niliazimia kupendwa. Ndani ya juma moja nikawa nimeelewana vyema na wote. Wateja ambao walikuwa wamezoea kuniona miongoni mwao ndani ya baa ile; na sasa wakiniona nimevaa sare ya wahudumu, walifurahia na kushangazwa; walinitendea kirafiki sana. Nami nilikuwa mkarimu mwenye kushawishi hasa”Kinywaji kingine? . . . Sasa hivi bwana . . . utapenda chakula? . . . kiko vizuri . . . unahitaji chakula gani bwana? . . . vipi kuhusu
sandwich?
Si tu wahudumu wa kaunta na wapishi, watu ambao niliona kuwa wanajua kila kitu juu ya kila kitu; lakini na wateja pia walianza kunifundisha kupitia mazungumzo wakati ambao hakukuwa na pilika nyingi. Wakati mwingine mteja aliniongelesha alipokuwa anakula. Na wakati mwingine nilisikia mambo kwa kirefu kutoka kwa wakongwe ambao wameishi Harlem tokea mwanzo wa watu weusi kuhamia hapa.
Hilo jambo lilinishangaza sana; kwamba hapo mwanzo Harlem haikuwa sehemu ya watu weusi.
Nilijifunza kuwa mwanzo lilikuwa ni eneo la Wadachi. Kisha ukaanza uhamiaji wa watu masikini wenye njaa kutoka Ulaya, wakiwa wamebeba mali zote walizomiliki kwenye mifuko waliyobeba migongoni. Kwanza walianza kuja Wajerumani; Wadachi wakawakimbia na Harlem ikawa ya Wajerumani.
Kisha wakaja Wa-Irish, wakikimbia njaa ya viazi. Wajerumani wakakimbia, wakiwanyanyapaa Wa-Irish, hao wakaichukua Harlem. Kutoka hapa wakaja Waitaliano, kitu kilekile kikatokea, Wa-Irish wakawakimbia. Kisha wakaja Wayahudi na Waitaliano wakawakimbia.
Leo hii, wajukuu hawa wote wa wahamiaji wanakimbia kwa nguvu zao zote, kuwakimbia wajukuu wa watu weusi waliosaidia kupakua meli zilizobeba babu zao.
Nilishangaa mkongwe mmoja aliponiambia kuwa, wakati mchezo huu wa wahamiaji kupokezana ukiendelea, mtu mweusi amekuwepo kwenye jiji la New York tokea mwaka 1683, kabla ya yeyote kati ya wahamiaji hao hajaja, na aliwekwa kwenye maeneo ya maghetto sehemu mbalimbali za jiji. Mara ya kwanza walikuwa kwenye eneo la Wall Street; kisha wakahamishiwa Greenwich Village. Baada ya hapo wakapelekwa eneo la Stesheni ya Pennsylvania. Na kituo cha mwisho kabla ya kuja Harlem kilikuwa ni mtaa wa 52, na ndiyo sababu ya mtaa wa 52 kujulikana kama mtaa wa kujirusha, sifa ambayo imedumu muda mrefu hata baada ya watu weusi kuondoka.
Kisha mnamo mwaka 1910, mfanyabiashara mmoja wa majengo mweusi kwa namna fulani aliweza kuweka familia mbili au tatu za weusi kwenye jengo la wayahudi. Wayahudi walikimbia nyumba hiyo, kisha wakakimbia mtaa, na watu weusi wengi zaidi wakazidi kuhamia kwenye nyumba walizohama. Baadaye wayahudi wakahama kutoka mitaa kadhaa na watu weusi wengi zaidi wakazidi kuja, ndani ya muda mfupi Harlem ikawa kama ilivyo leo—eneo la watu weusi.
Kwenye mwanzoni mwa miaka ya 1920, kazi ya muziki ikaibuka huko Harlem, hasa ikichagizwa na wazungu ambao walifika kila usiku. Ilianza wakati ambao kijana mpiga tarumbeta kutoka New Orleans aliyeitwa Louis “Satchmo” Armstrong aliposhuka kwenye treni New York na kuanza kupiga muziki na Fletcher Hebderson. Small’s paradise ilifunguliwa mwaka 1925 ikiwa na wateja kutoka kotekote kwenye barabara ya saba. Mwaka 1926 ilifunguliwa Cotton Club, mahali ambapo bendi ya Duke Ellington ilipiga muziki kwa miaka mitano; pia mwaka huohuo wa 1926 ukumbi wa dansi wa Savoy ulifunguliwa, ukimbi mkubwa wenye na eneo la kuchezea la urefu wa futi mia mbili na majukwaa mawili.
Harlem ikawa maarufu na kuanza kujaa watu weupe kutoka kila kona ya dunia. Mabasi ya watalii yakaanza kwenda. Cotton Club ilihudumia watu weupe tu. Kulikuwa na mamia ya club zingine na baa za vichochoroni zilizohudumia wazungu. Baadhi ya zilizokuwa maarufu ni pamoja na Connie’s Inn, The Lenox Club, Barron’s, The Nest Club, Jimmy’s Chicken Shack na Minton’s. Kumbi za Savoy, The Golden Gate na The Renaissance ziligombania wacheza dansi—Savoy walianzisha vitu kama Alhamisi ya jikoni. Mashindano ya urembo na walitoa gari jipya kila usiku wa jumamosi. Walialika bendi kutoka kila kona ya nchi. Kulikuwa na viongozi wa bendi waliojipamba sana, kulikuwa na mtu kama Fess Williams ambaye alikuwa na suti na kofia zilizopambwa kwa almasi, Cab Collaway na
zoot yake nyeupe iliyokuwa baba wa
zoot zote , pamoja na kofia yake nyeupe, akiiwasha Harlem kwa vibao vyake kama “Tiger Rag” na “St James Infirmary” na “Minnie the Moocher.”
Basi mji wa watu weusi ulijaa wazungu, makuwadi, makahaba, wauza pombe, wachakarikaji wa kila namna, na polisi na maafisa waliokuwa wakikamata pombe za magendo. Watu weusi walicheza dansi kama vile hawajawahi kucheza maishani mwao. Nafikiri nimewahi kuwasikia wakongwe kama ishirini na tano hivi pale Small’s wakidai kuwa walikuwa ndiyo wa kwanza kucheza Lindy Hop ndani ya Savoy, mahali ambapo mtindo huo ulizaliwa mnamo mwaka 1927, ukiitwa jina la Lindbergh ambaye alikuwa ndiyo ametoka tu kurusha ndege kwa mara ya kwanza kutoka New York hadi Paris bila kutua.
Hata kumbi ndogo zilizokuwa na nafasi ya kutosha kinanda tu nazo zilikuwa na wapigaji mahiri kama James P. Johnson na Jell Roll Morton, na waimbaji kama Ethel Waters. Na ilipofika saa kumi za usiku, muda ambao club zote halali zilitakiwa kufungwa, wanamuziki weusi kwa weupe kutoka mjini kote walifika Harlem kwenye eneo walilopanga kukesha na kupiga nyimbo thelathini au arobaini hivi hadi asubuhi.
Hadi kufikia mdodoro wa uchumi wa mwaka 1929, na mambo yote kuisha- Harlem ilikuwa imeishajizolea sifa kama kama ngome ya Marekani, Small’s iliishi yote hayo. Basi niliwasikia wakongwe wakikumbuka nyakati hizo nzuri na kujawa na hisia.
Kila siku niliwasikiliza wateja waliotaka kuongea kwa umakini sana, na hilo liliongeza elimu yangu. Masikio yangu yalinyonya kama sifongo pale mmoja wao-labda kutokana na kunywa sana, aliponiambia siri ya kazi anazofanya kuendesha maisha. Basi nikawa nimepata elimu kubwa kutoka kwa manguli wa mambo kama kamari, ukuwadi, utapeli wa kila aina, kuuza madawa ya kulevya, wizi na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Mwisho wa sura ya tano.