Kitabu: Shamba la wanyama. Tusome na kujadili

Kitabu: Shamba la wanyama. Tusome na kujadili

Red Giant

JF-Expert Member
Joined
Mar 9, 2012
Posts
15,657
Reaction score
20,967
Umewahi kusoma hiki kitabu?
1623873880760.png



Kimeandikwa na: George Orwell, 1945.
Kimetafsiriwa na: Pictuss

Email: Pictuspublishers@gmail.com.

©Pictuss2021

Haki zote zimehifadhiwa. Hakuna sehemu yoyote ya tafsiri hii inayoweza kunakiliwa, kutolewa kivuli(photocopy), kuhamishwa, kurekodiwa au kutolewa kwa namna yoyote ile bila ya taarifa ya awali ya kimaandishi kutoka kwa mmiliki.


SURA YA KWANZA

Mmiliki wa shamba la Mano, bwana Jones alikuwa amefunga banda la kuku. Lakini sababu ya ulevi, alikuwa amesahau kufunga tundu dogo la kwenye mlango ambalo kuku hupita. Alielekea ndani kwake huku mwanga wa taa ya chemli ukichezacheza na kufanyiza miduara ardhini. Alipofika mlango wa nyuma wa nyumba yake alirusha viatu vyake na kujimiminia glasi ya bia kutoka kwenye debe. Akanywa na kuelekea chumbani ambako mke wake alikuwa tayari anakoroma.

Mara tu taa ya chumbani kwake ilipozima pilikapilika zikaanza kusikika kwenye mabanda ya mifugo. Mchana taarifa zilikuwa zimesambaa kuwa Meja, nguruwe dume mkubwa, alipatwa na ndoto ya ajabu sana usiku uliopita na alitaka kuwashirikisha wanyama wengine. Walikubaliana kuwa wote wakutane kwenye banda kubwa mara tu bwana Jones atakapokuwa ameshalala. Meja aliheshimika sana pale shambani, hivyo wanyama walikuwa tayari kupoteza saa moja la kulala ili wakamsikilize.

Kwenye kona moja ya banda kubwa alikuwa ametulia Meja kwenye kitanda chake cha nyasi, chini ya taa iliyokuwa ikining'inia darini. Kitanda chake kilikuwa sehemu ya juu kama jukwaa hivi. Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili lakini bado alionekana ni mshupavu na nguruwe bora. Mwenye hekima na busara, na mwenye roho nzuri japo meno yake yaliyotoka hayakuwahi kukatwa.

Baada ya muda mfupi wanyama wengine wakaanza kuwasili na kukaa, kila mmoja kulingana na aina yake. Walioanza kuwasili walikuwa ni mbwa watatu, Bluebell, Jessie na Pincher, kisha wakaingia nguruwe ambao walienda kukaa mbele karibu na jukwaa alilokaa Meja.

Kuku walikaa kwenye fremu za madirishani na njiwa waliruka na kukaa kwenye mbao za darini. Ng'ombe na kondoo walikaa nyuma ya nguruwe na kuanza kujitafuna. Farasi wawili wa kukokota mkokoteni, Boxer na Clover waliingia pamoja, walitembea polepole wakikanyaga kwa uangalifu ili kama kuna mnyama mdogo kwenye nyasi wasimdhuru.

Clover alikuwa farasi wa kike wa umri wa kati, lakini toka uzazi wake wa mwisho umbo lake halikuwa sawa. Boxer alikuwa ni farasi mkubwa sana, karibu kimo cha mikono kumi na nane na alikuwa na nguvu za farasi wawili wakubwa. Alikuwa na mstari mweupe katikati ya pua yake. Hilo lilimfanya aonekane kama kituko, na kiukweli hakuwa mnyama mwenye akili. Pamoja na hilo, Boxer aliheshimika sababu ya uwezo wake wa kufanya kazi na tabia yake njema.

Baada ya farasi aliingia mbuzi aliyeitwa Muriel na punda aliyeitwa Benjamini. Benjamini alikuwa ndiye mnyama mwenye umri mkubwa kuliko wote pale shambani. Alikuwa si muongeaji na iwapo akiongea ilikuwa ni kutoa kejeli. Mfano, anaweza kusema kuwa Mungu amempa mkia kwa ajili ya kufukuzia nzi, lakini angependelea vyote, nzi na mkia visingekuwepo.

Benjamini hajawahi cheka hata siku moja. Akiulizwa kwanini, alikuwa akijibu kuwa hajawahi kuona kitu cha kumchekesha. Pamoja na hayo, alikuwa na urafiki wa karibu pamoja na Boxer. Mara nyingi walitumia mapumziko ya jumapili pamoja katika malisho yaliyo nyuma bustani. Urafiki wao ulikuwa wa kushangaza, walikaa huko na kula pamoja bila kuongea chochote.

Farasi walipokaa, kundi la bata likaja. Walikuwa ni bata wa umri wa kati waliofiwa na mama yao waliingia. Walikuwa wakishangaa huku na huko wakitafuta sehemu salama ya kukaa. Walipokaa, Clover alizungusha miguu yake ya mbele kuwazungunka, wakakaa humo na haikuchukuwa muda wakawa wamepitiwa na usingizi.

Kisha akaingia Moli. Farasi mweupe mzuri lakini mpumbavu. Alikuwa anatumika kuvuta mkokoteni wa bwana Jones. Aliingia akitembea kwa madaha huku akimung'unya kipande cha sukari guru. Alienda kukaa karibu na jukwaa, na kuanza kuringishia nywele zake ndefu ili wengine waone tepe alizovaa.

Wa mwisho kabisa kuingia alikuwa ni paka. Kama kawaida yake, akatafuta sehemu yenye joto na akajibanza katikati ya Clover na Boxer. Muda wote wa hotuba ya Meja alikuwa akinguuruma kwa raha. Hakuelewa chochote kilichoongelewa.

Wanyama wote walikuwa wamefika isipokuwa Musa. Yeye alikuwa ni kunguru wa kufungwa na aliishi ndani kwa bwana Jones.

Baada ya Meja kuona kuwa wametulia na wako makini kumsikiliza, alikohoa kidogo na kuanza kusema.

"Ndugu zanguni, natumaini wote mmesikia kuhusu ndoto ya ajabu niliyoota jana usiku. Lakini nitazungumza kuhusu ndoto hiyo baadaye. Kuna jambo ningependa niongee kwanza. Ndugu zangu, sidhani kama nina muda mrefu wa kuwa na nyinyi, kabla sijafa nahisi nina wajibu wa kuwapatia hekima na busara nilizonazo. Nimeishi miaka mingi na nilikuwa na muda mwingi wa kufikiri. Hivyo nafikiri naweza kusema kuwa nina uelewa mkubwa kuhusu maisha. Hili ndilo hasa lililonifanya nitake kuongea nanyi. Sasa ndugu zangu, maisha yetu ni ya namna gani?"

"Tuongee ukweli; maisha yetu ni ya taabu, ya kazi ngumu na mafupi. Tunalishwa chakula kinachotosha kutufanya kuishi tu. Wale wanaoweza kufanya kazi, hufanyishwa kazi hadi nguvu yao ya mwisho. Nguvu zinapoisha huchinjwa kwa ukatili wa ajabu. Hakuna mnyama mwenye umri wa zaidi ya mwaka mmoja anayeijua furaha na starehe maishani."

"Uingereza yote hakuna mnyama aliye huru. Maisha ya mnyama ni machungu na ya kitumwa; huo ndiyo ukweli. Lakini jambo hilo ni mpango wa Mungu? Je mazingira ya nchi yetu ni magumu sana kiasi kwamba hatuwezi kuishi vizuri?"

"Hapana ndugu zangu, hapana kabisa! Ardhi ya Uingereza ni yenye rutuba na hali ya hewa ni nzuri. Inaweza kulisha wanyama wengi kuliko waliopo. Hili shamba tunaloishi linaweza kulisha farasi kumi na mbili, ng'ombe ishirini na mamia ya kondoo. Wote hao wakiishi vizuri na kwa ustaarabu kuliko maisha wanayoishi sasa. Basi ni kwanini tunaendelea na maisha haya ya taabu? Ni kwa sababu chakula chote tunachozalisha kinaporwa na binadamu. Hilo ndilo jibu la tatizo letu ndugu zangu. Kwa neno moja jibu ni - binadamu. Binadamu ndiye adui pekee wa kweli tuliyenaye. Mtoe binadamu na chanzo cha njaa na kazi za kitumwa kitakuwa kimeondoka milele."

"Binadamu ndiye kiumbe pekee ambaye anakula bila kuzalisha. Hatoi maziwa wala hatagi mayai, na hana nguvu za kutosha kukokota jembe la kulimia wala hana mbio za kuweza kukamata sungura, lakini ndiye bwana wa wanyama wote. Anawatumikisha lakini anawapa chakula cha kuwafanya wasife njaa tu, kingine chote anachukua. Nguvu zetu zinalima shamba, kinyesi chetu ni mbolea, lakini kati yetu hakuna anayemiliki zaidi ya ngozi yake mwenyewe. Nyinyi ng'ombe mlio hapa, ni maelfu mangapi ya lita za maziwa mlitoa mwaka jana? Na nini kimetokeo kwa hayo maziwa ambayo yalitakiwa yatumike kukuza ndama wenye afya? Kila tone limepita kwenye koo la adui yetu."

"Nanyi kuku, ni mayai mangapi mmetaga mwaka jana, na ni mangapi yametotolewa kuwa vifaranga? Karibu yote yameuzwa na bwana Jones kajipatia pesa, yeye na wafanya kazi wake. Na wewe Clover, watoto wako wanne uliowazaa wako wapi? Watoto ambao walitakiwa wawe msaada na furaha yako katika uzee wako. Kila mmoja aliuzwa alipofikisha mwaka mmoja tu, hutaweza kuwaona tena. Umelipwa nini zaidi ya kibanda cha kuishi na chakula kidogo?"

"Mbaya zaidi, hata haya maisha ya taabu tunayoishi bado hatuachi tukaishi yote. Mimi binafsi siwezi laumu maana nimekuwa kati ya wenye bahati. Nina miaka kumi na mbili na nimepata watoto zaidi ya mia nne. Nilionao ndiyo umri halisi wa nguruwe, lakini mwisho wetu wote ni kuchinjwa kikatili. Nyinyi nguruwe vijana mliokaa hapa mbele yangu, kabla ya mwaka kuisha kila mmoja wenu atalia kwa uchungu wakati wa kuchinjwa. Hiyo ndiyo njia yetu sote, ng'ombe, nguruwe, kuku, kondoo, kila mmoja wetu. Hata mbwa na farasi hawana afadhali. Boxer, siku misuli yako ikiishiwa nguvu bwana Jones atakuuza kwa wanunuzi wa mizoga. Huyo atakuchinja na kukuchemsha kuwa chakula cha mbwa. Nanyi mbwa mkizeeka na meno yenu kung'oka, bwana Jones atawafunga tofali shingoni na kuwatupa dimbwini."

"Je, haiko wazi kuwa mabaya yote ya maisha yetu chanzo ni ukatili wa binadamu? Tunahitaji kumtoa binadamu na chochote tunachozalisha kitakuwa chetu wenyewe.
Kufumba na kufumbua tutakuwa matajiri na huru. Sasa nini kinahitajika kufanyika? Kwanini tusifanye kazi usiku kucha na kwa uwezo wetu wote ili kupindua utawala wa binadamu? Huu ndiyo ujumbe wangu kwenu: Uasi! Sijui uasi huo utatokea lini, inaweza kuwa baada ya wiki moja au inaweza kuchukua miaka miamoja lakini nina hakika utatokea. Kama nilivyo na hakika kuwa naona nyasi hapa chini yangu ndivyo nilivyo na hakika kuwa uasi na mapinduzi vitatokea na haki itapatikana. Kazieni fikra jambo hilo nduguzanguni. Liwekeni akilini kwenye maisha yenu mafupi yaliyobaki, na waambieni ujumbe huu wataokuja. Hakikisheni kizazi kijacho kinaendeleza mapambano hadi ushindi upatikane."

"Ndugu zangu naomba msije kulegea kwenye lengo hili, na hoja yoyote isiwatoe kwenye lengo hili. Msisikilize wala kukubali wawambiapo kuwa maslahi ya binadamu na wanyama ni mamoja. Kwamba mafanikio ya binadamu ndiyo mafanikio ya wanyama. Huo ni ulaghai mtupu, binadamu ni mbinafsi anayejijali mwenyewe tu. Acha kuwe na undugu kati ya wanyama na undugu katika mapambano. Binadamu wote ni adui lakini wanyama wote ni ndugu."

Baada ya kusema hayo kukatokea shangwe kubwa sana. Meja alipokuwa akihutubia, panya wanne wakubwa walitoka kwenye mashimo yao na walikaa kumsikiliza. Mbwa wakawa wamewaona. Ushapu wao wa kukimbilia mashimoni ndiyo uliowaokoa.

Meja akainua mguu kuashiria wanyama wanyamaze, kisha akasema. "Ndugu zangu, hapa kuna jambo linatakiwa tulitatue. Wanyama wa porini kama sungura na panya ni adui zetu au ni ndugu zetu? Naombeni tupige kura. Swali liwe; Je, panya ni ndugu zetu?"

Kura ilipigwa mara moja na kwa kura nyingi ikakubaliwa kuwa panya ni ndugu. Kulikuwa na kura nne tu zilipinga. Kura za mbwa watatu na ya paka ambaye hata hivyo aligundulika amepiga kura ya ndiyo na hapana.

Meja akaendelea kusema: "sina mengi ya kuongezea ila nitaruria tu. Siku zote kumbuka kuwa una wajibu wa kuwa adui wa binadamu na mambo yake yote. Chochote kinachotembea kwa miguu miwili ni adui. Chochote kinachotembea kwa miguu minne au chenye mabawa ni rafiki. Na kumbukeni kuwa, katika kupambana na binadamu hatutakiwi kuwa kama yeye. Hata tukimshinda hatupaswi kuiga mambo yake. Mnyama yeyote hatakiwi kuishi ndani ya nyumba, kulala kitandani, kuvaa nguo, kunywa pombe, kuvuta sigara, kushika pesa au kujihusisha na biashara. Zaidi ya yote, mnyama yeyote hatakiwi kutawala wengine kwa kwa ukatili."

"Wanyama wote ni ndugu, wenye nguvu na dhaifu, wenye akili na wajinga, sote ni ndugu. Mnyama yeyote hatakiwi kabisa kumuua mnyama mwenzake. Wanyama wote sawa."

"Sasa ndugu zanguni nitawaambia kuhusu ndoto niliyoota jana usiku. Siwezi kuwaelezea vizuri jinsi ilivyokuwa ila ni ndoto inayohusu hali ya dunia binadamu atakapokuwa ametoweka, lakini ilinikumbusha zamani sana nilipokuwa bado nguruwe mdogo.

Miaka mingi iliyopita, nilipokuwa mdogo, mama yangu na nguruwe wengine walipendelea kuimba wimbo mmoja. Wimbo wenyewe waliujua kwa ala na maneno matatu ya mwanzo tu. Nilipokuwa mdogo nilikuwa nimeishika ile ala. Ni muda mrefu umepita hivyo ilikuwa imenitoka. Lakini jana usiku imenijia ndotoni, na cha kushangaza zaidi, hadi maneno ya wimbo yamenijia. Maneno ambayo nina hakika yaliimbwa na wanyama hapo zamani za kale na yamepotea baada ya vizazi vingi kupita. Nitajaribu kuwaimbia wimbo huo ndugu zangu. Ila mimi ni mzee na sauti yangu ni ya kukwaruza, lakini nikiwafundisha ala yake natumaini mtauimba vizuri zaidi. Wimbo wenyewe unaitwa Hayawani wa Uingereza."

Meja alikohoa kidogo kisha akaanza kuimba. Sauti ya meja ilikuwa ya kukwaruza lakini alijitahidi kuimba vizuri. Ulikuwa ni wimbo wa kuchangamsha sana.

Maneno yake yalikuwa kama ifuatavyo:

Hayawani wa nchi na nyanda zote
Sikilizeni ujumbe wangu wa shangwe
Ni kuhusu wakati mzuri ujao
Siku ile inakuja
Siku ya kumpindua binadamu mkatili
Ardhi nzuri ya uingereza, itakanyagwa na hayawani tu
Pete zitatoweka katika pua zetu
Na kamba kutoka migongoni mwetu
Vyuma vya kutuendesha vitaliwa na kutu
Mijeledi ya ukatili haitachapa tena
Utajiri usioelezeka
Ngano, shayiri na nyasi
Maharage, mizizi ya beet na matunda
Vitakuwa vyetu siku hiyo
Mashamba ya Uingereza yatameremeta
Maji yake yatakuwa safi
Pepo zake zitakuwa mwororo
Katika siku tutakayo kuwa huru

Sote tutapambana kwaajili ya siku hiyo
Hata tukifa kabla haijatokea
Ng'ombe na farasi, bata bukini bata mzinga
Wote watapambana kwaajili ya uhuru
Hayawani wa Uingereza, hayawani wa Ireland
Hayawani wa nchi na nyanda zote
Sikilizeni vizuri na enezeni ujumbe wangu
Ujumbe juu ya wakati bora ujao

Wimbo huu uliwapamdisha sana mori wanyama wote, na kabla Meja hajamaliza kuimba nao wakaanza kuuimba. Hata wanyama wajinga kabisa wakawa wameweza kuimba ala ile na maneno machache. Wanyama wenye akili kama mbwa na nguruwe waliweza kuimba wimbo wote ndani ya dakika chache tu.

Baada ya mazoezi kidogo, wanyama wote wakaimba Hayawani wa Uingereza pamoja kwa sauti kubwa. Kila mnyama alitia vionjo vyake. Wimbo ulikuwa umewapandisha mori kiasi kwamba waliimba mara tano mfululizo. Na bila kukatishwa wangeweza imba usiku kucha.

Kelele zao zikimuamsha bwana Jones. Bwana Jones aliamka haraka akifikiri labda mbwa mwitu amevamia shamba. Alichukua bunduki iliyokuwa kwenye kona chumbani mwake kisha akatoka na kupiga risasi hewani. Vipande vya risasi vikaruka na kugonga ukuta wa banda lile kubwa walilokuwepo wanyama. Wanyama wote wakatawanyika kila mmoja kwenye eneo lake la kulala. Shamba likawa kimya kabisa.
 
SURA YA PILI

Baada ya siku tatu mzee Meja akafariki akiwa usingizini. Mwili wake ukazikwa pembeni ya bustani. Ulikuwa ni mwanzo wa mwezi wa tatu. Kwa miezi mitatu iliyofuata vikao vingi vya siri vilifanyika. Hotuba ya Meja ilikuwa imetoa mwanga mpya kwa wanyama wenye uelewa. Lakini Walikuwa hawajui ni lini uasi uliotabiriwa na Meja utatokea. Hawakuwa na sababu ya kutarajia kuwa utatokea wakati wa maisha yao lakini walijua kuwa wana wajibu wa kufanya maandalizi yake. Kazi ya kufundisha na kuwapanga wengine iliwaangukia nguruwe, sababu walitambulika kama wanyama wenye akili kuliko wote.

Nguruwe wawili ndiyo walijulikana sana, nguruwe vijana, Snowball na Napolioni.

Napolioni alikuwa ni nguruwe mkubwa, si muongeaji lakini asiyependa kupingwa. Snowball yeye alikuwa ni mjanja kuliko Napolioni. Alikuwa muongeaji sana. Mwenye kuongea haraka haraka na mbunifu sana. tabia za wawili hawa zilikuwa tofauti sana. Nguruwe wengine wote walikuwa wa kawaida waliokuwa wakifugwa kwaajili ya nyama tu. aliyekuwa marufu kati yao alikuwa ni nguruwe mmoja mdogo na mnene aliyeitwa Mpayukaji. Mpayukaji alikuwa na mashavu manene, macho ya kung'aa, mwendo wa mikogo na kasauti kakali sana. Alikuwa ni fundi sana katika kuongea. Mara nyingi akiwa kwenye mabishano makali alikuwa na tabia ya kutembea huku huku, akichezesha mkia. Ilisemwa kuwa Mpayukaji aliweza kubadili nyeusi kuwa nyeupe kwa uongeaji wake.

Hawa nguruwe watatu ndiyo waliopanga mafundisho ya Meja katika mpangilio mzuri na kuyaita unyama. Kila baada ya bwana Jones kwenda kulala waliitisha vikao vya siri kwenye banda na kuwafundisha misingi ya unyama wanyama wengine. Walifanya hivyo kwa siku kadhaa kila wiki.

Mwanzoni walikutana na wanyama wasioelewa na wengine walikata tamaa. Wanyama wengine walianza kuongea kuwa wana wajibu wa kuwa waaminifu kwa bwana Jones amvaye walimwita, "Bwana." Walisema kuwa bwana Jones anawalisha na iwapo ataondoka basi watakufa kwa njaa.

Wengine waliuliza maswali kama, "Kwanini tujali juu ya mambo yatakayotokea baada ya sisi kufa?" Au "Kama haya mapinduzi yametabiriwa kutokea kwanini tujihangaishe nayo, si yatatokea hata tusipoyafanyia kazi?" Nguruwe walikuwa na wakati mgumu kuwaaminisha kuwa hicho ni kinyume cha kanuni za unyama. Maswali ya kijinga kabisa yaliulizwa na ng'ombe aliyeitwa Moli. Swali lake la kwanza kumuuliza Snowball lilikuwa: "Baada ya mapinduzi kutaendelea kuwa na sukari guru?"
"Hapana!" Alijibu Snowball kwa msisitizo. Hatuna namna ya kutengeneza sukari guru hapa shambani, hata hivyo huhitaji sukari guru ili kuishi, utakula majani na shayiri kadri uwezavyo."

"Je, bado nitaruhusiwa kuvaa utepe kwenye nywele zangu?" Akaendelea kuuliza Moli.

"Ndugu yangu," akasema Snowball, "Hizo tepe unazozipenda sana ni alama ya utumwa. Unashindwa kuelewa kuwa uhuru ni bora kuliko hizo tepe?"
Moli akakubaliana naye, lakini kishingo upande.

Kazi nyingine ngumu ya nguruwe ilikuwa kukabiliana na uongo ulioenezwa na Musa. Musa alikuwa ni kunguru kipenzi cha bwana Jones. Aliishi ndani kama mnyama kipenzi. Huyu alikuwa ni mpelelezi na msambaza majungu. Alikuwa ni ndege mwenye akili sana katika uongeaji. Alikuwa amedai kuwa anafahamu sehemu ambayo wanyama wakifa wanaenda. Alidai kuwa wanaenda kwenye nchi yenye mlima wa sukari guru. Akasema eneo hilo linapatikana angani ukipita mawingu. Alisema kuwa kwenye mlima wa sukari guru kila siku ni jumapili. Matunda yaliota mwaka mzima na keki zilikuwa zikiota kwenye miti ya uzio.

Wanyama wengi walimchukia Musa sababu alikuwa ni muongeaji tu bila kufanya kazi. Lakini wanyama wengine waliamini uwepo wa mlima wa sukari guru. Nguruwe walikuwa na kazi ngumu sana kuwaaminisha kuwa hamna sehemu kama hiyo.

Wanafunzi wao wazuri walikuwa ni farasi, Boxer na Clover. Hawa waliweza kumeza kila kitu wakichofundishwa na nguruwe, sababu ni kuwa hawakuwa na akili ya kufikiri wenyewe. Walikariri waliyofundishwa na kujaribu kuwafundisha wanyama wengine bila hata ya wao kuelewa vizuri. Walikuwa hawakosi kwenye vikao vya siri bandani na waliongoza wengine kuimba Hayawani wa Uingereza. Wimbo huu uliimbwa kila baada ya kikao.

Lakini bila kutarajia, mapinduzi yakatokea mapema. Miaka ya nyuma bwana Jones alikuwa ni mkulima hodari japo alikuwa ni mkali sana. Lakini siku za karibuni hakuwa sawa. Hivi karibuni alikuwa amepoteza pesa nyingi baada ya kushindwa kesi na akawa mtu wa kunywa pombe kupita kiasi. Siku nyingine alitumia siku nzima akiwa amekaa kwenye kiti jikoni akisoma magazeti, akinywa pombe na kumlisha Musa mikate aliyochoviwa kwenye bia. Watu wake wakaanza kuwa wazembe na wasio waaminifu. Mashamba yalijaa magugu na mapaa ya majengo yalihitaji ukarabati. Miti iliyopandwa kuzunguka wigo haikusafishwa na wanyama hawakulishwa vya kutosha.

Mwezi wa sita ulifika na nyasi zilikuwa tayari kuvunwa. Jumamosi moja bwana Jones alienda Willingdon katika baa iliyoitwa Simba Mwekundu. Huko akanywa pombe kupita kiasi. Hakurudi nyumbani hadi jumapili mchana. Wafanyakazi wake walikuwa wamewakamua ng'ombe kisha wakatoka kwenda kuwinda sungura, wala hawakukumbuka kulisha mifugo.

Bwana Jones aliporudi alikwenda moja kwa moja chumba cha maktaba na kulala kwenye sofa. Hata ilipofika jioni wanyama walikuwa bado hawajala. Mwishowe njaa ilipokuwa kali walishindwa kuvumilia. Ng'ombe mmoja alivunja mlango wa ghala la chakula kwa pembe zake na wanyama wote wakaanza kula. Muda huohuo bwana Jones naye akawa anaamka. Punde tu, yeye na wafanyakazi wake wanne wakawa wamefika kwenye ghala la chakula wakiwa na mijeledi na kuanza kuwachapa wanyama.

Hili jambo halikuwezwa kuvumiliwa na wanyama wale wenye njaa. Bila hata kuambiana waliwavamia watesi wao kwa pamoja. Ghafla bwana Jones na wafanyakazi wake wakajikuta wakipigwa na pembe na mateke kutoka pande zote. Hawajawahi kuona wanyama wakifanya jambo hili hapo kabla! Suala la wanyama waliozoea kuwachapa na kuwanyanyasa wapendavyo kuasi ghafla liliwaogopesha kupita kiasi. Baada ya kujaribu kujilinda kidogo wakakata tamaa na kuanza kutimua mbio. Ndani ya dakika chache, wote wakaanza kukimbia wakishika njia kuu ya kutokea shambani. Wanyama nao wakaanza kuwakimbiza wakiwa wamepata mori kwa ushindi.

Mke wa bwana Jones aliona hayo yote kupitia dirisha la chumbani. Harakaharaka alifunga vitu vichache kwenye mfuko na kukimbia kutoka shambani akipitia njia nyingine. Musa naye aliruka na kumfuata huku akipiga kelele. Wakati huo wanyama wakawa wamemkimbiza bwana Jones na watu wake hadi nje ya shamba na kufunga geti. Kabla hawajajua kilichotokea, mapinduzi yakawa yamefanyika kwa mafanikio: bwana Jones amefukuzwa na shamba la Mano ni lao. Kwa dakika kadhaa hawakuamini jambo lililotokea. Kitu cha kwanza walichofanya ni kuzunguka shamba lote kama vile walikuwa wanahakikisha kuwa hakuna binadamu aliyejificha sehemu. Hapo wakarudi kwenye majengo ya pale shambani ili kufuta kabisa mambo ya utawala wa bwana Jones. Chumba cha kutengenezea na kutunza vifaa vya kufungia wanyama kilivunjwa na kamba, minyororo ya kufungia mbwa, pete za puani, na visu vya bwana Jones alivyotumia kuhasi nguruwe na kondoo vilitupwa ndani ya kisima.

Mijeledi, vifaa vya kuongozea farasi, mifuko ya kuziba pua, na vingine vingi vikatupwa kwenye moto uliowashwa uwanjani. Wanyama walicheza kwa furaha walipoona mijeledi ikiungua moto. Snowball akatupa tepe ambazo zilitumika kuwapamba farasi siku za kwenda sokoni.

"Tepe," alisema, "Tepe zinatakiwa kuonwa kama ni nguo, na nguo ni alama ya binadamu. Wanyama wote wanatakiwa kuwa uchi."

Boxer aliposikia hili, alitoa kofia ndogo ya majani aliyokuwa akivaa majira ya joto ili kuzuia nzi, na akaitupa motoni.

Ndani ya muda mfupi wanyama wakawa wameharibu kila kitu kilichowakumbusha bwana Jones. Napoleoni akawaongoza kurudi ndani ya ghala la chakula. Kila mnyama alipewa mara mbili ya mahindi aliyopewa siku zote. Kila mbwa alipata biskuti mbili. Baada ya kushiba wakaimba Hayawani wa Uingereza mwanzo hadi mwisho mara saba mfululizo. Baada ya hayo wakalala usingizi kama vile hawajawahi lala maishani.

Alfajiri na mapema waliamka kama ilivyo kawaida yao. Walipokumbuka mambo mazuri yaliyotokea wakakimbia pamoja wakielekea malishoni. Kuelekea malishoni kulikuwa na sehemu yenye muinuko kidogo. Hapo iliwezekana kuona shamba lote. Wanyama wote wakakimbilia juu yake. Ni lao! Eneo lote waliloliona lilikuwa lao! Kwa furaha na mori walirukaruka na kujirusha kwa shangwe kubwa. Walijigaragaza kwenye umande huku wakila nyasi tamu za kiangazi. Walipiga mabonge ya udongo na kunusa harufu yake nzuri. Baada ya hapo wakazunguka shamba lote kulikagua huku wakistaajabia vitalu vya kulima mazao, vitalu vya nyasi, bustani, dimbwi na vichaka. Ilikuwa kama hawajawahi kuona vitu vile. Walikuwa bado hawaamini kuwa ni vyao.

Kutoka hapo wakaenda kwa pamoja mpaka kwemye nyumba ya bwana Jones na kusimama kimya mlangoni. Nyumba hii nayo ilikuwa yao, lakini walikuwa wanaogopa kuingia. Baada ya kitambo kidogo, Snowball na Napolioni wakapiga mlango kwa mabega yao na kuufungua. Wanyama wote wakaingia wakiwa mstari mmoja na walitembea kwa tahadhari kwa uoga wa kuharibu vitu. Walinyata chumba baada ya chumba. Walikuwa wakiongea kwa kunong'ona tu, wakiogopa kupiga kelele. Walishangazwa na vitu vya anasa vilivyokuwemo mule ndani. Waliangalia vitanda vyenye magodoro ya manyonya, vioo vya kujitizamia, sofa zilizotengenezwa kwa nywele za farasi. Mazuria kutoka Brussels, na picha ya malkia Viktoria iliyoning'inizwa kwenye chumba cha kusomea.

Wakati wa kutoka waligundua kuwa Moli haonekani. Waliporudi kutafuta walimkuta amebaki kwenye chumba kizuri cha mule ndani. Alikuwa amechukua tepe kutoka kwenye urembo wa mke wa bwana Jones. Alikuwa amezishika huku akijitizama kwenye kioo kwa kujikubali, alionekana kama mpumbavu.

Walipomuona walimsema na kumshutumu kisha wakatoka nje. Jikoni walikuta vipande vya nyama ya nguruwe vikining'inia, walivichukua na kwenda kuvizika. Debe la bia lililokuwa jikoni lilipigwa teke na Boxer hadi likabonyea-bonyea. Zaidi ya hayo, hawakugusa kitu kingine ndani ya nyumba. Walikubaliana wote kuwa nyumba ya bwana Jones iachwe na kuwa makumbusho, na wote walikubaliana kuwa hakuna mnyama anayeruhusiwa kuishi mule. Baada ya kupata kifungua kinywa, Snowball na Napolioni wakawaita wanyama wote pamoja.

"Ndugu-zanguni," alianza kusema Snowball, sasa ni saa kumi na mbili na nusu ya asubuhi, bado tuna siku ndefu sana. Leo tutaanza na uvunaji wa nyasi, lakini kabla ya hilo kuna jambo inatakiwa tulifanye kwanza."

Hapo nguruwe waliweka wazi kuwa kwa miezi mitatu iliyopita walikuwa wanajifunza kusoma na kuandika. Walisema walitumia kitabu cha kujifunzia walichotumia watoto wa bwana Jones, walikipata kwenye lundo la takataka. Napolioni akatuma yaletwe makopo ya rangi nyeusi na nyeupe kisha akaongoza njia kuelekea kwenye geti la kuingilia shambani. Snowball ambaye alikuwa anajua zaidi kuandika akachukua brashi aliyoishika kati ya kwato zake na kupaka rangi kufuta neno; SHAMBA LA MANO, na kisha kuandika SHAMBA LA WANYAMA.

Hilo ndilo lilikuwa jina la shamba kuanzia wakati huo. Baada ya hayo wakarudi kwenye lile banda kubwa la shambani, Snowball na Napolioni wakaagiza iletwe ngazi na kuegemezwa ukutani. Walisema kuwa kwa waliyojifunza kwa muda wa miezi mitatu iliyopita wameweza kuiweka kanuni ya unyama katika amri saba. Hizo amri saba zitaandikwa kwenye ukuta wa lile jengo kubwa. Hizo zitafanya sheria isiyobadilika ambayo wanyama waishio ndani ya shamba la wanyama wanapaswa kuifuata siku zote.

Kwa taabu(Sababu si rahisi kwa nguruwe kusimama juu ya ngazi) Snowball alipanda na kuanza kuandika. Chini yake alikuwako Mpayukaji akiwa ameshika makopo ya rangi. Aliandika kwa maneno makubwa yaliyoweza kusomeka hata unbali wa mita 30, aliandika hivi;

1. Chochote kinachotembea kwa miguu miwili ni adui.

2. Ni marufuku kwa mnyama yoyote kuvaa nguo.

3. Chochote kinachotembea kwa miguu minne au chenye mabawa ni rafiki.

4. Ni marufuku kwa mnyama kulala kitandani.

5. Ni marufuku kwa mnyama kunywa pombe.

6. Ni marufuku kwa mnyama kumuua mnyama mwingine.

7. Wanyama wote ni sawa.

Sheria iliandikwa vizuri sana kasoro herufi moja kwenye neno rafiki lilikuwa limekosewa. Lakini yote iliandikwa vyema. Baada ya kuandika, Snowball akaisoma kwa sauti kwa faida ya wengine. Walipoisikia wanyama wote wakatingisha vichwa kwa kukubaliana nayo, wale wenye akili wakaweza kuikariri.

"Sasa ndugu-zanguni," alisema Snowball kwa sauti kubwa na ya kuhamasisha huku akitupa chini brashi. "Kwenye mavuno ya nyasi! Acheni tuweke mfano kwa kuvuna kwa haraka kuliko bwana Jones na watu wake." Lakini sasa, ng'ombe ambao walikuwa wanahangaika sababu ya kutokamuliwa kwa masaa ishirini na nne wakaanza kupiga kelele. Viwele vyao vilikuwa vimejaa karibu kupasuka.

Baada ya kufikiria kidogo, Nguruwe wakaagiza ndoo ziletwe, kisha wakawakamua kwa ustadi wakitumia kwato zao. Punde, ndoo tano zikawa zimejaa maziwa yanayofuka povu. Wanyama wengi waliyaangalia kwa uchu.

"Tutayafanyia nini maziwa yote haya?" Aliuliza mnyama mmoja.

"Siku nyingine bwana Jones alikuwa anatuchanganyia kidogo kwenye chakula chetu," alisema kuku mmoja.

"Msijali kuhusu maziwa ndugu-zanguni!" Alisema Napolioni huku akisimama mbele ya ndoo za maziwa. "Hilo tutalishughulikia baadaye, jambo la muhimu ni mavuno ya nyasi, ndugu Snowball atatuongoza. Mimi nitafuata muda si mrefu. Shime, twendeni ndugu-zanguni! Nyasi zinatusubiri."

Hapo wanyama wakaanza kusonga kuelekea kwenye vitalu vya nyasi. Lakini ilipofika jioni waliona kuwa ndoo za maziwa zimetoweka.
 
Kitabu hiki kiliandikwa kama dhihaka dhidi ya ujamaa wa Soviet Union.

Bwana Jones alimuwakilisha Tsar aliyepinduliwa na wajamaa.

Meja alimuwakilisha Karl Marx.

Shamba la wanyama/ mano liliwakilisha Soviet union.

Shamba la Pinchfield liliwakilisha Ujerumani

Shamba la Foxwood liliwakilisha Uingereza/Marekani.
 
SURA YA TATU

Walifanya kazi ya kuvuna kwa bidii sana. Kazi yao ilikuwa nzuri na mavuno yalikuwa makubwa sana.

Sababu vifaa vya kuvunia vilibuniwa kwaajili ya kutumia binadamu akiwa kasimama kwa miguu miwili, haikuwezekana kwa wanyama kuvitumia. Lakini pamoja na hayo, nguruwe walibuni njia nzuri ili kurahisisha kazi. Farasi walilijua shamba vizuri na walifanya kazi ya kuvuna vizuri, pengine zaidi ya bwana Jones na watu wake. Nguruwe wao hawakufanya kazi bali waliwaelekeza na kuwasimamia wengine. Sababu wao ndiyo walikuwa wenye akili zaidi, kazi ya uongozi iliwaangukia.

Boxer na Clover walijishikiza kwenye kifaa cha kukatis nyasi (hakukuwa na vifaa ya kwafunga kwenye vyombo hivyo)na kutembea kuzunguka wakikata nyasi. Nguruwe walifuata nyuma yao wakipaza sauti na kuwahamasisha wakisema, "mbele, mbele ndugu!" Au "nyuma sasa ndugu!"

Wanyama wote, hadi wadogo kabisa walishiriki uvunaji na kukusanya nyasi. Hata bata na kuku walifanya kazi siku nzima juani. Walibeba nyasi ndogondogo kwa midomo yao. Walitumia muda pungufu kwa siku mbili ya muda waliozoea kutumia bwana Jones na watu wake. Pia yalikuwa ni mavuno makubwa kuliko yote katika historia ya shamba. Hakukuwa na upotevu wowote sababu bata na kuku waliokota nyasi zote, pia hakukuwa na mnyama aliyeiba zaidi ya kula kidogo tu.

Majira yote ya joto kazi ziliendelea bila kukoma, na wanyama walikuwa na furaha sana. Kila mlo ulikuwa ni wenye kuburudisha, chakula chao na matunda ya kazi yao, si chakula cha kugawiwa na bwana mwenye kinyongo. Sasa baada ya binadamu mnyonyaji kuondoka, kulikuwa na chakula cha kutosha kila mmoja. Pia muda wa kupumzika ulikuwa mwingi zaidi. Lakini kazi yao haikuwa rahisi, na sababu ya kukosa uzoefu walikutana na vikwazo vingi. Mfano; walipokuwa wakipukuchua mahindi iliwabidi wayapukuchue kizamani(kwa kukakanyaga na kuyapiga) na kupepeta kwa kupuliza na midomo yao. Lakini akili ya nguruwe na nguvu za Boxer zilifanya yote hayo yawezekane.

Boxer alikubalika na kusifiwa na kila mnyama. Toka enzi za bwana Jones alikuwa ni mfanyakazi mwenye bidii, lakini sasa alifanya kazi kama vile ni farasi watatu ndani ya mmoja. Kuna siku ambazo kazi zote za shamba zilimtegemea yeye. Toka asubuhi hadi jioni alikuwa akivuta hiki au kusukuma kile. Muda wote alikuwepo sehemu ambapo kazi ilikuwa ngumu zaidi.

Alikuwa amemuambia jogoo mmoja awe anamuamsha nusu saa kabla ya muda wa kawaida. Hilo ni ili ajitolee kufanya kazi kwenye sehemu zilizohitaji msaada kabla ya siku ya kazi kuanza. Jibu lake kwa matatizo yote na vikwazo vyote lilikuwa, "Nitafanya kazi kwa bidii!" Hiyo ndiyo ilikuwa kauli mbiu yake.

Lakini si yeye tu, wanyama karibu wote walifanya kazi kwa bidii kadiri ya uwezo wao. Mfano, kuku na bata waliokoa magunia matano ya mahindi wakati wa mavuno kwa kuokota kila punje. Hakuna aliyekuwa akiiba wala aliyekuwa akinung'unika juu ya gawio lake.

Ugomvi, kuumizana na wivu, vitu vikivyozoeleka wakati wa bwana Jones vilikuwa kama vimetoweka. Hakuna aliyetegea kazi isipokuwa wachache tu. Moli! Moli alikuwa anachelewa sana kuamka na alikuwa na tabia ya kuwahi kuondoka kazini akisingizia kuna jiwe limemuingia kwenye kwato. Paka naye hakuwa na tabia njema. Iligundulika kuwa, kila kunapokuwa na kazi za kufanya paka alikuwa haonekani, alipotea kwa muda mrefu na kuonekana wakati wa chakula au jioni kazi ilipokwisha kama vile hamna hamna cha ajabu alichofanya. Lakini mara zote alitoa visingizio vizuri kiasi kwamba haikuwa rahisi kutomuamini.

Benjamini yeye aliendelea na maisha yake kama tu alivyokuwa akiishi kabla ya mapinduzi. Alifanya kazi zake polepole, na hakukubali kupelekeshwa kama alivyokuwa akifanya kipindi cha bwana Jones. Hakutegea lakini pia hakujitolea kufanya kazi zaidi. Hakutoa maoni yoyote kuhusu mapinduzi na maisha mapya. Alipoulizwa kama hafurahishwi na kuondoka kwa bwana Jones yeye alijibu, "Punda huishi muda mrefu sana, kati yenu hakuna ambaye ameona punda aliyekufa." Iliwabidi wanyama wengine kuridhika na majibu yake tata.

Jumapili ilikuwa ni siku ya mapumziko. Kifungua kinywa kilichelewa kwa muda wa saa moja na baada ya kifungua kinywa kulikuwa na sherehe iliyofanyika kila jumapili. Kwanza walianza kwa kupandisha bendera. Snowball alikuwa amepata kitambaa cha mezani na akakichora picha ya kwato na pembe kwa rangi nyeupe. Bendera hii ilipandishwa kila jumapili saa mbili asubuhi kwenye bustani karibu na nyumba ya bwana Jones. Rangi ya kitambaa cha bendera ilikuwa ni kijani. Snowball alisema kuwa inawakilisha uoto wa nchi ya Uingereza na pembe na kwato ziliwakilisha jamhuri ya wanyama ambayo itasimama Uingereza baada ya binadamu kupinduliwa. Baada ya kupandisha bendera wanyama wote walielekea kwenye lile banda kubwa kwaajili ya mkutano. Hapa walipanga kazi za wiki inayofuata na kujadiliana. Mara nyingi nguruwe ndiyo walikuwa wanafanya mipango na kuamua mambo yaende namna gani. Wanyama wengine walijua jinsi ya kupiga kura lakini hawakujua jinsi ya kupanga mipango na kutoa hoja.

Snowball na Napolioni ndiyo walikuwa hasa wakiendesha mijadala. Lakini ilionekana kuwa hakuna jambo walilokuwa wakikubaliana. Chochote alichoongea mmoja wao mara zote ilitazamiwa mwingine kupinga.

Kulikuwa na mjadala mkali juu ya umri sahihi wa kustaafu wa kila mnyama. Mara zote mkutano uliisha kwa kuimba Hayawani wa Uingereza na kisha wakaenda kujiburudisha siku nzima.

Nguruwe waliifanya ile stoo ya vifaa vya kufungia wanyama kuwa makao yao makuu. Muda wa jioni waliutumia humo wakijifunza ufundi chuma, useremala na stadi zingine. Walijifunza kutoka kwenye vitabu walivyochukua nyumbani mwa bwana Jones. Snowball alijishughulisha pia na kupanga wanyama katika kamati mbalimbali. Alikuwa na bidii sana na suala hili. Aliunda kamati ya uzalishaji wa mayai kwaajili ya kuku na bata, akaanzisha jumuia ya mikia misafi kwaajili ya ng'ombe, pia kukawa na kamati ya kuwaelimisha ndugu wa porini. Kazi ya kamati hii ilikuwa ni kuwastaarabisha panya na sungura. Pia alianzisha vuguvugu la sufi nyeupe kwaajili ya kondoo, na nyingine nyingi ikiwemo kuanzisha madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika.

Kiujumla, kamati zote hizi zilifeli. Mpango wa kuwastaarabisha sungura na panya ulishindwa mara tu ulipoanzishwa. Waliendelea na tabia zao za porini na walipoonyeshwa ustaarabu wao walitumia kama fursa.
Paka alijiunga na kamati hii na alikuwa mwenye bidii sana. Siku moja alionekana kwenye paa akiongea na shomoro waliokuwa mbali kidogo naye. Alikuwa akiwaambia kuwa sasa wanyama wote ni ndugu, na shomoro yoyote anayependa anaweza kutua kwenye miguu yake, lakini shomoro wale hawakuthubutu.

Madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika yalipata mafanikio fulani. Kufikia majira ya kupukutika, karibu wanyama wote wakawa na uwezo fulani wa kusoma. Nguruwe wote walikuwa wakisoma na kuandika vizuri kabisa. Mbwa waliweza kusoma kiasi lakini hawakupenda kusoma zaidi ya kusoma zile amri saba tu.

Muriel, yule mbuzi alikuwa anaweza kusoma vizuri zaidi ya mbwa, na muda mwingine wakati wa jioni alikuwa akiwasomea wengine kutoka kwenye vipande vya magazeti alivyopata jalalani. Benjamini aliweza kusoma kama tu nguruwe lakini hakutaka kabisa kujishughulisha na kusoma. Alikuwa akisema hakuna kitu cha maana cha kusoma.

Katika kujifunza kusoma, Boxer hakuweza kujifunza kupita herufi D. Aliweza kutambua A,B,C na D, kufika hapo alikwama kuendelea, akibaki kushangaa akijaribu kwa uwezo wake wote kukumbuka herufi inayofuata bila mafanikio. Kuna wakati aliweza kujifunza E, F, G na H, lakini alipojifunza hizo alijikuta kasahau A, B, C, na D. Mwishowe akakata tamaa na kuridhika na kujua herufi nne za mwanzo tu. Hizo alijizoeza kuziandika kila siku ili asizisahau.

Moli yeye alikataa kabisa kujifunza zaidi ya herufi nne zinazounda jina lake. Alikuwa akikusanya vijiti na kuunda jina lake vizuri kabisa chini na kisha akalipamba kwa maua. Hapo alianza kulizunguka akilistaajabia.

Wanyama wengine wote waliobaki hakuna aliyeweza kujifunza zaidi ya herufi A. Pia ilionekana wanyama wajinga kabisa kama kondoo, kuku na bata walishindwa hata kukariri zile amri saba. Baada ya kutafakari sana, Snowball akaona kuwa zile amri saba zinaweza kuwekwa katika sentensi moja:

"Miguu minne rafiki, miguu
miwili adui."

Alisema sentensi hii imebeba kanuni yote ya unyama. Yeyote aliyeielewa ataepuka ushawishi wa binadamu. Mara ya kwanza ndege walipinga wakisema wao nao wana miguu miwili, lakini Snowball akawahakikishia kuwa haiko hivyo.

"Ndugu-zanguni, mabawa ya ndege ni kiungo kwaajili ya mwendo na si kiungo cha kufanyia hila. Kwa mantiki hiyo kinachukuliwa kama ni miguu. Tofauti yetu kubwa na binadamu ni mikono yake, hiyo ndiyo anatumia kufanya hila zake."
Ndege hawakuelewa maelezo marefu ya Snowball lakini walikubaliana nayo. Wanyama wote wajinga wakaanza kufanya bidii kukariri, 'MIGUU MINNE RAFIKI, MIGUU MIWILI ADUI'

Maneno hayo yaliandikwa juu ya zile amri saba lakini kwa herufi kubwa zaidi. Kondoo walipoweza kuyakariri maneno hayo waliyapenda sana, na mara nyingi waliyasema kwa kurudiarudia.

"Miguu minne rafiki, miguu miwili adui. Miguu minne rafiki, miguu miwili adui." Waliyasema bila kuchoka.

Napolioni yeye hakujihusisha na kamati za Snowball. Alisema kuwa kuwaelimisha watoto ni muhimu zaidi ya kuhangaika na wanyama waliokua.
Katika kipindi hicho, baada ya mavuno, Jessie na Bluebell walikuwa wamezaa jumla ya watoto tisa. Mara tu walipowaachisha kunyonya, Napolioni akawachukua na kusema litakuwa ni jukumu lake kuwaelimisha. Aliwachukua na kuwapeleka kwenye chumba cha ghala la vifaa na kuwaweka darini. Waliweza kufikiwa kwa ngazi tu. Walikaa huko na baada ya muda mfupi wanyama wakasahau uwepo wao.

Baada ya muda mfupi ilijulikana mahali ambapo maziwa yalikuwa yanaenda. Yalikuwa yakichanganywa na chakula cha nguruwe kila siku. Pia matofaa yalikuwa yameanza kuiva na kuanguka bustanini. Yalikuwa yametapakaa chini. Wanyama walifikiri kwamba yatagawiwa sawa kwa sawa kwa wanyama wote. Kinyume na matarajio yao, siku moja likatoka tamko kuwa matofaa yote yakusanywe na kuwekwa katika chumba ambacho ndiyo makao makuu ya nguruwe. Kuna baadhi ya wanyama walilalamika kwa chinichini juu ya hiki lakini haikusaidia kitu.

Nguruwe wote walikubaliana juu ya uamuzi wa kuchukua matofaa. Hata Snowball na Napolioni walikubaliana juu ya hili. Mpayukaji alitumwa kwenda kuwaeleza wanyama wengine sababu ya nguruwe kuchukua matofaa yale.

"Ndugu-zanguni!" Alianza kusema. "Nadhani hamfikiri kuwa nguruwe tumechukua maziwa na matofaa yote kwa sababu ya ubinafsi na kujipendelea. Kwanza wengi wetu hatupendi maziwa na matofaa. Mimi mwenyewe sivipendi vitu hivyo. Lengo letu la kuchukua vitu hivyo ni kwaajili ya afya yetu. Sayansi imeonyesha kuwa ndani ya maziwa na matofaa kuna vitu ambavyo ni muhimu sana kwa afya ya nguruwe. Nguruwe tunafanya kazi kwa kutumia akiki. Mambo yote hapa shambani yanatutegemea ili yaende. Usiku na mchana tuko macho kushughulikia maslahi yenu. Kwa hiyo ni kwaajili yenu ndiyo maana tunakunywa maziwa na kula matofaa. Mnajua kitakachotokea iwapo tukishindwa kufanya kazi yetu vizuri? Bwana Jones atarudi! Ndiyo ndugu-zanguni, bwana Jone atarudi!" Aliongea Mpayukaji kama vile anawasihi huku akienda huku na huku na mkia wake ukicheza. "Nina hakika hakuna mnyama kati yenu anayependa bwana Jones arudi."

Kwa kweli hakuna mnyama hata mmoja aliyetamani bwana Jones arudi. Ilipozungumzwa hatari ya bwana Jones kurudi hakuna aliyesema neno kupingana na nguruwe. Umuhimu wa kuwaweka nguruwe katika afya njema ulionekana. Kwa hiyo wote wakakubaliana kuwa maziwa na matofaa yote yaliyodondoka na yatakapovunwa yatakuwa kwa ajili ya nguruwe tu.
 
SURA YA NNE

Mwishoni mwa majira ya joto taarifa za kilichotokea kwenye shamba la wanyama ilikuwa imeenea karibu nusu ya nchi yote. Kila siku Napolioni na Snowball walituma njiwa kwenda kwa wanyama wa mashamba ya jirani. Waliagizwa kuwaeleza kuhusu mapinduzi na kuwafundisha ala ya Hayawani wa Uingereza.

Katika kipindi hiki chote bwana Jones alikuwa anatumia muda mwingi kunywa pombe. Alikuwa anakaa kwenye chumba cha kunywea pombe katika baa ya Simba mwekundu huko Willingdon. Alikuwa akilalamika kwa yeyote aliyemsikiliza. Alilalamika jinsi ambavyo hakutendewa haki na kufukuzwa kwenye shamba lake na wanyama wasio na shukrani. Wakulima wengine walimuonea huruma lakini hawakumpa msaada wowote. Vichwani mwao walikuwa wakiwaza jinsi wanavyoweza kutumia janga la bwana Jones kujinufaisha. Bahati nzuri ni kuwa wamiliki wa mashamba yaliyopakana na bwana Jones walikuwa na uadui. Shamba moja lililoitwa Foxwood lilikuwa ni kubwa sana. Liliendeshwa kizamani na halikutunzwa vizuri. Mmiliki wake, bwana Pilkington alikuwa ni mtu asiyejali. Muda mwingi alitumia kuwinda au kuvua samaki, kulingana na msimu.

Shamba lingine liliitwa Pinchfield. Lilikuwa ni dogo na lilitunzwa vizuri. Mmiliki wake, bwana Frederick alikuwa ni mshupavu na mjanja sana. Alikuwa ni mtu wa kupenda kesi na kudai fidia kubwakubwa.

Wawili hawa hawakupendana, hivyo ilikuwa vigumu kwao kushirikiana kwa faida ya wote.

Pamoja na hilo, wote walikuwa wameogopeshwa na uasi uliotokea kwenye shamba la Mano. Na walijitahidi wanyama wao wasijifunze juu ya uasi huo. Mwanzoni walicheka na kukejeli suala la wanyama kuendesha shamba. Walisema ndani ya siku arobaini watakuwa wameshindwa kujiendesha. Kwanza walikataa kabisa kuliita shamba la wanyama. Walisisitiza kuliita shamba la Mano. Walisema kuwa wanyama ndani ya shamba la Manor walikuwa wakipigana siku zote na walikuwa karibu kufa kwa njaa.

Lakini baada muda kupita na wanyama wakawa hawajafa kwa njaa, bwana Frederick na bwana Pilkington wakabadili maneno. Wakaanza kusema juu ya mambo mabaya yanayoendelea kwenye shamba la Mano. Walisema kuwa wanyama walikuwa wakilana wao kwa wao, wakitesana kwa kuchomana na vyuma vya moto na walikuwa wakishirikiana majike. "Hayo ndiyo madhara ya kupingana na asili," walisikika wakisema.

Lakini habari hizo hazikuaminiwa zote. Kulikuwa na tetesi juu ya shamba zuri. Shamba ambalo binadamu amefukuzwa na wanyama wanajiendesha wenyewe. Habari hizo zilisambaa na katika mwaka huo kulikuwa na vuguvugu kotekote mashambani.

Mafahali wakaanza kuwa jeuri, kondoo walivunja uzio na kula matunda, Ng'ombe walipiga mateke ndoo za maziwa na farasi nao waligoma kuruka vizingiti na kuwatupa huko waliowapanda.

Na kubwa zaidi ni kuwa ala na hata maneno ya Hayawani wa Uingereza yalianza kujulikana kila mahali. Wimbo ulikuwa umesambaa kwa kasi ya ajabu.

Binadamu hawakuweza kuzuia hasira zao walipousikia wimbo huo, japo walijidai kwamba ni kitu cha kuchekesha tu. Walisema inawezekanje wanyama wakaimba kitu cha hovyo namna ile. Mnyama yoyote aliyekutwa akiuimba aliadhibiwa vikali kwa fimbo. Pamoja na hayo wimbo uliendelea kusambaa. Ndege wengi kwenye uzio waliuimba , njiwa nao waliuimba. Hata wahunzi chuma walipoponda na kengele za kanisa zilipolia, ilisikika ala yake. Binadamu walipousikia walitetemeka kwa hofu. Walikuwa wakisikia maneno ya utabiri wa kiama chao.

Mwanzoni mwa mwezi wa kumi, wakati ambao mahindi yalikuwa yameshavunwa na kuhifadhiwa na mengine yameshapukuchuliwa, lilikuja kundi la njiwa kwenye shamba la wanyama na kutua likiwa limehamaki.

Wakasema kuwa bwana Jones na watu wake wote, na wengine kutoka mashamba ya Foxwood na Pinchfield wameingia shambani na wanakuja huku. Wote waneshika fimbo isipokuwa bwana Jones, yeye yupo mbele na ameshika bunduki. Bila shaka walikuwa wanataka kukomesha uasi na kurejesha shamba kwa bwana Jones.

Jambo hilo lilitegemewa kutokea na maandalizi yote muhimu yalikuwa yamefanyika.

Snowball ambaye alikuwa amesoma kitabu cha zamani kinachohusu vita alivyopigana Kaisari, alichokuwa amekipata ndani ya nyumba ya bwana Jones, akawa kiongozi wa ulinzi. Haraka alitoa amri na ndani ya dakika chache kila mnyama akawa kwenye eneo lake. Binadamu walipokaribia kwenye majengo ya shambani Snowball akatuma kikosi chake cha kwanza.

Njiwa wote waliokaribia thelathini na tano waliruka na kuwazonga watu vichwani. Wakati watu wakipambana na hiki, bata bukini waliokuwa wamejificha kwenye miti ya uzio wakatokea na kuanza kuwadonoa vikali miguuni, Lakini hili lilikuwa ni shambulio dogo tu lenye lengo la kuzua taharuki. Hivyo watu walifanikiwa kuwatimua bata bukini kwa fimbo zao. Sasa Snowball akatuma kikosi cha pili, Muriel, Benjamin, Kondoo wote na Snowball akiwaongoza wakawashambulia binadamu kwa pembe na mateke toka pande zote. Lakini watu kwa kutumia fimbo na viatu vyao vyenye soli za chuma walifanikiwa kuwashinda, na Snowball akawaamuru warudi nyuma.

Binadamu walipiga kelele kwa shangwe ya ushindi baada ya kuona adui zao wakikimbia. Bila mpangilio wakaanza kuwakimbiza. Hilo ndilo jambo ambalo Snowball alilitaka, mara tu walipoingia uwanjani, farasi watatu, ng'ombe watatu, na nguruwe ambao walikuwa wanavizia walitoka na kuwashanbulia ghafla watu wale kutokea nyuma. Snowball naye akaashiria kikosi chake waache kukimbia na kugeuka kushambulia, yeye mwenyewe akakimbia kumshambulia bwana Jones. Bwana Jones akawa amemuona, akainua bunduki yake na kupiga. Vipande vya risasi vikampata Snowball mgongoni na kuacha damu ikichuruzika, na kondoo mmoja akaanguka amekufa. Bila kusimama, Snowball akamrukia bwana Jones miguuni na akamrusha kwenye lundo la kinyesi huku bunduki ikimtoka mkononi.

Lakini aliyeogopesha zaidi ni Boxer. Alikuwa akisimama kwa miguu ya nyuma na kupiga kwa kutumia ya mbele. Pigo lake la kwanza lilimpata mtu mmoja kutoka shamba la Foxwood kichwani na kumtupa chini akiwa hajitambui. Baada ya kuona hivyo baadhi ya watu wakatupa fimbo zao na kujaribu kukimbia. Wakawa wametaharuki, wakati huohuo wanyama wote wakaanza kuwashambulia pale uwanjani, waliwang'ata, waliwapiga mateke na kuwakanyaga. Hakuna mnyama ambaye hakushiriki kulipa kisasi. Hata paka naye aliruka toka kwenye paa na kumrukia mtu mmoja begani, akazamisha kucha zake shingoni mwake. Mtu yule alipiga kelele za kutisha sana. Upenyo ulipoonekana watu walitimua mbio kuelekea nje ya shamba.

Ndani ya dakika tano wakawa tayari wanakimbia kupitia njia waliyoijia. Nyuma, bata bukini waliwakimbiza na kuwadonoa miguuni. Watu wote wakakimbia isipokuwa mmoja. Pale uwanjani, Boxer alikuwa akijaribu kumgeuza yule mtu aliyempiga ambaye alikuwa anelala kifudifudi matopeni. Alimgeuza lakini hakugeuka wala kutikisika.

"Amekufa,"akasema Boxer kwa masikitiko, "sikuwa na nia ya kumuua, nilisahau kama nilikuwa na vyuma miguuni. Nani ataniamini kuwa sikudhamiria kumuua?"

"Ndugu hakuna haja ya kunung'unika!" Alisema Snowball ambaye bado damu ilikuwa inamtoka kwenye majeraha yake. "Vita ni vita. Binadamu mzuri ni yule aliyekufa."

"Sikutaka kabisa kumuua, hata kama ni binadamu," alisema tena Boxer huku machozi yakimtoka.

"Moli yuko wapi?" Aliuliza mnyama mmoja kwa sauti ya hamaki.

Moli alikuwa haonekani na hilo likazua taharuki. Waliogopa labda binadamu wamemdhuru au wamemchukua na kwenda naye. Lakini baadaye walimpata akiwa kajificha bandani mwake huku kichwa kakizamisha kwenye nyasi. Alikuwa amekimbilia bandani mara tu aliposikia mlio wa bunduki.

Wanyama waliporudi uwanjani wakamkuta yule mtu aliyelala chini ametoweka. Kumbe alikuwa amezimia tu.

Sasa wanyama wakakusanyika wakiwa na shangwe sana. Kila mmoja akisimulia matendo yake katika vita ile kwa sauti ya juu kabisa. Sherehe ya ghafla ya kusherekea ushindi iliandaliwa harakaharaka. Bendera ilipandishwa na Hayawani wa Uingereza ukaimbwa nara kadhaa. Baada ya hapo, wakamzika yule kondoo aliyekufa kwa heshima na kupanda mti juu ya kaburi lake. Kisha Snowball akatoa hotuba fupi. Alisisitiza umuhimu wa wanyama wote kuwa tayati kufa kwaajili ya shamba la wanyama itakapobidi. Baada ya hilo wanyama wakakubaliana kuanzisha nishani za kijeshi. Wakatengeneza medali za shaba. "mnyama shujaa daraja la kwanza." Nishani hiyo ilitolewa palepale kwa Snowball na Boxer. Ilikuwa ni medali.

Ilitakiwa kuvaliwa jumapili na siku za sikukuu. Pia kulikuwa na "Mnyama shujaa daraja la pili." Hii ilitolewa kwa yule kondoo aliyefariki.

Kulikuwa na majadiliano juu ya jina la kuiita vita ile. Mwishowe wakakubaliana kuiita vita ya kibanda cha ng'ombe sababu hapo ndipo walipojificha wale wanyama waviziaji. Bunduki ya bwana Jones ilipatikana ikiwa imelala matopeni, na wanyama walijua kuwa ndani ya nyumba ya bwana Jones kuna akiba ya risasi. Wakakubaliana kuiweka bunduki ile chini ya nguzo ya bendera iwe kama ni mzinga, na wataipiga mara mbili kwa mwaka. Tarehe 12 ya mwezi wa kumi, kama kumbukumbu ya vita ya kibanda cha ng'ombe, na katikati ya kipindi cha majira ya joto kama kumbukumbu ya mapinduzi yao.
 
SURA YA TANO

Kadri majira ya baridi yalivyokaribia ndivyo Moli alivyozidi kuwa mtata. Alichelewa kazini kila siku na kujitetea kuwa alipitiwa na usingizi. Pia alikuwa akilalamika kuhusu maumivu yasiyoeleweka japo chakula alikula vizuri tu. Alikuwa akitoa visingizio vya kila namna na kuondoka kazini mapema. Aliomdoka akielekea kwenye lambo la maji. Hapo alikuwa akitazama taswira yake majini kama mpumbavu.

Lakini pia kulikuwa na tetesi kuhusu jambo moja zito. Siku moja Moli alipokuwa akipita uwanjani huku akichezesha mkia wake kwa madaa, Clover alimuita pembeni.

"Moli," alianza kusema, "Nina jambo moja la muhimu ningependa nikuambie. Leo asubuhi nimekuona karibu na uzio ukiangalia kwenye shamba la Foxwood. Mfanyakazi mmoja wa Pilkington alikuwa upande wa pili, nilikuwa mbali lakini niliona akiongea na wewe na niliona ukimruhusu akupapase puani. Hilo lina maana gani Moli?"

"Hakufanya! Sikuwa mimi! Si kweli!" Alijibu Moli huku akichimbachimba chini kwa kwato zake.

"Moli! Niangalie usoni. Unaapa kuwa yule mtu alikuwa hakupapasi puani?"

"Si kweli!" Alijibu Moli lakini hakuweza kumuangalia Clover usoni, kisha akakimbia akielekea mashambani. Clover akapata wazo, na bila kuwaambia wengine akaenda kwenye kibanda cha Moli na kupekua kwenye nyasi za kulalia. Humo alikuta kipande cha sukari guru na tepe nyingi za rangi mbalimbali.

Baada ya siku tatu Moli akatoweka. Kwa wiki kadhaa hakuna aliyejua alikokwenda, lakini baadaye njiwa walikuja na taarifa kuwa wamemuona upande wa pili wa mji wa Willingdon. Alikuwa amefungwa kwenye mkokoteni mdogo.

Mtu mmoja nadhifu aliyeonekana kama ni mwanasiasa alikuwa akimpapasa puani na kumlisha sukari guru. Moli alikuwa amevaa tepe ya rangi nyekundu angavu, alionekana ni mwenye furaha sana. Hakuna mnyama aliyemtaja Moli tena.

Mwezi wa kwanza baridi ilikuwa kali sana. Ardhi iliganda na kuwa ngumu kama chuma. Kazi za shambani zilisimama sababu hakuna ambacho kingeweza kufanyika. Mikutano mingi ilifanyika ndani ya banda kubwa na nguruwe walikuwa wanashughulika muda wote wakipanga mipango ya kazi kwaajili ya msimu ujao. Ilikuwa imeshakubalika kuwa nguruwe ndiyo watakuwa wanapanga mipango yote kuhusu shamba, sababu wao ndiyo walionekana kuwa na akili kuliko wanyama wote. Lakini ilikubaliwa kuwa maamuzi yao lazima yapitishwe kwa kupigiwa kura. Mpango huu ungefanya kazi vizuri sana kama kungekuwa hakuna uhasama kati ya Snowball na Napolioni. Hawa walipingana karibu kwa kila kitu.

Kama mmoja alitoa wazi la kupanda shamba kubwa la shayiri, mwingine atataka shamba kubwa la uwele. Mwingine akisema shamba hili au lile linafaa kwa kabeji mwingine atasema halifai kitu isipokuwa mazao ya mizizi. Kila mmoja alikuwa na wafuasi wake na kulikuwa kunatokea majibizano makali sana. Mara nyingi Snowball alishinda kwa hotuba zake zenye nguvu, lakini Napolioni naye alikuwa yupo vizuri kwa kuvuta wafuasi upande wake. Wafuasi wake wazuri walikuwa ni kondoo. Siku hizo kondoo walikuwa wakisema "Miguu minne rafiki, miguu miwili adui" muda wote. Na hata walikuwa wakikatisha mikutano kwa kusema hivyo. Iligundulika kuwa walitamka sana haya maneno wakati hotuba za Snowball zinapokolea.

Snowball alikuwa amejifunza vitu vingi kutoka katika vitabu alivyovipata ndani ya nyumba ya bwana Jones. Hilo lilimfanya kuwa na mipango mingi ya kuboresha hali ya shamba. Alizungumza kuhusu mifumo ya kutolea maji, utunzaji wa majani mabichi, na alikuwa na mpango tata wa jinsi ya kufanya wanyama wadondoshe kinyesi chao moja kwa moja shambani eneo tofautitofauti kila siku. Alisema kusudi ni kupunguza kazi ya kusombelea mbolea. Napolioni yeye hakuwa na mipango yoyote lakini alikuwa anasema mipango ya Snowball haitafanikiwa na alionekana kuwa anasubiri kwa hamu hilo litokee. Lakini katika ubishani wote, hakuna uliokuwa mkubwa kama uliohusu ujenzi wa kinu cha upepo.

Umbali kidogo kutoka kwenye majengo ya shambani kulikuwa na muinuko mdogo. Hapo ndipo palikuwa sehemu iliyoinuka zaidi shambani. Baada ya kulichunguza eneo lile, Snowball akasema linafaa sana kujenga kinu cha upepo. Alisema kinu hicho kitaendesha dynamo ambayo itazalisha umeme kwaajili ya matumizi shambani.

Alisema hilo litasaidia kuwasha taa vibandani, kuwapasha joto wakati wa baridi, kuendesho msumeno, kuendesha mashine ya kukatia mabua, na mashine ya kukamulia maziwa.

Wanyama walikuwa hawajawahi kusikia kuhusu hivi sababu shamba lao lilikuwa ni la kizamani. Walisikiliza kwa kustaajabu Snowball alipokuwa akiwaeleza kuhusu mashine hizo za ajabu, mashine ambazo zitafanya kazi huku wao wakistarehe na kula majani shambani, au wakijielimisha kwa kujisomea na kujadiliana.

Ndani ya wiki mbili Snowball akawa amekamilisha kuandaa mpango wake wa kinu cha upepo. Alijifunza namna ya kuunda kinu hicho kutoka katika vitabu vitatu vya bwana Jones. Vitabu hivyo vilikuwa ni; umeme kwa wanaoanza, kila mtu ni mfyatua tofali na vitu elfu moja vyenye faida kufanya nyumbani.

Snowball alitumia chumba kilichokuwa kikitumika kutotoleshea mayai kama maktaba yake. Kulikuwa na sakafu ya mbao hivyo ilifaa sana kwa kuchora. Alitumia masaa mengi sana humo akijifunza na kubuni. Alikuwa akichora sakafuni kwa kutumia chaki alizoshika kwa kwato zake. Polepole mchoro ukawa mkubwa na tata, ukionyesha mashine na vitu mbalimbali. Wanyama wengi hawakuelewa kilichochorwa lakini walikistaajabia sana.

Wengi walifika kuona mchoro ule. Hata kuku na bata walifika kujionea, huku wakijitahidi wasiukanyage.

Ni Napolioni pekee ndiye hakujali, yeye toka mwanzo alikuwa anapingana mpango wa kujenga kinu cha upepo. Siku moja aliingia kwenye chumba kilichochorwa mpango na kuanza kuukagua. Aliuchunguza wote na kuguna kwa kebehi. Kisha akainua mguu mmoja na kuukojolea mchoro ule na kutoka nje bila kusema neno.

Shamba lote lililkuwa limegawanyika kuhusu ujenzi ujenzi wa kinu cha upepo. Snowball hakubisha kuwa kujenga kinu cha upepo itakuwa n kazi ngumu. Kutakuwa na kazi ya kubeba mawe, kujenga ukuta, watahitaji kujenga tanga, na kisha vitahitajika dynamo na nyaya. (Snowball hakusema vitu hivi vitapatikanaje) Lakini alisisitiza kuwa kazi inaweza fanywa ndani ya mwaka mmoja, na pia akasema umeme utarahisisha sana kazi kiasi kwamba wanyama watahitajika kufanya kazi siku tatu tu kwa wiki. Napolioni yeye alibisha na kusema kitu cha muhimu kwa wakati huo ni kuongeza uzalishaji wa chakula, na kuwa wakipoteza muda kwa kujenga kinu cha upepo watakufa njaa. Sasa wanyama wakawa wamegawanyika katika kambi mbili, "chagua Snowball na siku tatu kwa wiki," na "chagua Napolioni na chakula tele." Benjamini peke yake ndiye hakuwa na upande. Hakuamini kama chakula kitakuwa tele wala kuwa kinu cha upepo kitarahisisha kazi. Kuwe na kinu cha upepo au kusiwepo, maisha yataendelea kama yalivyo, machungu.

Mbali na ugomvi juu ya kinu cha upepo, kulikuwa na suala la ulinzi wa shamba. Walitambua kuwa, japo binadamu wameshindwa kwenye vita ya kibanda cha ng'ombe, lakini wanaweza kufanya shambulio lingine kubwa zaidi na kumrudisha bwana Jones. Walikuwa na kila sababu ya kufanya hivyo sababu habari za kushindwa kwao zilikuwa zimeshaenea mashambani kote. Hilo lilifanya wanyama katika mashamba yanayowazunguka kuwa wajeuri sana. Kama kawaida, Napolioni na Snowball walipingana juu ya hili.

Napolioni yeye alisema kinachotakiwa kufanywa, ni wanyama kununua bunduki na kujifunza kuzitumia. Snowball yeye alisema wanatakiwa kutuma njiwa kwa wingi na kuchochea uasi kwenye mashamba mengine. Napolioni alisema kama hawataweza kujilinda lazima watapinduliwa. Snowball yeye aliendelea kusema kuwa, kama uasi utaenea kila sehemu hawatakuwa na haja ya kujilinda.

Wanyama wakawa wamechanganyikiwa, hawakujua wa kumuunga mkono, na ilionekana walikubaliana na yule aliyekuwa akiongea kwa wakati huo.

Siku ikafika ambayo mpango wa Snowball wa kinu cha upepo ukawa umekamilika. Jumapili iliyofuata kura ikapigwa iwapo kinu cha upepo kijengwe au kisijengwe. Wanyama walikusanyika ndani ya lile banda kubwa, Snowball akasimama kuongea. Japo alikatishwa mara kwa mara na kondoo, lakini aliweza kutoa sababu zake kwanini kinu cha upepo kijengwe. Baada ya kumaliza, Napolioni naye akasimama kutoa hoja zake. Akasema kuwa kinu cha upepo ni upuuzi mtupu hivyo akashawishi wanyama wasipige kura kukiunga mkono. Aliongea kama kwa nusu dakika tu, na alionekan hajali kama kawashawishi au la.

Hapo Snowball akasimama tena huku akiongea kwa sauti kubwa, maana kondoo walianza tena kusema, "miguu minne rafiki, miguu miwili adui." Akazungumza kiufundi akitetea ujenzi wa kinu cha upepo. Kufikia hapo wanyama walikuwa wamegawanyika nusu nusu katika kupinga na kuunga mkono ujenzi wa kinu. Lakini baada ya maneno yenye ushawishi ya Snowball wakaanza kumuunga mkono. Katika maongezi yake aliwajengea picha ya jinsi shamba la wanyama litakavyokuwa iwapo umeme ukisaidia kupunguza mzigo wa kazi.

Aliongeza kuwa umeme utasaidia kuvuta jembe la kulimia, kuendesha mashine ya kupukuchulia, uvunaji, kupakia, kila banda litakuwa na taa ya umeme, maji ya moto na baridi, na mashine ya umeme ya kupasha joto. Alipomaliza kuongea kulikuwa hakuna shaka kuwa wanyama watapiga kura upande upi. Napolioni alipoona hivyo akamkata Snowball jicho kali na kisha akapiga mbinja ambayo hakuna aliyewahi akipiga hapo kabla. Ghafla ikatokea sauti ya kutisha kutoka nje ya banda na kisha mbwa tisa wakubwa wakaingia kwa kishindo ndani ya banda. Moja kwa moja walimrukia Snowball ambaye aliruka na kukwepa meno yao chupuchupu. Kufumba na kufumbua akawa nje akikimbia huku mbwa wale wakimfukuza. Wanyama wote wakapigwa na butwaa wasiweze kusema chochote. Wakakusanyika mlangoni kuona mfukuzano ule. Snowball alikuwa akikimbia kupita eneo pana la malisho kwenda nje ya shamba. Alikimbia kadri ya uwezo wote wa nguruwe na mbwa walikuwa nyuma yake wakimfukuza. Ghafla akateleza na kuanguka, ilionekana kuwa ndiyo mwisho wake, lakini akainuka tena na kukimbia kwa kasi zaidi. Mmoja wa mbwa wale akawa karibu kumuuma mkia lakini akawahi kuukwepesha na kuongeza kasi. Hapo akawa amefika kwenye uzio wa shamba na akapenya kwenye nafasi ndogo na kutokomea, hakuwahi kuonekana tena.

Wanyama wakarudi bandani huku wakiwa kimya na waliojaa woga. Punde kidogo mbwa nao wakarudi. Mwanzoni hakuna aliyeelewa walipotoka viumbe hawa lakini iligundulika haraka; walikuwa ni wale mbwa watoto ambao Napolioni aliwachukuwa na kwenda kuwalea mafichoni. Japo walikuwa hawajakomaa sana lakini walikuwa wakubwa kwa umbo na wakali sana. Walionekana kama mbwa mwitu. Walikuwa karibu sana na Napolioni. Walionekana wakitingisha mikia walipomuona kama vile tu mbwa walipokuwa wakitingisha mikia walipomuona bwana Jones.

Sasa Napolioni na mbwa wale wakiwa wanamfuata akapanda kwenye jukwaa, lile alilokaa Meja alipokuwa akitoa hotuba yake. Akasema kuwa kuanzia sasa hakutakuwa na mkutano wa jumapili asubuhi. Alisema haikuwa na umuhimu na ilipoteza muda.

Alisema kuwa masuala yote yanayohusiana na shamba yataamuliwa na kamati maalumu ya nguruwe itakayoongozwa na yeye. Kamati hiyo itakutana kwa siri na kisha kutoa maamuzi yao kwa wengine. Wanyama wataendelea kukusanyika siku za jumapili asubuhi kwaajili ya kupandisha bendera, kuimba Hayawani wa Uingereza, na kupokea maelekezo ya juma linalofuata, lakini hakutakuwa na majadiliano.

Mbali na bumbuwazi walilopigwa nalo kwa kufukuzwa kwa Snowball, wanyama walishangazwa sana na tukio hili. Wengi wangepinga iwapo wangekuwa na uwezo wa kujenga hoja. Hata Boxer hakufurahia hili. Alijitahidi kwa uwezo wake wote kujenga hoja kichwani wala hakuweza, akaishia kutingisha kichwa.

Nguruwe wao hawakupata taabu kuwaza la kusema. Nguruwe wanne waliokuwa mbele walipiga kelele za kupinga na wote wakasimama na kuanza kuongea kwa pamoja. Lakini ghafla mbwa waliokaa kumzunguka Napolioni wakaunguruma muungurumo wa kutisha na nguruwe wale wakanyamaza na kukaa chini.

Hapo kondoo kwa ghafla wakaanza kusema, "Miguu minne rafiki, miguu miwili adui". Walisema hivyo kwa kurudia karibu robo saa nzima na hivyo kuzuia majadiliano yoyote.

Baadaye Mpayukaji alitumwa kuzunguka shambani kuwafafanulia wengine mfumo mpya wa mambo.

"Ndugu-zanguni,"alisema. "Naamini kila mnyama anathamini jinsi ndugu Napolioni alivyojitolea kufanya kazi zote hizi peke yake. Ndugu zangu, msidhani uongozi ni kitu cha raha. Ni kinyume chake, uongozi ni mzigo mzito wa majukumu. Hakuna anayeamini kuwa wanyama wote ni sawa kama ndugu Napolioni. Wala hakuna anayefurahia akiona mkifanya maamuzi yenu wenyewe kama yeye. Lakini nyakati nyingine mnaweza kufanya maamauzi mabaya. Hapo tutajikuta katika hali gani? Mfano mngechagua kumfuata Snowball na hekaya zake za kinu cha upepo, Snowball ambaye sasa tumejua alikuwa ni mhalifu tu!"

"Lakini alipigana kishujaa kwenye vita ya kibanda cha ng'ombe." Alisema mnyama mmoja.

"Ushujaa tu hautoshi," akasema Mapayukaji. "Ushikamanifu na utii ni muhimu zaidi. Na kuhusu vita ya kibanda cha ng'ombe, naamini itafika wakati ambao tutaona jinsi mchango wa Snowball ulivyokuzwa. Nidhamu ndugu-zanguni, nidhamu! Hilo ndilo jambo la maana sana. Tukiteleza tu adui atatudhukia. Je, ndugu zangu, mnataka bwana Jones arudi?"

Kwa mara nyingine hoja hii ilishindwa kujibiwa. Hakuna mnyama aliyetaka bwana Jones arudi. Na kama kufanya mikutano jumapili asubuhi kunaweza kumrudisha basi ni bora mikutano isiwepo.

Boxer ambaye sasa alikuwa ameweza kufikiria aliongea yaliyomo moyoni mwa wenzake kwa kusema. "Kama ndugu Napolioni amesema hivyo basi itakuwa sahihi." Na kutoka siku hiyo akawa na msemo, "mara zote Napolioni yupo sahihi." Akiwa ameongeza kwenye kaulimbiu yake ya, "nitafanya kazi kwa bidii."

Muda huo tayari majira ya baridi yalikuwa yamekwisha na majira ya kuchipua yakaanza. Kazi za kulima zikaanza. Chumba ambacho Snowball alichora mchoro wa kinu cha upepo kilifungwa, na ikadhaniwa kuwa ule mchoro umefutwa.

Kila jumapili, saa nne asubuhi wanyama wote walikusanyika kwenye banda kubwa kupata maagizo yao ya wiki inayofuata. Fuvu la Meja ambalo sasa lilikuwa limetoka nyama zote lilifukuliwa na kuwekwa chini ya bendera pembeni ya bunduki. Na kila baada ya bendera kupandishwa wanyama walitakiwa kupita mbele ya fuvu kutoa heshima zao wakielekea bandani.

Siku hizo wanyama wote hawakukaa pamoja kama ilivyozoeleka. Napolioni, Mpayukaji na nguruwe mwingine aliyeitwa Minimus walikaa mbele ya jukwaa. Walikuwa wanazungukwa na wale mbwa. Huyu Minimus alikuwa hodari sana katika kutunga nyimbo na mashairi.

Nguruwe wengine walikaa nyuma yao. Wanyama wengine wote walikaa kutazamana na nguruwe. Napolioni alikuwa akisoma maagizo kwa ukali na amri kama mwanajeshi, na baada ya hapo waliimba Hayawani wa Uingereza mara moja na kutawanyika.

Kwenye wiki ya tatu ya kufukuzwa kwa Snowball, wanyama walishangaa kusikia Napolioni akitangaza kuwa kinu cha upepo kinatakiwa kujengwa. Hakutoa sababu yoyote ya kubadili maoni yake bali alisema kuwa kazi hii ya ziada itakuwa ngumu sana. Pia alizungumza umuhimu wa kupunguza ukubwa wa posho. Lakini wakati anatangaza hayo tayari mpango kazi ulikuwa tayari. Kamati maalumu ya nguruwe ilikuwa imefanya kwa wiki tatu zilizopita kuandaa. Ilionekana kuwa ujenzi wa kinu cha upepo na maboresho mengine vitachukua miaka miwili.

Usiku ule Mpayukaji aliwaeleza wanyama wengine kuwa Napolioni hakuwa anapinga ujenzi wa kinu cha upepo. Na badala yake yeye ndiye aliyeanzisha wazo la kujengwa kwake, na kuwa ule mchoro aliouchora Snowball alikuwa kauiba katika nyaraka za Napolioni. Hivyo, kinu cha upepo ni wazo la Napolioni. Mnyama mmoja alipouliza sasa ni kwanini aliupinga ujenzi vikali sana:

Mpayukaji akajibu, "zinaitwa mbinu! Mbinu ndugu-zanguni." Akasema ile ilikuwa ni mbinu na lengo lilikuwa ni kumtimua Snowball. Alisema Snowball alikuwa ni hatari na mchochezi. Lakini sasa kwa sababu Snowball hayupo, mpango utaendelea bila bughudha zake. Mpayukaji akasema hizo zinaitwa mbinu na alirudia neno hilo mara nyingi. "Mbinu ndugu-zanguni, mbinu!" Huku akitembea huku na huku, akichezesha mkua na kujichekesha. Wanyama hawakujua mbinu ni nini lakini Mpayukaji alikuwa kaongea kwa ushawishi sana na mbwa watatu ambao walikuwa naye wakaunguruma kwa kitisho hivyo wakakubaliana na maelezo yake bila maswali zaidi.
 
SURA YA SITA

Mwaka ule wanyama walifanya kazi kama watumwa. Pamoja na hilo lakini walifurahia kazi yao. Walijua kila walichofanya kilikuwa ni kwa faida yao wenyewe na vizazi vyao, na si binadamu wavivu na waporaji. Majira yote ya kuchipua na majira ya joto walifanya kazi kwa bidii kubwa. Walifanya kazi masaa sitini kwa juma. Ilipofika mwezi wa nane Napolioni akatangaza kuwa watafanya kazi na jumapili mchana. Hizi kazi zitakuwa ni ya kujitolea, lakini mnyama ambaye hatazifanya mgao wake wa chakula utapuguzwa nusu. Pamoja na bidii zote lakini iliwalazima kazi zingine kutozifanya.

Mavuno ya mwaka huo hayakuwa mengi kama ya mwaka uliopita na mashamba mawili yaliyotakiwa kupandwa hayakupandwa sababu yalichelewa kulimwa. Ilionekana kuwa wakati wa majira ya baridi kutakuwa na hali ngumu sana.

Matatizo yasiyotegemewa yaliibuka kwenye ujenzi wa kinu cha upepo. Kulikuwa machambo mazuri tu ya mawe pale shambani. pia walipata mchanga na saruji ya kutosha waliyopatw ghalani. Mahitaji yote kwaajili ya ujenzi walikuwa nayo. Tatizo la kwanza lilikuwa ni jinsi ya kukata mawe kuwa vipande vinavyofaa kujengea, wanyama hawakujua jinsi ya kufanya hivyo.

Njia pekee ya kufanya hivyo ilionekana ni kutumia mitalimbo. Lakini hakuna mnyama aliyeweza kutumia sababu ilihitaji kusimama kwa miguu miwili. Baada ya kuhangaika kwa wiki kadhaa bila mafanikio, mmoja wao akapata wazo. Lilikuwa ni kuyainua juu kwa kamba na kisha kuyaachia yapondeke vipandevipande.
Vipande. Ilikuww ni kazi ngumu na ya polepole sana. Mara nyingine walitumia siku nzima kupandisha jiwe moja juu. Na mara nyingine mawe hayakuvunjika.

Vipande vilivyopatikana vilisafirishwa kirahisi kwa mkokoteni uliovutwa na farasi. Kondoo walivuta jiwe moja moja, na Muriel na Benjamini walijifunga kwenye mkokoteni mdogo na kuvuta mawe. Mwishoni mwa majira ya joto wakawa wamekusanya mawe ya kutosha na ujenzi ukaanza chini ya usimamizi wa Nguruwe.

Ujenzi ulikuwa ni kazi ngumu na ulienda polepole sana.

Boxer alikuwa msaada mkubwa sana na bila yeye hakuna ambacho kingefanyika. Ilionekana kuwa ni mwenye nguvu kuliko wanyama wote wakiwekwa pamoja.

Kwa mara kadhaa Clover alimuonya kuwa asifanye kazi kupita kiasi lakini Boxer hakumsikikiza. Kaulimbiu zake mbili za, "nitafanya kazi kwa bidii" na "mara zote Napolioni yupo sahihi," zilikuwa ni jibu la matatizo yake yote. Kipindi hiki alikuwa amekubaliana na yule jogoo kuamshwa dakika arobaini na tano kabla ya muda wa kazi, na si nusu saa kama hapo awali.

Na katika muda wa mapumziko, ambao hata hivyo ulikuwa ni mchache, alikuwa akienda mwenyewe kwenye shimo la mawe kukusanya na kuyavuta mpaka kwenye eneo la ujenzi peke yake. Katika mahira hayo ya joto, wanyama hawakuwa na hali mbaya licha ya kazi ngumu walizofanya. Hata kama hawakuwa na chakula cha kutosha, lakini hakikuwa pungufu ya kile walichopata enzi za bwana Jones.

Kitendo cha kuacha kuwalisha binadamu watano walafi kiliwafaa sana upande wa chakula. Na pia wanyama walifanya kazi kwa ufanisi zaidi ya kipindi cha bwana Jones. Mfano; kazi ya palizi ilifanywa kwa ufanisi mkubwa ambao binadamu hangeweza. Na kwa sababu hakuna mnyama aliyekuwa akiiba, kukawa hakuna ulazima wa kutenganisha eneo la malisho na shamba. Hili lilisaidia kupunguza kazi ya kutunza na kurekebisha uzio, na mageti yake. Pamoja na hayo, majira ya joto yalipokaribia kwisha upungufu ukaanza kuonekana.

Kulikuwa na uhitaji wa mafuta ya taa, misumari, kamba, biskuti za mbwa na chuma kwaajili ya viatu vya farasi. Vitu hivyo vyote hawakuweza kuvitengeneza shambani. Pia baadaye ilitarajiwa uhitaji wa mbegu, mbolea ya kiwandani pamoja na vifaa vingine vya kinu cha upepo. Hakuna aliyejua vitu hivi vitapatikana namna gani.

Asubuhi moja ya jumapili, wanyama walipokuwa wamekusanyika kupata maagizo yao, Napolioni alifika. Alisema kuwa kuna sera mpya. Alisema kuanzia siku hiyo shamba la wanyama litajihusisha kufanya biashara na mashamba ya jirani. Na lengo siyo biashara na faida bali ni kupata vitu muhimu ambavyo hawana.

Alisema kuwa mahitaji ya kinu cha upepo ni muhimu kuliko kitu kingine chochote. Hivyo basi, alikuwa na mpango wa kuuza sehemu ya akiba ya nyasi na ngano. Na kama pesa zaidi zitahitajika basi atauza na mayai huko Willingdon. Alisema kuku wanatakiwa kuona fahari kujitolea mayai yao kwaajili ya ujenzi wa kinu cha upepo.

Kwa mara nyingine wanyama walitatizwa na maagizo hayo. Walitambua kuwa ni marufuku kufanya makubaliano yoyote na binadamu, kufanya biashara na kutumia pesa. Je, hayo si ndiyo yalikuwa maazimio ya kwanza kabisa kupitishwa baada ya kumfukuza bwana Jones? Wanyama wote walikumbuka kupitishwa kwa maazimio hayo, au walidhani walikumbuka hivyo.

Nguruwe wanne, wale ambao hapo kabla walipinga Napolioni kupiga marufuku vikao vya jumapili, walipaza sauti zao, japo kwa uoga kupinga. Lakini walinyamazishwa na kuunguruma kwa mbwa. Kisha kama kawaida yao, kondoo wakaanza kusema. "miguu minne rafiki, miguu miwili adui!" hapo dintofahamu ile ikatulia. Mwishowe Napolioni akawanyoshea ishara ya kuwanyamazisha na kusema tayari amekwisha fanya mipango yote. Hakutakuwa na ulazima wa mnyama yeyote kukutana na binadamu, kitu kisichotakiwa kabisa. Mambo yote atafanya yeye mwenyewe. Bwana Whymper, ambaye ni mwanasheria kutoka Willingdon amekubali kuwa wakala kati ya shamba la wanyama watu wengime. Hivyo atatembelea shamba kila jumatatu asubuhi kupokea maagizo. Napolioni alihitimisha hotuba yake kwa kauli aliyozoea kusema. "Lidumu shamba la wanyama!" Na kisha wakaimba Hayawani wa Uingereza na kutawanyika.

Baadaye Mpayukaji alipita kuzunguka mabandani kuwatuliza wanyama. Aliwahakikishia kuwa azimio la kutojihusisha na biashara halijawahi kupitishwa wala kupendekezwa lipitishwe. Ni wazo lililojengeka vichwani mwa wanyama lakini halikuwepo, na pengine lilianzishwa na uongo wa Snowball. Wanyama wachache walikuwa bado wana mashaka lakini Mpayukaji aliwauliza hivi kwa akili. "Ndugu-zanguni, mna uhakika kuwa hili si jambo mliloliota? Mnao ushahidi kuhusu kupitishwa kwa azimio hilo? Wapi liliandikwa?"kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa maandishi kuonyesha kuwa azimio lile lilipitishwa, wanyama wakaridhika na kukubali kuwa wao ndiyo wamekosea.

Kila jumatatu bwana Whymper alifika shambani kama ilivyokubaliwa. Alikuwa ni mtu mmoja mfupi na mjanja-mjanja, na mustachi wake ulikuwa mrefu. Alionekana kama mwanasheria hasa. Alikuwa ni mjanja kwa kujua mapema kuwa shamba la wanyama litakuwa na uhitaji wa wakala, na ada itakuwa nzuri sana.

Wanyama walikuwa wanamuangalia anapokuja na kuondoka kwa hofu sana. Walimuepuka kadri walivyoweza. Pamoja na hilo, walijisikia fahari walipomuona Napolioni akiwa amesimama kwa miguu minne na kumpa maagizo bwana Whymper aliyesimama kwa miguu miwili. Hilo liliwafanya kwa kiasi fulani wakubaliane na huu mpango wa biashara. Sasa uhusiano wao na binadamu umebadilika. Si ule wa hapo mwanzo kabla ya mapinduzi.

Kustawi kwa shamba haikuwa sababu ya binadamu kuacha kulichukia shamba la wanyama. Badala yake hilo lilifanya walichukie hata zaidi. Kila binadamu alikuwa anaamini kuwa shamba la wanyama litashindwa kujiendesha na kufirisika. Walisema kuwa mradi wa kinu cha upepo nao hautafanikiwa.
Walikuwa wakikutana na kuaminishana kuwa, kulingana na michoro yake, kinu cha upepo kitaanguka. Na iwapo kitasimama basi hakitafanya kazi.

Walisema hayo yote lakini mioyoni mwao walikuwa wakisifia jinsi wanyama wanavyoendesha mambo yao kwa ufanisi. Na kuonyesha hilo walikuwa wameanza kuliita shamba la wanyama na si shamba la Mano. Pia waliacha kumuunga mkono bwana Jones ambaye hata hivyo alikuwa amekata tamaa ya kupata shamba lake. Alikuwa ameenda kuishi sehemu nyingine ya nchi.

Isipokuwa kupitia bwana Whymper, hakukuwa na mawasiliano mengine kati ya shamba la wanyama na watu wengime, lakini kulikuwa na tetesi kuwa Napolioni alikuwa anataka kuingia kwenye makubaliano ya kibiashara na bwana Pilkington wa shamba la Foxwood, au bwana Frederick wa shamba la Pinchfield, lakini si wote kwa pamoja.

Ilikuwa ni kipindi hichi ambapo bila kutegemewa, nguruwe wakahamia kwenye nyumba ya bwana Jones na kuanza kuishi humo. Kwa mara nyingine wanyama wakakumbuka kuwa kulikuwa na azimio kupinga jambo hili. Lakini Mpayukaji akaweza kuwaaminisha kuwa hakukuwa na kitu kama hicho. Alisema kwa sababu nguruwe walikuwa wakitumia akili kuendesha shamba, kulikuwa na umuhimu wapate eneo tulivu la kufanyia kazi zao. Na pia lilikuwa ni jambo la heshima kwa kiongozi(alikuwa ameanza kumuita Napolioni kiongozi) kuishi ndani ya nyumba na si kwenye banda la nguruwe. Pamoja na hayo bado kulikuwa na wanyama ambao hawakuridhika. Hasa waliposikia kuwa, si tu nguruwe wanapata chakula chao jikoni na wanatumia cha kusomea kama sehemu ya burudani, bali pia wameanza kulala vitandani . Boxer yeye hakujali na aliendelea kusema, "Mara zote Napolioni yupo sahihi." Lakini Clover ambaye alifikiri kuna sheria inayokataza kulala vitandani, alienda pembeni ya lile banda kubwa na kusoma zile sheria saba. Baada ya kuona hana uwezo wa kusoma zaidi ya kutambua herufi tu, akaenda kumuita Muriel.

"Muriel naomba unisomee amri ya nne. Haisemi kuwa ni marufuku kulala kitandani?" kwa shida Muriel akaisoma.

"Inasema, 'Ni marufuku kwa mnyama kulala kitandani na kujifunika mashuka.'''

Kwa mbali Clover akawa hakumbuki kama sheria ya nne inataja kuhusu mashuka. Lakini kama imeandikwa hivyo ukutani pale bila shaka ilikuww hivyo tokea mwanzo. Wakati huo Mpayukaji alikuwa anapita pale akiwa ameongozana na mbwa wawili hivyo akasaidia kuliweka swala lile sawa.

"Ndugu-zanguni, mmesikia kuwa siku hizi nguruwe tunalala vitandani ndani ya nyumba? Kwani kuna tatizo? Sidhani kama mnafikiri kuna sheria inayokataza kulala vitandani? Vitanda ni sehemu tu ya kulala. Hata lundo la nyasi bandani ni kitanda. Sheria ilikataza juu ya mashuka, kitu ambacho ni kazi ya binadamu. Tumetoa mashuka yote vitandani na tunalala kwa kutumia mablanketi tu. Ni vitanda vizuri lakini si kama tulivyotaka. Nawaambieni ndugu zangu, kwa jinsi akili zetu zinavyofanya kazi siku hizi, tulihitaji usingizi mzuri kabisa. Hamuwezi kutunyima hilo, sivyo? Hamtataka tuwe tumechoka na hivyo kufanya kazi kizembe si ndiyo? Nina hakika hamna mmoja kati yenu anayetaka bwana Jones arudi." Aliposema hivyo wanyama wakakubaliana naye mara moja na suala la nguruwe kulala vitandani halikuzungumzwa tena.

Siku chache mbele likatoka tamko kuwa nguruwe watakuwa wanachelewa kuamka kwa saa moja zaidi ya muda wa kawaida, hakuna mnyama aliyepinga. Majira ya kupukutika yalipofika, wanyama walikuwa wamechoka lakini ni wenye furaha. Mwaka huo ulikuwa mgumu sana kwao. Baada ya kuuza nyasi na mahindi, maghala yalibakiwa na chakula kichache sana. Lakini kinu cha upepo kilikuwa kimefikia nusu kujengwa.

Baada ya mavuno kulikuwa na hali nzuri ya hewa kwa muda kidogo. Wanyama walitumia muda huo kufanya kazi kwa bidii zaidi.

Boxer alifanya kazi hata usiku, alifanya hadi masaa mawili ya ziada akitumia mwanga wa mwezi. Wakati wa mapumziko wanyama walikuwa wakitembea kuzunguka kinu cha upepo huku wakikistaajabia. Walishangaa jinsi kilivyo imara na kizuri. Hawakuamini kama ni wao wamejenga kitu bora namna ile. Ni Benjamini tu ndiye ambaye hakupatwa na matumaini juu ya kinu cha upepo. Na kama kawaida yake, hakusema maneno mengi zaidi ya kusema kuwa punda huishi miaka mingi.

Mwezi wa kumi na moja ukafika na upepo uliovuma kutoka kusini magharibi ukaanza. Ilibidi kazi ya ujenzi isimame sababu ulisababisha unyevuunyevu mwingi sana hivyo haikuwezekana kuchanganya saruji. Na usiku mmoja upepo ulikuwa mkali sana hadi majengo ya shambani yakawa yanatikisika. Baadhi ya vigae vikang'oka katika majengo.

Usiku ule kuku waliruka kwa taharuki, wote walikuwa wameota wamesikia mlio wa bunduki kwa mbali. Asubuhi wanyama walipotoka mabandani wakakuta nguzo ya bendera imeangushwa. Ghafla wanyama wote wakalia kwa uchungu mkubwa. Walikuwa wameona kitu cha kuhuzunisha kabisa. Jengo la kinu cha upepo lilikuwa limeharibiwa vibaya. Hapo wakakimbia kwenda kuangalia. Napolioni ambaye alikuwa akitembea mara chache ndiye alikuwa mbele akikimbia. Tazama! Kazi ngumu waliyofanya ilikuwa imeshushwa hadi kwenye msingi. Mawe waliyobeba kwa taabu yalikuwa yametawanyika huku na huko. Hakuna aliyeweza kuongea neno, walibaki wakishangaa kwa huzuni. Napolioni alikuwa akitembea huku na huku akiwa kimya kabisa, huku mkia wake umemkaza, ishara kuwa akili yake ilikuwa inafanya kazi kwa kasi. Ghafla akatulia kama vile amegundua kitu.

"Ndugu-zanguni," alisema kwa utulivu. "Mnamjua anayehusika na jambo hili? Mnamjua adui aliyekuja usiku na kubomoa kinu chetu? Ni SNOWBALL!" Alitaja jina hilo kwa sauti kubwa ya kuunguruma.

"Snowball ndiye aliyefanya jambo hili! Amefanya kwa husda tu ili kuturudisha nyuma na kulipa kisasi kwa kufukuzwa kwa aibu. Msaliti yule amejipenyeza usiku na kuharibu kazi tuliyofanya kwa mwaka mzima. Sasa ndugu zanguni, leo natangaza hukumu ya kifo kwa Snowball. Mnyama yeyote atakayemuua atapata nusu ya gunia la matofaa na nishani ya mnyama shujaa daraja la pili: gunia zima kwa atakayemkamata akiwa hai."

Wanyama walipigwa na bumbuwazi kugundua kuwa Snowball anaweza kufanya tendo kama lile. Kulikuwa na vilio vya uchungu na hasira, na kila mmoja akaanza kuwaza njia ya kumkamata Snowball kama ikitokea amerejea tena. Muda si mrefu alama za kwato za nguruwe zikawa zimegunduliwa. Zilionekana zinaelekea kwenye upenyo uliokuwa kwenye uzio.

Napolioni alizinusa na kusema ni za Snowball. Akasema Snowball atakuwa alitokea Shamba la Foxwood.

"Basi tusichelewe ndugu-zanguni!" Alisema Napolioni kwa sauti kubwa baada ya kuchunguza zile alama za kwato. "Kazi lazima iendelee. Asubuhi hii hii tutaanza kujenga tena kinu cha upepo, tutajenga majira yote ya baridi, lije jua, ije mvua. Tutamfundisha msaliti huyu kuwa hawezi kukwamisha kazi yetu kirahisi. Fahamuni ndugu-zanguni, lengo letu halitabadilika. Itafanyika kama tulivyopanga. Haya shime ndugu-zanguni! Kidumu kinu cha upepo! Lidumu shamba la wanyama!"
 
SURA YA SABA

Majira ya baridi yalikuwa makali sana. Upepo mkali ulivuma ukiambatana na theluji. Ardhi iliganda na kujaa barafu ambayo haikuyeyuka hadi mwezi wa pili. Licha ya hilo wanyama bado walifanya kazi kwa bidii sana kujenga upya kinu cha upepo.

Walijua kuwa watu wa nje ya shamba wanawafuatilia na wangefurahi sana iwapo kinu cha upepo kisingemalizika kwa wakati.

Kwa chuki tu, binadamu waligoma kuamini kuwa Snowball ndiye aliyeharibu kinu cha upepo: walisema kuwa ukuta ulianguka kwa sababu ulikuwa mwembamba sana. Wanyama waliamini hiyo siyo sababu, lakini hata hivyo waliamua kuongeza unene wa ukuta mara mbili. Kutoka nchi kumi na nane hadi nchi thelathini na sita. Hilo lilisababisha wakusanye mawe mengi zaidi. lakini kwa muda fulani hawakuweza kufanya chochote sababu machimbo ya mawe yalifunikwa na barafu. Ilipoyeyuka kidogo wakaanza kazi. Ilikuwa ni kazi ngumu kuliko yoyote waliyowahi kufanya.

Walipigana sana na baridi na mara nyingi walishinda njaa. Ni Boxer na Clover tu ndiyo hawakukata tamaa. Mpayukaji alitoa hotuba nzuri sana juu ya fuhari, utumishi na heshima viletwavyo na kazi. Lakini hasa wanyama wengine walitiwa moyo na jinsi Boxer alivyokuwa akijituma, na kaulimbiu yake ya, "nitafanya kazi kwa bidii!"

Ulipofika mwezi wa kwanza chakula kikawa kimepungua sana. Gawio la mahindi likapunguzwa, na ikatangazwa kuwa ili kufidia, wataongeza viazi kwenye posho. Lakini baadaye ikagundulika kuwa sehemu kubwa ya viazi ilikuwa imeharibiwa na baridi kali sababu havikufunikwa vizuri, vilikuwa vimelainika na kubadilika rangi.

Hali yao ilikuwa mbaya sana, nyakati nyingine hawakuwa na chochote cha kula isipokuwa mabua tu. Baa la njaa lilikuwa mlangoni mwao.

Ilikuwa ni muhimu sana kuficha hali hii isijulikane nje ya shamba. Baada ya kinu cha upepo kuanguka, binadamu wakaanza kutunga uongo mwingi kuhusiana na shamba la wanyama. Ilisemwa kuwa wanyama walikuwa wakifa kwa njaa na magonjwa, na kwamba muda wote wanapigana na wameanza kulana na kula watoto wao. Napolioni alijua madhara yake iwapo hali ya chakula ingejulikana. Hivyo akaamua kumtumia bwana Whymper kusambaza habari tofauti. Kwa kawaida wanyama walikuwa hawaonani na bwana Whymper, walimuona mara chache sana, lakini safari hii kondoo wachache waliandaliwa ili kujisemeshasemesha mbele yake kuwa chakula ni kingi na cha kutosha shambani pale. Napolioni pia aliagiza kwamba vyombo ambavyo ni tupu vijazwe mchanga, na kisha kuwekwa nafaka kwa juu. Whymper alitembezwa ili aweze kuona vyombo hivyo vilivyojaa chakula. Kwa udanganyifu huo aliendelea kutoa taarifa kuwa kwenye shamba la wanyama hakuna upungufu wa chakula.

Katika siku hizo Napilioni akawa anaonekana mara chache sana. Muda mwingi alikuwa akijifungia kwenye nyumba ya bwana Jones. Nyumba ilikuwa ikilindwa na mbwa kwenye kila mlango. Alitokea kwenye wakati maalumu tu akiwa ameongozana na mbwa sita, mbwa walimzunguka na kumtisha kwa kuunguruma mnyama yoyote aliyemsogelea. Pia akaanza kutoonekana jumapili asubuhi wakati wa kutoa maagizo na badala yake alimtuma mmoja wa nguruwe kufanya hivyo, mara nyingi alimtuma Mpayukaji

Asubuhi moja ya jumapili Mpayukaji akatangaza kuwa kuku wanatakiwa kukabidhi mayai yao. Napolioni alikuwa amekubaliana na bwana Whymper mkataba wa kumuuzia mayai mia nne kwa wiki. Mapato hayo yangetumika kulipia nafaka na chakula pale shambani hadi majira ya joto yajayo, na hali kuwa nzuri.

Kuku waliposikia jambo hilo walipinga vikali sana. Hapo mwanzo walikuwa wameshaambiwa kuwa kujitoa kwa namna hiyo kunaweza hitajika huko mbeleni, lakini hawakuamini kama jambo hilo linaweza kutokea. Walikuwa wameshaandaa viota kwaajili ya kuatamia wakati wa majira ya kuchipua, na walipinga wakisema kuchukua mayai ni sawa na mauaji. Kwa mara ya kwanza tokea wanyama wamfukuze bwana Jones kukatokea kitu kinachofanana na uasi ule.

Kuku wakiongozwa na kuku watatu, walipinga vikali mpango wa Napolioni. Mbinu yao ya kupinga ilikuwa ni kuruka hadi kwenye mbao za darini na kutaga mayai ambayo yakianguka na kupasuka sakafuni. Napolioni alipoona hilo akaamua kuzimisha mgomo vikali sana na haraka. Akaamrisha posho ya kuku isitishwe, na kutoa tamko kuwa mnyama yoyote atakayethubutu kuwapatia kuku hata punje moja ya mahindi adhabu yake itakuwa kifo. Mbwa waliagizwa kuhakikisha kuwa amri hiyo inatekelezwa. Kwa muda wa siku tano kuku waliendelea kugoma, lakini mwishowe wakakata tamaa na kurudi kutaga kwenye viota vyao. Kuku tisa walikuwa wamekufa kwenye mgomo ule. Walizikwa bustanini na ikasemwa kuwa wamekufa kutokana na ugonjwa wa Coccidiosis.

Bwana Whymper hakusikia chochote kuhusu suala hili na aliendelea kuyapat mayai bila tatizo lolote. Kila wiki gari lilifika kuyachukua shambani.

Katika kipindi hicho chote kulikuwa na tetesi kuwa Snowball alikuwa akijificha katika mashamba ya karibu. Walisema alikuwa katika shamba Foxwood au Pinchfield. Katika kipindi hicho uhusiano wa Napolioni na wakulima wengine ukawa umeimarika sana. Sasa pale uwanjani kulikuwa na lundo la mbao ambazo zilikuwa zimekusanywa pale miaka kumi iliyopita wakati wa kusafisha shamba.

Bwana Whymper akamshauri Napolioni kuziuza na kuwa bwana Pilkington na bwana Frederick walikuwa wanazitaka sana.

Napolioni hakujua ni nani anafaa zaidi kuuziwa, alipokuwa akitaka kukubaliana na bwana Frederick, ilikuwa inasemwa kuwa Snowball alikuwa amejificha katika shamba la Pilkington, akitaka kufanya biashara na Pilkington ilisemwa kuwa Snowball yupo katika shamba la Frederick.

Siku moja, mwanzoni mwa majira ya kuchipua jambo la kushtusha likawa limegunduliwa. Ilisemwa kuwa Snowball alikuwa akitembea shambani kwa siri nyakati za usiku; wanyama walitatizwa sana na habari hiyo hadi wakashindwa kulala kwacraha. Ilisemwa kuwa alifika shambani kila siku usiku akivizia na kufanya kila aina ya uhujumu. Aliiba mahindi, alivunja ndoo za maziwa, alivunja mayai, alikanyagakanyaga vitalu, na kubandua magome ya miti ya matunda.

Jambo lolote likiharibika lilihusishwa na Snowball. Kama dirisha likivunjika au mifereji ikiziba, basi kuna mnyama atatokea na kusema kuwa Snowball alikuja usiku na kutenda hayo. Na iwapo funguo za ghalani zimepotea basi shamba zima liliaminishwa kuwa Snowball amezitupa ndani ya kisima. Ajabu ni kuwa waliendelea kuamini hilo hata baada ya funguo kupatikana zikiwa chini ya mfuko wa chakula.

Ng'ombe nao walidai kuwa Snowball alivizia usiku wakiwa wamelala na kuwakamua maziwa. Panya nao ambao walikuwa wasumbufu sana katika majira ya baridi walisema kuwa wanashirikiana na Snowball.

Napolioni akatoa tamko kuwa, kunatakiwa kufanywa uchunguzi wa kina juu ya matendo ya Snowaball. Akiwa na mbwa wake akaanza kuchunguza kwa makini katika mabanda, wanyama wengine walimfuata nyuma kwa unyenyekevu. Kila baada ya hatua kadhaa Napolioni alisimama na kunusa-nusa chini. Alisema anaweza tambua harufu ya alimopita Snowball. Aliingia kila sehemu kwenye mabanda, ndani ya banda la kuku, banda la ng'ombe, bustani ya mbogamboga na alisema kwamba kote huko Snowaball alikuwa amepita. Alikuwa akiweka pua yake chini na kuvuta pumzi ndefu na kisha kusema, "Snowball! Alipita hapa! Nasikia harufu yake!" Mbwa kila waliposikia neno Snowball waliunguruma na kuonyesha meno yao.

Wanyama waliogopa sana, kwao ilionekana kama Snowball ni adui asiyeonekana, akizunguka na kuwaletea kila aina ya hatari.

Jioni ilipofika Mpayukaji aliwaita wanyama wote pamoja akiwa na uso ulioonyesha wasiwasi. Akawaambia kuwa ana jambo la muhimu sana anataka kuwaambia.

"Ndugu-zanguni!" Alianza kusema. "Jambo baya kabisa limegunduliwa. Snowball amejiuza kwa bwana Frederick wa shamba la Pinchfield, na sasa bwana Frederick anajiandaa kutuvamia na kutupora shamba! Snowball ndiye muongozaji wake katika shambulio hilo. Pamoja na hilo, kuna jambo baya zaidi. Mwanzo tulifikiri uasi wa Snowball ni sababu ya tamaa zake na kutaka kujikweza. Lakini tulikuwa tumekosea sana. Ndugu-zanguni, mnajua sababu hasa ya hila za Snowaball? Snowball alikuwa anashirikiana na bwana Jones tokea mwanzo! Alikuwa ni shushushu wa bwana Jones toka zamani. Hilo limethibitishwa na nyaraka alizoziacha ambazo tumezigundua hivi karibuni. Hili jambo limetutatiza sana ndugu zangu. Inamaana hatukuona jinsi alivyofanya hila ili tushindwe kwenye vita ya kibanda cha ng'ombe? Ni bahati tu hila zake hazikufanikiwa."

Wanyama wote walishikwa na mshangao . Jambo hili likionekana ni baya kushinda kitendo chake cha kuharibu kinu cha upepo. ilichukuwa dakika kadhaa kuelewa kilichosemwa.
Wote walikuwa wakikumbuka au walidhani wanakumbuka jinsi ambavyo Snowball alikuwa mstari wa mbele katika vita ya kibanda cha Ng'ombe, na jinsi alivyowakusanya na kuwahamasisha katika vita ile. Pia walikumbuka jinsi ambavyo hakusimama hata pale alipojeruhiwa mgongo kwa bunduki ya bwana Jones. Hawakuelewa jinsi ya kuhusianisha matendo hayo na suala la Snowball kuwa njama moja na bwana jones. Hata Boxer ambaye hakuwa mnyama wa kuhoji alishangazwa. Akakaa chini kisha akafumba macho na kujitahidi kufikiri kwa kina kuhusu jambo lile.

"Siamini kabisa," akasema hatimaye. "Snowball alipambana kishujaa kwenye vita ya kibanda cha ng'ombe. Mimi mwenyewe nilimshuhudia. Je, hatukumpa medali ya 'Mnyama shujaa daraja la kwanza' mara tu baada ya vita?"

"Hilo ndilo kosa letu ndugu-zanguni. Sasa tumejua mambo yote baada ya kupata nyaraka zake za siri, kiukweli alikuwa akijaribu kutuongoza kwenye kushindwa."

"Lakini alijeruhiwa," alisema Boxer." Wote tulimuona akikimbia huku damu zikimtoka."

"Ile ilikuwa ni sehemu ya mpango!" Akasema mpayukaji. "Risasi ya bwana Jones ili mparaza tu. Naweza kuwaonyesha hilo kwenye maandishi yake mwenyewe, ikiwa mnaweza kusoma! Mbinu yao ilikuwa ni Snowaball kutoa ishara ili wanyama wote wakimbie na kuacha uwanja wa mapambano kwa adui. Ilibaki kidogo afanikiwe, na niwaambie ndugu-zanguni, angefanikiwa kama isingekuwa sababu ya kiongozi wetu shujaa, ndugu Napolioni. Hamkumbuki mara tu bwana Jones na watu wake walipoingia uwanjani jinsi ambavyo Snowball aligeuka na kukimbia na wanyama kumfuata? Na hamkumbuki pia baada ya wanyama kutaharuki na kuanza kukata tamaa jinsi ambavyo ndugu Napolioni alivyokimbia kushambulia huku akipiga kelele 'kifo kwa binadamu!' na kisha kuzamisha meno yake katika mguu wa bwana Jones? Hakika mnakumbuka hilo ndugu-zanguni!" Alimaliza kusema mpayukaji huku akienda huku na huku.

Baada ya mpayukaji kueleza jambo hilo kwa namna yenye ushwawishi hivyo, ilionekana na wanyama nao wanakumbuka jambo hilo likitokea. Walikumbuka jinsi Snowball alivyogeuka na kuwahimiza kukimbia mwanzoni mwa vita. Lakini pamoja na hayo Boxer alikuwa bado hajaridhika.

"Siamini kama Snowball alikuwa ni msaliti," alisema Boxer. "Aliyoyafanya baada ya vita ni mabaya lakini naamini wakati wa vita ya kibanda cha ng'ombe hakuwa msaliti."

Mpayukaji akamjibu Boxer polepole, kwa sauti ya chini ila ya msisitizo, akasema.

"Ndugu yangu, kiongozi wetu , ndugu Napolioni amesema suala hili waziwazi na kwa ushahidi. Snowball alikuwa ni shushushu wa bwana Jones kabla hata ya mapinduzi."

"Kama ni hivyo sawa!" Akasema Boxer, "kama ndugu Napolioni amesema hivyi basi itakuwa sahihi "

"Huo ndiyo uzalendo ndugu yangu!" Akisema mMpayukaji lakini alimuangalia Boxer kwa jicho kali la chuki. Baada ya hilo, Mpayukaji akageuka kuondoka lakini akakumbuka kitu na kusema, "nawaonya wanyama wote shambani hapa kuwa macho. Tuna kila sababu ya kuamini kuwa kuna wafuasi wa Snowball miongoni mwetu!"

Baada ya siku nne, Napolioni akaagiza wanyama wote wakusanyike uwanjani wakati wa mchana. Wanyama wote walipokusanyika, Napolioni akatoka ndani ya nyumba akiwa amevaa medali zake zote(alikuwa amejipatia nishani ya mnyama shujaa daraja la kwanza na mnyama shujaa daraja la pili).
Akaingia akiwa na mbwa wake tisa waliokuwa wanaunguruma na kufanya wanyama wengine watetemeke kwa uoga. Wanyama wote walijikunyata na kukaa kimya, ni kama walikuwa wanajua kuna jambo baya linataka kutokea

Napolioni akasimama kikakamavu huku akichunguza wanyama waliokusanyika. Ghafla akatoa sauti kali na wale mbwa wakaruka ghafla na kuwakamata nguruwe wanne masikio, na kuwakokota hadi miguuni pa Napolioni. Masikio ya nguruwe wale yakaanza kutoa damu, sasa mbwa wakawa wameonja damu na wakawa kama wamerukwa na akili.

Kwa mshangao wa kila mnyama, mbwa watatu wajamrukia Boxer. Lakini Boxer aliwaona wakija hivyo akapiga teke lililompata mbwa mmoja akiwa hewani na kumuangusha chini. Kisha akamkandamiza chini kwa mguu wake, mbwa yule alilia kwa uchungu sana akiomba huruma. Wenzake wawili wakakimbia wakiwa wamefyata mikia. Boxer akamuangalia Napolioni akitaka kujua iwapo ammalize yule mbwa. Uso wa Napolioni ukabadilika na kumuashiria Boxer kumuachia mbwa yule. Boxer akatoa mguu wake na mbwa yule akatoka mbio huku akipiga kelele.
Vurugu zile zikaisha lakini wale nguruwe wanne wakakaa wakisubiri hatima yao huku wakitetemeka kwa uoga. Nyuso zao zilijaa mashaka. Napolioni akawataka wakiri makosa yao mbele yao wanyama wote. Nguruwe wale walikuwa ni wale nguruwe wanne waliokuwa wamepinga kitendo cha Napolioni kukomesha mikutano ya jumapili asubuhi. Na bila kuhojiwa zaidi, wakakiri kuwa wamekuwa wanawasiliana na Snowball kwa siri toka alipofukuzwa. Walisema kuwa walishirikiana naye katika kubomoa kinu cha upepo, na walikuwa wamekubaliana naye kumpatia shamba bwana Frederick. Waliongeza kuwa Snowball alikuwa amewaambia kuwa alikuwa ni shushushu wa bwana Jones toka zamani. Walipomaliza kukiri mbwa waliwararua makoo yao na kuwaua palepale.

Baada ya hayo, Napolioni, kwa sauti ya kutisha akasema kama kuna mnyama mwingine ana jambo anataka kukiri akiri. Kuku watatu, wale walioongoza uasi juu ya mayai walipita mbele na kusema kuwa Snowball aliwatokea ndotoni na kuwashawishi waasi na wasitii amri za Napolioni. Nao pia waliuwawa. Hapo bata bukini mmoja akapita mbele na kukiri kuwa wakati wa mavuno mwaka jana aliiba mahindi na kula wakati wa usiku. Kondoo mmoja naye akaja mbele na kuungama kuwa alikuwa akikojoa kwenye dimbwi la maji ya kunywa, na alisema alishawishiwa kufanya hivyo na Snowball. Kondoo wengine wawili nao wakaungama kumuua kondoo dume mzee, kondoo aliyekuwa mfuasi muaminifu wa Napolioni. Walisema walimuua kwa kitendo chao cha kumkimbiza- kimbiza uwanjani alipokuwa na tatizo la kikohozi.

Wanyama wote walioungama waliuwawa pale pale. Zoezi hilo la kinyama liliendelea hadi lundo la maiti likawa mbele ya Napolioni, na hewa yote ikawa nzito kwa harufu ya damu, harufu ambayo haikuwahi sikika tokea kufukuzwa kwa bwana Jones.

Zoezi hilo lilipokwisha, wanyama wote wakaondoka kwa pamoja isipokuwa nguruwe na mbwa. Waliondoka wakiwa wameshikwa na huzuni kubwa sana. Hawakujua ni kipi kibaya zaidi, hila za wanyama wale wakishirikiana na Snowball au mauaji ya kikatili waliyotoka kuyashuhudia!

Mauaji ma umwagaji damu waliouona ulikuwa mkubwa kuliko ule waliowahi kuhushuhudia nyakati za bwana Jones. Toka kuondoka kwa bwana Jones mpaka sasa, hakuna mnyama aliyemuua mnyama mwingine. Hata panya mmoja hakuuliwa!

Waliongozana kwa huzuni mpaka kwenye gofu la kinu cha upepo. Wakajilaza hapo wakiwa wamejikunyata kama vile wanaona baridi na wanataka kupashana joto. Wanyama wote walikusanyika isipokuwa paka ambaye alitoweka mara tu Napolioni alipotangaza wanyama wakusanyike.

Kwa muda kidogo hakuna mnyama aliyesema chochote, na ni Boxer pekee ndiye alibaki amesimama. Alikuwa akitembea huku na huku akichezesha mkia na kutoa miguno ya kushangaa, mwishowe akasema.

"Sielewi kabisa jambo hili. Sikutegeme mambo kama haya kutokea shambani mwetu. Itakuwa ni sisi ndiyo tuna makosa. Nafikiri nimepata tiba ya jambo hili, ni kufanya kazi kwa bidii. Kuanzia sasa nitakuwa naamka saa moja kabla ya muda wa kawaida."

Hapo Boxer akaanza kukimbia kichovu akielekea kwenye machimbo ya mawe. Huko alikusanya mawe na kuyavuta hadi kwenye eneo la ujenzi wa kinu, hapo ndipo aliweza kwenda kulala.

Wanyama wengine waliendelea kujikunyata kumzunguka Clover bila kusema neno lolote. Kwenye muinuko ule waliweza kuona sehemu kubwa ya shamba lote. Majira hayo ya kuchipua shamba lilivutia sana, mashamba ya kijani, mwanga mzuri wa jua ukipenya kwenye uzio. Lambo lilikuwa linang'aa na vigae vyekundu vya majengo ya shambani vilivutia sana. Clover alipokuwa akiangalia hayo, machozi yalimtoka. Kama angeweza kuongea mawazo yake angesema hili si lengo walilokuwa nalo walipoamua kumpindua binadamu. Mauaji na vitisho si mambo waliyotarajia siku ile Meja alipowahimiza kuasi. Siku ile alikuwa na picha ya shamba ambalo wanyama wakiwa huru dhidi ya njaa na mijeledi, wote wakiwa sawa, na wote wakifanya kazi kadri ya uwezo wao, wenye nguvu wakiwalinda walio dhaifu. Kama tu yeye alivyowalinda wale bata kwa miguu yake siku ile ya hotuba ya Meja. Hakujua imekuwaje hadi imefikia wanyama wote wanaogopa kusema wanachofikiri, mbwa wakali wanaunguruma na kuzunguka kutisha wanyama, na kushuhudia wanyama wenzake wakiuwawa!

Si kwamba kichwani mwake alikuwa na mawazo ya uasi, la. Alijua kuwa pamoja na yote hayo, hali yao ni bora kuliko ilivyokuwa wakati wa bwana Jones, na kuwa jambo la msingi kuliko yote lilikuwa ni kuzuia kurejea kwa binadamu. Kwa hiyo, kwa hali yoyote ile, alikuwa tayari kuendelea kuwa muaninifu, kufanya kazi kwa bidii, kutii anayoagizwa na kukubali uongozi wa Napolioni. Hata hivyo, yeye na wanyama wengine hawakufanya kazi kwa bidii wakitegemea maisha kama haya. Hawakukabilina na risasi za bwana Jones, wala hawakujenga kinu cha upepo ili waishi maisha ya namna hii. Hayo ndiyo yalikuwa mawazo ya Clover japo hakupata maneno ya kuyazungumza. Badala yake akaanza kuimba Hayawani wa Uingereza.

Wanyama wengine waliomzunguka nao wakaanza kuimba, waliimba mara tatu mfululizo. Waliimba wimbo ule kwa huzuni sana, hawajawahi imba namna ile. Walipomaliza kuimba kwa mara ya tatu Mpayukaji akatokea akiwa na mbwa watatu. Aliwakaribia kama vile ana jambo muhimu sana la kusema. Hapo akatoa tangazo kuwa, kwa tamko maalumu la ndugu Napolioni, wimbo wa Hayawani wa Uingereza umepigwa marufuku. Kuanzia sasa ni marufuku kuuimba.

Wanyama hawakuamini walichokisikia.

"Kwanini?" Aliuliza kwa huzuni Muriel.

"Ndugu zangu, wimbo huu hauhitajiki tena," akasema Mpayukaji kwa msisitizo. "Hayawani wa Uingereza ulikuwa ni wimbo wa mapinduzi. Kuuwawa kwa wasaliti leo mchana lilikuwa ni tendo la mwisho la mapinduzi hayo. Maadui wa ndani na maadui wa nje wameshindwa. Ndani ya Hayawani wa Uingereza tuliimba juu ya maisha bora. Maisha hayo tumeshayafikia. Ni jambo ambalo liko wazi kuwa wimbo huu hauhitajiki tena."

Japo wanyama walikuwa wamejawa na uoga lakini baadhi yao walikuwa tayari kupinga suala lile. Kabla hawajfanya chochote kondoo wakaanza kusema," Miguu minne, rafiki. Miguu miwili adui." Walisema hivyo kwa dakika kadhaa na kuzuia majadiliano yoyote kuendelea.

Kuanzia siku hiyo, Hayawani wa Uingereza haukusikika tena ukiimbwa. Badala yake, Minimus, yule mshahiri akatunga wimbi mwingine, ulianza hivi;

Kamwe sitasababisha udhurike!

Na huu uliimbwa kila jumapili asubuhi baada ya kupandisha bendera, lakini wanyama hawakuushika huu kama walivyokuwa wameushika Hayawani wa Uingereza.
 
SURA YA NANE

Siku chache mbele, baada ya taharuki iliyosababishwa na mauaji kupoa baadhi ya wanyama wakakumbuka au walifikiri wanakumbuka kuwa amri ya sita inasema "Ni marufuku kwa mnyama kumuua mnyama mwingine." Japo hakuna aliyesema hili wakati wa mauaji yale, lakini waliona kwamba mauaji yale yanaenda kinyume na amri hii. Clover akamuambia Benjamini amsomee amri ya sita, Benjamini akakataa kama ilivyo kawaida yake. Basi Clover akamtafuta Muriel. Muriel alimsomea, "Ni marufuku kwa mnyama kumuua mnyama mwingine bila sababu." Kwa namna fulani wanyama hawakukumbuka maneno haya mawili ya mwisho. Lakini kwa ilivyoandikwa wakaona kuwa amri hiyo haijavunjwa. Kulikuwa na sababu ya msingi kuwaua wasaliti wale walioshirikiana na Snowball.

Katika mwaka ule wanyama walifanya kazi ngumu ya kujenga upya kinu cha upepo. Kazi ilikuwa ngumu kuliko mwaka uliopita. Ukuta ulikuwa mnene mara mbili ya hapo mwanzo. Kulikuwa na kazi nyingi sana ukiongezea na kazi zingine za shambani. Kuna kipindi walihisi walifanya kazi kwa muda mrefu na walipata chakula kichache kuliko wakati wa bwana Jones. Kila jumapili asubuhi Mpayukaji alifika akiwa na karatasi refu kalishika kati ya kwato zake. Humo aliwasomea wanyama takwimu kuonyesha kuwa uzalishaji unepanda kwa asilimia mia mbili, mia tatu au mia tano. Wanyama hawakuwa na sababu ya kutomuamini hasa kwa kuwa wengi hawakukumbuka jinsi hali ilivyokuwa kabla ya mapinduzi. Lakini kuna siku walihisi ni bora wawe na takwimu za chini lakini chakula kiwe cha kutosha.

Maagizo yote yalitolewa kupitia Mpayukaji au mmoja kati ya nguruwe wengine. Napolioni hakuonekana kabisa, aliweza kuonekana mara moja tu ndani ya siku arobaini. Na siku hiyo alionekana akiwa ameongozana na mbwa wake pamoja na jogoo mweusi aliyetangulia mbele akiwa kama mpiga mbiu. Jogoo huyo alikuwa akipiga mbiu kabla ya Napolioni kuongea, "kokorikooo!"

Ilisemekana kuwa hata ndani ya nyumba waliyoishi nguruwe Napolioni aliishi chumba cha peke yake. Pia alikula peke yake huku akilindwa na mbwa wawili. Pia alitumia vyombo bora kabisa.

Mbali na zile sherehe mbili, ikatangazwa kuwa bunduki ile itapigwa kila mwaka mara moja katika siku ya kuzaliwa Napolioni. Napolioni hakuitwa tena "Napolioni," bali alijulikana kwa jina rasmi, "Kiongozi wetu, ndugu Napolioni," na mwenyewe alijipachika majina mengi kama; baba wa wanyama wote, kitisho cha binadamu, mlinzi wa kondoo, rafiki wa bata na mengine kama hayo.

Kwenye hotuba zake, Mpayukaji alikuwa akimuongelea Napolioni huku machozi yakimbubujika mashavuni. Aliongea kuhusu busara na moyo mzuri wa Napolioni, upendo aliokuwa nao kwa wanyama wote, na hasa wanyama walioishi kitumwa na bila furaha katika mashamba mengine.

Ikawa ni kawaida kumsifia Napolioni kwa kila mafanikio na hali nzuri iliyowapata wanyama.
Ungeweza kumsikia kuku mmoja akiwaambia wenzake , "Chini ya uongozi wa kiongozi wetu, ndugu Napolioni nimeweza kutaga mayai matano ndani ya siku sita." Au ng'ombe wawili wakiwa wanakunywa maji kwenye lambo wanaweza kusema kwa furaha, "Shukrani ziende kwa uongozi wa ndugu Napolioni, maji haya yana ladha nzuri ajabu."

Hali ya shamba iliweza kuelezwa kwa shairi lililoitwa 'Ndugu Napolioni' lililotungwa na Minimus, lilikuwa kama ifuatavyo;

Rafiki wa wasio na baba
Kidimbwi cha furaha
Bwana wa chakula! Oo, jinsi nafsi yangu ilivyo na shangwe!
Nikutazamapo naona moto
Macho yako matulivu lakini yenye mamlaka,
Kama jua angani,

Ndugu Napolioni!

Wewe ni mpaji wa vitu vyote vipendavyo na viumbe
Matumbo yaliyoshiba, mara mara mbili kwa siku, nyasi safi za kulalia
Hayawani wote, wadogo kwa wakubwa
Hulala kwa amani katika mabanda yao
Unawatazama wote

Ndugu Napolioni

Nguruwe mdogo anyonyae
Amekuwa mkubwa ghafla
Hata angekuwa chupa ya kileo, au kifaa cha kukandia
Angejifunza kuwa muaminifu kwako
Sauti yake ya kwanza itakuwa
"Ndugu Napolion!"

Napolioni aliagiza shairi hili liandikwe kwenye ukuta wa lile banda kubwa, karibu na zile amri saba. Pia picha ya Napolioni ikachorwa hapo. Kazi hiyo ilifanywa na Mpayukaji akitumia rangi nyeupe. Wakati huohuo Napolioni alikuwa kwenye majadiluano na bwana Frederick na bwana Pilkington, akiwakilishwa na bwana Whymper. Majadiliano yalihusu kununua lile lundo la mbao. Bwana Frederick alikuwa na hamu sana ya kununua lakini bei aliyotaja ilikuwa chini. Na pia wakati huohuo kulikuwa na tetesi kuwa bwana Frederick na watu wake walikuwa wanapanga kuvamia shamba la wanyama na kuharibu kinu cha upepo. Ilisemwa kuwa jengo lile liliwafanya wajawe na wivu. Pia bado ilikuwa inaaminika kuwa Snowball alikuwa amejificha katika shamba la Pinchfield.

Katikati ya majira ya joto katika mwaka huo wanyama walishikwa na taharuki waliposikia kwamba kuku watatu wameungama kwamba, kwa ushawishi wa Snowball walikula njama ya kutaka kumuua Napolioni. Hawa waliuwawa haraka na hatua zaidi zikachukuliwa ili kumlinda Napolioni. Kuanzia wakati huo, nbwa wanne walimlinda alipokuwa amelala, mbwa mmoja kwenye kila kona ya kitanda. Pia nguruwe mmoja mdogo aliyeitwa Pinkeye akapewa kazi ya kuonja chakula cha Napolioni kabla mwenyewe hajala, hii ilikuwa ni kuona kama kuna sumu.

Siku moja ikatangazwa kuwa Napolioni alikuwa amepanga kuuza zile mbao kwa bwana Pilkington, na pia atafanya makubaliano ya kibiashara kati ya shamba la Foxwood na shamba la wanyama. Japo ushirikiano wa Napolioni na bwana Pilkington ulifanyika kupitia bwana Whymper ila ulikuwa nzuri sana. Wanyama hawakumuamini bwana Pilkington, kama ambavyo hawakumuamini binadamu yeyote, lakini walionelea ni bora yeye kuliko bwana Frederick ambaye walimuogopa na kumchukia.

Majira ya joto yalipokuwa yanayoyoma kazi ya ujenzi wa kinu cha upepo ilikuwa jaribu kwisha. Katika kipindi hicho tetesi za kuvamiwa nazo zikazidi kuongezeka. Ilisemekana Frederick alipanga kuvamia akiwa na watu ishirini wenye bunduki, na pia ilisemwa kuwa amewahonga polisi na hakimu ili akishapata shamba la wanyama wasimhoji kuhusu uhalali wa kulimiliki.

Zaidi ya hilo, kulikuwa na habari zingine mbaya kutoka shamba la Pinchfield. Ilisemwa kuwa bwana Frederick alikuwa akiwatendea wanyama wake kikatili sana. Ilisemekana alimchapa farasi mzee hadi akamuua, aliwanyima ng'ombe wake chakula, alimuua mbwa wake kwa kumtupa kwenye tanuru la moto, na kuwa alikuwa akijiburudisha kwa kupiganisha majogoo ambayo yalifungwa viwembe miguuni. Wanyama walipandwa na hasira kali waliposikia mambo hayo wakifanyiwa ndugu zao. Kuna muda walipiga kelele kuwa wakavamie shamba la Pinchfield, lakini Mpayukaji aliwatuliza na kuwaambia waepuke haraka na wasubiri mipango ya ndugu Napolioni. Pamoja na hilo, chuki dhidi ya bwana Frederick ilizidi kuwa juu.

Asubuhi moja ya jumapili, Napolioni alifika bandani na kusema kuwa hajawahi kufikiria kumuuzia bwana Frederick mbao, na alisema ni jambo la dharau kwake kushirikiana na watu wa hovyo kama Frederick.
Njiwa ambao bado walikuwa wanaendelea kutumiwa kusambaza habari za uasi, walipigwa marufuku kukanyaga shamba la Foxwood, na waliagizwa kubadilisha kauli mbiu ya zamani ya, "Kifo kwa binadamu" kuwa, "kifo kwa Frederick."

Mwisho wa majira ya joto, njama nyingine ya Snowball iligunduliwa. Shamba la ngano lilikuwa limejaa magugu, hivyo ikasemwa kuwa Snowball alikuwa amefika usiku na kuchanganya mbegu za magugu na mbegu za ngano. Bata bukini mmoja Mmoja alikiri mbele ya Mpayukaji kuhusika kwenye njama hiyo na akajiua kwa kula matunda yenye sumu.

Wanyama pia wakajifunza kuwa Snowball hajawahi kupewa nishani ya "Mnyama shujaa daraja la kwanza." Ilisemwa hii ilikuwa ni hekaya tu iliyosambaa mara baada ya vita ya Kibanda cha ng'ombe. Na hekaya yenyewe ilianzishwa na Snowball mwenyewe. Ilisemwa, siyo tu hakupewa nishani bali alishutumiwa kwa kuonyesha uoga vitani. Kwa mara nyingine wanyama walionekana kushangazwa na habari ile, lakini Mpayukaji alifanikiwa kuwashawishi kuaminu kwamba hawakukumbuka vizuri.

Wakati wa majira ya kupukutisha, kazi ilikuwa ngumu zaidi. Iliwabidi kufanya kazi ya kuvuna huku wakimalizia kujenga kinu cha upepo. Jengo lilikuwa limeisha lakini mashine ilikuwa bado kufungwa. Bwana Whymper alikuwa akifanya mipango ya kuwanunulia.

Kwa bidii yao walikuwa wamemaliza kazi ya ujenzi kwa wakati uliopangwa, licha ya ugumu, kutokuwa na uzoefu, kutumia vifaa duni na hila za Snowball. Walikuwa wamechoka lakini walijivuna kwa kazi yao. Walitembea wakikizunguka kinu kile mara kadhaa, machoni pao kilionekana kizuri zaidi ya kikichojengwa mara ya kwanza. Na zaidi ni kuwa unene wa ukuta ulikuwa mara mbili ya ule wa kwanza. Huu hauwezi kuangushwa labda ulipuliwe!

Walipofikiria kuhusu magumu waliyopitia, na faida zitakazoletwa na kinu cha upepo, uchovu uliwaisha. Walizunguka na kupiga kelele za shangwe.

Napolioni mwenyewe alihudhuria akiwa na mbwa wake na yule jogoo. Alifika na kukagua kazi ilivyofanyika. Akawapongeza wanyama kwa kazi yao na kutangaza kuwa kinu kile kitaitwa kinu cha Napolioni. Baada ya siku mbili, wanyama waliitwa kwenye banda kubwa kwaajili ya mkutano muhimu. Walipigwa na butwaa pale Napolioni alipotangaza kuwa zile mbao ameziuza kwa bwana Frederick. Alisema kuwa kesho yake Frederick atafika na gari lake kuzibeba.

Katika kipindi chote ambacho alionekana ana urafiki na Pilkington kumbe alikuwa na makubaliano ya siri na Frederick. Ushirikiano wote na Pilkington ulikoma na ujumbe wa kejeli ukatumwa kwa bwana Pilkington. Njiwa waliagizwa kutoenda shamba la Pinchfield na wabadili kaulimbiu kutoka "Kifo kwa Frederick" kuwa " kifo kwa Pilkington."

Napolioni akawahakikishia wanyama kuwa, habari za shamba liko karibu kushambuliwa na Bwana Frederick si za kweli, na habari za kuwa bwana Frederick aliwafanyia wanyama ukatili zilikuwa ni uzushi. Alisema tetesi hizo zote zilianzishwa na Snowball na mawakala wake. Sasa ikasemwa kuwa Snowball hakuwa amejificha kwenye shamba la Pinchfield na wala hajawahi kukanyaga huko katika maisha yake. Ilisemwa kuwa alikuwa akiishi maisha ya anasa katika shamba la Foxwood, na amekuwa akilipwa marupurupu na bwana Pilkington toka afukuzwe.

Nguruwe walifurahia sana ujanja wa Napolioni. Kwa kujifanya rafiki wa Pilkington, alimfanya Frederick apandishe bei kwa shilingi kumi na mbili. Mpayukaji akasema akili na uwezo mkubwa wa Napolioni ulionekana kwa jinsi ambavyo hakumuamini mtu yeyote, hata bwana Frederick . "Bwana Frederick alikuwa ametaka kulipia mbao kwa kutumia kitu kinachoitwa hundi, hicho kilionekana ni kipande tu cha karatasi chenye ahadi ya malipo. Lakini Napolioni alikuwa na akili sana. Alitaka malipo yafanyike kwa pesa taslimu, na malipo hayo yafanyike kabla mbao hazijaondolewa. Hivyo bwana Frederick amekwisha lipa na pesa iliyopatikana inatosha kununulia mashine kwaajili ya kinu cha upepo."

Baada ya malipo kufanyika bwana Frederick alitoa mbao zile harakaharaka. Na baada ya biashara kuisha ukaitishwa mkutano maalumu ndani ya banda ili wanyama waone pesa zilizopatikana. Napolioni alikaa kwenye jukwaa akiwa amevaa nishani zake zote. Pesa zile ziliwekwa kwenye sahani ya udongo mbele yake. Wanyama wakajipanga mstari na kupita mmojammoja na kutazama pesa zile. Boxer akasogeza pua yake na kunusa noti zile.

Baada ya siku tatu kukatokea taharuki kubwa sana shambani. Bwana Whymper alifika shambani uso ukiwa umempauka. Alitupa baiskeli yake uwanjani na kukimbia moja kwa moja mpaka ndani ya nyumba ya kuishi. Baada ya dakika chache zikisikika kelele kubwa za hasira kutoka katika chumba cha Napolioni. Habari ya kilichotokea zikasambaa haraka kama moto wa nyikani. Noti zile zikikuwa ni feki! Bwana Frederick alikuwa amejipatia mbao bure kabisa. Napolioni akawaita wanyama pamoja haraka sana, na kwa sauti iliyojaa hasira akatangaza hukumu ya kifo kwa bwana Frederick. Alisema iwapo atakamatwa atachemshwa akiwa hai. Pia akaongeza kuwa, baada ya hila ile, wategemee hali mbaya zaidi. Frederick na watu wake wanaweza endelea na mpango wao wa kushambulia shamba la wanyama. Walinzi waliwekwa kwenye kila muingilio wa shambani. Zaidi ya hilo, walituma njiwa wanne kwenda katika shamba la Foxwood wakiwa na ujumbe wa kutaka maridhiano wakitumaini kurudisha uhusiano na bwana Pilkington.

Asubuhi iliyofuata shambulizi likatokea. Wanyama walikuwa wakipata kifungua kinywa ambapo walinzi walikuja wakikimbia wakileta habari kuwa bwana Frederick na wafuasi wake wanakuja na wameshapita getini. Kwa ushupavu wanyama wakakusanyika kuwakabili, lakini safari hii vita haikuwa rahisi kama ile ya Kibanda cha ng'ombe. Kulikuwa na watu kumi na tano na karibu nusu yao walikuwa na bunduki. Watu wale walipofika kama hatua hamsini kutoka mabandani wakaanza kufyatua risasi. Wanyama hawakuweza kuhimili vipande vya risasi vilivyowajeruhi na milio ya risasi yenye kuogopesha. Pamoja na jitihada zote za Boxer na Napolioni kuwakusanya pamoja na kuwahimiza kupambana lakini walikimbia. Walijificha kwenye mabanda ya shambani na kuchungulia yanayoendelea kupitia matundu. Sasa eneo kubwa la shamba, kutia ndani kinu cha upepo vilikuwa mikononi mwa adui. Muda huo hata Napolioni alionekana hajui cha kufanya. Alitembea huku na huku mkia umemsimama. Walikua wakiangalia upande wa Foxwood mara kwa mara wakitumaini labda bwana Pilkington na watu wake watakuja kuwasaidia, bado walikuwa hawajakata tamaa. Wakiwa na matumaini hayo, njiwa mmoja kati ya waliotumwa kupeleka ujumbe kwa Pilkington alirudi akiwa amebeba ujumbe kwenye karatasi. Juu yake kuliandikwa, "Shauri yenu."

Wakati huo Frederick na watu wake wakawa wapo kwenye kinu cha upepo. Wanyama walitazamana na minong'ono ya taharuki ilisikika kati yao. Watu wawili walikuwa wamebeba nyundo na nondo. "Haiwezekani," alipiga kelele kwa hamaki Napolioni. "Ukuta ule tumeujenga mnene sana, hawawezi kuuangusha kwa nyundo na nondo. Jipeni moyo ndugu-zanguni!"

Lakini Benjamini alikuwa akiangalia watu wale kwa makini sana. Wale watu wenye nondo na nyundo walikuwa wajichimba shimo karibu na msingi wa jengo la kinu cha upepo.

"Kama nilivyofikiria!" Akasema Benjamini. "Unaona wanachotaka kufanya? Muda si mrefu wataweka unga wa baruti kwenye lile shimo na kulipua jengo."

Wanyama hawakuweza kutoka nje, haikuwa salama kufanya hivyo. Walibaki wamejificha huku wamejawa na uoga. Baada ya dakika chache wakaona watu wakikimbia kutoka kwenye kinu wakielekea pande zote. Kisha wakasikia muungurumo mkubwa sana wa mlipuko.
Njiwa waliruka na wanyama wote wakalala chini kifudifudi isipokuwa Napolioni tu. Walipoinuka wakaona wingu la vumbi limetanda kwenye eneo walipojenga kinu cha upepo. Baada ya vumbi kuondolewa na upepo, jengo la kinu cha upepo halikuwepo tena!

Baada ya kuona hivyo moyo wa ujasiri ukawarudia wanyama wote. Uoga waliokuwa nao ukazimwa na hasira iliyowajaa, walipiga kelele kubwa kwa hasira wakidai kisasi, na bila kusubiri kuamrishwa walitoka kwa pamoja kumshambulia adui. Hawakujali vipande vya risasi vilivyowapata kama vile mvua ya mawe. Binadamu walipiga risasi na kupiga lakini wanyama walizidi kwenda. Wanyama walipokaribia, binadamu nao wakatoka wakiwa na fimbo na viatu vyao vyenye soli za chuma. Kufika hapo karibu kila mnyama alikuwa amejeruhiwa na kondoo wawili, ng'ombe mmoja na bata bukini mmoja walikuwa wamekufa. Hata Napolioni ambaye alikuwa akiongoza mapambano akiwa nyuma alijeruhiwa, ncha ya mkia wake ilikatwa na kipande cha risasi. Lakini watu nao hawakutoka salama. Watatu kati yao walivunjwa mafuvu yao kwa kwato za Boxer, mwingine alitobolewa tumbo kwa pembe ya ng'ombe na mmoja alichaniwa suruali yake baada ya kushambuliwa na Jessie na Bluebell.

Walipotokea wale mbwa tisa, walinzi wa Napolioni, ambao aliwaambia wazunguke na kushambulia watu kutokea pembeni. Watu walipigwa na taharuki na kuhamaki, waliona kuwa wako katika hatari ya kuzingirwa pande zote. Frederick akapiga kelele kuwaamuru watu wake wakimbie ingali bado kuna nafasi, kufumba na kufumbua binadamu wakawa wakikimbia kuokoa maisha yao. Wanyama waliwakimbiza hadi kwenye uzio wa shamba. Waliwapa kipigo cha mwishomwisho walipokuwa wakipenya kwenye uzio wa miiba.

Walikuwa wameshinda lakini walikuwa hoi wakivuja damu. Wakaanza kujikokota polepole kurudi mabandani. Ndugu zao waliosambaa wakiwa wamekufa walifanya wengine wabubujikwe na machozi.

Walipopita mahali pa ujenzi wa kinu cha upepo walisimama na kukaa kimya kwa huzuni. Jengo halikuwepo tena! Kazi yao yote imesambaratishwa! Hata msingi ulikuwa umeharibiwa kwa kiasi fulani. Na mbaya zaidi ni kuwa hata mawe ya kujengea upya hayakuonekana, nguvu ya mlipuko ilikuwa imeyarusha mbali kabisa. Ilikuwa kama eneo lile halijawahi kujengwa kitu.

Walipokaribia mabandani wakakutana na Mpayukaji, yeye hakushiriki vita ile. Alikuwa anawafuata huku akirukaruka na kuchezesha mkia wake kwa furaha. Ghafla wanyama wakasikia sauti kubwa ya bunduki.

"Kwanini bunduki inapigwa?" Aliuliza Boxer

"Kushangilia ushindi wetu?" Alisema mpayukaji

"Ushindi gani?" Alizidi kuhoji Boxer huku akivuja damu magotini. Alikuwa amepoteza kiatu kiatu na kwato yake ilikuwa imepasuka. Pia vipande vya risasi vilikuwa vimemuingia kwenye mguu wake wa nyuma.

"Ushindi gani! Ndugu zangu, hatujamfukuza adui kutoka kwenye ardhi tukufu ya shamba la wanyama?" Alisema Mpayukaji

"Lakini wameharibu kinu, na tumekijenga kwa miaka miwili?"

"Hilo ndilo litusunbue! Tutajenga tena kinu kingine. Tujenge hata vinu sita vya upepo kama tunataka. Ndugu zangu, hamuoni jambo kubwa tulilolifanya hapa? Adui alikuwa ameshajinyakulia ardhi hii ambayo tumesimama. Na shukrani ziende kwa uongozi wa ndugu Napolioni, tumeipata tena."

"Kwa maana hiyo tumepata kile tulichokuwa nacho hapo kabla." Akasema Boxer.

"Huo ndiyo ushindi wetu" akasema Mpayukaji.

Wakajikongoja mpaka kwenye uwanja karibu na mabanda. Vipande vya risasi vilivyomuingia Boxer mguuni vilimsababishia maumivu makali sana. Na alijua kuwa kutakuwa na kazi ngumu sana ya kujenga upya kinu cha upepo hivyo alijiandaa kiakili kwa kazi hiyo. Lakini sasa alitambua kuwa ana miaka kumi na moja na nguvu zake si kama zilivyokuwa hapo zamani.

Wanyama walipata moyo pale walipoona bendera ya kijani imepandishwa, bunduki imepigwa mara saba, na baada ya kusikia hotuba ya Napolioni akiwapongeza. Baada ya mambo hayo waliona kuwa ushindi waliopata ni mkubwa sana

Wanyama waliokufa kwenye vita ile walizikwa kwa heshima zote. Boxer na Clover walivuta mkokoteni ambao ulitumika kama gari la kubebea maiti. Napolioni alikuwa mbele akiongoza msafara wa mazishi.

Kwa muda wa siku mbili walisherekea ushindi wao. Waliimba, hotuba zilitolewa, bunduki ilipigwa tena, na zawadi maalumu ya matunda ilitolewa kwa kila mnyama, kila ndege alipata kibaba cha mahindi na biskuti tatu kwa kila mbwa. Ilitangazwa kuwa vita ile itaitwa vita ya Kinu cha Upepo, na Napolioni akaanzisha nishani mpya iliyoitwa nishani ya bendera nyekundu, kisha akajivika yeye mwenyewe nishani hiyo. Katika kusherekea huko wakawa wamesahau suala la noti bandia.

Siku kadhaa mbele, nguruwe wakawa wamepata debe la mvinyo ndani ya nyumba ya nyumba. Siku hiyo sauti kubwa za kuimba zilisikika ndani ya nyumba. Wanyama walishangaa kusikia ala za Hayawani wa Uingereza ikichanganywa-changanywa.

Kama saa tatu na nusu usiku, Napolioni alitoka ndani ya nyumba akiwa amevaa kofia ya bwana Jones, alitoka kupitia mlango wa nyuma na kuzunguka uwanjani na kisha kurudi ndani. Asubuhi ilipofika kulikuwa na ukimya mkubwa kutoka ndani ya nyumba. Hakuna hata nguruwe mmoja aliyeonekana. Ilikuwa karibu saa tatu asubuhi ndipo Mpayukaji alionekana. Alikuwa akitembea polepole. Macho yake yalikuwa mazito na mkia umemfyata. Alionekana kama ni mgonjwa sana. Aliwaita wanyama wote na kuwaambia kuwa ana habari mbaya sana anataka kuwaambia. Ndugu Napolioni yu karibu kufa.

Kilio cha maombolezo kililipuka na wanyama wakajikunyata wakiwa wanalia. Waliulizana watafanya nini iwapo kiongozi wao atafariki. Tetesi zilisambaa kwamba Snowball amefanya njama ya kutia sumu katika chakula cha Napolioni. Ilipofika saa tano ya asubuhi Mpayukaji akatoka akiwa na tangazo jingine. Alisema kuwa, kabla ya kufa ndugu Napolioni ametoa tamko kuwa; adhabu ya kosa la kunywa pombe ni kifo.

Ilipofika jioni Napolioni alianza kupata nafuu. Kesho yake asubuhi Mpayukaji akatangaza kuwa hali ya Napolioni imetengamaa. Jioni ya siku hiyo Napolioni alikuwa mzima kabisa akifanya kazi.

Siku iliyofuata Napolioni akamuagiza bwana Whymper aende Willingdon na kumnunulia majarida yanayohusu utengenezaji wa pombe.

Baada ya wiki kadhaa Napolioni akaagiza shamba dogo nyuma ya bustani, shamba lililotengwa kama malisho ya wastaafu lilimwe. Alisema malisho yalitakiwa kupandwa upya. Lakini baada ya muda kidogo ikagundulika kuwa Napolioni alitaka kupanda shayiri.

Katika kipindi hichohicho kulitokea tukio la ajabu ambalo wanyama walishindwa kulielewa. Siku moja usiku kama saa sita hivi kulikuwa na kishindo kikubwa sana uwanjani. Wanyama wote wakatoka mabandani kwenda kuona. Ulikuwa ni usiku wa mbalamwezi hivyo waliweza kuona.
Chini ya lile banda ambapo amri saba ziliandikwa ilionekana ngazi ikiwa imevunjika. Mpayukaji alikuwa pembeni yake akiwa amepigwa na butwaa. Kando yake kulikuwa na taa, brushi na kopo la rangi likiwa limepinduka. Mara noja mbwa wakamzunguka Mpayukaji na kumsindikiza ndani ya nyumba.

Hakuna mnyama aliyeelewa kilichotokea, isipokuwa Benjamin ambaye alitikisa kichwa kwa kuelewa kilichotokea, lakini hakusema neno.

Siku chache mbele, Muriel alipokuwa akisoma zile amri saba, akaona amri nyingine ambayo wanyama waliikumbuka vibaya.

Walifikiri amri ya tano inasema,"Ni marufuku kwa mnyama kunywa pombe" lakini walisahau maneno mawili. Amri hiyo ilisomeka, "Ni marufuku mnyama kunywa pombe kupita kiasi."
 
Back
Top Bottom