SURA YA TISA
Walianza kujenga upya kinu cha upepo mara tu sherehe zilipokoma. Wakati huo kwato za Boxer zilikuwa bado hazijapona, kakini alikataa kabisa kupumzika, na alihakikisha haonekani kama aliye kwenye maumivu. Lakini pamoja na hilo, jioni alikuwa akikiri kwa Clover kuwa kwato yake inamtesa sana. Clover alijitahidi kumtibu kwa kutumia mitishamba ambayo aliiandaa kwa kuitafuna na kisha kumpaka kwenye kidonda. Clover na Benjamini walimshawishi sana Boxer kupunguza kazi.
"Mapafu ya farasi hayadumu milele," Clover alikuwa akimwambia, lakini Boxer hakusikia. Alisema kuwa lengo lake maishani ni moja tu, kuona kinu cha upepo kikifanya kazi kabla hajastaafu.
Mwanzoni wakati wa kutengeneza sheria za shamba la wanyama, umri wa kustaafu wa nguruwe na farasi uliwekwa kuwa miaka kumi na mbili, ng'ombe miaka kumi na nne, mbwa miaka tisa, kondoo miaka saba na kuku na bata bukini miaka mitano.
Ilisemwa kuwa kiinua mgongo cha farasi kitakuwa kilo mbili za mahindi kwa siku, na wakati wa baridi, kilo saba za nyasi. Siku za siku kuu watapata karoti au tofaa ikiwezekana. Boxer alikuwa anatimiza kumi na mbili wakati wa majira ya joto ya mwaka unaofuata.
Maisha shambani yalikuwa magumu sana. Kwa misimu miwili mfululizo baridi ilikuwa imekuwa kali sana. Chakula kilikuwa kichache na posho ikapunguzwa hata zaidi, isipokuwa ile ya nguruwe na mbwa. Mpayukaji alisema kuwa kukazania kila mnyama apate posho sawa ni kwenda kinyume na kanuni ya unyama. Na mara zote aliwahakikishia kuwa hakuna upungufu wa chakula.
Mpayukaji alisema wanafanya mabadiliko ya posho na si kupunguza. Lakini alisema bado posho ilikuwa ni kubwa ukilinganisha na wakati wa bwana Jones.
Kwa sauti kali, na harakaharaka alikuwa akiwasomea takwimu kuwaaminisha kwanba sasa wana ngano, nyasi na shayiri nyingi kuliko ilivyokuwa wakati wa bwana Jones, na kuwa walifanya kazi kwa muda mchache na maji yao ya kunywa yalikuwa salama zaidi. Aliwaambia kuwa sasa wanaishi muda nrefu zaidi, vifo vya utotoni vilipungua, na sasa walikuwa na nyasi nyingi za kulalia na tatizo la viroboto lilikoma. Wanyama waliamini yote yaliyozungumzwa. Kikweli, bwana Jones na mambo yake vilikuwa vimefutika kabisa vichwani mwao. Walijua kuwa kwa sasa maisha ni magumu na machungu, walipigwa na baridi na sehemu kubwa ya maisha yao ilikuwa ni kazi na kulala tu. Pamoja na hayo, walikuwa na furaha wakiamini kuwa enzi za bwana Jones hali ilikuwa mbaya zaidi. Na zaidi ni kuwa, nyakati za bwana Jones walikuwa watumwa na sasa wako huru. Na hilo lilikuwa jambo kubwa sana. Mpayukaji alisisitiza sana hilo.
Shambani pale wanyama walikuwa wameongezeka sana. Wakati wa majira ya kupukutisha, nguruwe wanne walikuwa wamezaa kwa pamoja jumla ya watoto thelathini na moja. Kwa aina yao, haikuwa kazi kufahamu kuwa walikuwa ni watoto wa Napolioni.
Baadaye wakanunua mbao na tofali kwaajili ya kujenga darasa katika bustani ya nyumba. Lakini kabla ya hilo, nguruwe wale walikuwa wakifundishwa na Napolioni mwenyewe akitumia jiko kama darasa. Sehemu yao ya kucheza ilikuwa ni kwenye bustani ya nyumba. Walizuiwa kucheza na watoto wa wanyama wengine. Ni wakati huu ndipo ilipitishwa sheria kuwa, kama mnyama mwingine akikutana na nguruwe njiani, yule mnyama anatakiwa kukaa pembeni kupisha nguruwe. Na kuwa nguruwe wote watakuwa na pendeleo la kuvaa utepe mwekundu mikiani mwao siku za jumapili.
Mwaka huo walipata mafanikio kiasi japo bado walikuwa na uhitaji wa pesa. Ilihitajika kununua mchanga, tofali na chokaa na kwaajili ya ujenzi wa darasa. Pia walihitajika kuanza kuweka akiba kwaajili ya ununuzi wa mashine ya kinu cha upepo. Mbali na hayo, walihitaji pia mafuta ya taa na mishumaa kwaajili ya nyumba walimoishi nguruwe. Ilihitajika pia sukari guru kwaajili ya Napolioni(Napolioni alikuwa amekataza nguruwe wengine kula sukari akisema inawafanya wawe wanene). Mahitaji yalikuwa ni mengi sana; misumari, makaa ya mawe, nyaya, chuma na biskuti za mbwa.
Ili kupata pesa hizo waliuza kiasi fulani cha nyasi, viazi na wakaongeza mkataba wa mayai kufikia mayai mia sita kwa wiki. Katika wakati huo, vifaranga wa kuku waliototolewa walikuwa wachache sana kiasi kwamba idadi ya kuku ikaanza kupungua.
Mwezi wa kumi na mbili ulipofika, posho ilipunguzwa, ikapunguzwa tena mwezi wa pili. Na ilipigwa marufuku kuwasha taa mabandani ili kubana mafuta.
Pamoja na hali hiyo, nguruwe waliishi vizuri kabisa, na walionekana wakizidi kunenepa.
Mchana mmoja katika mwezi wa pili wanyama walisikia harufu tamu. Ilikuwa ikitokea kwenye chumba cha kutengenezea bia, bwana Jones alikuwa ameacha zamani kukitumia chumba kile. Wanyama hawajawahi kusikia harufu tamu namna ile. Mnyama mmoja alisema ni harufu ya shayiri ikichachushwa. Wanyana walinusa kwa matamanio huku wakijiuliza iwapo chakula kile kinaandaliwa kwaajili yao, lakini hawakuona kitu. Jumapili iliyofuata ikatangazwa kuwa kuanzia wakati huo, shayiri yote itakuwa kwaajili ya matumizi ya nguruwe tu. Shamba lililokuwa nyuma ya bustani lilikuwa limeshapandwa shayiri.
Taarifa zikaenea kwamba, kila nguruwe alikuwa anapata nusu lita ya bia kila siku, na kuwa Napolioni alipata lita mbili..
Kilichowafanya wanyama wavumilie hali hizo ngumu, ni kwa sababu ya kuamini kuwa sasa wanaishi maisha yenye heshima na huru kuliko wakati wa bwana Jones. Kulikuwa na nyimbo nyingi, hotuba nyingi na maonyesho mengi sana. Napolioni alikuwa ameagiza kuwa kila wiki kuwe na tamasha. Lengo lilikuwa ni kuonyesha mapambano na mafanikio katika shamba la wanyama. Wanyama walikuwa wakiandamana kama wanajeshi huku nguruwe wakiwa mbele, walifuatiwa na farasi, ng'ombe, kondoo na mwisho kuku na bata bukini. Mbwa walitembea pembeni ya maandamano hayo. Mbele kabisa ya msafara alikuwepo jogoo wa Napolioni. Boxer na Clover walikuwa wanabeba bango kubwa lililoandikwa, "Maisha marefu kwa ndugu Napolioni!"
Baada ya hapo, yaliimbwa mashairi ya kumsifia Napolioni, ikifuatiwa na hotuba ya Mpayukaji akitoa takwimu za jinsi uzalishaji ulivyoongezeka na wakati mwingine walipiga risasi hewani. Kondoo walipenda sana maonyesho hayo. Na iwapo kama kuna mnyama alilalamika(wakati nguruwe na mbwa hawapo karibu) kuwa maonyesho hayo ni upotevu wa muda na wanateseka tu wakisimama kwenye baridi, kondoo walimnyamazisha kwa kusema "Miguu minne rafiki, miguu miwili adui. Miguu minne rafiki, miguu miwili adui!" Asilimia kubwa ya wanyama walifurahia maonyesho hayo. Walifurahi kwa sababu yaliwakumbusha kuwa sasa wanajitawala na matunda ya kazi wanazofanya ni yao peke yao. Walipoimba nyimbo, walipoandamana, walipomsikia Mpayukaji akisoma takwimu za mafanikio, jogoo akiwika mbele ya msafara, sauti ya bunduki na bendera ikipepea walisahau kwa muda kwamba hawana kitu matumboni mwao.
Ulipofika mwezi wa nne ikatangazwa kwamba shamba la wanyama sasa ni jamuhuri. Hili likafanya walazimike kuchagua rais. Kulikuwa na mgombea mmoja tu, Napolioni, ambaye alichaguliwa kwa kura zote. Siku hiyo hiyo ikatangazwa kuwa nyaraka zingine zinazoonyesha ushirikiano wa Snowball na bwana Jones zimepatikana. Nyaraka zilionyesha kwamba, siyo tu Snowball alipanga hila ili washindwe vita ya Kibanda cha ng'ombe, bali alikuwa anapigana upande wa bwana Jones waziwazi. Na kiukweli yeye ndiye alikuwa kiongozi wa kikosi cha binadamu, na aliongoza uvamizi akipiga kelele akisema, "maisha marefu kwa binadamu!" Ikasemwa kuwa majeraha mgongoni mwa Snowball yalisababishwa na kuumwa na Napolioni.
Katikati ya majira ya joto, Musa, yule kunguru, akaonekana shambani baada ya kutoonekana kwa miaka kadhaa. Tabia yake ilikuwa haijabadilika kabisa, hakufanya kazi na aliendelea kusema kuhusu uwepo wa mlima wa sukari guru.
"Ndugu zanguni, kule juu," aliongea huku akionyesha angani kwa mdomo wake. "Kule juu nyuma ya lile wingu jeusi mnaloliona ndiko uliko mlima wa sukari guru. Huko ndiko wanyama tunapumzika milele!" Hata alisema kuwa amewahi kufika huko baada ya kuruka juu sana, aliwaambia kuwa aliona eneo lisilo na mwisho lililojaa keki na sukari guru iliyokuwa inajiotea. Wanyama wengi walimuamini. Kutokana na ugumu wa maisha waliona kuwa lazima kuna dunia yenye maisha mazuri zaidi.
Kitu ambacho hakikueleweka vizuri ni Mtazamo wa nguruwe juu ya Musa, ulikuwa tofauti kabisa. Walisema kwa dharau kuwa habari juu ya uwepo wa mlima wa sukari guru ni uongo mtupu. Pamoja na hilo walimruhusu aendelee kuwepo shambani, bila kufanya kazi yoyote na walimpatia bia kila siku.
Baada ya Boxer kupona kwato yake akaanza kufanya kazi kwa bidii kuliko alivyowahi kufanya. Lakini si yeye tu, mwaka ule wanyama wote walifanya kazi kama watumwa. Mbali na kazi za shambani na kujenga upya kinu cha upepo, pia kulikuwa na kazi ya kujenga shule kwaajili ya nguruwe wadogo. Ujenzi huo ulianza mwezi wa tatu. Haikuwa rahisi kuvumilia kazi ngumu huku wakiwa na njaa, lakini ilionekana hilo halimsumbui Boxer. Hakuonyesha dalili zozote za kuchoka japo kiukweli nguvu zake hazikuwa kama hapo mwanzo. Ukimuangalia ungegundua kama umri umeenda kwa ngozi yake kupoteza mng'aro, lakini si kwa jinsi alivyofanya kazi.
Wengine walikuwa wanasema, "Hali ya Boxer itarejea nyasi zikichipua katika majira ya kuchipua." Lakini hata majira ya kuchipua yalipofika bado hali ya Boxer haikuboreka. Kuna nyakati ni nia tu ndiyo ilionekana inamuwezesha kufanya kazi, lakini kimwili alikuwa hajiwezi kabisa.
Kwa mara nyingine, Clover na Benjamini walimuonya kuhusu afya yake lakini hakusikiliza. Aliwaambia katimiza miaka kumi na mbili lakini hakujali, alichojali yeye ni kukusanya mawe ya kutosha kabla ya kustaafu.
Siku moja jioni wakati wa majira ya joto, kulitokea tetesi kuwa kuna jambo limempata Boxer. Alikuwa ameenda kuvuta mawe machimboni akiwa peke yake na ikasemwa alianguka. Tetesi hizo zilithibitika kuwa kweli pale njiwa wawili walipokuja mbio na habari kuwa Boxer kaanguka. "Boxer ameanguka na hawezi kuinuka!"
Karibu nusu ya wanyama wote pale shambani wakatoka mbio kuelekea eneo la ujenzi wa kinu cha upepo. Hapo wakamkuta Boxer amelala mbele ya mkokoteni. Alikuwa amenyoosha shingo na hakuweza hata kuinua kichwa. Macho yalikuwa yamemtoka, na damu ilikuwa imemtoka mdomoni. Clover akapiga magoti pembeni yake na kwa sauti ya huzuni akasema, "Boxer, unajisikiaje?"
"Mapafu yananiuma," akasema Boxer kwa sauti dhaifu. "Lakini msijali, nafikiri mtaweza kumalizia ujenzi bila ya mimi. Mawe mengi yameshakusanywa. Hata hivyo nilibakiza mwezi mmoja tu kustaafu. Na sababu na Benjamin naye amezeeka, pengine naye ataruhusiwa tustaafu pamoja."
"Inabidi tutafute msaada mara moja," alisema Clover. "Mmoja aende kumwambia Mpayukaji kilichotokea." Wanyama wote wakatoka mbio kwenda kumwambia Mpayukaji, walibaki Clover na Benjamin tu. Benjamini alikaa pembeni ya Boxer, hakuongea chochote bali alikuwa akiwafukuza nzi waliomzonga Boxer kwa mkia wake. Baada ya kama robo saa, Mpayukaji akafika akiwa mwenye masikitiko makubwa. Akasema kuwa ndugu Napolioni kasikitishwa sana na kilichompata Boxer, mfanyakazi muaminifu kabisa pale shambani. Kwa msaada, alikuwa akifanya mpango wa Boxer kwenda hospitali huko Willingdon. Kidogo wanyama wakapata matumaini baada ya kusikia hilo.
Mbali na Moli na Snowball, hakuna mnyama mwingine ambaye amewahi kutoka nje ya shamba la wanyama. Na wanyama hawakupenda kumuona ndugu yao akitibiwa na binadamu, lakini Mpayukaji akawatoa wasiwasi kuwa daktari wa wanyama huko Willingdon atamtibu Boxer vizuri kuliko akiwa pale shambani.
Baada ya nusu saa, Boxer akapata nafuu hivyo walimsaidia kusimama na kumpeleka bandani mwake.
Nguruwe walikuwa wamepata kopo la dawa ndani ya nyumba ya bwana Jones na wakampatia Clover ampatie Boxer mara mbili kwa siku baada ya chakula. Jioni, Clover alikuwa akikaa na Boxer wakiongea. Boxer alisema kuwa hajutii kile kilichomtokea. Alisema, kama akipona anatarajia kuishi miaka mitatu zaidi. Hiyo ataitumia kustarehe na kujiburudisha kwenye malisho.
Atakuwa kwa mara ya kwanza amepata nafasi ya kujisomea na kujielimisha. Alisema alipanga kutumia maisha yake yaliyobaki kujifunza zile herufi ishirini na mbili zilizobaki.
Benjamini na Clover hawakuwa na Boxer muda wote, ni baada ya kazi tu. Siku ya pili mchana, mkokoteni ulifika kumchukua Boxer. Wanyama karibu wote walikuwa kwenye palizi, wakisimamiwa na nguruwe.
Walishangaa kumuona Benjamini akikimbia kutokea kwenye majengo huku akipiga kelele kwa sauti yake yote. Ilikuwa ni mara yao ya kwanza kumuona Benjamin katika hali ile, kiukweli ilikuwa ni mara yao ya kwanza kumuona akikimbia.
"Haraka! Njooni haraka! Wanamchukua Boxer!" Bila hata kusubiri maelekezo ya nguruwe wanyama wakaacha kazi na kutoka mbio kuelekea kuelekea kwenye mabanda. Uwanjani wakakuta mkokoteni wa kubebea wanyama. Sehemu ya kupakia wanyama ilikuwa imefungwa na farasi wawili walikuwa tayari kuukokota. Pembeni yake uliandikwa maneno maneno fulani na uliendeshwa na mtu mmoja aliyeonekana mjanja mjanja. Walipotazama kibandani mwa Boxer hawakumuona.
Wanyama wakasogele mkokoteni ule na kusema, "Kwa heri Boxer!"
"Wapumbavu! Wapumbavu wakubwa!" Akafoka Benjamin. "Inamaana hamuoni kile kilichoandikwa pembeni ya mkokoteni?"
Hilo liliwafanya wanyama watulie, Muriel akaanza kusoma yaliyoandikwa lakini Benjamin akamsukuma pembeni na kuanza kusoma.
"'Alfred Simmonds, Tunahusika na uchinjaji wa farasi, utengenezaji wa gundi. Tunauza ngozi, mifupa na chakula cha mbwa. Tunapatikana Willingdon.' Hilo linamaanisha nini? Wanampeleka Boxer kuchinjwa!"
Kilio cha uoga na uchungu kikalipuka kutoka kwa wanyama wote. Wakati huohuo yule muongoza mkokoteni akawachapa farasi wake na akaanza kuondoka. Wanyama wote wakafuata huku wakilia kwa sauti ya juu kabisa, Clover akiwa mbele. Mkokoteni ukazidi kushika kasi na Clover naye akajaribu kukimbia kuufuata, japo miguu yake ilikuwa imeanza kuwa dhaifu
"Boxer! Boxer! Boxer!" Aliita Clover kwa sauti. Boxer akatoa sura na akachungulia kupitia dirisha dogo lililokuwepo nyuma ya mkokoteni ule. "Boxer! Boxer toka haraka, wanaenda kukuua!" Alipaza sauti Clover.
Wanyama wote wakaanza kupaza sauti wakisema "Boxer toka haraka!" Lakini mkokoteni ukaongeza kasi na kuwaacha. Haijulikani kama Boxer alielewa kilichosemwa na Clover, lakini ndani ya muda mfupi akaanza kupiga mlango wa nyuma kwa miguu yake. Zamani teke moja tu la Boxer lingetosha kusambaratisha mkokoteni ule, lakini sasa hakuwa na nguvu hizo. Na baada ya muda mfupi sauti ya kupiga mlango haikusikika tena.
Wanyama wakaanza kuwaomba wale farasi wawili waliokuwa wakivuta mkokoteni. "Ndugu, ndugu! Msimpeleke ndugu yenu kufa," walipaza kwa sauti. Lakini wapumbavu wale hawakuelewa kinachoendelea na badala yake wakaongeza kasi zaidi. Mnyama mmoja aliwaza kukimbia na kwenda kufunga geti la shambani, lakini ikawa kuchelewa na mkokoteni ulipita, Boxer hakuonekana tena.
Siku tano baadaye ikatangazwa kuwa Boxer amekufa akiwa hospitali huko Willingdon. Ilisemwa kuwa wahudumu walijitahidi kumponya kadri wawezavyo lakini ilishindikana. Mpayukaji ndiye aliyeleta habari. Alisema alikuwa pembeni ya Boxer katika dakika zake za mwisho.
"Sijawahi shikwa na hisia kali kama wakati ule!" Alisema Mpayukaji huku akijifuta machozi kwa kwato zake. "Nilikuwa pembeni ya kitanda chake hadi nwisho. Mwishoni alipokuwa hoi hata hakuweza kuongea vizuri alininong'oneza, alisema kitu pekee anachosikitika ni kufa kabla ya kinu cha upepo kukamilika. Aliniambia, 'Shime ndugu-zanguni, tusonge mbele kwa jina la mapinduzi. Lidumu shamba la wanyama, aishi maisha marefu ndugu Napolioni! Mara zote Napolioni yupo sahihi.' Hayo ndiyo yalikuwa maneno yake ya mwisho."
Lakini ghafla Mpayukaji akabadilika, macho yakawa makavu huku akiyapepesa huku na huko. Kisha akaanza kusema kuwa kunatetesi amezisikia. Tetesi za kipumbavu na mbaya kabisa. Kuna wanyama waliona mkokoteni uliombeba Boxer umeandikwa "mchinjaji," nao wakafikia mkataa kuwa Boxer ameenda kuchinjwa! Siamini kama wanyama wanaweza kusema maneno kama haya, alisema Mpayukaji. Mnyama anawezaje kuwa mjinga kiasi hiki!
Maelezo ya kilichotokea yalikuwa rahisi tu. Ilisemwa kuwa zamani mkokoteni ule ulikuwa mali ya mchinjaji na ulikuwa umenunuliwa na daktari wa wanyama. Bahati mbaya alikuwa bado hajabadilisha maandishi. Hilo ndilo lililoleta mkanganyiko.
Wanyama wakaridhika na kushuka jazba baada ya kusikia hilo. Mashaka yote yakaondoka pale Mpayukaji alipowaeleza zaidi jinsi Boxer alivyohudumiwa vizuri na gharama kubwa ya dawa ambayo Napolioni alilipa bila hata kuuliza mara mbili. Huzuni ya kifo cha ndugu yao ikaondoka baada ya kujua kuwa alihudumiwa vizuri hata mwisho. Napolioni alitokea kwenye mkusanyiko wa jumapili iliyofuata, na akasema machache kwa heshima ya Boxer.
Akasema kwa bahati mbaya haikuwezekana kuleta mwili wa ndugu yao pale shambani kwa mazishi, lakini ameagiza taji kunwa litengenezwe na kwenda kuwekwa kwenye kaburi la Bixer. Pia siku chache zijazo nguruwe wamepanga kufanya karamu kwaajili ya kumbukumbu ya Boxer. Napolioni alimaliza hotuba yake kwa kusema kaulimbiu za Boxer. "Ndugu Napolioni yupo sahihi mara zote," na "Nitafanya kazi kwa bidii" akaongezea kuwa ni muhimu kila mnyama akazitumia kaulimbiu hizo maishani.
Siku ya karamu, gari la muuza mahitaji kutoka Willingdon lilifika katika nyumba ya shambani. Usiku huo kulisikika kelele za kuimba zilizofuatiwa na kelele za ugomvi ambazo ziliisha saa tano usiku. Siku iliyofuata hakuna nguruwe aliyeamka hadi ilipofika mchana. Habari zilisambaa kuwa, kwa namna fulani nguruwe walikuwa wamepata pesa za kununulia mvinyo.