Wakati Serikali ikiwasilisha tathmini ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024 na mpango wa maendeleo kwa mwaka 2025/26, baadhi ya wananchi na wachambuzi wameibua maswali kuhusu tafsiri ya ukuaji wa uchumi, hasa kufuatia kauli ya kuwa “uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara katikati ya mdororo wa uchumi wa dunia.”
Akizungumzia mjadala huo katika kikao cha 52 cha Bunge la 12 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu vipimo vya kimataifa vinavyotumika kupima afya ya uchumi wa taifa.
Prof. Mkumbo ameeleza kwamba licha ya changamoto zilizoikumba dunia, Tanzania imebaki na mwelekeo chanya wa kiuchumi huku mfumuko wa bei wa Tanzania ukionesha utulivu wa kipekee.