China ni nchi kubwa inayoendelea, na pia ni nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi nyingine zinazoendelea, hususan za barani Afrika, kujipatia maendeleo na kuinua uchumi wao. Katika kufanikisha hilo, China imekuwa na ushirikiano na nchi za Afrika katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, uchumi na biashara, elimu, na sekta nyingine nyingi.
Nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa umeme wa uhakika, jambo ambalo linadhoofisha juhudi za nchi hizo za kupambana na umasikini. Kutokana na hilo, China imeanzisha ushirikiano katika sekta ya nishati na nchi nyingi za Afrika kwa kujenga, kukarabati, na hata kupanua vituo vya umeme katika nchi hizo.
Tukitolea mfano nchini Zimbabwe, ambako kampuni ya Sinohydro ya China ilikarabati na kupanua kitengo cha 7 na cha 8 katika Kituo cha Uzalishaji wa Umeme kwa Joto la Ardhini cha Hwange. Hatua ambayo iliondoa tatizo sugu la ukosefu wa umeme na kuisaidia nchi hiyo kuwa na umeme wa uhakika.
Nchini Guinea, Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Maji cha Kaleta kilichojengwa na Ushirikiano wa Kimataifa wa Maji na Umeme (CWE), kampuni tanzu ya Kampuni ya Mawasiliano na Ujenzi ya China, kinaonekana kando ya Mto Konkoure, ambao unatiririsha maji yake kutoka nyanda za juu za Fouta Djallon, katikati ya nchi hiyo. Kituo hicho ambacho kinatoa huduma ya umeme kwa mji mkuu wa nchi hiyo, Conakry, pamoja na vijiji vilivyo katika maeneo ya milima kaskazini mwa nchi hiyo, kwa sasa picha yake inaonekana katika noti ya franca 20,000 ya Guinea.
Mwezi Agosti mwaka 2015, Kituo cha Umeme wa Maji cha Kaleta kilianza rasmi kufanya kazi rasmi, na kwa mwaka, kinaweza kutoa saa za kilowati bilioni 1.125 za umeme na kuweza kuziba karibu nusu ya pengo la umeme kitaifa.
Alhassane Bangoura, aliyefanya kazi kama mkalimani katika mradi huo, anasema kabla ya ujenzi wake, umeme kukatika ilikuwa ni jambo la kawaida katika jamii yake, tatizo ambalo lilikuwa linatokea katibu kila siku, na wakati mwingine kudumu kwa saa kadhaa.
Meneja fedha wa Kampuni ya Kusimamia Kituo cha Umeme cha Kaleta, Djenabou Diallo anasema, mtandao wa usambazaji wa umeme uliojengwa kando ya kituo hicho unapeleka umeme kutoka mji mkuu wa nchi hiyo hadi wilaya 11, na kwa mara ya kwanza, maeneo ya ndani zaidi yanaweza kupata umeme.
Mwaka 2021, Kituo cha Umeme wa Maji cha Souapiti, ambacho pia kilijengwa na kampuni ya CWE sehemu ya juu ya Mto Konkoure, kilianza rasmi kufanya kazi. Vikiwa na uwezo wa kutoa megawati 690 za umeme, vituo hivyo viwili, Kaleta na Souapiti, kwa sasa vinachangia asilimia 80 ya upatikanaji wa umeme nchini Guinea, na kuikomboa nchi hiyo kutoka utegemezi wa mafuta.
Nishati hii ya kijani pia imeigeuza Guinea kutoka nchi yenye uhaba wa umeme hadi kuwa muuzaji, ikitoa umeme kwa nchi sita za jirani, ikiwemo Senegal, Gambia, Guinea-Bissau na Sierra Leone.