Kwenye ghorofa ya tatu ya Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, majora mengi ya vitambaa yaliyopangwa vizuri yamejaza rafu huku wateja kutoka kila pembe ya nchi na nje ya nchi wakiingia ndani.
Na kwa Ayoub Katuga, mfanyabiashara wa Tanzania ambaye biashara yake ya jumla ya vitambaa imepata kasi mpya ndani ya jengo hili la kisasa katika eneo la Ubungo, uso wake umejaa bashasha.
"Mazingira haya yamebadilisha kabisa jinsi tunavyofanya biashara," Katuga alisema, akionesha kwenye chumba angavu na kilichopangiliwa vizuri.
"Wateja wetu wanafurahia kuja hapa, na jambo hilo pekee linaleta tofauti kubwa," aliambia Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni.
Katuga ni mkurugenzi mkuu wa Ascon Africa, shirika mama. Alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara wa kwanza wazawa kufungua duka katika kituo hicho ambacho ni kitovu cha biashara kilichojengwa na Wachina kwa lengo la kupunguza vikwazo vya biashara kati ya China, Tanzania na eneo pana la Afrika Mashariki.
"Nilikuja hapa mwezi Agosti na kufungua duka chini," alikumbuka. "Sasa tumeongeza duka jingine jipya hadi ghorofa ya pili, tukiuza vitambaa kwa jumla. Ukuaji huo unatosha kuelezea hadithi."
Kituo hicho kikiwa katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, ni zaidi ya soko la kawaida. Kikiwa kimeundwa kama jukwaa la biashara na usambazaji la kituo kimoja, kina vyumba vya maonyesho, ghala, uratibu wa usafirishaji, huduma ya msaada wa forodha na biashara chini ya jengo moja.
Kwa Katuga, ambaye wateja wake wanatoka Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi na Uganda, kituo hicho kimefungua milango mipya.
"Mwanzoni, biashara nyingi za jumla zilikuwa zimejazana Kariakoo," alisema, akimaanisha wilaya ya Dar es Salaam iliyokuwa maarufu huko nyuma kwa biashara. "Lakini miundombinu yake imejaa watu. Na hapa, kila kitu ni cha kisasa na kimepangwa vizuri. Wateja wanajisikia vizuri, na hilo lijenga uaminifu."
Alisema jukwaa hilo limeimarisha mnyororo wake wa biashara na China, ambako bidhaa zake nyingi hutoka huko. "Linatuunganisha moja kwa moja na wauzaji wa China na kuwavutia wanunuzi wa kikanda kuja Tanzania. Huo ni mtindo mpya wa biashara," alisema.
Katika sehemu ya chini ya kituo hicho, saa za kisasa, power banks na vifaa vya sauti vinang'aa chini ya taa za kuonyesha katika Wawlyn Limited, kampuni ya teknolojia iliyoanza shughuli katika kituo hicho mapema Agosti na kumilikiwa na mfanyabiashara wa Somalia.
"Biashara inaendelea vizuri," alisema Esther Benedictor Patrick, meneja wa duka na mwakilishi wa kampuni. "Wawlyn imejikita sana Afrika, na lengo letu ni kukua kote barani. Kuwa hapa kunatusaidia kufikia soko pana la Afrika."
Wawlyn imejikita kwenye usanifu, utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya kielektroniki vya kisasa vinavyovaliwa. Kwa mujibu wa Patrick, uamuzi wa kampuni hiyo kufanya biashara katika kituo hicho unaendana sana na mkakati wake wa muda mrefu.
"Tunaona EACLC kama daraja la asili kati ya China na Afrika," alisema. "Ushirikiano kati ya China na Afrika hauhusu kununua na kuuza tu, bali unahusu ushirikiano wa muda mrefu, uhamisho wa teknolojia na vifaa vya kuaminika."
Makampuni ya Kichina pia yanaanzisha kwa kasi biashara zao katika kituo hicho. Mojawapo ya kampuni kama hiyo ni MAFC, inayohusika na uuzaji wa samani, taa na vifaa vya ujenzi. Baada ya kukarabati chumba chake cha maonyesho mwezi Agosti, kampuni hiyo ilifunguliwa rasmi Oktoba mwaka huu.
"Biashara imekuwa ikiimarika siku hadi siku," alisema Wang Xinggang, mwakilishi wa kampuni ya China, akibainisha kuwa Tanzania ilichaguliwa kwa faida zake za kimkakati, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu, upatikanaji wa bahari, utulivu wa kisiasa na uwezo mkubwa wa maendeleo.
Cathy Wang, meneja mkuu wa EACLC, anasema kuanzishwa kwa kituo hicho kulichochewa na mahitaji ya kuboresha ufanisi na muundo wa biashara kati ya China na Afrika.
"Nia yetu ya awali ilikuwa kujenga jukwaa la biashara rahisi, lenye ufanisi zaidi na salama," alisema. “Tukiwa tunashughulikia ukosefu wa ulinganifu wa taarifa na gharama kubwa za usafirishaji, tunalenga kuiondoa biashara kati ya China na Afrika kwenye shughuli ndogo zilizogawanyika na kuipeleka kwenye mfumo uliopangwa zaidi na unaotegemea jukwaa."
Alisisitiza kwamba kituo hicho kimeundwa kama mlango kamili wa biashara ya pande mbili badala ya soko la kawaida tu.
"Mbali na kufanya biashara ya jumla na rejareja, kituo hiki kinaunganisha uratibu wa usambazaji, ghala la kisasa, vifaa vya kuvuka mipaka, huduma za maonesho na ununuzi wa hapohapo," meneja alisema. "Kwa kuchanganya biashara, maonesho na vifaa katika eneo moja, lengo ni kutaka kuongeza muunganisho, kuboresha ufanisi wa mzunguko na kuongeza faida ya pande zote pamoja na maendeleo kati ya China na Afrika."
Kwa sasa, kituo hiki kinawakaribisha wafanyabiashara kutoka China na Tanzania, pamoja na wafanyabiashara kutoka nchi jirani, ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda na Somalia. Kinauza bidhaa mbalimbali kuanzia vifaa vya ujenzi na mashine hadi vifaa vya elektroniki, vitambaa na mahitaji ya kila siku.
Ikitupia macho mbele, EACLC inapanga kuimarisha ushirikishi wa kidijitali. Mifumo ya kisasa ya ghala, ufuatiliaji wa hesabu kwa wakati halisi na muunganisho wa biashara ya mtandaoni yote ni sehemu ya mpango.
"Wafanyabiashara hawatahitaji tena kutafuta watoa huduma za usafirishaji waliogawanyika," meneja alielezea. "Wataweza kufuatilia hesabu na oda zao kwa wakati halisi, na kuboresha ufanisi wa uendeshaji."
Mbali na biashara, kituo hicho pia kimekuwa jukwaa la ushirikiano mpana wa kiuchumi kati ya China na Afrika. Kimesaidia kurahisisha ushiriki wa Tanzania katika maonesho makubwa ya biashara nchini China, huku kikiwezesha uwepo wa makampuni ya Kichina katika Maonesho makubwa ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ya kila mwaka nchini Tanzania.
Kwa wafanyabiashara kama Katuga, matokeo ya kituo hicho tayari yanaonekana.
"Mahali hapa pamenisaidia kupanua biashara yangu na kufikia masoko mapya," alisema. "Wateja kutoka kote Afrika sasa wanakuja Tanzania kununua bidhaa zao hapa."