Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Katika mkusanyiko huu wa Waislam chini ya Muslim Development Fund (MDF) Mwenyekiti wake akiwa Mzee Kondo, Mzee Kitwana Kondo alisema kuwa nia ya MDF ni kuwa na Chuo Kikuu na kujenga shule nchi nzima.
Maneno haya Mzee Kondo anawaambia Waislam na Rais Mkapa mwaka wa 2004.
Ikiwa huijui historia ya Waislam katika kutafuta elimu maneno ya Mzee Kondo kwako ni kama vile Waislam ndiyo kwanza wametupa shuka chini wanaamka usingizini kitandani wanataka na wao sasa wajenge shule na Chuo Kikuu.
Haikuwa hivyo.
Ukweli ni kuwa Waislam walianza kujenga shule zao toka ukoloni.
Ukweli ni kuwa baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 Waislam waliitisha Muslim Congress mwaka wa 1962 kujadili na kupanga upya mipango ya ujenzi wa shule na mwaka wa 1968 Waislam waliweka jiwe la msingi wa Chuo Kikuu.
Jiwe hili liliwekwa na Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akishuhudiwa na Mufti Sheikh Hassan bin Ameir na Tewa Said Tewa Rais wa EAMWS upande wa Tanganyika.
Wakati huo mwaka wa 1968 Rais Benjamin William Mkapa alikuwa Mhariri Mkuu wa magazeti ya TANU - The Nationalist na Uhuru.
Kitwana Kondo siku ile pale ukumbini anamueleza Rais Mkapa historia ambayo yeye Rais Mkapa si mgeni nayo kwani habari ya Waislam kujenga Chuo Kikuu ilikuwa habari kubwa mno na anaijua vyema kwani na ilichapwa na magazeti yake.
Si hilo tu magazeti haya ambayo yeye alikuwa Mhariri Mkuu yalikuwa mstari wa mbele kuandika mgogoro wa EAMWS uliosababisha EAMWS kuvunjwa na serikali na kuundwa BAKWATA.
Nilikuwa mmoja wa Waislam waliokuwa ndani ya ukumbi ule siku hii Rais Mkapa alipowapa Waislam majengo ya TANESCO Morogoro ili yawe Chuo Kikuu Cha Waislam.
Laiti EAMWS isingepigwa marufuku na serikali Waislam wangekuwa na Chuo Kikuu toka mwaka wa 1968.
Kuvunjwa kwa EAMWS na kuundwa BAKWATA ndiyo mwisho wa juhudi za Waislam kujenga shule na Chuo Kikuu walichokusudia.
Historia ya Waislam wa Tanzania katika juhudi ya kutafuta elimu ni ndefu na imejaa misukosuko mingi.
Hotuba hii ya Mzee Kondo imenikumbusha maneno ya Mufti Sheikh Hassan bin Ameir alipowaambia Waislam mara tu baada ya kupata uhuru kuwa, "Waislam tumeupigania uhuru hadi umepatikana sasa tujenge shule tujielimishe tutawale nchi pamoja na wenzetu."