Klabu ya vvip ya vilio: Mtihani wa kupoteza "watu wa maana" na ile gesi ya kusahaulishwa

Klabu ya vvip ya vilio: Mtihani wa kupoteza "watu wa maana" na ile gesi ya kusahaulishwa

Kijana wa Ifoza

JF-Expert Member
Joined
Oct 31, 2025
Posts
1,180
Reaction score
2,302
Wana-JF,
Inavyoonekana, ulimwengu una aina fulani ya mzaha mchungu sana kwetu sisi walala-hoi. Katika miezi miwili hii iliyopita, msiba wa kitaifa umehamishwa rasmi kutoka kwenye vumbi la mitaa ya pembezoni ambako mamia ya walala-hoi walizikwa kwa haraka baada ya ile ishu ya Oktoba 29 ya mwaka jana. Badala yake, mitambo yote ya vilio, ving'ora, na taarifa za rambirambi za kitaifa imeelekezwa kwa daraja la juu kabisa la "Wateule".

Katika mchezo huu wa kuigiza, wenye nchi wamegundua ghafla jinsi inavyouma kumpoteza mtu wa karibu—ingawa wao wanalia huku wakiwa wamezungukwa na viyoyozi na posho za vikao vya dharura vya maombolezo.

1. Ukata vs. "Bajeti ya Pole": Msiba wa Mamilioni na Zero ya Walala-Hoi
Hakuna kitu kinachoonyesha ubaguzi wa kifo nchini kama hesabu za gharama za mazishi. Kwa familia za raia 500 (kwa Mujibu wa yule babu Jaji mustaafu) waliotangulizwa mbele ya haki kwenye ghasia za Oktoba 29, akaunti ya fidia ya serikali imeganda kwenye shilingi sifuri. Inavyoonekana, Bajeti Kuu ya Serikali haina fungu la "watu waliopotezwa na demokrasia".

Tofauti kabisa na kule juu, mitambo ya huzuni ya VVIP inalainishwa na mafuta ya kodi za wananchi. Ukumbi wa msiba umetandikwa mazulia mekundu, mashangingi ya V8 yanajazwa wese la mamilioni ili kwenda kutoa pole, na vyombo vya habari vya taifa vinakatisha vipindi ili kuonyesha jinsi "wenzetu" wanavyohuzunika. Ujumbe kutoka Hazina upo wazi kabisa:

“Tanzania kuna aina mbili za vifo: Kifo cha VVIP kinachogharamiwa na kodi zako, na kifo chako wewe unayegharamiwa na machozi ya ndugu zako tu.”
2. Diplomasia ya Mashaka: Sanaa ya "Kulaani Bila Kutaja Jina"
Hatuwezi kusahau mchango wa "marafiki zetu wa maendeleo"—mabalozi wa nchi za nje na mashirika ya kimataifa. Wakati wa maafa ya Oktoba 29 ya mwaka jana, mabalozi hawa walionyesha umahiri mkubwa wa kutumia lugha ambayo imesomewa vyuo vikuu vya Oxford na Harvard: lugha ya "Kuhuzunika Kidiplomasia."
Wakati miili ikiokotwa mitaani, matamko yao yalijaa sentensi kama: "Tunafuatilia kwa karibu sana hali inayojiri, na tunatoa wito kwa pande zote mbili kujizuia." Hii ni lugha tamu ya kiingereza inayomaanisha: "Tunajua nani anapiga watu, lakini bado tunahitaji saini yake kwenye mikataba ya madini na ile gesi ya Mtwara, kwa hiyo tutajifanya hatuoni."
Ajabu ni kwamba, katika miezi hii miwili ya misiba ya wakubwa, diplomasia hii imebadilika ghafla kuwa ya vitendo. Wale mabalozi waliokuwa wanatoa matamko ya kurasa mbili yenye maneno magumu ya kisheria kufuatia vifo vya raia 500 (kufuatana na jaji Mstaafu), sasa wameonekana wakisukumana milangoni kwenda kusaini vitabu vya maombolezo ikulu na nyumbani kwa IGP. Ghafla, lugha imekuwa nyepesi, haina mzunguko, na imejaa "majonzi makubwa ya dhati." Ni uthibitisho kwamba hata kwa marafiki zetu wa nje, haki za binadamu ni bidhaa inayopimwa kwa uzito wa cheo cha marehemu.
“Mabalozi wa nje wana akili sana; mwaka jana walitoa wito wa 'pande zote mbili kujizuia' kulia, lakini mwezi huu wamesukumana wenyewe kusaini kitabu cha maombolezo.”

3. Miujiza ya Tezi za Macho: Ghafla Machozi Yanatoka!
Sehemu inayosisimua zaidi katika tasnia hii ya maombolezo ni miujiza iliyotokea kwenye tezi za macho za wanasiasa wetu. Kwa mwaka mzima, nyuso za wakuu wa mikoa, mawaziri, na chawa wa chama zilikuwa ngumu kama jiwe la kusagia. Walitazama taarifa za vifo vya watu 500 ( kwa mujibu wa Jaji Mstaafu) bila hata kupepesa macho, wakiwa wamekauka kabisa utu.
Katika miezi hii miwili, lile kundi lililokuwa likiita waathirika wa Oktoba 29 kuwa ni "wavunja sheria", wamewasili Dar es Salaam wakiwa wamebana vitambaa vyeupe mkononi, wakilia kwa sauti mbele ya kamera.
“Machozi ya viongozi wetu yana algorithm ya ajabu sana; yanatoka tu pale msiba unapokuwa na namba ya usajili ya STK au STL.”
Wakati serikali ikitoa machozi ya dhati kwa vifo vya kiasili vya wazee na wenza wa kisiasa, wananchi wanabaki kutazama tamthilia hii. Ukweli unaouma ni mmoja tu:
“Ukiona unataka kupotea au kufa nchini, hakikisha kwanza unatafuta undugu na Mkuu wa Jeshi la Polisi, la sivyo utaishia kuwa 'collateral damage' kwenye ripoti ya habari ya saa mbili usiku.”

Nawasilisha. Je, tunaamini kuna siku kifo cha mnyonge kitakuwa na thamani mbele ya mfumo huu?
 
Back
Top Bottom