Wizara ya Ardhi
Govt Institution
- May 14, 2024
- 306
- 165
Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imewataka wananchi kutumia mfumo wa kidijiti wa E-Ardhi ili kupata huduma mbalimbali kwa urahisi, ikiwemo kupata hati miliki bila kulazimika kufika katika ofisi za ardhi.
Wito huo umetolewa na Afisa Ardhi Mteule kutoka Manispaa ya Kahama, Richard Mayiku, wakati akizungumza kwenye zoezi la kliniki ya ardhi linaloendelea hivi sasa katika Ofisi za Kata ya Mwendakulima.
Mayiku ameeleza kuwa Serikali imeanzisha mfumo huo wa E-Ardhi kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa njia ya mtandao, jambo ambalo linaongeza ufanisi na kupunguza kwa kiasi kikubwa muda ambao wananchi wamekuwa wakiutumia kufuatilia masuala ya ardhi.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kuhudumiwa kupitia mfumo huo wakati wa kliniki hiyo wameipongeza Serikali kwa hatua hiyo madhubuti, wakibainisha kuwa imesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa kero na urasimu uliokuwepo awali.
Ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma, Ofisi ya Ardhi Kahama imeandaa dawati maalumu kwa ajili ya kuwasaidia na kuwaelekeza wale wote wasiofahamu namba au namna ya kutumia mfumo huo pamoja na huduma nyinginezo zinazopatikana kwa njia ya mtandao.