Wizara ya Ardhi
Govt Institution
- May 14, 2024
- 306
- 165
TABORA: Kliniki ya Ardhi Kidijiti mkoani Tabora imehitimishwa kwa mafanikio makubwa, huku wananchi wakiondoka na tabasamu baada ya kukabidhiwa jumla ya Hati Milki za Ardhi 389, hatua inayochangia kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa hati hizo, Msajili wa Hati Msaidizi Mkoa wa Tabora, Bw. Samweli Ibrahimu, amesema Kliniki ya Ardhi Kidijiti imekuwa na mafanikio makubwa katika kurasimisha na kuimarisha umiliki wa ardhi mkoani humo.
Amesema matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi yameendelea kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, kwa kuwezesha kushughulikia huduma za ardhi kwa ufanisi, haraka na kwa uwazi zaidi.
“Kliniki hii imeleta mafanikio makubwa katika kurasimisha umiliki wa ardhi mkoani Tabora. Wananchi wamepata fursa ya kupata huduma za ardhi kwa urahisi na hatimaye kupata hati zao,” amesema Bw. Samweli.
Amesema hati hizo ni muhimu katika kuwapa wananchi uhakika na usalama wa umiliki wa ardhi, pamoja na kuwawezesha kutumia ardhi zao kama nyenzo ya kiuchumi na maendeleo.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliopokea hati hizo wameeleza furaha yao, wakisema upatikanaji wa hati unawapa uhakika zaidi juu ya umiliki wa maeneo yao na kuwaondolea hofu ya migogoro ya ardhi.
Kliniki ya Ardhi Kidijiti Mkoani Tabora imetoa pia fursa kwa wananchi kupata elimu na huduma mbalimbali zinazohusiana na ardhi, ikiwa ni pamoja na uhamasishaji kuhusu matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi katika kupata huduma kwa njia ya kidijiti.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kusisitiza matumizi ya mifumo ya kidijiti katika kuboresha huduma za ardhi kwa wananchi, kwa kuzingatia kaulimbiu: “e-Ardhi – Huduma Popote.”