Zanzibar Yaibanjua Zambia 4-3, Yatinga Nusu Fainali
Timu ya soka ya Zanzibar imefanikiwa kutinga nusu fainali ya kombe la Chalenji linaloendelea nchini Kenya baada ya kuitupa nje ya mashindano timu ya taifa ya Zambia kwa kuilaza kwa magoli 4-3. Timu ya soka ya Zanzibar imewatupa Zambia nje ya mashindano ya kombe la Chalenji kwa kuifunga magoli 4-3 katika maguu 12 ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana kwenye dakika 90 za mchezo huo uliochezwa jioni hii.
Hadi dakika 90 zinaisha hakuna timu iliyofanikiwa kuliona lango la mwenzake na kupelekea mechi hiyo iamuliwe kwa penalti.
Alikuwa ni golikipa wa akiba wa Zanzibar Mohamed Khamis aliyepeleka chereko kwenye visiwa vya Zanzibar kwa kuokoa penalti mbili za Zambia.
Akiongea baada ya kipigo hicho, kocha wa Zambia alieleza kusikitishwa na kutolewa kwa kikosi chake ambacho kitashiriki kombe la mataifa ya Afrika mwezi ujao nchini Angola.
Naye kocha wa Zanzibar, Mmoroko Hemed Abdelatif alikipongeza kikosi chake kwa uwezo mkubwa waliouonyesha kwenye mechi hiyo.
"Nawapongeza wachezaji wangu kwa kuweza kuwadhibiti wachezaji wa Zambia na kuonyesha ubora wao, Zambia ni timu bora katika mashindano haya na tunajivunia tumecheza vizuri sana katika mechi dhidi yao", alisema kocha wa Zanzibar.
Katika mechi nyingine ya robo fainali, wenyeji Kenya walitupwa nje ya mashindano na mabingwa watetezi Uganda kwa kutandikwa 1-0.
Zanzibar sasa itapambana na Uganda siku ya alhamisi kwenye mechi ya nusu fainali kuwania nafasi ya kucheza fainali ya kombe hilo kubwa kwa nchi za Afrika Mashariki.
Source: www.Nifahamishe.com