WAKATI timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes' jana ilianza kwa kishindo michuano ya Kombe la Chalenji kwa kuinyuka Burundi mabao 4-0, wenzao Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars' walichapwa mabao 2-0 na Uganda ‘The Cranes'.
Ndio kwanza safari ya mashindano hayo imeanza, lakini inaweza kutoa picha angalau ya wapi wawakilishi hao wa Tanzania mashindano hayo watafanya mwaka huu.
Kombe la Chalenji mara ya mwisho kuchukuliwa na timu za Tanzania ilikuwa mwaka 1995, lakini tangu hapo limekuwa likija nchini pale mashindano hayo yanapofanyika hapa na timu za nje zimekuwa zikiondoka nalo zinavyotaka.
Katika mchezo wa jana wa Stars na Uganda uliofanyika Uwanja wa Mumias mjini hapa, ambao ulitanguliwa na ule wa Zanzibar na Burundi kwenye uwanja huo huo, ulitawaliwa zaidi na Uganda hasa kipindi cha kwanza kabla ya Stars kuzinduka dakika za mwisho za kipindi cha pili.
Uganda ilipata bao la kwanza dakika ya pili, mfungaji akiwa Kasule Ousen akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Daniel Wagaluka aliyefanyiwa madhambi na beki Kelvin Yondani.
Wachezaji wa Uganda Steven Bengo anayechezea Yanga na Wagaluka anayechezea Azam zote za Dar es Salaam walikuwa hatari kwa beki za Kilimanjaro Stars zilizoonekana kupata tabu namna ya kuwakaba.
Kwa nyakati tofauti waliingia kwenye eneo la hatari, lakini walipiga mashuti ambayo ama yalikuwa dhaifu na kudakwa na kipa Muharami Mohammed anayechezea Ferroviario ya Msumbiji au yalitoka nje ya lango.
Kipa huyo, jana ulikuwa mchezo wake wa kwanza kuchezea timu ya Taifa, ambapo alionesha uwezo mkubwa, ingawa kuna wakati alikuwa akilaumiana na mabeki wake hasa Shadrack Nsajigwa, ambaye pia kwa nyakati tofauti alikuwa akizozana na beki mwenzake wa Stars Salum Sued ‘Kusi'.
Stars inayonolewa na Mbrazili Marcio Maximo, kipindi cha kwanza ilifanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa Uganda mara mbili, dakika ya 11 wakati shuti la Kigi Makasi lilipotoka nje na dakika ya 37 shuti hafifu la John Bocco lilipodakwa na kipa Hamza Muwonge.
Muda mwingi katika kipindi hicho walikuwa wakicheza kati au kufanya kazi ya ziada kuhakikisha hawafungwi na kuonekana kana kwamba wanacheza nusu uwanja.
Watanzania waliohudhuria mchezo huo waliingiwa na simanzi dakika ya 38 pale mwamuzi Michele Kasingua wa Rwanda alipomuonesha kadi nyekundu kiungo Juma Nyoso kutokana na kumchezea madhambi Wagaluka.
Awali alioneshwa kadi ya njano kwa kosa pia la mchezo mbaya.
Stars ilicharuka zaidi dakika za mwisho kipindi cha pili hasa baada ya kutolewa Shaaban Nditi, John Bocco na Kigi Makasi na kuingia Henry Joseph, Mrisho Ngasa na Jerry Tegete, lakini umaliziaji haukuwa mzuri.
Bao la ushindi la Uganda lilifungwa dakika ya 88 na Serumaga Mike aliyepiga mpira wa adhabu na kutinga moja kwa moja wavuni.
Baada ya mchezo huo, Maximo alisema hawezi kuwalaumu vijana wake na kwamba wameonesha kiwango kizuri na bado wana nafasi kubwa ya kufuzu robo fainali kwani wamempa matumaini makubwa.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Cranes, Robert Williamson, alisema mechi ilikuwa ngumu kwao, lakini wanashukuru wameshinda na kwamba haogopi timu yoyote bali wanaziheshimu.
Stars: Muharami Mohammed ‘Shilton', Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Salum Sued, Juma Nyoso, Danny Mrwanda, Shaaban Nditi, John Bocco, Kigi Makasi na Nurdin Bakari.
Cranes: Hamza Muwonge, Simeon Masa, Geofrey Walusimbi, Joseph Owino, Andrew Mwesigwa, Kasule Ousen, Daniel Wagaluka, Tonny Maweje, Geofrey Massa, Peter Senyonjo na Steven Bengo.
Katika mchezo wa Zanzibar, timu hiyo ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0. Zanzibar ilipata bao la kuongoza dakika ya 16 mfungaji akiwa Aggrey Morris kufuatia kona ya Nadir Haroub ‘Cannavaro', kabla ya dakika mbili baadaye Burundi kujifunga wenyewe pale beki Hakizimana Hassan alipotumbukiza mpira wavuni kwake.
Beki huyo alikuwa katika harakati za kuokoa, lakini akajikuta mpira unamzidi nguvu kipa wake Vladmir Nyonkuru anayechezea Azam FC ya Dar es Salaam inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Zanzibar Heroes inayonolewa na makocha wazalendo Ally Kiddy na Hemedi Moroko, ilipata bao la tatu dakika ya 25 mfungaji akiwa Selemani Kassim kufuatia krosi ya Ahmed Malik.
Burundi walijaribu kubadilika kipindi cha pili kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza, lakini idadi kubwa ya mabao ya kipindi cha kwanza yalionekana kuwanyong'onyesha.
Baada ya kosakosa za hapa na pale, Zanzibar ilipachika bao la nne dakika ya 67 baada ya Mbazumitima Henry kujifunga alipokuwa akijaribu kuokoa shuti la Selemani Kassim.
Vumbi linatarajiwa kutimka kesho wakati Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes zitakapoumana katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa wa vuta nikuvute.
Mara nyingi timu hizo zinapokutana matokeo huwa hayatabiriki, hivyo ni wazi kesho itakuwa vita ya aina yake uwanjani kutokana na baadhi ya wachezaji kujuana kwa