SURA 36. SURAT YA-SIN

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ya-Sin (Y.S.).

2. Kwa Haki ya Qur'ani yenye hikima!

3. Hakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,

4. Juu ya Njia Iliyo Nyooka.

5. Uteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

6. Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa , basi wao wamekuwa wenye

kughafilika.

7. Bila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo

hawaamini.

8. Tumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao

viko juu tu.

9. Tumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao;

kwa hivyo hawaoni.

10. Ni sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.

11. Hakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi

wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema.

12. Hakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo

yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha.

13. Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa.

14. Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine

wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.

15. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema

hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.

16. Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu.

17. Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.

18. Wakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa

yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.

19. Wakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama

nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.

20. Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu

wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.

21. Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka.

22. NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa?

23. Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema,

akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.

24. Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri.

25. Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!

26. Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua

27. Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio

hishimiwa.

28. Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si

wenye kuteremsha.

29. Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa!

30. Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.

31. Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei

tena kwao.

32. Na hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu.

33. Na Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani

yake nafaka, wakawa wanazila!

34. Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua

chemchem ndani yake,

35. Ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je,

hawashukuru?

36. Subhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea

katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua.

37. Na usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani.

38. Na jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu,

Mwenye kujua.

39. Na mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.

40. Haliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea

katika njia zao.

41. Na ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio

sheheni.

42. Na tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda.

43. Na tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi,

44. Isipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.

45. Na wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili

mpate kurehemewa...

46. Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni

wenye kuipuuza.

47. Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru

huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli

walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri.

48. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?

49. Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana.

50. Basi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei.

51. Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao

Mlezi.

52. Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo

yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.

53. Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu.

54. Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo

kuwa mkiyatenda.

55. Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.

56. Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari.

57. Watapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka.

58. "Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.

59. Na enyi wakosefu! Jitengeni leo!

60. Je! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye

ni adui dhaahiri kwenu.

61. Na ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.

62. Na bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je,

hamkuwa mkifikiri?

63. Hii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa.

64. Ingieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru.

65. Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu

yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.

66. Na tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia.

Lakini wange ionaje?

67. Na tungeli taka tunge wageuza SURA hapo hapo

walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi.

68. Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii?

69. Wala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo.

Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha.

70. Ili imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri.

71. Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama

wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.

72. Na Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao

wanawala.

73. Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?

74. Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate

kusaidiwa!

75. Hawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao

hudhurishwa.

76. Basi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na

wanayo yatangaza.

77. Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la

manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri!

78. Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo

atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?

79. Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi

wa kila kuumba.

80. Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo

mnawasha.

81. Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye

ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.

82. Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.

83. Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake

Yeye mtarejeshwa.