Nakumbuka niliwahi kuwa na kaduka kule barabara za namba Tanga mjini🤣🤦♀️ Mwanzoni kalinipa heshima kidogo angalau pesa ya mboga nyumbani haikukosekana, angalau kipindi mambo ya mishahara yanasumbua basi kifaida kikawa kinakidhi mahitaji.
Likaja wazo la ushauri mbalimbali la kuikopea biashara ili ikue, Benki zetu hazina hiyana nyie kukupa Ile mikopo yao, huku na huku Corona ikaja, nani akanunue nguo avae aache kusevu pesa kwa ajili ya chakula, biashara ikabuma, pesa ya pango ikagoma, malipo ya TRA hayapo, ushuru hulipi, posho ya msaidizi hakuna, bills zote hazilipiki na bado una rejesho Benki.
Huu mwaka wala haukuondoka hivyo, likatokea sekeseke nikaikosa ajira nikajionea wala isiwe shida kuwa tu na Jina mjini kwamba namiliki duka lisilonipa chochote, nikaamua kubeba virago vyangu na kurudisha mlango wa watu. Sikuishia hapo tu, baada ya mambo kuwa magumu zaidi ilibidi nijiambie kwa dhati kabisa kwamba kuanza moja si ujinga, nikashuka chini nikatafakari, nikakubali matokeo ya mabadiliko ya Maisha na nikakubali fedheha zote, kejeli, masimango na vicheko ili tu nijitafute nijipate.
Hadi sasa bado najitafuta, na ninakutia moyo usijichoke, endelea kujitafuta na ikibidi kuanza moja Anza tu maana kupotea njia ndio kujua njia