NIMEINGIA JF, nimekutana na tuhuma nyingi. Zote hizi si za kweli. Kwanza, napenda kusema wazi kuwa madai yote haya hayana ukweli na ni uzushi mtupu.
1.Mimi sina mpango wowote wa kugombea ubunge katika jimbo la Mafia kwa sasa. Siwezi kuacha gazeti langu na kukimbilia ubunge, wakati kigazeti chenyewe bado kichanga. Hivyo basi, madai kuwa kuna vigogo wa CCM nimezungumza nao kuniunga mkono katika hilo, hayana ukweli wowote.
2.Mimi sijawahi kuwa kada wa CUF. Nitakuwaje kada wakati sijawahi kuwa mwanachama? Kama kuna mtu ana ushahidi kwamba niliwahi kuwa mwanachama wa CUF, alete hapa ushahidi wake. Aseme kadi yangu namba ngapi? Imesajiliwa tawi gani? Alete ushahidi si hisia.
3.Lakini ni kweli kwamba mimi na Profesa Lipumba ni marafiki, lakini narudia tena sijawahi kuwa mwanachama wa CUF.
4.Kuonyesha kwamba huyu aliyeandika hapa hanijui, bali anaendesha hisia, mimi sijawahi kushirikiana na CUF kuendesha gazeti lao. Gazeti la CUF linaitwa FAHAMU, tafuta mahali popote kama utaona jina langu katika gazeti hilo.
5. Mimi nilikuwa naendesha gazeti la HALIHALISI ambalo lilikuwa la Kambi ya Upinzani Bungeni, wakati huo kiongozi wa kambi alikuwa Willifred Muganyizi Lwakatare. Kambi ilikuwa inaundwa na vyama vya CUF, Chadema, TLP na UDP. Kabla ya Bunge kuvunjwa mwaka 2005, Kambi ya upinzani ililiuza gazeti hilo kwangu.
6.Lakini baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 kumalizika ambapo wabunge wengi wa upinzani wa wakati huo walishindwa kurejea Bungeni, akiwamo Lwakatare na Isaack Cheyo ambaye alikuwa Naibu Kiongozi, Hamad Rashid Mohammed alitumia mabavu na urafiki wake na Mohammed Seif Khatibu ambaye alikuwa Waziri wa Habari wakati ule kunidhulumu gazeti langu.
Mimi nilikwenda mahakamani kufungua kesi dhidi ya Hamad na serikali kwa kuingilia gazeti langu.
7.Mambo haya yanafahamika MAELEZO, Wizara ya Habari na Ofisi ya Waziri Mkuu. Ni katika zogo hilo, Mkurugenzi wa Maelezo wakati huo, Kasim Mpenda akanishauri nisajili gazeti langu jingine. Nikasajili hili la MwanaHALISI. Hata mtaji wa kuanzisha MwanaHALISI ulitokana na matangazo ya waastafu wa Afrika Mashariki niliyoyachapisha katika gazeti la HALIHALISI.
8.Lakini bado naamini mpaka sasa, gazeti la Halihalisi ni langu. Ndiyo maana hata jina la kampuni yangu inaitwa Halihalisi. Hata ukija hapa ofisini kwangu bango letu linaonyesha gazeti hilo ni letu. Je, kama gazeti lilikuwa la CUF, ningewezaje kuweka jina la gazeti hilo katika bango langu?
9.Kuhusu kulalamikiwa na baadhi ya waandishi wa habari wenzangu, inawezekana wanaolalamika ni wale ambao tumekuwa tukiwataja katika stori zetu. Mfano kilichotokea katika mkutano wa DK. Mwakyembe na waandishi wa habari
.
10.Gazeti la MwanaHALISI stori zake haziandikwi na waandishi wa nje, nami kuweka jina langu kama huyu jamaa anavyopotosha ulimwengu. Huo ni upuuzi. Je, mimi sina uwezo wa kuandika? Sina vyanzo vya habari?
Mbona hata lugha inayoandikwa MwanaHALISI na magazeti mengine inatofautiana? Kama ingekuwa stori hizo zinaandikwa na waandishi kutoka magazeti mengine, mbona lugha haifanani na magazeti hayo yanaondikwa na waandishi wanaolalamika? Je, huko nilikopita kabla ya hapa, nani alikuwa anaadika stori zangu?
11.Kuhusu siasa za fitina mimi si wa aina hiyo. Tabia yangu ni kusema ukweli. Kama kitu sikikubali, nakisema papo hapo. Hiki sikikubali. Basi!
12.Kuhusu dai kwamba MwanaHALISI inaendeshwa na Bodi ya Chadema, huu nao ni uwongo mwingine. Nenda BRELA, ona mwanaHALISI ni la nani. Mimi namiliki asilimia 90 ya hisa. Asilimia 10 zingine zinamilikiwa na Athony Bahati. Huyu na mimi tumeoa nyumba moja, kwa makubaliano kwamba akitokea mtu makini, ambaye hana harufu ya ufisadi, nitachukua asilimia 10 ya hisa zake na kuziuza kwa huyo mbia. Hili lilifanyika baada ya waandishi wengi kuogopa kuacha kazi na kuja kuanzisha MwanaHALISI. Wengi walidhani kwamba gazeti halitafika mbali na hivyo wakaogopa kupoteza kazi.
13.Bodi ya MwanaHALISI haina hata mtu mmoja wa Chadema. Kuna watu huru watatu, pamoja na mwanasheria Marando Mabere.
14. Kuhusu gazeti kupewa matangazo na serikali, nadhani wa kuulizwa ni serikali. Lakini muhimu hapa ni kuwa serikali labda imeanza kuona umuhimu wa kutangaza katika MwanaHALISI, hasa ukitilia maanani kuwa gazeti letu linaongoza kwa kuchapa nakala nyingi.
MwanaHALISI linachapa nakala 60,000 (elfu sitini) kwa wiki. Nenda Kiwandani kapate taarifa yetu.
Chanzo cha haya nakijua. Soma taarifa hii, ambayo imetumwa na huyu aliyeibandika hapa JF.
Wengi wamekuwa wakilalamika na tabia ya Kubenea ya kuendesha fitina dhidi yao ili yeye ndiye aonekane wa muhimu na wengine wote ni wabaya. Baadhi ya majeruhi wa majungu na fitina za Kubenea ni pamoja na waandishi kadhaa wa habari na wanasiasa vijana ambao yeye kwa kutumia fitina ameweza kujenga uaminifu mkubwa kwake kwa staili hiyo ya kuwafitini wenzake na kuwafanya wanasiasa muhimu na wapambanaji kuchukiwa na wengine kupoteza nafasi zao.
Sasa hao wanaoitwa wanasiasa vijana, marafiki zangu ni akina nani? Mimi sijawahi kuwa na urafiki mkubwa na mwanasiasa kijana William Ngeleja. Sijawahi kuwa na urafiki mkubwa na Emmanuel Nchimbi. Mimi nimekuwa na urafiki na Zitto na Nape. Sasa nani niliyemchafua na kupoteza nafasi yake? Nape? Au Zitto? Uchaguzi wa Chadema usiwafikishe huko