Kubenea: Tulishambuliwa kwa chuki
na Asha Bani
MKURUGENZI na Mhariri Mtendaji wa magazeti ya MwanaHalisi na Mseto, Saed Kubenea, ameiambia mahakama kwamba kushambuliwa kwake kulitokana na chuki za viongozi wa serikali wanaoandikwa na magazeti yake juu ya vitendo vya ufisadi.
Alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya kumwagiwa tindikali, akiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi Charles Kanyella, mbele ya Hakimu Addy Lyamuya.
Akielezea zaidi, Kubenea alidai kuwa wakati akiwaanika viongozi wanaofanya ufisadi serikalini, mawakili wanaotumiwa na viongozi hao ambao aliwaita mafisadi, wamekuwa wakimwandikia barua za vitisho ili aache kufanya hivyo, vinginevyo watampeleka mahakamani.
Mbali na vitisho vya mawakili wa viongozi hao, alidai kuwa Msajili wa magazeti nchini amekuwa akitumiwa kumkaripia kwa kumwandikia barua za kumuonya mara kwa mara na kumkataza kuandika habarai hizo huku akimtaka kubadili msimamo wa gazeti hilo.
Kuvamiwa kwangu kunatokana na mambo ya kisiasa, ambayo kwa miaka miwili tangu kuanzishwa kwa gazeti la MwanaHalisi, nimekuwa na msimamo wa kuandika habari za uchambuzi wa masuala ya siasa, jamii, biashara ikiambatana na kuwaandika viongozi mafisadi, alidai Kubenea.
Aliendelea kueleza kuwa, siku ya tukio akiwa katika ofisi za MwanaHalisi saa mbili usiku, alisikia mlango wa ofisi yake ukigongwa na kusukumwa kwa nguvu. Kubenea alidai baada ya kusikia hivyo aliamua kwenda mlangoni na kumhoji aliyegonga huku akichungulia kupitia katika vioo lakini hakufanikiwa kumtambua mgongaji kwa vile alikuwa gizani.
Alieleza kuwa siku hiyo alikuwa na mshauri wa magazeti hayo, Ndimara Tegambwage, aliyemtaka kufungua ili amjue anayegonga mlango huo. Alidai baada ya kufungua mlango, aliamriwa kukaa chini na watu watatu walioingia ndani ya ofisi hizo, lakini walikaidi amri hiyo na ndipo walipoanza kumshambulia.
Baada ya kuniambia nikae chini niligoma ndipo wakaanza kunishambulia kwa panga na mtu mwingine ambaye sikumuona alikuwa ameshika kikopo na kunimwagia maji maji usoni ambayo yalikuwa yanauma sana, alidai Kubenea.
Alidai baada ya kushambuliwa zaidi, aliingia katika chumba kingine cha ofisi ambapo alikwenda kutafuta silaha ya kupambana nao lakini alishindwa kupata, akaamua kuvunja kioo cha ofisi akidhani atafanikiwa kupata kioo cha kupambana nao lakini kioo kile kilidondoka kwa nje.
Alieleza baada ya kuona hakuweza kufanikiwa, aliamua kutoka ili kuweza kupambana nao hivyo hivyo, lakini aliwakuta wameshaondoka na kumuona Ndimara akiwa anavuja damu nje ya ofisi na watu wakiwa wamemzunguka.
Kubenea alidai baada ya hapo walifanikiwa kupata usafiri na kuelekea hospitali, huku Polisi kutoka Kituo cha Oysterbay walikuwa wamefika katika eneo la tukio tayari kwa kuchukua maelezo.
Mbali ya maelezo hayo, Kubenea alidai kumtambua aliyekuwa anamjeruhi ambapo alimtaja kuwa ni mtuhumiwa namba moja Alex Anyimike, ambaye mbali na kumtambua mahakamani, aliweza pia kumtambua katika gwaride la utambulisho lililofanyika katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Katika utambuzi wa watuhumiwa, Kubenea alikana kuwatambua watuhumiwa wengine kwa kuwa hakuwaona wakati wa tukio na kudai waliokuwepo katika tukio ni watuhumiwa wengine, ambao hawajakamatwa na akiwaona atawatambua pia.
Wakati akiendelea kutoa ushahidi wake alidai hadi sasa kutumiwa meseji za vitisho na kwamba kabla ya kutokea kwa tukio alitumiwa meseji nzito kupitia namba 0787 775 692, aliyodai ilikuwa ikitumika mara kwa mara kumtumia ujumbe wa vitisho.
Mwendesha Mashitaka alimuomba hakimu kupokea meseji hizo kama kielelezo kitakachotumika mahakamani kama ushahidi lakini kutokana na ujumbe huo haukuchapishwa kwenye karatasi (IT) haukupokelewa.
Hakimu Lyamuya alimwambia Mwendesha Mashitaka Kenyella kulifanyia kazi hilo kwa kuchapisha ujumbe huo na kuutoa kama kielelezo Juni 16. mwaka huu.
Hata hivyo ushahidi wa Kubenea ulikatishwa baada ya Kenyella kuiomba mahakama kuendelea kutolewa Mei 19 na leo Ndimara atapanda kuendelea na ushahidi wake.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Alex Mwandemele (Chusu), mfanyabiashara na mkazi wa Kigogo; Hashim Mdoe (Madilu), dereva wa teksi na mkazi wa Tegeta; Augustino Joseph (Cheusi), mfanyabiashara na mkazi wa Mwananyamala.
Wengine ni Hamis Almasi Ramadhani; fundi wa kuchomea na mkazi wa Mwananyamala; Alfred Bernard Moshi (Chambya), fundi umeme, mkazi wa Kinondoni; na Ferdinand Msepa.
Source: Tanzania Daima