Polisi yafafanua tamko lao na Shimbo
Na Romana Mallya
14th October 2010
B-pepe
Chapa
Maoni
Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Abdulrahman Shimbo.
Jeshi la polisi limefafanua kuhusu kauli iliyotolewa hivi karibuni na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu namna vilivyojipanga kufanikisha uchaguzi mkuu, na kusema kuwa kauli hiyo haikulenga kutishia wananchi bali kuimarisha amani kwenye kampeni, wakati wa uchaguzi na baada.
Mkuu wa jeshi hilo IGP, Said Mwema, alitoa ufafanuzi huo jana baada ya baadhi ya viongozi wa siasa na wa dini kuilalamikia kauli hiyo kuwa imelenga kuwatisha Watanzania.
Viongozi hao wa dini na wanasiasa walitoa malalamiko hayo katika mkutano uliofanyika jana jijini Dar es Salaam uliolenga kujadili kuhusu masuala ya amani, usalama na utulivu wakati wa uchaguzi na baada.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi hao, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na jeshi la polisi ambapo kwa pamoja waliweka maazimio 11 yatakayowawezesha kila mmoja na nafasi yake kuielimisha jamii.
Katika mkutano huo, baadhi ya viongozi hao walitoa malalamiko kuwa, kauli iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Abdulrahman Shimbo, ililenga kutishia umma wa Watanzania.
Mwema akijibu malalamiko hayo alisema kuwa, tamko hilo halikuwa na nia wala mpango wa kuitishia jamii, bali lilimaanisha kuwa, vyombo hivyo vya ulinzi kila kimoja kwa nafasi yake vihakikishe kuwa vinalinda amani.
JWTZ kwa nafasi yake itahakikisha amani inaendelea kuimarishwa vile vile, jeshi langu siku hiyo tutaingia mitaani kutekeleza hilo, lakini kauli hiyo haikumaanisha JWTZ watafanya kazi zetu, hofu imetokana baada ya yule aliyetoa tamko kuwa JWTZ, alisema.
Alisema vyombo vya dola kote duniani huwa na mbinu na mikakati ya ulinzi.
Hapa kwetu vyombo vya usalama huwa tunakutana kila mwezi kujadili jinsi ya kuimarisha ulinzi hasa kutokana na kukua kwa teknologia ya mawasiliano, kuna masuala ya ugaidi, pia kipindi hiki kumejitokeza ujumbe mfupi unaotumwa kwenye simu unaotishia umwagaji damu na kuchochea vurugu, hivyo lazima vyombo vya usalama tufanye kazi kukabiliana navyo, alisema.
Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa wadau hao viongozi wa dini waendelee kuelimisha amani na utulivu vyombo vya habari kuhakikisha mambo ya amani na utulivu yanapewa kipaumbele.
CHANZO: NIPASHE