Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo
Elias Msuya
MAMBO yalikuwa yametulia kabisa, lakini sasa yametibuka baada ya viongozi wa majeshi kuanza kutoa kauli za vitisho kuelekea uchaguzi mkuu.
Hivi karibuni, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo akiwa na baadhi ya viongozi wa jeshi la Polisi walitoa onyo kali kwa wanasiasa kujiepusha na vurugu wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu. Shimbo alidai kuwepo kwa dalili za kuvurugika kwa amani kutokana na taarifa za baadhi ya vyama vya siasa kujiandaa kukataa matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi.
Alisisitiza kuwa hakutakuwa na umwagikaji wa damu na kuwa jeshi hilo litahakikisha kuwa amani inatawala wakati wote wa uchaguzi.
Pamoja na ukweli kuwa suala la amani ni la muhimu, siyo tu wakati wa uchaguzi, lakini hadi sasa sijaelewa lengo la onyo hilo la viongozi wa majeshi wakati huu.
Kwani kama jeshi limejipanga kulinda amani wakati wa uchaguzi, kuna haja gani ya kuwatangazia wananchi?
Badala yake naona Shimbo anatafuta maneno zaidi kwani sasa amejiingiza kwenye mijadala na wana siasa jambo ambalo hata yeye mwenyewe alikiri kuwa jeshi halihusiki huko.
Jambo jingine ninaloliona hapa ni upotoshwaji wa neno hili Amani. Baadhi ya watu (akiwamo Shimbo) wanadhani amani huja kwa kuwatisha watu kwa kuwaamuru kutii kila linalosemwa hata kama halina msingi.
Ndiyo maana Shimbo alisema kuwa ana taarifa ya kuwepo kwa baadhi ya vyama vya siasa vimejipanga kukataa matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi.
Hadi hapo mimi sioni dalili yoyote ya kuvunjika kwa amani, kwasababu mtu huwezi kukubali matokeo yasiyo sahihi eti ili tu kulinda amani.
Kabla sijaenda mbali, kwanza tuona maana ya amani. Nakumbuka mwezi Februari wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini, Jaji Mkuu Augustino Ramadhan alifafanua vizuri maana ya amani.
Alisema, (namnukuu) Amani ya kweli ni pale haki inapotawala, vyombo vya dola havihitajiki, utunishaji wa misuli siyo lazima, bali wananchi wenyewe wanakuwa watulivu kwa sababu kila mmoja au wengi wao wanakuwa wamekinai.
Kwa maana hiyo, Jaji mkuu, alimaanisha kwamba amani haiji kwa vitisho au kuwa na majeshi mengi, bali watu waridhike na kile wanachokitaka.
Sasa kitendo cha viongozi wa majeshi kutishia kuwa watahakikisha amani inadumishwa wakati huu wa uchaguzi, siyo dawa, tena wasipoangalia ndiyo itavunjika zaidi.
Kitu cha msingi wanachopaswa ni kuhakikisha kuwa kila mtu anaridhishwa na mwenendo wa uchaguzi. Tangu wakati huu wa kampeni, wakati wa kupiga kura, kuhesabu na kutangaza matokeo, watu waridhike.
Kama kutakuwa na upendeleo, au uvunjwaji wa sheria yoyote na vyombo vinavyosimamia uchaguzi tusitegemee kuwa na amani.
Hata kama majeshi yatafanikiwa kuwatisha wananchi, hiyo haitakuwa na amani bali ni ukandamizwaji wa haki za biandamu.
Ieleweke pia kwamba, vyama vya siasa au wagombea kupinga matokeo, siyo kosa na ndiyo maana zipo taratibu za kuwasilisha malalamiko yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi na mahakamani.
Ingawaje, sheria inakataza vyama au mgombea kupinga matokeo ya rais mara yanapotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hata hivyo haijazuia watu kutoa maoni yao kama iliyo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nawakumbusha viongozi wa majeshi kuwa makini na matamshi yao katika kipindi hiki kwani badala ya kutibu yanaweza kuamsha ugomvi usiokuwa na sababu za msingi.
Tunakumbuka uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, aliyekuwa mkuu wa jeshi la Polisi, Omar Mahita akupokuwa akitoa kauli zenye utata dhidi ya vyama vya upinzani.
Aliwahi kusema kuwa kama wao ni ngangari, sisi ni ngunguri akikiponda chama cha upinzani kilichokuwa kiktumia neno hilo.
Siku moja kabla ya uchaguzi akadai kuwa kuna visu na silaha nyingine zimekamatwa zikiwa na alama ya chama fulani cha upinzani.
Baada ya uchaguzi ule, Chama cha Wananchi, CUF kililalamika kuhujumiwa kwa kauli za Mahita.
Inatia shaka kuona viongozi wa majeshi ambao ni wateule wa Rais ambaye pia ni mgombea wa CCM wanapotoa kauli za vitisho kwa wananchi. Kauli hizi zinaweza kutafsiriwa kuwa ni maagizo ya mgombea huyo.
Wakati mwingine viongozi wa jeshi wanajipendekeza tu ili baada ya uchaguzi kupita au watakapostaafu wakumbukwe kwenye uteuzi wa nafasi mbalimbali serikalini, kama vile ukuu wa mikoa, wilaya au vitengo mbalimbali serikalini.
Viongozi wa majeshi wanapaswa kuwaachia kazi za propaganda wanasiasa. Hata kama wamegundua hali mbaya, wanapaswa kuwashauri viongozi wa serikali, badala ya kuanza kulumbana na wanasiasa.
Chanzo:
Kauli za viongozi wa majeshi zinatia mashaka