Dk. Slaa ashangaa majeshi
Awapa siku saba kuwakamata wachochezi
na Mwandishi wetu
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kitendo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuingilia siasa kwa vitisho ni kielelezo kingine kuwa serikali inafanya jitihada za kuhujumu uchaguzi na kukinusuru Chama Cha Mapinduzi (CCM), kabla ya upigaji kura Oktoba 31, mwaka huu.
Akihutubia umati wa wananchi waliofurika kumsikiliza mjini hapa jana, Dk. Slaa alitoa siku saba kwa Mnadhimu Mkuu wa jeshi hilo, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, kuwakamata watu wote waliotishia kumwaga damu ndani ya siku hizo.
Hata hivyo alimtaka Luteni Jenerali Shimbo kuwaomba radhi Watanzania kwa vitisho alivyotoa katika kipindi hicho cha siku saba, huku akijinasibu kuwa kuna uwezekano wa yeye kupita bila pingamizi kama serikali ya CCM itaendelea na vitisho kama hivyo.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo katika viwanja vya Mdete, wilayani Njombe, akiwa katika mwendelezo wa kampeni zake katika Mkoa wa Iringa.
Dk. Slaa alisema Luteni Jenerali Shimbo hakupaswa kutoa kauli kama hiyo, kwa kuwa ni vitisho kwa Watanzania, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, na kwamba kauli kama hiyo ilipaswa itolewe na IGP Mwema, kwa maana ya kushughulikia watu wanaotaka kuvunja amani ya nchi.
Tunaitaka JWTZ na Polisi kuwakamata wale wote waliotoa kauli ya kutaka kumwaga damu
kama haitafanya hivyo, tujue ni propaganda chafu za Kikwete na vyombo vyake vya usalama za kuiba kura na kutaka kuvunja amani, alisema.
Alisema yeye kama Dk. Slaa asingependa kuwa rais wa Tanzania kwa Watanzania kumwaga damu, lakini anatambua kauli kama hizo ni mbinu za CCM za kutaka kuchakachua matokeo ya Uchaguzi Mkuu.
Dk. Slaa alisema atahakikisha Watanzania hawadanganyiki na kauli za viongozi mbalimbali, wakiwamo wale wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao wamekuwa wakitumika kisiasa kutaka kuisaidia CCM, ambayo inaonekana kushindwa, kwa kutoa kauli za vitisho na nyaraka mbalimbali za kutaka kusaidiwa.
Nataka kumwambia Shimbo, kama hajui siasa atuachie wenyewe, yeye arudi kambini kuendelea na kazi yake, badala ya kutumika kutoa vitisho kwa Watanzania ambao wamechoka kubebwa katika malori kwenda katika mikutano ya CCM
.lakini hii ni dalili kuwa mgombea urais wa CCM na chama chake wameona hali ni mbaya kwao, alisema Dk. Slaa.
Hata hivyo, alisema hofu za mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, kutumia vyombo vya dola kutisha, ni sawa na kuonyesha kushindwa kabla ya dakika 90, na kumtaka afanye kampeni za kunadi sera badala ya kutumia dola kumfanyia kampeni.
Alimtaka aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Njombe Kusini, Anne Makinda, kuacha kuendelea kuwatisha wananchi wa jimbo hilo na kudanganya umma kuwa yeye ni mbunge wa kupita bila kupingwa.
Alisema hiki ni kipindi chake cha mwisho na kama mwaka 2015, atafanya hivyo atakuwa tayari kuacha urais na kwenda kugombea kwenye jimbo hilo.
Kwa upande wake, Meneja Kampeni kitaifa wa CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu, alisema ameshangazwa na kauli hiyo ya Mnadhimu Mkuu Shimbo kuwataka wananchi wakubaliane na matokeo yatakayopatikana katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Baregu alisema tamko hilo liliashiria kuwepo kwa hali ya hatari, kitu ambacho kinaonyesha kuwatia hofu wananchi, ambapo hadi sasa haijaeleweka kwanini wafikie hatua hiyo.
Tumeshangazwa na tamko hilo ambalo linaonyesha limezingirwa na hali ya hatari na hadi sasa hatujaelewa kwa nini wafikie hatua hiyo, alisema Prof. Baregu. Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, haikupaswa kutolewa kwa tamko kama hilo, kwa kuwa linaonyesha kutaka kujenga mazingira ya kuufanya uchaguzi kutokuwa wa haki. Isije ikawa wanaandaa mazingira ya kufuta au kuahirisha uchaguzi kwa kuzidiwa na CHADEMA, alisema Profesa Baregu.