SHIMBO HIZI NDOSHUGHULI ZAKO ZA KUSIMAMIA
Miaka 44 ya JWTZ
JWTZ limepata mafanikio lukuki
o Kwa kulinda mipaka, watu na mali
o Kusaidia Ukombozi wa Afrika
o Kushiriki katika Ulinzi wa amani
o Uokoaji wakati wa maafa
Kila ifikapo Septemba Mosi ya mwaka, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huadhimisha sikukuu ya kuanzishwa kwake miaka 44 iliyopita yaani Septemba Mosi 1964.
Kuanzishwa kwa jeshi hilo la kizalendo, ambalo jukumu lake la msingi ni ulinzi wa mipaka ya nchi, watu na mali zao pamoja na rasilimali za taifa ndiko kumeifikisha Tanzania hapa ilipo likiwa ni taifa la kupigiwa mfano kwa amani, usalama na utulivu.
JWTZ lilianzishwa mwaka 1964 baada ya maasi ya jeshi la Tanganyika yaani Tanganyika Rifles (TR) ambalo lilirithiwa kutoka kwa wakoloni na kuasi miaka minne tu tangu Tanganyika (Tanzania Bara) ipate uhuru wake.
Maasi hayo ambayo yalitokea wakati taifa likiwa bado changa, yalileta mashaka, hofu na wasiwasi mkubwa hasa katika jiji la Dar es Salaam.
Sababu za maasi ya vikosi vya TR zilikuwa nyingi ikiwemo kuboreshewa mishahara na marupurupu pia makamanda wa Kiafrika kupewa hadhi sawa na makamanda wa Kizungu.
Itakumbukwa kuwa baada ya Tanganyika kupata uhuru wake Disemba 9,1961, vikosi vya King's African Rifles (KAR) vilibadilishwa jina na kuwa vikosi vya ulinzi wa Tanganyika yaani Tanganyika Rifles (TR), lakini sheria, kanuni na taratibu za uongozi zilibaki zile zile za wakati wa ukoloni.
Aidha, makamanda wake wote akiwemo Mkuu wa Majeshi alibakia yule yule wa KAR yaani Brigedia Jenerali Sholto Douglass huku makamanda wa kizungu wakiwa wameshikilia nyadhifa mbalimbali za juu jeshini.
Kutokana na hali hiyo, wanajeshi wazalendo hawakuna na namna ya kuwasilisha matakwa yao ya kutaka mabadiliko kwa uongozi wa kitaifa na kuamua kuasi Aprili 19,1964.
Maasi hayo yalianzia katika kikosi cha Colito (Lugalo) Dar es Salaam na kuungwa mkono na vikosi vya Kalewa (Mirambo) Tabora na Godar (Nachingwea) hali iliyoleta hofu, mashaka na kuwafanya watu kukimbia ovyo.
Maasi hayo ya kukataa kunyanyaswa na makamnda wa kizungu yaliyodumu kwa siku kadhaa na kuzimwa na kikosi cha makomandoo kutoka Uingereza cha Royal Marine Comandoes hali inayoweza kutafsiriwa kama Waingereza walikuja kuokoa wenzao.
Baadaye makamanada hao walirejeshwa kwao huku kikosi kutoka Nigeria kilipewa jukumu la kufundisha jeshi jipya ambalo lilipewa jina la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kuundwa kwa JWTZ
Itakumbukwa kuwa siku chache baada ya maasi hayo, Tanganyika na Zazibar ziliungana aprili 26,1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni muungano wa pekee barani Afrika.
Kutokana na muungano huo, vijana wapatao 1000 waliandikishwa kutoka bara na visiwani wakiwemo vijana kutoka chama cha Tanganyika African Union (TANU) cha Tanzania bara, vijana kutoka chama cha Afro Shiraz Party (ASP) kutoka Zanzibar na kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Vijana 30 kati ya hao walikuwa wanawake sawa na asilimia 30 ya wanajeshi wapya.
Mafunzo ya awali ya 'kuwanoa" askari wapya yalifanyika chini ya makamanda kutoka Nigeria na kuhitimu rasmi Septemba Mosi 1964 na kula kiapo cha utii na uaminifu mbele ya Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Tangu hapo JWTZ likaanza kuandika historia mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo ukombozi wa bara la Afrika, ushindi wa vita ya Kagera, nidhamu na utiifu, uokoaji wakati wa majanga, ulinzi wa amani na hivi karibuni ukombozi wa kisiwa cha Anjouan.
Ukombozi wa Afrika
Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, jeshi hilo lilianza kazi ya ulinzi wa nchi lilikiwa pia na jukumu la kusaidia ukombozi Kusini mwa Afrika ikiwemo Msumbiji, Afrika Kusini, Angola, Namibia, Zimbabwe na nchi nyingine kwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wapigania uhuru wa nchi hizo.
Tanzania ilianzisha makambi katika sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwafundishia ikiwemo Kongwa Dodoma, Mgagao Kilolo Iringa, Farm 17 Nachingwea, Masonya Tunduru, Shelala Lindi, Kidogozero Pwani, Pongwe Msungura Msata Pwani, Mkuyu Tanga, Matekwe Songea likuyu sekamaganga Namtumbo Ruvuma na nyinginezo
Aidha, Wapiganaji walifunzwa nchini waliongeza vuguvugu la ukombozi katika nchi zao kwa kuanzisha mapigano yaliyozikomboa nchi hizo kutoka katika minyororo ya ukoloni na ubaguzi wa rangi na kufanikisha nchi zote kujikomboa hadi kufikia mwaka 1975.
Jeshi la Kujenga taifa JKT
Mapema mwaka 1963 lilianzishwa Jeshi la Kujenga Taifa hapa nchini kwa lengo la kuwalea vijana kwa kuwafundisha umoja na uzalendo, kuwafundisha mbinu za uzalishaji mali na mafunzo ya ulinzi.
Kuanzia mwaka 1964 JWT ilisaidia pia kutoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wa JKT kazi ambayo inaendelea hadi sasa.
Mgambo
Jukumu jingine la JWTZ ilikuwa ni kuwashirikisha wananchi katika ulinzi wa taifa kwa kufundisha jeshi la mgambo. Jukumu hilo ambalo lilipata muitikio mkubwa lilifanyika katika mikoa yote na watu kwa maelfu walipata mafunzo hayo.
Matunda ya kazi hiyo yalionekana mwaka 1978 pale majeshi ya Iddi Amini wa Uganda yalipovamia na kuchukua eneo la Kaskazini la mto Kagera mwaka 1978 na jeshi la Mgambo kushirikiana na JWTZ katika kutoa "Dozi" kwa majeshi ya adui.
Kwa kuwashirikisha Mgambo, Tanzania ilionesha kwa vitendo kuwa kweli jukumu la ulinzi ni wa nchi ni la wananchi wote.
Vita vya Kagera
Kama ilivyoelezwa awali, mtihani wa kwanza wa JWTZ ulikuwa mwaka 1978 pale vikosi vya Dikteta Idd Amini vilipovamia na kuteka Kaskazini ya mto Kagera na kutangaza kuwa eneo hilo ni lao.
Kutokana na uchokozi huo, Amiri jeshi Mkuu wa kwanza Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza vita dhidi ya jeshi la uvamizi na kuwahakikishia wananchi kuwa, "Tanzania kupitia JWTZ ilikuwa na nia ya kumpiga, sababu ya kumpiga na uwezo wa kumpiga Iddi Amini na vikosi vyake.
Baada ya hapo Tanzania iliingia vitani Novemba mwaka 1978 na kwa kipindi kifupi majeshi ya Amini kwanza yalitolewa katika eneo la Kagera baada ya kipigo na hatimaye kazi ya kumuondoa Amini ilifanyika ndani ya nchi yake.
Mashujaa wa vita hivyo walirejea nchini na kupokelewa rasmi na amiri Jeshi Mkuu wa kwanza Hayati Julius nyerere katika eneo la Bunazi julai 25, 1979 siku ambayo sasa ni sikukuu ya mashujaa.
Kwa kuyashinda majeshi ya Nduli Amini JWTZ iliandika historia nyingine ya kuwa makini katika ulinzi wa nchi kwa kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda nchi, mipaka yake, watu na mali zao.
Kusaidia Msumbiji
Pamoja na majukumu yake ya msingi ya kulinda nchi JWTZ pia ilishiriki katika kusaidia ulinzi wa nchi nyingine za Kiafrika kwa mfano kuanzia mwaka 1976 nchi ya Msumbiji ilipambana na waasi wa Renamo ambao walitishia uhuru wa taifa hilo.
Katika harakati hiyo, wanajeshi wa Tanzania zaidi ya 101 walipoteza maisha yao na kuzikwa katika majimbo mbalimbali ya Tete, Manica, Qulimani. Mabaki ya miili ya wahanga hao zilizikwa upya katika eneo la Naliendele Mtwara Septemba Mosi, 2004.
Ulinzi wa amani
Jeshi la Ulinzi laWananchi wa Tanzania (JWTZ) pia limeshiriki katika ulinzi wa amani duniani mara ya kwanza mwaka 1993-95 nchini Liberia na hatimaye nchi hiyo kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.
Aidha kuanzia mwaka 2007 wanajeshi wa JWTZ wameshiriki kama sehemu ya majeshi ya kulinda amani nchini Lebanon. Kazi ambayo inafanyika kwa kwa ufanisi mkubwa.
Ukombozi wa Anjouan Comoro
Vilevile Tanzania iliweka historia mwaka huu Machi 25, 2008 pake vikosi vya Tanzania vilipoongoza majeshi ya Afrika katika kukikomboa kisiwa cha anjouan. Katika vita hivyo vya kisayansi, majeshi ya AU yalipenya hadi ndani nya kisiwa na kuzingira maeneo yote mhimu.
Tendo hilo la kijasiri liliyaacha mataifa mengine yakiwa midomo wazi kwa mshangao kwani kwa kawaida silaha kubwa ikiwemo mizinga, ndege na hupiga kwanza kabla ya vikosi vya miguu kukamata eneo husika. Hiyo iliwezekana kwa Tanzania kutumia Makomando wake kuzingira eneo bila kutumia silaha kubwa.
Kutokana na ujasiri huo, JWTZ iliandika historia ya kupata ushindi bila kuua wala kuharibu mali za wananchi jambo ambalo ni nadra sana kutokea katika vita.
Aidha ujasiri wa JWTZ na Tanzania ni wa kihistoria tangu wakati wa mababu ambao waliosimama kidete kutetea heshima ya taifa letu na kupigana kiume dhidi ya wakoloni wa Kijerumani.
Mashujaa hao ni pamoja na Chifu Mkwawa wa Wahehe, Abushiri wa Pangani, Kinjeketile Ngwale wa Kilwa na wote wote waliojitoa muhanga kulinda heshima na utu wa Mtanzania.
Tunapoadhimisha siku hii tutambue, kuthamini na kuenzi mchango unaotolewa na JWTZ na kuwapa moyo maafisa na wapiganaji kuendelea kulinda mafanikio yetu ambayo yanaifanya Tanzania kuwa nchi ya kujivunia kwa kuwa na amani na utulivu ukilinganisha na nchi nyingi barani Afrika na sehemu nyingine duniani.
Sikukuu ya kuanzishwa kwa JWTZ inatoa funzo kuwa amani, usalama na utulivu uliopo unapaswa kulindwa na kudumishwa kwa faida ya vizazi vijavyo ili nao waje washerehekee kama tufanyavyo sisi.