Na Christopher Maregesi, Bunda
MKUTANO mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa Chadema mkoani Mara uliokuwa ukifanyika kwenye ukumbi wa Manjebe Annex mjini hapa, jana uliahirishwa baada ya wagombea nafasi ya uenyekiti kurushiana makonde ukumbini.
Ilifikia wakati mmoja wa wagombea hao alidiriki kutaka kuvua nguo ili adhihirishe kuwa ni mwanamume rijali mbele ya mgombea mwenzake, lakini jitihada za wapambe wake ziliepusha kutokea kwa kitendo hicho cha aibu.
Sakata hilo lilitokea majira ya saa 1.08 jioni wakati zoezi la kuhesabu kura za duru la pili likiendelea baada ya washindi wa nafasi hiyo na wengine wa nafasi mbalimbali za uongozi kutofikisha nusu ya kura zilizopigwa katika duru ya kwanza na hivyo kulazimisha upigaji kura kurudiwa.
Wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea, ndipo wagombea mmoja, Mwita Mwikwabe Waitara na Machage Waryoba Machage walipoanza kurushiana maneno, kila mmoja akimbeza mwenzake kuwa hastahili kuongoza chama hicho kwa vile ana tuhuma mbalimbali zikiwemo za ufisadi.
Ni katika ugomvi huo wa maneno ndipo Machage na wapambe wake walipomvamia Waitara aliyekuwa amekaa upande mmoja wa ukumbi huo na kuanza kumrushia makonde na viti, lakini alifanikiwa kuvikwepa na viti hivyo vikatua kwa wajumbe waliokuwa karibu naye na kuwajeruhi, hali iliyowalazimu kupatiwa huduma ya kwanza.
Baada ya sekeseke hilo lililochukua zaidi ya saa moja na nusu, msimamizi wa uchaguzi huo, Charles Mwera ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Tarime, aliamua kusitisha kutangaza matokeo na badala yake kuahirisha uchaguzi huo hadi hapo utakapopangwa tena na makao makuu ya chama hicho.
Habari zinadai kuwa chanzo cha ugomvi huo ni shinikizo lililotolewa na Machage, ambaye pia ni diwani wa kata ya Matongo wilayani Tarime na makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, la kutaka atangazwe mshindi bila ya kuzingatia katiba.
Lakini Waitara alipinga vikali madai hayo akisema yeye kama mmoja wa wagombea hawezi kukubaliana na matokeo yaliyo kinyume na katiba na kuonya kuwa kutoifuata kunaweza kukiletea chama hicho hali ya kujijengea umaarufu na kusababisha mpasuko.
Kauli hiyo ya Waitara iliungwa mkono na msimamizi wa uchaguzi na kumfanya Machage, aliyekuwa ametangazwa kuongoza katika duru la kwanza, kupandisha jazba na kuanza kutoa maneno makali kwa mgombea mwenzake na msimamizi akiwatuhumu kupendeleana kw alengo la kulipana fadhira.
Alidai kuwa Waitara analipwa fadhira hizo kwa vile aliipigia debe Chadema katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Tarime ambao Mwera alishinda kwa kura nyingi.
Jazba na ghadhabu za mgombea huyo zilivuka mpaka wakati alipotaka kuvua nguo ili kumwonyesha Waitara kuwa ni mwanaume aliyetahiriwa kwa jadi ya Kikurya, lakini akazuiliwa kufanya hivyo na wapambe wake, ambao walimtoa nje ya ukumbi wakimtaka aachane na hasira na badala yake aangalie kile kinachoendelea na kama akionewa akate rufani.
Hata hivyo maneno hayo matamu ya wapambe hayakufua dafu kwa mgombea huyo ambaye alizidi kupandisha hasira akifanya kila mbinu ya kumfikia Waitara ili wapigane, lakini hakufanikiwa na hivyo kuamua kutoka nje na wapambe kwa lengo la kususia mkutano huo.
Hata hivyo alirejea ukumbini baada ya kubembelezwa na diwani wa kata ya Tarime Mjini, John Iheche.
Akiongea na waandishi wa habari ukumbini hapo msimamizi wa uchaguzi huo, Charles Mwera aliyeonekana kusikitishwa na kitendo hicho na kuongeza kuwa alilazimika kuahirisha uchaguzi huo ili kuepusha maafa ambayo yangeweza kutokea kama matokeo hayo yangetangazwa na mmoja wa wagombea hao kutangazwa kushindwa.
"Napenda kuwatangazia kuwa nimeuahirisha uchaguzi kwa sababu za kiusalama. Hatuwezi kufanya uchaguzi katika hali hii inayoashiria kuwepo kwa maafa makubwa mbeleni kama tukiendelea nao,"alisema Mwera.
Akiongea na Mwananchi kabla ya uchaguzi, Machage alielezea kuwepo kwa hujuma za wazi dhidi yake ili asipate nafasi hiyo kwani mfumo wa kumpata mshindi katika uchaguzi huo umekuwa tofauti na chaguzi nyingine za kata, majimbo na wilaya.
Alisema kwa kawaida mgombea ambaye amewazidi wenzake ndiye alitangazwa mshindi bila kuangalia kama amepata zaidi ya asilimia 50 ya kura kama ilivyotakiwa katika uchaguzi huo wa jana.
"Hizi ni hujuma za wazi kwangu, huko mawilayani mwenye kura nyingi ndiye aliyehesabiwa msindi leo kwangu imekuwa mpaka zaidi ya asilimia 50 eti ndo katiba inavyotaka, huko nyuma katiba ilikuwa wapi," alihoji mgombea huyo na kutaka chaguzi nyingine zote katika wilaya, majimbo na kata zibatilishwe ili katiba ifuatwe.
Naye Waitara alisema kinachowasumbua wengi ni ufahamu wa katiba kwa kuwa inafafanua wazi jinsi ya kumpata mshindi katika chaguzi mbalimbali ndani ya chama hicho na kuwaomba wanachama kuisoma ili kukiepushia chama balaa la kupata viongozi wabovu.
Katika uchaguzi huo, Machage alipata kura 26 na kufuatiwa na Waitara aliyepata kura 24. Uchaguzi huo ulilenga kuziba nafasi ya udiwani iliyoachwa wazi na Chacha Wangwe, ambaye pia alikuwa mbunge wa Tarime. Mgombea mwingine, John Koyi alipata kura 14.
Wakati huohuo Claud Mshana anaripoti kutoka jijini Dar es Salaam kuwa wanachama 55 Chadema wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho katika uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi kwenye makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam jana, ofisa kampeni na uchaguzi wa Chadema, Susan Kiwanga alisema: Sina idadi kamili (ya waliojitokeza) kwa kuwa fomu zinatolewa hadi mikoani, lakini kwa Dar es Salaam pekee watu waliojitokeza ni zaidi ya 55.
Source: Mwananchi