Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini pamoja na Mama wamedhihirisha uwezo wao wa kisiasa kwa kufanikiwa kuwazidi kete vijana wakati wa uchaguzi wa Baraza la Vijana wa CHADEMA(BAVICHA) katika kinyanganyiro cha uchaguzi kilichofanyika jana.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa dalili za kuwazidi vijana hao zilianza toka juzi usiku ambao Zitto na mama yake walikuwa wakizunguka usiku kuwashawishi wajumbe katika maeneo mbalimbali. Habari zinaeleza kuwa Zitto aliongoza vikao Manzese na Tamali Hotel iliyopo Mwenge na kufanikiwa kuwaka sawa wajumbe ili kumuunga mkono David Kafulila kushinda nafasi ya uenyekiti wa Baraza hilo.
Wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa uamuzi wa Zitto kujitokeza wazi wazi kumuunga mkono Kafulila inatoka na mgombea huyo kutoka katika wilaya yake mkoani Kigoma. Bwana Kafulila anaelezwa kuwa mpanga mikakati mkuu wa kampeni za Zitto kushinda uenyekiti wa CHADEMA taifa na hatimae kuwa mgombea Urais kwa tiketi za chama hicho katika siku za baadaye.
Nafasi ya uenyekiti wa BAVICHA ina unyeti wake katika chama hicho kwa kuwa mwenyekiti huyo ni mjumbe wa kamati kuu ya chama na ni msemaji katika masuala yote yanayohusu vijana
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari zinaonyesha kuwa Bwana Kafulila ni msemaji mkuu wa Zitto kuanzia wakati wa Sakata la Dowans na hata katika suala la Zitto kugombea uenyekiti wa CHADEMA; akiwa kama Afisa Habari wa CHADEMA, katika makao makuu ya chama hicho.
Uamuzi wa kupeleka nguvu za ziada kwa CHADEMA umekuja baada ya mpiga kampeni mkuu wa Zitto, Bwana Msafiri Mtemelwa kuangushwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Temeke ambapo alipata kura tatu.
Katika uchaguzi huo Zitto alifika mapema asubuhi akiwa pamoja na Mama yake ambaye alifika kama mgeni mwalikwa akiwa ni mwenyekiti wa chama cha walemavu(CHAWATA). Kurugenzi ya vijana ilialika Umoja wa Vijana wa CHAWATA kushiriki mkutano huo, na mwenyekiti wao akahudhuria kwa niaba ya vijana hao wenye ulemavu.
Wakati wa mchana, Zitto aliweka meza maalum nje ya ukumbi wa mkutano katika restaurant ya Keys Hotel Mbezi Beach akawa anaita mjumbe mmoja mmoja. Baada ya muda mgombea mwingine wa nafasi ya uenyekiti, John Heche Suguta ambaye ni Diwani wa Tarime mjini akawasiliana Zitto na kumlaumu kwa kutoa hongo kwa wajumbe na kutumia nafasi yake ya kitaifa ya kichama kushinikiza wajumbe kumchagua Kafulila. Bwana Heche akamueleza kwamba yeye kama Naibu Katibu Mkuu, ni sehemu ya Katibu Mkuu ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi(returning officer) anayepaswa kutokuwa na upande wowote. Hata hivyo, Bwana Zitto alimjibu kwa ufupi Subiri Maumivu jioni.
Hatimaye ilipofika jioni ulipokuwa ukiendelea Bwana Heche aliamka na kutaka uchaguzi ufanyike kwa uwazi zaidi kwa kuwa makaratasi ya kura yalikuwa yakigawanywa bila utaratibu, msimamizi wa uchaguzi huo Mbunge wa Tarime akasema uchaguzi uendelee. Bwana Heche akataka pia, maboksi ya kura yawekwe wazi kuonekana kama hakuna kura tayari lakini msimamizi bado akata uchaguzi uendelee. Baadhi ya wajumbe wakataka kura zipigwe kimikoa, lakini bado msimamizi akashikilia msimamo wa kutaka uchaguzi uendelee.
Mbunge Mwera alishindana na Heche katika kura za maoni wakati wa uchaguzi wa marudio wa ubunge mwaka 2008 na wamekuwa na malumbano ya muda mrefu kuhusiana na uenyekiti wa halmashauri ya Tarime.
Zitto aliendelea kuwazidi kete vijana hao kwani wakati mgombea mmojawapo alipoulizwa swali mara baada ya kumaliza kujieleza; Zitto aliingilia kati na kusema halikuwa swali, hivyo mgombea asilijibu. Mgombea huyo aliulizwa kuwa kwa kuwa anagombea nafasi ya uenyekiti wa taifa, ajibu swali nchi ina wilaya ngapi na kata ngapi ili kuona kama anafahamu muundo wa kitaifa wa nafasi anayotaka kuigombea. Msimamizi hakusema chochote pamoja na kuwa Zitto hakuwa meza kuu bali sehemu ya wajumbe.
Kura zilipopigwa katika nafasi ya uenyekiti Bwana Kafulila alikuwa amepata kura 90, Heche kura 80, wagombea wengine wawili wakagawana kura zilizobaki. Lakini katika hali ya kushangaza, kura zaidi ya 40 zilizidi katika uchaguzi huo. Kwa mujibu wa kanuni, msimamizi akata uchaguzi urudiwe kwa awamu ya pili kwa kuwa hakuna mgombea aliyefikisha asilimia zaidi ya 50% kama katiba inavyohitaji. Hata hivyo, mjumbe wa Kamati kuu kutoka Kigoma Aidan Ndowa ambaye alijitangaza tangu kuanza kwa mkutano kuwa ni mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi alitaka mshindi atangazwe kwa matokeo hayo hayo. Hata hivyo, sehemu kubwa ya wajumbe wakataka uchaguzi urudiwe upya kutokana na kura kuzidi ukilinganisha na idadi ya wajumbe waliokuwepo kwenye mkutano.
Msimamizi, Mbunge Mwera akatoa fursa kwa wajumbe kuchangia ambao Wenyeviti wa Vijana wa Mikoa ya Mbeya, Mwanza, Singida, Kilimanjaro, Iringa, Mara nk walitaka uchaguzi huo urudiwe upya chini ya msimamizi mwingine kabisa. Aidha wenyeviti hao walimkosoa wazi wazi Zitto kwa kuvuruga uchaguzi huo kwa kutoa rushwa na kushinikiza wajumbe. Mwenyekiti mmoja wapo akaeleza mkutano kuwa dalili za hujuma zilifahamika mapema kwa kuwa wakati kura zinahesabiwa, Zitto alikwenda kwenye sehemu ya kuhesabu kura akarudi na kumwambia wajumbe kuwa leo vijana lazima wachapane makonde, mara baada ya kusema maneno hayo alikwenda kumchukua mama yake na kuondoka naye kabla ya matokeo kutangazwa.
Mwenyekiti mwingine wa mkoa alieleza kwamba hakuna sababu ya vijana kupigana wakati kiongozi aliyesababisha hali hiyo ameondoka, na kueleza kwamba yeye alishuhudia kura za ziada zikipigwa na Aidan Ndowa, akapewa Danda Juju Martin, Afisa wa Halmashauri wa chama hicho na kuzisambaza. Aidha akamlaumu Msimamizi kwa kukubali watu hao ambao hawakuteuliwa kusimamia uchaguzi akiwemo Afisa wa Vijana Chitanda, kusimamia mchakato huo wakati walikuwa wapiga kampeni wa mgombea mmojawapo David Kafulila. Wajumbe walieleza kwamba waliwasilisha malalamiko yao kwa msimamizi tangu mwanzo lakini msimamizi aliyapuuzia.
Kutokana na malumbano hayo, msimamizi alitoa nafasi kwa mmoja wa waalikwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa mambo ya nje, Bwana John Mnyika kushauri hatua za kufuatwa. Bwana Mnyika alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ratiba na maelekezo ya uchaguzi yanapangwa na Baraza Kuu. Akaendelea kufafanua kuwa kwa mujibu wa Kanuni, Mikutano ya uchaguzi wa kitaifa inasimamiwa na Wazee wastaafu. Wazee hao walimteua Mwera kwenda kusimamia uchaguzi wa vijana kwa niaba yao, hivyo, kutokana na muda kuwa usiku; uchaguzi huo usimamishwe, mkutano uharishwe. Alisisitiza kuwa hii ingetoa nafasi kwa vikao vya kikatiba kukaa ikiwemo sekretariati na kikao cha Wazee kuchambua mapungufu yaliyopo na kutoa mwelekeo kwa kuwa matokeo bado hayajatangazwa rasmi. Hivyo, vijana walekekezwe wabaki Dar es salaam kwa siku moja, ili kujua kama uchaguzi utafanyika kesho yake au katika siku nyingine kwa kadiri ya maamuzi. Mkutano huo uliahirishwa kwa wajumbe kutawafanyika kwa amani kusubiri maamuzi ya kikao cha wazee wastaafu kinachotarajiwa kukutana leo.
Ndugu zangu,
Katika kipindi hiki sikutaka kabisa kuingia na kujibu hoja yeyote ndani ya JF kuhusiana na uchaguzi wa vijana Taifa. Hata hivyo mtaniwia radhi kujibu hili ili kuweka rekodi sahihi kutokana na upotoshaji ambao unafanyika kwa makusudi kabisa ili kushusha heshima yangu katika jamii.
Moja, mimi ni mumbe wa Baraza la Vijana la CHADEMA kwa nafasi yangu ya kuwa mjumbe wa Kamati Kuu wa kuchaguliwa kuwakilisha vijana na nikiwa Mbunge mwenye umri wa ujana (miaka 33). Hivyo kushiriki kwangu kwenye vikao ni jambo la kawaida kabisa kwani nina haki ya kupiga kura. Vile vile nina haki ya kuamua mgombea gani wa kumuunga mkono katika uchaguzi. Niseme waziwazi kuwa David Kafulila ndiye mgombea niliyemwunga mkono na kumfanyia kampeni waziwazi bila kificho chochote kile. Hii inatokana na tabia yangu ya kutokuwa mnafiki. Nilimwunga mkono David Kafulila na alishinda kwa kupata kura 99 dhidi ya kura 73 ambazo alipata mgombea mwingine John Heche ambaye alikuwa anaungwa mono na kundi lililonipinga kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa.
Huyu aliyeandika post hii ni mmoja wa vijana wa makao makuu ya CHADEMA ambaye amekuwa akinipinga siku zote kwa chuki tu ya kuwa mimi nimepaata umaarufu wa kisiasa kuliko yeye na kundi lake.
Mama yangu mzazi ni mwanachadema. Ni kiongozi mwandamizi wa CHADEMA kutoka mkoa wa Kigoma na amekuwa msaada mkubwa wa chama katika Manispaa ya Kigoma. Ninaomba sana masuala yangu ya kisiasa na mahasimu wangu wasimhusishe mama yangu mzazi. Ninaomba sana sana mumuweke mama yangu pembeni. Mwandishi wa post hii tafadhali naomba usimhusishe mama yangu na tofauti zetu za kisiasa. Ninaomba sana hili liheshimiwe.
Pili, ni dhahiri kulikuwa kuna makundi katika uchaguzi wa BAVICHA. Mimi niliweka wazi msimamo wangu wa kumwunga mkono kafulila. Wakurugenzi wa Makao makuu ya chama kuanzia Katibu Mkuu mpaka wakurugenzi kama John Mnyika, John Mrema na hata maafisa kama Halima Mdee walikuwa wanampinga David Kafulila. Hawa wanaogopa uwezo wa Kafulila wa kukataa kutumika na kuwa independent katika maamuzi yake.
Hii sio mara ya kwanza kwa Kafulila kuzuiwa haki yake. Kijana huyu alipitishwa kugombea Ukurugenzi wa vijana na jina lake kwenda katika Kamati Kuu. Ajenda ya uteuzi wake ikasitishwa baada ya kuhofia kuwa atashinda. Mtindo huo huo wameutumia sasa kufuta uchaguzi na kuupeleka mbele mpaka baada ya miezi 6. Mimi nimekataa
1. Uchaguzi umefanyika.
2. Matokeo hayakutangazwa
3. Hakuna aliyekata rufaa
Hivyo, wazee wanapata wapi 'locus' ya kufuta uchaguzi?
Hata hivyo wenye mamlaka ya kufuta uchaguzi ni Kamati Kuu ya chama maana kuna taratibu za rufaa ndani ya chama chetu. Nimetaka Kamati Kuu iitishwe ili taratibu zifuatwe.
Huyu mtu aliyeleta post hii hapa anataka kuspin ili kupinda ukweli bila aibu.
David Kafulila kashinda round ya kwanza zaidi ya 50%. Wamekataa kutangaza matokeo na kuleta fujo kwenye mkutano.
Kuna tuhuma dhidi yangu kuwa nimetoa rushwa. Huku ni kutapatapa kwani tuhuma hizi zinatolewa bila ushahidi. Hivi huyu mwandishi na akili zake timamu anaweza kuweka akilini kwake kuwa mimi naweza kutoa rushwa hadharani? Eti nimevuta kiti na kuita watu kutoa rushwa. Bila adabu anamhusisha mama yangu mzazi.
Mama yangu ana maamuzi yake binafsi na mfano dhahiri ni uchaguzi wa chaha wangwe ambapo mimi nilimwunga mkono arfi na yeye akamwunga mkono Chacha wangwe waziwazi na bila kificho.
Uchaguzi wa vijana haukua na rushwa. Uchaguzi wa vijana wa chadema umefanyika kwa amani kabisa na matokeo hayakutangazwa kwa kuwa mgombea 'wao' hakushinda.
Wanasema eti Mtemelwa aliyekuwa ananiunga mkono alishindwa Temeke. Hawasemi watu waliowatuma kwa kutumia fedha za chama kugombea mikoa 15 na kutupwa chini na watu wanaoniunga mkono. Ukiwemo mkoa wa Dodoma na Shinyanga ambao walitumwa wakurugenzi wa chama kama Benson Kigaila na Erasto Tumbo na kushindwa.
Habarindiyohiyo nakuomba ukumbuke kuwa baada ya uchaguzi kinachofuata ni ukaguzi wa fedha za chama katika kipindi hiki na jinsi zilivyotumika. Nashukuru Mungu kuwa ukaguzi huo sasa utafanywa na CAG
Katika spirit ya umoja na mshikamano wa chama tutamaliza suala hili katika Kamati Kuu ya chama.
Ninaomba sana vijana wa Makao Makuu - hasa Mrema, Mnyika na wengineo waache spinning za kipumbavu ambazo hazijengi umoja na mshikamano wa chama. Waache kuchafua jina langu. Wakumbuke kuwa kuna maisha mbele yetu na kuna kazi ya kujenga chama chetu.
Vijana hawa wakumbuke kuwa majungu hulipwa hapa hapa duniani. Wasubiri nao watakuwa wabunge na watapata ajenda zao za kuwafanya kuwa maarufu.
Wakumbuke pia mimi na Mbowe tunafahamiana kabla yao na tutakaporekebisha tofauti zetu na kugundua wapambe nuksi watakuwa kwenye aibu kubwa. Dunia hadaa!
Haya ambayo nimeyaandika hapa JF nimewaambia vijana hawa 'face to face' ili waache uwongo, uzandiki, majungu, fitna na chuki.
Kafulila kashinda uenyekiti wa vijana. Mpeni ushindi wake. Msibake demokrosia.
Poleni wana JF. Haya hayakuwa ya hapa lakini imebidi. Mwenyekuelewa kaelewa.