Kufungiwa JamiiForums: Mahakama Kuu yayatupilia mbali mapingamizi ya Jamhuri. Kesi rasmi kuendelea

Kufungiwa JamiiForums: Mahakama Kuu yayatupilia mbali mapingamizi ya Jamhuri. Kesi rasmi kuendelea

Aliefungua kesi akamatwa na polisi na kuhojiwa hapo kazi ipo aisee...
Wanatumia nguvu zote ili mradi wafanye wanalolitaka wao..
 
Hii ni kesi muhimu na hii ni issue muhimu sana!, kitu cha ajabu ni angalieni wangapi watachangia uzi huu!
P
Kuna shida kwa viongozi wetu..Serikali inaifungia mtandao flani then inatumia VPN kutuma taarifa kupitia mtandao husika..inafikirisha sana.

Kuna siku nilitembelea wizara ya Nishati pale Mtumba Dodoma, kwenye mbao za matangazo kuna tangazo inahimiza watumishi wa wizara kuwa na account kwenye mitandao ya kijamii kama vile X (tweeter), jamaiiforum, Facebook na zingine ili wawe wa kwanza kuelezea mambo mazuri ya wizara kwa wananchi.

Ila nikajiuliza hivi wizara ya Madini haijui kuwa Serikali imezifungia Jamiiforum pamoja na X (zamani tweeter)? Hao watumishi wa wizara waingie kwa kutumia njia gani?

Hivi kabla ya kufungia mitandao ya kijamii, mawaziri hawapewi briefing kwenye baraza kujua sababu ya kuzifungia ni nini?

Viongozi wetu wanazingua sana.
 
NCHI Ina mambo mengine ya ovyo sana…

Wamefungia mtandao "X" lakini na wenyewe wanaposti taarifa kupitia VPN.... inatuchafua kimataifa sana sana!!
Nadhani Mamlaka nyingine na Viongozi wana uelewa tofauti na wa TCRA.

TCRA hadi walifuta akaunti X lakini Rais wa Nchi yupo.

Inafikirisha sana. Mamlaka hii chini ya uongozi wa Bakari imekuwa sehemu ya kuumiza wananchi na si kuwasaidia. Bakari anasifiwa lakini anachofanya kinaharibu kwa kiwango kikubwa taswira ya Taifa letu.

Ikulu, Rais, Bunge, Mahakama etc kuwa X na kwenye mitandao iliyofungiwa na TCRA ni kichekesho.
 
Kesi hii ikisha, tufungue mashatka kuidai fidia Serikali waliyotusababishia kutokana na madhira waliyotusababishia

Hii itawafanya siku nyingine wasiweze kutoa adhabu za mlengo huu tena
 
watu hawachangii au hatuchangii kwa wingi sio kwa kupuuza ila kwakua hatuna tunachojua, au tunajua kidogo sana kinachofanya kushindwa kujenga hoja na kuchangia kitu kinachoekeweka.
Inashangaza sana hii.. kwa hiyo watz wao hufuatilia nini hasa katika maisha yao? sayansi❌️, geopolitics ❌️, uchumi ❌️, local politics❌️, labda ngono na uchawa. hii siyo nchi ya kuishi kwa mtu yeyote mwenye akili timamu.. baasi tu
 
HIvi siku 90 zinahesabiwaje - maana naona hazifiki mwisho!
Aliyekataa kufunguliwa baada ya siku 90 ni Gerson Msigwa...
Sasa inabidi Mahakama iangalie japo ipo under pressure ya Serikali...haipo huru kwa kipindi hiki
 
Naomba kuuliza? Siku 90 zimepita mbona App ya JF bado imefungiwa?

Machi 25, 2026​


DODOMA, TANZANIA – Katika kinachoweza kuonekana kuwa ni ushindi mkubwa kwa watetezi wa uhuru wa kidijitali barani Afrika, Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali mfululizo wa mapingamizi ya Serikali yaliyolenga kuzuia shauri la kikatiba linalopinga kufungiwa kwa mtandao wa JamiiForums kwa siku 90. Uamuzi huo, uliotolewa Machi 16, 2026, unaashiria hatua muhimu katika sakata lililoanza wakati serikali ilipofunga uwanja mkubwa zaidi wa kidijitali nchini kufuatia matangazo ya moja kwa moja (livestream) yaliyoibua utata.

Kesi hii, Fortunatus Boniphace Buyobe dhidi ya Vapper Tech Limited (JamiiForums), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Kesi ya Kikatiba Na. 000031115 ya 2025), sasa itaendelea kusikilizwa kikamilifu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma. Ijapokuwa awali Serikali ilijenga hoja kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, jopo la majaji watatu: Mhe. Dkt. L. Mongella, A. Kirekiano, na H. Kinyaka, liliamua kuwa kesi hiyo ni "halali" na lazima isikilizwe kwa mapana yake.

Matokeo ya kesi hii yanaweza kuchora upya mipaka ya Mamlaka ya Udhibiti dhidi ya Majukwaa ya Mtandaoni barani kote — lakini safari iliyoifikisha hapa tayari imetuma ujumbe mzito kuhusu gharama binafsi wanazokumbana nazo raia katika kudai haki zao za kikatiba kwenye anga la kidijitali nchini Tanzania.

View attachment 3562777

Asili ya "Kiza" hiki cha Kidijitali​

Mgogoro huu uliibuka Septemba 6, 2025, wakati TCRA ilipotoa taarifa kwa umma kutangaza kusimamishwa mara moja kwa leseni ya Vapper Tech Limited, kampuni mama inayoendesha JamiiForums. Mamlaka hiyo ilidai kuwa jukwaa hilo lilichapisha "maudhui potoshi" ambayo "yalimtukana na kumdhalilisha" Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake.

Kwa miongo miwili sasa, JamiiForums imekuwa uwanja muhimu na adimu wa kidijitali ambapo mamilioni ya watumiaji hujadili masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, na kufichua maovu nchini Tanzania — nchi ambayo uhuru wa habari umekuwa ukikabiliwa na shinikizo la mara kwa mara.

Chanzo kilichotajwa na TCRA kilikuwa ni matangazo ya moja kwa moja (livestream) yaliyofanywa Septemba 4, 2025, na Humphrey Polepole, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, kupitia mitandao kadhaa ya kijamii, ikiwemo JamiiForums. Kulingana na wito rasmi wa TCRA kwa JamiiForums uliotolewa Septemba 5, 2025, mtandao huo ulituhumiwa kuchapisha picha na maoni yanayohusu kikao kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na mfanyabiashara wa Zimbabwe Wicknell Chivayo, pamoja na madai yaliyotolewa na Polepole kuhusu kuuzwa kwa bei ya hasara kwa mgodi wa makaa ya mawe kwa mfanyabiashara Rostam Aziz — yote haya yakidaiwa kufanyika bila kutafuta maoni rasmi ya serikali au kuthibitisha maudhui hayo.

Siku iliyofuata, TCRA ilisimamisha leseni ya mtandao huo kwa siku 90 chini ya Kifungu cha 114 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA), ikidai kukiukwa kwa Kanuni za Maudhui Mtandaoni (2020), zilizofanyiwa marekebisho 2022 na 2025. JamiiForums ilipewa saa chache tu kujitetea mbele ya Kamati ya Maudhui usiku wa Septemba 5, na kufikia asubuhi ya Septemba 6, uamuzi wa kuifungia ulikuwa tayari umetoka.

Akizungumza na BBC Swahili, Maxence Melo alinukuliwa akisema kuwa hatua hiyo ilikuwa kali kupita kiasi na inatishia uhuru wa kujadili masuala ya kiraia nchini, akionya kuwa "inaweka ishara hatari kwa mustakabali wa haki za kidijitali na uhuru wa kujieleza Tanzania."

Mpambano wa Kisheria: Buyobe dhidi ya Dola​

Mnamo Desemba 4, 2025, Fortunatus Boniphace Buyobe — mwanachama aliyethibitishwa (verified) wa JamiiForums tangu Novemba 2011 akiwa na machapisho 463 — alifungua shauri la kikatiba Mahakama Kuu, akiwakilishwa na wakili John Seka wa kampuni ya Seka & Associates.

Hoja ya Buyobe ilikuwa wazi: Serikali haikuiadhibu JamiiForums tu, bali iliwanyamazisha raia wake. Alidai kufungiwa huko kulikiuka haki zake za kikatiba za kutafuta, kupokea, na kusambaza taarifa chini ya Ibara ya 18, na haki yake ya kujumuika chini ya Ibara ya 20.

Kitu cha kipekee ni kwamba Vapper Tech Limited (mjibu maombi wa kwanza), kupitia Afisa wake Mkuu Maxence Melo, iliwasilisha majibu yake Desemba 25, 2025, ikimuunga mkono Mleta Maombi (Buyobe). JamiiForums ilikubaliana kwamba kufungiwa huko kulikiuka haki za kikatiba na ikaongeza ombi lake: kwamba kuendelea kuzuiwa kwa mtandao huo hata baada ya siku 90 za awali kupita, kunaunda "kizuizi endelevu" kinachominya ushiriki wa raia.

Kupotea: Siku 2 Baada ya Kufungua Kesi, Buyobe Atoweka​

Kile kilichotokea ndani ya saa 48 baada ya Buyobe kufungua shauri lake kilibadilisha mgogoro wa kisheria kuwa janga la haki za binadamu. Mnamo Desemba 6, 2025, Buyobe alitoweka. Hakuweza kupatikana na familia yake, marafiki, wala mawakili wake.

Kwa siku 10, alikokuwa hakukujulikana, huku kukiwa na ukimya mzito kutoka kwa mamlaka za serikali. Ni baada tu ya shinikizo kubwa kutoka kwa mitandao ya wanasheria na asasi za kiraia ndipo Jeshi la Polisi lilipokiri kumshikilia kwa mahojiano. Desemba 16, 2025, Buyobe aliachiwa kwa dhamana bila maelezo ya kina kuwekwa wazi juu ya makosa yaliyomkabili.

Utetezi wa Serikali: Mapingamizi Matatu​

Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TCRA waliwasilisha Mapingamizi ya Awali matatu wakitaka kesi hiyo itupiliwe mbali kabla ya kusikilizwa. Jopo la mawakili wa serikali likiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Vivian Method, lilidai:
  1. Kutomaliza Ngazi za Rufaa: Kuwa Buyobe alipaswa kukata rufaa kwenye Baraza la Ushindani (FCT) na sio kuja Mahakama Kuu moja kwa moja.
  2. Res Judicata: Kwamba uhalali wa Kanuni za Maudhui Mtandaoni ulishaamuliwa kwenye kesi zilizopita.
  3. Locus Standi: Kwamba Buyobe, kama "mtumiaji tu" wa mtandao, hana uhalali wa kisheria wa kushtaki juu ya mgogoro wa leseni ya biashara.

Uamuzi wa Mahakama: "Mwananchi Sio Mgeni Kwenye Haki Zake"​

Jopo la Mahakama Kuu lilipangua mapingamizi haya moja baada ya jingine. Kwenye suala la rufaa, Majaji walibainisha kuwa utaratibu huo unamhusu "mwenye leseni" na si mtumiaji. Mahakama ilisema, "Hatuoni mantiki ya kumlazimu Mleta Maombi kutafuta haki kwenye Baraza ambalo yeye atakuwa mgeni."

Zaidi ya yote, Mahakama ilikubali "Locus Standi" ya Buyobe (uhalali wa kufungua kesi), ikikubaliana na hati yake ya kiapo iliyoeleza jinsi kufungiwa kwa mtandao kulivyomzuia kupata na kusambaza habari. Mahakama ilionya kuwa kumlazimu mtumiaji kuthibitisha mengi zaidi katika hatua hii ya awali "ingekuwa sawa na kuzuia upatikanaji wa haki."

Mwangwi wa Kimataifa: Afrika Inatazama na kufuatilia kwa karibu​

Hatua za Serikali zimeshtua jumuia za kimataifa, huku Muungano wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) ukikemea kitendo hicho, na Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (CPJ) ikionya juu ya hatari ya kunyamazisha jukwaa kubwa la kiraia kuelekea uchaguzi.

Wakati kesi hii ikielekea kusikilizwa kikamilifu, Tanzania ipo kwenye njia panda ya kidijitali. Sakata hili si mgogoro wa ndani tena; ni kipimo cha jinsi Mahakama barani Afrika zitakavyoshughulikia mvutano kati ya udhibiti wa Serikali na haki za kidijitali za raia.

Kitu kinachotofautisha kesi hii ni picha nzima inayoijenga: Mamlaka (TCRA) ilivyochukua hatua kwa kasi isiyo ya kawaida; zuio lililovuka muda wake wa kisheria; kampuni iliyoamua kusimama na watumiaji wake badala ya kufanya makubaliano ya siri na Serikali; Asasi za Kiraia zilizopaza sauti kwa umoja; na hatimaye, Mahakama Kuu ambayo imekataa wazo la kwamba raia wa kawaida hawana haki ya kuhoji kile kinachotokea kwenye nyanja za kidijitali wanazozitegemea.

Kwa watumiaji wa JamiiForums na Watetezi wa Haki za Kidijitali, vita hii si ya kugombea leseni tu—ni vita ya kutetea roho ya demokrasia ya Tanzania katika karne ya 21.
 
Naomba kuuliza? Siku 90 zimepita mbona App ya JF bado imefungiwa?
Mkuu,

Umesoma ujumbe uliounukuu? Ujumbe unasema wazi TCRA waliendelea kufungia bila kufuata hata utaratibu wa Sheria. Hapo ni kuomba Mahakama ifanye maamuzi yenye maslahi ya umma.

Labda JF wakija wakatupa updates, lakini kwa inavyoonekana na nyarama zinavyosoma, kuna shida mahali hapo TCRA.
 
Kesi ipo mahakamani

-
Uamuzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha leseni ya mtandao wa Jamiiforums kwa siku 90 umesababisha mtumiaji wa jukwaa hilo, Fortunatus Buyobe, kufungua shauri la kikatiba kupinga uamuzi huo.

Buyobe, anayewakilishwa na wakili John Seka, amevuka hatua ya awali baada ya Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma, kutupa mapingamizi yaliyowasilishwa na TCRA pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Shauri hilo linasikilizwa na jopo la majaji watatu---Arnold Kirekiano, Dk Lilian Mongela na Hadija Kinyaka, likiwahusisha Vapper Tech Limited, kampuni inayomiliki Jamiiforums, kama mlalamikiwa wa kwanza, huku TCRA na AG wakiwa wa pili na wa tatu.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Buyobe anapinga uamuzi wa TCRA wa Septemba 6, 2025, wa kusitisha leseni ya Jamiiforums kwa madai ya kuchapisha maudhui yanayokiuka sheria, tamaduni na desturi za nchi.

Kwa mujibu wa shauri hilo, TCRA ilidai maudhui hayo yaliathiri umoja wa kitaifa, amani, utulivu na kudhalilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Buyobe, ambaye ni mtumiaji aliyethibitishwa wa mtandao huo, anadai hatua hiyo inakiuka haki zake za kikatiba za kutafuta, kupokea na kutoa taarifa na imeathiri uhuru wake wa kutoa maoni.

Pia, anapinga Kanuni namba 9(a), (c), (e), (g) na (j), lakini pia Kanuni za 12(a)(i), 15(A), pamoja na aya ya 3(a), 9 na 10 ya Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2020, kwani zinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara za 18(a), (b), (c), (d), 20(1) na 29(1).

Buyobe anaiomba mahakama itamke kuwa kusitishwa kwa leseni kunakiuka haki za kimsingi kama zilivyoainishwa katika Ibara za 18 na 29 za Katiba.

Mbali na maombi hayo, anaomba mahakama itamke kuwa baadhi ya vifungu vya Kanuni ya 9, 12, 15 na 16 na GN namba 538 ya mwaka 2020 vinakiuka Ibara za 18(a), (b), (c), (d), 20(1) na 29(1) za Katiba.

Pia, anaiomba mahakama itoe tamko kuwa kusitishwa kwa leseni kulikiuka Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), kifungu cha 9 cha Mkataba wa Kiafrika wa Haki za Binadamu na Watu na kifungu cha 19 cha Tamko la Kimataifa la Haki za Kibinadamu.

Awali, TCRA na AG waliwasilisha pingamizi mbiili wakidai shauri hilo halina uwezo wa kisheria kwa kushindwa kutumia njia mbadala, kinyume na masharti ya kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (BRADEA), Sura ya 3, toleo lililorekebishwa la mwaka 2023.

TCRA na AG wamewakilishwa na wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method, wakati Jamiiforums inawakilishwa na wakili Peter Manjanjala.

Katika pingamizi la pili, walidai ombi la namna hiyo lilishatolewa uamuzi kuhusiana na masharti yaliyopuuzwa ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2020 kama ilivyorekebishwa, kwa kuamuliwa na mahakama hiyo.

Hata hivyo, wakili Seka alipinga hoja hizo akieleza kuwa kifungu cha rufaa ndani ya sheria ya TCRA kinamhusu mwenye leseni pekee, si mtumiaji kama mlalamikaji.

Alisisitiza kuwa shauri hilo linahusu ukiukwaji wa haki za kikatiba za mtu binafsi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mahakama iliamua kuwa pingamizi zilizowasilishwa hazina mashiko, na kwamba mlalamikaji amekidhi vigezo vya sheria ya Bradea na kwamba, kwa uchambuzi wa hoja zote za kisheria, wanaona shauri hili liko kisheria kwenda katika hatua ya pili ya kusikilizwa kwa shauri la msingi.

Uamuzi huo ulitolewa Machi 17, 2026, na kuchapishwa katika tovuti ya TanzLII, ukiruhusu kesi hiyo kuingia hatua inayofuata ya usikilizwaji wa hoja za msingi.

Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi Aprili 9, 2026, kuhusu ombi la Buyobe la kutaka kuhoji kiapo cha TCRA, akidai hakijitoshelezi.

Upande wa Serikali umesisitiza kuwa kiapo hicho kinatosha, hivyo uamuzi huo utaelekeza hatua inayofuata ya mwenendo wa kesi.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom