Tarehe 4 Septemba 2024, kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Africa (FOCAC) uliofanyika mjini Beijing, China, makubaliano kati ya China, Tanzania na Zambia kuhusu kuihuisha reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) yalisainiwa mbele ya marais wa nchi hizo tatu. Hatua hiyo inafuatia majadiliano ya muda mrefu kati ya pande tatu kuhusu njia bora za kuihuisha reli hiyo na kuifanya itoe huduma za kisasa zinazoendana na mazingira ya sasa ya kiuchumi, katika kanda ya Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na sehemu nyingine za Afrika.
Tangu mwaka 1976 ilipoanza kutoa huduma, reli ya TAZARA ambayo kimsingi ilijengwa kwa ajili ya kuzikwamua nchi za Afrika dhidi ya utegemezi wa bandari za serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini, na hata kuchangia katika juhudi za ukombozi wa eneo la kusini mwa Afrika, ilitoa mchango mkubwa sio tu katika harakati za ukombozi, bali pia katika kuhimiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo ambako reli hiyo inapita.
Kuanzia bandari ya Dar es salaam, Tanzania hadi Kapiri Mposhi, Zambia ikiwa na kilometa 1860, reli ya TAZARA ilikuwa ni chaguo bora kwa watu wa maeneo ya kando ya reli hiyo, ambayo ilikuwa ndio njia kuu ya usafiri kwa wao wenyewe na usafirishaji wa mizigo yao, wakati hakukuwa na njia nyingine ya kuaminika.
Hata hivyo baada ya shughuli za ukombozi wa eneo la kusini mwa Afrika kukamilika baada ya Zimbabwe kujipatia uhuru, na hasa baada ya mwaka 1994 serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini ilipoondolewa madarakani, polepole reli ya TAZARA ikaanza kukumbwa na changamoto. Changamoto ya ushindani kutoka kwenye bandari nyingine, uchakavu wa injini na mabehewa, ushindani kutoka usafiri wa njia ya barabara, na hata kuachwa nyuma na teknolojia za kisasa, kukafanya uwezo wa kujiendesha kibiashara kwa reli hiyo upungue siku hadi siku. Juhudi za kuihuisha reli hiyo zimekuwa zikigonga mwamba mara kwa mara, hasa kutokana ukosefu wa fedha na teknolojia za kisasa.
Tanzania na Zambia ziliamua kujadiliana na China kuhusu njia bora ya kujikwamua reli hiyo, na kufikia makubaliano kuwa Kampuni ya Uhandisi na Ujenzi ya Umma ya China (CCECC), moja ya mashirika makubwa ya umma ya kimataifa ya China na kampuni ya awali iliyojenga TAZARA, zitashiriki kwenye kazi ya kuhuisha reli hiyo.
Kwa mujibu wa makubaliano, ukarabati wa miundombinu pamoja na mali za TAZARA utachukua takriban miaka miwili. Usimamizi wa mradi utadumu kwa kipindi cha hadi miaka 30, ambapo inatarajiwa kuwa uwezo wa uendeshaji wa TAZARA utaongezeka kwa kiasi kikubwa. Inakadiriwa kwamba usafirishaji wa mizigo wa kila mwaka utaongezeka kutoka wastani wa sasa wa tani laki 5 hadi takriban tani milioni 2, na kupunguza shinikizo kubwa kwenye barabara ya TANZAM, ambayo imekuwa ikiharibika mara kwa mara kutokana na malori mazito kupita, na hata ajali nyingi hutokea barabarani kutokana na msongamano kati ya malori makubwa, mabasi ya abiria na magari madogo.
Waziri Mkuu wa China Bw. Li Qiang leo Alhamisi amefika mjini Lusaka na kuanza ziara yake rasmi nchini Zambia, ambapo ameripotiwa kuenzi zaidi moyo wa ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Afrika ambao TAZARA ndio alama yake muhimu. Ziara hiyo ni ukumbusho wa juhudi za China kusaidia ukombozi wa eneo la kusini mwa Afrika, lakini kinachofanyika sasa ni mwendelezo wa juhudi za China kuhimiza maendeleo ya nchi za Afrika kutokana na mazingira ya sasa ya kiuchumi duniani, na kujenga jumuiya yenye mustakbali wa pamoja kati ya China na nchi za Afrika.