"Miezi saba iliyopita, Rais William Ruto wa Kenya alipowasili Beijing, China ilimkaribisha kwa zulia jekundu. Safari hii anapoelekea Washington, anapokelewa tena kwa zulia jekundu." Katika wakati ambao sera za serikali ya rais wa Marekani Joe Biden kuhusu Afrika zimekuwa zikilalmikiwa, tovuti ya kituo cha televisheni cha Marekani CNN ilianza kwa maneno haya ikielezea ziara ya siku tatu ya rais Ruto nchini Marekani ambayo imehitimishwa hivi karibuni — "kupambana na ushawishi wa China" kwa mara nyingine imekuwa mada ambayo haiwezi kuepukwa.
Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Kenya kutembelea Marekani baada ya miaka 20, na pia ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa taifa la Afrika kufanya ziara rasmi nchini Marekani baada ya miaka 15. Serikali ya Biden ilimpeleka "mke wa rais" Jill Biden kumkaribisha Ruto katika uwanja wa ndege, na pia iliandaa dhifa kubwa ya kitaifa. Zaidi ya hayo, Marekani ilitangaza kuiorodhesha Kenya kama "mshirika mkuu asiye wa NATO" wa kwanza katika kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Wakati huo huo, Marekani imeahidi kuimarisha ushirikiano na Kenya katika masuala ya usalama, teknolojia, na msamaha wa madeni. Miaka michache iliyopita, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alitumia neno "shimo la choo" kuelezea baadhi ya nchi za Afrika, lakini sasa serikali ya Biden inajitahidi kuibembeleza Kenya. CNN inaona kuwa Afrika ya leo imekuwa uwanja wa majaribio ya ushawishi wa kisiasa wa kimataifa kwa Marekani, na moja ya sababu kuu za kuzingatia ziara hii ya rais Ruto ni kupambana na ushawishi unaokua wa China barani Afrika. Pia, gazeti la The Hill lilisema wazi kuwa ikiwa ziara hii haitashughulikia masuala yanayohusu China na Afrika ambayo yanawatia wasiwasi wabunge wengi wa Marekani, basi wabunge wa Marekani hawataangalia wala kuunga mkono ziara hii pamoja na taarifa ya pamoja inayoweza kutolewa.
Kwa kweli, wasiwasi wa Marekani una sababu. Hivi karibuni, kampuni ya ushauri ya Marekani Gallup ilitoa Ripoti ya Mwaka ya 2023 ya Uongozi wa Kimataifa, ambayo ilionyesha kuwa China imeipiku Marekani na kuwa nchi yenye ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika. Asilimia 58 ya wahojiwa walidhani kuwa China ina ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika, ikilinganishwa na asilimia 56 kuhusu Marekani. Hili kwa Marekani inayozingatia sana fikra za ushindani wa nchi zenye nguvu kubwa, bila shaka ni jambo lisilokubalika. Hasa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo jeshi la Marekani lililazimishwa kuondoka Niger na Chad, serikali ya Marekani inafikiria tena mkakati wake kwa Afrika. Kwa sababu hii, serikali ya Biden inatafuta kwa njia mbalimbali kudhoofisha ushawishi wa China barani Afrika, na kutumia Kenya kama ngazi ya kupambana na China ni hatua muhimu kwa Marekani. Hata hivyo, kama mtandao wa Politico hivi karibuni ulivyonukuu afisa wa Marekani anayefahamu undani kuwa, Marekani inaposhughulika masuala kuhusu Afrika inasisitiza sana itikadi, na kulazimisha nchi za Afrika kuchagua kati ya Marekani na China ni sababu kuu ya kupungua ushawishi wa Marekani barani Afrika.
Kabla ya ziara yake nchini Marekani, Rais Ruto alipoulizwa jinsi atakavyosawazisha mahusiano kati ya nchi yake na China na Marekani alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Harvard jijini Nairobi, alisema wazi kuwa "Kenya inataka kuwa rafiki wa wote, si adui wa yeyote... Kenya haielekei Magharibi wala Mashariki, bali 'inaelekea mbele'." Nchi za Afrika zinahitaji washirika wa kweli wa maendeleo kama China, na siyo wale wanaotoa ahadi zisizotekelezeka pamoja na kuhubiri bila vitendo kama "walimu". Kwa kusema kweli, ikiwa Marekani inataka kuongeza ushawishi wake chanya barani Afrika, badala ya kuiangalia China, ni bora itoe michango ya kweli kwa Afrika.