The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Watu wengi wanaamini kwamba kupambana na uhalifu ni jukumu la vyombo vya usalama pekee. Lakini ukweli ni kwamba vyombo hivyo haviwezi kudhibiti uhalifu peke yao. Ushiriki wa wananchi katika kupambana na uhalifu ni jukumu muhimu la kiraia na kizalendo.
Miongoni mwa mipango inayoweza kutumika katika kuzuia/kupunguza uhalifu katika jamii ni pamoja na ulinzi shirikishi, mabaraza ya usalama wa raia kwenye mitaa, kuripoti uhalifu kwa siri n.k. Serikali nyingi duniani zinatoa wito kwa raia wake kuripoti uhalifu kwa mamlaka husika. Watoa taarifa za uhalifu na mashahidi ni sehemu muhimu ya uchunguzi wa polisi.
Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa kufichua uhalifu katika maeneo yetu, bado kuna mambo mbalimbali yanayowafanya wananchi kutoripoti uhalifu pindi unapotokea au wanapogundua mipango ya utekelezaji wa uhalifu.
Baadhi ya watu huwa na hofu ya kulipizwa kisasi kwa kuripoti uhalifu unapotokea katika maeneo yao au wanapoathiriwa na uhalifu huo moja kwa moja. Kwa mfano, wanaoathirika na unyanyasaji wa kijinsia mara nyingi hupata hofu ya kulipiziwa kisasi na hivyo kulazimika kunyamaza.
Pia, watu ambao wana imani ndogo na mfumo wa haki, wakiamini kuwa haufanyi kazi au hautafanya kazi vizuri, wana uwezekano mdogo wa kuripoti uhalifu. Lakini pia kuna wengine huwa wanapata uzito kuripoti uhalifu kwakuwa wanawafahamu wahalifu na hivyo wanawalinda kutokana na ukaribu au mahusiano yaliyopo kati yao.
Hata hivyo, kwa sababu yoyote ile, si sawa kunyamazia uhalifu unaotekelezwa kwa wengine kwani mhalifu akimalizana na mhanga mmoja kuna siku anaweza kukufikia mwenyewe au watu wako wa karibu. Kutoripoti uhalifu unaotekelezwa kwako moja kwa moja ni hatari kwani anayekutendea hatoacha na kuna hatari ya kuwaathiri wengine.
Ukiogopa kuitwa "snitch" kwenye jambo linaloweza kusababisha hatari au hasara kwa wengine, basi wengine nao watakaa kimya kwenye jambo linalokuhusu na uhalifu utaendelea kushamiri. Ikiwezekana ni vema kutafuta namna ya siri kuripoti.
Ni nuhimu kujijengea utamaduni wa kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii zetu kwa kuhakikisha kuwa hatukalii kimya matendo maovu tunayoyashuhudia au kuyasikia. Hili ni jukumu la kiraia na linapaswa kutekelezwa na kila mmoja wetu. Haijalishi ni nini kilitokea au ni lini, uhalifu wote ni mbaya na unaweza kuacha makovu yasiyofutika katika jamii.