SoC01 Kukosekana kwa Upendo na Msongo wa mawazo, Chanzo cha mauaji ya wanawake nchini

SoC01 Kukosekana kwa Upendo na Msongo wa mawazo, Chanzo cha mauaji ya wanawake nchini

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
May 7, 2021
Posts
29
Reaction score
64
Hapa nchini kumekuwa na mauaji mengi na kujeruhiana kati ya wapenzi .Taarifa ya kufunga mwaka ya 2020 ya Jeshi la polisi nchini inaeleza kwamba idadi kubwa ya matukio ya mauaji kwa mwaka 2020 yalikuwa yanahusiana na sababu za wivu wa mapenzi ikilinganishwa na sababu nyingine.

Pia jeshi la polisi lilitoa taarifa julai 20,2021 taarifa hiyo ilionesha kuanzia mwezi mei 2021 hadi juni 2021 kumetokea mauaji 21 yaliyotokana na wivu wa mapenzi.Waathirika wakubwa wa mauaji haya ni wanawake na hii inatokana na maumbile yao na jinsi wanavyowaamini wapenzi wao kupita kiasi,kiasi kwamba huwa hawaioni au hawawezi kutabiri hatari inayokuja.

Mwezi Septemba 2021 nchini Tanzania kumetokea matukio ya mauaji manne ya wanawake na matukio mawili ya wanawake kujeruhiwa.Septemba 9,2021Jacob Mwajenga(35) mkazi wa Bushushu manispaa ya Shinyanga alimkata mkono mke wake Debora Rwekwama(34) kwa sababu za wivu wa mapenzi. Septemba 5,2021 Godfrey Pius Mandai(48) mkazi wa Mlandizi mkoa wa Pwani alimuua mpenzi wake Veronica Gerald(42) kwa kumpa juisi yenye sumu baada ya kufa na yeye akajiua sababu inatajwa ni wivu wa mapenzi.

Septemba11,2021 Richard Daniel mkazi wa Kiteto alimvunja mkono mke wake Eliza Anton.Eliza alisema siku ya tukio alitakiwa na mume wake ampe fedha alizozifanyia kibarua ili akawatafutie watoto wao chakula,yaliibuka mabishano yaliyosababisha kupigwa hadi kuvunjwa mkono.Septemba16,2021 Mwanaidi Hamisi mkazi wa Mwanga,Kilimanjaro alifariki Dunia kwa kuchinjwa na mume wake chanzo kikiwa wivu wa mapenzi.Septemba 18,2021 Jeshi la polisi lilitangaza mkazi mmoja wa kijiji cha Mkolye,Sikonge Tabora alimua mke wake na watoto wao wawili kwa kuwapiga na mchi wa kutwangia.

Tukio lingine la hivi karibuni ni la tarehe 19,Septemba 2021 ambalo Alpha Chawe(42) mkazi wa Tonya Ilomba mkoani Mbeya alimuua mkewe Shukuru Luoga(30).Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Kamishna msaidizi Mwandamizi wa polisi Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa nne asubuhi baada ya Chawe kumshambulia mkewe kwa vipande vya kuni maeneo ya kichwani chanzo kikiwa ni imani za kishirikina ambapo Chawe alikuwa anamtuhumu mkewe kuwa ni mshirikina kwa muda mrefu.

Matukio haya na mengine ambayo hayajapelekwa Polisi yamekuwa yakiongezeka nchini.Kutokana na kushamiri kwa mauaji ya aina hiyo nilimtafuta na kufanya mahojiano na Joseph Hyera ambaye ni mwanasaikolojia na mshauri wa masuala ya ndoa na mahusiano alisema kuna sababu kuu na sababu ndogo ndogo zinazosababisha mauaji ya wapenzi kutokea Hyera alisema sababu kuu ni kukosekana kwa upendo.''Upendo ni vitendo vya ukarimu,upendo ni tendo tufanyalo,upendo siyo kujisikia,upendo ni kuzungumza maneno ya upole na fadhili.Upendo ni kutoa na kusameheana,upendo ni kusaidia, ni shukrani,ni kutabasamu ni kupongeza na vingine vingi zaidi,kwahiyo kukiwa na upendo watu watasameheana watafanyiana vitendo vya ukarimu na kuzungumza kwa upole panapotokea mikwaruzano baina yao'' alisema Hyera.

Hyera anashauri mahusiano yoyote ya kimapenzi lazima yaanze kwa kujengwa na msingi madhubuti wa upendo''watu wapendane kwanza yasijengwe kwa pesa,rangi,umbo,kazi,elimu,yasijengwe kwa watu kulazimisha hawapendani lakini wanalazimisha kwa sababu wanataka ndoa au wanataka mpenzi''alisema Hyera.

Hyera anasema shinikizo la kuoa au kuolewa kutoka kwa jamii,ndugu,marafiki na wazazi inasababisha watu watafute mtu yoyote ili mradi na wao waonekane wameoa au wameolewa bila kuzingatia kama wanapendana au la.''Unapotaka kuoa au kuolewa isikilize nafsi yako inasema nini,usisikilize maneno ya watu,huyo mtu utaishi naye wewe si ndugu zako,jamaa zako wala marafiki zako''

Nguzo tatu za kupenda

Hyera anasema kuongea maneno ya kushukuru,kufanya vitendo vya ukarimu na kumkubali mwenzio kama alivyo ndio nguzo tatu za kupenda.''Neno shukrani linaweza kuwa dogo lakini lina maana kubwa sana kwenye mapenzi kwani shukrani ni namna ya kujali,kukubali na kukithamini kile anachokifanya mpenzi wako.Unaposhukuru pia ni njia ya kumpa hamasa mpenzi wako na ataendelea kufanya jambo hilo vizuri zaidi.Lawama na malalamiko haviwezi kumbadili mpenzi wako lakini neno moja tu la nashukuru linaweza''.

Hyera pia anawataka wapenzi kufanyiana vitendo vya uungwana na ukarimu,vitendo hivyo vikifanyika wapenzi hawataweza kupigana wala kuuana.Pia anawataka wapenzi kukubaliana jinsi walivyo''mkubali kama alivyo hata kama ana kasoro kadhaa,vitu kama uzinzi na kupigana ndivyo haviwezi kukubalika.Upendo husitiri wingi wa dhambi,upendo hukubali na kuvumilia kasoro nyingi''

Hyera anasema sababu nyingine ya wapenzi kujeruhiana na kuuana ni msongo wa mawazo.Msongo wa mawazo ni mfadhaiko wa akili anaoupata mtu kutokana na shida,tabu,dhiki,matatizo au changamoto za kimaisha mhusika anapokosa uvumilivu anaweza kujiua mwenyewe au kuua mtu mwingine''unapopata msongo wa mawazo shirikisha jamaa zako wa karibu na unaowaamini ambao hawatayatangaza matatizo yako,unapotoa lililo moyoni mwako kwa mtu mwingine ndiyo njia ya kwanza ya kutibu tatizo,pia kukubaliana na yale yanayokukabili na yaone ya kawaida tu,kudili mazingira kwa kwenda kwenye misitu,ufukweni,milimani au kuhama kwa muda eneo hilo ni njia nyingine ya kutibu msongo wa mawazo.Pia tembea jichanganye na watu shiriki kwenye shughuli za kijamii kama harusi na michezo,pia kusoma na kuangalia filamu ni njia nyingine ya kutibu msongo wa mawazo ''

Pia Hyera anashauri kuanzishwe vitengo vya ushauri wa kisaikolojia kwenye zahanati,vituo vya afya na hospitali ambazo zitoe huduma bure''kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na mabadiliko ya mfumo wa kimaisha wenye tekinolojia kubwa pia namna yetu ya kuishi imebadilika,wanawake wamepata elimu na wanazijua haki zao,wanauelewa mpana wakati huo huo wanaume wanaendelea kuukumbatia mfumo dume,vitu hivyo vinaweza kusababisha watu wengi wapatwe na msongo wa mawazo,watu wanapata majukumu mengi,wanapata changamoto nyingi ambazo wanashindwa kuzikabili kwahiyo wakiwepo watoa ushauri kuanzia ngazi ya zahanati itasaidia sana kutibu watu wenye msongo wa mawazo''

Mwisho Hyera anashauri ikitokea wapenzi au wanandoa wakashindwa kuelewana wanaweza kutengana kwa muda,wakapeana likizo huku kila mmoja akitafakari na kama ikishindikana kabisa ni bora kuachana kuliko kuvunjana mikono au kuuana ''kama wapenzi wakiona hawawezi kuendelea kuwa pamoja ni bora kuachana kisheria kuliko kung'ang'ania mapenzi ambayo yanaweza kumpeleka mmoja jela na mwingine kaburini,ukiona dalili za kupeleka jela au kaburini yakimbie mahusiano hayo hayafai'' alimalizia Hyera.

Imeandikwa na Simulizi za kweli.
Shukrani kwa Joseph Hyera.

Naomba mnipigie kura nyingi.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom