Wednesday, 06 October 2010 08:13
James Magai
MLALAMIKAJI katika kesi inayomkabili katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa sasa atalazimika kujenga hoja kukabili utetezi uliowasilishwa na mgombea huyo wa urais ambaye amedai kuwa hakufahamu kwamba mwanamke aliyemtangaza kuwa ni mchumba wake, alikuwa mke wa mtu.
Mlalamikaji huyo, Aminiel Mahimbo, ambaye amefungua kesi ya madai namba 122/2010, anataka alipwe fidia ya Sh1 bilioni akidai kuwa kitendo cha Dk Slaa kumtambulisha mkewe, Josephine Mushmbuzi kuwa ni mchumba wake, kilimdhalilisha.
Lakini sasa, Mahimbo na wakili wake watakuwa na siku saba za kuandaa hoja dhidi ya utetezi wa upande wa walalamikiwa na kuziwasilisha mahakamani, kama utaratibu wa kesi za madai unavyotaka.
Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Zainabu Muruke alitoa muda huo wa siku saba baada ya wakili wa mlalamikaji, Abduel Kitururu kuomba muda wa kujibu hoja za utetezi wa mlalamikiwa.
Upande wa utetezi, ambao unawakilishwa na kampuni ya uwakili ya Marando & Mnyele Advocates ulisema hauna pingamizi na ombi hilo na Jaji Muruke alimtaka mlalamikaji kuwasilisha majibu ya hoja hizo za utetezi wa mlalamikiwa ifikapo Oktoba 12.
Pia mahahakama hiyo imepanga Oktoba 15 pande zote katika kesi hiyo kukutana pamoja kwa lengo la kuandaa na kupanga lini na namna ya kuendesha kesi hiyo.
Katika maelezo ya utetezi wake wa maandishi aliyoyawasilisha mahakamani Septemba 29, Wakili Mabere Marando alisema kuwa Dk Slaa alikiri kuwa na uhusiano na Josephene lakini akajitetea kuwa hakujua kuwa mwanamke huyo ni mke wa mtu kwa kuwa hakumwambia kuwa ameolewa.
Alidai kuwa alisikia kwa mara ya kwanza habari za ndoa baina ya mlalamikaji na mwanamke huyo aliposoma habari hizo kwenye vyombo vya habari na hivyo kumtupia mzigo mlalamikaji athibitishe kuwa mteja wake alikuwa akijua kuwa mwanamke huyo ameolewa.
Dk Slaa pia amekana madai ya kufanya uzinzi na Josephine wala kumtangaza kama mke wake na hivyo anamtaka mlalamikaji atoe ushahidi wa madai hayo.
Kuhusu madai ya kumdhalilisha, kumshushia hadhi na kumsababishia usumbufu mlalamikaji, Dk Slaa pia ameyakana na kudai kuwa mlalamikaji mwenyewe ndiye aliyejisababishia hayo kwa kukubali kutoa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari.
Kama vile haitoshai Dk Slaa amemtuhumu mlalamikaji huyo kulipwa na chama cha siasa kuruhusu habari zake hizo ziandikwe kwenye vyombo vya habari kwa malengo ya kisiasa
Dk Slaa anadai kuwa kwa kitendo cha mlalamikaji huyo kuruhusu habari hizo zitangazwe na vyombo vya habari kimemfanya apoteze heshima yake na hivyo hata madai yake hayana msingi na hayana budi yatupiliwe mbali.
Mahimbo alifungua mashtaka hayo Septemba 7 mwaka huu akitaka alipwe fidia ya Sh1 bilioni kwa madai kuwa mwanasiasa huyo ameingilia ndoa yake na kufanya uzinzi na mke wake huyo.
Source: Mwananchi
MY TAKE:
kwa kuwa suala hili limeletwa ('kisiasa?') kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, nimeona bora niweke kwenye jukwaa hili. aidha, kwa kuwa suala lenyewe bado liko mahakamani, napendelea zaidi kuliwasilisha kwenu kama habari ila discussion yoyote ni at your risk.