Mgawanyo wa mikopo mingine ambayo ilichukuliwa na JMT ilikuwaje?
Je! Kulikuwa na uwazi wowote katika kufanya hivyo?
Endapo kama upande Tanganyika umenufaika mno kwa kipindi cha miaka iendayo 58 ya uwepo wa JMT, Zanzibar nayo inapaswa kuanza kufanya hivyo sasa. Kwani tulipoingia kwenye huu muungano hatukujua kuwa Zanzibar ina watu wachache?
Bila kujali ina watu wangapi, Zanzibar ina hadhi yake ya asili ya kuwa nchi hata kama ipo ndani ya JMT, na pia haijawahi kupoteza hadhi yake ndani ya katiba. Ni mawazo finyu kuongelea uwiano wa mgawanyo wa mkopo husika bila ya kuangalia mgawanyo wa mikopo mingine iliyokwisha kutolewa hapo awali kwa JMT.
Hebu tufanye tathimini ya haraka haraka kuhusu jinsi nchi hizi mbili zimefaidika kwa miundombinu kupitia mikopo iliyotolewa kwa idhini ya JMT na kulifikisha deni la taifa kufikia kiasi chaTZS 75Tn.
Tanganyika wala haipo, haishi na wala haina hadhi ya kukopa yenyewe kwa jina lake. Hivyo basi mkopo wowote ule unaochukuliwa ili uinufaishe Tanzania Bara peke yake ni lazima uchukuliwe kwa jina la JMT. Zanzibar nayo kama nchi inayoishi na yenye kutambulika inaweza kukopa kwa kupitia jina lake, na pia inastahiki zake kwa kile chote kinachokopwa kwa jina la JMT.
Ndiyo maana watu wenye akili wanaona kuna haja ya kufanya mabadiliko ndani ya katiba mpya ambapo muundo wa JMT utafanyiwa mabadiliko. Kuna kila haja ya katiba kutambua uwepo wa serikali tatu ndani ya huu muungano, kwa mantiki hiyo kuna haja ya kuifufua hadhi ya nchi ya Tanganyika ndani ya muungano wetu na kutenganisha shughuli zake za serikali na iwe pia na bunge lake kama ilivyokuwa kwa Baraza la Wawakilishi kule upande wa wenzetu wa nchi ile ya Zanzibar.