Nimesoma historia rasmi. Kuna majina umeyataja na kusema ukweli ndiyo nayasikia hapa.
Ndiyo kusema AMNUT lengo lao haswa lilikua ni uhuru usitolewe kwa TANU kwakua hiyo ingepelekea TANU kujiimarisha? Na hii inamaanisha kua sababu zilizotajwa, za kuzuia uhuru kisa waislamu kukosa nafasi za juu TANU, ni sababu za kupikwa?
Castr,
Niwie radhi lakini hujui sababu ya kuundwa kwa AMNUT.
AMNUT haikuanzishwa kwa sababu Waislam hawakuwa wameshika
nafasi za juu katika TANU.
Hadi kufika mwaka wa 1958 hapakuwa na tatizo wala chokochoko
yoyote ndani ya TANU.
Chokochoko ndani ya TANU na kuanza kwa minong'ono ya hali ya
baadae ya Waislam Tanganyika ilianza kusikika baada ya Uchaguzi
wa Kura Tatu uliofanyika mwaka wa 1958.
Waingereza waliweka masharti ya kibaguzi katika kupiga na kuchagua
wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la kikoloni (Legislative Council).
Mpigaji kura alitakiwa kwanza awe na elimu ya darasa la 12, awe na
kipato cha pauni 400 za Kiingereza kwa mwaka, awe na kazi ya maana
na kura kupigwa kuwa kufuata utaifa, yaani kura kwa mgombea Mzungu,
Muasia na Mwafrika.
Baadae sharti la elimu ya darasa la 12 likabadilishwa ikawa darasa la 10.
Wanachama wengi wa TANU walipinga masharti haya ya ubaguzi kiasi
walikuja na kauli mbiu isemayo, ''kuingia katika Uchaguzi wa Kura Tatu
ni sawasawa na kujipaka kinyesi.''
Wanachama wa TANU wengi waliokuwa mstari wa mbele kupambana na
ukoloni hadi mwaka wa 1958 walikuwa Waislam na waliona masharti haya
yalikuwa yameletwa ili kuwaondoa wao katika kugombea na pia katika
kupiga kura.
Lakini katika mkutano wa Tabora juu ya pingamizi iliyokuwapo TANU ilipiga
kura kuamua kuingia katika Uchagzi wa Kura Tatu.
Hili liliwezekanaje ilhal viongozi wakubwa katika TANU kama Sheikh Suleiman
Takadir Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU, Zuberi Mtemvu, na wajumbe
takriban wote wa Baraza la Wazee, walikuwa wanapinga Kura Tatu?
Nyerere hakupata kueleza ni mkakati gani aliweka akishirikiana na uongozi wa
TANU Tanga wa Sheikh Rashid Sembe, Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Abdallah
Rashid Sembe, Ng'anzi Mohamed, Mustafa Shauri na Abdallah Makatta kutafuta
kuungwa mkono kuiingiza TANU katika Uchaguzi wa Kura Tatu.
Wala hakupata kusema kwa nini katika kwenda Tanga kutafuta kuungwa mkono
alimweka pembeni Zuberi Mtemvu Katibu wa TANU badala yake akamchukua
Elias Kissenge na ndiye aliyekwendanae kwenye mkutano wa Tabora.
Uamuzi wa kuingia kwenye Uchaguzi wa Kura Tatu ulipita kwa tabu kuonyesha
upinzani uliokuwapo.
Matokeo ya TANU kuingia katika Uchaguzi wa Kura Tatu ikawa kuwa Waislam
kwa kuwa hawakuwa na elimu hawataweza kugombea wala kupiga kura na ili
TANU ipate wagombea wa kuingia katika uchaguzi ule lazima sasa wawapate
watu nje ya TANU kuja kugombea nafasi zile, watu ambao hawakushiriki hata
kidogo kuifikisha TANU pale ilipofika.
Haya ya kuleta sura mpya ndani ya TANU na kupewa nafasi za uongozi
ndiyo yaliyosababisha kuundwa kwa AMNUT.
Historia hii ya Uchaguzi wa Kura Tatu haiwezi kukamilika bila ya kueleza ugomvi
uliozuka kati ya Sheikh Suleiman Takadir na Julius Nyerere na matokeo yake
Sheikh Suleiman Takadir akafukuzwa chama kwa kosa la ''kuchanganya dini na
siasa.''
Historia hii ya Sheikh Suleiman Takadir inaogopwa kuelezwa hadi hii leo kwa
sababu ambazo sasa ziko wazi.
Nisimame hapa kwani bado yako mengi ya kueleza.