Mag3,
Yericko si makamo yangu kabisa.
Wewe unajua, yeye anajua na dunia nzima inajua.
Kama unafuatilia vizuri nadhani utaona ninapomwandikia na kumwekea
majibu ya maswali yake huwa harejei tena nyuma.
Mimi kwa ustaarabu huwa simkumbushi arejee kwani kufanya hivyo ni
kuleta ubishani.
Huwa nachukulia ukimya wake kuwa kajifunza kitu na huu ndiyo mtindo
wangu.
Maalim Haruna alikuwa akitufunza anasema mwanachuoni kalamu yake
haifedheheshi bali inasomesha.
Ukiandika lazima utakosolewa hili ni jambo la kawaida na mimi sikatai
kukosolewa khasa ukichukulia kuwa kazi yoyote ya binadamu lazima
itakuwa na makosa.
Nakupeni hapa utangulizi wa kitabu kinachotuweka kwenye mjadala huu....
UTANGULIZI
Naam. Ili mtu awe Afisa wa Idara ya Ujasusi yampasa awe mwenye akili zilizotulizana. Yaani, razini. Ndipo basi, pasi na kutafuna maneno, kitabu hiki ni mahususi hususan kwa wasomaji weledi. Kitabu hiki ni motifu, kinachoangazia masuala umuhimu ya ujasusi na jinsi yalivyo ya kipekee, kikitilia uzito umuhimu wake katika maisha ya wanadamu. Kutokana na upekee huo, taaluma ya ujasusi itumike kuleta ustawi katika jamii badala ya kudhuru kama ambavyo mashirkika mbalimbali ya ujasusi yamekuwa yakifanya kwa njia moja au nyingine, hii au ile. Ama kitabu hiki kinakusudiwa kutoa mwanga wa jinsi taaluma hiyo inavyopasa kuendeshwa pamoja na kuonesha uhalisia wa utendaji wake, kinyume na ilivyo kwa baadhi ya mashirika ambapo sasa imefikia hatua jasusi, kachero au afisa usalama kutangaza hadharani, “Unanijua mimi nani? Mimi ndimi, afisa usalama. Sichezewi!” Kwa lengo duni, ili kuwatisha watu kwa sifa za Mfalme Juha.
Mintarafu, kitabu hiki ni bashraf kwa baadhi ya mataifa yanayoendelea kuhusiana na suala zima la ujasusi, mathalani ujasusi wa kidola wa Idara ya Usalama wa Taifa la Tanzania (TISS) na Ujasusi wa Kimataifa unaofanywa na mashirika kama MOSSAD la Israel katika harakati zake za kutimiza dhamira ya kutawala eneo zima la Mashariki ya Kati na dunia kwa ujumla. Zaidi ya hayo, kitabu hiki kinatoa maarifa pevu ya kijasusi ili kuelewa misingi ya ujasusi na umuhimu wake pamoja na kukamilisha shughuli zake mbali mbali. Mathalani kuna Ujasusi wa Kiushindani (Competitive Intelligence) ambao zaidi hutumika katika ulimwengu wa biashara na harakati waweza kuainishwa kama utaratibu wa kiufundi wa kupata habari nyeti za biashara na harakati za malengo, wateja, washindani, maadui, teknolojia na mazingira ya jumla ya harakati na biashara. Habari hizi zaweza kutoka kwa mtu yeyote au vyanzo vyovyote katika eneo husika.
Ujasusi unatajwa kama ni taaluma ya pili kongwe duniani. Yaani, ulikuwapo tangu utanguni, ulimwengu ulipopata maarifa. Mashujaa katika vita vya kale wanasema kuwa ujasusi ni sehemu muhimu ya kimkakati, wakati wa vita. Kinachomuwezesha kamanda hodari kushambulia, kuteka na kufanya mambo yasiyo ya kawaida, yaliyo nje ya uwezo wa kawaida, ni ule ujuzi anaokuwa nao kabla ya pambano lenyewe. Na, ujuzi huo anaokuwa nao kabla, hautokani na uzoevu ama uhodari wa kufanya mahesabu, bali unatokana na taarifu za siri za adui ambazo hupatikana kutoka kwa watu wengine.
Aidha, ujasusi umekuwa sehemu muhimu ya taasisi za kijeshi na kibiashara. Na pia, ujasusi ulikuwa na hadi leo umekuwa ni chachu ya harakati za Kanisa Katoliki. Punde taarifu zinapopatikana, husambazwa kwa usahihi na kwa wakati kwa watoaji maamuzi wa ngazi zote. Ujasusi wa Kiushindani (Competeteve Intelligence) ni ujasusi unaoshughulika zaidi na harakati za kibiashara ambao unatofautiana kidogo na ule wa serikali. Hata hivyo, serikali pia huuwa na idara ya ujasusi wa kibiashara. Ujasusi wa Kiushindani unafuata taratibu na maadili ya biashara ambayo hayafuatwi na taasisi za ujasusi unaohami serikali. Ujasusi wa Kiushindani haufanywi chini ya mwavuli wa kidiplomasia bali, una lengo zaidi la kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kuimarisha huduma na kukabili mikikimikiki ya ulimwengu kwa ajili ya kujipatia faida na ufanisi wa shughuli husika. Kadhalika, Ujasusi wa Kiushindani unatofautiana na ukachero mwingine wa kiserikali ambao huweza kukiuka au kupuuza sheria na taratibu za wengine.
Nyuma ya pazia, mara nyingi, ujasusi hautazamwi kwa wema. Badala yake, ujasusi umeonekana kama shughuli isiyo na uhalali wa kimaadili au utu. Kwa ajili hiyo, kitabu hiki kinatoa changamoto kwa wajuzi na wajuvi wa taaluma hiyo, washiriki na watu wa kawaida kuonesha iwapo fani ya ujasusi itafanywa kitaalamu, inaweza kuwa ya muhimu kwa kurejea mifano ya wakongwe hasa MOSSAD (Israeli), CIA (Marekani), KGB (Urusi), M16 (Uingrereza) na wengineo, wameweza kutawala nyanja hio na kuweza kudhibiti kila sehemu kwa minajili ya kulinda na kuendeleza maslahi yao sehemu mbali mbali duniani.
Wataalamu wa ujasusi wa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939-1945), wametoa tafsiri nyingi kuhusiana na neno ujasusi. Licha ya tafsiri hizo, tafsiri ambayo pengine yaweza kukubalika na wote ni inayoafanua ujasusi kama shughuli za uchunguzi wa mambo mbalimbali kwa njia za kificho, mienendo na harakati za siri za usakaji wa habari au nyaraka muhimu na za uhakika kuhusu watu na matendo yao, yaliyo ya dhahiri na ya uficho, yanayoyafanywa dhidi ya watu wengine, serikali, jumuiya, taasisi, nchi, taifa, kabila, biashara au maslahi ya wengine. Kwa upande mwingine, kitaaluma, ujasusi ni ufundi wa kunasa taarifu au uwezo wa kupata taarifu nyingi kutoka vyanzo tofauti zenye kulenga kuhami, kushambulia kwa ufanisi zaidi, na kuangamiza adui ni shughuli za kimyakimya zenye malengo mazuri au mabaya kwa maslahi ya mtu, kundi, jumuiya, taasisi au Serikali.
Kwa tafsiri ya kiutendaji, ujasusi ni ukusanyaji na uchambuzi wa data na taarifu zinazotoka katika chanzo chochote kile (iwe kwa mtu au chombo). Taarifu hizo huwa zenye mitazamo ya mbali na zinazotoa taswira ya dhamira, nguvu, harakati na athari au matokeo yanayoelekea kutokea. Shughuli za kijasusi ni muhimu katika maisha ya kila siku ya ulimwengu huu wenye matukio mengi.
Tanbihi: Upelelezi/Ushushu/Ukachero ama Ujasusi kamili, usiishie ndani ya vyombo vya Ulinzi na Usalama tu mathalani Jeshi la JWTZ, Usalama wa Taifa, Polisi, Magereza na Uhamiaji tu, bali uende mbali zaidi kama Vyuoni au kwenye kampuni mbalimbali kunatakiwa kuwe na wapelelezi; mashirika ya umma yanatakiwa kuwa na wapelelezi, viwanda vya ndani vinatakiwa kuwa na wapelelezi na wote hawa wanatakiwa kufanya kazi pamoja ili kuleta maendeleo kwa jamii ya watu wao hasa Watanzania. Nchi zenye maendeleo yaliyotia fora, zinaendelea na kuendeleza ushindani mkubwa kwenye nyanja hii. Mathalani, Taifa la Jamhuri ya Watu wa China, lilianzisha utaratibu wa kupeleka wapelelezi nchi nyingi duniani ili wakadukue na kuiba teknolojia/tunduizi na maarifa kuzileta kwao. Hivi sasa, China wana mafanikio makubwa sana si tu kwenye teknolojia bali na kwenye vitivo vingine. Mfano mwingine unaturejesha wakati wa Vita Kuu Pili ya Dunia ambapo Marekani waliiba wanasayansi wengi wa Ujerumani ambao walikuja kusaidia kujenga uwezo mkubwa wa jeshi lao na taasisi nyingine. Kwa ujanja huo, Marekani limekuwa taifa lenye nguvu duniani kwa kipindi kirefu.
Tunapaswa kukumbuka kazi za ujasusi ni ngumu na zenye siri nyingi na kubwa sana. Majasusi wengi pia wana mafunzo ya kujilinda, kupambana, kushambulia na kufisha maisha. Tendo la kufisha katika medani za kijasusi ni tendo la hitimisho katika misheni au zoezi lolote lile ikiwa kutakuwa na ulazima huo na halina kinga ya kisheria wala msingi wa huruma ya kiutu. Muhimu ni kuwa kufisha huwa ni kwa maslahi ya Taifa.
Kwa kuhitimisha, ujasusi hautumiki kutafuta taarifu mbaya tu. La hasha. La mara elfu la. Kuna taarifu nyingi nzuri zinazoweza kutumika Vyuoni au Ndakini, Wizarani, jeshini na sehemu nyingine kwa minajili ya kuimarisha au kujenga zana na vifaa vya kisasa katika utandawazi wa dunia mpya.