The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Wakati viongozi wakitazamia kusimika mabavu yao, kwa kawaida huwa wanashambulia haki zetu za uhuru wa kujieleza kwanza. Tumeona mchezo huu mara nyingi. Kwanza wanashambulia vyombo vya habari, kisha taasisi za kidemokrasia, na kisha, taratibu, wanachukua uhuru wetu.
Namna ambayo serikali zimekuwa zikipambana na maandamano zimekuwa za kikatili na za kukandamiza zaidi kwa sababu wao na sisi tunajua kuwa kujieleza ni muhimu katika kuongeza ufahamu na kuleta mabadiliko.
Kwa mfano, kuna uhalali wa kuzuia mikusanyiko kwa kuzingatia afya ya umma, lakini baadhi ya yale tuliyoona miaka au miezi ya karibuni yalikuwa matumizi mabaya ya marufuku hizo. Nchini Tanzania, kwa mfano, mikutano ya kisiasa ilikabiliwa na mkono wa chuma wa serikali, huku shughuli nyingine (mfano sherehe za soka) zikiruhusiwa.
Tunahitaji kuruhusiwa kusema tunachotaka; ili mradi maneno yetu hayaleti madhara kwa miili ya watu au mali, la sivyo jamii itadumaa na tutakuwa wafungwa kwenye mafuvu yetu wenyewe -- kwa kusema tu mambo ambayo wenye mamlaka ndiyo wameidhinisha.
Bila uhuru wa kuzungumza, hatuwezi kamwe kutatua matatizo ambayo yanahitaji kutatuliwa. Bila Uhuru wa Kuzungumza, serikali inaweza kuwa dhalimu kama inavyotaka, na kuwaua/kuwadhuru wapaza sauti bila kuadhibiwa. Pale ambapo Uhuru wa Kuzungumza haupo, wenye mamlaka wanaamini kuwa wana haki ya kuwafanya chochote wanaosema mambo wanayoona kuwa ya kuudhi kwao.
Uhuru huo wenye thamani unaendelea kupotezwa polepole lakini kwa nguvu kubwa. Kwa mujibu wa ripoti ya Uhuru wa Kujieleza mwaka 2021 iliyotolewa na taasisi ya Article 19, kuanzia hali ya uhuru wa kujieleza/kutoa mawazo binafsi imekuwa ikidorora kadiri muda unavyosogea katika maeneo mengi duniani, na bara la Afrika halikuachwa.
Tanzania, kwa mfano, tangu mwaka 2010 imekuwa ikizama zaidi katika shimo hili. Ripoti hiyo inaonesha kuwa hali mbaya zaidi zimekuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2020 ambapo katika miaka hiyo uhuru wa kujiezela uliainishwa kama “Highly Restricted” (Umezuiwa Sana); mwaka 2015 hadi 2017 ulikuwa “Restricted” (Umezuiwa), huku mwaka 2010 hadi 2015 ukiwa “Less Restricted” (Vizuizi Vidogo).
Kielelezo 1: Hali ya Uhuru wa Kujieleza Tanzania kuanzia mwaka 2010-2020
Chanzo: Article 16 Org (2021)
Katika maeneo mengi ya Afrika na mengine duniani ambayo Uhuru wa Kujieleza/Kuzungumza unakandamizwa kila uchao, mambo yanayotajwa yamekuwa ni yaleyale: Unyanyasaji, vitisho kwa wanahabari na watendaji wa vyombo vya habari wanaoonekana kukosoa sera za serikali, kufungwa kwa vyombo vya habari vya kibinafsi; kupitishwa kwa sheria kandamizi au marekebisho ya sheria iliyopo ambayo inazuia uhuru wa kujieleza na mtiririko huru wa habari.
Pia, hali hiyo imeendelea kuimarishwa zaidi na taarifa za kupotea, kukamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini kwa waandishi wa habari na watendaji wa vyombo vya habari, ambao katika baadhi ya matukio wanashikiliwa bila kujulikana na kwa muda mrefu bila kufunguliwa mashtaka au kufuata sheria.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hakuna nchi katika bara la Afrika iliyokadiriwa kuwa na uwazi/uhuru wa kuzungumza; watu wengi wanaishi katika hali tete (crisis) na vikwazo lukuki (highly restricted). Katika nchi 42 zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, nchi 13 zipo katika hali ambapo uhuru huo umezuiwa sana - yaani kuna vikwazo lukuki; 14 kati ya hizo zipo katika hali ya vizuizi vidogo (less restricted); nchi 1 ipo katika hali ambayo uhuru umezuiwa (restricted) na nchi 8 zipo katika hali tete (crisis).
Kielelezo 2: Hali ya Uhuru wa Kujieleza katika nchi 42 za Afrika - Kusini mwa Jangwa la Sahara kuanzia mwaka 2010-2020
Chanzo: Article 16 Org. (2021)
Mdororo huu wa Uhuru si tu unaathiri Tanzania na mataifa ya Afrika pekee, bali hata katika mataifa makubwa. Majina ya China, Uturuki na Poland yamejitokeza katika kadhia hii.
Ripoti ya Article 19 inasema mnamo mwaka 2020, waandishi wa habari 62 waliuawa na 274 walifungwa kote duniani. Waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu wanaharakati wa kisiasa na watoa taarifa walikamatwa, kuzuiliwa na kuhojiwa, mara nyingi kiholela, na kufunguliwa mashitaka kwa kukosoa majibu ya serikali kwa COVID-19, kutoa maoni yao kuhusu janga hilo, au kushiriki habari, ikiwa ni pamoja na huko Palestina, Poland, Madagascara, Eswatini, India, Tunisia, Niger na Cameroon. Wafungwa wengi walikuwa ni katika nchi za China, Uturuki na Misri.
Kati ya visa 620 vya ukiukwaji wa uhuru wa yombo vya habari uliorekodiwa ulimwenguni kote katika miezi 14 ya kwanza ya janga hili, 34% yalikuwa mashambulizi ya kimwili na ya maneno kwa waandishi wa habari; 34% walikuwa kukamatwa kwa waandishi wa habari, au mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya waandishi wa habari na mashirika ya vyombo vya habari na serikali; na 14% zaidi vilikuwa vikwazo vilivyowekwa na serikali katika upatikanaji wa habari.
Pamoja na mabavu ya tawala za Afrika, uhuru wa kujieleza ni jambo linalopuuzwa. Linapuuzwa na pengine kutopewa nafasi kuanzia ngazi za familia na hata kwenye taasisi za kiimani na elimu. Watoto na vijana wanafundishwa kunyamaza. Misemo kama “Mkubwa hakosei” ni mambo tunayoyasikia kila siku na hakuna anayeona hatari ya kutamka hivyo na aina ya kizazi kinachotengenezwa.
Huenda ni moja ya changamoto za tamaduni zetu. Wengi wetu tumenyon’gonyea; tusio na nguvu za hoja. Ni kawaida tu kuwa imekuwa ni kosa la kumfukuzisha mtu au kumtenga katika jamii fulani endapo atadai haki zake au kuwa na mawazo tofauti. Kinachofundishwa ni kutii mamlaka, hata kama kuna haki ya msingi ya kudai.
Inaweza kuanza na wewe. Ni vema kutafakari athari za mwanadamu ambaye anashindwa kuzungumza kwa ajili ya nafsi yake na kutamani isitokee kwa uwapendao. Tujifunze, tuwafunze na tusisitize umuhimu huo. Maana, kusudi na utekelezaji wake ujadiliwe. Hata wanahabari wengi siku hizi, ambao taaluma zao zimeegemea kwenye Uhuru wa Kuzungumza, hawaamini nguvu ya uhuru huo kwasababu hawasomi na kuelewa.
Bila mtiririko huru wa mawazo na ukosoaji jamii haiwezi kuchochea ustawi wa wengi. Jamii iliyofungwa, iliyodhibitiwa itakuwa kama serikali ya kiimla yenye udhalimu ambayo watu wake wanakuwa kama watumishi waoga badala ya kuwa raia huru wa nchi yao. Wapende wasipende, watu walio madarakani wanahitaji kukosolewa na taarifa za wazi.
Kuweza kushughulikia changamoto ya ukosefu wa Uhuru wa Kujieleza kutamaanisha kuongeza uwezo wetu wa kurudisha udhibiti wa pamoja wa rasilimali za umma, taasisi na watu binafsi.
Katika kila jamii na kila nchi, kukabiliana na changamoto hizi kutahitaji sauti, uwazi na ukweli.
