Katika madai yaliyosikilizwa kwenye Mahakama ya Ajira ya London (Central London Employment Tribunal), imeelezwa kuwa kampuni ya simu za mkononi ya Tigo ilihusishwa na kutoa taarifa za mawasiliano ya simu za kiongozi wa upinzani wa Tanzania, Tundu Lissu kwa serikali ya Tanzania. Taarifa hizi zilihusisha maelezo ya mawasiliano pamoja na eneo alilokuwepo, kipindi kifupi kabla ya jaribio la mauaji dhidi yake mnamo Septemba 2017.
View: https://youtu.be/zYRidz0K_AU?si=0soRX46Vt7IwsnRg
Madai haya yamewasilishwa katika kesi inayomhusisha Michael Clifford, afisa wa zamani wa Polisi wa Metropolitan (Uingereza) na mpelelezi wa ndani wa kampuni mama ya Tigo, Millicom. Clifford anadai alifutwa kazi kwa sababu ya kufichua taarifa za ndani (whistleblowing) kuhusu hatua ya kampuni hiyo kutoa taarifa za simu za Lissu kwa mamlaka za serikali ya Tanzania, jambo ambalo linaashiria ushirikiano katika jaribio la kumuua mwanasiasa huyo.
Mnamo Septemba 2017, Tundu Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki na mmoja wa viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari lake alipokua akielekea nyumbani kwake jijini Dodoma. Gari lake lilishambuliwa na risasi kadhaa na Lissu alijeruhiwa vibaya sana. Licha ya jaribio hili la wazi la kumuua, hadi leo hakuna mtu yeyote aliyekamatwa au kushtakiwa kwa kuhusika na tukio hilo, hali iliyozua maswali mengi kuhusu ufanisi wa upelelezi na usalama wa wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania.
Kesi hii inazungumzia ushirikiano unaodaiwa kuwepo kati ya kampuni ya Tigo na mamlaka za Tanzania ambapo Tigo inadaiwa kutoa taarifa za mawasiliano na mahali alipo Lissu kwa mamlaka za serikali kabla ya jaribio la kumuua. Taarifa hizo zilifuatiliwa na kutumwa kwa maafisa wa serikali kwa njia ya ujumbe wa WhatsApp. Madai hayo yanaeleza kuwa baada ya kutumwa kwa taarifa hizo, Millicom ilitoa maelekezo ya kufuta mawasiliano hayo ili kuficha ushahidi wa kuhusika kwake.
Michael Clifford anadai alipewa jukumu la kuchunguza suala hili baada ya kusikia kwenye mkutano wa Tigo kuwa taarifa za Lissu zilikuwa zikitolewa kwa serikali ya Tanzania. Baada ya uchunguzi wake, Clifford alitoa ripoti kwa wakuu wake, akionyesha kuwa ufuatiliaji wa mawasiliano ya Lissu ulianza tarehe 22 Agosti 2017, na ufuatiliaji huo uliimarishwa zaidi kuanzia tarehe 29 Agosti 2017, ambapo kampuni hiyo ilianza kufuatilia kwa muda wa saa 24 taarifa za simu za Lissu.
Clifford anadai kuwa baada ya kutoa taarifa hizo, uhusiano wake na wakuu wake wa kazi uliyumba, na hatimaye alitengwa ndani ya kampuni na kufutwa kazi mnamo mwaka 2019 kwa madai ya kuwa nafasi yake haikuwa ya lazima (redundant).
Kwa upande wao, Millicom walikataa madai yote ya Clifford, wakisisitiza kuwa Clifford aliombwa kufanya uchunguzi kuhusu suala la Lissu kama sehemu ya kazi yake ya kawaida, na kuwa aliripoti matokeo ya uchunguzi huo kama ilivyotarajiwa. Kampuni hiyo inadai kuwa hatua za kinidhamu zilichukuliwa dhidi ya baadhi ya wafanyakazi kutokana na uchunguzi huo, lakini wanapinga tuhuma kuwa walihusika katika jaribio la kisiasa la mauaji. Aidha, Millicom inadai kuwa kufutwa kazi kwa Clifford kulihusiana na mpango wa kampuni kupunguza shughuli zake barani Afrika, na siyo kwa sababu ya ripoti zake.
Kampuni hiyo pia inadai kuwa Clifford alikuwa akifanya kazi kama mpelelezi wa ndani wa kampuni, na sasa anadai kwamba taarifa zake ni za kufichua ukiukwaji wa sheria (whistleblowing) kinyume na jukumu lake la kawaida la kazi.
Kwa Watanzania, jaribio la mauaji ya Tundu Lissu limeacha alama kubwa katika siasa za nchi, huku maswali mengi yakiibuka kuhusu usalama wa wanasiasa wa upinzani, na hasa namna vyombo vya usalama vinavyoshughulikia kesi zinazohusisha viongozi wanaopinga utawala wa serikali. Jaribio hilo lilibadilisha hali ya kisiasa nchini, na kusababisha hofu na mashaka miongoni mwa wanasiasa wa upinzani na wananchi wanaotetea demokrasia.
Kesi hii inaibua maswali mapya kuhusu ushirikiano kati ya mashirika ya kibinafsi na serikali katika kufuatilia mawasiliano ya raia, suala linaloweza kuonekana kama matumizi mabaya ya teknolojia dhidi ya haki za faragha za wananchi. Ikiwa madai haya yatathibitishwa, itakuwa pigo kubwa kwa Millicom na Tigo, na pia itazua maswali zaidi kuhusu ushiriki wa mashirika ya kibiashara katika masuala ya kisiasa na kiusalama.
Habari hii imeripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari nchini UK, ikiwa ni pamoka na
The Guardian. Kiukweli kesi hii imenikumbusha ile kesi ya kiongozi wetu
Maxence Melo mnamo mwaka 2016, nadhani tunaikumbuka.
Wacha tuone yatakayojiri, mi napita tu👨🏾🦯