Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema idadi ya waliopoteza maisha katika ajali ya kuanguka kwa jengo la ghorofa eneo la kariakoo nchini imefikia 16.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wananchi kwenye viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiongoza shughuli ya kuaga miili ya waliopoteza maisha.
Amesema athari ya kuanguka kwa ghorofa ni pamoja na kuharibika kwa mali nyingi, majeruhi wengi na mbaya zaidi ni vifo, ambapo amesema mpaka sasa waliookolewa wakiwa hai wamefikia watu 86.
Majeruhi walifikishwa kwenye hospitali mbalimbali za jijini na wengi wao wameruhusiwa huku watano wakiwa chini ya uangalizi wa karibu.
''Kutokana na athari hizi serikali imeendelea kuchukua hatua kunusuru maisha ya wenzetu ambapo shughuli za uokoaji zinaendelea''
''Kazi hiyo isisimame, usiku na mchana mpaka tuhakikishe mtu wa mwisho anaokolewa'' alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Serikali imesema inaendelea kugharamia matibabu kwa walioathirika, kwa kutoa mahitaji na gharama za mazishi kwa marehemu wote.
Waziri mkuu Majliwa amesema serikali itafanya uchunguzi maalumu kujua chanzo cha ajali na kumsaka mmiliki wa jengo ili kuisaidia polisi kwenye uchunguzi.
Imeunda tume ya watu 19 ili kuyapitia majengo yote ya maghorofa ili kujua ubora wa majengo na kuishauri serikali nini ifanye baada ya uchunguzi.