Na Mwamba wa Kaskazini, Ngarenaro, Tanzania
WIKI hii wakati ndugu zetu waislamu wakiwa katika tafakuri kuu ya Mfungo wa Ramadhani, kwa sisi Wakatoliki Tafakuri ya Pasaka ilishapita. Hata hivyo nimekuwa katika tafakuri binafsi juu ya hoja ya Katibu Mkuu wa CCM, kamaradi Dkt. Bashiru Ally, kuhusu umuhimu wa vijana kuandaliwa leo ili kuwa viongozi wazuri wa baadaye.
Nikiwa katikati ya tafakuri hiyo, napokea taarifa njema kutoka Bungeni Dodoma kuwa Serikali imeamua kusitisha maombi ya Uwekezaji wa Bandari ya Bagamoyo yaliyokuwa yatekelezwe na kampuni ya China Merchant Group yenye makao yake Hong Kong na Shengzhen, China.
Hata hivo, wakati furaha yangu ikiwa juu, hasa kwa sisi tunaojua kwa kina undani wa mfumo ambao Wachina walikuwa wanaupendekeza na madhara yake kwa Taifa, ghafla, na kama kawaida yake ya kukurupuka, anajitokeza Kiongozi wa ACT Zitto Zuberi Kabwe na kubeza uamuzi huo wa Seikali.
Katika makala yake aliyoipa anuani ya “Kufutwa Kwa Mradi wa Bagamoyo SEZ Kumedhihirisha Udhaifu wa Wa Rais Magufuli Kwenye Uchumi na Diplomasia,” Zitto anajenga hoja nyingi za kuonesha anataabikwa kwa uamuzi huo lakini hoja zake ni hizi kuu mbili:
Mosi, Kwamba kwa Serikali ya Awamu ya Tano kuachana na uwekezaji huo wa Wachina wa China Merchant na wabia wao wa Oman, Tanzania itapoteza fedha nyingi za kigeni, mapato na ajira kwa watu wake (faida za kiuchumi); na
Pili, Kwamba kidiplomasia mradi huu unagusa uhusiano wa muda mrefu wa Tanzania na China na kwamba kuusitisha ni kuathiri diplomasia.
Nitazijadili hoja hizi kwa kifupi sana leo ili nione kwanza pumzi ya Zitto katika uelewa wake wa uchumi na diplomasia.
*Ya Bandari ya Bagamoyo na Uchumi wa Nchi*
Nianze kwa kumshauri Zitto Kabwe, najua amesoma uchumi bila kuufanyiakazi, atafute sehemu akapige “kafield” kauchumi ili kujipa uhalali wa kuchambua masuala mazito ya kiuchumi kama uwekezaji mkubwa wa aina ya Bandari ya Bagamoyo bila kujipotosha wala kupotosha umma.
Katika miradi kama hii inayohusisha nchi na raslimali ya Taifa kama ardhi na bahari hoja mbele ya wachumi waliobobea sio kama Zitto anavyoziwasilisha kiwepesi sana kama kuonesha idadi ya watu watakaoajiriwa, kodi (dhaniwa) zitakazokusanywa wala si sahihi kuangalia kwanza masuala madogo madogo na yenye taathira ya kishamba kama kusema “tutakuwa Dubai ya Afrika?” au maneno matamu tu ya kizungu eti kuwa “main logistics hub!”So what?
Badala yake, katika mambo haya hoja pana ni mapana ya kufaidika kwa nchi, umiliki wa mindombinu itakayojengwa na maslahi mengine mapana ya nchi.
Ndio maana kwa hoja ya umuhimu wa mradi licha ya MoU yake kupitishwa mwaka 2013 hata Mstaafu Kikwete mwenyewe ambaye Zitto anamtajataja sana hakuweza kuuharakisha mradi huo. Aliweka umakini fulani.
Alipoingia madarakani Rais Magufuli (rejea hotuba yake ya 6 Februari, 2018 jijini Dar es Salaam) aliweka bayana kuwa Serikali yake imeridhia mradi huo na kuruhusu majadiliano ya wataalamu yaanze.
Wanaofahamu yaliyotokea katika majadiliano ya mradi wanaweza kucheka mpaka kuvunjika mbavu wakimuona Zitto anavyotetea mradi asioujua na akitumia nadharia nyepesi sana kiuchumi za “ajira, mapato na kuwa Dubai ya Afrika.”
Taarifa kutoka kwenye majadiliano zinapasha kuwa ghafla Wachina walipoona Serikali mpya imebariki mradi wakaanza “kupanua goli” kwa kuja na madai mapya kila siku. Hapa ndipo linapokuja suala la maslahi mapana ya nchi sio ujinga wa vitu kama ajira na mapato.
Mara wakaleta sharti la pamoja na kuiendesha bila kuingiliwa wao ndio wawe wanapanga bei wakishaijenga Bandari ya Bagamoyo, mara wakaja nasharti kwamba ikijengwa Banadari ya Bagamoyo kusiendelezwe Bandari yoyote nyingine kutoka ukanda wa Mtwara hadi Tanga!-hii maana yake ni kwamba Bandari za Mtwara, Mafia, Kilwa, Dar es Salaam mpaka Tanga zingebaki kama zilivyo sasa na zingekufa!
Kubwa zaidi na ambalo bado nasisitiza hoja yangu kuwa Zitto akatafute “field” ajinoe upya kuhusu uwezo wake katika masuala ya kiuchumi ya sasa, ni jinsi Wachina anaowatetea, durusu za majadiliano zinapasha, walivyokuja na dai la KiCarl Peters.
Mnaukumbuka Mkataba wake na Sultani Mangungo wa Msovero uliosainiwa Novemba 29, 1884?
Hayo ndiyo yalikuwa yajirudie. Kama ambavyo Zitto ametaja bayana kuwa mradi huu sio Bandari tu-sahihi kabisa, unahusisha mambo mengi ikiwemo ujenzi wa eneo la viwanda na mji wa kisasa. Safi kabisa, ahadi tamu kama za Carl Peters kwa Sultan Mangungo.
Sasa sikiliza hii-katika eneo lote la viwanda na mji wa kisasa Wachina wakataka si tu hati ya eneo hilo lote isomeke kwa jina lao bali walimiliki kabisa eneo hilo kwa zaidi ya miaka 33!!!
Na si kumiliki tu, wakataka kwa kuwa wao ndio “wamiliki” wa kipande hicho cha ardhi ya Tanzania ndio wawe wasimamizi, wasajili na wenye uamuzi juu ya viwanda vyote vitakavyotaka kuwekeza kwenye eneo hilo kuanzia kuvisajili, kodi wanazolipa hadi uamuzi wa mwisho wa nani aweke kiwanda na nani asiweke! Bandari ya Eritrea leo nje kumejaa viwanda vya China vitupu. Nasi tulikuwa tunawelekea huko.
Kwa kifupi mbaya zaidi wanasema, imeelezwa, kuwa hata hiyo miaka 33 haitaisha “automatically” inaweza kuongezeka hadi umilikiwa miaka 99 iwapo watakuwa hawajarejesha faida yao.
Nani atahakiki urejeshaji wa faida?Hii ni hatari heri wakupe mkopo ufanye mwenyewe, ulipe mkopo hata kama ni wa ghali.
Kwa nini mfumo huu kiuwekezaji ni hatari heri ukope na kulipa, tofauti na uelewa mdogo sana wa Zitto, kwa wao kuwekeza hizo Dola bilioni 10, Wachina wangeendesha wenyewe biashara zote na wao ndio wangekuwa wanaandaa mahesabu na kila mwaka wangekwambia wanapata hasara lakini wangeendelea kuwepo kwa zaidi ya hiyo miaka 33.
Wachina wanapataje hasara ili kujustify kuendelea kukutawala katika biashara?
Uzoefu wa nchi nyingi zilizoingia mkenge huu wa kusubiri “faida ya Mchina” unaonesha haya: Mosi, watacheza na hesabu kwa kutumia mifumo yao ya kisasa ya kidigitali na iliyo kwenye codes na lugha ya Kichina pekee.
Pili, zabuni zote watapewa makampuni rafiki (third party companies and related parties) ambao watawachaji kwa makusudi China Merchant bei kubwa ili gharama ya uwekezaji uwe kubwa kiasi mapato yawe chini kila mwaka.
Hapa utaambiwa kwa miaka 100 “hakuna faida” kwa hiyo Bndari na mji na eneo la viwanda vinabaki kwenye umiliki wao!!
Katika hili Tanzania inayo mifano mingi ya aina hii lakini moja ya uwekezaji unaotukumbusha falsafa ya Wachina na staili zao za upigani ni ubia wa TBC na StarTimes ya China ambao hata Zitto Kabwe, Bunge na CAG wameupigia kelele weee lakini miaka zaidi ya 10 sasa Wachina wanatangaza kupata hasara lakini kuondoka hawataki!
Kwa hiyo katika uelewa, maono na kutetea maslahi mapana ya Taifa namuona Zitto na Magufuli kuwa viongozi wenye mitazamo miwili yenye tofauti ya “mlima na kichuguu.”
Wakati Zitto anawaza vitu vya kishamba shamba (sawa na Sultan Mangungo wa Msovero aliyepewa shanga na maua akauza ardhi), Magufuli ni kiongozi imara, makini na anayefuatilia mambo kwa umakini “wa mawinguni.’
*Bandari na Diplomasia ya Tanzania na China.*
Katika hili nimshauri tu Ndugu Zitto yapo maeneo ni ya kukaa kimya. Hajui misingi ya diplomasia ya Tanzania, hajui sayansi na sanaa katika utekelezaji wa diplomasia za dunia, hivyo kamwe hawezi kuhitimisha kuhusu diplomasia ya Tanzania na China kwa sababu ya Bandari ya Bagamoyo.
Labda nianze hivi-msingi wa diplomasia ya China na Tanzania haukujengwa katika ubepari unaooneshwa sasa na baadhi ya kampuni za China na Serikali ya China inajua hilo.
Msingi wa diplomasia ya mataifa haya mawili na ambao hauwezi kutetereshwa na mradi wa Bagamoyo ni manufaa na imani.
Ndio maana makubaliano ya awali kabisa rasmi ya mataifa haya mawili yaliyofikiwa mwanzoni mwa miaka ya 1960 mataifa haya mawili yote yakiwa maskini wa kutupwa yalijengwa katika “udugu na ujamaa,” uliounganishwa na imani na ushirikiano/ubia wenye manufaa kwa pande mbili
Misingi hii iliendelezwa na kuhuishwa miaka ya 1970 Tanzania ailipotumia ushawishi wake wa kisiasa kuisaidia China kurejea kwenye Baraza la Usalama la UN na China ikatumia nguvu yake kidogo wakati huo kuisaidia Tanzania na Zambia kutekeleza mradi wa Tazara.
Labda kwa faida ya Ndugu Zitto anayevamiua mawanda asiyoyaelewa, nimesema msingi wa kwanza wa diplomasia ya Tanzania na China ni imani. Asome andiko la mwandishi mahiri wa historia Goran Hyden katika *“Mao and Mwalimu; The Soldier and the Teacher as Revolutionary”* la mwaka 1967.
Atabaini kuwa uhusiano wa China ya Mwanajeshi Mao na Tanzania ya Mwalimu Nyerere uliunganishwa kwanza na “imani” yao katika mageuzi, maendeleo ya watu wao na usawa katika jumuiya ya kimataifa.
Msingi wa pili ni nimetaja ni ubia wenye manufaa kwa pande zote. Nikimnukuu Mwalimu Nyerere, ushirikiano wa Tanzania na China, haukuwa wa kuwekeana masharti, kuingiliana katika sera na mipango ya ndani bali ubia wenye manufaa kwa wote.
Katika hotuba yake akishukuru Serikali ya China kuhusu mkopo wa ujenzi wa Reli ya Tazara iliyochapishwa katika uk. Wa 232 hadi 239 katika kitabu “Freedom and DevelopmentiIUhuru na Maendeleo” Nyerere anafafanua msingi huu wa ushirikiano wa Tanzania na China akisema:
*"Let me state quiet clearly that we appreciate this loan, and we appreciate the fact that it is interest free…And I repeat-the Chinese people have not asked us to become communist to qualify for this loan! They know that we would not sell our independence, even for the railway; and they have never at any point suggested that we should change any of our policies-internal or external (uk. 235)”*
Kwa hiyo nimwambie tu Ndugu Zitto wakati katika eneo la uchumi anahitaji tu “field” tena, katika eneo la diplomasia asiingize kabisa miguu kujaribu kupima kina cha maji, atazama. China anayoizungumzia yeye si hii na Tanzania inayoitolea mfano ilikuwa sambamba na China sio hii ingawa misingi yao inabaki ile ile lakini mchezo wa diplomasia umebadilika sana.
Ingawa ushirikiano wa Tanzania na China uliojengwa katika misingi hiyo miwili mikubwa unaendelezwa sawa sawia katika uongozi wa sasa wa Mwalimu Magufuli na ‘Mwanajeshi’ Xi Jinping, wabobezi wa diplomasia watakwambia ukweli: Hii sio China ya kukaa nayo kichwa kichwa kama ya mwaka 1970.
Kwa sababu hiyo, nihitimishe kwa kumtaka Zitto kuachana na mkakati wake unaojulikana wa kubeza kila jambo au uamuzi wa Rais Magufuli bila kujipa muda wa kutafakari kwa kina. Serikali hii nimeifahamu kuwa makini sana hata kama wanaweza kukosea hapa na pale kama wanadamu lakini si katika hili la kuwatosa Wachina.
Narudia tena na tena, China ya mwaka 2019 sio ya mwaka 1969, muda umepita sana. Ndio maana Zitto akitaka anaweza kuangalia kelele zinazowaandamana Wachina sehemu mbalimbali duniani kwa sasa. Na kuna miradi yao mingi tu imesitishwa.
Akitaka kujua madudu na kashikashi ambazo uwekezaji mwingine wa kampuni anayoitetea ya China Merchant unaendelea nchini Djibouti kwenye Bandari kama ya Bagamoyo asome na sasa kuna kesi kubwa kwenye Mahakama ya Hong Kong, asome makala iitwayo “China Tightens Grip on East African Port” na makala nyingine iitwayo “A legal Tussle over a Strategic African Port sets up a Challenge for China’s Belt and Road Plan”
Lakini pia kwa rejea yake Ndugu Zitto kuhusu mawanda ya “kigeopolitics” (kama anaelewa vyema diplomasia) kuhusu uamuzi wa China kutaka Bandari nyingi katika nchi za Asia na Afrika anaweza kujibidiisha na kusoma hapa na kuona Je, ni malengo ya kiuchumi pekee:
https://www.scmp.com/comment/insigh...-key-success-all-sides-belt-and-road-projects
Lakini nimgusie tu Zitto, rafiki yake mpendwa Mzee Mahathir Mohammed wa Malaysia naye majuzi tu amesitisha mkataba wa Dola za Marekani takribani bilioni 20 (mara mbili ya huu wa Tanzania) na kuziondoa kampuni za China zilizokuwa na mradi wa kujenga reli ya “SGR” kwa nini?Atueleze katika andiko lake lijalo kama ataendelea kuwa na pumzi.
Lakini Zitto anajua kuwa nchi za Pakistani, Myanmar na hata Nepal nazo zimesitisha mikataba kadhaa ya matrilioni na kampuni za China? Kwa Pakistani asome:
https://www.nytimes.com/2018/12/19/world/asia/pakistan-china-belt-road-military.html lakini kwa yaliyoikuta Sri Lanka hadi Bandari yao kuchukuliwa kabisa na China asome:
https://www.nytimes.com/2018/06/25/world/asia/china-sri-lanka-port.html?module=inline
Nisisitize tu kama kuna wakati Tanzania imempata kiongozi anayetazama mbali na si mbele tu, anayetazama keshokutwa na si kesho tu basi tumshukuru Mungu kumpata Rais Magufuli anayesimamia maslahi mapana ya nchi yetu. Leo kuna watu wangekuwa kwenye mamlaka tungeshauza kipande hicho cha Bagamoyo.
Ndio maana nilianza na namalizia kwa hoja ya Dkt. Bashiru ya kutafakari kama kweli katika viongozi vijana tulionao na waina ya hoja za Zitto tunao kweli vijana walio tayari kurithi uongozi wa nchi hii na wakaendeleza safari sahihi ya kufikia Ndoto Ya Taifa na kutuepusha na makosa yale yale ya akina Mangungo wa Msovero?
Tuendelee kutafakari.
*Mwandishi wa makala haya ni mimi Mwamba (sema mara tatu) wa Kaskazini.*