Kutekwa na kuuawa watanzania na tafsiri ya uwajibikaji

Kutekwa na kuuawa watanzania na tafsiri ya uwajibikaji

Joined
Apr 8, 2023
Posts
30
Reaction score
23
KUTEKWA NA KUUAWA WATU NA TAFSIRI YA UWAJIBIKAJI.

Hayati Ali Hassan Mwinyi wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi (1975-1977) alijiuzulu nafasi yake ya Uwaziri kwa sababu ya kosa la kiutendaji la watendaji wa Wizara yake lililogharimu maisha ya Watanzania kadhaa. Historia ikaandikwa na hata alipostaafu Urais hadi mauti yanamkuta, ukurasa huu kwenye historia binafsi ya Hayati Ali Hassan Mwinyi, Wizara ya Mambo ya ndani ya Tanzania na Tanzania kwa ujumla, haitafutika kwa miaka mingi ijayo.

Huenda ni kwa vile hatukuwa tumefikia kwenye kizazi cha "homo egoisticus" tulipo leo ambapo watu wenye siraha wanaweza kuingia kwenye jamii na kukamata mtu kama kuku, na kesho mtu huyo kukutwa amekufa, na bado Mawaziri, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na watendaji wengine wa umma wako maofisini na hakuna hata anayejigusa kuwajibikia vitendo hivi: tunatoa tu memoranda na matamko tukizunguka kwenye viti na viyoyozi vya kodi za umma, kwani wadharauliwa sisi tutakutendeni nini waheshimiwa ninyi!!?

Kama Viongozi na watendaji wa umma wangekuwa na matarajio ya malipo ya uhalifu unaofanywa kwa mgongo wa taasisi wanazoziongoza dhidi ya raia, wangehakikisha kwamba utaratibu unafuatwa na mamlaka zinaheshimu sheria katika utendaji wake, lakini sasa watawala wanajua kwamba wanaweza kufanya lolote na kisha kuja kwenye media na kujibu watakavyo na hakuna madhira ya kauli ama matendo yao. Zamani "majambazi" waliofunika vitambaa usoni waliteka magari na kuwavua abiria nguo zote wakitumia mitutu ya bunduki, na kuwataka waimbe "Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe" kisha kuwaibia mali zao; lakini ilikuwa nafuu hao maana waliwaachia watu uhai wao, sasa "majambazi" wanajificha nyuma ya "mamlaka za nchi" wanakamata watu na 'kuondoka nao' na ama watu hao wanapotea jumla au wanaokotwa maiti na hakuna anayewajibika. Kwani nini kitafanywa!!?

Najiuliza, huyu aliyeshushwa ndani ya gari, na kesho yake kuokotwa maiti, waliomshusha walijitambulisha wao ni nani!!? Wanatoka jeshi gani, 'wanamchukua' (maana hatuwezi kusema walimkamata) marehemu kwa tuhuma gani, wanampeleka kituo gani cha Polisi!!? Au ndiyo "hayawahusu wananchi na abiria waliokuwa kwenye gari!!? Najiuliza, kama abiria wangeamua kwamba 'yanawahusu' kwa vile sheria, kanuni na taratibu hazijazingatiwa', waheshimiwa majambazi wale "wangelazimika kutumia nguvu" katika kile ambacho kingeitwa baadaye kwenye vyombo vya habari "kutekeleza majukumu yao" na tungeowaona wakuu wa taasisi na vyombo vya dola "wakiwataka wananchi kutoingilia utendaji wa vyombo"!!? Tumekuwa jamii ya watu holela wasio na mipaka wala heshima ya utu wa watu!!? Zana, taasisi na watu tuliowaamini kutulinda wamegeuka majahiri tunaopaswa kuishi nao kwa hofu sasa!!? Hivi sasa kila mmoja akiweza tu kupata aina fulani ya magari na silaha, anaruhusiwa kuingia popote na "kumchukua" mtu yeyote na kwenda naye popote hata bila sababu yoyote!!?

Sawa, endeleeni kuwaua Watanzania wenzenu kwa kutumia zana, ofisi na mamlaka za watanzania wenyewe maana ni kosa la Watanzania kukupeni dhamana ya kutumia vitu hivyo, lakini jikimbusheni tu kwamba hata ugali ukiubinya sana mkononi, utatafuta mahala pa kupenyeza utoke!!
 
Back
Top Bottom